JAJI mstaafu Mark Bomani, amesema wakati wa kujadili Katiba mpya, Watanzania hawataepuka kuzungumzia mfumo wa Rais, awe Rais mtendaji au asiye mtendaji na nani asimamie mamlaka ya utendaji wa Serikali.
Bomani pia alitaka Watanzania wajadili kwa kina kila kitu bila uoga, ikiwemo muundo wa Muungano, uwe wa Serikali mbili, moja au tatu.
Alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la maadili ya wanahabari kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoandaliwa na Baraza la Habari nchini (MCT).
Pia alizindua vitabu viwili vilivyochapishwa na MCT vilivyohusu kanuni za maadili kwa wanahabari na Mwongozo wa kuandika habari za mahakamani.
Alisema kila kitu kijadiliwe bila uoga kwani Watanzania wana uzoefu wa kutosha kujadili hata aina ya Muungano na kufikia muafaka.
Pia alipendekeza mjadala wa wazi kuhusu idadi na aina ya mihimili kama vile Bunge, Serikali Kuu, Mahakama na asasi nyingine kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Tume ya Maadili ya Viongozi.
“Suala la haki za binadamu pia lizungumziwe na kuwekewa vifungu vya kutosha,” alisema na kuongeza: “Unapozungumzia mhimili wa Bunge, je uwe na baraza moja tu la Bunge au labda uwe na zaidi ya baraza moja, na kama ni hivyo mabaraza hayo yapatikaneje na mgawanyo wa madaraka uweje.”
Jaji huyo alitaka wakati wa mjadala wa mhimili wa Bunge, Watanzania waamue suala la upatikanaji wa wajumbe wake na kuwe na aina ngapi za wabunge wa kuchaguliwa kwenye majimbo ya uchaguzi au kwa mtindo wa uwiano au njia zote mbili.
Aidha, Jaji Bomani alitaja masuala mengine muhimu kuwa ni ya wagombea binafsi; waruhusiwe au la; mawaziri wawe wabunge au wasiwe; uwepo uwakilishi wa makundi mbalimbali ndani ya jamii na kama hivyo hayo makundi yafahamike.
Hata hivyo alisema mchakato huo ni lazima mjadala wake uanzie mahali fulani na hadidu za rejea zilizo wazi ziwepo na zijulikane ili mjadala uwe na tija.
No comments:
Post a Comment