Monday, June 6, 2011

Wanasheria kuandaa rasimu ya Katiba

CHAMA cha Wanasheria wa Tanzania Bara (TLS) kinaandaa rasimu yake ya Katiba mpya kwa ajili ya kushawishi mabadiliko muhimu ya Katiba.

Aidha, kimezindua rasmi Kamati Maalumu ya Katiba itakayoandaa rasimu hiyo pamoja na masuala mengine mbalimbali yanayohusu mchakato mzima wa Katiba mpya.

Akizindua kamati hiyo ya watu wanane Dar es Salaam jana, Rais wa TLS Francis Stolla alisema wajumbe wake walichaguliwa kwa kuzingatia vigezo muhimu pamoja na uhitaji wa mchango wa chama hicho katika Katiba mpya.

“TLS inapaswa kuonesha mchango mkubwa katika mchakato wa Katiba mpya, ndio maana mkutano wetu wa mwaka wa Februari mwaka huu uliona umuhimu wa kuwa na Kamati Maalumu itakayoshughulika na mchakato wa Katiba pekee.

“Kwa sababu hiyo, tulifanya uchaguzi wa kina na kupata wajumbe wenye vigezo vyote watakaofanya kazi hiyo kwa karibu na Baraza la Uongozi la chama lenye wajibu wa kuishauri Serikali, kamati za Bunge na Mahakama kuhusu masuala ya kisheria na yenye maslahi kwa Taifa,” alisema.

Wajumbe hao ni Godwin Ngwilimi, Daimu Halfani, Fatma Karume, Dk. Angelo Mapunda, Dk. Tulia Ackson, Athanasia Soka, Alute Mughwai na James Jesse ambao wote ni mawakili.

“Hatujamchagua Mwenyekiti wa Kamati hadi sasa lakini wajumbe watafanya hivyo mara watakapokutana, kabla ya kuanza rasmi kazi yao,” alisema Stolla.

Akieleza majukumu mengine ya kamati hiyo yatakayotekelezwa kulingana na hadidu za rejea zitakazotolewa na Baraza la Uongozi la TLS, Stolla alisema ni pamoja na kulishauri baraza hilo kuhusu mambo muhimu ya kuishauri Serikali kuhusu Katiba mpya.

Mengine ni kuchambua na kujumuisha mapendekezo ya wananchi juu ya Katiba mpya ambayo hutumwa kwa TLS kupitia mawasiliano ya aina mbalimbali, kuhakikisha jamii inaielewa vyema Katiba iliyopo na kutumia nafasi iliyopo kushiriki mchakato huo.

Akifafanua kuhusu rasimu hiyo, Stolla alisema itabeba mambo yanayotakiwa kujumuishwa katika Katiba mpya kama ushawishi kwa wahusika kuyaingiza kwenye majumuisho ya rasimu kuu ya Katiba na kueleza kuwa haina maana kuwa ndiyo itakuwa rasimu yenyewe ya Katiba.

No comments: