KAMBI ya Upinzani Bungeni imewasilisha Bajeti mbadala ya mwaka 2011/12 ya Sh. trilioni 14.16, huku ikipendekeza mchakato uanze ili kila Mtanzania awe anajaza fomu za kodi kila mwaka, kwa sababu kuna wengi ambao wanapata mapato makubwa lakini hawalipi kodi.
Hata hivyo, bajeti hiyo mbadala kwa kiasi kikubwa, imebeba mambo mengi ambayo yamependekezwa na Serikali katika Bajeti ya Mwaka 2011/12 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16). Bajeti ya Serikali ni ya Sh Trilioni 13.52.
Akiwasilisha bajeti hiyo jana, Waziri Kivuli wa Fedha, Kabwe Zitto, alitoa mfano wa watu wasiolipa kodi, akisema wenye nyumba za kupangisha mijini, wanapata fedha nyingi na wengine hutoza kodi ya pango kwa kutumia dola za Marekani, lakini hawalipi kodi ya mapato.
“Watu hawa hutumia barabara na huduma nyingine za umma ambazo gharama zake zinatokana na kodi lakini hawalipi kodi. Kambi ya Upinzani inapendekeza kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Majengo (RERA) na kila mwenye nyumba ya kupangisha atambuliwe na kulipa kodi inavyostahili,” alisema Zitto.
Kuhusu kurekebisha kodi, alisema wanapendekeza ushuru wa bidhaa kwenye bidhaa za mafuta upunguzwe kwa asilimia 40 na tozo nyingine zote kwenye mafuta zipunguzwe kwa asilimia kama hiyo pia.
Aidha, walipendekeza kufuta msamaha wa kodi kwenye mafuta kwa kampuni za madini na kampuni za ujenzi, kwani imethibitika kuwa msahama huo unasababisha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Zitto alisema pia wanapinga mapendekezo ya sasa ya kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji wa mafuta na gesi.
“Kambi ya Upinzani inapendekeza pia kuwianisha viwango vya bei ya mafuta ya taa na ya mafuta ya dizeli na petroli, ili kudhibiti uchakachuaji wa mafuta ambao unaligharimu Taifa fedha nyingi na kuleta uharibifu mkubwa,” alisema Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Eneo lingine walilopendekeza wapinzani ni marekebisho ya kushusha kiwango cha chini cha Kodi ya Lipa kwa Kadri Unavyopata (PAYE) mpaka asilimia 90 na kiwango cha juu mpaka asilimia 27.
Kuhusu ada za leseni za biashara, Zitto alisema wanataka kurejeshwa kwa leseni za biashara ndogo licha ya kuongeza mapato ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji, ambako kutarejesha ugumu wa kufanya biashara; hivyo kushauri uamuzi huo uangaliwe upya.
Alipendekeza magogo yote yanayosafirishwa nje ya nchi yalipiwe kodi, huku ikiipongeza Serikali kwa kukubali wazo la kupunguza misamaha ya kodi mpaka kufikia asilimia moja ya Pato la Taifa.
Katika umeme, alisema umefika wakati sasa kutangaza kuwa umeme ni janga la Taifa na Bunge lipitishe Azimio la Uzalishaji wa Umeme kwa viwango vya Mpango wa Maendeleo na kuweka adhabu ya kumfukuza kazi Waziri iwapo miradi hiyo haitakuwa imekamilika kila mwaka.
Kuhusu posho, alisema Kambi ya Upinzani inapendekeza mfumo mzima wa kulipana posho za vikao katika utumishi wa umma uondoke, na kwamba hawapingi posho za kujikimu ambazo viongozi au maofisa wa umma hulipwa wanaposafiri nje ya vituo vyao vya kazi.
“Posho hizi zirekebishwe kuendana na gharama za maisha za sasa. Lakini posho za vikao zifutwe mara moja. Ili kuonesha kuwa viongozi wa kisiasa tunaelewa kilio cha wananchi kuhusu gharama za maisha na kupunguza matumizi ya Serikali, waheshimiwa Wabunge tunaanza na posho za vikao vya Bunge.
“Iwapo sisi tukiendelea kujilipa posho za kukaa humu ndani na kwenye kamati zetu, tunakuwa tunatoa ruhusa kwa watumishi wa Serikali kulipana posho hizi na hatutakuwa na mamlaka ya kuhoji na kuwawajibisha,” alisema Zitto.
Akizungumzia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), alipendekeza irudi tena katika biashara, huku akishauri Serikali iangalie uwezekano wa kurekebisha umiliki wake kwa kuhusisha taasisi za umma ambazo zinafaidika kwa kuwapo shirika hilo moja kwa moja.
“Kambi ya Upinzani Bungeni inapendekeza ufanyike uchunguzi maalumu kwenye Deni la Taifa ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atwambie madeni haya tunayokopa kwa kasi ya namna hii, tunayapeleka kwenye miradi gani na namna gani tunaweza kudhibiti Deni la Taifa,” alisema Zitto akizungumzia deni hilo ambalo sasa ni dola za Marekani bilioni 11.4.
Katika vipaumbele vya Bajeti, wapinzani wanapendekeza kuondolewa kwa ‘mashangingi’ ya mawaziri na badala yake wakopeshwe magari; kufutwa kwa ada za shule kwa wanafunzi wa kutwa, kuongeza kima cha chini cha mshahara wa mtumishi wa umma hadi Sh 315,000.
Zitto alimpongeza Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, kwa kusikiliza maoni yao kwa baadhi ya mambo na kuyazingatia katika bajeti yake, hivyo kuonesha umma moja ya faida ya mfumo wa vyama vingi.
“Tunatarajia kuwa Serikali itaendelea kusikiliza maoni yetu na kuyafanyia kazi. Changamoto hii ni kwa uzito ule ule pia, ipo kwetu sisi wa Kambi ya Upinzani kusikiliza pia maoni ya Serikali,” alisema.
No comments:
Post a Comment