Friday, January 29, 2010

Sitta na Lowassa wagongana tena


-Kamati ya Mwinyi yawashindwa
-Ujasusi watumika kuwinda vigogo wa CCJ

KIWEWE cha kuanzishwa kwa Chama Cha Jamii (CCJ) kinachohusishwa na baadhi ya vigogo maarufu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinashika kasi huku kamati ya wazee iliyoongozwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, ikishindwa kumaliza makundi kama ilivyokusudiwa, blogu yetu imefahamishwa.

Habari za ndani ya CCM na Serikali zinaeleza kwamba kamati ya Mzee Mwinyi imekumbana na vizingiti kadhaa kutokana na baadhi ya vigogo wa juu wa chama hicho kuanza kutegeana katika kufikia makubaliano ya kumaliza tofauti zao.

Tayari CCJ kinaelezwa kuwa chama ambacho kitategemea zaidi matokeo ya kamati ya Mzee Mwinyi na baadhi ya wachambuzi wamekwisha kuonyesha kuwa chama hicho ambacho hata usajili wa muda hakina, kimeitikisa vilivyo CCM ambayo viongozi wake wamekuwa wakitoa kauli za kukiponda.

Pamoja na kuwapo makundi manne ndani ya CCM, makundi mawili ndiyo yanayotajwa kuwa chachu ya misuguano ndani ya chama hicho, yakiongozwa na wanasiasa wawili wazito, Spika wa Bunge, Samuel Sitta na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa kiasi kwamba Kamati ya Mwinyi imekuwa ikiyazingatia zaidi makundi hayo katika kazi yake.

Kundi jingine ndani ya chama hicho ni la viongozi wastaafu ambao ni pamoja na mawaziri wakuu wastaafu; Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye ambalo linaelezwa kuwa na nguvu kubwa inayowaumiza vichwa wakubwa ndani ya CCM kiasi cha kuanzisha propaganda ya kuwahusisha wastaafu hao na CCJ.

Soma zaidi

Thursday, January 28, 2010

MSWADA WA SHERIA YA GHARAMA ZA UCHAGUZI
Jana katika mfululizo wa Semina za kila siku ya Jumatano mada iliyojadiliwa ni kuhusu mswada wa sheria ya gharama za uchaguzi mwezeshaji bw. Hebron Mwakagenda aliukosoa mswada huo kwa kushindwa kuweka ushindani ulio sawa katika uchaguzi kwa mfano:- Wakati CCM ikipata ruzuku ya Shilingi bilioni moja kuna baadhi ya vyama havipati kabisa ruzuku hiyo mfano CHAUSTA na vinginevyo.
Kwa hiyo mswada huu unalenga kuua demokrasia iliyopo na kuendeleza mfumo mbaya wa utawala.

Katika maoni yake mchangiaji mada Bw. Eliab Maganga alisema mswada huu unalenga kuleta matabaka nchini kwani sehemu kubwa ya vyama vya siasa nchini vinapata msaada kutoka nchi wahisani hivyo mswada huu kuzuia vyama hivyo kupata misaada ni sawa na kuwagawa watanzania kivipato na kushindwa kugombea nafasi mbalimbali nchini kwani wenye nacho tu ndio watakaoweza kushiriki katika chaguzi mbalimbali nchini.

Mjamzito auawa kwa risasi mlangoni kwake

MKE wa mchimbaji maarufu wa madini ya tanzanite katika machimbo ya Mererani wilayani Simanjiro, Jacqueline Minja (28), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake.

Marehemu ambaye pia alikuwa na ujauzito wa miezi minane, ni mke wa Deo Minja ambaye ni mdogo wa mfanyabiashara maarufu mjini Arusha, Anselmi Minja, anayemiliki maduka makubwa katika miji ya Arusha na Nairobi.

Tukio hilo ambalo limewashtua wakazi wengi wa hapa na ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, lilitokea juzi saa 3.30 usiku nje ya lango la kuingilia nyumbani kwa mchimbaji huyo eneo la Lemara mjini hapa.

Kamanda Matei alisema jana kuwa Jacqueline alipigwa risasi kichwani na mmoja wa watu wawili waliokuwa na pikipiki akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Nadia wakati akisubiri mtumishi amfungulie lango la nyumba yake.

“Wakati anasubiri kufunguliwa geti, ghafla walitokea watu wawili wakiwa na pikipiki aina ya Toyo rangi nyekundu na mmoja alishuka na kumfuata na kumwuliza aliko mumewe, kabla ya kuchomoa bastola na kumpiga risasi iliyompata kwenye paji la uso,” alisema Kamanda Matei.

Alisema baada ya tukio hilo, mtu aliyempiga risasi alipanda pikipiki iliyokuwa akiendeshwa na mwenzake na kutoweka kwa kasi kutoka eneo hilo huku mtumishi aliyekuwa akifungua lango akipiga kelele za kuomba msaada.

“Watu walijitokeza kutoa msaada wa kumkimbiza mama huyo katika Hospitali ya KKKT Selian, lakini alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini,” alisema.

Kamanda alisema tukio hilo limeacha maswali mengi kwa polisi na wameshindwa kufahamu iwapo tukio hilo linahusiana na ujambazi au ni mauaji ya kukusudia kutokana na wahusika kutopora chochote.

“Kwa kweli tunajiuliza kama tukio hili linahusiana na ujambazi au ni mauaji ya kupangwa, kwani watuhumiwa hao hawakuchukua chochote … tumehoji ndugu na jamaa wa karibu wa wanafamilia hao, wanasema hawakuwahi kuwa na ugomvi wa aina yoyote na mtu yeyote,” alisema Matei.

“Kwa sasa tumeanzisha uchunguzi mkali wa tukio hilo na mwili wa marehemu uko katika mochari ya Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru ukisubiri taratibu za mazishi kutoka kwa ndugu zake,” alisema Kamanda.

Hata hivyo, moja wa ndugu za marehemu aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliiambia HabariLeo kuwa watu hao waliondoka na funguo za gari na simu ya mkononi ya marehemu.

“Baada ya tukio, tumekuta funguo za gari hazipo na pia simu yake ya mkononi haionekani na tunahisi kuwa majambazi hao waliondoka navyo,” alisema ndugu huyo.

Mji wa Arusha umekuwa na matukio makubwa ya uhalifu unaohusisha mauaji kwa muda mrefu sasa pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Jeshi la Polisi kupambana na matukio hayo, lakini bado kiwango kiko juu.

Tuesday, January 26, 2010

Gharama za uchaguzi kutawala Bunge

MKUTANO wa 18 wa Bunge unaanza leo mjini hapa, huku ukitarajiwa kutawaliwa na mjadala kuhusu mambo mbalimbali, ikiwamo Miswada ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi.

Huu ni mkutano wa kwanza kati ya mitatu iliyobakia ambayo inakamilisha kipindi kilichoanza mwaka 2005 huku baadhi ya wabunge wakisema muswada wa gharama za uchaguzi umekuja wakati muafaka.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zulu, alisema kikao cha leo kitaanza na maswali na majibu.

Baadaye kutakuwa na kikao cha wabunge kinacholenga kutoa ufafanuzi kuhusu maazimio yaliyofikiwa na Kamati ya Uongozi kuhusu Mkutano wa 18 kabla ya kuanza vikao vya Kamati za Vyama vya Siasa.

Katika mkutano huu miswada minane inatarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa. Nayo ni wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2009; Sheria ya Mawasiliano na Eletroniki na Posta 2009; Sheria ya Kurekebisha Sheria mbalimbali, Sheria ya Usajili wa Wabunifu Majengo, Wakadiriaji Majengo 2009 na wa Sheria ya Nyongeza wa 2009/10.

Pamoja na miswada hiyo ambayo baadhi yao inatarajiwa kuanzisha mjadala mkali bungeni, pia maazimio matano yatawasilishwa likiwamo la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa pamoja wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Lingine ni la kulinda hakimiliki za wagunduzi wa aina mpya za mimea; la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jinsia na Maendeleo ya SADC na la Kuridhia kuanzishwa Mkataba wa Kamisheni ya Maji ya Mto Zambezi ambalo lilibaki katika maazimo yaliyopitishwa katika mkutano wa 17 uliomalizika mwaka wa jana. Katika mkutano huu, Bunge litapata taarifa ya ufafanuzi kuhusu hoja binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Ngorongoro, Aika Telele (CCM) katika mkutano wa 17 kuhusu vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika kuhamisha jamii ya wafugaji katika msitu wa hifadhi ya Loliondo.

Ingawa taarifa kamili ya yatakayojiri katika mkutano huu wa Bunge haikutolewa rasmi jana, ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini itawasilisha taarifa ya utekelezaji ya Serikali kuhusu mkataba tata wa kampuni ya Richmond.

Mambo mengine yanayotajwa kuchukua nafasi katika mkutano huu ni madai ya Mgodi wa North Mara ya kutiririsha maji ya sumu katika Mto Tigite. Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili, walisema miongoni mwa miswada muhimu ikizingatiwa na wakati uliopo wa kuelekea uchaguzi, ni wa gharama za uchaguzi.

“Bunge hili litakuwa limefanya kazi nzuri likipitisha muswada huu. Ipo changamoto kubwa, kwa sababu kuna baadhi ya watu hawaupendi. Lakini ni vizuri sheria hii iwepo,” alisema Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga (CCM).

Alisema anaona suala kuhusu mgodi wa Kiwira ambalo pia litajadiliwa bungeni na la Richmond, kwake hayana umuhimu mkubwa kama ilivyo kwa muswada wa Sheria ya gharama za uchaguzi.

“Muswada huu umekuja wakati muafaka. Naipongeza Serikali. Haya masuala sijui Richmond, Kiwira haya ni mambo ya kawaida. Kwa mfano suala la Richmond, Serikali inakuja kusema imefanya nini katika kutekeleza mapendekezo 23 na hatimaye suala hili lifungwe,” alisema Kaboyonga.

Mchakato kugawa majimbo waanza

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza uchunguzi wa majimbo ya uchaguzi wa Bunge na kuyagawa kama itahitajika, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Omary Makungu, alisema katika kubaini vigezo vitakavyotumika katika kuchunguza mipaka na kugawa majimbo, Tume imezingatia vigezo vilivyotajwa katika Katiba sambamba na utafiti iliyoufanya katika nchi zingine za Afrika, ikiwamo idadi ya watu.

Uchunguzi umeonesha kuwa maeneo mengi yatagawanywa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu wanaozidi wastani wa 206,130 vijijini na watu 237,937 mijini.

Jaji Makungu alivitaja vigezo hivyo kuwa ni mawasiliano, jiografia, idadi ya watu, uwezo wa ukumbi wa Bunge, hali ya uchumi na ukubwa wa eneo husika; pia mipaka ya kiutawala, mazingira ya Muungano na mgawanyiko wa wastani wa idadi ya watu.

“Kwa kutumia vigezo vilivyopo, baada ya Tume kukokotoa, imebainika kuwa mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu katika majimbo ya uchaguzi yaliyo katika maeneo ya vijijini ni watu 206,130 na mijini wastani wake ni 237,937, majimbo yatakayokidhi kigezo hiki, ndiyo yatakayoendelea kufikiriwa na vigezo vingine vilivyowekwa,” alisema Makungu.

Alivitaja vigezo vingine vitakavyotumika kugawa majimbo hayo ni pamoja na uzingatiaji wa jimbo moja kutokuwa ndani ya wilaya au halmashauri mbili, kata moja kutokuwa ndani ya majimbo mawili ya uchaguzi, uwezo wa ukumbi wa Bunge na idadi ya viti maalumu vya wanawake.

Alisema Katiba ya Nchi ya Mwaka 1977 imetenga kiasi kisichopungua asilimia 30 kwa ajili ya wabunge wanawake wa viti maalumu, ili kuleta usawa wa kijinsia, hivyo Tume haina budi kuzingatia idadi hiyo ya wabunge.

“Licha ya kuwapo matakwa ya asilimia 50 kwa 50 ya idadi sawa kwa wabunge wanawake na wanaume, mpaka sasa hatujapata uthibitisho wake, hivyo tutazingatia idadi hiyo kama ilivyoainishwa na Katiba,” aliongeza Makungu.

Akizungumzia gharama za uchaguzi huo utakaofanyika baadaye mwaka huu, Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu, alisema mchakato wa uchaguzi umegawanyika katika awamu tatu tofauti; ya kwanza na ya pili ilihusisha uboreshwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura huku awamu ya tatu ikiwa ni uchaguzi wenyewe.

Alisema katika Daftari, zaidi ya Sh milioni 27 zilitumika huku awamu ya pili ikitumia Sh milioni 47 kwa ununuzi wa vifaa vipya zikiwamo kamera huku Uchaguzi Mkuu kwa ujumla ukitengewa kiasi kisichopungua Sh bilioni 64, tofauti na Sh bilioni 63 zilizotumika katika uchaguzi uliopita.

Kuhusu karatasi za kupigia kura, Kiravu alisema kwa kawaida Tume ina utaratibu wa kutangaza zabuni ya kuchapa karatasi hizo na anayeshinda ndiye hupewa. Alikanusha uvumi kuhusu mchakato wa kuchapa karatasi hizo katika moja ya kampuni za uchapaji nchini.

Monday, January 25, 2010

Warioba aacha ‘maswali’ CCJ

TUHUMA za kuwepo kwa wanasiasa waandamizi na wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaopanga kujitoa katika chama hicho tawala na kujiunga na chama kipya wanachodaiwa wamekiandaa kinachoitwa Chama Cha Jamii, zimeendelea kutoa sura tofauti miongozi mwa wanasiasa hao.

Wakati juzi Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Mtera, John Malecela alikanusha vikali kuhusika na uasisi wa chama hicho, jana Habari Leo liliwapata viongozi wengine waandamizi wanaotuhumiwa kuazisha chama hicho ambao hawakuthibitisha kuwa miongoni mwa waasisi wa chama hicho wala kukana tuhuma hizo.

Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba alizungumza na Habari Leo kuhusu tuhuma kwamba yeye ni mmoja wa mawaziri wakuu watatu wanaotuhumiwa kuunda CCJ, alisema hawezi kuzungumzia chochote kuhusiana na madai kuwa yeye ni miongoni mwa waasisi wa chama hicho.

“Siwezi kusema chochote kuhusiana na taarifa zinazosambazwa na mtu asiyejulikana,” alisema.

Aidha Waziri Mkuu huyo wa zamani alishauri mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na uongozi wa CCJ kuhusiana na shauri hilo.

Habari Leo lilimpata mwanasiasa mwingine mkongwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na kumuuliza iwapo anahusika na uanzishwaji wa chama hicho, kama ilivyo katika waraka wenye tuhuma hizo na yeye alisema hajaona nyaraka zinazomuhusisha yeye na CCJ.

“Sijaona nyaraka hizo,” alisema Butiku na kukataa kuendelea na mahojiano na mwandishi wa habari hii hata baada ya kuhakikishiwa kuwa waraka huo upo.

Mwandishi wa habari alitaka kujua kama mwanasiasa huyo alikuwa ameona nyaraka za chama hicho na kama ana maoni yoyote kuhusiana na madai kwamba anahusika katika kuiasisi CCJ.

Kuomba usajili kwa chama hicho kipya cha siasa kumezua maswali mengi miongoni mwa watu kadhaa wakiwemo wanasiasa kutokana na madai kuwa viongozi wakubwa wa CCM wamekiandaa na wanapanga kujiunga nacho kwa nia ya kuiangusha CCM katika uchaguzi mkuu ujao.

Tayari Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba ametoa kauli kuwa CCJ hakiwatishi huku Katibu wa Uenezi wa Kamati Kuu ya CCM (NEC), John Chilighati akisema kuwa watakaotoka CCM, watakuwa wamejimaliza wenyewe.

Licha ya viongozi hao waliokwisha zungumzia CCJ, viongozi wengine wanaodaiwa kuhusika nacho ni pamoja na kundi la wabunge wanaojipambanua kuwa makamanda wanaopiga vita rushwa.

Kutokana na misimamo ya vigogo hao wanaotuhumiwa kutaka kujiunga na chama hicho, ilidaiwa pia kuwa vigogo hao wameandaa kongamano la kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, litalaotumika kama uwanja wa kukitangaza chama hicho.

Kongamano hilo limedaiwa kuwa lingefanyika kwa mgongo wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Aford ambayo haijapata usajili lakini lengo lake likiwa kutoa ishara za awali za chama hicho cha CCJ.

Habari Leo lilifanikiwa kumpata kiongozi wa taasisi hiyo ya Aford, Julius Miselya ambaye alianza kuvishutumu vyombo vya habari kwa kutumia vibaya jina la taasisi yake kuisakama serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

“Ni nyie waandishi wa habari mnaosambaza taarifa hii inayotoka kwa mtu asiyejulikana na kuleta mtafaruku nchini,” alisema.

“Mimi sifungamani na chama chochote, nimewatambua watu wanaojihusisha na CCJ kwa kusoma magazeti asubuhi hii,” alisema Miselya.

Amesema kongamano hilo ambalo bado lipo katika maandalizi limeibuliwa kwa waandishi wa habari kwa lengo la kupotosha ukweli.

“Muulize Waziri Mkuu kama amethibitisha kushiriki, sitazungumzia kitu hicho,” alisema. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ametajwa katika waraka huo kuwa ndiye atakayefungua kongamano hilo.

Alipohojiwa kama kongamano hilo litaendelea kama lilivyopangwa, alisema kwamba hatasema chochote kwa vyombo vya habari.

Baadhi ya viongozi wa CCM waliounganishwa na uanzaji wa chama kipya cha siasa nchini walipoulizwa walisema kwamba ndio kwanza wanajua kuwa kuna chama kipya.

Mwanasiasa mwingine aliyehusishwa na chama hicho kipya na kukanusha ni mbunge wa Maswa, Magale Shibuda.

Juhudi za gazeti hili kupata maoni ya wahusika wengine zilishindikana jana na bado zinaendelea.

Juzi Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, aliliambia Habari Leo kuwa chama hicho kipya kina safari ndefu kwa kuwa taratibu za kusajili chama huchukua muda.

Alisema licha ya chama hicho, tayari kuna vyama vingine vingi ambavyo vinasubiri kupewa usajili na kuongeza kuwa huenda CCJ kikapata usajili wa muda kabla ya Machi mwaka huu.

Wednesday, January 20, 2010

Kashfa gari la wagonjwa Ikulu yatupiwa zigo

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imesema mkanganyiko uliotokea Ikulu Dar es Salaam juzi, mbele ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu nani anastahili kupokea msaada wa gari la kubeba wagonjwa kati ya halmashauri ya wilaya ya Longido na Ngorongoro, ulitokana na Ikulu kwenyewe.

“Binafsi ninavyofahamu na maandishi (barua) niliyonayo ofisini kwangu, yanaonesha kwamba, gari hilo ni la Longido na si Ngorongoro, sasa sijui ilikuwaje lakini taarifa nilizonazo ni kwamba Mkurugenzi wa Ngorongoro alipata taarifa kutoka kwa Mkuu wake wa Wilaya, ambaye naye alipokea simu kutoka Ikulu kwamba wakachukue gari,” alisema Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha (RAC), Nuru Milao, alipozungumza na gazeti hili kwa simu jana.

Milao, ambaye mbali ya ufafanuzi huo alidai hana taarifa ya kilichotokea Ikulu kwa kuwa yuko nje ya ofisi, kwa shughuli za ukaguzi wa serikali za mitaa, alisema anachofahamu ni kwamba kama Rais amesema gari ni la Longido ni kweli, kwa kuwa hata taarifa za ofisi yake zinaonesha hivyo na si vinginevyo.

Katibu Tawala huyo wa mkoa alisema kama kuna mkanganyiko wowote basi umeanzia Ikulu kwenyewe kwa kuwa kabla hajawa nje ya ofisi kikazi, Mkurugenzi wa Ngorongoro, Kayange Jacob, alimweleza kuwa ameambiwa na Mkuu wa Wilaya (Ngorongoro) kuwa aende Ikulu, wilaya imeitwa kuchukua msaada wa gari la wagonjwa.

“Unajua unapopewa taarifa kama hiyo, tena kutoka Ikulu, huwezi kuhoji sana, lakini hata hivyo Mkuu wa Wilaya (Ngorongoro) naye alielewa kuwa si yeye, alipata wasiwasi, maana alikuwa na taarifa ya msaada kama huo kwa halmashauri ya Longido si yake, ila alivyodai, alikuwa ameona Mkurugenzi wake aende tu, huenda magari yamepatikana zaidi ya mahitaji aliyoahidi Rais Kikwete,” alisema na kuongeza:

“Hata mpaka jana, Mkuu wa Wilaya aliyekuwa akitafutwa kwenye simu na Ikulu baada ya mkurugenzi wake kuchelewa eneo la makabidhiano, ni wa Ngorongoro na si wa Longido, akielezwa katika simu na maofisa wa Ikulu ‘mbona mkurugenzi wako haonekani?’ Na nijuavyo mkurugenzi huyo ni mgeni Ikulu, bila shaka alichanganya aingie kwa mlango gani.”


Milao alisema kama Rais amekataa kumpa wa Ngorongoro, basi yuko sahihi, maana ni kweli alikiahidi kijiji cha Engarinaibo, Longido alipofanya ziara Arusha mwaka jana na taarifa (dokezo) za mkoa zimeshaandikwa kuwa ahadi ya Rais kwa kijiji hicho, imetimia.

Huku akionesha naye kuchanganyikiwa na hali hiyo, alisema watu wengi wamekuwa wakichanganya majina kati ya Longido na Loliondo, jambo linalochangia nyaraka na taarifa nyingi kuchanganywa na kwamba Longido ilipewa taarifa mapema na ofisi ya mkoa kuhusu msaada huo na kuahidi kuwa ingawa mawasiliano ni duni, atawasiliana na halmashauri hizo kupata taarifa zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali aliliambia gazeti hili kuwa alipokea taarifa kwa simu kutoka Ikulu ikimtaka ampeleke Mkurugenzi wake akapokee msaada huo wa gari na kwa kuwa idara zake kadhaa zinauhitaji, hakusita kufanya hivyo.

“Nilipigiwa simu wala si barua, nikaelezwa nimpeleke mkurugenzi akapokee msaada wa gari kutoka kwa Rais, tunauhitaji hapa, hivyo sikuhoji, wala sikuuliza jina la aliyenipigia baada ya kuelezwa kuwa ni Ikulu na asubuhi nikapigiwa tena kama amefika, nikawajibu yupo nje ya lango la Ikulu,” alisema Wawali.

Juzi, Rais Kikwete aligoma kukabidhi gari la msaada la kubeba wagonjwa katika hafla iliyokuwa ifanyike kwenye viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, baada ya utata kuibuka kuhusu halmashauri inayopaswa kukabidhiwa gari hilo baada ya Mkurugenzi wa Ngorongoro kufika kupokea msaada huo badala ya wa Longido.

Kwa mujibu wa kauli ya Rais Kikwete kwa maofisa wa Ikulu, wakati ulipozuka mkanganyiko huo, gari hilo moja kati ya mawili yaliyokuwa yakabidhiwe, badala yake likakabidhiwa moja, yalitolewa na kampuni ya CMC Automobiles Limited na ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa mwishoni mwa mwaka jana kwa wananchi wa kijiji cha Engarinaibo na kituo cha Afya cha Kamsamba, Mbozi, alipofanya zaira katika mikoa hiyo.

“Mimi mwenyewe nilifika katika kijiji hicho cha Engarinaiko, Longido, nikiwa katika ziara mkoani Arusha, hali niliyoikuta pale katika kituo cha afya cha kijiji, ilinifanya nikaahidi nikipata gari la wagonjwa, nitawapa na si hawa wa Loliondo, hii ni nini! Ni kashfa kubwa hii,” aliwaeleza maofisa wa Ikulu waliokuwa katika tukio hilo akiwamo Katibu wa Rais, Prosper Mbena.

Mwandishi wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, alifafanua mkanganyiko huo kwa waandishi wa habari walioalikwa Ikulu kuandika kuhusu makabidhiano hayo, akikiri kuwapo udhaifu katika mawasiliano na kusema Ikulu inaendelea na mawasiliano ili kumpata anayepaswa kupewa gari hilo na si watu wa Ngorongoro.

