Tuesday, June 14, 2011

RAI YA JENERALI: Hatari ya vurugu inatoka kwa watawala, Slaa asiwape kisingizio



KATIKA kipindi hiki tunapoikazania Serikali ya Rais Jakaya Kikwete isifanye mchezo na suala la Katiba, tunalo jukumu la kutuliza akili zetu na kupima kwa kina kila tunachokisema na kukiandika.

Nasema haya kwa sababu naona kama tunalo tatizo linalotokana na Serikali yetu kuonekana kama vile haina msimamo kuhusu suala hili kubwa na zito. Hakuna dalili za wazi zinazoonyesha kwamba Baraza la Mawaziri limeketi na kulijadili kwa undani na kupata msimamo wa pamoja, na wala hakuna dalili kwamba mkuu wa Serikali hiyo, Rais Kikwete amewapa watu wake maagizo kuhusu nini wafanya na nini waseme kuhusu mada hii ya Katiba.

Kinachojitokeza ni taswira ya kuparaganyika kwa mawazo na kutokuelewana miongoni mwa wale wanaotarajiwa kutuongoza. Kwa bahati mbaya, ingawaje sasa naamini watakuwa wamegundua kwamba walichokifikiria kuwa kitu rahisi, ni kigumu kweli kweli na wanatakiwa wajiandae kukishughulikia kwa umakini mkubwa kuliko huo walioudhihirisha hadi sasa.

Ningependa nirejee jambo ambalo nimekuwa nikilishadidia kwa muda mrefu kidogo: Suala la Katiba mpya limeshika kasi isiyokuwa ya kawaida, na wala haliwezi kuondoka kirahisi. Linahitaji kufanyiwa kazi itakayowaridhisha wananchi, na hiyo kazi haiwezekani ikafanyika ila kwa kuwahusisha wananchi kwa kiwango kikubwa kinachowezekana.

Ukweli ni kwamba, hata kama hatukuwa tumezowea hili, hivi sasa wananchi wanataka mabadiliko makubwa katika maisha yao, na wanataka kuanza na Katiba watakayoiandaa wenyewe.

Ni kwa nini wananchi wamefikia kiwango hiki cha utashi, mimi binafsi sina jibu la haraka, na kila mtu anaweza kuwa na maoni yake. Lakini naamini kwamba wananchi wengi wameanza kung’amua kwamba mambo hayaendi kama ambavyo yanatakiwa yaende.

Wanayaona maisha yao yakiwa hayana matarajio tena. wanaona hali zao za kiuchumi na kijamii zikizidi kuzorota. Wanaona maisha bora waliyoahidiwa kama ni mzaha wamechezewa. Wanawaona watawala wao kama waongo na wanafiki, wasiojali, wala rushwa na wauza nchi. Hawaamini lo lote linalosemwa na watawala kwani wamekwisha kudanganywa mara nyingi.

Sasa wamehamanika na wanataka mabadiliko, tena wanataka mabadiliko makubwa.

Nimekuwa nikifuatilia kwa kiasi fulani maandamano na mikutano ya viongozi wa CHADEMA katika mikoa ya Kusini, na nimekuwa nikiangalia maelfu ya watu wanaoshiriki katika maandamano hayo na mikutano hiyo. Ningekuwa mtawala ningeshitushwa na mikusanyiko ile kwa sababu ningetambua kwamba inabeba ujumbe mzito kwangu.

Ujumbe unaotoka katika maandamano yale na mikutano ile ni kwamba wananchi wamechoka. Ukiona kaumu ya watu kama tuliyoiona katika miji midogo na ya ‘pembezoni’ kama Sumbawanga wanaandamana na kukaa mkutanoni wakisikiliza kama watotot wa shule wanavyokaa darasani kumsikiliza mwalimu, unajua kwamba kuna kitu kimebadilika katika jamii ya Watanzania.

Lakini papo hapo ningependa kutoa angalizo. Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma, hii si mara ya kwanza tunashuhudia hamaniko la aina hii la kutaka mabadiliko. Nimeandika kwamba tuliwahi kuona, hapa nchini, hamasa walizozua wanasiasa kama Chistopher Mtikila na Augustine Mrema wakati ule. Watu wengi waliwachukulia hawa kama wakombozi wao. Baadaye bila shaka walikuja kugundua kwamba matumaini yao yalikuwa yamegonga mwamba.

Lakini shauku ikiisha kujengeka kwamba hali iliyopo haifai na ni lazima ibadilike, shauku hiyo haiishi kwa sababu manabii waliotarajiwa kufanya kazi ya ukombozi wamedondoka kando ya njia, bali shauku hiyo huhamishwa na jukumu la ukombozi likatafutiwa manabii wengine. Na kwetu ndivyo ilivyokuwa.

Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005 shauku hiyo ilikuwa imehamishiwa kwake. Bila shaka mwenyewe atakuwa anakumbuka kwamba ilifika mahali wakati wa kampeni ndani ya CCM ikasemwa kwamba hata kama CCM wasingemchagua yeye kuwa mgombea, angepata kuwa rais kwa kupitia chama kingine cho chote. Hayo yalisemwa na wana CCM na wanachama wa vyama vya upinzani pia.

Hili nalisisistiza kwa makusudi mazima: Hizi ni dalili za kuhamanika na kukata tamaa kwa Watanzania wengi. Na hali hii imekuwapo kwa muda mrefu toka utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi hadi ule wa Rais Benjamin Mkapa. Sasa inajirudia katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Wananchi wengi wanaona mkombozi wao mpya, nabii wao mpya, ni CHADEMA. Wanachosema katika lugha ya miili yao ambayo naiona kupitia televesheni na kupitia magazeti, ni kwamba wakipata fursa ya kupiga kura na uchaguzi ukawa “huru na wa haki” wanaweza (na uwezekano huo ni mkubwa) watapiga kura kuichagua CHADEMA.

Sasa, kama tunavyojua, uchaguzi mwingine ni mwaka 2015. Bado tunayo miaka minne hadi tupate fursa nyingine ya kupiga kura. Ni vyema kwa wale wanaotaka kufanya mabadiliko katika utawala wa nchi hii kwa njia mbali mbali wakautumia muda uliosalia kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi huo, na wale wanaotaka kuiondoa CCM madarakani wafanye kampeni ya nguvu ya kuwahamasisha wapiga kura kimawazo lakini pia na kuwahamasisha wajitokeza siku ya kupiga kura ili watimize azima yao.

Ndiyo maana nilijikuta nikiwa na wasiwasi (wiki chache zilizopita) nilipomsikia Katibu Mkuu wa CHADEMA, Willbrod Slaa akizungumza kama vile anao mpango wa kufanya mabadiliko anayotaka kuyafanya kabla ya uchaguzi ujao. Aliposema kwamba kuiondoa serikali ya Kikwete kabla ya 2015 hautakuwa uhaini anaweza kuwa anasema kweli, kwani uwezekano huo upo.

Kwa mfano Bunge linaweza, katika mazingira mahsusi yaliyoainishwa na Katiba, likamshitaki Rais kwa kosa la kuidhalilisha Ofisi yake, na kama akikutwa na hatia likamvua madaraka. Hiyo imeandikwa katika Katiba tuliyo nayo hivi sasa, na wala halina haja ya kusubiri Katiba mpya. Ndiyo maana nasema kwamba anachosema Slaa ni cha kweli kwa maana ya vifungu vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano kama ilivyo leo.

Kinachonitia hofu ni kwamba napata hisia kwamba Slaa hakujikita katika vifungu vya Katiba, angalau maelezo niliyoyasoma hayakusema hivyo, jambo ambalo linaweza kuzaa tafsiri kwamba njia mojawapo inayofikiriwa ni kuung’oa utawala wa Kikwete kwa maandamano, kama ilivyokuwa Medani Tahrir.

Kama hivyo ndivyo alivyokusudia kusema Slaa, kuna tatizo. Tatizo hilo, kwa mtazamo wangu, linakuwa kubwa zaidi kwa kuangalia matukio ya siku hizi chache zilizopita.

Tatizo lenyewe si kwamba haiwezekani kuung’oa utawala uliopo kupitia maandamano na bado kitendo cha kuung’oa kikawa si uhaini. Nchi nyingi zimeshuhudia hilo likifanyika, ikiwa ni pamoja na Indonesia, Philippines, Georgia na sasa Tunisia na Misri. Kilichotokea katika nchi hizo ni mapinduzi ya umma uliosimama na kusema “Utawala huu sasa basi!” Ni mantiki ya mapinduzi kama hayo kwamba yanapofanikiwa walioyaongoza wanakwenda moja kwa moja Ikulu, lakini wakishindwa wanatiwa kitanzi.

