Pato halisi la taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 6.0 mwaka huu na asilimia 7.2 mwaka 2012.
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo ametoa mwelekeo huo leo bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2010 na malengo ya uchumi katika kipindi cha muda wa kati 2011/12-2015/16.
Amesema, malengo ya sera ya uchumi jumla katika mwaka 2011/12 yatakuwa kuendelea kudhibiti kasi ya upandaji bei ili ibaki kwenye viwango vya tarakimu moja.
Mkulo amesema , lengo lingine litakuwa pia kuongeza mapato ya ndani yatakayofikia uwiano wa asilimia 17.2 ya pato la taifa mwaka 2011/12 na kuendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 17.5 kwa mwaka kwa kipindi cha muda wa kati.
Malengo mengine ni kudhibiti ongezeko la usambazaji wa fedha unaotarajiwa kukua kwa asilimia 19.0 mwaka 2011/12 na asilimia 18.6 mwaka 2012/13 ukilenga kuwiana na malengo ya ukuaji wa uchumi na kasi ya upandaji bei, kuwa na akiba ya fedha za kigeni itakayokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma toka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 4.6.
Mkulo amesema malengo ya sera za uchumi pia ni kupunguza tofauti ya viwango vya riba na kuwa na kiwango imara cha ubadilishanaji wa fedha kitakachotokana na mwendo wa soka la fedha.
“Napenda kusisitiza mambo muhimu ambayo tunahitaji kuyapa msukumo zaidi katika utekekelezaji na ufuatiliaji wa karibu kwa mwaka 2011/12 kama ifuatavyo: kuongoza msukumo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kukuza Pato la Taifa; kuongeza uwekezaji katika maeneo ya kimkakati na yenye mwingiliano kisekta hususan umeme, bandari, reli, maji na chakula cha hifadhi na kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika maeneo hayo.
Kutumia fursa ya nchi yetu kuwa kiungo muhimu kibiashara na nchi zinazotuzunguka ambazo hazina bandari; kuhimiza na kuhamasisha uekelezaji wa kilimo kwanza na kuongeza na kusimamia mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi na kuimarisha usimamizi katika matumizi ya fedha za kigeni” amesema Mkulo.
Mkulo amewaeleza wabunge kuwa, mapato ya ndani yaliongezeka kwa asilimia 8.2 mwaka 2009/10 kufikia shilingi Bilioni 4, 661.5 kutoka shilingi Bilioni 4,293.1 mwaka 2008/09 ingawa kiasi hicho ni pungufu ya makadirio kwa asilimia 8.8 kwa mwaka 2009/10.
Amesema, hadi kufikia Desemba 2010, deni la taifa lilikuwa dola za Kimarekani Milioni 11,380.2 ikiwa ni ongezeko la dola Milioni 654.28 ikilinganishwa na deni la kipindi kama hicho mwaka 2009.
Kwa mujibu wa Waziri Mkulo, Ongezeko hilo linatokana na mikopo mipya ya ndani na nje yenye masharti nafuu kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia idadi ya watu, Mkulo amesema, Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 43,187,823 mwaka 2010.
“Kati ya hao, wanawake walikuwa 21,935,400, sawa na asilimia 50.8 na wanaume walikuwa 21,252,423 sawa na asilimia 49.2.
Tanzania ilikadiriwa kuwa na jumla ya watu 41,914,311 sawa na asilimia 97.1 ya watu wote ambapo Tanzania Zanzibar ilikuwa na watu 1,273,512 sawa na asilimia 2.9 ya watu wote,” amesema Mkulo.
No comments:
Post a Comment