Hata hivyo siku hiyo jioni, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu ilisema Rais Kikwete alikabidhi gari moja kwa halmashauri ya Mbozi ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Levison Chilewa alipokea msaada huo kwa niaba ya wananchi wa Kamsamba na maeneo jirani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya CMC Automobiles Limited ya Dar es Salaam, iliyotoa msaada huo wa magari hayo aina ya Land Rover Defender 110 Hard Top yenye thamani ya dola 108,000 za Marekani, Abdul Haji, alimkabidhi Rais Kikwete magari hayo hivi karibuni ikiwa ni kumbukumbu ya mkewe, Claude Haji, aliyewahi kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 30 na kusaidia wasiojiweza enzi za uhai wake.

Tuesday, January 19, 2010

TRL kuvunjwa mwezi ujao,Serikali kujitwisha mzigo wa kuendesha reli

SERIKALI imesema mkataba kati yake na Kampuni ya Rites kutoka China inayoendesha Kampuni ya Reli (TRL), utavunjwa mwezi ujao.

Uamuzi huo unatokana na kile kilichoelezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omari Chambo, kuwa ni migogoro inayoikabili kampuni hiyo iliyotokana na uongozi mbovu.

Katibu Mkuu huyo alitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam alipokutana na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali, chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Pangani, Mohamed Rished (CCM).

Rished ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ndiye aliyeanza kuhoji sababu za serikali kuwa na kigugumizi cha kuvunja mkataba wa TRL.

Baada ya Chambo kujibu kwamba wako katika mchakato wa kuuvunja, Mbunge wa Viti Maalumu, Rosemary Kirigini (CCM) alisisitiza kwa kutaka kamati ielezwe muda kamili uliopangwa kutekeleza uamuzi huo.

Chambo alijibu kwamba utavunjwa mwezi ujao na akafafanua sababu za kutofanya haraka kutekeleza hilo. Alisema sababu kubwa ni kutokana na vipengele vya kisheria ambavyo kama wangeharakisha, serikali ingeweza kuingia hasara ya mamilioni ya fedha.

Alisema kwa sasa, wizara imekaa pamoja na Mwanasheria Mkuu na idara nyingine na kwamba muda mfupi ujao watatoa taarifa kamili.

Mbunge wa Nkasi, Ponsiano Nyami (CCM), alihoji sababu za wanasheria nchini kutoweka vipengele vizuri vya sheria kabla ya kuingia mkataba. Chambo alisema baada ya mkataba kuvunjwa, wataingiza vipengele vigumu vya sheria.

Chambo alipoulizwa na gazeti hili ni namna gani baada ya mkataba kuvunjwa serikali itatoa huduma kwenye Reli ya Kati iliyokuwa ikihudumiwa na TRL, hakupenda kufafanua kwa undani zaidi ya kusema suala hilo liachwe hivyo.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Naibu Katibu Wizara ya Fedha na Uchumi, John Haule alipokutana na Kamati hiyo, alikaririwa na baadhi ya vyombo habari akisema mazungumzo kuhusu mkataba wa TRL yanaendelea kuelekea kwenye kuuvunja na kwamba serikali itatafuta mwekezaji mwingine au kuendesha yenyewe.

Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Hundi Chaudhary alipoulizwa na gazeti dada la Daily News kuhusu maoni yake juu ya uamuzi huo, alisema hana la kusema.

Tangu mwaka 2006, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipokodishwa kwa mwekezaji wa kigeni na kuzaa TRL kwa ajili ya kutoa huduma kwenye Reli ya Kati, kumekuwepo migogoro isiyoisha baina ya menejimenti na wafanyakazi.

Licha ya migogoro, vile vile utendaji wa kampuni hiyo umekuwa ukinyooshewa kidole na watu wa kada mbalimbali wakiwemo wabunge ambao wamekuwa wakishinikiza mkataba huo uvunjwe mara moja kutokana na kukosekana ufanisi katika kuendesha reli hiyo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni miongoni mwa walioonesha wasiwasi juu ya utendaji wa kampuni hiyo chini ya uongozi wa Kampuni ya Rites ya India.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu huyo aliiambia kamati kuwa serikali inaendelea kutafuta mbia atakayeendesha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Alisema wapo watano walioonesha nia ya kuendesha kampuni hiyo na wako katika mchakato wa kupata mmoja. Kwa mujibu wa Chambo, kampuni hiyo ina ndege tatu.

Akielezea tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliotokana na mafuriko mkoani Morogoro na Dodoma, Katibu Mkuu huyo alisema maeneo 18 yameainishwa kuwa yaliharibika na kwamba zinahitajika takribani Sh bilioni sita.

Hata hivyo, alisema zinahitajika Sh bilioni 10 kwa ajili ya kukabili uharibifu utakaoendelea. Alisema taarifa zilipelekwa kwa Waziri Mkuu na ujenzi utaanza mara moja.

Mgogoro wa ardhi Hanang': Kwanza wakulima, sasa wafugaji

BAADA ya jamii ya wafugaji wa Kibarbaig wa vijiji vya Mogitu, Ming’enyi na Dawar wilayani Hanang’ mkoani Manyara kuizuia serikali wilayani humo kugawa ardhi yao, mgogoro huo sasa umehamia kwa wakulima wa vijiji hivyo baada kamati iliyokuwa ikisuluhisha kupendekeza ardhi ya wakulima hao imegwe kwa ajili ya wananchi wanaohamishwa kutoka eneo la Mlima Hanang’.

Wafugaji wa Kibarbaig kati ya Desemba 16-19 mwaka jana walitangaza “vita” dhidi ya serikali kupinga mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ wa kugawa ardhi ya iliyokuwa shamba la mradi wa ngano la Warett lenye ukubwa ekari zaidi ya 16,000.

Wafugaji hao wakiwa wamejihami kwa silaha za jadi walikimbilia katika msitu ulioko jirani na kijiji hicho baada Polisi kuwakamata baadhi ya wafugaji hao wakiwamo viongozi wa serikali za vijiji.

Wananchi hao pia walitoa madai mazito kuwa Polisi na watendaji waliokuwa wakiendesha operesheni ya kuwakamata walikiuka haki za binadamu kwa kuwapiga, kuwanyima chakula, na kuwaweka mahabusu kwa siku tatu bila ya kuwafikisha mahakamani.

Hata hivyo, baada vurugu hizo na kuhofiwa kutokea kwa umwagaji damu uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara ukiongozwa na Mwenyekiti Luka ole Mukusi, uliunda kamati maalumu ya kutafuta muafaka kuhusu mgogoro huo.

Baada ya kufanyika vikao vya usuluhishi kwa wiki nzima kamati hiyo ilikubaliana na wananchi kuwa Halmashauri imesitisha mpango wa kugawa eneo lililokuwa limetengwa kwa ajili malisho lakini kungefanyika uhakiki wa ardhi iliyogawiwa kwa wakulima.

Katika mapendekezo hayo kamati hiyo iliweka bayana kuwa wakulima ambao walikuwa na maeneo makubwa yangemegwa ili wananchi wanaohamishwa kutoka mlima Hanang’ wapatiwe ardhi.

Ole Mukusi alithibitishia Raia Mwema kuwa ni kweli walikubaliana kufanya zoezi la kuhakiki watu waliogawiwa ardhi na ukubwa wa maeneo yao kwa wananchi wenye kuhitaji ardhi.

“Zoezi tayari limekwisha kuanza kuanzia tarehe 5 Januari na linatarajiwa kumalizika Januri 20 ili wananchi waweze kuendelea na shughuli ya kilimo kwani huu ni msimu wake…..tumechukua uamuzi huu kutokana na wasiwasi kuwa ugawaji ardhi uliofanywa awali haukufuata taratibu,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo viongozi na watendaji wa serikali watashirikiana na wazee wa kimila wa makabila ya Wabarbaig na Wairaq na kila mkulima atalazimika kusimama katika eneo lake.

“Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kutokana na madai kuwa kuna baadhi ya watu wamepewa maeneo makubwa ya ardhi wakati wa mgao wa kwanza uliosimamiwa na viongozi wa vijiji husika, ”alisema.

Ole Mukusi alisema CCM kama chama tawala kiliona umuhimu wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo kutokana na mazingira yaliyojitokeza ambapo wananchi walitaka kujichukulia sheria mkononi.

Soma zaidi

Monday, January 18, 2010

KAMATI YA BUNGE YAKATAA RIPOTI YA BODI YA MIKOPO!!!

Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma imekataa kupokea ripoti ya hesabu ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) baada ya bodi hiyo kushindwa kuchanganua matumizi ya Sh33.9 bilioni.
Kati ya fedha ambazo bodi hiyo ilishindwa kutoa mchanganuo, Sh12.9 bilioni ni marejesho ya mikopo iliyotolewa kwa wanafunzi katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kama ada ya masomo na posho.
Ripoti hiyo iliyowasislishwa na bodi ya wakurugenzi wa HESLB ikiongozwa na mwenyekiti wakezi, Anselim Lwoga haina mchanganuo wa matumizi ya Sh21 bilioni zilizotolewa na Wizara ya Fedha.
"Hii ripoti hatutaipitisha lakini nendeni mkaipitie tena tukutane Dodoma... kabla vikao vya Bunge havijaanza muilete ikiwa imechanganuliwa nama fedha hizo zilivyotumika,"alisema Kilasi na kuongeza.
"Ripoti hii tulishaipitia wakati fulani na tukawaandikia barua ya kutaka watuletee kwa maandishi lakini hawakufanya hivyo."
Kilasi alisema matumizi ni makubwa kuliko hata kiasi cha fedha wanazoingiza kitu ambacho ni hatari kwenye utawala wowote ule.
Kama hiyo haitoshi bodi hiyo imebainika kufanya uzembe kwa kushindwa kuomba serikalini Sh58 bilioni katika bajeti yao ya kila mwaka ili iweze kulipa deni inalodaiwa kwa kuwa serikali ndio iliyoidhamini mkopo huo.
"Hawa walitakiwa kila bajeti watoe mchanganuo wa deni la Sh58 bilioni ambalo serikali iliwadhamini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, lakini wameshindwa kufanya hivyo hali ambayo inawalazimu kuangalia namna watakavyweza kulilipa deni hilo," alisema Kilasi.
Hata hivyo kamati hiyo ilishangazwa na bodi hiyo kwa kutokuwa na mkurugenzi kwa muda wa miaka miwili. Nafasi hiyo inashikiliwa na kaimu mkurugenzi, Yusufu Kisare.
Kamati hiyo ilibaini kutokuwepo kwa mkurugenzi wakati wa utambulisho baada ya Kisare kujitambulisha kuwa anakaimu na alipoulizwa mwenye nafasi hiyo yuko wapi, alijibu kuwa alisimamishwa kazi na serikali tangu mwaka 2007
Kumekuwa na utata mkubwa katika swala la wanafunzi kupewa mikopo na serikali kupitia bodi ya mikopo, Je mnafikiri tatizo hili liko wapi katia ya watekelezaji na sera au sera zenyewe? Leo jioni tutatuma maoni mbali mbali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar-es-salaam UDSM wakiongelea juu ya mikopo kwa wanafunzi.

Friday, January 15, 2010

Pinda ataka ubunge usizidi miaka 15

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amependekeza kuwepo kwa ukomo wa nafasi ya ubunge kama ilivyo kwa nafasi ya urais na akapendekeza iwe ni miaka 15.

Aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano wake jana Dar es Salaam, kwamba hiyo itasaidia kupatikana kwa damu mpya katika uongozi, lakini akabainisha kuwa suala hilo ni gumu kwa baadhi ya wanasiasa.

“Ukiniuliza mimi, nitakwambia inafaa kuweka kipindi maalumu cha ubunge…hii itasaidia kuondoa vimaneno maneno na kutafutana uchawi. Viwepo vipindi maalumu kama ilivyo kwa urais. Nadhani miaka kumi na tano inatosha (vipindi vitatu),” alisema Pinda ambaye ni Mbunge wa Mpanda Mashariki mkoani Rukwa.

Kwa kauli yake, Pinda mwenye umri wa miaka 61, akifanikiwa kuteuliwa na chama chake, CCM na kuchaguliwa tena kuongoza jimbo hilo, atakuwa anamaliza miaka yake mitano ya mwisho aliyojiwekea baada ya kuingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2000.

“Nadhani baada ya miaka kumi na tano, itakuwa imetosha, na hata watu hawatakuparamia, watasema Mzee Pinda tumwache, hawatakupa taabu,” aliongeza Pinda, lakini akawa mwepesi wa kuonesha jinsi pendekezo lake lilivyo gumu kwa kueleza kuwa baadhi yao (wabunge), wangependa waendelee kuwemo katika Bunge.

“Sisi wenyewe ndio lazima tuone haja hiyo, sasa ugumu ni kwamba wengine tunaona tabu kutoka humo, tunataka kuendelea na ubunge tunauhitaji sana…uheshimiwa pekee ni hadhi. Lakini kwa kweli hili lingetusaidia sana. Lakini linahitaji busara. Tulitazame kwa maslahi mapana,” alisema Pinda.

Alisema Mkoa wa Rukwa umeonesha mfano baada ya wabunge wake wawili, Paul Kimiti (Sumbawanga Mjini) na Dk. Chrisant Mzindakaya (Kwela), kutangaza kutosimama tena katika uchaguzi ujao kutetea majimbo yao.

“Rukwa tumetoa mfano, kwa kweli nawapongeza sana wale wazee…na baada ya kutangaza tu wamejitokeza watu wengine, tena wengine maprofesa. Napenda kutoa mwito kwa wazee wengine walione hili, miaka kumi na tano inatosha. Ni busara zaidi,” alisema.

Awali, Pinda aliwachekesha wahariri baada ya kuuliza swali kugusiana suala la uzee, kiasi cha Waziri Mkuu kuhoji kuwa “kwa hiyo, na mimi unaniweka katika kundi hilo (la wazee)? Utakuwa unanionea.”

Alisema kinachoelezwa hapo ni ule utumishi wa muda mrefu katika umma na umri mkubwa, na si kwamba mtu amekaa ubunge kwa miaka mingi.

“Hapa naona wanazungumzia kipindi kirefu cha utumishi wa umma na umri mkubwa. Yaani wanakuona na kuuliza, yaani bado umo, umo tena. Hiyo ndiyo changamoto,” alisema.

Waziri Mkuu alirudi kauli yake aliyoitoa katika salamu za serikali kwenye maziko ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa zamani, hayati Rashidi Kawawa, Januari 2, mwaka huu, alipomsifu kwa kustaafu kwa hiyari ubunge baada ya miaka 27 na pia nyadhifa nyingine kwenye Chama Cha Mapinduzi.

Hivi karibuni, baada ya Kimiti na Mzindakaya kutangaza kutogombea ubunge, kumekuwa na mjadala wa kutaka wazee waliokaa muda mrefu bungeni na walioitumikia nchi kwa muda mrefu kuachia ngazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda mkoani Mara ambaye pia ni Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira, alisema hanyimwi usingizi na wanaojitokeza jimboni kwake kwa kuwa nafasi hiyo haina hati miliki.

Hata hivyo, alisema ni vyema wanaowania nafasi hizo wakajitangaza kwa kutumia masuala ya maendeleo badala ya kung’ang’ania kigezo cha uzee na ujana ambacho hakina umuhimu bungeni kwa kuwa chombo hicho kinatumiwa na wawakilishi wa wananchi bila kujali umri.

“Pale bungeni wapo wazee, vijana, walemavu na wazima, cha muhimu ni uwezo wao katika kuwakilisha wananchi wao na kujadili na kuweka mikakati ya kimaendeleo kwa faida ya Watanzania, hakuna sehemu iliyosema bungeni ni sehemu ya vijana,” alisema.

Pinda ataja mali zake, ana sh milioni 25 benki

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, jana alitaja mali anazomiliki ambazo miongoni mwake ni nyumba mbili pamoja na akaunti katika benki zenye fedha zisizozidi Sh milioni 25.

“Kama shilingi milioni ishirini na tano ni utajiri, basi nami nimo.” amesema Waziri Mkuu ofisini kwake, Magogoni, Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani ya nchi.

Pinda amesema, anamiliki nyumba moja mjini Dodoma na nyingine kwao Mpanda mkoani Rukwa eneo la Makanyagio, na ana kibanda shambani kwake Pugu nje kidogo ya Dar es Salaam.

“Mimi kila mwaka nataja mali zangu kwa Tume, sijaulizwa, sijagombana na Tume. Ukiniuliza ni masikini kiasi gani, nitakwambia nina property (nyumba) Dodoma, nimejenga kwa utaratibu wa serikali wa kuomba mkopo, ninayo nyingine kwetu Mpanda pale Makanyagio,” alisema Pinda.

“Dar es Salaam sina nyumba, pale Pugu nina nyumba kidogo, inahitaji kazi ya ziada…kijijini nilikuwa nafikia kwa babu, babu ana kanyumba kake ka ovyo ovyo…kile ambacho mlikiona, ana vyumba viwili nilikuwa nalala pale, lakini baada ya Uwaziri Mkuu, jamaa wakaniambia aah…haiwezekani pale, nilijua nitaweza kulala pale na hawa jamaa (wasaidizi wake) watalala mjini humo, nikaambiwa hapafai.”

Pinda ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mashariki alisema hana gari lolote zaidi ya gari alilopewa kwa kuwa Mbunge, na kwamba katika akaunti zake zote, ana fedha kiasi cha Sh milioni 22 hadi 25.

“Akaunti zangu zote jumla yake haizidi shilingi milioni ishirini na tano…basi kama shilingi milioni ishirini na tano ni utajiri, basi nami nimo,” alisema Pinda na kusababisha wahariri hao waangue kicheko.

Lakini kubwa Pinda alisema kwamba kwa jinsi serikali inavyowajali watu wanaoshika wadhifa kama wake, haoni ni kwa nini awe na tamaa ya fedha na mali, kwa sababu serikali inamjali kwa kumtunza kwa kila kitu.

“Kwa utaratibu wa serikali, unapewa nyumba, magari, unalishwa na serikali…kwa mshahara wake unaweka akiba ya

kutosha, unataka utajiri wa nini? Maisha yako ni mazuri, unataka nini zaidi ya hapo? Ukitoka nje ya utumishi wa serikali, akiba yako inakusaidia kusomesha watoto wako,” alifafanua Waziri Mkuu.

Alisema hana sababu ya kuwa na tamaa na jukumu lake kubwa aliloomba kwa Mwenyezi Mungu ni kumpa uwezo wa kuwatumikia Watanzania vizuri zaidi.

“Sina hisa popote, labda huko mbele ya safari nitafikiria. Yaani ukiwa Waziri Mkuu ndio mwanya wa kujinufaisha, kwa nini? Labda mimi watu wanaweza kusema Waziri Mkuu wa sasa ni mjinga,” aliongeza Pinda.

Akizungumzia utendaji wa serikali yake, kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali, alisema anaridhika na utendaji huo kwa yale yote yanayokubaliwa katika Baraza la Mawaziri yanatekelezwa ipasavyo.

“Naridhika kwamba yale yote tunayokubaliana katika Baraza la Mawaziri yanatekelezwa ipasavyo, kwa pamoja. Tunakwenda vizuri, si mbaya. Lakini kama watu wanasema kuhusu utendaji wetu, ni mzuri, watuhukumu vizuri,” alisema.

Pinda amesema, Rais aliyemteua ndiye atakayeamua kama amteue tena baada ya Uchaguzi Mkuu.

Thursday, January 14, 2010

Mafisadi kutoswa kumuokoa Kikwete

MKAKATI wa kuwajibishana katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za baadhi ya vigogo kuunda mitandao ya kisiasa, kuhusika na vitendo vya ufisadi na wengine kutoa matamko makali nje ya vikao vya chama hicho, imekamilika na wakati wowote utekelezaji utafanyika Raia Mwema limeelezwa.

Mambo mawili makubwa yanatarajiwa kujitokeza ndani ya chama hicho. Mosi, vigogo watuhumiwa wa ufisadi kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria. Pili, wenye kutoa kauli kali nje ya vikao vya chama hicho, wakiwamo baadhi ya wabunge watapewa onyo na kutakiwa kuwa makini.

Tayari mkakati huo umeanza kupata upinzani miongoni mwa watu ndani ya CCM na hata baadhi ya wajumbe wa Sekretariati ya chama hicho, ambayo Mwenyekiti wake ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Mbali na katibu Mkuu wa CCM, sekretarieti hiyo inaundwa na manaibu katibu wakuu wa CCM, ambao ni Saleh Ramadhan Feruzi (Zanzibar) na George Mkuchika (Bara), katibu wa NEC Taifa wa Organaizesheni, Kidawa Yusuf Himid, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Uchumi na Fedha, Amos Makala.

Majukumu ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na kusimamia shughuli zote za utendaji za CCM kitaifa na kuandaa shughuli za vikao vya chama hicho ngazi ya Taifa.

Kwa mujibu wa habari zilizotufikia, katika kikao cha sektretariati hiyo kilichoketi Dar es Salaam hivi karibuni, sehemu kubwa ya wajumbe wake wanaunga mkono chama kuwawajibisha watuhumiwa wenye kashfa za ufisadi wakiwamo wanachama wake ambao wanaelekea kuwa mzigo baada ya kuchukuliwa hatua na vyombo vingine.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa katika kikao hicho ambacho pia kimepanga Kamati Kuu ya CCM, kukutana Januari 23, mwaka huu na NEC kukutana kwa siku mbili, Januari 25 na 26, mjini Dodoma, ni mjumbe mmoja tu aliyeonekana kuwakingia kifua watuhumiwa wa ufisadi ambao kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa kufaidika nao, lakini upingaji wake haukuweza kubadili misimamo ya wajumbe wenzake walio wengi.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo, inaelezwa kuwa vigogo wa juu serikalini wamekuwa wakiunga mkono uamuzi huo unaotarajiwa kufanywa na chama hicho na baadhi wakiwa tayari kukumbatia lawama za kiuongozi ikiwa ni hatua ya kumtenganisha Rais Kikwete na chuki zinazoweza kuibuka kutokana na kile kinachoweza kuitwa “uamuzi mgumu”.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa hali ya kujadiliwa kwa watuhumiwa wa ufisadi wakitajwa kuwa na mikakati yao binafsi ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikikisumbua chama hicho imewakera na kuwachosha viongozi wengi waadilifu serikalini na baadhi wakihoji; “wao (kwa majina) ni kina nani kwenye hii nchi hadi wawanyime watu usingizi?”

Vyanzo vyetu vya habari vilivyo karibu na viongozi waandamizi nchini vimedokeza kuwa hatua hiyo inachukuliwa ili kukisafisha CCM mbele ya majukwaa ya kampeni baadaye mwaka huu.

Mwelekeo huo wa kufikia “maamuzi magumu” unatajwa kuhusishwa na kile kinachotarajiwa kujitokeza katika ripoti ya Kamati ya Rais mstaafu, Ali HAssan Mwinyi, itakayowasilishwa kwenye kikao kijacho cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM.

Kamati ya Mwinyi inayowashirikisha Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdulrahman Kinana, iliundwa na NEC katika kikao chake kilichopita mjini Dodoma ili kutoa mapendekezo ya kumaliza kile kilichotajwa kuwa uhasama miongoni mwa wabunge wa chama hicho pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliowahi kupishana kauli na viongozi wa juu wa Serikali ya Muungano.

Tayari imekwisha kuripotiwa kuwapo kwa hali ya mgongano wa kimtazamo miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo katika uandaaji taarifa na kwamba kutokana na mgongano huo, wajumbe wa kamati wanaandaa ripoti tofauti watakazowasilisha kwenye Sekretarieti ya CCM.

Hali halisi ya mwelekeo wa CCM katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, inatajwa kuwa tete zaidi endapo chama hicho hakitafanya uamuzi wowote uliopachikwa jina la “uamuzi mgumu” wa kujitenga na watuhumiwa wa vitendo vya ufisadi, ambao tayari wamewajibika serikalini.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM wanahusishwa na matukio makubwa ya ufisadi, yakiwamo wizi wa mabilioni ya fedha kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na baadhi yao tayari wakiwa wamefikishwa mahakamani na kesi zikiendelea, akiwamo Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM, mkoani Kigoma, Rajabu Maranda.

Mbali na vigogo hao chama hicho kinadaiwa pia ya kuwa kimekuwa kikichangiwa fedha za uchaguzi na baadhi ya wafanyabiashara wanaohusishwa na vitendo vya ufisadi nchini, ambao pia baadhi wamefikishwa mahakamani.

Tayari pia hali ya kuwapo mpasuko imebainika si tu miongoni mwa wabunge pekee bali hata miongoni mwa viongozi serikalini na hasa mawaziri.

Mwishoni mwa mwaka jana, Kamati ya Mwinyi iliwahi kuripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa imeanza kuparaganyika, ikielezwa kuwa sehemu ya mapendekezo katika taarifa yake ya pamoja kwa ajili ya kuwasilishwa NEC-CCM imevuja.

Katika habari hizo ilielezwa kuwa baadhi ya viongozi CCM wamedokezwa kuhusu mapendekezo ya kamati hiyo, yaliyodaiwa kuwa ni pamoja na kuwang’oa madarakani baadhi ya watuhumiwa.

Kutokana na mapendekezo hayo ya kung’oana, baadhi ya vigogo wanatajwa kuwa na mwelekeo wa kupingana na kamati kwa madai kuwa hiyo ni hatua kali, bila kujali kuwa wanaotakiwa kuachia madaraka ili wabaki wanachama wa kawaida walikwishafanya hivyo kwa kuacha nyadhifa zao serikalini.

Monday, January 11, 2010

Wasichana 6,000 wanaacha shule kila mwaka

WASTANI wa wanafunzi wa kike 5,720 nchini wanaacha shule kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonesha kuwa, tangu mwaka 2004 hadi 2008, wanafunzi wa kike 28,600 wameshindwa kuendelea na masomo huku sababu nyinginezo ikiwa ni utoro na vifo.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Selestine Gesimba, amesema, kati ya idadi hiyo ya walioshindwa kuendelea na masomo, 17,000 ni wanafunzi wa shule za msingi na 11,600 ni wa sekondari.

Tatizo kubwa linalotajwa kuchangia wanafunzi hao wa kike kutomaliza masomo, linadaiwa kuwa ni utoro.

Kwa upande wa mimba, Gesimba, amesema, takwimu zinaonesha idadi ya wanafunzi walioacha shule kutokana na mimba haizidi wastani wa asilimia saba kwa mwaka.

Amesema, takwimu za mwaka 2007 zinaonesha Mkoa wa Mtwara unaongoza kwa kuwa na wanafunzi 435 walioacha shule kutokana na ujauzito.

Mikoa inayofuatia na idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito katika mabano ni Mwanza (308), Tanga (290), Pwani (280), Rukwa (265), Ruvuma (204), Lindi (144), Shinyanga (137), Dodoma (111) na Mbeya wanafunzi 105.

Kwa mujibu wa toleo jipya la Sera ya Elimu na Mafunzo 2009, waliopata ujauzito katika ngazi ya elimu ya msingi mwaka 2007 ni asilimia 0.3 na upande wa sekondari ya kawaida ni asilimia 0.6.

Gesimba alisema miongoni mwa njia za kukabili mimba kwa wanafunzi ni pamoja na kujenga hosteli kwa watoto wa kike.

Kuhusu utoro, mtendaji huyo alitaja kuwa unachangiwa na ukosefu wa lishe shuleni hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Ingawa Gesemba alisema wizara haijafanya utafiti unaojitegemea kubaini hali halisi ya wanafunzi kuozwa kabla ya kumaliza masomo, hilo pia ni tatizo ambalo limekuwa likiyakumba hususan maeneo ya vijijini.

“Bado hatujawa na utafiti wa kubaini kiwango cha ndoa za utotoni kinavyochangia tatizo.

Haya mambo mara nyingi yanafanyika kwa kificho, inategemea na uzalendo wa watu ambao huamua kufichua kwamba mtoto fulani kaachishwa shule kwa ajili ya kwenda kuolewa,” alisema Naibu Katibu Mkuu, Gesimba.

Tathmini ya miaka minane ya ripoti ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) ya mwaka 2000 hadi 2008, imeainisha kuwa mimba na ndoa za utotoni ni matatizo yanayoendelea kuchangia watoto wa kike kutomaliza masomo vijijini na mijini.

Kuendelea kuwepo wanafunzi wanaoacha masomo kutokana na sababu mbalimbali, kunaipa serikali changamoto kubwa ikizingatiwa wafadhili wa elimu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kwa kuhimiza usawa wa kijinsia katika elimu.

Serikali ya Uholanzi ni miongoni mwa nchi wafadhili ambazo Balozi wake, Ad Akoekkoek alikaririwa hivi karibuni na moja ya tovuti akihimiza umuhimu wa kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika elimu nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa MDGs. Hata hivyo, serikali imekuwa katika mikakati ya kuwezesha elimu kwa wasichana.

Tathmini ya ripoti ya MDGs inaonesha kwamba serikali imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2015, hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi anayekatiza masomo.

Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2009 pia inaainisha umuhimu wa kuwepo marekebisho ili kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi zote za elimu na mafunzo ikizingatiwa kwamba ushiriki wa wasichana ngazi ya elimu ya sekondari kwenda ngazi ya juu ni mdogo ikilinganisha na wavulana.

Sera inaelekeza kuweka utaratibu wa kuwabaini na kuchukua hatua dhidi ya watu watakaosababisha wanafunzi wa kike kukatisha masomo yao kwa sababu yoyote ile; iwe utoro, kufanyishwa kazi ngumu na ujauzito.

Friday, January 8, 2010

Manji, Jeetu Patel waichezea Serikali


-Wachelewesha matrekta ya 'Kilimo Kwanza'

MRADI wa matrekta kwa ajili ya mpango wa uboreshaji wa kilimo nchini-Kilimo Kwanza- umekwama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni mgogoro kati ya wafanyabiashara wawili nchini, Yussuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel (Jeetu Patel), Raia Mwema limebaini.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba mvutano kati ya Jeetu na Manji, umechangia kwa kiasi kikubwa kuchelewa kwa mchakato wa upatikanaji wa matrekta hayo kwa ajili ya mradi wa Kilimo Kwanza, mradi wenye thamani ya Sh bilioni 50.

Habari zinaeleza kwamba, kwa kutumia mtandao wa mmoja wa wafanyabiashara hao, baadhi ya maofisa wa Serikali wametumika kuuchelewesha na hivyo kuhujumu mchakato wa kukamilishwa kwa taratibu za uidhinishwaji wa fedha za ununuzi wa matrekta hayo.

Mradi huo uliokabidhiwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia kampuni yake ya SUMA JKT, ulitakiwa kuanza mapema mwaka huu, lakini hauna dalili za kuanza kutokana na utata wa kisheria ulioilazimu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuingilia kati.

Raia Mwema imethibitishiwa kwamba kampuni mbili za nchini India zilizoshiriki zabuni hiyo moja ikiwa imepata sehemu kubwa ya kazi ya kuingiza matrekta hayo, zimeridhishwa na mchakato wa zabuni hizo, lakini tatizo limekuwa kwa mawakala wao nchini ambao ni Manji na Jeetu.

Malumbano hayo yameelezwa kuwagusa hata watendaji wa juu serikalini kabla ya uongozi wa juu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuingilia kati na kuamuru suala hilo likamilishwe na taarifa ziwasilishwe Wizara ya Fedha na Uchumi.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Kijjah, ameliambia Raia Mwema kwamba Wizara yake haikuhusika kwa namna yoyote na ucheleweshaji wa mchakato wa Kilimo Kwanza kwa maelezo kwamba kilichochelewesha ni ushauri wa kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, jambo ambalo amesema sasa limeshapatiwa ufumbuzi.

“Hakukuwa na tatizo la kiuhasibu ama kiuchumi. Lilikuwa ni tatizo la kisheria ambalo sisi hatuhusiki. Watu wa Exim Bank ambao ndio watoaji wa mkopo walitaka maoni ya kisheria kutoka serikalini na sisi tulilazimika kuwapelekea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa sasa ndiyo wametuletea na tumewapelekea Exim, wakishapitia watatujulisha kama wameridhika ama la,” alisema Kijjah.

Kijjah alisema fedha hizo ni mkopo kutoka serikali ya India kupitia Exim Bank, japo ni kwa riba nafuu mno kuliko ile ya taasisi nyingine za fedha na kwamba utalipwa na Watanzania wote wakati wake ukifika na hivyo ni lazima Serikali ijiridhishe na kila hatua kuhusiana na matumizi yake.

Kumekuwa na maoni tofauti kuhusiana na jinsi Serikali ilivyolibeba suala la ununuzi wa matrekta hayo kutokana na kuhusishwa tena kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakihusishwa katika kashfa mbalimbali ikiwamo kashfa maarufu ya wizi wa Fedha za Mfuko wa Madeni ya Nje Benki Kuu ya Tanzania (EPA).

