Tuesday, September 16, 2014

Ratiba ya Bunge Maalum la katiba kuanzia Septemba 16 hadi Oktoba 4, 2014Ratiba ya Bunge Maalum la katiba kuanzia Septemba 16 hadi Oktoba 4, 2014

Mwenyekiti wa bunge Maalum la Katiba mh. Samuel Sitta amesema Oktoba 4 bunge maalum la Katiba litakamilisha rasmi kazi ya kutoa rasimu ya Pili ya Katiba itakayokabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar itakayopigiwa kura na wananchi katika Serikali ya awamu ya 5.
Amesema kamati ya uandishi wa KATIBA itaendelea kuanzia leo Septemba 16  hadi jumatatu Septemba 22 ambapo rasimu ya pili ya katiba itawasilishwa bungeni ambapo Septemba 23, 24 na 25 wajumbe wa bunge Maalum la KATIBA watahakiki rasimu hiyo kuangalia Kama masuala yote yaliyopendekezwa na wabunge hao yameingizwa Kama walivyokubaliana.
Kamati ya uandishi itaendelea kufanya marekebisho ya rasimu ya KATIBA hiyo Septemba 26 na 27 na Septemba 28 wajumbe wote wanatakiwa kukutana katika kamati zao kujielimisha kuhusu rasimu ya pili ya KATIBA mpya.
Septemba 29 ni siku ya wajumbe hao kupiga kura kuipitisha rasimu ya KATIBA hiyo ambayo itakabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar tayari kwa hatua ya kupelekwa kwa wananchi kupigiwa kura katika serikali ya awamu ya Tano baada ya uchaguzi Mkuu 2015.

Monday, September 15, 2014

TGNP Mtandao yapeleka vuguvugu la katiba Mpya vijijini
 TGNP Mtandao wiki hii utaendesha semina za kuwajengea uwezo wananchi wa vijijini juu ya hali halisi ya mchakato wa katiba ulipofikia na namna ya wao kuendelea kuufuatilia na kuchukua hatua.

Lengo ni kuwaeleza wananchi juu ya kuendelea kufuatilia mchakato wa katiba mpya hatua kwa hatua ili kuhakikisha wanalinda masuala yao muhimu yaliyoko kwenye rasimu ya pili yasiondolewe au kutupiliwa mbali.

Akizungumza mratibu wa mradi huo kutoka TGNP Anna Sangai alisema kuwa TGNP baada ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na kuendesha mabaraza ya katiba ya kitaasisi imeona kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea uwezo wananchi waweze kuendelea kufuatilia mchakato huu  hatua kwa hatua, kuendelea kudai masuala ya haki za wanawake  na makundi yaliyoko pembebozoni yanapata nafasi ya kuingizwa kwenye katiba mpya.

“Tunaandaa mikutano mikubwa miwili vijijini  kufuatia hali halsisi ya mchakato wa katiba hivi sasa. Tutawakutanisha wanawake na wanaume  vijijini kuweka uelewa wa pamoja juu ya mchakato wa katiba mpya,  na kuendesha mijadala ya wazi (GDSS) ili kuwapa wananchi fursa ya kupaaza sauti zao juu ya kile wanancho kiona katika mchakato huu”alisema na kuongeza:
“Hatuwezi kuwapeleka watu wote Dodoma kushinikiza masuala yao yaingizwe na kama tunavyojua Bunge linaahirishwa Oktoba 4, lakini kila mmoja akipata uelewa anaweza kupaaza sauti yake pale alipo na akasikika”

Sangai alisema kuwa semina zitaendeshwa kwenye vituo vya taarifa na maarifa ambavyo vitachaguliwa katika wilaya za Mbeya Vijijini, Morogoro Vijijini, Kishapu, Bagamoyo, Kisarawe na Maneromango.

 Pia katika mikutano hiyo ya wazi itakayowashirikisha wananchi wote wa kata husika  wanaharakati hao watajadili juu ya kuhakikisha sauti za wananchi waliko pemeboni zinapata nafasi, kujadili namna watakavyoshiriki mchakato unaofuata ukiwepo kura za maoni,  kujadili hatima ya katiba mpya na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.


Friday, September 12, 2014

Uwasilishwaji taarifa za kamati Bunge Maalum la Katiba; Je, Masuala ya Kijinsia yamezingatiwa?MTANDAO WA JINSIA TANZANIA - (TGNP)  
GDSS 10/09/2014
MADA; Uwasilishwaji taarifa za kamati Bunge Maalum la Katiba; Je, Masuala ya Kijinsia yamezingatiwa?
Mtoa Mada: TGNP Mtandao na Timu ya ufuatiliaji na uchambuzi (MAT)
Mchakato wa kutafuta katiba mpya unaendelea mjini Dodoma kwa wajumbe wa Bunge maalum la Katiba katika kuwasilisha mapendekezo ya mijadala yao kutoka kwenye kamati zao. Kamati zote 12 zimepata fursa ya kuwasilisha maoni ya waliowengi na hata wachache ambao kwa namna moja ama nyingine walishindwa kukubaliana katika baadhi ya mambo.
Kulingana na uwasilishwaji wa taarifa za kamati zimeibuka hoja nyingi zenye kuleta mustakabali mzuri kama taaifa. Licha ya hoja tata kama muundo wa serikali ya muungano, na mambo mengine yenye msisimko wa kipekee kwenye rasimu ya katiba pendekezwa na Tume ya kukusanya maoni iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Walioba.
Katika mchakato wa katiba moja ya madai ya msingi kabisa ni usawa wa kijinsia kikatiba, wananchi wanapendekeza katiba yenye mrengo wa kijinsia (Gender Sensitive Constitution). Lakini itapendeza tukikumbushana dhana ya usawa wa kijinsia kabla ya kujadili hoja iliyo mbele yetu juu ya katiba na masuala ya kijinsia. Usawa wa kijinsia “ni hali ya mwanamke na mwanaume kuwa na fursa sawa na upatikanaji wa haki zenye kuleta tija, katika Nyanja mbalimbali za maendeleo ya Jamii, kati ya makundi haya mawili”.
Kwa nini usawa wa kijinsia uwepo katika katiba mpya?
Katiba ni sheria mama inayolinda haki za raia wote (wanawake na wanaume na watoto) nchini, na kuhakikisha mfumo wa kuendesha nchi na wajibu wa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza. Hivyo ni muhimu sheria hii mama iwe imebeba masuala au haki za makundi haya mablimbali nchini kwa kudumisha maendeleo yenye tija.
Wote tunatambua jitihada  za TGNP na asasi nyingine za kiraia kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha katiba ya wananchi inapatikana yenye kubeba msingi kuu wenye mrengo wa kijinsia. TGNP kwa kushirikiana na Mtandao wa wanawake ana Katiba (WFT) Ilitoa mapendekezo ya msingi kabisa yanayotakiwa kuingizwa kwenye rasimu na klatiba mpya ili kuleta msingi wa usawa wa kijinsia katika nyanja zote. Kulingana na mapendekezo hayo na mchakato wa katiba mpya unaoendelea, napenda sasa tujadili kwa pamoja;  je uwasilishwaji huu wa mapendekezo umezingatia masuala ya kijinsia?
Kulingana na mawasilisho yote ya sura zilizoweza kuwasilishwa baadhi ya mambo yamejitokeza katika ibara mbalimbali pia maeneo mengine yako kimya kabisa kama ifuatavyo;
Haki ya mtoto ibara ya 43(2), wajumbe wamependekeza iweke tafsili rasmi ya nani ni mtoto? Kwa kuzingatia zaidi haki za mtoto wa kike, ulinzi na usalama wake. Wajumbe walio wengi wamependekeza tafsili ya mtoto iwekwe bayana kikatiba. Isomeke wazi - mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakaowezesha utekelezaji na usimamizi wa haki za mtoto, hususani mtoto wa kike.
Pia, Ibara ya 44 inayotambulisha haki na wajibu wa kijana katika shughuli za maendeleo. Mapendekezo ya wachache yameonyesha kwa kiasi kikubwa jinsi ibara hii ilivyo jumla jumla, aidhi kukosekana kwa dhana inayonyambua na kuonyesha jinsi zote mbili. Hivyo kamati zimeshindwa kutoa pendekezo msingi itakayobainisha haki na wajibu wa kijana katiaka kujiletea maendeleo. Bila kusahau pendekezo muhimu litakalo tambua “vijana kufaidi fursa na haki sawa; kuwa na usawa katika kufikia na kumuliki rasilimali na usawa katika ulinzi”.
Vile vile, haki ya mtu mwenye mlemavu, limezungumzwa Kwa uzito wake ikiwemo haki ya kutobaguliwa, kupata huduma za Jamii Kama wengine, kulindwa juu ya vitendo vya unyanyasaji, ukatili na kuabaguliwa. Lakini haki ya mwanamke mweleulemavu zimepewa nguvu sana na walemavu wenyewe na si wajumbe kutoka makundi mengine. Hivyo basi wabunge wote bila kujali nakundi yao inatakiwa kwa pamoja kutetea haki za walemavu kikatiba has haki za wanawake walemavu kikatiba.
Suala la Katiba kutambua usawa wa jinsia katika umiliki wa rasilimali na kutumia. Ibara mpya inayounda Tume ya taifa ya ardhi itakayo hakikisha misingi na falsafa ya umiliki wa ardhi inazingatia usawa wa kijinsia katika matumizi ya ardhi imependekezwa na kamati zilizo nyingi. Suala hili ni zuri kwasababu limeweka bayana dhamira ya katiba kufikia usawa wa kijinsia kwa kumpa mwanamke fursa ya kutumia rasilimali. Ibara hii ikipitishwa itampa mwanamke fursa ya kujitegemea kiuchumi kwa kutumia ardhi. Hata hivyo, tunaona  kwamba ibara hii haijafafanua mbinu au utaratibu utakaotumika na Tume katika kuzingatia usawa na nafasi ya mwanamke katika mgawanyo wa hizo rasilimali. Pia, ibara hii itamke bayana kwamba wanawake wanahaki ya kumiliki ardhi isiyo hamishika, ikiwemo ardhi ya ukoo na haki ya kurithi. Itambulike kuwa, takribani 5% tu ya wanawake wanafanya kazi ya kilimo ya ardhi chini ya miliki yao, 44% ya wanawake wanafanya kazi ya kilimo katika ardhi inayo milikiwa na waume zao na 35% ya wanawake wanafanya kazi katika ardhi inayomilikiwa na ukoo. (chanzo: Dailynews.co.tz/index/php/feature/24296-tanzania).
Wajumbe wamependekeza iundwe tume ambayo itakua kituo kikuu cha serikali itakayoratibu na kusimamia masuala yote yanayohusu usawa wa jinsia na maendeleo ya jinsia.Tume hii itapewa nguvu kusimamia masuala ya upangaji wa jinsia katika mipango yote ya Taifa. Imependekezwa ibara namba 214 iongezewe kipengele (a)Itakayosomeka,kutakua na tume ya jinsia itakayoongozwa na mwenyekiti  na makamu mwenyekiti na wajumbe wasiopungua watano; 2. Majukumu yatakua ni pamoja na kuendeleza, kulinda na kutetea haki na usawa jinsia na kutoa taarifa yake bungeni angalau mara moja kwa mwaka. Na mwisho bunge litatunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa ibara hii.
Hata hivyo wajumbe waliwasilisha mapendekezo kuhusu usajili wa Vyama vya siasa kwamba ili chama cha siasa kiweze kusajiliwa lazima kioneshe suala la usawa wa kijinsia katika taratibu za uendeshwaji wake. Katika sura ya 12(a) ibara ya 197 inayozungumzia juu ya usajili wa vyama vya siasa pia kusisitiza katiaka uteuzi wa masajili wa vyama vya siasa uzingatie usawa wa kijinsia ili kutekeleza usawa katika uongozi unaozingatia jinsia zote sawa.
Wajumbe pia,  walitoa mapendekezo kuhusu kuwa na Tume huru na ya haki ya Uchaguzi kwa kupendekeza kwamba uteuzi wake uzingatie usawa wa kijinsia na walemavu kutoka pande mbili za Jamuhuri ya muungano, ibara ya 190 na 191 na fasili zake zote. Wamependekeza iwepo ibara maalum inayotamka bayana juu ya uteuzi unaozingatia swala hili. Pia mapendekezo yamezingatiwa wajumbe ambao watajiliwa kusimamamia tume ya uchaguzi wasiwe wanajihusisha na chama chochote cha siasa ili kuepusha ukosefu wa haki na usawa wakati wa uchaguzi.
Katika kutetea haki na usawa wa kijinsia katika utumishi wa umma, kamati zilizo nyingi zimepedekeza kuwa usawa wa kijinsia utambulike kuwa moja juu ya ajira na uteuzi wa Viongozi wa taasisi katika serikali kutambua usawa wa kijinsia. Hivyo basi katika ibara ya 185 (1) iongezwe fasili inayo beba dhana ya usawa wa kijinsia katika uteuzi wa viongozi na wa taasisi za kiserikali ili kufikia malengo kama taifa ya 50/50 katika nafasi za utumishi wa umma.
Pia katika ibara ya 186(3)inayotoa sifa za Mwenyekiti na Wajumbe katika Tume ya Utumishi wa Umma, katika uteuzi wa wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Umma itakayo undwa na Rais, fasili inayotambua uzingatiaji wa usawa wa kijinsia iongezwe na kuwa fasili (e) katika ibara hii . hii ni kutokana sifa pendekezwa hazitoi fursa sawa kwa jinsia na usawa wa uwakilishi wa jinsia.
Katika uteuzi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, rasimu ya katiba haijasema wazi juu ya usawa wa jinsia kwani pia wanawake wanstahiri kuteuliwa katika nafasi nyeti na muhimu kama ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama. Mapendekezo yote ya kamati hakuna hata moja iliyosema kuwa jinsia izinagatiwe katika taasisi hizi za serikali bali walijikita zaidi katika uwianao sawa wa pande mbili za muuungano. Ibara ya 240,245 na 249 ziko kimya kabisa juu ya haki hii ya msingi kwa wanawake katika idara hizi. Pia kuna changamoto kubwa sana pia kuwa idara ya Magereza imesahaulika kabisa; haijatajwa kwa kuzingatia ni taasisi muhimu sana katika maswala ya ulinzi na usalama wa raia katika Taifa letu.
Huduma bora ya afya ibara ya 47(1) rasimu haukunyumbua vilivyo fasili hii iliyobeba uhai na usalama wa wananchi juu ya mazingira bora kiafya. Wajumbe wamepndekeza kifungu hiki kiongezewa uzito kwa kutamka wazi haki ya uzazi salama,kupata huduma bora ya afya kutambulika kikatiba. Katiba itunge fasili inayolipa  Bunge nguvu ya kutunga sheria itakayoweka  msingi muhimu  ya haki ya uzazi  salama kwa kuhakikisha huduma hizi zinatolewa bure, zenye ubora na usalama wa miindombinu ambayo ni rafiki pia kuwalinda wajawazito na kazi ngumu ambazo zinaweza hatarisha usalama wa afya ya mama na mtoto aliyetumboni. Vilevile kuzingatiwa kwa uzazi salama kwa walemavu, lugha za kibaguzi, mazingira rafiki kimiundombninu inawafanya wakati mwingine kupata rapsha zisizokuwa na sababu katika hali nguvu waliyokuwa nayo.
Kwa kiasi fulani, masuala ya kijinsia yamezingatiwa kwenye uwasilishaji na kutiliwa mkazo wakati wa majadiliano ya mjumbe mmoja mmoja yanayoendelea. Kuna changamoto bado katika kuyazungumzia maswala haya kwa kutetea haki na usawa wa kijinsia, maswala hayo hayajazungumzwa kwa undani unaotakiwa ukilinganisha na mapendekezo yaliyotolewa na asasi mbalimbali zinazotetea haki za wanawake ikiwepo Jukwaa la Wanawake na katiba kwa mfano uundwaji wa chombo cha kitaifa kitakacho ratibu masuala yote yahusuyo jinsia ambayo itakuwa mkombozi na mtetezi wa masuala ya kijinsia ikisaidiwa na asasi za kiraia na mashirika yanayotatea kimataifa. Kulingana na mwenendo wa Bunge bado inahitajika kuendelea kusisitizia kwa mkazo mambo haya na kumpa mwanamke heshima anayo stahili.haya ni baadhi ya masuala machache tuu kati ya yale yaliyogusiwa, pia  yapo mengi hayakuguswa juu haki na usawa wa kijinsia.

Hali kadhalika uwasilishwaji wa ibara ya 98 imesahau kabisa haki sawa ya uteuzi licha ya swala la ubunge na uwaziri, ibara hii ibainishe misingi ya haki kijinsia katiba uteuzi wa nafasi hizo na kuleta uwiano wa kijinsia (50/50%) katika nafasi hizo.
Katika suala la Uteuzi wa majaji, kamati nyingi zimeshindwa kuonyesha jinsi usawa wa kijinsia ulivyo zingatiwa. Tungependa kuona usawa wa asilimia hamsini kwa hamsini katika uteuzi wa majaji.

MAJADILIANO YA MAPENDEKEZO YA KAMATI BUNGE MAALUM LA KATIBA KIKAO CHA 36-37MTANDAO WA JINSIA TANZANIA - (TGNP)  
  MAJADILIANO YA MAPENDEKEZO YA KAMATI BUNGE MAALUM LA KATIBA      
 KIKAO CHA 36-37
Katika bunge la 36 na 37 lilianza rasmi kujadili rasimu ya katiba na Mwenyekiti wa bunge maalum la katiba mheshimiwa Samwel Sitta aliwaelekeza Wajumbe kujikita katika  majadiliano kwa kuzingatia sura ya 9 na 15 ambazo zinahusu Kuundwa na madaraka ya bunge la jamhuri ya muungano na Ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano, sambamba na kujadili sura mpya ambayo haikuwepo katika rasimu nayo ni  sura ya uchumi na maendeleo, utawala,Muundo wa serikali na muungano. Haya ndiyo maeneo walioelekezwa wajumbe kujikita katika majadiliano yao na kujenga hoja ambazo zinagusa maeneo hayo .
 Mwelekeo wa majadiliano ulijikita zaidi kwenye masuala yafuatayo: Wajumbe wengi walipendekeza kuwepo na kipengele ambacho kitatambulika kikatiba ambacho kitaruhusu haki ya kugoma kama wafanyakazi au watu wengine wowote ambao watakua na sababu za msingi za kufanya hivyo, mgomo wao utambulike kuwa halali na bunge litatunga sheria itayoongoza uwepo na usimamizi wa kipengele hicho.Na hii inaweza kuwekwa chini ya ibara ya 36 ambayo inazungumza juu ya haki ya mfanyakazi.

Hata hivyo, wajumbe walionekana kuelekeza majadiliano yao kwenye Ibara ya 47ambayo inazungumzia  haki ya mwanamke wakiongozwa na Mheshimiwa, Avemarie Semakafu na Doreen Maro, wajumbe walipendekeza kiongezwe  kipengele (h) ambacho kipekee kitazungumzia haki ya  kupata huduma bora na salama ya uzazi bure ili kuepusha vifo vingi vinavyotokana na ujauzito. Pia wajumbe walipendekeza kiongezwe kipengele (i) ambacho kitazungumzia haki ya mwanamke mjamzito kulindwa na kazi ngumu zinazohatarisha maisha yake na ya mtoto aliye tumboni. Na ili kulisimamia hili bunge litatunga sheria ambayo itasimamia na kuelekeza utekelezaji wa haki hii.
 Hoja nyingine iliyozungumzwa sana ni kuhusu suala la mahakama ya kadhi kwa Waislamu, suala hili lilijadiliwa sana  na wajumbe waliowengi na wajumbe walitofautiana, lakini wengi walipendekeza kwamba suala la mahakama ya kadhi libaki chini ya ibara ya 32 ambayo inahusu uhuru wa imani ya dini kwani taifa letu halina dini na kama tutaanza kuingiza masuala ya dini kwa upande mmoja katika  katiba tutakua hatujawatendea haki upande mwingine ambao ni wa wakristo.
Vilevile suala la  Haki ya mtoto lilijadiliwa sana na wajumbe walio wakiongozwa na Mheshiwa:Mary Mwanjelwa, Avemarie Semakafu, Askofu Thomas Maige, Paul Mapunda, wengi walipendekeza kuwepo na kipengele ambacho kitafafanua mtoto ni kuanzia miaka mingapi, ili kuondoa tatizo la unyanyasaji kwa watoto suala ambalo limekua sugu katika taifa letu na limeathiri watoto wengi.
Suala la 50/50 nalo lilizungumzwa sana na wabunge walio wengi wakiongozwa na Mheshimiwa: Doreen Maro,Faustina, na kukubaliana litambulike na liingizwe katika katiba na bunge litatunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa suala hili. Suala hili linaweza kuongezewa kipengele chini ya ibara ya 47 ambayo inazungumzia masuala ya haki za wanawake.
Kwa kiasi kikubwa majadiliano yaligusa masuala mbalimbali ya kijinsia na wajumbe waliowengi walionekana kuwa na uelewa kuhusu masuala ya jinsia maana kila mara mjumbe aliposimamam kuelezea hoja Fulani alikua akitamka maneno uwiano wa kijinsia,jinsia na uzingatiaji wa makundi yote.Hivyo basi hii inatoa taswira ya jitihada ya mapendekezo yaliyotolewa na asasi mbalimbali zinazotetea haki za wanawake ikiwepo Jukwaa la Wanawake na Katiba.