Friday, January 28, 2011

Kizungumkuti Dowans

-Kikwete atofautiana na Ngeleja, Jaji Werema
-Sitta, Mwakyembe waombwa kutoa mwongozo

RAIS Jakaya Kikwete ametofautiana na kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, akikubaliana na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokimbilia kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, Raia Mwema, imeelezwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, badala yake, Rais ameungana na wabunge hao kutafuta namna ya kuepuka malipo au kuyapunguza kwa kutumia mianya ya kisheria.

Awali, mara baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara kutoa hukumu ikitaka Dowans ilipwe na Tanesco (serikali) shilingi bilioni 94 ikiwa ni faini kwa kuvunja mkataba, AG Werema na Waziri Ngeleja walitoa kauli za kuilipa Dowans endapo tu itasajili hukumu hiyo Mahakama Kuu.

Walitoa uamuzi huo wa kuilipa Dowans bila kueleza nia ya kukata rufaa au mazingira yanayokwamisha ukataji rufaa, huku Waziri Ngeleja akisisitiza kuwa, hatua zozote za kutofanya malipo hayo ni kupoteza muda na kwamba ni kusababisha nchi kutozwa riba.

Uamuzi huo wa Ngeleja na Werema uliungwa mkono na baadhi ya viongozi mashuhuri nchini, akiwamo Jaji Mark Bomani, lakini ukipingwa na wengine wakiwamo wasomi.

Rais atofautiana na Waziri, AG

Sakata hilo la Dowans sasa limechukua sura mpya, likiweka kitendawili hatima ya Waziri Ngeleja pamoja na Mwanasheria Mkuu, Werema.

Wiki hii imependekezwa na wabunge wa CCM katika azimio maalumu kwamba; Serikali isikimbile kulipa na badala yake, mianya ya kisheria ivumbuliwe ili kukwepa malipo au kuyapunguza.

Mapendekezo hayo ni kinyume cha kauli ya Waziri Ngeleja na Jaji Werema. Vitisho vya Ngeleja kwamba kutolipa kwa sasa ni kusababisha nchi kutozwa riba ni kama vimepuuzwa na wabunge hao.

Taarifa za ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika kuanzia wiki iliyopita na kilichomalizika Jumatatu, zinaeleza kuwa Rais Kikwete ameungana na wabunge wa chama hicho, ambao pia Ngeleja ni miongoni mwao.

Msimamo huo wa wabunge hao unaungana na mitazamo ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Kwa nyakati tofauti, tena hadharani viongozi hao walimpinga Ngeleja, kiasi cha kufichua kuwa suala hilo halijajadiliwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, hoja kwamba suala hilo halikuwa limejadiliwa na Baraza la Mawaziri ilipingwa na Ngeleja akisema hakukuwa na haja ya kujadili suala hilo huko kwa kuwa liko wazi mno.

Kauli ya Mwanasheria Mkuu

Wiki hii Raia Mwema liliwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema ili kufahamu mambo mawili katika taswira hii mpya ya Dowans.

Kwanza, madai ya baadhi ya wabunge wa CCM wakati wa mjadala kwamba; amejigeuza msemaji wa Serikali katika baadhi ya masuala badala ya kubaki mshauri.

Kati ya masuala ambayo AG aliyazungumzia kwa vyombo vya habari katika tafsiri inayotajwa kuwa alijigeuza msemaji (mkuu au mwisho) wa Serikali ni suala la Dowans na Katiba mpya. Akisema Dowans italipwa na Katiba mpya hakuna, isipokuwa marekebisho.

Suala la pili katika mawasiliano hayo na AG Werema lilihusu uamuzi wa ofisi yake kutotaka kukata rufaa na badala yake kutaka Dowans ilipwe endapo itasajili tozo (hukumu) yake Mahakama Kuu.

Msingi wa maswali hayo ni uamuzi wa wabunge wa CCM, waliokutana chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, ubungo, jijini Dar es Salaam, Januari 22 hadi 24, mwaka huu.

Akijibu Werema alitoa majibu ya jumla akisema; “Kuhusu hayo ya wabunge wa CCM kwa kweli sikuwapo katika kikao hicho, kwa hiyo bado sijui kumetokea nini au wameazimia nini.

“Lakini kwa sababu chama (CCM) ndicho kinaongoza Serikali basi yakiletwa kwetu (ofisi ya Mwanasheria Mkuu) tutayashughulikia.”

Hatima ya Sitta, Mwakyembe

Kwa mujibu wa mwenendo wa kikao cha wabunge hao wa CCM, hali ya mjadala wa Dowans ilionekana kukera wengi katika malipo yanayopaswa kufanywa kwa kampuni hiyo.

Inadaiwa na baadhi ya watoa habari kuwa; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete walikuwa wakiongoza mjadala huo katika mwelekeo wa kutokuridhika na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Inaelezwa kuwa Rais Kikwete wakati wa mjadala huo alionekana kuwapa nafasi Sitta na Mwakyembe kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mianya ya kukwepa malipo hayo, akitumia lugha ya “watoe mwongozo.”

Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge lililoshiriki mijadala ya Richmond na Dowans, wakati Mwakyembe akiwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond na kusababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wanatajwa kujenga hoja zao kwa kuegemea zaidi uhalali wa Dowans ambayo kimsingi imetokana na kampuni ya mfukoni ya Richmond.

Sitta na Mwakyembe ambao ni wanasheria kitaaluma kwa sehemu kubwa wanatajwa kufanikiwa kuwashawishi wabunge hao kuridhia azimio la kusaka fursa za kisheria ili kutolipa mabilioni hayo kwa Dowans.

Wengine wanaotajwa kuwapo katika harakati hizo kiasi cha kujitolea kupambana kisheria ili Dowans ama isilipwe au malipo yapunguzwe ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.

Mkono aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi dhidi ya kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya City Water, iliyoshindwa kutekeleza mkataba wake wa kusambaza hudumu ya maji safi Dar es Salaam na mkataba wake kuvunjwa, baada ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri, chini ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Mbali na Mkono, mwingine aliyeshiriki kuzungumzia suala la malipo kwa Dowans katika wigo wa kisheria ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge, ambaye wakati wa Awamu ya Tatu, nchi iliingia mikataba mingi yenye utata.

Pinda ajaribu kufukia mashimo

Hata hivyo, katika kumuondolea ‘kiwingu’ Waziri Ngeleja, Waziri Mkuu Pinda ameeleza kuwa; kitendo cha kupishana kauli kati ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Ngeleja, kilitokana na ugeni katika kazi za uwaziri.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda bado inatajwa kuwa tata kwa kuzingatia rekodi za uzoefu katika uwaziri kati ya Ngeleja na Sitta.

Utata wa kauli Pinda unaibuka kwa kuzingatia ukweli kuwa Sitta ni mzoefu katika utendaji wa Serikali na amewahi kuwa waziri na wizara mbalimbali.

Kati ya Wizara alizopata kuongoza ni Ujenzi na ile iliyokuwa Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba (sasa ni Wizara ya Katiba na Sheria).

Kwa upande wake, Waziri Ngeleja amekuwa katika nafasi hiyo kwa takriban miaka minne sasa, kuanzia Februari, mwaka 2008.

Chiligati katika tuhuma nzito

Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, John Chiligati, ambaye pia ni Mbunge, naye yuko katika wakati mgumu.

Anadaiwa kutia chumvi hasa mtazamo au hisia binafsi tamko la kikao cha Kamati Kuu kuhusu sakata la Dowans. Chumvi anayotajwa kuikoleza Chiligati ni kutokana na kudai kwake kuwa Kamati Kuu “imebariki” malipo kwa Dowans.

“Suala hilo limewekwa wazi na Mwenyekiti kwamba haukuwa uamuzi wa Kamati Kuu kubariki malipo kwa Dowans, isipokuwa Kamati Kuu ilishauriwa kuruhusu michakato ya kisheria kuchukua nafasi na si kutoa uamuzi wa kulipa,” kilisema chanzo cha habari katika kikao hicho.

Kauli ya Msekwa kuhusu Kamati Kuu

Gazeti hili liliwasiliana na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, kufahamu kilichojiri kwenye Kamati Kuu, hadi ielezwe kulikuwa na upotoshaji.

Msekwa alijibu; “Achana na uamuzi wa Kamati Kuu, umekwishapitwa na wakati. Uamuzi wa sasa wa wabunge wa CCM ndiyo uamuzi wa Chama.

“Kama ilivyopendekezwa zichukuliwe hatua za kisheria na si kuchukua hatua za kulipa, huo ndiyo msimamo wa sasa wa chama.”

UVCCM walia na Dowans

Katika hali isiyotarajiwa, wakati Kamati Kuu ikikutana Ikulu, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ulikutana na waandishi wa habari, Hoteli ya Peacok, Dar es Salaam.

Hawa walitoa tamko wakisema Dowans isilipwe lakini kama kuna ulazima wa kulipa basi, wasibebeshwe mzigo huo Watanzania wote, bali walipe wanasiasa waliolifikisha hapo Taifa.

Taarifa za uhakika zinabainisha kuwa hatua hiyo imewakera baadhi ya viongozi wa sekretariati ya CCM na mmoja wa viongozi wa Serikali anatajwa kuanza kuwanunia vijana hao, akisema wamemuhujumu.

Katika utaratibu usio rasmi, vijana hao wanadaiwa kufokewa na baadhi ya viongozi wa sekretariati ya CCM inayoongozwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, lakini wamekuwa wakiweka msimamo wao wazi kuwa; “Ni jumuiya huru katika kutoa mitazamo yake kuhusu hali ya kisiasa na mwenendo wa Taifa.”

Upinzani wamezea mate Dowans

Uamuzi wa hivi karibu wa wabunge wa CCM umetanguliwa na nia ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliyeweka bayana tangu kutolewa hukumu hiyo ya Dowans kwamba; atawasilisha suala hilo bungeni.

Kwa mujibu wa Kafulila, alipanga kuhoji nchi imefikishwaje hapo kuilipa kampuni hiyo ambayo kimsingi imetokana na kampuni ya mfukoni ya Richmond.

Kafulila alikuwa tayari kuliomba Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani ya Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja au na serikali nzima.

Kama ilivyo kwa Kafulila wa NCCR-Mageuzi, CHADEMA kwa upande wao walikuwa wakitazama suala hilo kwa ukaribu na taarifa zinabainisha wamepanga kulifikisha Bungeni wao binafsi au kwa kumuunga mkono Kafulila.

Hata hivyo, kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa suala hilo halitafikishwa bungeni kwa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kujadili siasa wakati suala ni la kisheria zaidi, ni kama inakwamisha ndoto za wanasiasa hao wa upinzani nchini.

Mtiririko wa sinema ya Dowans

Suala la Dowans limekuwa likichua sura tofauti kila kukicha. Mara baada ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa kibiashara kutolewa, Desemba mwaka jana, vyombo vya habari vimeonyesha wakati fulani mwelekeo wa ushabiki.

Lakini wakati baadhi ya vyombo vya habari vikiwa katika ushabiki, huku wasomi na wanasiasa mashuhuri wakiwa katika mgongano wa maoni, wananchi wa kawaida walionyesha kutokubali kulipa deni hilo.

Msimamo huo wa wananchi wa kawaida umebebwa na asasi za kiraia ambazo zimefungua kesi katika Mahakama Kuu kuitaka Mahakama hiyo kutoridhia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa, kuilipa Dowans mabilioni hayo.

Mahakama ilipokea ombi hilo la asasi za kiraia. Katika hatua nyingine, kwa kuwa Dowans walipaswa kuwasilisha hukumu hiyo ili ipate nguvu za kisheria nchini, wanadaiwa kutofanya hivyo.

Badala ya kuwasilisha hukumu hiyo ambayo imejumuisha uovu wa kampuni ya Richmond ndani yake, Dowans wanadaiwa kuwasilisha viambatanishi tu mahakamani hayo. Mahakama kwa sasa inasubiri hukumu hiyo kutoka mikononi mwa Dowans.

Hisia za wananchi mitaani

Kutokana na uamuzi wa Shirika la Umeme Tanzania kupandisha bei za umeme, kumekuwapo na hisia miongoni mwa wananchi kuwa, ongezeko hilo la bei linalenga kukusanya fedha za kuilipa Dowans Sh bilioni 94.

Hisia hizi zimewahi kupingwa na Waziri Ngeleja katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema mwezi huu, bali hali iko hivyo kutokana na Tanesco kutaka kujimudu kiuendeshaji.

DOWANS YAWASILISHA MAOMBI YA MADAI YA USAJILI WA TUZO MAHAKAMA KUU


Kampuni ya Dowans leo imewasilisha rasmi maombi ya madai ya usajili wa TUZO katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam na kusajiliwa kwa kupewa namba ya usajili nane ya mwaka huu.

Kampuni ya Dowans ilishinda kesi ya madai dhidi ya TANESCO katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na kuamuliwa TANESCO kumlipa Dowans Sh Bilioni 94.

Naibu msajili mwandamizi wa mahakama hiyo Mh. Salvatory Mwongole,ameiambia Globu ya Jamii kwamba maombi hayo yameifikia mahakama hiyo januari 25 mwaka huu na yamewasilishwa na wakili wa kampuni hiyo hapa nchini kutoka kampuni ya uwakili ya Kennedy Fungamtama.

Mh. Mwongole amesema maombi hayo yamekwishapangiwa jaji lakini kulingana na unyeti wa suala hilo jina la jaji linahifadhiwa kwa sababu ndio kwanza ameteuliwa kushughulikia maombi ya usajili huo na jalada halijamfikia.

Alisema maombi hayo ya usajili yameombwa na kampuni ya Dowans Holdings S.A na Dowans Tanzania dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa mujibu wa sheria TUZO hiyo haitasajiliwa hadi mahakama itoe nafasi kwa mdaiwa kuwasilisha pingamizi kupinga usajili wa Tuzo hiyo kama anaona haifai kusajiliwa, na kama hana pingamizi itasajiliwa kama imekidhi sheria na mdaiwa kulazimika kulipa fedha hizo.

Wadau wengine pia wana nafasi ya kuwasilisha maombi yao kama wanadhani usajili wa TUZO hiyo haustahili nayo pia yatapokelewa, Mahakama ikishasikiliza kama kuna mapingamizi itatoa maamuzi kama ni kuisajili au la.

Thursday, January 27, 2011

Zisikumbatiwe NGOs zisizowajali wanawake, Tanzania yaiasa UN

TANZANIA imeutaka Umoja wa Mataifa (UN) kutozikumbatia taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazojinufaisha kupitia matatizo ya wanawake.

Balozi wa Tanzania UN, Ombeni Sefue alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa Bodi ya chombo kipya cha UN, kinachoshughulikia masuala ya wanawake, UN-Women.

Balozi Sefue alisema wakati Tanzania ikiunga mkono na kukaribisha ushirikiano wa wadau mbalimbali zikiwamo NGOs katika kuchagiza maendeleo na haki za wanawake, tahadhari ichukuliwe dhidi ya wale wanaotaka kujinufaisha kupitia matatizo hayo.

“Tunakaribisha wazo hili la kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo NGOs, na hasa waliodhamiria kuonesha kwa vitendo nia hiyo na si wale wanaolenga kujinufaisha,” akasisitiza Balozi.

Aidha Mwakilishi huyo wa Tanzania, ambayo ni kati ya nchi za kwanza kuunda Bodi ya UN-Women, amekitaka chombo hicho kukidhi kiu na matarajio ya nchi wanachama na hasa wanawake.

Alisema licha ya watendaji wa chombo kuwa na ubunifu na wanaojituma, lakini pia wanapaswa kujielimisha kuhusu mazingira watakayofanyia kazi.

Alisema kila nchi ina changamoto zake linapokuja suala la kushughulikia haki, usawa na maendeleo ya wanawake zikiwemo za mila, desturi na tamaduni hivyo ni vyema watendaji wa chombo hicho wakafahamu kuyazingatia hayo.

Balozi Sefue amesema ni vyema chombo hicho katika utekelezaji wa majukumu yake na hasa kwa kuzingatia kwamba kitalenga zaidi kufanya kazi ndani ya kila nchi husika, kizingatie mipango ya kila nchi na vipaumbele ambavyo nchi hizo imevichagua.

Pia alielezea hatua mbalimbali za kisera, kisheria na kimipango ambazo zimefanywa na Serikali ya Tanzania katika kutatua kero za wanawake.

Alisema Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameonesha utashi mkubwa wa kisiasa katika kushughulikia haki za wanawake ambao upo pia kwa viongozi wengine wa Serikali.

Matokeo Kidato IV: Wasichana nafasi 8 za kwanza

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika Oktoba mwaka jana yametoka huku katika watahiniwa bora wa kitaifa, wasichana wakiongoza kwa asilimia 80 na wavulana kuambulia asilimia 20.

Matokeo hayo yanaonesha kati ya watahiniwa 10 bora kitaifa, wavulana ni wawili huku shule za seminari hasa za wasichana zikiendelea kuongoza kama ilivyo ada.

Akitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Joyce Ndalichako, amesema pamoja na mafanikio hayo kwa wasichana, kiwango cha ufaulu cha jumla kimeshuka.

Mwanafunzi wa kwanza bora Tanzania ni Lucylight Mallya wa sekondari ya wasichana ya Marian mkoani Pwani akifuatiwa na wasichana wenzake Maria-Dorin Shayo (Marian) na Sherryen Mutoka (Barbro-Johansson, Dar es Salaam).

Aliyeshika nafasi ya nne kitaifa ni Diana Matabwa akifuatiwa na Neema Kafwimi wote wa St. Francis na Beatrice Issara (St Mary Goreti, Kilimanjaro).

Nafasi ya saba ndiyo iliyoshikwa na mvulana Johnston Dedani (Ilboru, Arusha) na ya nane Samwel Emmanuel (Ufundi Moshi, Kilimanjaro). Lakini nafasi za tisa na kumi zilichukuliwa na wasichana, Bertha Sanga (Marian) na Bernadeta Kalluvya (St. Francis).

Moja ya vituko vilivyofanywa na baadhi ya watahiniwa ni pamoja na kuandika matusi kwenye karatasi za kujibia mitihani.

Dk. Ndalichako alisema wanafunzi hao walitukana kwenye karatasi za Biolojia, Historia, Kemia na Jiografia na kwa kosa hilo, wanafunzi hao wamefutiwa matokeo.

Licha ya mafanikio hayo kwa wasichana yanayodhihirisha kaulimbiu kwamba mwanamke akiwezeshwa anaweza, ubora wa kufaulu kwa madaraja unaonesha watahiniwa 40,388 sawa na asilimia 11.50 wamefaulu katika madaraja ya kwanza hadi la tatu.

Kati yao, wasichana waliofaulu ni 12,583 sawa na asilimia 7.81 na wavulana ni 27,805 sawa na asilimia 14.62.

Hata hivyo, wavulana ndio waliokuwa watahiniwa wengi katika mtihani huo, kwa kuwa wasichana waliosajiliwa walikuwa asilimia 45.88 na wavulana asilimia 54.12.

Mafanikio hayo kwa wasichana ni makubwa ikizingatiwa kuwa mfumo dume umekuwa ukiwaathiri katika masomo yao, ikiwamo kupangiwa kazi nyingi za nyumbani, kuliko wavulana na pia wengi waliacha shule kutokana na mimba.

Pia katika mlinganisho wa ufaulu wa mwaka jana na mwaka huu, matokeo hayo yameonesha kiwango kushuka. Wakati mwaka jana waliofaulu walikuwa asilimia 72.51 mwaka huu ni asilimia 50.40 tu.

Hali hiyo inaonesha tatizo si shule za kata kwa kuwa matokeo hayo, kwa shule hizo ni ya pili, lakini wadau wanahusisha matokeo mabaya na uamuzi wa Serikali wa mwaka 2008 wa kuruhusu waliofeli mtihani wa kidato cha pili, kuendelea na masomo bila kurudia mtihani.

Wanafunzi wengi waliofeli mtihani wa kidato cha pili, ndio waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana na matokeo yao kuwa mabaya kuliko mwaka uliopita.

Dk. Ndalichako alisema waliofanya mtihani walikuwa 352,840 sawa na asilimia 97.04 ambapo watahiniwa 10,749 sawa na asilimia 2.96 hawakufanya mtihani huo.

Shule 10 bora kwa kigezo cha ‘Grade Point Average A=1 na F=5 zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni Uru Seminari ya Kilimanjaro, Marian na St.Francis.

Nyingine ni Cannosa, Feza Boys na Barbro Johanson za Dar es Salaam, Msolwa ya Morogoro, St Mary Goreti ya Kilimanjaro, Abbey ya Mtwara na St Joseph Sem Iterambogo ya Kigoma.

Shule 10 bora kwa kigezo hicho pia zenye watahiniwa chini ya 40 ni seminari ya Don Bosco, sekondari ya wasichana ya Bethelsabs ikifuatiwa na Seminari ya St. Joseph- Kilocha na seminari ya Mafinga zote za Iringa.

Nyingine ni Feza Girls ya Dar es Salaam, seminari ya Maua ya Kilimanjaro, Queen of Apostles Ushirombo ya Shinyanga, seminari ya Sengerema ya Mwanza na seminari ya Dungunyi Singida.

Alisema shule 10 za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni sekondari za Changaa, Thawi, Hurui, Kikore, Kolo zote za Dodoma, sekondari ya Pande Darajani ya Tanga, Igawa ya Morogoro, Makata ya Lindi, Mbuyuni na Naputa za Mtwara.

“Shule 10 za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni Sanje ya Morogoro, Daluni ya Tanga, Kinangali ya Singida; Mtanga, Mipingo na Pande za Lindi; Imalampaka ya Tabora, Chongoleani ya Tanga, Mwamanenge ya Shinyanga na Kaoze ya Rukwa,” alisema Ndalichako.

Akizungumzia watahiniwa wa kujitegemea, alisema waliosajiliwa walikuwa 94,525 wakiwamo wasichana 49,252 sawa na asilimia 52.10 na wavulana 45,273 sawa na asilimia 47.90 na mwaka jana walikuwa 96,892 hivyo watahiniwa kupungua kwa 2,367 sawa na asilimia 2.44.

Alisema watahiniwa 88,586 wakiwamo wasichana 46,358 na wavulana 42,228 walifanya mitihani huku watahiniwa hao 5,939 sawa na asilimia 6.28 wakiwa hawakufanya mtihani.

Katika ufaulu ni watahiniwa 8,295 sawa na asilimia 35.17 ya waliofanya mtihani ndio waliofaulu ikilinganishwa na asilimia 28.82 ya waliofaulu mwaka jana, hivyo kiwango cha ufaulu kuongezeka kwa asilimia 6.35.

Matokeo ya watahiniwa 1,448 waliofanya mtihani bila kulipa, yamesitishwa hadi watakapolipa ada wanayodaiwa na faini katika kipindi cha miaka miwili na baada ya muda huo kumalizika, matokeo yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

Ndalichako alisema wamesitisha matokeo ya wanafunzi wawili waliotumia sifa zinazofanana hadi wakuu wa shule watakapowasilisha nyaraka zinazothibitisha uhalali na mmoja mwenye namba S 3484/0014 kutokana na kutumia sifa za mtu mwingine hadi uchunguzi utakapokamilika.

Alisema pia Baraza limefuta na kuwaondoa katika usajili wa mitihani watahiniwa wanne wa sekondari za Kisaka na Nguvu Mpya kwa kutumia sifa za watahiniwa wengine.

Aidha, watahiniwa wengine 35 wa sekondari ya Bara wamefutiwa matokeo kwa kuwa walisajiliwa katika shule hiyo kwa kutumia majina ya watahiniwa waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo lakini hawakuripoti.

Dk. Ndalichako alisema pia wamemfutia mwanafunzi wa sekondari ya Ludewa aliyefanya mitihani bila usajili.

Wengine waliofutiwa ni wanne wa sekondari ya Ibanda waliokuwa si wanafunzi halali wa shule hiyo na 42 walioondolewa baada ya kubainika sifa za kidato cha pili walizowasilisha hazikuwa sahihi.

“Watahiniwa wengine 56 wa kujitegemea tumewafutia matokeo baada ya kuondolewa kwenye usajili kwa kutokuwa na sifa za kufanya mtihani, lakini wakafanya mitihani katika vituo vya Mwigo Sekondari 29 na Twitange Sekondari walifanya 27,” alisema Dk. Ndalichako.

Aliongeza kuwa watahiniwa 311 wa shule na wawili wa kujitegemea, wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika kufanya udanganyifu.

Alisema Baraza pia limefuta usajili wa kituo cha watahiniwa wa kujitegemea na mba P1189 cha Biafra, Dar es Salaam, kwa kukiuka taratibu za uendeshaji mitihani.

Kituo hicho kwa mujibu wa Dk. Ndalichako kilikuwa na watahiniwa wengi kuliko uwezo wake na kusababisha usumbufu uliofanya Kamati ya Mitihani ya Mkoa kuhamishia watahiniwa katika vituo vingine bila ushirikiano wa uongozi wa kituo.

Hukumu ya kesi ya EPA kutolewa Aprili 29, 2011

HUKUMU ya kesi ya katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili aliyekuwa Mweka Hazina wa CCM Mkoa wa Kigoma Rajabu Maranda na binamu yake Farijala Hussein itatolewa hukumu Aprili 29, mwaka huu.

Mbele ya jopo la mahakimu Sauli Kinemela, Ilvin Mgetta na Focus Bampikya wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, Wakili wa washitakiwa hao Majura Magafu alidai kuwa kesi hiyo imefikia ukomo wake jana ambapo Mahakama imesikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kwamba wanaiachia Mahakama ifanye kazi yake.

Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus alidai anaungana na upande wa utetezi kwamba upande wa mashitaka hauna la kuongeza na wanaiachia Mahakama iamue lini itatoa hukumu dhidi ya shauri hilo.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi tisa na vielelezo 17 ambapo washitakiwa hao pia walijitetea wenyewe.

Kwa mujibu wa kesi hiyo, Maranda na Farijala wanadaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Septemba 2, mwaka 2005 katika Mkoa wa Dar es Salaam, waliiba kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sh 1,864,949,294.45 baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Kiloloma & Brothers ililipwa deni na kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai nchini India.

Maranda anakabiliwa na kesi nne za aina hiyo katika Mahakama hiyo wakati Farijala anakabiliwa na kesi tatu za aina hiyo mahakamani hapo na wote wapo nje kwa dhamana.

Wednesday, January 26, 2011

KESI YA JERRY MURO YAZIDI ILIVYOUNGURAMA LEO

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imepokea risiti ya pingu kama kielezo cha ushahidi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa TBC 1 Jerry Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa.

Risiti ya Pingu hiyo iliwasilishwa na shahidi wa tano katika kesi hiyo ofisa mpelelezi Anthony Mwita (45), ambaye aliieleza Mahakama kuwa risiti hiyo yenye namba 341573B, aliipata katika duka la silaha la Mzinga lililoko Upanga jeshini jijini Dar es Salaam.

Alisema alifika katika duka hilo kupata uthibitisho kama pingu aliyokutwa nayo Jerry ilinunuliwa kwao ambapo nao walithibitisha kumuuzia pingu hiyo yenye thamani ya sh.25000 Mei 26, mwaka 2009 .

Mbali na kuwasilisha risiti hiyo pia shahidi huyo alidai katika upelelezi wake alienda katika Hoteli ya Seacliff ili kuthibitisha kama Jerry alifika hotelini hapo Januari 29, mwaka 2010.

Alidai alifika hotelini hapo Januari 31, mwaka jana na kumuona mlinzi wa KK Security aliyemtaja kwa jina la Brightone Babamika na kumuomba daftari la kuandikisha magari yaliyoingia hotelini hapo Januari 29 ambapo aliwapatia na kuona gari ya Jerry yenye namba za usajili T 545
TEH aina ya Cresta ambayo iliingia saa 7:33 mchana na kukabidhiwa kadi namba 673 na kuondoka saa 8:44 mchana.

Mwita alidai aliingia hotelini na kuuomba uongozi kuwaonyesha picha katika kamera ya CCTV ya matukio ya Januari 29 ambayo walionyeshwa na kupatiwa nakala ya picha hizo, lengo likiwa ni kuthibitisha kama kweli Jerry alifika hapo siku hiyo.

Naye shahidi wa nne alidai mahakamani hapo kuwa malalamikaji Michael Wage alikuja na fedha kiasi cha Sh milioni 10 kwenye ‘briefcase’ lakini hakuzihesabu.

Kesi hiyo itaendelea tena kesho mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo Gabriel Mirumbe.

Tuesday, January 25, 2011

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAARIFA YA WIZARA KULAANI MAUAJI YA WATOTO WANNE (4) YALIYOTOKEA WILAYA YA KARATU, ARUSHA.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesikitishwa na kuwepo kwa taarifa za mauaji ya kutisha ya watoto katika familia mbalimbali nchini ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiripotiwa kuhusika na mauaji ya watoto hao.

Hivi karibuni ilitaarifiwa kuwa baba mzazi Samweli Daudi aliwauwa watoto wake wawili kwa kuwakata mapanga hadi kufa katika kijiji cha Mwenei wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambaye anaye aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kubaini kuwa amewaua wanaye. Katika tukio hilo watoto Kulwa Daudi (5) na Abel Daudi (4) waliopoteza maisha yao. Watoto wengine wawili Elizaberth Kashirima (1), Dotto Kahabi (5) na mzee Daudi Kahabi (50) walijeruhiwa na wanaendelea na matibabu.

Tukio lingine la aina hiyo lilitokea januari 4 mwaka huu katika kijiji cha Makere mkoani Kigoma ambapo mwanakijiji Filbert Kafonogo aliwauawa watoto wake watatu kwa kuwakata mapanga naye akajinyonga kwa kamba. Ilielezwa kwamba alifika uamuzi huo baada ya kutuhumiwa na familia yake kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa watoto wake wa kuzaa.

Ukatili mwingine wa kutisha ni wa mauaji ya watoto wanne wa familia moja, waliouawa kwa kukatwa na shoka kisogoni kitendo kilichofanywa na baba yao mzazi, ambaye naye alijinyonga hadi kufa baada ya mauaji ya watoto hao. Taarifa inaeleza kuwa Evans Damian (43) ambaye ni baba wa watoto hao alikuwa na ugomvi wa kifamilia kwa muda mrefu na kusababisha kumfukuza mkewe na kisha akafanya mauaji hayo dhidi ya watoto wake wanne.

Wizara inakemea vikali mauaji ya watoto hao ambao ni Theophil Evans (10) mwanafunzi wa darasa la tatu, Ritha Evans (8), na watoto wawili mapacha Dibimo Evans (4) na Theodory Evans (4) wote wanafunzi wa darasa la awali katika wilaya ya Karatu. Taarifa kutoka kijijini zinaeleza kuwa, kabla ya tukio hilo la marehemu Evans alimuua nyani na kunywa damu yake.

Aidha, kitendo cha mauaji haya dhidi ya watoto wasio na hatia ni cha kikatili na kinapotokea katika ngazi ya familia kinarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukiukwaji wa Haki na Ustawi wa Mtoto. Mauaji haya yamewakosesha watoto hao haki yao ya msingi ya kuishi kitendo kinachopingana na katiba ya nchi yetu pamoja na mikataba ya Kimataifa ya Haki na Ustawi wa Mtoto ambayo nchi yetu imeridhia.

Hivyo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inahimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndiyo kitovu cha jamii yote panakuwa ni mahala salama penye upendo, amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia; na kuwapatia watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kuendelezwa. Ni vema wanafamilia wakawa wavumilivu na kuchua maamuzi yenye kuzingatia maslahi ya watoto ili kuepusha maafa.

Aidha, Wizara inatoa wito kwa wanajamii kubaini matukio yasiyo ya kawaida yanayotendwa na baadhi ya wanafamilia na kuyafuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika vyombo husika ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea na kuhatarisha uhai na usalama wa jamii.

Wizara inatoa rambirambi kwa mama, ndugu na jamaa wa watoto waliouawa maana maisha yao yamekatishwa kwa kupokonywa haki yao ya kuishi katika umri mdogo kutokana na kufanyiwa mauaji hayo ya kikatili. Wizara inawaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi mazito.Hussein A. Kattanga

KAIMU KATIBU MKUU

24 Januari, 2011

KESI YA JERRY MURO ILIVYOUNGURUMA JANA

MHASIBU wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo aliyesimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa ubadhirifu wa fedha za Umma Michael Wage, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alikubali kutoa Sh milioni 10 alizoombwa na aliyekuwa mtangazaji wa shirika la Habari Tanzania (TBC1) Jerry Muro kwa kuogopa kubambikiziwa kesi kama Liyumba.

Wage, ni shahidi wa tatu katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10, inayomkabili Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgassa, walidai mahakamani hapo kuwa alitishiwa maisha na washitakiwa hao na alikiri kutoa Sh milioni moja kwa ahadi ya kumalizia nyingine tisa
kesho yake.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo Gabriel Mirumbe, alidai kuwa mfululizo wa matukio hayo ulianza Januari 28, mwaka 2010 jioni, akiwa nyumbani kwake Bagamoyo ambapo alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa jina la Jerry Muro na mtangazaji
wa TBC1.

Alidai Muro alimtaka kufika Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya naye mahojiano kwamba kuna taarifa za tuhuma zinazomkabili zilizoanza kusambaa ambazo alitaka kuweka sawa ambapo alikuja na kukutana na Muro katika mgahawa wa Carlifonia kama walivyoahidiana ambapo baada ya kukutana Muro alimwambia alikua akiandaa kipindi kuhusiana na tuhuma zake ambapo alimtaka waende katika Hoteli ya Seacliff ambako mahojiano hayo yangefanyika.

Alidai wakiwa njiani kwenye gari ya Muro kuelekea Seacliff Muro alimpigia mtu simu na katika maongezi yake alimtaja yeye (Wage) na alipokata simu alimuuliza alikuwa akiongea na nani, Muro akamjibu kuwa huyo ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambaye pia alikuwa na maongezi na yeye.

Wakiwa bado njiani Wage alidai kuwa Muro alimwambia kuwa yeye ni Ofisa wa jeshi, ana nyota tatu na amesomea Marekani, ambapo alifungua ‘dashboard’ ya gari akatoa pingu na kumwambia kama akifanya vurugu au fujo ya aina yoyote angemfunga pingu na kisha alitoa bastola yenye
kitako cha rangi ya damu ya mzee na kumwambia kama yote yangeshindikana basi angempiga risasi na kumuua.

Alidai walipofika Seacliff walipokelewa na mtu mmoja mrefu, mweupe na mnene aliyejitambulisha kuwa yeye ni Kaimu mkurugenzi wa TAKUKURU anaitwa Mussa na baada ya muda akaja mwingine aliyejitambulisha kuwa ni msaidizi wa Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU.

Wakiwa wamekaa meza moja Kaimu Mkurugenzi akamwambia kuwa ana tuhuma za ufisadi na kwamba hajafikishwa mahakamani aseme kama atahitaji msaada wao ambapo aliwajibu kuwa yeye sio fisadi.

Wage alidai Kaimu Mkurugenzi alimwambia kuwa hata Liyumba hakufanya kosa bali alimuambukiza Ukimwi bibi wa jamaa yake ambaye wanafanya naye kazi.

Alidai baada ya maelezo hayo alimuomba Muro amsaidie ambapo alimuomba atoe Sh milioni 10, naye akawajibu hakuwa nayo pale alikuwa na Sh. milioni moja tu, na hizo nyingine angekwenda kuwatafutia na kuziwasilisha kesho yake.

Alieleza akiwa na watu hao aliamua kumpigia mke wake aliyekuwa Morogoro simu na kuweka kipaza sauti ambapo alimtaka kumletea Sh. milioni tisa kesho, mkewe huyo alidai asingeweza kupata milioni tisa kwa kesho badala yake angeleta milioni nne tu.

Alidai kutokana na matukio ya siku hiyo aliwapigia simu ndugu zake ambao walimshauri kuripoti polisi ambapo kesho yake alienda kuripoti katika kituo cha polisi kati jijini Dar es Salaam, ambapo walimwambia ampigie simu Muro amwambie wakutane katika mgahawa wa City Garden maeneo ya Posta mpya mkabala na klabu ya Billicanas.

Wage alidai alimpigia simu Muro na kukubaliana kukutana hapo ambapo alifika saa 4:30 asubuhi na kumpigia simu kumfahamisha kama ameshafika na ndipo akajitokeza akiwa na polisi waliovalia kiraia ambapo Muro alipowatambua akataka kukimbia lakini polisi wakalizuia gari lake.

Shahidi huyo aliwatambua washitakiwa hao mahakamani na pingu, bastola na miwani ambavyo viliwasilishwa na upande wa mashitaka kama utambulisho katika kesi hiyo. Shauri litaendelea kusikilizwa tena leo kwa mashahidi upande wa mashitaka kuendelea kutoa ushahidi wao.

Monday, January 24, 2011

Sumaye atetea mawaziri kupingana

WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, ametetea hoja ya mawaziri kuzungumza na kupingana hadharani kama jambo linalozungumziwa halikujadiliwa ndani ya Baraza la Mawaziri.

Sumaye alisema hayo jana Dar es Salaam katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya za Chama cha Maendeleo ya Wilaya za Mbulu, Hanang, Babati na Karatu.

Alisema yapo mambo ya pamoja ya Serikali, lakini pia kila mtu ana uhuru na utashi wa kuzungumza analoona linafaa.

“Tatizo ni kwamba suala la Dowans (kampuni inayotarajiwa kulipwa Sh bilioni 94 baada ya Serikali kuvunja mkataba wake wa kufua umeme) halikwenda katika Baraza la Mawaziri ambako mtu angetoa dukuduku lake kule, kila mtu ana utashi, si kwamba ukiwa Waziri ndio usizungumze,” alisema Sumaye.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe, alisema ni kosa kwa mawaziri kupingana hadharani na kuongeza kuwa kama kuna mwenye dukuduku kuna namna ya kuwasilisha maoni yao.

Kwa mujibu wa Chikawe, taratibu hizo ni kwa mawaziri husika kuwasiliana na kushauriana na inapotokea anayeshauriwa haelewi, upo utaratibu wa kupeleka maoni hayo kwa Waziri Mkuu.

Waziri huyo alitoa kauli hiyo, kufafanua kauli ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe kupingana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Mawaziri hao walipingana na tamko la Ngeleja kwamba Serikali itailipa Dowans deni lake na waziri huyo alifanya hivyo baada ya kushauriwa na Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema.

Katika hatua nyingine, Sumaye pia aliunga mkono kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba Mpya.

Lakini pia aliunga mkono hoja ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ya kupeleka hoja hiyo bungeni ili ijadiliwe na kuongeza kuwa hata yeye angekuwa mbunge, angepeleka hoja hiyo bungeni.

Alifafanua kuwa wakati hoja hiyo ikijadiliwa na wakati wananchi wakipewa elimu kuhusu uzuri na upungufu wa Katiba iliyopo, hali hiyo itatoa fursa kwa wananchi kufanya uamuzi wa kuwepo kwa Katiba mpya au la na maundhui ya katiba hiyo.

Friday, January 21, 2011

Kilio cha Dk. Slaa chaiponza REDET

-Mfadhili wake mkuu ajitoa rasmi

BAADA ya miaka 18, Denmark, kupitia Shirika lake la Misaada ya Maendeleo (DANIDA), limejitoa kufadhili Mpango wa Elimu ya Demokrasia na Utafiti (REDET) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Raia Mwema imethibitisha.

Ingawa taarifa za kujitoa kwa DANIDA zinahusishwa na mwenendo wa REDET katika matokeo ya utafiti wa kisiasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, yaliyodaiwa yalikuwa yanachakachuliwa, Mwenyekiti Mwenza wa REDET Dk. Benson Bana, amepuuza taarifa hizo akieleza sababu nyingine.

Miongoni mwa waliolalamikia taarifa za utafiti wa REDET ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, aliyekuwa anagombea urais na aliyeshindwa na Jakaya Kikwete wa CCM, alipata kudai kwamba matokeo ya utafiti wa REDET yaliyokuwa yakikitabiria chama chake na yeye kushindwa katika uchaguzi wa mwaka jana yaliongozwa na tafiti batili zilizokuwa zikikipendelea chama tawala.

REDET ni miongoni mwa asasi zilizotoa taarifa za utafiti, kabla ya Uchaguzi Mkuu, zilizotabiri kwamba mgombea wa CCM, Kikwete, angeshinda huku Dk. Slaa na wagombea wengine, akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wakifuatia kwa mbali.

Akizungumzia kujitoa kwa DANIDA kufadhili REDET wiki hii, Dk. Slaa ameliambia Raia Mwema katika mahojiano maalumu kwamba hatua hiyo ya DANIDA ni ya kupongezwa japo “walipaswa kujitoa muda mrefu uliopita, maana tulikwishakulalamika mara nyingi sana. Hawa (REDET) wanapanga matokeo halafu wanatafuta njia ya kuyachakachua.”

Taarifa zilizosambazwa awali zilieleza kuwa DANIDA, mfadhili mkuu wa REDET, ilijitoa kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa taasisi hiyo ya kitaaluma hasa baada ya kulalamikiwa na baadhi ya makundi ya kijamii, wakiwamo wanasiasa.

Hata hivyo, katika mahojiano yake na Raia Mwema, Dk. Bana alithibitisha kujiondoa kwa DANIDA lakini akisema sababu ya kitendo hicho si mwenendo wa REDET bali ni kwamba majukumu ya asasi hiyo yamefikia hitimisho.

“REDET katika majukumu yake ilikuwa na awamu sita za utendaji ambazo zilipaswa kukamilishwa Desemba 31 mwaka 2010. Kila programu ilikuwa na madhumuni na zilipangwa kukamilishwa Desemba mwaka jana. Hata mikataba ya ajira za watendaji ilieleza kwisha wakati huo,” alisema Dk. Bana, akisisitiza kwamba ‘maisha’ ya REDET kimajukumu yalipaswa kukamilika mwishoni mwa mwaka jana.

Lakini kuhusu kujitoa kwa mfadhili na sababu za kujitoa kwake alisema; “DANIDA ni mfadhili mkuu na kwa kweli tunawashukuru sana; wamekuwa wakitufadhili tangu mwaka 1992.

“Sera zao zimebadilika hasa katika masuala ya utawala bora na ubinafsishaji; kubadilika kwa sera zao huko kwao ni lazima kutaathiri sisi tunaofadhiliwa.

“Kujitoa kwao si suala la ghafla. Ilikuwa ikijulikana watajitoa kwa sababu hata kazi za REDET zilikuwa na ukomo ambao umekwisha kufika Desemba 31, 2010.

“Haijawahi kutokea Afrika kwa mfadhili kuendelea kufadhili taasisi moja kwa miaka 18. Hiyo inaonyesha jinsi gani REDET imekuwa na hadhi kubwa na kazi zake ni za viwango vya kitaaluma.”

Kwa upande mwingine alisema kuna baadhi ya kazi ambazo zilipaswa kukamilishwa na REDET lakini hazikufanyika kwa wakati kutokana na Uchaguzi Mkuu (wa mwaka jana) na kwamba zitakamilishwa katika mwaka huu.

Alizitaja kazi hizo ambazo tayari zimekwisha kutolewa fedha kwa ajili ya utekelezaji kuwa ni pamoja na utafiti kuhusu hali ya kisiasa nchini na uwezeshaji, lengo likiwa ni pamoja na kuitazama Serikali ilivyotimiza wajibu wake kwa umma.

Kazi nyingine kiporo aliitaja kuwa ni mkutano wa mabadiliko ya kidemokrasia Afrika Mashariki.

Mbali na kujitoa kwa mfadhili huyo, uchunguzi wa gazeti hili pia ulibaini kuwa REDET iko katika mchakato wa ‘kufumuliwa’ ikiwa ni pamoja na kubadilisha muundo wake na hata majukumu yake ya awali.

Kutokana na taarifa hizo, Dk. Bana aliulizwa na kukiri kuwapo kwa mpango huo akibainisha kuwa tayari rasimu ya mapendekezo imeridhiwa na Bodi ya Baraza la Chuo cha Fani na Sayansi ya Jamii.

“Nikwambie tu kwamba tayari rasimu ya mapendekezo ya kuibadili REDET imekwisha kupitishwa na Bodi ya Baraza la Chuo cha Fani na Sayansi ya Jamii.

“REDET kama sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itabadilishwa na kuwa taasisi au kituo cha utafiti na shughuli nyingine hasa za kitaaluma.

“Wakati inaanzishwa, utakumbuka, ndio ulikuwa mwanzo wa mfumo wa vyama vingi na lengo lilikuwa kutoa elimu ya uraia na uwezeshaji kidemokrasia; sasa shughuli zitaweza kubadilika kulingana na mambo mawili:

“Kwanza ni theme (maudhui) na pia mwenendo wa hali ya kisiasa nchini Tanzania. Programu zetu za awali zilikuwa katika awamu sita kwa mihula mitatu mitatu, na tulikuwa tunafanya tathmini baada ya kila kipindi. Sasa, katika mtazamo mpya, tunaweza kuwa na programu za muda mrefu na zitakazofanyiwa tathmini, kwa mfano, kila miaka mitano,” alisema Dk. Bana.

Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri wa CHADEMA John Mrema ameiambia Raia Mwema kwamba ni kweli chama chake kimekuwa na malalamiko kuhusiana na jinsi REDET ilivyokuwa inatumika kisiasa kwa maslahi ya CCM.

“Ni kweli tulilalamika kwa kukutana na watu mbalimbali ana kwa ana na pia kwa kuandika barua rasmi kuelezea kutoridhishwa kwetu na tafiti za REDET kabla ya uchaguzi wa mwaka jana. Kwanza walikuwa wakienda mikoani wanafikia kwa wakuu wa wilaya ambao wanawapa maelekezo ya nini cha kufanya.

“Halafu wanaelekezwa kwa makatibu tarafa na wajumbe wa nyumba kumi ambao wote ni makada wa CCM. Viongozi hao wa CCM ndio waliokuwa wakiwaongoza watafiti wa REDET juu ya watu wa kuwahoji,” anasema Mrema.

Juhudi za kuupata ubalozi wa Denmark nchini kuzungumzia sababu za kujitoa kwa DANIDA kufadhili REDET hazikuzaa matunda, ingawa zinaendelea.

Hata hivyo, taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark, zinaonyesha kuwa Ubalozi wa nchi hiyo Tanzania umekuwa ukifanya mapitio ya mipango-kazi ya REDET. Taarifa hizo zilitolewa Julai 1, mwaka jana.

Ubalozi huo umekuwa ukifanya uhakiki wa mipango ya REDET kwa kutumia jopo la wataalamu ili kujiridhisha kuwa asasi hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa malengo yake ambayo ni kuwezesha mchakato wa kidemokrasia kupitia tafiti, machapisho na elimu ya moja kwa moja inapobidi.

Katika awamu yake ya sita kwenye mipango yake, ubalozi wa Denmark unaeleza kuwa kazi ya REDET ilikuwa ni uwezeshaji kidemokrasia, elimu ya uraia na uwajibikaji.

Tathmini ya kazi za REDET inaonyesha kufanyika kwa mara ya mwisho na timu maalumu ubalozini kuanzia Februari 4 hadi 14, mwaka 2009.

Walioshiriki katika tathmini au mapitio hayo ni pamoja na Anders Baltzer Jørgensen, aliyekuwa mshauri wa masuala huduma za kiufundi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Denmark.

Wengine ni Bornwell Chikulo, Jan Kees van Donge na Steen Skovgaard Larsen wote washauri wa masuala ya nje wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark.

Jopo hilo la tathmini katika kufanya kazi yake lilipata kukutana na baadhi ya wafanyakazi wa REDET, akiwamo mwanzishili na Mwenyekiti wa kwanza wa REDET, Profesa Rwekaza Mukandala. Pia jopo hilo lilikutana na wadau wengine wa REDET Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hatua nyingine, Dk. Bana pia alirejea kauli yake ya mara kwa mara kuwa wale ambao wamekuwa hawaridhishwi na matokeo ya tafiti za REDET, wamekuwa wakitoa hoja zao nje ya misingi ya taaluma ambayo ndiyo iliyokuwa ikitumiwa na REDET kutafiti.

“Nimekuwa nikiwaeleza, kama unapinga utafiti wa REDET fanya hivyo kwa kutumia utafiti pia Mara nyingi wengi wao wamekuwa wakipinga kwa kelele zisizozingatia tafiti. Sisi ni wanataaluma, tunatumia mipango ya kitaaluma na matokeo yetu yanazingatia taaluma,” alisema.

Matokeo ya mwisho ya utafiti wa REDET kuhusu nafasi ya urais, siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, yalionyesha kuwa mgombea wa CCM, Kikwete angepata asilimia 71.2, Dk. Slaa (CHADEMA) asilimia 12.3 na Profesa Lipumba (CUF) 10.1 ya kura zote, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza Kikwete kuwa mshindi kwa asilimia 61.17 akifuatiwa na Dk. Slaa asilimia 26.34 na Profesa Lipumba aslimia 8.06.

Chanzo: Raia mwema

Thursday, January 20, 2011

Serikali yafunga kesi ya Mramba, Yona na Mgonja leo

Upande wa Serikali leo umefunga kesi inayomkabili Waziri wa zamani wa Wizara ya Fedha, Basil Mramba, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Fedha, Gray Mgonja.

Maelezo hayo ya kufunga kesi hiyo yametolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, na mwendesha mashtaka Wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus alipotakiwa na kiongozi wa jopo la majaji watatu wanaosikiliza shauri hilo, Jaji John Utamwa kumleta kizimbani Shahidi wa 14 aendelee kutoa ushahidi wake.

Jaji Utamwa aliwataka mawakili wa pande zote mbili kuongea lolote kama wana hoja yoyote ya msingi kabla jopo halijatoa uamuzi wake.

Wakili wa Mgonja, Profesa Leonard Shahidi alidai kwa niaba ya mawakili wenzake upande wa utetezi hauna pingamizi juu ya hilo lakini aliiomba Mahakama kuwapatia nakala ya mwenendo wa kesi ili waweze kuongea kupitia majumuisho hayo.

Jaji Utamwa alikubali maombi hayo ambapo alisema shauri hilo litatajwa Februari 18, mwaka huu na kwamba kama uchapwaji wa nakala hizo utakuwa umekamilika itapangwa tarehe ya kusikiliza shauri hilo.

Hata hivyo, Prof. Shahidi aliutaka upande wa utetezi kuwapatia majumuisho ya ya hoja za mashahidi kwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ambapo alidai atawasilisha hoja kuitaka Mahakama iwaone wateja wao hawana kesi ya kujibu.

Kesi hiyo Namba 1200 ya mwaka 2008, ilianza kusikilizwa Novemba 2009, imefungwa baada ya kupitiwa kwa vielelezo 26 na mashahidi 14 kukamilisha ushahidi wao mahakamani hapo.

Katika kesi hiyo, mawaziri hao wa zamani kwa pamoja wanatuhumiwa kuingia mkataba na kuisamehe kodi kinyume cha sheria kampuni ya Alex Stewart jambo linalodaiwa kuisababisha Serikali hasara ya Sh bilioni 11.

Wednesday, January 19, 2011

Siri hadharani


WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo kinatikisa mji wa Arusha kuomboleza mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi, hali bado si shwari kutokana na kuendelea kuibuka kwa mambo kadhaa yaliyofichwa katika tukio hilo la aibu katika mji huo wa kitalii.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrord Slaa na Mbunge wa Ubungo kupitia chama hicho, John Mnyika, kwa nyakati tofauti wiki hii wamekuwa wakisema chama hicho leo kimeandaa maombolezo ya wahanga wa vurugu za Arusha katika viwanja vya NMC ambako nako kulikumbwa na ghasia wiki iliyopita.

“Tutawaaga marehemu katika viwanja vya NMC Arusha Januari 12 siku ya Mapinduzi (leo). Ombi langu kwenu tujitokeze kuadhimisha mapinduzi ya kweli ya madai yetu,” unaeleza ujumbe mfupi wa Dk. Slaa katika mtandao na kupata wachangiaji karibu 300; huku kwa upande wake Mnyika akisema;

“Heshima ya mwisho ya ndugu zetu waliopoteza maisha Arusha itafanyika Januari 12 Uwanja wa NMC. Kwa rambirambi au mchango wa matibabu kwa wahanga wasiliana na kamati kupitia 0764150747."

Tayari imeelezwa kwamba Polisi imekataa CHADEMA kufanyia maombolezo katika viwanja vya NMC ingawa taarifa za maombolezo hayo zilikwishakutangazwa.

Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Arusha, Samson Mwigamba, amenukuliwa akisema kwamba hawatabadili eneo na kwamba walikuwa wakiendelea na mazungumzo na Polisi kuhusiana na suala hilo hali inayoashiria mvutano mwingine kati ya CHADEMA na Polisi.

Mauaji hayo yaliyofanywa na Polisi wakati wa kuzima maandamano ya amani ya viongozi na wanachama wa CHADEMA wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu kadhaa yamekuwa yakiibua utata na sasa yanaelezwa kugusa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya baada ya kubainika kuwa mmoja wa watu hao watatu waliouawa kwa kupigwa risasi za moto na polisi, ni raia wa Kenya.

Katika maandamano hayo ya amani yaliyofanyika Januri 5 mwaka huu, Polisi wanataja watu watatu ndio waliopoteza maisha baada ya kupigwa risasi za moto na polisi huku wengine zaidi 30 wakijeruhiwa vibaya kwa risasi na vipigo kutoka kwa polisi wa kutuliza ghasia lakini hakuna taarifa huru juu ya idadi kamili ya watu walioathirika na tukio hilo.

Marehemu hao walitambuliwa kuwa ni Denis Michael Ngowi (30) mkazi wa Songambele-Sakina, ambaye alipigwa risasi moto ubavu wa kulia, Ismael Omary (40) ambaye pia alipigwa risasi ya moto ubavuni na raia mmoja wa Kenya.

Raia huyo wa Kenya ametambuliwa kuwa ni Paul Njuguna Kaiyehe (26) ambaye maelezo yake yanayopatikana katika kitambulisho chake yanaonyesha kuwa ni mkazi wa wilaya ya Kajiado eneo la Ngong na mwili wake bado uko katika chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Njuguna amefahamika baada ya kupatikana kwa kitambulisho hicho katika nyumba aliyokuwa akiishi katika eneo la Sakina ambapo kitambulisho chake kinamtambulisha kama raia wa Kenya kina namba 25066938 na seriel namba yake ni 218733089.

Awali polisi katika taarifa yao walimtaja marehemu huyo kwa jina la George Mwita Waitara huku ikihofiwa kwamba lengo ni kuficha jina lake kuepuka mgogoro wa kidiplomasia na nchi hiyo jirani na mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hata hivyo wakati polisi katika maelezo yao wakidai kuwa marehemu huyo ni Mtanzania na mkazi wa mkoa wa Mara, viongozi wa CHADEMA wakioongozwa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, siku ya Ijumaa, walifanya juhudi za ziada kwa kutafuta nyumba aliyokuwa akiishi marehemu huyo.

Viongozi hao wakishirikiana na viongozi wa mtaa huo walivunja mlango wa nyumba hiyo na kupekua ambapo walifanikiwa kupata kitambulisho hicho na hivyo kubaini kuwa alikuwa raia wa nchi hiyo jirani.

Habari zilizopatikana mwishoni mwa wiki mjini hapa zilieleza kuwa lengo la polisi kubadilisha jina la marehemu huyo ilikuwa ni kukwepa fedheha na kujaribu kuepusha kuingia dosari kwa uhusiano wa kidiplomasia na Kenya.

Mmoja wa maafisa wa polisi ambaye si msemaji wa jeshi hilo aliimbia Raia Mwema kwamba taarifa zilizoibuliwa baadaye na viongozi wa CHADEMA kuwa marehemu huyo ni raia wa Kenya zimelifedhehesha sana jeshi hilo na sasa maafisa wa polisi wanahaha kutoa maelezo ya kutosholeza kwa ubalozi wa Kenya kuwafahamisha jinsi raia huyo alivyopoteza maisha kwa kupigwa risasi.

“Kwa kweli wakubwa wa jeshi letu wameshtushwa sana na taarifa hizo kufahamika….na kuna vikao vinaendelea katika makao makuu ya polisi pale mkoani ili kuweka mambo sawa maana tayari ubalozi wa Kenya umeshaanza kufuatilia kifo cha raia huyo,” alisema mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya jeshi la polisi.

Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa Kenya imechukulia mauaji hayo kwa uzito wake hasa kutokana na nchi hiyo kupitisha Katiba yake mpya mapema mwaka jana na Katiba hiyo mpya imetoa nafasi kubwa kwa masuala ya haki za msingi za binadamu.

“Tumepata taarifa kuwa Ofisa wa Ubalozi wa nchi hiyo na mshauri wa masuala ya siasa wa Rais Mwai Kibaki hapa nchini ambaye ana ofisi ya kudumu mjini Arusha atakutana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenya siku ya Jumatatu kupata maelezo ya msingi jinsi raia huyo wa Kenya alivyoauwa kwa kupigwa risasi na polisi,” alieleza ofisa huyo.

Kwa mujibu wa Afisa huyo, Kenya inataka maelezo ya kuridhisha kuhusu mauaji ya raia wake ambaye habari zinaeleza kuwa alipigwa risasi katika eneo la Kaloleni akitembea barabarani kwa shughuli zake na hakuwa katika maandamano yaliyovunjwa.

“Kwa kuwa wenzetu sasa wana Katiba hiyo mpya ambayo imeweka bayana haki za msingi kuhusu maisha ya watu wake, basi, suala hilo wamelichukulia kwa uzito wa juu sana na wiki hii itakuwa moja ya wiki ngumu kwa maofisa wa polisi mkoani Arusha kueleza sababu za msingi za mauaji hayo,” alieleza ofisa huyo.

Raia Mwema ilifanikiwa kuzungumza na Balozi mdogo wa Kenya anayeshughulikia masuala ya siasa ambaye yuko mjini Arusha, Robert Mathenge, Januari 9 (Jumapili) na alithibitisha kuwa ni kweli marehemu Paul Njuguna ni raia wa nchi hiyo jirani na kuongeza kuwa wamesikitishwa sana na mauaji ya raia yaliyotokea.

“Ni kweli siku ya Ijumaa nilifika chumba cha maiti baada ya kupewa taarifa kuhusu marehemu kuwa ni raia wa Kenya na nimethibitisha kutokana na vitambulisho alivyokutwa navyo na tayari nimetoa taarifa kwa ubalozi wetu mjini Dar es Salaam”, alisema Mathenge.

Alisema pia ametoa taarifa hiyo nchini mwake ili mamlaka zinazohusika ziwatafute ndugu zake ili wakabidhiwe mwili wa marehemu huyo kwa ajili ya maziko na serikali ya nchi hiyo itatoa msaada unaohitajika kufanikisha mazishi ya raia huyo.

Mathenge alieleza kuwa kwa ujumla Kenya imesikitishwa sana na mauaji hayo ya raia lakini ni kwasasa ni mapema kusema kuwa mauaji hayo yataathiri uhusiano uliopo baina nchi hizo mbili ambazo zote ni wanachama waanzilishi wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Ni kweli nitakuwa na kikao na Kamanda wa Polisi mkoani Arusha (Thobias Andengenye) ili kupata taarifa kamili ya kipolsi kuhusu mauaji hayo na baada ya hapo tutakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuzungumzia jambo hilo,” alisema Mathenge.

Wakati wananchi Arusha wakiwa bado na kumbukumbu ya kutisha kuhusu mauaji hayo ya polisi, madai mapya yamezidi kuibuka kuhusu mbinu mbalimbali za kutisha zilizotumiwa na askari hao, ambapo sasa inadaiwa kuwa askari hao waliwapiga risasi baadhi ya watu hata katika nyumba za ibada na pia kuwapora majeruhi, na wale waliokamatwa.

Madai mazito yalitolewa juzi na watumishi na watawa wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia iliyopo jirani na Kituo kikuu cha polisi cha mjini Arusha ambapo walidai kuwa polisi walimpiga risasi mmoja wa vijana waliokimbilia kanisa hapo kuomba hifadhi.

Mmoja wa watawa wa Kanisa hilo akielezea mkasa huo kwa mwandishi wa gazeti hili alieleza kuwa kijana huyo alipigwa risasi majira ya saa 10:30 za jioni katika eneo la Kanisa hilo na kuvunjwa mguu na baadaye walimwacha hapo akivuja damu na maumivu makali.

“Baada ya kumpiga risasi sisi tulikuwa tumekimbilia ndani ya moja ya majengo ya Kanisa kutokana na hofu ya milipuko ya mabomu na risasi za moto kutoka kwa askari hao na askari hao walikuja kutuamua tufungue milango la sivyo wangelipua nyumba nzima”, alieleza Mtawa huyo.

Aliongeza: “Tulipofungua nyumba wakaanza kuwapiga makofi watumishi (wafanyakazi) wa kiume waliowakuta ndani wakiwatuhumu kuwa ni waandamanaji waliokimbilia huku kujificha…..ikabidi mmoja wetu aingile kati na kuwatetea ndipo walipowaacha.”

Mtumishi huyo wa Kanisa alieleza kuwa kijana aliyejeruhiwa aliachwa katika eneo la Kanisa bila msaada kwa zaidi ya nusu saa hadi polisi walipoitwa tena na Padre Elkana Tenges ambaye ni mkuu wa idara ya mawasiliano katika jimbo Katoliki la Arusha.

“Padre Tenges aliwaita ili wamchukue majeruhi huyo wampeleka hospitali na wasimwache katika eneo la Kanisa….na kwa bahati walirejea wakiwa na gari na kumchukua majeruhi huyo ambaye tulikuwa hatujapata jina lake,” alieleza.

Habari zaidi zinaeleza kuwa tukio hilo ndilo lililowasukuma maaskofu wa madhehebu ya Kikristo mkoani Arusha, wakioongozwa na Askofu Josephat Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, kutoa tamko na kali kulaalni mauaji hayo na pia Polisi kutumia nguvu nyingi kuzima maandamano ya amani.

Maaskofu hao pia walitamka kuwa hawako tayari kushirikiana na Meya ambaye uchaguzi wake uligubikwa na utata na ndiyo chanzo cha kutokea kwa machafuko hayo ya kisiasa ambayo yamepeleka maisha ya watu na mali kuteketea.

Aidha katika hatua nyingine ambayo imelitia doa jeshi la polisi mkoani Arusha, majeruhi na wahanga wa tukio hilo wanadai kuwa pamoja na vipigo walivyopata kutoka kwa polisi pia walitumia mwanya wa vurugu hizo kuwapora fedha na vitu vingine vya thamani kama simu, saa na mikufu ya dhahabu.

Miongoni mwa waliotoa madai hayo mazito ni Mbunge wa viti maalumu wa CHADEMA, Lucy Owenya ambaye anadai kuporwa simu zake mbili za mkononi zote zikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi 900,000.

Mbunge huyo juzi alikaririwa katika mkutano wa waandishi wa habari akieleza kuwa atafungua mashitaka dhidi ya jeshi hilo kufuatia askari wake kuhusika na uporaji huo.

Aidha madai kama hayo pia yametolewa na majeruhi Joackim Andrew (31) aliyelazwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru ambaye anadai kuwa aliporwa kiasi cha shilingi 490,000 na simu yake ya mkononi ambayo ina thamani ya Shilingi 200,000.

Madai ya majeruhi huyo pia yameorodheshwa katika taarifa ya tukio hilo iliyokusanywa na viongozi wa CHADEMA ambayo iliwasilishwa kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha, Thobias Andengenye hakupatikana kuthibitisha au kukanusha madai hayo kwani kila alipopigiwa simu tangu kutokea kwa tukio hilo amekuwa hapokei simu yake na jeshi hilo limeshindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari wanaotaka kufahamu taarifa mbalimbali kuhusu tukio hilo.

Tayari matamko mbalimbali yametolewa na viongozi wa dini na wale wa kisiasa kulaani vurugu hizo huku jeshi la polisi likitakiwa kujisafisha na tuhuma zinazoelekezwa kwake ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa tume huru kuchunguza chanzo cha vurugu hizo zilizopeleka mauaji hayo.

Moja ya kauli kali zilizotolewa ni ile ya Maaskofu wa Makanisa ya Kikristo mkoani Arusha ambapo pamoja na kulaani mauaji ya wananchi hao walieleza wazi kuwa hawatakuwa tayari kushurikiana na Meya aliyechaguliwa Gaudance Lyimo kwani uchaguzi huo unalalamikiwa na wananchi.

Baada ya kauli hiyo kali ya Maaskofu Katibu wa CCM mkoa wa Arusha Mary Chatanda ambaye anaelezwa kama kiini cha machafuko hayo aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwataka Maaskofu hao wavue majoho yao na kuingia katika ulingo wa siasa.

Hata hivyo kauli hiyo ya Chatanda nayo ilipingwa na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Samwel Malecela ambaye alisema kauli hiyo ya Chatanda ni utovu wa nidhamu kwa Maaskofu hao ambao wanaheshimika sana katika jamii na alikwenda mbali kwa kumtaka Katibu huyo wa CCM awaombe radhi viongozi hao wa dini.

Akizungumza na Raia Mwema, juzi, Chatanda alisema bado anasimamia kauli yake kwake Maaskofu hao waliingilia siasa pale walipohoji uchaguzi wa Meya ambao kimsingi ulikuwa halali na ufafanuzi wake ulishatolewa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri.

“Kwa Maaskofu kulaani mauaji mimi sina malalamiko juu ya hilo ila sikubaliani nao pale wanapohoji kuhusu uchaguzi wa Meya kwani kwa kufanya hivyo wanaingilia siasa……na kama kuna wanafikiri kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu basi waende mahakamani, wakati tafsiri ya kisheria badala ya kuleta vurugu mtaani,” alisema Chatanda.

Akizungumzia kauli ya Chatanda mmoja wa Maafisa wa Idara ya Mawasiliano katika jimbo Katoliki la Arusha aliimbia Rai Mwema kuwa Askofu Josephat Lebulu ambaye ndiye aliyewaongoza maaskofu kutoa kauli ya kulaani mauaji na kutotambua uchaguzi wa Meya, hawezi kulumbana na Katibu wa Mkoa wa CCM kwa kuwa ni mtu mdogo sana katika mamlaka ya nchi.

