Friday, June 24, 2011

Zitto matatani

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), amedai kuwa Baraza la Mawaziri limerubuniwa na watu wenye maslahi ya kuliua Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), hivyo kubadili mapendekezo ya Bunge ya kulipa muda wa kutosha shirika hilo kukamilisha kazi zake.

Kwa kauli hiyo, Zitto ameingia matatani baada ya mawaziri kumtaka athibitishe ukweli wake na Spika wa Bunge, Anne Makinda amempa siku saba awasilishe ushahidi kwamba Baraza la Mawaziri lilishawishiwa kubadili uamuzi huo na watu ambao hakuwataja.

Akiwa mchangiaji wa kwanza wa Azimio hilo lililowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma, alisema Azimio hilo limegeuzwa kutoka vile lilivyokuwa awali baada ya mawaziri kushawishiwa.

Hoja ya msingi ya Mkulo ilikuwa ni kuliomba Bunge kupitisha Azimio hilo ili CHC iongezewa kipindi cha mpito cha miaka mitatu limalize majukumu yake na baadaye majukumu hayo yahamishiwe Ofisi ya Msajili wa Hazina, lakini hoja hiyo ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM na upinzani na hatimaye ikafanyiwa marekebisho.

“Mheshimiwa Spika, ndani ya Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma na hata katika Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, tulikubaliana kwamba CHC wapewe muda wa kutosha kukamilisha kazi na majukumu yao halafu baada ya hapo Waziri ndio alete Azimio hapa na si kuwapa kipindi cha mpito cha miaka mitatu kama Azimio lilivyowasilishwa leo.

“Nawaombeni wabunge wenzangu wote, tukatae maamuzi haya ya Baraza la Mawaziri kwa kuwa yametokana na kurubuniwa na watu wenye lengo la kuua CHC kwa ajili ya maslahi yao. Ikumbukwe kuwa chombo hiki kinaangalia mali za umma na mashirika, hivyo kutaka kukiua na kupeleka majukumu haya kwa Msajili wa Hazina ambaye uwezo wake wa kulinda mali za umma ni mdogo sana ni kutaka kuiba mali za Watanzania,” alisema Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni.

Alisema azimio la Serikali la kuipa CHC kukamilisha majukumu yake limelenga katika kuwasaidia wafanyabiashara walioiba mali za umma, ikiwemo kukopa mabilioni ya fedha kutoka iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambao kesi zao zipo mahakamani, kupata ahueni kwa vile hatua hiyo itapoteza ushahidi.

Baada ya kueleza hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika, aliomba Mwongozo kwa Spika akitaka Zitto athibitishe kauli yake kwamba mawaziri wamerubuniwa kwa vile imewadhalilisha mawaziri hao ambao wanafanya kazi kwa maadili na kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Mkuchika alisema kitendo cha kusema maamuzi hayo yanatokana na kurubuniwa kwa mawaziri yanaleta picha mbaya kwa Watanzania ambao wamewaamini.

Baada ya maelezo hayo ya Mkuchika, Spika alimtaka Zitto kuwa makini na kauli anazozitoa anapochangia, ikiwemo ile ya kudai mawaziri wanashawishiwa na kurubuniwa, lakini Zitto aliposimama tena ili kuendelea kuchangia, alitamka tena kuwa anao ushahidi kwamba mawaziri walikuwa wameshawishiwa na kurubuniwa hadi wakatengeneza Azimio hilo jipya.

“Mheshimiwa Spika, siwezi nikatafuna maneno hapa, nina uhakika na ninachokisema, maamuzi ya Baraza la Mawaziri ni matokeo ya ma-lobbyist na kama Serikali mnabisha, leteni hapa mapendekezo ya awali ambayo yaliwasilishwa katika Kamati ya Makatibu Wakuu na Baraza la Mawaziri ili tuone yalikuwa yanasemaje,” alisema Zitto katika mchango wake.

Kutokana na msimamo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alimuomba Spika Makinda kumtaka Zitto kuwasilisha bungeni ushahidi kutokana na kauli yake hiyo, hatua iliyomfanya Spika kumpa Mbunge huyo kumpa muda wa kuandaa ushahidi huo na kuuwasilisha bungeni Juni 29, mwaka huu.

Hata hivyo, mjadala kuhusu Azimio hilo, ulionekana kuwa mwiba mkali kwa Serikali kutokana na wabunge ambao mara nyingi wamekuwa wakigawanyika kivyama, kuungana na kuwa kitu kimoja wakiipinga vikali serikali kwa mpango wake huo na kuitaka ichane nao mara moja.

Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Lugola (CCM), alisema kitendo cha kuweka muda huo ni kutoa mwanya wa maandalizi ya wizi wa mali za mashirika ya umma ambayo yamekuwa yakitumiwa na wachache kujitajirisha.

“Mheshimiwa Spika mimi ni Mbunge wa CCM, lakini katika hili napingana kabisa kwa kuwa nilipata fursa ya kuchungulia na kuwahoji walioko kwenye mashirika ndio maana nina uchungu kwa kuwa fedha zinaliwa bila sababu ya msingi...hicho kipengele cha majukumu ya CHC kuwa chini ya Msajili wa Hazina ambaye hata ukimuuliza ana mashirika mangapi hajui, wala hajui hisa za serikali zipo wapi na wapi, itakuwa ni kuwafikisha Watanzania mahala pabaya,” alisema.

Alisema kuwa imefikia mahali ambapo maamuzi yanatolewa na Bunge yanapuuzwa na Serikali na kufanya hivyo si kuwatendea haki Watanzania, akaitaka serikali kubadilika na kukubali kutoa muda wa kutosha kwa shirika hilo na lijengewe uwezo.

Pamoja na Lugola, Mbunge wa Kalenga, Dk. William Mgimwa (CCM) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), walikomelea msumari wa mwisho katika kupinga hoja hiyo, hatua iliyotosha kuifanya Serikali kupitia kwa Waziri Mkulo, kukubali kulifanyia marekebisho Azimio hilo kwa kuondoa baadhi ya maneno na wabunge kwa kauli moja walilipitisha.

Maneno yaliyoondolewa ni yale yaliyokuwa yakisema kuwa Bunge liipatie CHC ambayo muda wake wa utendaji utakwisha Juni 30, 2011, muda mwingine wa kipindi cha mpito cha miaka mitatu hadi Juni 30, 2014, ili baada ya muda huo kazi za CHC zihamie Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kutokana na mabadiliko yaliyofanywa, CHC imepewa kipindi hicho cha miaka mitatu, lakini bila kuwepo kipengele kinachosema baada ya muda huo, kazi zake zitahamishiwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, badala yake baada ya muda huo, Serikali itawasilisha tena Bungeni Azimio kuhusiana na kipi kifanyike kama kuiongezea tena muda CHC au vinginevyo.

Shughuli zinazofanywa na CHC ambazo mpaka sasa hazijakamilika ni pamoja na urekebishaji wa TRL baada ya kampuni ya Rites kuondoka, kushughulikia uuzaji wa hisa za Serikali katika NBC (T) Limited, uperembaji na uhakiki wa vitendo na mashirika yaliyobinafsishwa, urekebishaji wa mashirika 34 yaliyobaki na kukamilisha ufilisi wa mashirika ya umma 24 yaliyobaki.

Nyingine ni ukusanyaji wa madeni ya iliyokuwa NBC yenye thamani ya Sh bilioni 15.8 na urekebishaji wa Kampuni ya TTCL baada ya hatua ya awali ya ubinafsishaji kushindikana na mwekezaji wa Airtel kuonesha nia ya kutoka katika ubia.

No comments: