SPIKA wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, amesema yupo tayari kuhojiwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge, kama itamwita kutokana na hatua yake ya kumzuia Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kumuuliza swali Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni.
Katika hatua nyingine, Spika huyo mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania,
amesema hamuogopi Mbunge yeyote anapokuwa anaendesha vikao vya Bunge, zaidi ya
kuwa na hofu na Mungu.
Ameyasema hayo katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma, alipozungumza na baadhi
ya waandishi wa habari wanaoripoti habari za Bunge.
“Bado sijaitwa na Kamati ya Kanuni ya Bunge, nikiitwa ingawa mimi ndiye Mwenyekiti, nitajiweka pembeni na Naibu wangu, halafu wajumbe wa Kamati watachagua Mwenyekiti wa kuendesha kikao kitakachonihoji, ili mradi uamuzi huo ufanywe na zaidi ya asilimia 50 ya wajumbe wa Kamati,” alisema Spika Makinda.
Alisema, hadi sasa bado hajaarifiwa na Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila, kama
Chadema wamewasilisha barua ya kutaka ahojiwe kwa hatua yake hiyo, kama
walivyoeleza kwa vyombo vya habari.
“Kanuni ya 5 kifungu kidogo cha 4 cha kanuni za Bunge, kinasema Mbunge
asiporidhishwa na jambo lolote kutoka kwa Spika, anaweza kuandika barua ya
kupinga kwa Katibu wa Bunge, ili hatua zingine zichukuliwe ikiwa ni pamoja
na hii ya kutumia Kamati ya Kanuni ya Bunge ili kumhoji Spika.
“Lakini kuhusu hili la Chadema, sijaambiwa, nikiambiwa nitatii kanuni za Bunge
nitaiachia Kamati ifanye kazi yake na mimi na Naibu wangu ambao kimsingi ndiyo
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, tutakaa pembeni ili mjumbe mwingine aendeshe
kikao hicho.
“Baadaye uamuzi wa Kamati utaletwa kwangu Spika na nitautangaza mbele ya Bunge
kwa namna uamuzi utakavyochukuliwa na Kamati ya Kanuni,” alisema Makinda.
Akizungumzia mazingira anayokumbana nayo anapoendesha vikao hivyo, alisema:
“Unapokaa katika kiti kile unaongozwa na Mungu na si watu kama inavyodhaniwa,
kabla hujakaa ni lazima umwombe Mungu, vinginevyo unaweza kuharibikiwa, maana
Bunge si chombo cha mchezo.”
Alisema, ni kutokana na kuzingatia kanuni na haki, Bunge la Tanzania limeshinda
katika tathmini iliyofanywa kwa mabunge ya Jumuiya ya Madola, kwa kuendeshwa
kwa uwazi na kuzingatia haki kwa pande husika.
Hivi karibuni, Chadema walieleza msimamo wao wa kumshitaki Spika Makinda kwa
Kamati ya Kanuni ya Bunge, baada ya kumzuia Lissu kumwuliza swali Waziri Mkuu, kuhusiana na mauaji yanayofanywa na polisi katika mgodi wa dhahabu wa North Mara Barrick, Nyamongo wilayani Tarime, wakati kesi kuhusu suala hilo iko mahakamani.
No comments:
Post a Comment