Ni kwa jinsi hii akina Fidel Castro (Cuba) na Nelson Mandela (Afrika Kusini) walikwenda jela lakini hatimaye waliingia madarakani, lakini Pierre Mulele (Kongo) na Mahjoub (Sudan) walitiwa kitanzi.

Naamini kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA alitaka kupeleka ujumbe mzito kwa wakuu wa nchi, lakini kila siku ujumbe unaohusu mambo kama haya hauna budi uandaliwe kwa uangalifu na weledi mkubwa ili usije ukazaa tafsiri zaidi ya moja.

Ingekuwa vyema kama Slaa angeonyesha subira katika matamko yake. Hivi sasa watu wengi wanamwangalia kama “rais mtarajiwa.” Angechukua muda kujiandaa kwa umakini mkubwa, hasa wa kuyasoma matatizo ya nchi yetu na kufikiria njia mbali mbali za kuyakabili kuanzia na hili la Katiba ambalo sasa naamini kwamba iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka 2015 ( na nasema hili linawezekana kabisa), atalikuta bado lipo kwa sababu sioni dhamira ya kweli ya kulishughulikia.

Akijipa muda wa kujifunza zaidi na kukusanya maoni, na kujenga mitandao ya utafiti itakayowahusisha wataalamu wa kumshauri na kukishauri chama chake, akichukua muda kujadili matatizo ya nchi hii na makundi mbali mbali ya kijamii katika shughuli zao mbali mbali na wakamweleza matatizo yao; naye akajadiliana nao... atakuja kugundua kwamba hakuna muda wa kutosha kwa ajili ya maandalizi hayo.

Najua mara nyingi umefanyika uchokozi dhidi ya vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani. Uchokozi huo unafanywa makusudi ili kipatikane kisingizio na wapinzani waweze kushutumiwa kwamba ndio waliodhamiria kuvunja “amani na utulivu” na misemo mingine ya kuchekesha ukiangalia “amani na utulivu” vinavyotawala shughuli za chama-tawala.

Kwangu ni dhahiri kwamba kama kuna ghasia kubwa zitakazotokea nchini humu, zitaanzia katika vurugu zinazoendelea ndani ya chama hicho tawala. Hata hivyo, Slaa angejiweka mbali na kila kinachoweza kumfanya yeye ama chama chake waonekane, hata kama si kweli, kwamba wao ndio wanaochochea vurugu.

Naandika haya nikijua kwamba sasa kuna hamaniko ndani ya duru za watawala, kwa sababu wanajua wamepoteza nguvu za ushawishi na wanachokiona kwamba kinaweza kuwasaidia ni ushawishi wa nguvu, kama ambavyo wanaonekana kutumia mitulinga isiyokuwa na sababu yo yote alimradi tu waonyeshe kwamba wanazo nguvu, kama vile hatujui kwamba wanazo.

Katika kutapatapa wamewaingiza na wakuu fulani wa dini ambao nao sasa wanatoa ‘onyo’ kwa CHADEMA kama vile wamegeuka kuwa idara ya usalama ya serikali au wasemaji wa Jeshi la Polisi.

Hali hii inatisha, lakini si mpya. Imetokea kila mahali utawala ulipozeeka, ukapoteza njia, ukasahau hata asili yake, ukapuyanga na kubahatisha, ukababaisha na kubangaiza, ukayumba na kutetereka, ukatekwa na waporaji, ukaendelea kujitutumua kwa kuonyesha ukali wa kijeshi kumbe ndani ya roho yake kiini chake kilikwisha kugugunwa na mapanya-buku kwa muda mrefu. Utawala kama huo unao uwezo mkubwa wa kusababisha maafa kutokana na udhaifu wake.

Slaa akae chonjo, apunguze hisia, awe m-rais (presidential). Ajifunze zaidi, kwani kama bado ana nia ya kuwania urais mwaka 2015, kazi iliyo mbele yake ni kubwa. Akumbuke tu kwamba, Rais Jakaya Kikwete alikuwa na (angalau) miaka kumi ya kujiandaa kuwa rais, na hii kumi ni ile tunayoijua sisi.

Hata baada ya muda huo wa miaka kumi kupita, na hata baada ya miaka mitano ya kuendesha Serikali, inaelekea bado hajajifunza mambo mengi ya msingi kabisa yanayohusu uongozi na utawala. Slaa afanye hadhari, asije akawa vivyo hivyo.

No comments: