WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema suala la posho za vikao hasa kwa wabunge limekuzwa kuliko ukubwa wa jambo lenyewe.
Pinda amebainisha kuwa, zipo baadhi ya posho ambazo haziwezi kutenguliwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ikiwamo posho hiyo ya Mbunge hadi sheria na Katiba vitakaporekebishwa.
Pia amewataka wabunge wawe wakweli kuhusu suala la kutaka kufutwa kwa posho zao za vikao, kwa kuwa pamoja na kupewa fedha hizo, bado hazitoshelezi mahitaji na majukumu mengi yanayomkabili Mbunge, jambo ambalo linawafanya wengine kuendelea kukopa.
Amelieleza Bunge mjini Dodoma kuwa, pamoja na kwamba jambo hilo linazungumzwa sana na kushikiliwa kidedea na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (Chadema), anafahamu kuwa wapo baadhi ya wabunge wa chama hicho ambao bado wanazimezea mate posho hizo za vikao.
Pinda alikuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF)
aliyetaka kujua Serikali ina tamko gani kuhusu posho za vikao, suala ambalo baadhi ya wabunge wamekuwa wakilijadili na kutoa matamko yao dhidi yake na kusababisha kujenga fitna na kadhia kwa wabunge wengine kutoka kwa wananchi wao.
“Katiba Ibara ya 73, inazungumzia masharti ya kazi ya wabunge, kwamba watashika madaraka yao na watalipwa mishahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa kanuni na kwamba kila mbunge ana wajibu wa kufuata sheria hiyo.
“Sasa hivi karibuni kumeibuka kadhia iliyoanzia kwa baadhi ya wabunge na vyombo vya habari na kusababisha fitna na wananchi wetu, naomba jibu mheshimiwa Waziri Mkuu,” alisema Mnyaa.
Waziri Mkuu, alikiri kuwa stahili za wabunge zipo kwa mujibu wa Katiba na Sheria nyingine zilizotungwa na Bunge.
Alianisha kuwa, zipo posho ambazo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha hana mamlaka ya kuzirekebisha, kwa kuwa zipo kwa mujibu wa Katiba na Sheria, hivyo ili zibadilike, Katiba na Sheria hizo hazina budi kubadilishwa pia.
Lakini pia alisema zipo posho ambazo Katibu Mkuu ana mamlaka ya kuzirekebisha kwa jinsi anavyoona inafaa. “Katika kundi la posho za kwanza ambazo hadi sheria zirekebishwe wapo pia madiwani ambao hawana malipo ya aina yoyote zaidi ya posho ambazo ndizo zinazowawezesha kutimiza majukumu yao, hivyo mnapozungumzia posho mtambue kuwa kuna madiwani,” alihadharisha.
Alitolea mfano pia posho wanazopewa polisi, za chakula, kuwa huo ni utaratibu uliopo ndani ya Jeshi la Polisi ambao hauwezi kubadilishwa, kwa kuwa upo kwa ajili ya kumwezesha askari atimize majukumu yake.
“Jamani tuangalie na posho zenyewe tunazozingumzia, mfano makatibu wakuu wakati wa maandalizi ya Bajeti wamekuwa wakikesha, mimi nikikesha hadi asubuhi sawa, lakini sheria hizi zimeona ni vizuri watu wa aina hii kuwapa motisha, si dhambi hata kidogo kuwapa posho.
“Najua kumekuwa na maneno mengi kama vile kuna jambo kubwa, nashangaa suala hili
lilivyokuzwa, lakini liko wazi kabisa ni masuala ya sheria, Katiba na utaratibu tu wa kufuatwa, kwani hata Spika wa Bunge akitaka kuongeza posho za vikao za wabunge hulazimika kwanza kumwandikia Rais kuomba kibali, huyu mbunge mnayempigia kelele posho hizo hata wakati mwingine hatumii mwenyewe,” alisema Pinda.
Alisema hakuna Mbunge asiyefahamu kadhia wanayoipata ya kushikwa mashati na
kuombwa fedha kila kukicha, hali inayowafanya fedha wanazopata kutowatosheleza na ndiyo maana posho hizo za vikao zinazolalamikiwa na kukuzwa, zimewekwa kwa ajili ya kuwasaidia wabunge hao kutimiza wajibu wao.
Aliongeza kuwa, tamko la Serikali ni kuziangalia fedha hizo namna zilivyowekwa ili angalau zihuishwe na hata ikibidi kuziweka kwenye mishahara ya watumishi wakiwamo wabunge.
Akijibu swali la nyongeza la Mnyaa aliyetaka kujua ni hatua zipi Serikali
inawachukulia wabunge ambao wamekiuka Katiba na Sheria zilizowekwa kwa kukataa
posho hizo za vikao, Pinda alisema hakuna sababu ya kuwachukulia hatua kwa kuwa Zitto si mbunge wa kwanza kutaka fedha zake za posho zitumike katika matumizi mengine na kwamba hakuna mbunge anayekatazwa kuiandikia Hazina kuwa fedha zake za posho ziingizwe katika mipango ya maendeleo.
“Hofu yangu ni kukuzwa sana kwa jambo hili na ninajua hata wabunge wa Chadema
wanazimezea mate fedha hizi za posho za vikao, ila hawana cha kufanya,” alisema
Pinda na kushangiliwa.
Juzi Bajeti Mbadala ya Kambi ya Upinzani iliyosomwa na Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na baadaye Waziri Kivuli Zitto, ilibainisha dhamira ya kufuta posho zote za vikao kwa watumishi wa umma wakiwamo wabunge, jambo lililozua mjadala.
No comments:
Post a Comment