“Baba Askofu hayuko tayari kujibizana na Katibu wa Mkoa wa CCM. Ni mtu mdogo….kimsingi Maaskofu walikuwa na ujumbe wao kuhusu yaliyotokea na ujumbe wao umefika kwa hiyo kama watawala wamesikia wayafanyie kazi waliyoelezwa”, alisema Afisa huyo.

Mauaji ya watu hao watatu huku wengine zaidi ya 30 wakiachwa na majeraha makubwa ya risasi za moto, kipigo na mabomu ya machozi yameweka historia mpya ya kuwa mauaji ya kwanza kutokana na vurugu za kisiasa kwa upande wa Tanzania Bara tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini ulirasimishwa miaka ya 90.

Tukio la aina hiyo liliwahi kutokea visiwani Zanzibar Januari 26 na 27 ambapo polisi wenye silaha walipambana na wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba mwaka 2000.

Wanachama hao wa CUF walikuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi huo uliokuwa na utata ambapo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilimtangaza Aman Abeid Karume kuwa mshindi hivyo kuzua malalamiko kutoka kwa mgombea wa CUF Maalim Seif Shariff Hamad na wafuasi wake.

Katika tukio hilo la Zanzibar watu 21 waliuawa na polisi na wengine zaidi ya 1000 walikimbilia eneo la Shimoni Mombasa nchini Kenya na kuweka historia ya Tanzania ambayo ilikuwa maarufu kupokea wakimbizi kutoka nchi jirani zilinazokumwa na vita ya mara kwa mara nayo kuzalisha wakimbizi.

Tukio la Arusha nalo sasa limeingia katika kumbukumbu mbaya za kihistoria nchini kutokana na kumwagika kwa damu ya wananchi wasio na hatia huku mali za mailioni fedha nazo zikiteketea kufuatia vurugu kubwa zilizodumu kwa siku nzima.

Maandamano hayo yaliitishwa na CHADEMA kwa lengo la kupinga uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha uliofanyika Desemba 18 mwaka jana ambapo madiwani wa CCM na TLP walimchagua Gaudance Lyimo kuwa Mstahiki Meya wa jiji hilo huku Diwani wa TLP Michael Kivuyo akichaguliwa kuwa Naibu Meya.

Uchaguzi hupo uligombewa na madiwani wa CHADEMA wakipinga hatua ya msimamizi wa uchaguzi huo ambaye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kumruhusu Mbunge wa Viti maalumu kutoka mkoa wa Tanga ambaye pia Katibu wa CCM mkoa wa Arusha Mary Chatanda kuwa mjumbe na kupewa fursa ya kupiga kura.

Awali maandamano hayo yalikuwa yafanyike Desemba 22 mwaka jana lakini yaliahirishwa baada ya kukosa kibali cha polisi na ndipo CHADEMA walipopanga kuyafanya Januria 5 huku wakitoa masharti kwa serikali kukaa mezani na kufanya mazungumzo nao kabla ya muda huo pia kutengua uchaguzi wa nafasi ya umeya.

Katika kipindi hicho chote kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CHADEMA chama hicho kilikuwa katika mawasiliano na ofisi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda,Waziri wa TAMISEMI George Mkuchika na Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa na lengo la mawasiliano hayo ilikuwa ni kufikia muafaka wa suala hilo.

Alisema alisema mwishoni mwa wiki mjini Arusha kuwa pamoja na mawasiliano hayo Jeshi la Polisi mkoani Arusha liliwapatia barua ya kufanya maandamano Januari 4 na barua hiyo ilisainiwa na Kamanda wa Polisi wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji.

Barua hiyo ambayo nakala yake tunayo ina kumbukumbu namba AR/B.5/VOL.11/63 na inaeleza kuwa:”Kimsingi mmekubaliwa kufanya maandamano na mkutano wenu wa hadhara tarehe 5 Januari na pia rejea mazungumzo yetu ya tarehe 3 saa 6 mchana ofisini kwa Kamanda wa polisi wa mkoa…….Katika mazungumzo hayo tuliona kuna umuhimu wa kuchagua route moja itakayotumika kwa maandamano.

Barua hiyo inaeleza kuwa maandamano hayo yataanzia eneo la Philips na kupita barabara kuu ya Arusha-Moshi ,Sanawari kushuka AICC,Sokoine Road,Friends Corner hadi viwanja vya NMC.

Dk. Slaa aliimbia Raia Mwema kuwa baada ya viongozi wa wilaya ya Arusha wa chama chake kupata barua hiyo waliendelea na maandalizi ya mkutano huo hadi jioni yake IGP Mwema alipotangaza kupitia vyombo vya habari kuwa hawataruhusiwa kuandamana na badala yake wamekubaliwa kufanya mkutano wa hadhara tu.

“Sisi hatukukubaliana na kauli hiyo ya IGP na kwanza hakuandika barua yoyote kama taratibu zinavyoeleza kwani sisi ni chama cha siasa na hatufanyi kazi kwa kutumia vyombo vya habari”alieleza Slaa.

Maandamano hayo Januari tano yalianza majira ya saa 6:20 za mchana nje ya hoteli ya kitalii ya Mount Meru iliyopo eneo la Sekei katika Manispaa ya Arusha na yalioongozwa na viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA Dk. Wilbroad Slaa, Freeman Mbowe,P hilemon Ndesamburo, na Wabunge Godbless Lema (Arusha Mjini) na Peter Msigwa (Iringa Mjini).

Waandamanaji wote walikuwa wamefunga vitambaa vyeupe katika mikono yao kuashiria kuwa maandamano yao ni ya amani na vijana wa chama hicho walikuwa wakilinda usalama kuhakikisha kuwa hakkuna waandamanaji wanaoingia miongoni mwao na kuanzisha vurugu.

Wengine ni Wabunge wa viti maalumu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Suzan Lyimo, Rebeca Mngodo, Joyce Mukya na viongozi wa ngazi ya wilaya, Mkoa na na madiwani wote wa chama hicho.

Viongozi hao waliandamana na wafuasi wao wachache waliopata ujasiri wa kujitokeza kufuatia vitisho vya polisi kuwa maandamano yalikuwa haramu , hadi eneo la Kaloleni na muda wote polisi walikuwa wanawatangazia kupitia vipaza sauti kuwa wavunje maandamano hayo na ndipo walipofika eneo hilo polisi walianza kurusha mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi kadhaa hewani kwa lengo la kutawanya maandamano hayo.

Katika eneo hilo polisi waliwatia mbaroni baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao ni Mbowe, Godbless Lema, Lucy Owenya, Basil Lema,Joseph Selasini na wafusi kadhaa.

Wakati viongozi hao wakitiwa mbaroni Slaa na Mbunge wa Moshi Mjini Philemon Ndesamburo walikuwa wameshatangulia katika viwanja vya NMC kwa lengo la kuwapokea waandamanaji na pia kuendelea kuwahamasisha wananchi kuhudhuria mkutano huo.

Ni baada ya kubainika kuwa viongozi wengine wamekamtwa wananchi walioko katika mkutano huo walipoanza kuhamasishana kwenda polisi kwa lengo la kuwatoa na ndipo vurumai ilipoanza upya ambapo polisi walianza kukabiliana na umati mkubwa wa watu kwa kupiga mabomu ya machozi eneo hilo lote.

Vurugu hizo zilisambaa haraka mpaka katikati ya mji wa Arusha ambapo shughuli nyingi za kuchumi zilisimamama huku polisi ambao walionekana kuzidiwa nguvu wakitumia risasi za moto kuwathibiti waandamanaji ambao nao walikuwa wakirusha mawe, matofali na vipande vya mbao.

Hadi kufikia jioni tayari vurugu hizo zilikuwa zimegharimu maisha ya watu na mali ambazo hata hivyo ilikuwa vigumu kufahamu hasara iliyosababishwa na ghasia hizo lakini tayari Arusha ilikuwa imeingia katika historia mbaya ya kuwa mji wa kwanza watu wake kupoteza maisha kwa sababu za kisiasa.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

Tume Utawala Bora kutoa tamko vurugu Arusha

KAMISHNA mpya wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ali Hassan Rajab ameahidi kutoa tamko kuhusu vurugu zilizojitokeza jijini Arusha kati ya polisi na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kufafanua kama kulikuwa na uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora.

Kamishna huyo aliyasema hayo jana Ikulu Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete, yeye pamoja na Katibu wake Mtendaji, Mary Massay.

Alisema, anafahamu kuwa suala hilo limeanza kushughulikiwa na wenzake walioko kwenye Tume hiyo kuahidi kuhakikisha mambo yaliyosababisha vurugu hizo yanafuatiliwa.

“Wananchi wasiwe na wasiwasi, ingawa naamini wenzangu tayari wameanza kulifanyia kazi suala hili, tutafuatilia na kuchukua hatua iwapo itabainika kulikuwa na uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora,” alisema Rajab.

Massay alisema kazi yake ya kwanza itakuwa kuhakikisha Tume hiyo inafanya majukumu yake kwa mujibu wa Katiba, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Serikali inawezesha Tume katika upande wa rasilimali watu na vitendea kazi.

“Pia kazi kubwa itakuwa ni elimu kwa umma ili wananchi watambue haki zao pamoja na kufuatilia matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu na utawala bora,” alisema.

Aliwataka wale wote wanaokiuka haki za binadamu kuwa macho kwani Tume hiyo kamwe haitowavumilia lakini pia aliahidi kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa katika Tume hiyo na kuhakikisha haki inatendeka.

Hivi karibuni mkoani Arusha wakati Chadema ikifanya maandamano yaliyozuiliwa na Polisi, vurugu ziliibuka baina ya wafuasi wa chama hicho na polisi ambapo watu watatu waliuawa baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa kuagiza wafuasi hao kuvamia kituo cha Polisi kuwatoa watuhumiwa.