Tuesday, July 31, 2012

Zitto ahojiwa kwa rushwa

SAKATA la wabunge kuhusishwa na rushwa limeingia sura mpya, baada ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe kuhojiwa na chama chake cha Chadema kwa saa tatu jana.
Wakati Zitto akihojiwa, kambi rasmi ya upinzani bungeni, iliwataja wabunge saba wa CCM na kueleza kuwa ndiyo wanaolichafua Bunge kwa kujihusisha na mambo yenye maslahi binafsi wakiwa watumishi wa umma.

Kadhalika, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) ilikuwa ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge kuhusu tuhuma za rushwa na kwamba uchunguzi ukikamilika taarifa zitawekwa wazi.

Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, jana aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Tweeter kwamba alihojiwa na Sekretarieti ya chama chake kutokana na tuhuma za rushwa zinazowagusa badhi ya wabunge.
Katika maelezo yake, Zitto alisema aliiambia sekretarieti ya chama hicho kwamba Chadema kifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa suala hilo na kwamba yuko tayari kuwajibika ikiwa itathibitika kwamba alihusika kula rushwa.

“Kwa saa tatu nimejieleza mbele ya sekretariati ya chama kuhusu tuhuma za rushwa dhidi yangu. Niliomba kutaka kutoa maelezo kwa Katibu Mkuu, nimekiomba chama kufanya uchunguzi na ikibainika hatua zichukuliwe,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo kwenye Tweeter.

Lissu ataja wengine
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu aliwataja wabunge wa CCM ambao wanatuhumiwa kuwa ni Nasir Abdallah (Korogwe Mjini), Mariam Kisangi (Viti Maalumu), Vicky Kamata (Viti Maalumu) na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) ambao hata hivyo, wote wamekanusha madai hayo.

Wabunge wengine watatu tumeshindwa kuwataja kwa kuwa hawakupatikana kuzungumzia tuhuma dhidi yao.

Katika orodha hiyo wamo wawili wa Viti Maalumu na mmoja wa jimbo na Lissu alidai kwamba wamekuwa wakishiriki vikao vya Kamati ya Nishati na Madini huku wakijua kuwa wana maslahi binafsi na wengine kutumia fursa hiyo kujinufaisha.
“Kwa takriban juma moja sasa kumekuwa na mjadala mzito wa ufisadi hapa bungeni, sasa Kambi Rasmi ya Upinzani imejitathmini na kuona kwamba wabunge wake hasa walioko kwenye Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa, John Mnyika, David Silinde na Mwanamrisho Abama hawahusiki,” alisema Lissu na kuendelea:

“Ila uchunguzi wetu umefanikiwa kupata majina ya wabunge wanaohusika moja kwa moja na mgongano wa kimaslahi ambao tunaona tuwataje kwa maslahi ya umma.”
Lissu alikwenda mbali zaidi na kutaja tuhuma zinazowahusu wabunge hao akisema wawili ambao gazeti hili halikuwaja, wamejihusisha kufanya biashara na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hivyo wana mgongano wa kimaslahi.

Alisema Mwijage ana mgongano wa kimaslahi katika mchakato mzima wa kuipa zabuni ya kusambaza mafuta kampuni ya Puma Energy kwa kuwa yeye ni mtalaamu mwelekezi wa kampuni hiyo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 50.
“Nasir Abdalah na Mariam Kisangi; Hawa wanamiliki vituo vya mafuta. Sasa kwa namna yeyote ile kuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini hawawezi kutenda haki katika mchakato wowote unaohusu suala la mafuta,” alisema na kuendelea;

"....(jina limehifadhiwa) hana mgongano wa moja kwa moja wa maslahi, lakini kwa kadri tunavyofahamu, yeye ndiye aliyekuwa akiyafanyia kampeni ya kupata zabuni makampuni ya mafuta ya Oryx na Camel na ....(jina limehifadhiwa), suala lake ni complicated kidogo. Maslahi aliyonayo katika suala hilo ni kuwa ana uhusiano wa Kimapenzi na kigogo mmoja katika Wizara ya Nishati na Madini.”

“Hawa ndiyo wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini ambao sisi Kambi ya Upinzani tunawafahamu kuwa ndiyo waliojihusisha na mgongano wa kimaslahi. Tumewaangalia wabunge wetu wote watatu hawamo ila kama kuna mtu ana taarifa zinazowahusu, aseme na tutazifanyia kazi.”

Lissu alisema kitendo cha wabunge kujihusisha na mgongano wa kimaslahi na taasisi za umma ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 na ni kinyume na maadili ya kibunge.
Katika hatua nyingine Lissu amemshauri Spika wa Bunge Anne Makinda kuzivunja pia kamati za Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) akisema nazo zina madudu mengi.

“Hili lisiishie tu kwa kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, tunataka pia kamati za POAC na LAAC zivunjwe, uchunguzi ufanyike na wahusika waitwe kujitetea na hatimaye wenye hatia watajwe hadharani bungeni na majina yao yachapishwe kwenye magazeti ili haki itendeke,” alisema.

Alipoulizwa Chadema imefanya nini dhidi ya Mbunge wake, Zitto Kabwe kutajwa katika orodha hiyo, alijibu: “Nikiri kwamba sisi taarifa tunazo ila hatujamwita kumwuliza. Naomba ieleweke kwamba kama chama au Kambi Rasmi ya Upinzani hatuna maslahi na mbunge yeyote anayeonekana kujihusisha na masuala hayo.”
“Katika hili tunaomba uchunguzi ufanyike na matokeo yake yatangazwe ili tupate msingi wa tuhuma hizo na ninaahidi kwamba tutazifanyia kazi ipasavyo.”

Majibu ya tuhuma
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Kisangi alikiri kumiliki kituo cha mafuta lakini akasema sheria haimzuii mtu kama mambo yake anayafanya kwa uwazi.

“Nimekuja bungeni nikitokea kwenye ualimu, nilikuwa nafundisha Shule ya Msingi ya Mianzini na biashara hii ni ya familia. Inaendeshwa kwa uwazi na mwanangu wa kwanza ndiye anayeisimamia. Kutokana na uwazi katika shughuli zangu, mwaka jana Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilinipongeza. Mimi ni msafi na siko huko wanakofikiri wao (Chadema).”

Kwa upande wake, Mwijage alikanusha kuwa mtaalamu mwelekezi wa Kampuni ya Puma, badala yake akasema ni mtaalamu wa petroli anayefanya kazi ya kuishauri Serikali kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu nishati hiyo.

"Siyo kweli, hawa wanadandia hoja. Mimi ni mtaalamu wa petroli ambaye mchango wangu kimsingi una faida kubwa bungeni na hata kwa jamii kwa ujumla. Sijafanya maamuzi yeyote ya kulihujumu taifa hili na hata kwenye Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini pekee, nilitoa mchango wa kurasa 10 kuhusu masuala hayo ya petroli,” alisema

Aliishauri kambi hiyo ya upinzani kuvuta subira, akieleza kuwa jambo lililoko bungeni linahusu ufisadi na uhujumu uchumi hivyo kauli zinazotolewa bila utafiti zinaweza kuvuruga mchakato mzima uliokwishaanzwa na Kamati ya Maadili ya Bunge.

Awali, Abdallah alipoulizwa kuhusu tuhuma za kumiliki vituo vya mafuta hivyo kuwa na maslahi binafsi, alicheka na kuahidi kwamba angepiga simu baadaye, lakini hakufanya hivyo na alipopigiwa baadaye alikata simu. Hata hivyo, alizungumza na waandishi wa habari na kukanusha kumiliki vituo vya mafuta.

Kamata kwa upande wake alisema: “Kuna kamati maalumu imepewa kazi ya kuchunguza mambo hayo, hivyo yote yanayoulizwa yatakuwa wazi na ukweli utajulikana tu. Nina maslahi au sina ukweli mtaujua, haraka ya nini?.

Mjadala Bungeni
Mjadala huo wa wabunge kuhusishwa na mgongano wa kimaslahi ulianza kulipuka bungeni jana asubuhi baada ya wabunge watatu; Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Salum Barwany (Lindi Mjini) na Mbunge wa Nkasi Kaskazni, Ali Kessy kutaka wabunge wanaotuhumiwa kwa ufisadi watajwe bungeni ili kuisafisha taasisi hiyo ya kutunga sheria.

"Mheshimiwa Naibu Spika juma lililopita Mheshimwa (Vita) Kawawa alitoa hoja kutaka suala la ufisadi lishughulikiwe kwa kuvunjwa Kamati ya Madini na Spika akaridhia na kulipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Maadili. Kwa nini Kamati nyingine zilizohusishwa na ufisadi huo nazo zisivunjwe?” alihoji Nassari na kuendelea:

“Kuna Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) inayoongozwa na Mheshimiwa Mrema na Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) inayoongozwa na Zitto. Kuna tabia ya wabunge kuzikimbia kamati zisizokuwa na mikataba kama Kamati ya Huduma za Jamii na wanazikimbilia kamati zenye mikataba.”

Barwany alitaka Bunge litajiwe majina ya wabunge waliotuhumiwa kwenye kashfa hiyo mpaka wakapelekwa kwenye Kamati ya Maadili, akieleza kuwa hili litasaidia kulisafisha... “Tumeambiwa Kamati ya Maadili inajadili suala hilo, lakini hatujatajiwa ni wabunge gani waliopelekwa huko, tunaomba mtutajie ili Bunge lijisafishe.”

“Mimi naungana na wazo la Barwany na Nassari. Majina yatajwe wabunge tunadhalilishwa na wananchi huko mitaani. tuwataje hadharani,’ alisema Kessy.

Akitoa mwongozo wa hoja hiyo, Ndugai aliiagiza Kamati ya Uongozi ya Bunge kutoka kwenye ukumbi wa Bunge ili wakajadili suala hilo na baadaye apelekewe taarifa.
“Naamini wenyeviti wote wa kamati mmo humu ndani, naomba sasa hivi mwende kwenye Ukumbi wa Spika mkajadili suala hilo halafu nipate majibu sasa hivi,” alisema.

Baadaye jioni, Ndugai alisema kuwa Spika hawezi kuwataja kwa majina wabunge ambao wanajihusisha na rushwa kwa kuwa hawajui.

Alisema Kamati ya Uongozi iliyokutana jana mchana ilikubaliana kuwa ufanyike uchunguzi wa kina kwa ajili ya kuwabaini wale wanaoshukiwa na kwamba ikibainika Bunge litawaanika hadharani.

“Kamati imerejea kumbukumbu za hansard ya Jumamosi kuwa ufanyike uchunguzi wa kina juu ya jambo hilo na wabunge mtaitwa kwa ajili ya kutoa ushirikiano, ikumbukwe kuwa mbunge akiitwa siyo kwamba ndiyo amekuwa mtuhumiwa, bali pale itakapothibitika majina yatawekwa hadharani,’’ alisema Ndugai.
Naibu Spika alitahadharisha kuwa ndani ya Kamati hiyo utafanyika uchunguzi wa kutosha kubaini kama kuna mjumbe mwenye maslahi kwa wale wahusika basi ataondolewa ili kutoa nafasi kwa kamati kufanya kazi yake ipasavyo.

Aliwatahadharisha wabunge kuwa Kamati hiyo haitaingilia utaratibu wa vyombo vya dola ambao wamekuwa wakiufanya ikiwemo wa Takukuru wa kuwahoji baadhi ya wabunge.

Monday, July 30, 2012

Maganzo: Mji wenye utajiri wa almasi usio na huduma ya maji

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Masagala nje kidogo ya Mji mdogo wa Maganzo akitoka kuchota maji bwawani bwawa hili lilichimbwa na mkandarasi huyo.
Binti akichota maji katika moja ya mabwawa ambayo si salama kwa matumizi anuai bwawa hili lilichibwa na mkandarasi aliyekuwa akitengeneza barabara.
Mabinti wakitoka kusaka maji kwa matumizi anuai.

Na Joachim Mushi, Kishapu

KWA mtazamo wa kawaida ni kitendo cha kawaida kwa mji wowote kuendelea kutokana na rasilimali zake zinaouzunguka mji huo. Maeneo mengi nje ya nchi na hata Tanzania yamekuwa yakipata maendeleo ya jamii na mazingira yake kutokana na rasilimali na shughuli za kijamii zinazolizunguka eneo lenyewe.

Hali hii ni tofauti na ilivyo katika Mji mdogo wa Maganzo uliopo wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, ambao umefanikiwa kuwa na rasilimali ghali yenye thamani kubwa ulimwenguni. Mji huu una madini ya almasi yanayopatikana karibia sehemu kubwa ya eneo la Maganzo.

Kihistoria Mji wa Maganzo unachimbwa madini ya almasi tangu kitambo kidogo. Wananchi wanachimba madini hayo katika mashamba, viwanja na maeneo mengine ambayo yanaaminika kuwa na almasi. Huu ni utajiri mkubwa ambao Mji mdogo wa Maganzo umefanikiwa kuwa nao.

Baadhi ya wananchi wamefanikiwa kunufaika na utajiri huu. Nasema hivyo maana ukifika katika eneo hilo utashuhudia nyumba za thamani na za kisasa na hata magari ya kifahari ambayo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameyapata kutokana na almasi.

Mji huo unahuduma ya umeme, afya (japokuwa kunachangamoto kadhaa), mawasiliano (mtandao wa simu) na pia umefanikiwa kupitiwa na barabara kuu ya lami inayotoka Shinyanga mjini kuelekea Mkoa wa Mwanza. Kwa kiasi fulani mji unavutia.

Wapo wawekezaji kadhaa wa madini akiwemo Kampuni ya Williamson Diamonds ambayo licha ya kumiliki eneo kubwa la machimbo ya almasi inamiliki maeneo mengine kadhaa ya ndani ya mji huo. Wachimbaji hawa wanaendesha shughuli za uchimbaji madini eneo hilo.

Lakini pamoja na rasilimali hii ya Mji Mdogo wa Maganzo hauna huduma ya maji safi na salama ya uhakika. Mji mzima hauna maji ya bomba na badala yake hutegemea maji ya kuletwa kwa madumu kwa baiskeli kutoka mjini Mwadui ambapo ni kilometa kadhaa kutoka katika mji huo.

Wachuuzi wa maji kwa kutumia baiskeli ndio wanaotoa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Mji wa Maganzo. Wachuzi hawa zaidi ya 100 ndio wanaotegemewa kuupatia mji huu maji kibiashara. Dumu moja la maji huuzwa kati ya sh. 400 hadi 500 kulingana na umbali alipo mwananchi anayeitaji maji hayo.

Benard Lucas ni mmoja wa wachuuzi (wauzaji wa maji kwa kutumia baiskeli) Maganzo, anasema alianza kufanya biashara hiyo ya uuzaji wa maji tangu mwaka 2009 baada ya kupata mtaji. Anasema uuzaji wa maji eneo hilo unaitaji muhusika awe na baiskeli pamoja na madumu ya kubebea maji pekee.

“Sehemu ambayo huyachota maji haya sisi hatulipii...huyachota bure kazi yako ni kusafirisha kwa kutumia baiskeli na kuwatafuta wateja walipo. Dumu moja la maji tunauza kati ya shilingi 400 na 500 kulingana na umbali anapopatikana mteja,” anasema Lucas.

Anasema kwa upande wake huuza madumu 14 hadi 16 kwa siku kulingana na uchakarikaji wa siku hiyo. Mwanambelembe Machia ni muuzaji mwingine wa maji katika Mji mdogo wa Maganzo, anasema amekuwa akifanya biashara hiyo kwa muda mrefu sasa na inalipa.

“Mimi nina watu wangu maalumu ambao tumekubaliana kupeleka maji kiasi fulani kwa kila siku. Huwa napata wastani wa shilingi 5,000 kwa siku kama kukiwa na biashara mbaya lakini kiasi hiki kinanitosha kabisa kwa matumizi yangu,” anasema Machia.

Kwa upande wake Frank Simba mchuuzi wa maji eneo hilo anasema alimaliza elimu ya msingi mwishoni mwa 2011, lakini baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari alinunuliwa baiskeli na wazazi wake na kuanza biashara hiyo ya uuzaji maji ili aweze kujitegemea.

Anasema msimu mbaya wa biashara hiyo ni kipindi cha masika ambacho wananchi hutegemea maji ya mvua ili kukwepa gharama. “Kutokana na wingi wetu kipindi hiki huwa kibaya kwa biashara maana wateja huadimika kabisa,” anasema kijana huyu anaeomba shida ya maji isitoweke Maganzo.
 
Hata hivyo Sera ya Maji ya nchi ya mwaka 2002 inaeleza kuwa madhumuni ya jumla ya sera kuhusu utoaji wa huduma ya maji vijijini ni kuboresha afya ya jamii na kusaidia kuondoa umaskini vijijini ikiwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa maji safi, salama na ya kutosha.

Madhumuni mahsusi ya sera hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu ya maji safi, salama na ya kutosha, kwa gharama iliyo ndani ya uwezo wa wananchi vijijini. Pia kuweka bayana majukumu na wajibu wa wadau mbalimbali. Lakini kama hiyo haitoshi sera pia imesisitiza kuhusu wananchi kulipia sehemu ya gharama za ujenzi wa miradi, na pia kulipia gharama zote za uendeshaji na matengenezo ya miradi yao, tofauti na dhana iliyokuwepo ya kuchangia tu sehemu ya gharama za uendeshaji na matengenezo.

Hii haipingwi kuwa maji ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu. Na kwa kutambua kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni hitaji la msingi na haki ya kila mtu, utoaji wa huduma ya maji vijijini utaimarishwa. Hata hivyo haki kama hii haipo kwa wakazi wa Mji mdogo wa Maganzo ambao unautajiri mkubwa wa almasi. Wakazi wa eneo hili kutokana na shida ya maji wamekuwa wakitumia maji kutoka kwenye madimbwi kukwepa gharama za kununua maji kila kukicha, huku wakihatarisha maisha yao kiafya.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Maganzo, Lwinzi Kidiga anakiri huduma ya maji ni kero kubwa kwa wakazi wa vijiji vyote vinavyo zunguka eneo hilo. Anabainisha kuwa zipo juhudi ambazo yeye na viongozi wenzake wanazifanya kuhakikisha wanakabiliana na hali hiyo.

Anasema kwa sasa tayari uongozi wa kijiji umefanya mazungumzo na mwekezaji wa madini ya almasi eneo hilo, ambaye pia ni mmiliki wa mgodi wa Williamson unaochimba almasi eneo hilo na mwekezaji huyo amekubalia kuwaletea maji wananchi kwenye moja ya tanki kubwa ambalo lipo jirani na soko kubwa eneo hilo. Anaongeza kuwa mradi huo unatarajia kuanza kati ya mwezi Julai, 2012.

Lakini huenda miaka kadhaa ijayo kero hiyo ya maji ikatoweka kwani, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Lucas Said akizungumzia kero hiyo anasema kwa sasa wataalamu wanafanya utafiti katika vijiji kadhaa kuhakikisha vinapatiwa huduma ya maji pale mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria kwa matumizi eneo hilo utakapo kamilika.

Friday, July 27, 2012

Vigogo waliopata mgawo Viwanja Dar waongezeka

MLOLONGO mrefu zaidi wa majina ya vigogo umebainika kugawiwa viwanja katika eneo la Gezaulole, jijini Dar es Salaam, ambapo safari hii imo familia ya Rais  mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassani Mwinyi.

Jana, gazeti hili lilichapisha katika ukurasa wa mbele habari iliyoonyesha baadhi ya majina ya vigogo waliogawiwa viwanja na kufanya wananchi wa kawaida kulalamika.

Katika uchunguzi zaidi, imebainika kuna orodha ndefu ya majina ya vigogo waliopewa viwanja katika mradi huo wa Gezaulole ambayo inahusisha mawaziri, wabunge, wakuu wa taasisi za Serikali na familia za baadhi ya watu maarufu.

Kwa upande wa familia maarufu, imo ya mzee Mwinyi ambaye pia amegawiwa eneo, wengine wana majina ya ukoo yanayofana na ya kwake ambao ni, Asina Mwinyi, Maimuna Mwinyi, Salama Mwinyi na Steven Ali Mwinyi, huku kutoka katika familia yenye jina la Kikwete yumo Ali J. Kikwete.

Viongozi wengine maarufu waliogawiwa viwanja hivyo ni Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emanuel Nchimbi, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.

Kwa upande wa watendaji wa taasisi za dola, yumo Katibu  wa Bunge, Dk Thomas Kashilila, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Polisi, Clodwig Mtweve, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, Balozi wa Tanzani nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, SACP Hamdan Makame, ACP John Gudaba, ACP Saada Juma Haji na  ACP Mohamed Usi.

Mlolongo huo pia unaonyesha majina ya baadhi ya wabunge ambao ni Murtaza Mangungu wa Kilwa Kaskazini (CCM), Mohamed Misanga, (Singida Kusini CCM), Jenister Mhagama (Peramiho CCM), Kheri Ameir (Matemwe, CCM), Kaika Telele (Ngorongoro, CCM), Amina Clement (Koani, CCM) na Ali Hamis Seif (Mkoani, CUF)  

Pia kuna orodha ya wabunge wa Viti Maalum CCM ambao ni Subira Mgalu, Alshaiymaa Kweygir, Elizabeth Batenga, Josephine Genzabuke, Betty Machangu, Lediana Mng’ong’o na Mwanakhamis Kassim Said.

Wabunge wengine wa Viti Maalum CCM ni  Mariam Mfaki, Mariam Kasembe, Agnes Hokororo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa pamoja na  Suzan Kiwanga ambaye ni mbunge wa Viti Maalum, Chadema na Ania Said Chaurembo ambaye ni mbunge mstaafu. 

Majina mengine ambayo koo zake ni za watu maarufu ni pamoja na  Ahmed Dau, David Kandoro, Asila Ditopile, Alice Koka, Gemini Suchak, Fidelis Owenya, Filoteus Msigwa, Evelyne Manumba, Fatma Ismail  Rage, Jamhuri Kihwelo, Issack Mwang’onda, Hijjal Makamba, Joseph Nyambibo, Mbwana Samata, Mohamed Mzimba na Mohamed Mtonga.

Wengine ni pamoja na Masanja Manumba, Mariam Mkama, Mansour Al-Maamry, Onesmo Mtasiwa, Musa Chagonja, Omary Shein, Shimbo Shimbo, Sikitu Kijazi, Solomon Kivuyo, Thomas Nyalile na Aisha Sululu (diwani Jangwani, CCM).

Pia wamo maofisa watatu wa Bunge ambao ni Herman Berege, Anslem Mrema na Theonest Ruhilabake pamoja na mmoja wa maofisa waandamizi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Boniface Njombe.

Wananchi waja juu
Baadhi ya maofisa wa Manispaa ya Temeke walisema fomu zilizochukuliwa ni zaidi ya 20,000 na kwamba kila fomu ilikuwa ikiuzwa Sh30,000, hivyo kufanya fedha zilizokusanywa kuwa zaidi ya Sh600 milioni.

Tayari mlolongo huo wa majina ya vigogo umesababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wakisoma majina hayo kulalamikia mchakato wa utoaji viwanja hivyo, huku wengine wakidai kuwa, warejeshewe fedha zao.

“Tumelipa Sh20,000 kila fomu ya kuombea kiwanja na wananchi tuliojitokeza ni karibu 30,000, lakini majina yanaonyesha kuwa asilimia kubwa ya waliopata ni vigogo ambao tunaamini wana viwanja mahali pengine,” alisema mwananchi mmoja(jina limehifadhiwa).

Mwananchi huyo alisema kuwa, hakukuwa na umuhimu wa kutangaza zabuni hiyo kwa sababu tayari walikuwa na majina yao, hivyo  walitakiwa kuwakabidhi viwanja vyao badala ya kuwasumbua na kuwatoza fedha.

“Hali hii inaonyesha kuwa Serikali ipo kwa ajili ya watu wachache, wenye fedha na si wananchi wa kawaida,” aliongeza.

Mwananchi mwingine (jina tunalo), alisema idadi kubwa ya watu waliokabidhiwa viwanja hivyo ni watoto wa vigogo na wabunge.

Aliongeza kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, hakuna kiongozi atakayewatetea wananchi, kwa vile kila mmoja wao yupo kwa ajili ya kupigania maslahi yake.

“Wabunge ambao tuliwategemea kutetea maslahi ya wananchi ndio wanaoongoza kwenye orodha ya kujichukulia viwanja, hii inaonyesha wazi kuwa hakuna kiongozi atakayeacha shughuli zake ili kutetea maslahi ya wananchi,” alisema.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Manispaa hiyo vinaonyesha kuwa, halmashauri hiyo imeingiza zaidi ya Sh600 milioni kutokana na uuzaji wa viwanja hivyo.

Wednesday, July 25, 2012

Sheria mpya mifuko ya jamii yazua mtafaruku nchini

Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya 2012 yaliyofanywa na Bunge yamezua mtafaruku na sintofahamu, huku wafanyakazi wa sekta mbalimbali wakiyapinga kwa maelezo kwamba ni kandamizi na yanalenga kuwanyima haki ya fedha wanazokatwa kwa mujibu wa sheria kuchangia mifuko hiyo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicolaus Mgaya aliliambia gazeti hili jana kuwa, watafungua kesi katika Mahakama ya Kazi nchini, kupinga hatua ya Serikali kubadili Sheria ya muda wa lazima wa kuchukua mafao hayo ambao ni kati ya miaka 55 na 60.

Tangu juzi watu kutoka sehemu mbalimbali hasa jijini Dar es Salaam wamekuwa wakipiga simu katika chumba cha habari cha Mwananchi kwa lengo la kupata ufafanuzi wa mabadiliko hayo ya sheria yaliyopitishwa na mkutano wa saba wa Bunge, Aprili 13 mwaka huu.

Kadhalika sheria hiyo inayozuia mwanachama wa mfuko wowote wa hifadhi ya jamii kuchukua mafao kabla ya umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ambao ni miaka 55, lilichukua nafasi kubwa katika mijadala ya mitandao ya kijamii ambako wengi wa wanaliochangia, wameiponda sheria hiyo na kuiita kuwa ni ya ‘kinyonyaji’.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka alisema jana kuwa: “Hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi, maana sheria hii itafuatiwa na kanuni na miogozo mingine ambayo ninaamini kwamba itaondoa wasiwasi uliopo”.
Isaka alisema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa katika miongozo hiyo ni iwapo mwanachama atafukuzwa au kuachishwa kazi, wanachama ambao wako kwenye kazi za mikataba na wale wanaopata ulemavu wa kudumu wakiwa kazini.

“Kimsingi ni kwamba suala la mafao ya kuacha kazi kabla ya umri wa kisheria wa kustaafu limefutwa kwa mifuko yote, isipokuwa katika mazingira hayo niliyoyaeleza litawekewa miongozo, na hii ni kwa faida ya wachangiaji,”alisema Isaka.

Alisema baada ya sheria hiyo kuwa imepitishwa na Bunge, kisha kusainiwa na Rais Jakaya Kikwete mwezi Juni mwaka huu, SSRA ilianza mchakato wa kuweka miongozo na baada ya hapo kinachofuatia ni kutoa elimu kwa umma na baadaye kuanza kutumika kwake rasmi.

“Lakini sasa tumelazimika kuanza kutekeleza sheria hiyo mapema kuliko tulivyopanga hasa baada ya kutokea kwa suala hili kwenye public (umma) kabla ya muda tuliokuwa tumekusudia,”alisema mkurugenzi huyo.

Isaka aliongeza kuwa chimbuko la sintofahamu iliyojitokeza ni baadhi ya mifuko kuchezeana rafu kwa lengo la kupata wanachama wapya kwenye migodi na kwamba wao kama wadhibiti tayari wametoa onyo kwa mifuko iliyohusika.

“Kwanza hakuna mfuko wowote ambao una mamlaka ya kutangaza kuanza kutumika kwa sheria, ni SSRA tu wenye mamlaka hayo, kwa hiyo tumewapa onyo, kama wanajitangaza wajitangaze kwa kueleza uzuri wa mfuko wao ni siyo kuchafuana au kuchafua wengine,” alisisitiza.
Wasemavyo wafanyakazi
Mgaya alisema sheria hiyo ni kandamizi kwani inamnyima fursa mfanyakazi aliyestaafu au kufukuzwa kazi kupata malipo yake ambayo ni halali.

“Sheria hii sisi hatuikubali na tunaipinga kwa nguvu zote na tutakwenda Mahakama ya Kazi kufungua kesi ya kupinga kutumika,” alisema Mgaya na kuongeza:

“Tutafanya mawasiliano na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuwaeleza kuhusu sheria hii ili watusaidie na ikishindikana azma yetu ni kwenda mahakamani.”
Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba haiwezekani mtu anafukuzwa kazi akiwa na miaka 45 na baadhi yao hawataki tena kuajiriwa wanataka kufanyabiashara halafu unamnyima mafao yake hadi afikishe miaka 55,  kitu ambacho kitamfanya mtu huyo aishi maisha magumu.

“Sheria hiyo ingekuwa na usawa ingetumika kwa wafanyakazi wote wa Serikali na kutowabagua kama inavyojieleza kwamba, Mbunge akimaliza miaka yake mitano anachukua mafao yake. Sasa  kwa nini iwe kwao tu na si kwetu pia?,” alihoji Mgaya.

Kwa upande wao Chama cha Wafanyakazi wa Migodini (Tamico) Wilaya ya Geita, kimesema kitapeleka maombi maalumu kwa Rais Kikwete kupinga marekebisho ya Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Katibu wa Tamico Wilaya ya Geita, Benjamin Dotto alisema wameamua kupiga kura ya maoni juu ya mabadiliko ya sheria hiyo, ili wanachama wao waamue wenyewe kama wanaitaka au la.

”Tunamwomba Rais aagize kupelekwa muswada wa marekebisho bungeni, kwa ajili ya  kipengele ambacho kimeleta mtafaruku,” alisema Dotto.

Alisema kipengele cha kuzuia mfanyakazi kuchukua mafao yake hadi afikishe umri wa miaka 55, kinakandamiza masilahi ya mfanyakazi mnyonge ambaye kwa kiasi kikubwa amekuwa akichangia mapato ya nchi kupitia kodi anayokatwa.
Chimbuko la sheria
Mabadiliko ya sheria hizo za mifuko ya hifadhi ya jamii yalifanywa na Bunge Aprili 13 mwaka huu, baada ya muswada husika kuwa umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni Februari 1, 2012.

Ibara ya 107 ya muswada huo ndiyo ilipendekezwa kufutwa kwa Ibara za 37 na 44 za Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) ambavyo vilikuwa vikiruhusu mafao ya kujitoa.

Meneja uhusiano wa SSRA Sara Mssika alisema jana kuwa kufutwa kwa ibara hizo kulimaanisha kwamba hakuna mfuko wowote unaoruhusiwa kutoa tena mafao ya aina hiyo hadi hapo miongozo mipya itakapotolewa.

“Hakuna sheria ya mfuko mwingine iliyokuwa ikiruhusu mafao ya kujitoa, na kama wapo waliokuwa wakifanya hivyo, basi walikuwa wanafanya hivyo pengine kwa taratibu nyingine ambazo ni nje ya sheria za kuanzishwa kwa mifuko yao,”alisema Mssika.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka akiwasilisha maelezo ya muswada huo bungeni alisema lengo la marekebisho katika Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuiwezesha SSRA kufanya kazi yake kikamilifu na kusimamia na kudhibiti Sekta ya Hifadhi ya Jamii.

Alisema muswada huo uliandaliwa kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, wakiwamo wafanyakazi, waajiri na Serikali, pia
mifuko yenyewe kupitia vikao vya wadau na Baraza la Ushauri wa Masuala ya Kazi Jamii na Uchumi.

“Kimsingi, wadau wote waliunga mkono mapendekezo yaliyomo katika muswada huu,” alisema Kabaka na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yatawezesha kupanuliwa kwa wigo wa wanachama kwenye mfuko kwa kuruhusu wafanyakazi wanaoingia kwenye ajira kwa mara ya kwanza ama kujiajiri wenyewe ili waweze kujiunga.

Tuesday, July 24, 2012

Asilimia 30 ya watoto hufanyiwa ukatili nchini

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sofia Simba amesema ripoti ya utafiti wa ukatili dhidi ya watoto nchini, imeonyesha takribani wanawake watatu kati ya 10 na mwanaume mmoja kati ya saba, walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na watu wazima walipokuwa watoto chini ya umri wa miaka 18.

Alisema matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia na kukabiliana na tatizo hilo.

Aidha, Simba, alisema matokeo hayo yatasaidia katika kuanzisha taratibu za kuboresha huduma kwa waathirika wa ukatili na kuandaa miongozo na kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009.

“Katika mwaka huu wa fedha wizara itasambaza kanuni na miongozo hiyo katika halmashauri zote nchini, ili wananchi waweze kuzielewa na kuzizingatia…pia itatayarisha mwongozo wa kukusanya takwimu za watoto wanaonyanyaswa,” alisema.

Simba alieleza hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13.

Wizara hiyo imeomba bajeti ya Sh. bilioni 15.6 ambapo kati ya hizo Sh. bilioni 12.1 ni matumizi ya kawaida.

Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imemshambulia Waziri Simba, kwa kumhadaa, kumdanganya na kumteleza Nasra Mohamed ambaye alifariki dunia baada kufanyiwa unyama na mumewe.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Conjesta Rwamlaza, alitoa kauli hiyo alipokuwa akisoma maoni ya kambi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2012/13.

“Waziri Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Taifa alieleze Bunge hili ni kwanini alimhadaa, kumdanganya na kumtelekeza Nasra Mohamed bila msaada wowote wakati aliahidi kwa kinywa chake mwenyewe kuwa angemsaidia?” alisema na kuongeza:

“Kambi ya Upinzani inataka kujua Waziri anawasaidiaje watoto walioachwa na marehemu na pia hatua gani zitachukuliwa dhidi ya aliyetenda ukatili huu?”

Alisema wanasikitishwa kuona kwamba Serikali haiko mstari wa mbele katika kupigania haki kwa wanawake wanaonyanyaswa.

Rwamlaza alisema tukio hilo lilitokea Februari 19  mwaka huu, katika Wilaya ya Bunda Mkoani Mara, ambako Nasra Mohamed, alifanyiwa unyama na mumewe Elisha Mkumbati ambaye alimgonga kwa makusudi na gari na baadaye kumburuza na gari hilo jambo lililomsababishia maumivu makali na hatimaye umauti.

 
CHANZO: NIPASHE

Wednesday, July 18, 2012

Hoja Za Kambi Ya Upinzani Mambo Ya Ndani Yazuiwa Bungeni

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA VINCENT JOSEPHAT NYERERE (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)

UTANGULIZI
 
Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, napenda kuchukua fursa hii kuwasilisha maoni yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, napenda kuwashukuru askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza wanaoishi Kambi iliyoko katika Kata ya Mkendo kwa kunichagua kuwa Diwani wao. Vile vile, nawashukuru wananchi wote wa vyama vyote na dini zote Jimbo la Musoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge na mtetezi wao. Pia napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi katika Wizara hii. Kwa upekee kabisa, Mheshimiwa Spika, kwa wanaoeneza propaganda kwamba CHADEMA inachukia au kudharau askari polisi wetu, naomba nitoe shukrani zangu kwa mke wangu Helen V. Nyerere ambaye pia ni askari wa Jeshi la Polisi. 
 
UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI 
 
Mheshimiwa Spika,
Katika mwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji matukio mbali mbali ya mauaji ya raia yaliyowahusisha askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wa vyombo vingine vya dola. Aidha, tulihoji matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi wetu hasa katika maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabu kama vile Nyamongo, Arusha na kwingineko katika nchi yetu. Vile vile, tulihoji sababu za Serikali kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria na za kiutendaji watuhumiwa wa makosa haya makubwa. 
 
Mheshimiwa Spika,
Wakati anatoa hoja yake ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka jana, Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali ingefanya uchunguzi wa matukio yote ya mauaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania. Kwa maneno yake mwenyewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema: “vifo ... ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya Vyombo vya Dola, ni lazima vichunguzwe.” Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hadi wakati tunaandika maoni haya, hakuna Mahakama ya Korona hata moja ambayo imeitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokana na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama kauli ya Waziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuwahadaa Watanzania. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke ni lini Serikali itaunda Mahakama za Korona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wananchi katika maeneo yote tuliyoyataja mwaka jana. 

Mheshimiwa Spika,
Kwa sababu ya Serikali kutotimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio ya mauaji kwa mujibu wa Sheria tajwa, vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vimeendelea kutokea katika nchi yetu. Kwa mfano, katika taarifa yake ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2011, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinaripoti kwamba “mwenendo wa matukio ya ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo vya dola umeendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kati ya Januari na Desemba 2011 tayari watu 25 wamekwisharipotiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa usalama, wakati ambapo watu wengine 50 walijeruhiwa.” Taarifa hii inaungwa mkono na taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania iliyotolewa mwaka huu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department) inayoonyesha kuwa bado yapo mauaji yanayotokea mikononi mwa vyombo vya dola ikiwemo jeshi la polisi, utesaji na wananchi wanaotuhumiwa kujikuta wakipata vipigo kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.

MAUAJI YENYE SURA YA KISIASA 
 
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Serikali kutochukua hatua kukabiliana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi la mauaji na matukio ya majaribio ya mauji yenye sura ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini. Matukio hayo ni pamoja na mauji ya kada wa CHADEMA Mbwana Masudi yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga, na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River, Marehemu Msafiri Mbwambo, mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki. 
 
Aidha, Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge wa CHADEMA Mheshimiwa Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Mheshimiwa Salvatory Machemli wa Jimbo la Ukerewe, walioshambuliwa kwa mapanga mbele ya maafisa polisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM mkoani Mwanza. Vile vile, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) alivamiwa na wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa. 

Mheshimiwa Spika,
Matukio ya mauaji au majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa yamewahusu pia watu ambao sio wanachama au viongozi wa vyama vya siasa lakini wanaonekana kupinga matakwa ya watawala. Haya yamemkuta Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Dr. Steven Ulimboka ambaye alitekwa nyara na kuteswa kwa kikatili na watu ambao taarifa za vyombo vya habari zimewataja kuwa maafisa wa vyombo vya dola. Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru kukamatwa kwa watuhumiwa wote ambao wametajwa kuhusika na utekaji nyara na jaribio la kumuua Dr. Ulimboka ili kufuta dhana kwamba vyombo vya dola viko juu ya sheria na vinaweza kuua au kutesa wananchi bila mkono mrefu wa sheria kuwaangukia. 
 
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 14 Julai 2012, mtu anayesemekana kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Kata Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi, Yohana Mpinga, ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA katika Kata ya Urughu alifariki dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa CHADEMA katika Kata ya Ndago. Kwa vile, tayari baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge hili tukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba CHADEMA inahusika na kifo cha Marehemu Yohana Mpinga, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina haya ya kueleza kuhusiana na tukio hili. 
 
Kwanza, mkutano wa hadhara wa CHADEMA ulihudhuriwa pia na maafisa polisi waliokuwepo wakati wote wa mkutano huo. Pili, licha ya kuwepo kwa maafisa polisi hao, kundi la wahuni wanaodaiwa kukodiwa na makada wa CCM wa Jimbo la Iramba Magharibi walivuruga mkutano huo kwa kupiga mawe watu waliohudhuria mara mbili lakini mara zote polisi waliokuwepo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la wahuni. Aidha, mara ya wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa CHADEMA walitoa taarifa rasmi katika Kituo cha Polisi cha Ndago na kufunguliwa jalada namba NDG/RB/190/2012. 

Tatu, mara baada ya kutoa taarifa hiyo kwa polisi, mkutano wa hadhara uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafara wa viongozi wa CHADEMA kuondoka eneo la Ndago na kuelekea Kinampanda ambako kulikuwa na mkutano mwingine wa hadhara. Wakati huo, kundi la askari polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika katika eneo la mkutano na kukuta mkutano umemalizika. Nne, kwa vile mkutano wa hadhara wa CHADEMA ulimalizika kwa amani mbali na matukio ya kihuni yaliyoripotiwa kwa Jeshi la Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha FFU na askari polisi wengine katika eneo la mkutano baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka, ni wazi kwamba watu wanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi Marehemu Yohana Mpinga alivyofikwa na mauti ni Jeshi la Polisi lenyewe. 
 
Aidha, Mheshimiwa Spika, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaeleza Watanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliowarushia mawe viongozi wa CHADEMA na wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara hawakuchukuliwa hatua zozote na polisi waliokuwepo kwa muda wote wa mkutano huo au askari wa FFU waliofika baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa sana na mauaji ya kijana huyo na inatuma salamu za pole na rambi rambi kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu. Hata hivyo, Kambi yetu inasikitishwa na kushangazwa sana na ushabiki wa kisiasa ambao umejitokeza humu Bungeni na kauli za kutoa hukumu ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali bila hata kusubiri uchunguzi kamili juu ya jambo hili. 
 
MASLAHI YA POLISI NA MAGEREZA 
 
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yake ya mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia utamaduni wa Serikali kupuuza maslahi ya askari polisi na wale wa Jeshi la Magereza. Utamaduni huu ni wa muda mrefu sana. Kwa mfano, katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2006/2007, aliyekuwa Waziri wakati huo alikiri kwamba “... kutokana na kipato kidogo cha askari polisi, inawawia vigumu kukopa katika mabenki nchini kutokana na riba kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika. Hivyo, askari polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao.”
 
Mheshimiwa Spika,
Toka wakati huo hadi sasa, maslahi ya askari polisi yamekuwa mabaya zaidi kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei hasa za vyakula kupanda wakati ambapo mishahara yao haijaongezeka sambamba na ongezeko la gharama halisi za maisha. Aidha, katika hali inayoonyesha kutokujali kabisa maslahi na hali za maisha za askari wetu, Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyotolewa tarehe 17 Novemba, 2011 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani Mheshimiwa Khamis Sued Kagasheki, aliyeliambia Bunge hili tukufu kwamba “... posho ya askari imepandishwa na ... kwamba (inatakiwa) itoke kwenye shilingi laki moja mpaka shilingi laki moja na hamsini.... Ni jambo ambalo tunalo na tumelifanyia kazi na tuna uhakika kwamba, litaweza kutimia….”

Mheshimiwa Spika,
Ni ukweli usio na mjadala kwamba askari polisi na magereza bado wanapokea posho ya kujikimu ya shilingi laki moja badala ya shilingi laki moja na elfu hamsini iliyoahidiwa na Serikali mbele ya Bunge hili tukufu. Aidha, katika mazingira ya kushangaza kabisa, mara baada ya Serikali kutoa ahadi Bungeni juu ya posho hiyo, uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi ulituma maelekezo kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa kufanya uchunguzi ili kubaini askari wote waliokuwa wanadai walipwe posho ya shilingi laki moja na nusu kama ilivyoahidiwa ili askari hao wafukuzwe kazi.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu ni lini italipa malimbikizo ya baki ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi kwa kila askari polisi na magereza ambayo haijawalipa askari hao hadi hivi sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ianze kuwalipa askari polisi na magereza posho ya kujikimu ya shilingi laki moja na nusu kwa mwezi kuanzia mwaka huu wa fedha, kwa vile ahadi ya Serikali iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani haijawahi kukanushwa, kubatilishwa au kubadilishwa na Serikali.
 
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Serikali haitekelezi ahadi inazotoa Bungeni juu ya malipo ya askari polisi na magereza. Serikali pia imekuwa inawakopa watumishi hao bila ridhaa yao. Kwa mfano, randama ya fungu la 29 inaonyesha kuwa Jeshi la magereza linadaiwa jumla ya shilingi bilioni 23.65. Kati ya fedha hizo, watumishi wa Jeshi la Magereza wanaidai Serikali jumla ya shilingi bilioni10.34 ambazo ni malipo ya stahili zao mbali mbali kama vile fedha za likizo, uhamisho, mafunzo, n.k. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kama, na lini, italipa madeni haya ya askari magereza wetu wanaokesha magerezani usiku na kushinda juani mchana wakiwalinda wafungwa na mahabusu waliojaa katika magereza ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Kuna hatari kwa askari wa Jeshi la Magereza kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo tumeyaeleza katika maoni haya. Mfano ni katika Jimbo langu la Musoma Mjini. Mbali na makazi duni ya askari magereza, vile vile kuna umbali mrefu kati ya kambi ya askari magereza ya Nyasho na Gereza la Mkoa lililopo Kata ya Mkendo na askari magereza wamekuwa wakitembea kwa miguu usiku wanapokuwa zamu gerezani. Hii inahatarisha usalama wao kwani wanaweza kuvamiwa na kudhuriwa na wafungwa au mahabusu waliokwisha kumaliza adhabu zao lakini wakawa na visasi na askari hao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwapatie gari askari wa kambi ya Nyasho na makazi mengine ya askari magereza yaliyoko mbali na magereza wanakofanyia kazi ili kunusuru maisha ya askari magereza wetu. 
 
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba “... utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja, kwani unawanyonya kwa sababu vipato vyao ni vidogo. Badala yake ... serikali ibebe jukumu hilo.” Hata hivyo, hadi tunaandika maoni haya, Serikali imeendelea kupuuza mapendekezo haya kwa kisingizio kwamba ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ ni wa hiari ilhali askari polisi wanaendelea kukatwa mishahara yao kwa lazima. Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatamka kwamba kukata mshahara wa mfanyakazi bila ridhaa yake wakati hadaiwi chochote na mwajiri wake ni kinyume cha sheria husika za nchi yetu na kitendo cha jeshi la Polisi kuendelea kukata mishahara ya askari polisi kwa ajili ya ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ bila ridhaa ya askari polisi wenyewe kikome mara moja.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba askari polisi wanaofanya kazi za lindo katika mabenki yote ya biashara hapa nchini hulipwa posho ya shilingi elfu kumi kwa siku. Hata hivyo, Serikali haijawahi kutamka hadharani kiasi ambacho mabenki hayo hulipa serikalini kwa ajili ya kazi hiyo ya kulinda mabenki binafsi. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikli kulieleza Bunge lako tukufu kiasi ambacho mabenki ya biashara hulipa serikalini kwa ajili ya huduma ya ulinzi inayotolewa na askari polisi ili Bunge lako lifahamu kama askari polisi wanaofanya kazi hiyo wanalipwa inavyostahili. 
 
VITENDEA KAZI VYA POLISI
 
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa, makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchini yalikuwa 62,133. Ripoti inasema kwamba kwa mwaka 2011 makosa 63,703 ya jinai yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini. Kwa kiasi kikubwa, ongezeko hili la uhalifu linasababishwa na askari wa doria kushindwa kufika kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu kwa haraka pindi wapatapo taarifa kwa kisingizio cha kukosa mafuta kwa ajili ya magari ya doria. 
 
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, nyaraka za Serikali zinaonyesha kwamba Bunge lako tukufu limekuwa likiidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa mujibu wa randama ya Fungu la 28 kwa mwaka huu wa fedha, matumizi halisi ya mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 yalikuwa shilingi bilioni 2.81. Aidha, katika mwaka wa fedha uliopita Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi bilioni 2.61 kwa ajili ya mafuta, wakati ambapo kwa mwaka huu wa fedha Serikali inaomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 2.56 kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi. 

Wakati Bunge limekuwa lkiidhinisha mafungu haya makubwa ya fedha kwa ajili ya mafuta, askari polisi wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya doria hivyo kusababisha askari polisi kushindwa kufanya kazi zao hizo ipasavyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze zinakopelekwa fedha za mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kama gari moja la doria linapatiwa lita 5 za mafuta kwa kutwa na/au usiku. 
 
IDARA YA UHAMIAJI NA PAKACHA LA MIPAKA
 
Mheshimiwa Spika,
Mipaka yetu na nchi jirani zinazotuzunguka imekuwa pakacha linalovuja. Ndio maana katika hotuba yetu ya mwaka jana tuliliambia Bunge lako tukufu kwamba “... kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje ... kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini.” Tulionyesha jinsi ambavyo kumekuwa na ongezeko la wageni haramu kutoka nchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan, Nigeria, China, India na Bangladesh “ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.” Tulitahadharisha kwamba “utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake ni hatari kiusalama, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa ... ugaidi na uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu ...” n.k.

Mheshimiwa Spika,
Maneno na tahadhari zetu ziliangukia kwenye masikio ya Serikali kiziwi. Na sasa yale tuliyoyasema yameanza kutimia kwani ni mwezi mmoja tu umepita tangu wahamiaji haramu zaidi ya arobaini kutoka Ethiopia kukutwa wamekufa ndani ya lori la mizigo ambalo kwa vyovyote vile lilitokea nchi jirani. Watu hawa waliingiaje nchini na kusafiri hadi katikati ya nchi yetu bila kujulikana na maafisa wa Uhamiaji, polisi wa usalama barabarani na usalama wa taifa kama kweli nchi yetu iko salama? Ni afisa gani wa Idara ya Uhamiaji aliyewapitisha katika mpaka wetu wa Namanga au Horohoro au Sirari au Kogaja au Borogonja? Na ni askari polisi gani aliyewasindikiza hadi Kongwa? Aidha, ni afisa mizani gani wa TanRoads aliyepitisha lori walimokuwa watu hao bila kulikagua na kujua kilichokuwamo?
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea – kwa kuzingatia ukubwa na uzito wa kashfa hii – viongozi waadilifu katika Wizara, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi wangewajibika kutokana na uchafu huu. Hata hivyo, hakuna hata mmoja ambaye amefanya hivyo. Kwa vile uwajibikaji wa hiari unaelekea kushindikana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibisha wale wote waliohusika kuanzia viongozi wa Wizara walioko humu Bungeni na uongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi ili kuondokana na aibu hii ya nchi yetu kuwa transit route ya biashara ya kusafirisha binadamu katika sehemu hii ya Bara la Afrika.
 
Mheshimiwa Spika,
Matatizo ya ongezeko la wahamiaji haramu katika nchi yetu linatokana na Idara ya Uhamiaji kuendekeza vitendo vya kifisadi katika kuajiri, kupandisha madaraja au vyeo wa maafisa wa Idara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, ajira katika Idara ya Uhamiaji haizingatii tena elimu, uwezo na weledi wa maafisa husika. Bali, kwa mujibu Taarifa ya Utafiti wa Mpango Mkakati wa Mageuzi Katika Utumishi wa Uhamiaji (Immigration Service Reform Programme Strategic Plan Research Report) iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 27 Novemba, 2011, “mara nyingi mgawanyo ya kazi (katika Idara) hautegemei sifa bali unategemea upendeleo, rushwa, kujuana na urafiki vitu ambavyo viko kinyume na maana halisi ya mgawanyo wa kazi.” (“Most of the time placement is not based on merits but depends on nepotism, bribery and technical know-who, friendship and favouritism that have been contrary to the whole meaning of placement.”)

Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa kauli hii unapatikana katika Taarifa hiyo ya Utafiti inayoonyesha kwamba maafisa wengi wa ngazi za juu katika Idara ya Uhamiaji ni watu wenye uwezo mdogo kielimu kulinganisha na maafisa wa ngazi za chini wa Idara hiyo. Kwa mfano, katika ngazi ya Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji kwenda juu hadi kwa Kamishna Mkuu, kuna maafisa kumi wenye shahada ya uzamili (masters degree), wawili wenye post-graduate diploma (PGD), ishirini na nne wenye shahada ya kwanza, tisa wenye stashahada, saba wenye diploma, kumi na moja wenye kidato cha sita na 248 wenye elimu ya kidato cha nne. Katika maafisa hawa wa ngazi za juu, kuna Kamishna mmoja mwenye elimu ya kidato cha nne wakati kuna Makaimu Kamishna 216 wenye elimu hiyo ya kidato cha nne na Kamishna Wasaidizi Wakuu 31. 

Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Spika, kuanzia ngazi ya Mrakibu Mwandamizi (Senior Superintendent) kwenda chini mpaka koplo kuna maafisa wenye shahada ya uzamili 36, wenye post-graduate diploma wako saba, wenye shahada ya kwanza wako 340, wenye stashahada wako 78, diploma wako kumi wenye cheti (certificate) wako 52, waliomaliza kidato cha sita wako 585 wakati waliohitimu kidato cha nne wako 337. Katika mazingira ambayo maafisa wenye uwezo mkubwa wa elimu hawapewi nafasi za juu katika Idara badala yake uongozi wa juu umejazwa na wenye elimu za mashaka kama inavyoonyeshwa katika Taarifa ya Utafiti ya Wizara, ni wazi kwamba matukio kama ya maafa ya wahamiaji waliokutwa wamekufa Jimboni kwa Naibu Spika wa Bunge hili tukufu hayawezi kuepukika! 
 
Aidha, Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya upendeleo na rushwa katika ajira ya Idara ya Uhamiaji ya aina hii, maafisa uhamiaji hawawezi kuacha kutumiwa na wanasiasa wa chama tawala kuwatuhumu washindani wao kisiasa kuwa sio raia wa Tanzania ili kuwaondoa katika kinyang’anyiro cha chaguzi zetu. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mheshimiwa Ali Mohamed Keissy alipotaka kugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA na kuzushiwa tuhuma kuwa siyo raia. Hata hivyo, alipojiunga na CCM bila ridhaa yake tuhuma za kutokuwa raia ziliyeyuka na sasa ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini katika Mkoa anakotokea Waziri Mkuu!

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu juu ya mambo haya ambayo yamethibitishwa na Ripoti ya Utafiti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Kambi inaitaka Serikali itoe kauli kama kuna haja yoyote ya kutumia mamilioni ya fedha za wananchi kusomesha maafisa wa Idara ya Uhamiaji ambao baada ya kufuzu hawapatiwi vyeo na majukumu yanayolingana na uwezo wao wa kielimu. 

JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI

Mheshimiwa Spika,
Ni dhahiri kuwa umuhimu wa Jeshi hili unaonekana pale yanapotokea majanga ya moto, mafuriko au maafa mengine kama vile tetemeko la ardhi ambapo athari za matukio haya ni makubwa sana na mara nyingi hupelekea wananchi kupoteza maisha. Malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali juu ya Jeshi la Zimamoto kuchelewa kufika katika maeneo ya tukio yamekuwepo kwa miaka mingi na yamepigiwa kelele sana hapa Bungeni. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia ushauri wake kuwa Serikali iboreshe mfumo mzima wa zimamoto katika nchi yetu ili kukabiliana na majanga ya moto yanayoongezeka kutokana na kupanuka na kukua kwa miji yetu.
 
Mheshimiwa Spika, 
Baada ya maelezo na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninaomba kuwasilisha.


.....................……………………………………..
VINCENT JOSEPHAT NYERERE
MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
17/07/2012

Thursday, July 12, 2012

Nusu ya Bajeti ya Ardhi kujenga Kigamboni mpya

Na Florence Majani, Dodoma
 WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imetenga zaidi ya nusu ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha, 2012/2013 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.Fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza mji huo ni Sh60 bilioni ambazo ni sawa na asilimia 59 ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo, ambayo ni Sh101.731 bilioni.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema Bungeni jana kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi huo ni sawa na asilimia 10 tu ya mahitaji ya kiasi cha Sh605.
“Kwa hiyo tutatumia mbinu za kisasa kutafuta pesa nyingine Sh605 bilioni nje ya Bajeti kutekeleza mradi huu bila kuchelewa zaidi. Mradi huu unahitaji kiasi hicho cha fedha kwa miaka mitatu ya kwanza,” alisema Profesa Tibaijuka alipokuwa akiwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara yake jana na kuongeza:

“Nitasimamia mradi huu kwa kasi, ari na nguvu mpya. Ingawa pia sitakuwa nimetenda haki iwapo sitawashukuru wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu na ushirikiano wanaotuonyesha.”

Katika Bajeti ya wizara hiyo ya Sh101.7 bilioni, matumizi ya kawaida ni Sh30.7 bilioni na Sh71 bilioni ni za maendeleo. Katika fedha hizo za maendeleo, Sh61 bilioni ni fedha za ndani na Sh10 bilioni ni fedha za nje.

Kuhusu wananchi wanaoishi katika eneo hilo, Profesa Tibaijuka alisema hakuna mkazi yeyote wa Kigamboni atakayehamishwa kwani idadi ya wananchi waliopo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya makazi mapya yanayotakiwa kujengwa katika eneo hilo.
Alisema ni ushauri wake kwamba wakazi wote wa Kigamboni wachague kubaki katika mji huo kwani wawekezaji wa ndani na nje watapewa maeneo kwa ajili ya kujenga makazi ambayo yatatumika kuwahamishia wananchi watakaoamua kubaki.

“Tunashauri wote wabaki kwa kuwa sasa hivi kuna wananchi takribani 82,000 wakati tunajenga mji mpya wenye uwezo wa wakazi 400,000. Hakuna sababu ya wananchi kuhama eneo hili ila makazi yao yatapangwa upya na kuboreshwa,” alisema.

Gharama za mradi
Profesa Tibaijuka alisema ujenzi wa Mji wa Kigamboni utafanywa kwa awamu tatu, ambazo zitatekelezwa kati ya mwaka huu na 2032 na gharama zinazotarajiwa kutumika hadi utakapokamilika ni Sh11.6 trilioni.

Alisema awamu ya kwanza itakuwa kati ya mwaka 2012 na 2022, awamu ya pili kati ya 2022 na 2027 na awamu ya tatu ni kati ya 2027 na 2032.
Profesa Tibaijuka alisema miongoni mwa kazi zitakazofanywa katika mwaka huu wa fedha ni kuundwa kwa wakala mpya wa kusimamia mradi huo anayejulikana kama Kigamboni Development Agency (KDA).

Kazi nyingine ni kuidhinisha mpango na kuanza utekelezaji, kufanya uthamini wa mali zilizomo katika maeneo ya miundombinu, huduma za maji na eneo mbadala na kulipa fidia kwa mali zilizomo katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini.

Kuhusu fidia, Waziri Tibaijuka alisema wananchi ambao hawajakiuka maagizo ya mradi kwa kufanya maendelezo haramu, wasiwe na wasiwasi kuhusu fidia kwa sababu mradi utazingatia haki na ni endelevu... “Fidia itatolewa kwa mujibu wa sheria kwa tathmini ya kiujumla ambayo itakokotolewa kutokana na viwango vya soko na kuhusishwa ili iwe sahihi.”

Alisema atafanya ziara ya mafunzo kwa wawakilishi kutoka Kigamboni kutembelea mji mpya ili uwepo uelewa wa pamoja juu ya jinsi mji huo utakavyokuwa.

Hazina ya Ardhi
Katika hatua nyingine, Profesa Tibaijuka alisema wizara yake inakamilisha uanzishaji wa Hazina ya Ardhi pamoja na Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Alisema vyombo hivyo vitasimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje kwa misingi ya kuingia ubia wa kumiliki pamoja hisa zitakazotolewa kwa uwiano kati ya wananchi na wawekezaji husika.

Kuhusu kuweka na kutunza alama za mipaka ya Tanzania na nchi jirani, Profesa Tibaijuka alisema majadiliano ya kupima maeneo hayo yalishakamilika.
Alisema majadiliano yalishafanyika baina ya Tanzania na nchi za Comoro na Msumbiji na mkataba wa kwanza kati ya Tanzania, Msumbiji na Comoro kwenye alama za utatu baharini inayotenganisha nchi hizo ulikamilika na kutiwa saini Desemba 5, mwaka jana.

“Mkataba wa pili kati ya Tanzania, Shelisheli na Comoro ulitiwa saini Februari 17, mwaka huu. Hivyo basi, Tanzania imekamilisha upimaji wa mipaka katika Bahari ya Hindi na itatangaza eneo lake la ukanda wa kiuchumi baharini bila kipingamizi kwa nchi jirani,” alisema.

Alisema wizara yake imewasilisha andiko la kudai nyongeza ya eneo ya ukanda wa kiuchumi baharini Januari, mwaka huu na Tume ya Mipaka ya Baharini ya Umoja wa Mataifa, inapitia andiko hilo.

Profesa Tibaijuka alisema kupatikana kwa eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 61,000 kutaiwezesha Tanzania kuvuna rasilimali za chini ya bahari kwa manufaa ya sasa na kwa vizazi vijavyo.

Kurasini kulipwa fidia
Kuhusu mradi wa uendelezaji wa eneo la Kurasini ulioanza 2006 kwa ajili ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Profesa Tibaijuka alisema wizara imetenga fedha chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo katika eneo la Kurasini na Shimo la Udongo.

“Wizara itaendelea na malipo hayo kwani hata mwaka jana tulilipa kiasi cha Sh550 milioni kwa wakazi wa Mtaa wa Kurasini waliopo jirani na Mabwawa ya Majitaka,” alisema.

Alisema wizara yake itaendelea kutatua migogoro ya ardhi, urasimishaji wa makazi holela, mikopo ya nyumba, ujenzi wa nyumba unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na ujenzi wa nyumba za biashara na makazi.

‘Katiba mpya itoe miaka 10 tu kwa wabunge, wawakilishi’

Na Masoud Sanani, Zanzibar
BAADHI ya wakazi wa Zanzibar wametaka Katiba Mpya iweke kipindi cha ubunge na uwakilishi kiwe miaka 10 kama ilivyo kwa Rais ili kuimarisha demokrasia nchini.Wakitoa maoni kwenye Mkutano wa kusaka maoni ulioandaliwa na Tume ya Katiba mjini hapa walisema  lazima wabunge wawe na miaka 10 kama ilivyo kwa Rais badala ya kutaka wawe wabunge milele.

Abdallah Khamis Abdallah (54) na Bakar Mwinyi Mussa (63) wa Mitakawani walitaka wabunge wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wawe na muda maalumu wa uongozi wa miaka 10 kama ilivyo kwa Urais.
Abdallah pia alitaka Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na vyeo vingine vya juu wakistaafu wawe kama wananchi wa kawaida wasienziwe kama ilivyo sasa kwani ni gharama kubwa kwa uchumi wa Taifa.

“Rais ana pensheni kubwa na marupurupu mengi kwa hiyo alipwe akawe kama mwananchi wa kawaida asiendelee kutunzwa ma Serikali,” alitoa maoni yake kwa Tume inayochukua maoni juu ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.Alitaka pia rasilimali za Taifa ziwe za Muungano na zimilikiwe na dola.


Katika hatua nyingine wakazi wengi waliotoa maoni yao juu ya kuandikwa Katiba Mpya nchini walitaka mfumo wa sasa uendelee, lakini Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Rais wa Muungano.

Wakitoa maoni yao katika maeneo ya Mgeni Haji, Mitakawani na Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja jana walipendekeza mfumo wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar uendelee.

Lakini wananchi hao walitaka Rais wa Zanzibar awe Makamu wa Rais wa Muungano badala ya kuwa waziri katika Muungano kama ilivyo sasa.Pia wananchi hao walitaka kero zote za Muungano ziondolewe ili Muungano uimarike na misaada kutoka nje igawiwe kwa pande zote mbili za Muungano yaani Bara na Zanzibar.

Awali mkazi Zanzibar, alishauri Katiba Mpya iwe na kipengere kitakachowatoa Ikulu Marais wanaomaliza muda wao na kutaka kugombea awamu nyingine ili wanapogombea wawe wanatoka nyumbani kwao badala ya kutoka Ikulu.

Akitoa maoni yake mbele ya Tume ya Katiba iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja, Hassan Pandu Ibada (40) mkazi wa Mpapa, Wilaya ya Kati alieleza kuwa Rais anapaswa kutoka Ikulu wakati wa uchaguzi.
Alitaka Katiba Mpya itoe nafasi ya kuwapo kwa Rais wa muda ambaye baada ya uchaguzi atamkabidhi madaraka aliyeshinda katika uchaguzi mkuu.

“Rais akiwa wa Muungano au wa Zanzibar asitoke Ikulu na kwenda kwenye viwanja vya kampeni kuwania urais, aondoke Ikulu ili awe sawa na wagombea wengine,” alieleza mwananchi huyo .

Baraza La Habari La Kiislamu Kuwafungulia Kesi Mahakamani Madaktari Waliogoma

Baraza la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA) limesema linakusudia kuwafungulia mashitaka Madaktari Mabingwa wote pamoja na Madaktari waliokuwepo kwenye Mafunzo kwa Vitendo (Interns) ambao walishiriki katika mgomo kwenye hospitali mbalimbali nchini na kusababisha wagonjwa kukosa huduma za matibabu huku wengine wakipoteza maisha yao.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya baraza hilo kukaa na Madaktari waliokua katika mgomo na kukubaliana kuwa waiombe radhi Serikali pamoja na wananchi kisha warudi kazini, lakini Madaktari hao wamekiuka makubaliano hayo na kuendelea na mgomo jambo lililoonyesha kwamba hawakuwa tayari kupata suluhu.

Katibu wa BAHAKITA, Said Mwaipopo amesema wameshauriana na Wanasheria wao na kuamua kuwafungulia kesi ya mauaji Madaktari hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam tarehe 16 Julai 2012.

Amesema, “kwa tukio zima jinsi lilivyokwenda, limeonyesha kwamba Madaktari hawataki wala hawana shida tena ya kurudi kazini kwa sababu ni wazi kwamba kuna mtu yuko nyuma yao wanaemtumikia. Sisi kama Watanzania, sehemu ya jamii tumekaa na Wataalamu wetu wa Sheria tumekubaliana kwamba Jumatatu tunakwenda kufungua kesi Mahakamani kwa Madaktari wote waliogoma wakati wamesomeshwa na kodi zetu na Serikali yetu imewasomesha, tutawafungulia kesi ya kusababisha mauaji pale Muhimbili, kwa hiyo tunachofanya hivi sasa ni kwenda pale Muhimbili kwa mganga mkuu kuchukua orodha ya watu waliopoteza maisha.”

“Sisi tuliingilia kati mgomo huu kwa nia njema ya kutapata suluhu kati ya madaktari na serikali…lakini baada ya taarifa zetu kutoka kwenye vyombo vya habari Ikulu ilitoa tamko la kukataa kukutana na sisi... ...lakini Ikulu walieleza vizuri kwamba hawajawahi kukataa kukutana na viongozi wa madaktari kwa maana hiyo basi serikali imeonekana dhahiri kutaka suluhu. Baada ya taarifa hizo sisi tuliwatafuta viongozi wa MAT ambao tuliwaeleza kwamba kutokana na taarifa hizo wao waombe msamaha kwa serikali na umma wa watanzania kwa kuendesha mgomo ambao umesababisha vifo. Lakini baada ya kuwaeleza hivyo hawa viongozi wa MAT hawakukubali…sisi kama viongozi ambao lengo letu ilikuwa kutafuta suluhu tukaona hawa vijana (madaktari) wana nia mbaya. Lakini sisi si kujitoa tu bali tutawafungulia mashtaka ya mauaji wote walioshiriki katika mgomo huo. Tutafanya hivyo ili fundisho kwa wengine ambao wana nia kama za madaktari wanaoendesha migomo.

Kwa hiyo sisi tunaunga mkono kufikishwa mahakamani kwa Rais wao ni njia sahihi kabisa ya kurudisha nidhamu, lakini pia tunaunga mkono matamko yote yaliyotolewa na serikali dhidi ya madaktari,”alisema Mwaipopo.

Akijibu hoja hizo, Katibu wa MAT, Dkt. Edwin Chitage amesema hawaogopi kufikishwa mahakamani na kwamba wao waliwapokea viongozi hao kwa nia njema wakiamini ni viongozi wa dini.

“Kama wamesema watatufikishwa mahakamani wao waende halafu tutakutana nao…sisi tuliwapokea kwa nia njema kabisa kwa sababu walituomba wenyewe..lakini baada ya kikao cha Jumamosi siku ya Jumapili wakatupigia simu kuomba tukutane nao,sisi tulikutana nao lakini cha kushangaza walitueleza kwamba wamepigiwa simu na mtu wa Ikulu akiwataka kutuambia kwamba inabidi tuandike barua ya kuomba msamaha halafu tuwape wao ili waipeleke…sisi tulishangaa jambo hili… sisi hatutafanyi kazi hiyo,” alisema Dkt.Chitage.

Chanzo: http://www.wavuti.com

Wednesday, July 11, 2012

MGOMO:Madaktari 319 wafutiwa leseni

BARAZA la Madaktari Tanganyika limewafutia usajili madaktari wote waliokuwa katika mafunzo ya vitendo  (Internship), baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mgomo wakiwa kazini.Taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa Dar es Salaam jana imeeleza kuwa madaktari 319 wamepoteza sifa ya kuendelea na taaluma hiyo hivyo usajili wao umesitishwa rasmi kuanzia jana.Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk Donan Mmbando amewataka madaktari hao kurudisha hati zao za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari.

“Kwa kuzingatia masharti ya sheria kuhusu kupata usajili wa muda, Baraza la Madaktari Tanganyika limeridhia kwamba madaktari wote ambao walijihusisha na mgomo, wamepoteza sifa na kwa sababu hiyo usajili wao umesitishwa kuanzia tarehe 11 Julai, 2012.”

“Madaktari wote wanaohusika wanatakiwa kurejesha hati za usajili wa muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari kabla ya terehe 17 Julai, 2012.”

Dk Mmbando alisema, awali Baraza hilo lilipokea malalamiko kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwamba baadhi ya madaktari waliopata usajili wa muda ili kuwawezesha kufanya mafunzo kwa vitendo (Internship), waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kati ya Juni 23 na Juni 29 mwaka huu.

Alisema madaktari hao walipangiwa kutoa huduma katika Hospitali za Muhimbili, KCMC, Rufaa Mbeya, Sekou Toure na Bugando za Mwanza, Amana, Temeke na Mwananyamala za Dar es Salaam, Haydom - Arusha, St Francis-Ifakara na Dodoma.

Alisema kutokana na mgomo huo, uongozi wa hospitali husika uliwaandikia barua iliyomtaka kila daktari aliyeshiriki kwenye mgomo huo kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.Dk Mmbando alisema kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa kwenye Baraza hilo, Msajili wa Baraza, alimwandikia kila daktari aliyelalamikiwa Taarifa ya Kusudio la kufanya Uchunguzi dhidi yake, juu ya malalamiko yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Alisema baada ya kuyafanyia kazi malalamiko hayo, Baraza limebaini kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madaktari, Sura ya 152, madaktari waliokuwa kwenye mgomo na ambao kwa sasa wameondolewa katika hospitali walizokuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo, wamepoteza sifa za kupata usajili wa muda.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk Edwin Chitage alisema alikuwa hajapata rasmi taarifa hizo licha ya kusikia fununu... “Sijapata taarifa rasmi lakini ni jambo tulilolitarajia na hatutashangaa tukisikia hilo kwa sasa subiri nithibitishe halafu nitatoa msimamo wetu.”
Kiongozi wa madaktari kortini

Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kudharau amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ya kuwataka kusitisha mgomo kupitia vyombo vya habari.

Amri hiyo ilitolewa Juni 22, mwaka huu na Jaji Sekela Moshi na kuwataka madaktari kurejea kazini mara moja, lakini amri hiyo haikutekelezwa.

Jana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alimsomea Dk Mkopi hati ya mashtaka na kumweleza Hakimu Faisal Kahamba kuwa kati ya Juni 26 na 28, mwaka huu, Dk Mkopi akiwa Rais wa MAT, alidharau amri  iliyotolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi Juni 26, mwaka huu ikimtaka kutoa tangazo kwa wanachama wa chama hicho kupitia vyombo vya habari kwamba wasishiriki katika mgomo.

Kweka alidai kuwa Juni 27, mwaka huu Dk Mkopi aliwashawishi wanachama kushiriki kufanya mgomo kitu ambacho ni kinyume na amri iliyotolewa Juni 26, mwaka huu.

Hata hivyo, Dk Mkopi alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kiongozi huyo wa madaktari yupo nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8, mwaka huu itakapotajwa na kuangaliwa kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.

Afya ya Dk Ulimboka
Wakati huo huo, afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imezidi kuimarika.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage alisema jana kwamba: “Tofauti na ilivyokuwa mwanzo, kwa sasa afya yake imezidi kuimarika, anakula mwenyewe lakini pia anazungumza mwenyewe na rafiki zake wa hapa nchini kwa  njia ya simu.”

Katika siku za karibuni, hali ya Dk Ulimboka ilielezwa kubadilika ghafla na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kutokana matatizo mbalimbali, yaliyotokana na kupigwa ikiwamo figo kushindwa kufanya kazi.

Alisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi Juni 28, mwaka huu kwa ushauri uliotolewa na jopo la madaktari lililokuwa likimhudumia.

UN yanena
Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Dk Alberic Kacou amepokea barua ya MAT kuomba ulinzi kwa Dk Ulimboka anayeendelea na matibabu Afrika Kusini kwa madai kuna kikosi kilichotumwa kuhakikisha harudi nchini akiwa hai.

Akizungumza jana Dar es Salaam jana, Dk Kacou alisema suala hilo la kutoa ulinzi watalitoa baada ya kuwasiliana na wote waliohusishwa kwenye waraka wa ombi hilo.

Mgomo wamalizika
Mgomo uliokuwa ukiendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Mifupa (Moi), Dar es Salaam umemalizika na huduma katika hospitali hizo zimerejea kama kawaida jana.

Waandishi wa habari waliotembelea hospitali hizo waliona wagonjwa wakiwa wanaendelea kupokewa na kupatiwa huduma kama ilivyokuwa awali, kabla ya mgomo uliodumu kwa takriban majuma mawili yaliyopita
Habari hii imeandikwa na Tausi Mbowe, Tausi Ally, Leon Bahati na Issa Lazaro, Geofrey Nyang’oro

SEMINA: Je,Ukatili wa Kijinsia ni Suala la Kikatiba?


SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

 UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII KIWOHEDE  WATAWASILISHA

MADA: Je,Ukatili wa Kijinsia ni Suala la Kikatiba? 

Lini: Jumatano Tarehe 11/7/2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA