Thursday, June 16, 2011

Rushwa bado ni tatizo kubwa nchini

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora , Mathias Chikawe amekiri kuwa tatizo la rushwa limeendelea kuwa kubwa nchini na mbinu za kutenda makosa hayo zinabadilika siku hadi siku.

Kutokana na hali hiyo, Chikawe amewataka wadau wa rushwa nchini kubuni mikakati shirikishi na endelevu ya kukabiliana na adui huyo mkubwa wa maendeleo na ambaye anazifinyanga haki za wanyonge katika jamii.

Alitoa mfano kuwa, wakati wa uchaguzi mkuu, wanasiasa walilazimika kutoa rushwa kutokana na kulazimishwa na wapiga kura kupewa rushwa ili wawachague.

“Katika mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita mwaka jana kwa mfano haikuwa wagombea ndiyo waliowashawishi wapiga kura kupokea rushwa bali ilikuwa ni kinyume chake,” alisema Chikawe wakati akizindua kongamano la rushwa lililoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Waziri huyo pia aliwataka viongozi wote katika maeneo yao ya kazi kusimamamia utawala bora na kuhakikisha maadili ya kazi yanafuatwa.

“Kwa kufanya hivi naamini tutapunguza kwa kiasi kikubwa kero ya rushwa katika maeneo yetu ya kazi,” alisema Chikawe.

Pia alitoa mwito kwa viongozi wote wa jamii wakiwemo viongozi wa dini na wanasiasa kukemea rushwa na vitendo vya ufisadi kila wanapopata nafasi ya kuzungumza na wananchi.

Chikawe alisema, jitihada za wadau ni lazima zilenge kuwafikisha wananchi katika kuuona ukweli kwamba rushwa ni adui wa haki na kikwazo cha maendeleo na ni chimbuko la dhuluma na umaskini kwa Mtanzania.

Balozi wa Norway nchini Ingunn Klepsvik alisema, rushwa bado ni tatizo la kidunia na kwa hapa Tanzania imechangia kukithiri kwa umasikini. Alisema Norway itaendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na rushwa nchini.

Mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Phillipe Poinsot alisema, ofisi yake itaendelea kusaidia katika mapambano dhidi ya rushwa na wamekuwa wakitoa mafunzo kwa watendaji wa Taasisi ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kuwajengea uwezo wa namna ya kufanya kazi zao za kupambana na rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hosea alisema, kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu ni ‘Kila sekta kujitafakari na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma’.

Alisema, washiriki 200 kutoka sekta zote ambazo takukuru imekuwa inashirikiana nao katika utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (UNCAC) wamealikwa kwenye kongamano hilo. Mada 17 ziliwasilishwa kwenye kongamano hilo

No comments: