Wednesday, June 15, 2011

Makinda- Bungeni si sokoni, tunatia aibu

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, amewatolea uvivu wabunge na kuwaeleza kuwa wanajidharaulisha na kukigeuza chombo hicho cha kutunga sheria kuwa kama eneo la sokoni Kariakoo, Dar es Salaam.

Amesema utaratibu wa baadhi ya wabunge kusimama wakati wa vikao vya Bunge na kupaza sauti ya ‘Mwongozo au Utaratibu’, haupendezi na wabunge wanapaswa kurudi kwenye mstari.

Spika Makinda alisema hayo jana bungeni wakati akizungumzia matukio yaliyotokea juzi jioni wakati wa mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambapo wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi, kulikuwa na kukatishana kuzungumza kwa wabunge kwa kutumia kauli za ‘Mwongozo na Utaratibu’.

Wakati huo, Bunge lilikuwa likiongozwa na mmoja wa wenyeviti wa Bunge, George Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe (CCM). “Kuhusu hili la ‘Utaratibu na Mwongozo’, kwa kweli sasa tunatia aibu. Waheshimiwa mnajidharau, yaani imekuwa kelele, huku Mwongozo, mara kuhusu Utaratibu, tumegeuka kama watu wa Kariakoo!

“Naomba sana, tunasikilizwa na wananchi, tusikilizane, watu wana hamu sana ya kutazama Bunge … mimi jana nilikuwa natazama kwenye televisheni, lakini sikuona hamu ya kutazama. Naomba sana, sana, tufuate utaratibu,” alisema Spika Makinda.

Alisema, kutokana na hali hiyo ya pengine wabunge kutofahamu vizuri kanuni, kutakuwa na semina kuhusu upitishaji wa vifungu wakati wa mijadala ya Bajeti ambayo inaanza leo kwa Bajeti ya Serikali.

Spika Makinda alifikia hatua ya kuwatolea uvivu wabunge hao, baada ya Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), kusimama na kutaka mwongozo wake juu ya jibu alilopewa wakati wa kipindi cha maswali.

Makinda alimsifu kiongozi huyo wa Upinzani Bungeni kwa kutafsiri vyema kanuni kwa kuomba mwongozo kwa wakati unaostahili.

“Alichofanya Mbowe ni sahihi kabisa … unasubiri suala linafika mwisho, yaani hadi kitendo kinakamilika, ndio unaomba mwongozo. Si katikati, unasimama na kudai mwongozo, mara mwingine huku kuhusu utaratibu uliovunjwa … hatueleweki wabunge,” alisema Makinda.

Baadaye akifafanua kauli yake kuhusu Kariakoo, Makinda aliomba radhi kwa wakazi na wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa hakumaanisha vibaya kutumia neno hilo, ila maana yake ilikuwa ni kwa vile eneo hilo kuna soko kuu, hivyo watu huzungumza bila mpangilio, tofauti na bungeni ambako kuna utaratibu.

“Kariakoo ni sokoni kila mtu anazungumza anavyotaka na hakuna wa kuwazuia, lakini hapa ndani kuna utaratibu si sokoni,” alisema Makinda.

Hii ni mara ya pili kwa Spika Makinda kuonya wabunge kwani hata mkutano uliopita, baadhi ya wabunge walisahau kanuni na kuanza kupiga kelele hadi mwingine akasema “mlango ufungwe tupigane”.

No comments: