Thursday, May 31, 2012

Wanafunzi Chuo Kikuu wabakwa, walawitiwa

WANACHUO wa Chuo Kikuu cha St John mjini Dodoma, leo wamegoma kuingia madarasani hadi wawasilishe malalamiko yao kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zelothe Stephen kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kupigwa nondo, kuibiwa kadi za benki, kompyuta za mkononi, kulawitiwa na kubakwa. Hali hiyo ilisababisha wanafunzi kukusanyika huku wakiwa wamebeba mabango mbalimbali ambayo yalikuwa yakisomeka, ‘Tunaomba ulinzi ili kubaka na kulawitiwa kukomeshwe’, ‘Ulinzi ni haki yetu ya msingi polisi Mko wapi?

 Tumechoka kuwa wajinga katika jamii yetu na Ulinzi Shirikishi stop crime.’ Baadhi ya wanafunzi hao walilaani vitendo vya wenzao kubakwa na kulawitiwa na kudai kuwa katika siku za hivi karibuni, mwanafunzi wa kiume ambaye anasoma mwaka mwaka wa pili aliibiwa na kisha kulawitiwa hali iliyolazimu alazwe hospitali. “Kesi kadhaa zimepelekwa polisi lakini hakuna chochote kinachofanyika,” alisikika mwanachuo moja akizungumza kwa jazba.

Walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu kutokana na kuibiwa vifaa muhimu zikiwemo kompyuta za mkononi hali ambayo hulazimika kuishi kwa hofu. “Juzi wenzetu wamevamiwa usiku na kuporwa simu tano na laptop tatu sasa tunaona maisha yanakuwa magumu sana kwetu kwani usalama wetu sasa ni mdogo,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Walisema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi ambao wanaishi nje ya chuo kwani hata kujisomea nyakati za jioni kumekuwa kwa mashaka kutokana na kuogopa kuvamiwa na vibaka. Walisema baadhi ya wenzao wanaanza mitihani Juni, hali ambayo inawatia hofu kama wimbi hilo la kuvamiwa na vibaka linaweza hata kupunguza ufaulu mioungoni mwao.

Pia walitaja sababu kadhaa ambazo zinadhaniwa kuwa zinasababisha matukio hayo ni chuo hicho kukosa uzio na hivyo kufanya mwingiliano wa watu na wanachuo kuingia chuoni bila kuwa na utaratibu. Walisema kundi lisilojulikana limekuwa na kawaida ya kuvamia sehemu ambazo wanachuo wanakaa na baada ya kuiba vitu mbalimbali humalizia kwa kubaka wasichana au kwa kulawiti kama ni mvulana.

Hata hivyo, juhudi za wanafunzi wao kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa na majukumu mengine ya kikazi, na kutuma mwakilishi wake ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya, Dominic Mlei na Mkuu Mpya wa Polisi wa Wilaya atakayeanza kazi hivi karibuni, Thadeus Malingumu. Kwa upande wake, OCD Mlei alisema ulinzi unaanza rasmi leo, kufanya doria maeneo yanayozunguka chuo hicho na maeneo jirani, pia chuo kijenge hosteli za kutosha na kwa kila hosteli za nje na nyumba walizopanga wanafunzi zitakaguliwa kesho na mapungufu ya kiusalama kwenye makazi hayo yataainishwa na wamiliki wataitwa na hosteli zote zitatakiwa kuwa na mageti na ulinzi wa makazi hayo kuboreshwa.

 Pia alitaka kuundwa kwa mara moja kwa vikundi vya ulinzi shirikishi. Hata hivyo, mtumishi wa Chuo hicho, Mzee Muganda alishauri Kituo Kidogo cha Polisi kijengwe Kikuyu na bidii ya doria iongezwe

Tuesday, May 29, 2012

Mchakato wa Katiba Mpya:Je, Masuala ya Wanawake na Makundi Yaliyoko Pembezoni Yatabebwa?



SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

 UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII Deus Kibamba/TCIB  ATAWASILISHA

MADA: Mchakato wa Katiba Mpya:Je, Masuala ya Wanawake na Makundi Yaliyoko Pembezoni Yatabebwa?   

Lini: Jumatano Tarehe 30 Mei, 2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Monday, May 28, 2012

Sumaye ataka ujasiri kukabili rushwa

WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amewataka Watanzania kujenga ujasiri kukabiliana na rushwa, huku akiwataka viongozi kuwa mfano katika hilo kwa lengo la kulikomboa Taifa kutokana na hali ya umasikini.

Sumaye aliyazungumza hayo jana wakati wa muda wa ‘Busara za kiongozi’ iliyofanyika katika
Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe jijini Dar es Salaam, linaongozwa na Askofu Josephat Gwajima.

Katika busara zake alizozitoa kwa zaidi ya nusu saa, Sumaye alisema matatizo mengi yanayoikumba nchi, yanasababishwa na viongozi wengi wa nchi kukumbatia vitendo vya rushwa huku wakiwaacha wananchi wao wakihangaika.

“Japo kuna gharama zake katika kuzungumzia suala hili, ukweli upo wazi kuwa rushwa,
ufisadi utajiri kwa watu wachache ni matatizo yanayolifanya Taifa hili liendelee kukandamizwa hivyo ni lazima tuwe wajasiri dhidi ya mambo yote mabaya ili tuweze kulikomboa,” alisema Sumaye na kuongeza: Huku akitumia vifungu mbalimbali vya Biblia, Sumaye alisema maendeleo ya nchi yanayoliliwa yamesababishwa na baadhi kuwapa nafasi ya kuongoza viongozi wanaoingia madarakani kwa kutoa rushwa.

Alisema japo wananchi wengi wamekuwa wakishawishika kupokea rushwa kutokana na hali
yao ya umasikini, wanapaswa kubadilika kwa kuepuka kuwachagua viongozi hao ili wasije kujutia kwa kutopata maendeleo pindi kiongozi huyo anapokuwa amechaguliwa.

“Nikisema msipokee bahasha ni sawa na kubeba maji katika gunia, kikubwa ukipokea fikiria
mambo mengi atakayokutendea kiongozi huyo ukijua wazi kuwa kwanza lazima atafute fedha alizowapatia wakati wa kutafuta kura kabla ya kuanza kuwaletea maendeleo,” alisema Sumaye.

Zanzibar yachafuka

KANISA la Assemblies of God liliopo Kariakoo mjini Unguja, limechomwa moto na kuharibiwa vibaya katika vurugu zilizoibuka jana asubuhi.

Waumini wa kanisa hilo walishindwa kufanya Ibada ya Jumapili katika kanisa hilo kutokana na uharibifu mkubwa huku wakiwa na hofu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Aziz Juma alithibitisha kuchomwa moto kwa kanisa hilo juzi usiku wa saa nne na gari moja aina ya Corolla kuharibiwa vibaya.

“Ni kweli Kanisa la Assemblies of God liliopo Kariakoo limechomwa moto na watu wasiojulikana na uchunguzi zaidi kujuwa nani waliohusika unaendelea,” alisema Juma.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo, Dickson Kaganga alisema watu wasiojulikana, walivamia
kanisa hilo saa nne za usiku juzi na kuanza kuwashambulia walinzi ambao walizidiwa na kukimbia.

Kaganga alisema uharibifu mkubwa umefanyika ndani ya kanisa hilo na vifaa vya muziki na vipaza sauti vyote vimeharibiwa.

“Kanisa limeharibiwa vibaya na linahitaji matengenezo makubwa sehemu ya ndani na nje,” alisema. Kanisa hilo lilivamiwa na kutiwa moto mara baada ya viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho kukamatwa na Polisi kwa kufanya maandamano kinyume cha sheria.

Askofu Kaganga aliitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ambalo linahatarisha amani na utulivu pamoja na uhuru wa kuabudu.

Alisema tangu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, amani na utulivu vimeimarika Zanzibar, lakini katika siku za hivi karibuni kumeibuka vikundi vinavyotoa mihadhara ya kidini vimeonesha kutishia amani hiyo.

Polisi, CCM kwavamiwa Awali wafuasi wa jumuiya hiyo inayojishughulisha na mihadhara ya kidini pamoja na kisiasa, walivamia Kituo cha Polisi cha Madema kuwatoa viongozi wao
waliokamatwa.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Khamis alisema Polisi ilifanikiwa kuzima jaribio la
wafuasi wa jumuiya hiyo kuvamia kituo cha Polisi na kuwatoa wafuasi wao.

“Ni kweli wapo baadhi ya viongozi tunawashikilia kwa ajili ya maelezo zaidi na wafuasi wao
wakaja kundi na kuvamia kituo, lakini polisi walipambana na watu hao,” alisema Mussa.

Mussa alisema Polisi inawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhusika na vurugu za jumuiya hiyo pamoja na viongozi wawili wa kikundi hicho.

Alisema Polisi inaendelea na kazi za kuwatafuta zaidi viongozi wakuu wa mihadhara inayotolewa na jumuiya hiyo.

Viongozi wengine wanaotafutwa na Polisi ni Amiri wa jumuiya hiyo, anayetajwa kwa jina moja la Azani pamoja na kiongozi wa Jumuiya ya Mihadhara, Farid Hadi.

Aidha, Polisi imeimarisha ulinzi kwa kutumia helikopta yake ambayo ilionekana ikiruka angani mara kwa mara kwa ajili ya kuimarisha doria.

Kamishna Mussa alithibitisha kuchomwa moto kwa gari moja jirani na Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kisiwandui mjini hapa na uchunguzi zaidi unaendelea.

Mabomu, risasi
Shughuli zote za kibiashara pamoja na kijamii katika eneo la Mji Mkongwe wa Unguja zilisimama kuanzia asubuhi baada ya Polisi kufyatua risasi pamoja na mabomu ya machozi ili kutawanya vikundi vya watu walioaminika kuwa wafuasi wa jumuiya hiyo.

“Shughuli zote za kibiashara hapa zimesita ikiwemo usambazaji wa magazeti hata wauza magazeti wote wameshindwa kufika mjini kufanya biashara,” alisema Farouk Karim ambaye ni Wakala wa Magazeti.

Muuza magazeti maarufu wa Darajani Mji Mkongwe Zanzibar, aliyejitambulisha kwa jina moja la Abel alisema ameshindwa kufika mjini kutokana na fujo pamoja na mabomu ya machozi yanayopigwa na polisi.

“Narudi nyumbani leo sikufanya kazi kwa sababu huko mjini kwenyewe hakufikiki kutokana
na mabomu ya machozi,” alisema Abel.

Vizuizi, doria
Polisi waliweka vizuwizi katika baadhi ya sehemu za miji ikiwamo Michenzani pamoja na barabara za kwenda Ikulu ili kuhakikisha hakuna vikundi vya watu wanaofika maeneo muhimu yakiwamo ya ofisi za Serikali.

Vizuizi hivyo viliwekwa katika maeneo ya kwenda vijijini katika mikoa ya Kusini Unguja na
Kaskazini Unguja ili kuhakikisha hakuna vikundi vya wafuasi wa jumuiya hiyo wanaoweza kuingia mjini kuungana na wenzao waliopo mjini.

Aidha, Polisi walikuwa wakifanya doria hadi katika maeneo ya Ng’ambo ikiwamo Mikunguni
pamoja na Saateni na kurusha mabomu ya machozi kwa lengo la kusambaza vikundi vya watu.

Vikundi hivyo vilikuwa wakiwasha mipira ya gari na kuweka vizuwizi katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Unguja.

Jumuiya hiyo kwa muda wa miezi minne sasa imekuwa ikitoa mihadhara kuhusu marekebisho ya Katiba ya Muungano kwa kuhamasisha wananchi kuukataa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kikundi hicho kilifanya mhadhara wake juzi asubuhi Lumumba na kuanza kufanya maandamano ambayo yalizuiwa na Polisi.

Friday, May 25, 2012

Mnyika Mbunge halali Ubungo

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kilikuwa katika furaha baada ya Mbunge wake wa Ubungo, John Mnyika kuthibitishwa na Mahakama Kuu kuwa Mbunge halali wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Ubunge wa Mnyika ulikuwa unapingwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng’humbi.

Mahakama hiyo jana kupitia kwa Jaji Upendo Msuya, ilitamka kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni halali.

Aidha, Jaji Msuya alisema maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa kwa kuwa hakuthibitisha madai yake na kutakiwa kulipa gharama za kesi hiyo aliyoifungua mwaka 2010, siku chache baada ya kubwagwa na kijana huyo.

Awali kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mahakama hiyo jana ilijaa wanachama na wapenzi wa Chadema na CCM na kusababisha askari Polisi kufanya kazi ya ziada ya kutanda kila mahali katika mahakama hiyo na katika Barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari ili kuimarisha ulinzi.

Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Msuya mahakamani hapo kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi ambapo pia amuru gharama za kesi hiyo kubebwa na Ng’humbi ambaye kabla ya kuwania ubunge mwaka 2010, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Jaji Msuya alisema Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na kutoa ushahidi kuonesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.

Alisema Ng’humbi na mashahidi wake aliowaita mahakamani, hawakuonesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa hapo kwamba yalitendeka na namna gani madai hayo yaliathiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka juzi.

“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii, lakini nimeshangaa ni kwa nini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,” alisema Jaji Msuya.

Alisema hakuelewa ni kwa nini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na kuhoji kama kweli madai hayo yalitokea, ni kwa nini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba cha majumuisho hawakulalamika?

Katika madai ya Ng’humbi ya dosari ya kura zaidi ya 14,000 alizodai hazieleweki zimetoka wapi, Jaji alisema alipata nafasi ya kuhesabu kura walizopata wagombea wote wa vyama vilivyogombea jimbo hilo ambavyo ni 16 na kubaini ilikuwa ni kosa tu la kibinadamu na halina uhusiano wowote na mdaiwa wa pili, Mnyika.

Kwa mujibu wa Jaji Msuya, fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi kwa kuwa ilikosewa kuandika.

Alisema Mnyika alitangazwa kuwa ni mshindi baada ya kupata kura 66,742 wakati Ng’humbi alipata kura 50,544 na wagombea wote kuwa kura 132,496.

Jaji Msuya alisema katika ushahidi wa Ng’humbi, hakuonesha ni vipi ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na vipi Mnyika alihusika na ongezeko hilo.

Kabla ya kuanza kuchambua hoja za Ng’humbi, Jaji Msuya aliwapongeza mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na kuhoji maswali ya msingi.

Alisema mawakili hao hawakupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na msingi wala kuwasilisha pingamizi zinazosababisha shauri kuwa na mlolongo mrefu.

Mnyika aliwakilisha na wakili Edson Mbogoro wakati wakili wa Ng’humbi alikuwa Issa Maige na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Justus Mlokozi.

Kuhusu madai ya Ng’humbi kuwa alidhalilishwa kwa kuitwa fisadi na Mnyika katika mkutano alioufanya katika kampeni kwamba aliuza nyumba ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu wasichague CCM inakumbatia mafisadi, Jaji Msuya alisema hayakuwa na ushahidi.

Alifafanua kwamba Ng’humbi alidai maneno hayo yalizungumzwa na Mnyika katika mkutano uliokuwa na watu zaidi ya 500, lakini yeye hakuwapo. Kutokana na kukosekana kwa uwepo wake, Jaji Msuya alisema Mahakama haichukui maneno ya kuambiwa, bali mtu aliyesikia mwenyewe au kushuhudia.

“Katika watu wote hao 500 waliokuwa katika mkutano huo, hakuja hata mtu mmoja kutoa ushahidi na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.

Kuhusu madai kwamba Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa Chadema katika kujumlisha matokeo, Jaji Msuya alisema ushahidi pekee ni wa Ng’humbi na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi.

Alisema mbali na ulinzi, hata wagombea wengine wangelalamikia jambo hilo, lakini Ng’humbi hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.

Kuhusu madai kuwa Msimamizi wa Uchaguzi alitumia kompyuta za mkononi (laptop) za Mnyika badala ya kompyuta rasmi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na pia hazikukaguliwa kiasi cha kutia shaka kuwa pengine kulikuwa na taarifa zisizo rasmi katika kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na ongezeko lile la kura 14,000, Jaji Msuya alisema ushahidi umeonesha kuwa kompyuta hizo hazikutumika.

Alifafanua kwamba kompyuta zilizotumika zilikuwa za mawakala na kwamba katika madai hayo, Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi kuthibitisha akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu.

“Tofauti ya kura kama nilivyosema nimepiga hesabu na nimeona kuwa ni matatizo ya kibinadam na hakuna athari yoyote katika matokeo ya uchaguzi, ni shahidi wa tatu pekee aliyekuja kutolea ushahidi hili na Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi,” alisema Jaji Msuya ambaye alianza kuisikiliza kesi hiyo kuanzia Aprili 19, mwaka huu na majumuisho ya pande zote yalifanywa Mei 4, mwaka huu.

Baada ya hukumu hiyo, Mnyika alikumbatiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuwapo mahakamani hapo. Pamoja walitoka nje, Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema wakiimba na kushangilia kwa ushindi huo.

Hata hivyo, hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.

Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi ya Sh bilioni mmoja na kutaka kabla ya kusikiliza kesi kama hiyo, uchunguzi ufanyike kwanza ili ikionekana haina hoja za msingi, itupwe mapema.

“Mahakama imetenda haki na hii inaonesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani,” alisema Mbowe.

Naye Ng’humbi alisema amepokea uamuzi uliotolewa, lakini hawezi kusema lolote kwa sasa na kuwataka wana CCM wawe na utulivu kwa sababu anaamini ni watulivu na kama kuna jambo tofauti, atazungumza baadaye.

Hadi sasa, Mahakama imekwisha kutengua matokeo ya ubunge ya mwaka 2010 katika majimbo mawili pekee, Arusha Mjini kwa Godbless Lema wa Chadema na Sumbawanga Mjini lililokuwa la Aeshi Hilary wa CCM.

Majimbo ambayo kesi zao zilitupwa na mahakama na wabunge wake kuendelea na nafasi zao ni Segerea, Kasulu Mjini, Biharamulo, Singida Mashariki, Ilemela, Nyamagana, Kilwa Kusini, Muhambwe na Meatu.

Tuesday, May 22, 2012

Umbali wazuia wanafunzi kuripoti shuleni

WANAFUNZI 200 wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Ulyankulu wilayani hapa mkoani Tabora, hawajaripoti shuleni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hofu ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa, Mkuu wa Shule Msaidizi, Alphonce Makaza alisema kuwa mwaka huu walitegemea kuwa na wanafunzi 602 wa kidato cha kwanza na kwamba walioripoti hadi sasa ni wanafunzi 400.

Alisema umbali uliopo kati ya shule na makazi ya watu, unawakatisha tamaa baadhi ya wanafunzi hususani wa kike ambao wanapolazimika kutembelea umbali mrefu wanaweza kukutana na watu wenye tabia ya unyanyasaji wa kijinsia.

Mwalimu Makaza alitaja sababu nyingine za wanafunzi kutoripoti shuleni kuwa ni mtazamo wa jamii kuhusu watoto wa kike kuwa hawana umuhimu wa kusoma kama ilivyo kwa watoto wa kiume.

Aidha alibainisha kuwa mfumo wa maisha katika ngazi ya familia unawanyima watoto hao fursa ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya elimu na kwamba wanatumika zaidi katika shughuli za kilimo na uzalishaji mali.

Mkuu huyo wa shule msaidizi alisema pamoja na kwamba shule hiyo ina bweni la wanafunzi wa kike lenye uwezo wa wanafunzi 80, lakini waliopo kwa sasa ni 46.

Mwalimu wa nidhamu shuleni hapo, Bahati Msengi alisema kuwa wanafunzi wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga jambo ambalo linahatarisha usalama wa wanafunzi wa kike.

Chikawe Akutana Na Jukwaa La Katiba

Serikali imeombwa kuendelea kuifanyia marekebisho Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayosimamia mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya kwa lengo la kupata Katiba bora na inayoakisi maoni ya wananchi wote.

Akizungumza kwa niaba ya Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Mei 21, 2012) Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Jukwaa hilo Bw. Hebron Mwakagenda alisema ingawa kwa ujumla sheria hiyo ni nzuri, lakini ina mapungufu yanayohitaji kurekebishwa ili kuufanya mchakato huo kuwa huru zaidi.

“Kwanza tunadhani Tume imepata Wajumbe wenye sifa na weledi wa kufanya kazi na kupata Katiba nzuri wakiwemo wajumbe wa Jukwaa wawili walioteuliwa kupitia asasi nyingine,” alisema Bw. Mwakagenda alipomtembelea Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias Chikawe ofisini kwake.

Kwa mujibu wa Bw. Mwakagenda, pamoja na uzuri huo, baadhi ya vifungu katika sheria hiyo kikiwemo kifungu cha 21 kinachozuia wananchi kukusanya na kutoa maoni kinyume na ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Tunadhani kifungu hiki inabidi kibadilishwe ili kuzungatia matakwa ya Katiba,” alisema Bw. Mwakagenda ambaye aliongozana na wajumbe wengine watano kutoka Jukwaa hilo.

Wengine ni Bi. Ussu Mallya, Bw. William Kahale, Bi. Sara Mkenda, Bi. Gloria Mafore na Bw. Almando Swenya. Pamoja na mambo mengine, kifungu hicho kinatoa adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya shughuli ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi kinyume na Sheria hiyo.

 Bw. Mwakagenda pia alipendekeza kuwa kifungu cha 22 cha Sheria hiyo kifanyiwe marekebisho na kujumuisha makundi mbalimbali ya kijamii kutoka nchini kote yaingizwe. Kwa upande wake Bi. Mallya alipendekeza Serikali kuendelea kuzingatia usawa wa kijinsia katika utekelezaji wa majukumu yake hasa katika uteuzi wa nafasi muhimu.

 “Ukiangalia wajumbe wa Tume, kuna wanawake 10 na wanaume 20, nadhani wakati mwingine Serikali izingatie usawa,” alisema Bi. Mallya. Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo, Chikawe alisema ni nia ya Serikali kuona Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawezeshwa ili itekeleze majukumu yake kwa uhuru. “Serikali kupitia Mheshimiwa Rais ndiyo iliyoanzisha mchakato huu.

Ni nia yake kuona jukumu hili linatekelezwa kwa uhuru na wazi ili tupate Katiba nzuri,” alisema Waziri Chikawe na kuongeza: “Hili la usawa wa kijinsia tunakwenda vizuri na kama unavyofahamu tumeongeza usawa kwa kiasi kikubwa. Ni dhamira ya Serikali kuona tunasonga mbele zaidi…sasa tuna kiongozi wa mhimili mwanamke,” alikumbusha Chikawe.

Pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali, Waziri Chikawe aliwasihi wadau mbalimbali kupelekeza maoni yao kwa Tume hiyo yenye ofisi zake jijini Dar es Salaam. “Kile ni chombo huru, wadau mbalimbali wasisite kwenda na kutoa maoni yao kwa uhuru,” alisema Chikawe aliyeteuliwa hivi karibuni kuongoza Wizara hiyo kutoka Ofisi ya Rais, Utawala Bora.

Friday, May 18, 2012

‘Madaraka ya Rais yajadiliwe’

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wazi masuala kitakayotetea kuwa katika Katiba mpya huku kikiruhusu wananchi kuamua kuhusu masuala ya madaraka ya Rais na uteuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi.

“Sisi CCM tumeona suala hili tuwaachie wananchi walijadili na kuamua wenyewe wanaona Rais apewe madaraka ya aina gani. Ni fursa yao kupendekeza apunguzwe, aongezwe madaraka au madaraka yake yaweje,” alisema Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.

Katika eneo la Tume Huru ya Uchaguzi, Nape aliyezungumza na vyombo vya habari jana, alisema eneo hilo limekuwa gumzo hasa nyakati za uchaguzi huku malalamiko mengi yakiegemea katika utaratibu uliotumika kuteua wajumbe wa Tume hiyo.

Alisema mapendekezo hayo yaliamuliwa katika semina ya wajumbe wa NEC kuhusu mchakato wa Katiba mpya iliyomalizika hivi karibuni Dodoma.

“Chama kimeona suala hilo lijadiliwe na wananchi na wapendekeze utaratibu mwafaka wa kuteua Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema Nape.

Alitaja masuala mengine ambayo chama hicho kimeona wapewe wananchi fursa ya kuchangia maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi na ikiwezekana yabadilishwe, kuwa ni masuala yanayosababisha kero za Muungano na utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Uteuzi wa mawaziri Alitaja pia maeneo ya kujadiliwa kuwa ni eneo la uteuzi wa mawaziri, waziri mkuu, muundo wa Bunge, Baraza la Wawakilishi na aina ya wabunge na wawakilishi, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais ambapo kwa sasa, mfumo hauruhusu suala la mgombea binafsi.

“Kuna watu wanadhani kuwa CCM inaogopa mgombea binafsi, si kweli, hatuna tatizo na hilo na ndiyo maana tumeliweka hili watu walijadili na kuamua watakavyo, ingawa kwa mtazamo wangu, mgombea binafsi ni kitanzi kwa upinzani,” alisema.

Aidha alitaja maeneo mengine kuwa ni uwepo wa Baraza la pili la Kutunga Sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa Serikali ya Muungano na mfumo wa Mahakama.

Pia chama hicho kilitoa mapendekezo yake juu ya masuala ya msingi yanayofaa kuingizwa kwenye Katiba, kuwa ni pamoja na maadili ya viongozi kupewa nguvu kikatiba na Serikali kuendelea kuwa mmiliki mkuu wa rasilimali zote za nchi.

Katika masuala ya msingi ya kuingizwa katika Katiba yaliyopendekezwa na chama hicho, ilikuwa suala la maadili ya viongozi kuingizwa na kutambuliwa kikatiba ili kudhibiti wabadhirifu na wasio na maadili, kwa kuwa kwa sasa hata Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi haina meno ya kutosha kama inavyotarajiwa.

“Kutokana na yaliyotokea juzi ya mawaziri kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma, ni vema suala hili la maadili likajengewa nguvu ya kikatiba, kuliko ilivyo sasa lakini pia sera ya sasa ya Serikali kuwa mmiliki wa rasilimali kuu za nchi, iendelee hususan eneo la ardhi,” alisisitiza.

Serikali mbili Aidha, alitaja maeneo mengine ambayo chama hicho kimependekeza yaingizwe kwenye Katiba mpya kama msimamo wake, kuwa ni kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuendelea kubaki na muundo wa serikali mbili ya Muungano na ya Zanzibar.

“Serikali mbili ndiyo sera ya CCM, tumejadili na kuona haina upungufu, ila ukumbi uko wazi kwa wanaoona tofauti kutoa maoni yao kwa Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba Mpya,” alisema.

Alitaja maeneo mengine yaliyopendekezwa kuingizwa kwenye Katiba mpya kuwa ni kuendelea na mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama), kuendelea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na umoja wa kitaifa, amani, utulivu, usawa na haki.

Maeneo mengine aliyotaja ni kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalumu na kuzingatia haki ya kupiga kura.

“Eneo hili limetujengea heshima kidemokrasia, kwani kuna nchi ambazo marais wao wako madarakani muda mrefu na hawataki kuondoka.”

Katika kipengele cha uchaguzi mdogo alisema CCM ilishatoa msimamo wake, ambapo ilipendekeza inapotokea mbunge amefariki dunia au kung’olewa madarakani kisheria, chama kilichokuwapo madarakani kipewe nafasi ya kuteua mrithi wake kama inavyofanyika sasa kwa wabunge wa viti maalumu. “Tulishasema hili tukaambiwa CCM tunaogopa uchaguzi mdogo.”

Aidha, Nape alitaja maeneo mengine ya kuingizwa kwenye Katiba, kuwa kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa haki za binadamu, kuheshimu usawa mbele ya sheria, kuendeleza sera ya Dola kutokuwa na dini rasmi na kuruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka.

Maeneo mengine ni kuimarisha madaraka ya umma, kuhamasisha sera ya msingi wa kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine maalumu katika jamii, kusimamia hifadhi ya mazingira na kuendelea kuwapo kwa Rais Mtendaji.

Nape alisema mapendekezo hayo yataandaliwa kimaandishi na kukabidhiwa kwa Tume ya Kukusanya Maoni kwa ajili ya Mchakato wa Katiba Mpya na masuala ya kujadiliwa yatapelekwa kwa wanachama wa chama hicho ili waweze kujiandaa kuchangia.

Thursday, May 17, 2012

Chadema ‘wamvaa’ Shibuda

BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha) limeeleza kushitushwa na kauli ya Mbunge wake wa Maswa Mashariki, John Shibuda kwamba atagombea urais mwaka 2015 kwa tiketi ya Chadema.

Akiwa kwenye semina ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyoandaliwa na Taasisi ya Kutathmini Utawala Bora Afrika (APRM) juzi Dodoma, Shibuda alisema atafanya hivyo na kumwomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake. Kikwete atakuwa amemaliza muda wake wa uongozi.

Taarifa iliyotolewa jana na Bavicha ikiwa imesainiwa na John Heche ambaye ni Mwenyekiti wake, ilieleza kushangazwa na kutoa kauli hiyo katika kikao cha NEC ya CCM; kumtangaza Kikwete kuwa meneja wake wa kampeni na kusema hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi zaidi ya CCM, na kutoa kauli kwa niaba ya APRM.

“Mambo hayo manne ndiyo yametushtua na kutufedhehesha sana sisi vijana wa Chadema na ndiyo maana tumelazimika kutoa kauli kuhusu suala hili,” ilisema taarifa.

Ikifafanua kuhusu kauli yake, Bavicha ilisisitiza kwamba kamwe haitaruhusu mgombea urais wa Chadema awe na Meneja wa Kampeni ambaye ni Mwenyekiti wa CCM hata siku moja, “ kwani tunao watu wa kutosha na wenye uwezo wa kutosha kufanya kazi hiyo na hatuhitaji msaada huo.”

Taarifa pia ilisema haitaruhusu mgombea urais wa Chadema awe anatangaza nia kwenye vikao vya CCM, kwa kuwa chama hicho tawala hakina mamlaka ya kuteua mgombea wa Chadema. “Kama Shibuda alikuwa hajui hilo, anapaswa kulifahamu kuanzia sasa, kuwa vijana wa Chadema hatuchaguliwi mgombea na NEC ya CCM, kwani Chadema kuna vikao na taratibu zetu za kuteua wagombea,” ilisema taarifa.

Kuhusu kauli ya kutokuwapo chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi, taarifa ilisema ni kudhalilisha vijana wa Chadema na Watanzania ambao wanaiona Chadema kama tumaini pekee la kuwakomboa.

“Kauli hii tunaamini vijana wa Chadema, kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuiachia bila kutakiwa maelezo ya kina, tutaitisha kikao cha Baraza na tutaijadili na kuwasilisha mapendekezo yetu kwenye vikao halali vya chama,” ilisema taarifa ya Bavicha.

Walimwambia Shibuda, kuwa kama anaona haendani na utamaduni wa chama hicho na kuwa hakina uwezo wa kuongoza Dola aondoke.

“Ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza Dola, kwani lengo la chama chochote ni kuchukua Dola na si vinginevyo”.

Taarifa hiyo iliwahakikishia vijana nchini, kwamba wawe tayari kwani Chadema imejiandaa kikamilifu kuongoza Dola na kwamba wasiwe na hofu na maneno yaliyotamkwa na Mbunge huyo.

Heche katika taarifa hiyo, aliwataka vijana wote Chadema wajiandae kukabiliana na mtu yeyote atakayeonekana kuwa kikwazo kwa chama chao kuelekea kuchukua Dola mwaka 2015.

Monday, May 14, 2012

BoT- Nchi ina ‘dola’ za kutosha

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hazina ya Taifa inazo fedha za kigeni za kutosha za kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.

Aidha, imehadharisha kwamba taarifa zozote zisizo na ukweli zinazotolewa kuhusu hali ya fedha za kigeni ya nchi, zinaweza kuleta matatizo makubwa ya kiuchumi.

Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema jana kwamba hazina ya taifa ina akiba ya Dola za Marekani bilioni 3.6 inayotosheleza mahitaji ya kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.

“Akiba ya fedha za kigeni hivi sasa ni Dola za Marekani bilioni 3.6, hizi zinatosheleza kuendesha nchi kwa miezi minne ijayo.

Tumewahi kulisema hili, tumezungumzia haya katika Kamati ya Bunge na hata taarifa hizi zipo IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa),” alisema Profesa Ndulu alipozungumza na gazeti hili kwa simu.

Profesa Ndulu alisema kiasi hicho cha hazina ya taifa kinakidhi vigezo vya IMF ambavyo vinataka akiba hiyo itosheleze mahitaji ya nchi husika siyo chini ya miezi mitatu. Aliongeza kuwa hata pamoja na ukweli kwamba thamani ya Euro imeshuka duniani, lakini hali hiyo haijaathiri hazina hiyo ya Taifa, na kwamba uingizaji wa bidhaa ndani ya nchi umeongezeka.

Gavana huyo alitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti hili kutaka kujua ukweli wa hazina ya taifa na hasa kutokana na taarifa ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), akihoji ukimya wa BoT katika masuala mbalimbali ikiwamo hazina hiyo na taarifa zinazohusu uchumi hasa suala la mfumuko wa bei.

“Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu. Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kupata habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011,” alieleza Zitto katika taarifa hiyo aliyoituma kwa vyombo vya habari. Hata hivyo jana jioni BoT iliongeza taarifa za Januari mwaka huu.

“Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya Novemba mwaka 2011! Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Novemba mwaka 2011.

“Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.Taarifa zinafichwa,” alidai Zitto na kumshauri Profesa Ndulu.

“Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka. Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili). Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.”

Hata hivyo, katika ufafanuzi wake Profesa Ndulu alisema wamebadilisha mfumo wa utoaji wa taarifa kila mwezi na sasa wanatoa kila baada ya miezi miwili na kwamba Kamati maalumu ilikutana Februari mwaka huu na taarifa zake zilitarajiwa kuwekwa katika tovuti ya benki hiyo jana.

“Tumebadilisha mfumo wa Kamati ya Sera ya Fedha ambayo sasa inakutana kila baada ya miezi miwili…mara ya mwisho ilikutana Februari na leo (jana) taarifa zao zitakuwa katika website (tovuti). Kulikuwa na matatizo ya kiufundi, lakini taarifa hizo zitakuwapo pamoja na taarifa rasmi kuhusu hazina ya taifa,” alisema Gavana.

Lakini Profesa Ndulu alionya kuwa si vyema kutoa taarifa zisizo sahihi zinazoweza kusababisha matatizo ya kiuchumi, ikiwamo soko la kubadilisha fedha kwenda ovyo na hivyo thamani ya Shilingi kuporomoka ghafla.

Wednesday, May 9, 2012

Kima cha chini kuwa Sh180,000

  • NI BAADA YA MAJADILIANO YA SERIKALI NA TUCTA
KUNA taarifa kwamba Serikali imekubali kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma kwa kati ya asilimia 20 na 33.3 katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13.Hatua hiyo inamaanisha kwamba kima cha chini cha mshahara sasa kitakuwa kati ya Sh180,000 hadi Sh200,000 kutoka Sh150,000 zinazolipwa sasa.Vyanzo vya habari kutoka serikalini vimeeleza kwamba nyongeza hiyo ya kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 ni matokeo ya mazungumzo kati ya Serikali na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta).Mbali ya kutaja kima hicho, vyanzo hivyo vimeeleza kuwa nyongeza hiyo inaweza kuvuka Sh50,000 kutegemea uwezo wa Serikali.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), George Yambesi alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo alijibu kwa kifupi kuwa hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia hilo.

“Sipo katika ‘position’ (nafasi) nzuri ya  kuzungumzia hilo, nadhani suala la mishahara. Mheshimiwa Rais alishalizungumzia kwenye hotuba yake ya Sikukuu ya Wafanyakazi,” alisema.

Katika hotuba yake kwenye kilele cha sherehe hizo zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Rais Jakaya Kikwete alisema Serikali inatambua mazingira magumu ya kazi waliyonayo wafanyakazi na kwamba ipo tayari kuyaboresha.

Alisema imesikia madai ya wafanyakazi na itaendelea kuyafanyia kazi. Madai aliyoahidi kuyafanyia kazi ni pamoja na kupunguziwa kodi ya mapato.

Kwa upande wa Tucta, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicolaus Mgaya alipoulizwa jana alisema hajui Serikali itaongeza mshahara kwa kiasi gani lakini akasema anaamini kuwa ni sikivu.

Alisema kwa miaka mingi wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia mishahara midogo ambayo haikidhi mahitaji, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa migongano ya hapa na pale na Serikali akasema kutokana na hali hiyo, wanaamini kuwa wataongezewa.

“Tunaamini linaweza kutekelezeka (suala la kuongezewa mishahara), lakini hakuna anayejua nyongeza hiyo itakuwa ni kiasi gani, kwa hiyo ukinitajia kiwango nashindwa kuelewa umekitoa wapi,” alisema Mgaya alipoulizwa kama nyongeza hiyo ni kati ya Sh30,000 na 50,000.

Mgaya alisema mbali na kuomba nyongeza mshahara, Tucta pia imeiomba Serikali kupunguza gharama za tozo za mifuko ya hifadhi ya jamii huku ikienda pamoja na udhibiti wa mfumuko wa bei ambao umekuwa kikwazo kwa wafanyakazi na kuwafanya kuishi katika mazingira magumu kiasi cha kushindwa kujituma ipasavyo na wengine kukimbilia kwenye sekta binafsi.

“Wafanyakazi ni tabaka kubwa, lakini limesahaulika. Hii inatokana na Serikali kushindwa kusikiliza kilio chao cha kuwaongezea mishahara jambo ambalo limechangia kulipwa ujira mdogo na kusababisha wengi wao kukimbilia kwenye sekta binafsi, kutokana na hali hiyo tunaamini kuwa Serikali itasikilia kilio chetu,” alisema.

Madai ya wafanyakazi

Sakata la mshahara wa wafanyakazi liliibua mgogoro mkubwa baina ya Serikali na Tucta na mwaka 2010, Shirikisho hilo liligoma kumwalika Rais Kikwete kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa kama ilivyokuwa utamaduni wake.

Hatua hiyo ya Tucta ilitokana na kile lilichodai kuwa Serikali siyo sikivu na lilitumia siku hiyo kujadili na kutoa tamko la kuitaka kutangaza kima kipya cha mshahara cha Sh315,000 ndani ya siku mbili la sivyo wafanyakazi wa umma wangeingia katika mgomo nchi nzima.

Hatua hiyo ilimlazimu Rais Kikwete kuitisha mkutano na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam Mei 3, 2010 na kujibu hoja mbalimbali za Tucta na kuweka msimamo wa Serikali kuwa haiwezi kulipa kiasi hicho cha fedha.

Rais Kikwete aliwatuhumu viongozi wa Tucta kuwa ni waongo na kwamba walikuwa hawasemi ukweli juu ya kile walichokuwa wanabaliana katika vikao vyake na Serikali.

Alisema Serikali ikifanya kima cha chini kuwa Sh300,000 kwa watumishi wa umma, itabidi iwalipe Sh6.9 trilioni kwa mwaka wakati makadirio ya makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwaka 2010/11 ni Sh5.8 trilioni.

Tuesday, May 8, 2012

Mkapa aunguruma mahakamani Dar es Salaam

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (73) amepanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam kumtetea aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Katika kesi hiyo, Profesa Mahalu anadaiwa kuiibia Serikali Sh. bilioni 2 katika ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini humo.

Huku Mahakama hiyo ikiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, Mkapa aliwasili saa 4.45 na kutoa ushahidi kuanzia saa 5.32 asubuhi na kumaliza saa 7.08 mchana.

Katika ushahidi wake, Mkapa alimmwagia sifa Profesa Mahalu kuwa ni mchapa kazi, mwenye heshima na mwaminifu mkubwa.

Alidai kuwa hajui aliyemshitaki mahakamani ni nani kwa sababu mpaka anaondoka madarakani, mchakato wa ununuzi wa jengo hilo anajua ulikwenda sawa.

“Namfahamu Balozi Mahalu kama msomi mzuri, mtumishi mwadilifu …na balozi wetu Bon, Ujerumani,” alidai mahakamani Mkapa alipoulizwa anamfahamu vipi Profesa Mahalu.

Huku akiongozwa na Wakili wa Upande wa Utetezi, Alex Mgongolwa mbele ya Hakimu

Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta; mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:
Wakili: Mwaka 1995 hadi 2005 ulikuwa wapi?

Mkapa: Nilikuwa Dar es Salaam nikishika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania.

Alipoulizwa uzoefu wake katika mambo ya kimataifa, alifafanua kuwa alipata kuwa Ofisa wa Mambo ya Nje na Balozi wa Tanzania katika nchi za Nigeria, Canada na Marekani.

Wakili: Ukiwa Rais unafahamu nini kuhusu ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia?

Mkapa: Nilifahamu Balozi wetu alifanya ununuzi wa jengo kwa euro 3,098,741.40 kwa maagizo ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa wakati huo alikuwa Profesa Mahalu.

Wakili: Katika ununuzi mlipewa masharti yoyote?

Mkapa: Ndio, mimi nilielezwa kuwa mmiliki wa jengo alitaka alipwe mara mbili, kiasi kimoja akaunti moja na kiasi kingine akaunti nyingine na akaunti zote ni za mtu mmoja ambaye ndiye mmiliki wa jengo.

Maelezo mengine ya Mkapa

Mkapa aliendelea kudai kuwa Serikali ilitoa baraka na yeye alitaarifiwa na hakuzuia, kwa sababu nia yake ilikuwa ni kupata jengo kwa ajili ya ofisi za ubalozi, hivyo masharti hayo hayakuwa kizuizi kwake.

Kuhusu mikataba miwili iliyosainiwa katika ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa yeye hakumbuki kama alijulishwa, anachojua ni kwamba fedha zingelipwa katika akaunti mbili.
Amshangaa Lumbanga

Rais huyo mstaafu alidai kumshangaa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashitaka katika kesi hiyo, Matern Lumbanga, kwa madai yake mahakamani hapo kuwa Serikali haitambui ununuzi wa jengo hilo.

“Namshangaa sana, kwa nini alisema hivyo wakati mimi Rais nilikuwa na taarifa!” Alisema huku akionesha mshangao.

Mkapa katika ushahidi wake alidai kuwa angeweza kuzuia ununuzi wa jengo hilo, lakini aliona umuhimu wa kulinunua akatoa amri linunuliwe, ingawa nchi ilikuwa kwenye matatizo ya fedha na fedha za ununuzi huo zingeweza kwenda katika mambo mengine.

JK atajwa

Mkapa alipewa taarifa ya kumbukumbu za Bunge ambamo Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo (Rais Jakaya Kikwete), akitoa taarifa bungeni kuwa mwaka 2001/02 wizara hiyo ilinunua jengo hilo la ofisi ya ubalozi Italia kwa Sh bilioni 2.9.

Kikwete katika taarifa hiyo ya Bunge, alieleza kuwa lengo ni kuondokana na adha ya kupanga kwenye majengo ya watu na kwamba ununuzi wake ulifuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na ushauri wa watathimini wa Wizara ya Ardhi na Wizara ya Ujenzi.

Baada ya kusomewa taarifa hiyo, Mkapa aliulizwa na Wakili Mgongolwa kama kuna usahihi katika taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, akajibu kuwa taarifa hiyo ilikuwa sahihi na ndicho anachotambua yeye akiwa Rais wakati huo.

Mkapa alipoulizwa kama kuna malalamiko yoyote kuhusu mchakato wa ununuzi wa jengo hilo yaliyotolewa na Serikali ya Italia au mmiliki wa jengo kuwahi kuyapata baada ya ununuzi, alijibu kwa kifupi. “Hapana.”

Kuhusu mawasiliano kati ya Serikali na Balozi Mahalu, Mkapa alidai kuwa balozi anaweza kuandika barua kwa waziri wake ambaye ni wa Mambo ya Nje, au Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Rais moja kwa moja na kuongeza kuwa mawasiliano mengine yanaweza kufanyika kwa mdomo tu.

Aliongeza:“Inategemeana na unyeti wa jambo mnalowasiliana.”

Mawakili wa Serikali

Katika maswali na majibu na mawakili wa Serikali, Wakili Vincent Haule alitaka kujua tofauti kati ya kiwango alichodai kufahamu cha ununuzi wa jengo hilo cha euro milioni 3.09 na kiwango kilichotajwa bungeni kuwa ni gharama ya jengo hilo Sh bilioni 2.9.

Mkapa alijibu kuwa yeye mambo ya viwango vya kubadilisha fedha hakuyajua kwa wakati huo, ndiyo maana akataja bei aliyokuwa akiijua na kwamba hiyo haikuwa kazi yake kujua.

Ashtuka Mahalu kushitakiwa

Mkapa alidai kuwa hajui aliyeagiza upelelezi dhidi ya ununuzi wa jengo hilo na pia hajui kama upelelezi ulifanywa akiwa madarakani au la, ila alipata taarifa za kushitakiwa Mahalu siku aliyoletwa mahakamani kusomewa mashitaka na pia aliona kwenye magazeti kesho yake.

Alipohojiwa na Wakili Haule kuhusu ruhusa aliyoitoa kwa mdomo kwa Mahalu kama ilikuwa ya kuridhia mikataba miwili au kuingiza malipo ya jengo katika akaunti mbili alijibu: “Mimi niliagiza ununuzi huo mambo mengine sijui, si kazi yangu mambo ya makaratasi.

“Nilitoa maelekezo … utekelezaji ni kazi ya wizara, lakini mwisho tulipata ubalozi nilioutaka,” alisisitiza Mkapa.

Alipohojiwa na Wakili Ponziano Lukosi kuhusu uhusiano wake na Lumbanga, Mkapa alidai alimwamini Katibu Mkuu Kiongozi huyo wa zamani na kumshirikisha katika mambo yote na pia alijua ununuzi wa ubalozi si Italia tu, ila ni pamoja na Marekani, Uingereza na India na akashangaa kudai kwake mahakamani hapo kuwa hajui.

Alipoulizwa kama anakumbuka jengo lingine walilowahi kununua kwa mfumo huo wa kuingiza fedha katika akaunti mbili, alijibu kwa ukali kidogo; “nakumbuka lakini siwezi kusema…kwa sababu mambo mengine yanaweza kuharibu uhusiano wa nchi na nchi.”

Baada ya kuonesha ukali kidogo, Hakimu Mgeta aliuliza kama mazingira hayo yapo na Mkapa akajibu kwa kifupi: “Yapo”.

Akijibu swali la Lukosi, aliyetaka kujua kama kulipwa katika akaunti mbili muuzaji wa jengo hilo, haoni kuwa alikuwa akikwepa kodi katika nchi yake, alijibu: “Nitasema kuwa hilo ni tatizo la nchi yake, mimi nimepata jengo nililolitaka nasema alhamdulilah!”

Kuna wizi?

Akijibu swali la mwisho la Lukosi kuwa kwa ulipaji huo wa akaunti mbili haoni kuwa ulikuwa ni wizi wa mshitakiwa Mahalu, alijibu; “nitashangaa sana na nitakushangaa wewe, Mahalu ni mwaminifu sana.”

Baada ya jibu hilo, Mkapa alitaka kuongeza neno, lakini akasita akidai: “Unanichokoza utanifanya niongee mengine mengi (anacheka).”

Kesi hiyo inaendelea leo mahakamani hapo ambapo mshitakiwa wa pili, Grace Martin ambaye alikuwa ofisa wa ubalozi Italia atatoa ushahidi wake.

Friday, May 4, 2012

Rais Kikwete ateua wabunge wapya

WAKATI kukiwa na shauku ya kutaka kujua Rais Jakaya Kikwete atakuja na Baraza gani la mawaziri, amefanya uteuzi wa wabunge watatu wapya.

Amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa mamlaka ya uteuzi aliyonayo chini ya Ibara ya 66(i) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, iliwataja wateule hao kuwa ni Profesa Sospeter Muhongo, Janet Mbene na James Mbatia. Uteuzi huo unaanza mara moja.

Kuteuliwa kwa wabunge hao watatu kunaleta hisia kuwa huenda miongoni mwao wakapata nafasi ya kuwa mawaziri kama Rais atafanya mabadiliko katika Baraza lake kutokana na tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa baadhi ya mawaziri wake.

Kwa mujibu wa Ibara iliyotajwa hapo juu, Rais ana mamlaka ya kuteua wabunge 10 kujiunga na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wabunge hao walioteuliwa wanafanya idadi ya waliokwishateuliwa kufikia sita.

Wengine wa awali ni Zakia Hamdan Meghji, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa ambaye hivi sasa ni Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Shamsi Vuai Nahodha ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanadai kuwa uteuzi huo unaonesha dalili zote za Rais kuwa tayari kutangaza mabadiliko katika Baraza lake, katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Pia ripoti tatu za Kamati za Bunge za mwaka 2009/10, ambazo zimependekeza kuwajibishwa kwa baadhi ya watendaji serikalini, wakiwamo mawaziri wanane.

Taarifa iliyowasilishwa katika mkutano uliopita wa Bunge, ilizua mjadala mkali miongoni mwa wabunge hata kufikia kutaka kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Hata hivyo, lengo lao lilikuwa ni kushinikiza mawaziri waliotajwa kwa ubadhirifu na CAG wajiuzulu kama si kuondolewa.

Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi anakuwa mpinzani wa pili kuteuliwa na Rais Kikwete tangu aingie madarakani mwaka 2005.

Mpinzani wa kwanza kuteuliwa na Kikwete ni Ismail Jussa Ladhu wa CUF, ambaye ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Zanzibar ambaye aliteuliwa katika muhula wa kwanza wa Rais Kikwete.

Hii ni mara ya pili kwa Mbene kuteuliwa na Rais Kikwete kuwa mbunge na hivi karibuni aligombea ubunge wa Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM lakini hakufanikiwa.

Profesa Muhongo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye anateuliwa kwa mara ya kawanza, ni Profesa wa Heshima wa Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini; mjumbe wa Taasisi ya Kitaaluma ya Jiolojia ya London, Uingereza; Mjumbe wa Heshima wa Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya China, Mjumbe wa Heshima wa Taasisi ya Kitaaluma ya Sayansi ya Nchi Zinazoendelea (FTWAS).

Pia ni mjumbe wa Taasisi ya Kitaaluma ya Jiolojia ya Afrika (FGSAf) na Mjumbe wa taasisi zingine nane za kitaaluma za Sayansi duniani.

Alikuwa mtu wa kwanza kushinda tuzo ya Robert Shackleton mwaka 2004 baada ya kufanya utafiti kuhusu Jiolojia Afrika. Ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Ramani ya Jiolojia ya Dunia (CGMW). Hakupata kuingia katika masuala ya siasa huko nyuma.

Mawaziri ambao walitawala mjadala wa Bunge huku wabunge wakiwatolea macho ili wang’oke ni Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, William Ngeleja (Nishati na Madini), Omari Nundu (Uchukuzi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Waziri wa Viwanda na Biashara).

Hata hivyo taarifa ya Ikulu haikusema wabunge hao wateule wataapishwa lini na wapi, lakini Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alipoulizwa jana alisema alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, mtu yeyote anayeteuliwa kuwa mbunge, ataapishwa katika mkutano wa Bunge unaofuata baada ya uteuzi wake, bila kujali ni mbunge wa kuteuliwa au wa jimbo.

Ndugai alisema kwa msingi huo, wabunge hao wateule wataapishwa wakati wa Mkutano wa Nane wa Bunge la Bajeti unaotarajiwa kuanza mjini Dodoma, Juni 12.

Alipoulizwa itakuwaje ikitokea wateule hao wa Rais wakateuliwa pia kuwa mawaziri na kuendelea na kazi kabla ya kuapishwa kuwa wabunge, Naibu Spika alisema kwa hali ya kawaida, hilo haliwezekani.

“Kwa mujibu wa Katiba, mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na anakuwa mbunge mteule hadi pale anapoapishwa, na ndiyo maana baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu, kazi ya kwanza ya Bunge ni kuchagua Spika na Naibu Spika, ambao baadaye watafanya kazi ya kuwaapisha wabunge, na ndipo atateuliwa Waziri Mkuu na kisha mawaziri,” alifafanua Naibu Spika.

Thursday, May 3, 2012

TGNP Yawapiga Msasa Waandishi wa Habari


Na Deogratius Temba
WAANDISHI wa habari wameaswa kubeba sauti za wananchi walioko pembezoni katika  kudai haki zao hasa wakati wa  mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kwaajili ya kuandaa katiba mpya.
Akizungumza Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia kilichoko chini ya Mtandao wa  Jinsia Tanzania (TGNP) Dorothy Mbilinyi, amesema watanzanzia masikini walioko pembezoni wanategemea kupata taarifa na kutoa taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

“ Wananchi wameamka  wameanza kujieleza  vyombo vya habari vinatakiwa kufanya kazi yake kuwa sauti ya wanyonge, viwe mdomo kwa makundi yaliyowekwa pembezoni, ili kuibua changamoto zilizojificha na kuyafanya makundi haya kuwa na haki sawa na wengine,” amesema Mbilinyi.

Mbilinyi amesema kuwa vyombo vya habari vya Tanzania vimefanya kazi kubwa ya kuibua kero  za wananchi na ufisadi, ikiwepo kudai uwajibikaji katika misingi ya demokrasia na haki za biandamu.
Aidha amewataka waandishi wa habari kufanya  kazi kwa bidii mwaka huu kwasababu ni mwaka wenye changamoto nyingi ambazo zitahitaji  weledi, uadilifu, ukweli na uwazi.” Huu nini mwaka wa kukusanya maoni ya katiba, mwaka wa kudai uwajibikaji kwa viongozi wasio waadilifu, na ni mwaka wa Sensa ya idadi ya watu…” amesema Mbilinyi.

Akieleza malengo ya mafunzo hayo ya siku tatu yaliyoanza mei 3 hadi 5, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na habari, Lilian Liundi amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia waandishi wa habari kujitadhimini upya jinsi ambavyo wanaandika habari za kijinsia.
Pamoja na kujitadhimini waandishi wa habari watajifunza juu ya hali ya sasa ya  ujenzi wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi, kampeni ya haki uchumi,  mfumo dume na mfumo uleberali mambo leo.

Pia watajifunza namna ya kuandika habari za kijinsia na kuchambua maoni yanayotolewa na wananchi juu ya katiba mpya, kufanya  habari za kiuchunguzi vijijini na kuibua changamoto za wananchi.
Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni siku chache baada ya TGNP kukutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es alaam wiki iliyopita.

Warioba- Msituingilie, Msitushinikize

MWENYEKITI wa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba, Jaji Joseph Warioba amevitaka vikundi na wananchi waliopendekeza wajumbe wa Tume hiyo, kuiacha ifanye kazi iliyopewa kufanya.

Pamoja na hayo, Tume hiyo jana ilikabidhiwa rasmi jengo la ofisi ya kufanyia kazi, kuahidiwa magari 30, kuajiri watumishi wa sekretarieti watakaosaidia na kuanzishiwa fungu maalumu la kuiwezesha kufanya kazi.

Akizungumza wakati Tume hiyo inakabidhiwa ofisi Dar es Salaam, Jaji Warioba ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, alisema waliopendekeza majina ya wajumbe hao, wasitarajie kuwa wajumbe hao watafanya watakavyo wao kwani Tume hiyo ni ya Watanzania wote na si watu wachache.

“Naomba kwa dhati kabisa, waliotupendekeza watuache tufanye kazi, tumepewa jukumu la nchi tuacheni tufanye kazi bila shinikizo,” alisema Jaji Warioba.

Alisema iwapo waliopendekeza Tume hiyo wanadhani kuwa wameweka watu wao hivyo mambo yatafanyika kama wanavyotaka wao, watakuwa wanajidanganya kwa kuwa kazi ya Tume ni moja tu ya kutumikia wananchi.

Alisema majukumu ya Tume hiyo si kuandika Katiba bali kukusanya maoni, kuyachambua na kuandika rasimu ya Katiba ambayo itazaa Katiba mpya.

Alihamasisha wananchi kujiandaa na kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. Alisema Tume hiyo iliyoanza kazi juzi, inaandaa utaratibu utakaoiwezesha kufikia wananchi wengi ili kupata maoni mengi.

“Sisi Tume tunatarajia Watanzania watatwambia wanataka Tanzania iweje katika Katiba,” alisema. Aliziomba Serikali za Mitaa kuanzia vijiji, tarafa, kata, wilaya na mikoa, kujiandaa kwa kutengeneza mazingira mazuri kwa Tume hiyo kufikia wananchi wengi zaidi.

Awali akimkabidhi funguo za jengo hilo la ghorofa 10 kuwa ofisi ya Tume hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema pamoja na jengo hilo, pia kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Tume hiyo itapewa magari 30 ili kuiwezesha kiusafiri.

Usalama wao Alisema Serikali pia imeandaa ulinzi wa kutosha utakaotumia mitambo maalumu katika jengo hilo, ili kuwahakikishia wajumbe usalama wao, kuwawekea vifaa vya kisasa vya kukusanyia na kutunza kumbukumbu na kuwafungulia tovuti rasmi ya Tume.

Pia alisema Serikali imejiandaa kuongeza sekretarieti yenye utaalamu, ili kufanikisha kazi zake ambayo katika eneo la makazi, wajumbe wote ambao hawaishi Dar es Salaam, watapewa nyumba mpya zenye samani wakati wote watakaokuwa wanafanya kazi za Tume.

Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, aliitaka Tume kujipanga kutoa elimu kuhusu Katiba ya sasa, ili kuwapa welewa wananchi kuhusu Katiba hiyo ambapo pia Wizara yake itaendelea kutoa elimu hiyo.

Alisema Tume imepewa kazi nzito isiyohitaji ubaguzi wa aina yoyote ambayo inahitaji uaminifu, nguvu, maarifa na uvumilivu. “Najua mtalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu usiku na mchana, ila tambueni kuwa Serikali iko pamoja nanyi,” alisema Balozi Sefue.

Wajumbe Wajumbe 30 wa Tume hiyo pamoja na Jaji Warioba ni Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu mstaafu Augustine Ramadhani, Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Mngwali, Dk. Sengondo Mvungi, Jesca Mkuchu na Alhaji Said El-Maamry.

Wengine ni Profesa Palamagamba Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Kashonda, Al-Shaymaa Kwegry, Richard Lyimo, John Nkolo, Mwantumu Malale na Joseph Butiku.

Kutoka Zanzibar ni Dk. Salim Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohamed, Simai Mohamed Said na Muhammed Yussuf Mshamba.

Wengine ni Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar Mohamed Ali, Ally Abdullah Saleh na wajumbe wa Sekretarieti ni Assa Ahmad Rashid ambaye ni Katibu na msaidizi wake, Casmir Kyuki. Tume itafanya kazi kwa miezi 18.

Wednesday, May 2, 2012

SEMINA: Changamoto za Sheria Kandamizi Kwa Wanawake Katika Muktadha wa Katiba



SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

 UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII BAHATI SEMWANO; TAHURIFO, ATAWASILISHA:

MADA: Changamoto za Sheria Kandamizi  Kwa Wanawake Katika Muktadha wa Katiba   
Lini: Jumatano Tarehe 02 May, 2012

Muda: Saa 09:00 Mchana – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  
WOTE MNAKARIBISHWA