MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amegonga mwamba katika hatua yake ya kwanza ya utetezi dhidi ya madai mazito aliyoyatoa dhidi ya Baraza la Mawaziri, kwamba lilirubuniwa ili kutaka kuliua Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC).
Spika wa Bunge la Tanzania , Anne Makinda jana alimbana Mbunge huyo, akisisitiza kuwa awe amewasilisha kwake vielelezo vya ushahidi kuhusu kauli yake hiyo ifikapo Jumatatu.
Kukwama kwa Zitto kunatokana na Spika Makinda kumgomea Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, kumwombea serikalini nyaraka alizotaka kuzitumia kutetea hoja yake hiyo, baada ya Spika kusema nyaraka hizo ni za siri.
Akitangaza bungeni mjini Dodoma, Spika Makinda alisema mara baada ya kumtaka Zitto kuwasilisha ushahidi wa kauli yake hiyo aliyoitoa bungeni Juni 23, Zitto alimwandikia barua akimwomba kumwombea serikalini nyaraka mbili ili azitumie katika ushahidi wake.
Spika alizitaja nyaraka alizoomba Zitto kuwa ni Waraka wa Wizara ya Fedha na Uchumi uliowasilishwa kwenye Kamati ya Makatibu Wakuu kuhusu CHC na Waraka uliowasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri kuhusu CHC, akitumia kifungu cha 10 cha Kanuni ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
“Taratibu za Baraza la Mawaziri ni za siri na haziwezi kutolewa hapa bungeni. Spika hawezi kumsaidia Mbunge ili aweze kupewa nyaraka hizi za Baraza la Mawaziri kwa vile ni za siri.
“Mheshimiwa Zitto alitamka hapa ndani ya Bunge, kwamba anao ushahidi wa kauli yake hiyo na hata baada ya mimi kumwonya, Mheshimiwa Zitto aliendelea kuzungumza kwa kurudiarudia kwamba ana ushahidi wa kauli hiyo.
“Kutokana na uhakika aliodai kuwa nao, nilimwagiza awe amewasilisha kwangu uthibitisho wa kauli yake hiyo. Sasa kwa vile yeye aliomba nimpe nyaraka hizo ambazo siwezi kumpa, naomba kumwongeza siku awasilishe ushahidi kwa njia zake mwenyewe hadi ifikapo Jumatatu, Julai 4,” alisema.
Spika alitoa mfano wa suala kama hilo ambalo lilitokea bungeni Julai mosi, 2008, ambapo aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi (CCM), akiwa tayari amejiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, alisimama bungeni na kudai kuwa kitendo cha Serikali kuiongeza muda Kampuni ya Upakiaji na Uondoshaji Kontena Bandarini (TICTS) kwa miaka mingine 15, kilifanywa na Baraza la Mawaziri.
Kutokana na kauli hiyo, Spika wa Bunge la 10, Samuel Sitta alimtaka Mbunge huyo kutoa uthibititisho kwamba alijuaje Baraza la Mawaziri ndilo lililoamua kuhusu suala hilo wakati yeye hakuwa Waziri wakati huo na wakati taratibu za uendeshaji wa Baraza la Mawaziri ni za siri, hatua iliyomfanya Karamagi kuonywa na Bunge.
Akiwa mchangiaji wa kwanza wa Azimio hilo lililowasilishwa bungeni Juni 23 na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alisema Azimio hilo liligeuzwa kutoka vile lilivyokuwa awali baada ya mawaziri kushawishiwa.
Hoja ya msingi ya Waziri Mkulo ilikuwa ni kuliomba Bunge kupitisha Azimio hilo ili CHC iongezwe kipindi cha mpito cha miaka mitatu, ili imalize majukumu yake na baadaye majukumu yake yahamishiwe Ofisi ya Msajili wa Hazina, lakini hoja hiyo ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM na upinzani na hatimaye ikafanyiwa marekebisho.
“Mheshimiwa Spika, ndani ya Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na hata katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, tulikubaliana kwamba CHC wapewe muda wa kutosha kukamilisha kazi na majukumu yao, halafu baada ya hapo Waziri alete Azimio hapa na si kuwapa kipindi cha mpito cha miaka mitatu kama Azimio lilivyowasilishwa leo.
“Nawaombeni wabunge wenzangu wote, tukatae uamuzi huu wa Baraza la Mawaziri kwa kuwa yametokana na kurubuniwa na watu wenye lengo la kuiua CHC kwa ajili ya maslahi yao. Ikumbukwe kuwa chombo hiki kinaangalia mali za umma na mashirika, hivyo kutaka kukiua na kupeleka majukumu haya kwa Msajili wa Hazina ambaye uwezo wake wa kulinda mali za umma ni mdogo sana, ni kutaka kuiba mali za Watanzania,” alisema Zitto.
Alisema Azimio la Serikali la kuipa CHC kukamilisha majukumu yake lililenga kusaidia wafanyabiashara walioiba mali za umma ikiwa ni pamoja na kukopa mabilioni ya fedha kutoka iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao kesi zao ziko mahakamani, kupata ahueni kwa vile hatua hiyo itapoteza ushahidi.
Baada ya kueleza hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), George Mkuchika, aliomba Mwongozo wa Spika akitaka Zitto athibitishe kauli yake kwamba mawaziri walirubuniwa, kwa vile imewadhalilisha mawaziri hao ambao wanafanya kazi kwa maadili na kwa kuzingatia maslahi ya nchi.
Mkuchika alisema kitendo cha kusema uamuzi huo unatokana na kurubuniwa kwa mawaziri kinaleta picha mbaya kwa Watanzania ambao wamewaamini.
Baada ya maelezo ya Mkuchika, Spika alimtaka Zitto kuwa makini na kauli anazotoa anapochangia, ikiwamo ya kudai kwamba mawaziri wanashawishiwa na kurubuniwa; lakini Zitto aliposimama tena ili kuendelea kuchangia alitamka tena kuwa anao ushahidi kwamba mawaziri walikuwa wameshawishiwa na kurubuniwa hadi wakatengeneza Azimio hilo jipya.
“Mheshimiwa Spika, siwezi nikatafuna maneno hapa, nina uhakika na ninachokisema, uamuzi wa Baraza la Mawaziri ni matokeo ya ma-lobbyist (washawishi) na kama Serikali mnabisha, leteni hapa mapendekezo ya awali ambayo yaliwasilishwa katika Kamati ya Makatibu Wakuu na Baraza la Mawaziri ili tuone yalikuwa yanasemaje.”
Kutokana na msimamo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alimwomba Spika Makinda kumtaka Zitto awasilishe bungeni ushahidi kutokana na kauli yake hiyo, hatua iliyomfanya Spika kumpa Mbunge huyo muda wa kuandaa ushahidi huo na kuuwasilisha bungeni jana.
Shughuli zinazofanywa na CHC ambazo mpaka sasa hazijakamilika ni pamoja na urekebishaji wa TRL baada ya kampuni ya Rites kuondoka, kushughulikia uuzaji wa hisa za Serikali NBC (T) Limited, uperembaji na uhakiki wa vitendo na mashirika yaliyobinafsishwa, urekebishaji wa mashirika 34 yaliyobaki na kukamilisha ufilisi wa mashirika ya umma 24 yaliyobaki.
Pia ukusanyaji wa madeni ya iliyokuwa NBC yenye thamani ya Sh. bilioni 15.8 na urekebishaji wa kampuni ya TTCL baada ya hatua ya awali ya ubinafsishaji kushindikana na mwekezaji wa Airtel kuonesha nia ya kutoka kwenye ubia.
No comments:
Post a Comment