Mwishoni mwa mwaka jana baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu Manji akizungumzia kwa kina kuhusiana na zabuni hiyo ya matrekta ya Kilimo Kwanza, lakini Jeetu Patel amekuwa kimya kuhusiana na suala hilo akikwepa kuhusishwa nalo.

Raia Mwema ilipomuuliza Jeetu Patel kuhusiana na suala hilo alikataa kata kata kulifahamu akidai kwamba hajawahi kuhusika kwa vyovyote katika zabuni hiyo na hana cha kuzungumza akisema, “sifahamu lolote kuhusu biashara hiyo… sina cha kuzungumza, ama unataka nikudanganye?”

Kwa upande wake Manji alitoa taarifa akidai kutoridhishwa kwake na mchakato wa zabuni hiyo ambayo imeelezwa kwamba tatizo kubwa lilikuwa ni “kuzidiana kete” kati ya wafanyabiashara hao wa Tanzania, katika kamisheni ambayo ingetokana na biashara hiyo kutoka kampuni za nchini India.

Katika mradi huo, Jeetu anatajwa kuwa mwakilishi wa Kampuni ya Escort hapa nchini, yenye makao makuu yake nchini India, ambayo imeshinda zabuni hiyo, wakati Manji anatajwa kuwakilisha kampuni ya Mahindra ya India, ambayo nayo imepata kiasi kidogo cha zabuni hiyo.

Hata hivyo, baadaye Manji ambaye ni mmiliki kampuni ya Quality Group, alinukuliwa na gazeti la serikali la Habari Leo akisema kwamba ameridhishwa na mchakato wa zabuni hiyo na kukanusha taarifa za awali kwamba amekuwa akitaka kuanika anachofahamu kitakacholenga kuchafua wahusika katika zabuni hiyo ikiwamo JKT.

Awali ilielezwa kwamba zabuni hiyo ya matrekta ilipitishwa ngazi zote ikiwamo hatua ya Baraza la Mawaziri na kupatiwa baraka zote za kulitekeleza na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk. Hussein Mwinyi, alinukuliwa akisema kwamba hakuna utata wowote katika utekelezaji wa mradi huo, isipokuwa linaweza kufanywa ajenda ya kuchafuana na watu ambao wana malengo binafsi na mradi huo.

Dk. Mwinyi alinukuliwa akisema kwamba kampuni zaidi ya 10 ziliomba zabuni hiyo na hatua zote zilipitiwa kwa uangalifu mkubwa na kwamba watakaolalamika wanalenga kuchafuana kwa malengo binafsi.

Wednesday, January 6, 2010

Seif, Karume waitibua CCM

-Yadaiwa wamekwenda kinyume cha maagizo ya NEC Butiama
-CUF: Ni uoga wa vigogo CCM

MARIDHIANO ya Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad yamewachanganya wana Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hasa wa Zanzibar, wanaoona kuwa ni mbinu ama ya kuendeleza utawala wa Karume au kumlinda kama ikilazimu Seif ndiye akawa mkuu wa nchi, Raia Mwema imeambiwa.

Tayari vigogo kadhaa wa CCM Zanzibar wameanza kuamini kuwa maridhiano hayo yanaweza kuhitimishwa kwa Rais Karume, kuwania tena urais wa Zanzibar, baada ya Katiba ya Visiwa hivyo kufanyiwa mabadiliko mahsusi.

Aidha, vigogo hao ambao wengine wangetamani kumrithi Karume, wanayatazama maridhiano hayo kwa hadhari kubwa, wakiamini kuwa yanakwenda kinyume cha maelekezo ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) iliyokutana kijijini Butiama, mwishoni mwa mwaka jana.

Katika kikao hicho cha NEC iliazimiwa kuwa Serikali ya mseto iundwe baada ya kufanyika kwa kura ya maoni Zanzibar (referendum), ambayo yatakuwa chanzo cha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.

Hata hivyo, baada ya kikao hicho CUF walipinga wakisema hapakuwa na haja ya kura za maoni na kwamba mabadiliko ya Katiba yamekuwa yakifanyika kila inapobidi kwa kuzingatia hali halisi na mahitaji ya nchi kwa wakati husika.

Kutokana na msuguano huo, CUF walikataa kuendelea na mazungumzo ya muafaka wakitaka utekelezaji lakini CCM, akiwamo Rais Jakaya Kikwete walitoa wito wakitaka warejee kwenye meza ya mazungumzo.

Lakini upepo umegeuka wiki kadhaa zilizopita, baada ya Rais Karume na Seif kukutana katika kikao kisicho rasmi lakini kilichoonekana kuwa na nguvu kuliko hata vikao vilivyokuwa na nguvu za kisheria.

Katika kikao hicho kulifikiwa maridhiano ambayo matokeo yake ni pamoja na CUF kutambua urais wa Karume, na yeye kuwateua baadhi ya viongozi wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwamo Juma Duni Haji.

Wakati hayo yote yakitokea mtafaruku umeibuka CCM Zanzibar, Karume na Seif wakitajwa kuwa na ajenda zenye malengo ya kuwanufaisha kama timu mpya ya watu wawili, iliyolenga kubeba siasa za Visiwa hivyo.

Wao wenyewe wamekuwa wakinukuliwa kusema kwamba kwa hali ya siasa zilivyo tete Zanzibar wanaona kwamba bila hatua kama hii uchaguzi wa mwakani unaweza kuzua machafuko makubwa ambayo yataweza kusababisha hata damu kumwagika.

Kwa hali hiyo wamedai kwamba wao kama viongozi hawawezi kuruhusu hayo yatokee na hivyo wameingia katika maridhiano kuepuka wao kama watu binafsi kushitakiwa baadaye katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, Uholanzi kwa kusababisha maafa.

Kwa nyakati tofauti, vigogo ndani ya CCM wameieleza Raia Mwema kuwa kuna uwezekano wa kutaka kuunda serikali ya mseto Zanzibar, ndoto ambayo haiwezi kutimia hadi Katiba ibadilishwe na mabadiliko hayo yatahitaji muda jambo ambalo litalazimu Rais Karume kubaki madarakani mwakani, hadi uchaguzi ufanyike, hoja ambayo inaelezwa pia kubeba ajenda ya viongozi hao wa vyama pinzani.

Hoja nyingine inayochomoza ni kwamba mkewe Rais Karume, Shadya ana Upemba kiasi kwa kuwa mama yake ana asili ya Pemba, ikibidi Seif kuibuka kuwa kiongozi mkuu wa Zanzibar, familia ya Karume, ambaye inadaiwa sasa ana mali nyingi zinazomfanya abandikwe jina la Hapa Pangu itazidi kuwa katika neema endapo itafanikisha ushindi wa Maalimu Seif Shariff Hamad, kuwa Rais ajaye wa Zanzibar, ikidaiwa na vigogo hao kuwa hayo ni sehemu ya makubaliano yao ya siri.

Kama si Maalim Seif, vigogo hao wameieleza Raia Mwema kuwa mabadiliko ya Katiba mahsusi kuruhusu serikali ya mseto, yanaweza kumbakisha kwa muda Karume na baada ya baadhi ya vipengele kumruhusu agombee kwa mujibu wa Katiba hiyo mpya au yenye mabadiliko, na ikiwa hivyo naye pia atalinda maslahi ya Maalim Seif, kwa hoja ya mwingiliano wa asili ya familia (kutoka Pemba).

Lakini duru huru za habari zimedokeza kuwa msingi wa Rais Karume na Seif kuridhiana katika wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni kuhofia machafuko na vifo na hivyo kuepusha mashitaka ya mauaji, kama ilivyo kwa Omar Bashiri wa Sudan, anayewindwa kufikishwa mahakamani The Hague kwa makosa anayodaiwa kuruhusu ukiukwaji wa haki za binadamu Darfur.

Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya vigogo wa CCM Zanzibar, Raia Mwema iliwasiliana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kujua maazimio ya NEC iliyokutana Butiama kuhusu kura ya maoni yamefutika vipi na jambo gani hasa linaloendelea kwa kuzingatia mwongozo wa CCM kama chama kwenda kwa Rais Karume.

Lakini Makamba alisema yupo likizo na akapendekeza Raia Mwema imtafute Naibu Katibu Mkuu George Mkuchika ambaye hata hivyo alikataa kuweka bayana hali halisi ya mambo.

Soma zaidi