Thursday, June 9, 2011

TGNP ‘yararua’ mwongozo wa bajeti 2011/2012

WIKI hii Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, atasoma Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2011/2012 katika mkutano wa Bunge, utakaofanyika mkoani Dodoma.

Anafanya hivyo baada ya kutolewa kwa mwongozo wa bajeti hiyo. Wachambuzi wa mambo ya uchumi na siasa, tayari wameanza kuzungumza au kuandika na kuchambua maeneo mbalimbali kulingana na umuhimu wake.

Wanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia kikundi kazi chake cha uchambuzi wa bajeti, wakishirikiana na wanaharakati wengine, wana mawazo kwamba bajeti hiyo inatakiwa kulenga kujenga uchumi, ambao utajenga maisha ya watu wake kwanza; na si kuangalia maslahi ya wawekezaji wa ndani na nje.

Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya katika uchambuzi wake wenye mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, aliongozwa na kauli mbiu ya ‘Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake walioko Pembezoni’.

Amechambua upungufu uliomo katika mwongozo huo huku akishauri kuwa wananchi wapewe kipaumbele.

“Mwongozo wa bajeti ni lazima ulenge namna uchumi wa nchi, utakavyojenga maisha ya watu wake kwanza; na si kuangalia tu wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Suala la ajira na maisha endelevu kwa wote, liwekewe kipaumbele,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kwamba masharti yawekwe kwa wawekezaji ili kila mmoja, awe wa ndani au nje, aongeze idadi ya wafanyakazi kwa asilimia kadhaa kufuatana na sekta husika.

Uchambuzi huo, ambao unaeleza kwamba umefanyika baada ya uchaguzi mkuu wa 2010; na baadaye kushuhudia harakati za kudai katiba mpya, unasema jamii ina matarajio makubwa, kuona msimamo wa serikali katika kutetea haki na usawa wa kila mwananchi.

Jamii inatarajia kuona serikali ikielekeza rasilimali za kutosha ili kufanikisha mchakato wa kuandikwa katiba mpya, ambao ndio mhimili kwa wapiga kura wengi, hasa wanawake walioko pembezoni, ikiwa ni pamoja na makundi mengine ya watu wanaoishi na ulemavu au magonjwa ya aina zote, wakiwemo wenye VVU na Ukimwi.

“Tumeshangaa kuona kuwa hakuna mikakati mahususi ya kuelekeza rasilimali katika eneo la katiba,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, vipaumbele vilivyoainishwa katika mwongozo wa bajeti ya 2011/12 hadi 1015/16 ambavyo ni kilimo, miundombinu, viwanda, uwekezaji katika rasilimali watu, mazingira endelevu, usimamizi wa ardhi, mipango miji na makazi, kuimarisha mahusiano kati ya sekta ya umma na binafsi na kuendeleza mafanikio katika sekta za kijamii.

Taarifa hiyo inahoji iwapo vipaumbele hivyo, vinatokana na mpango wa uibuaji wa fursa na vikwazo kwa ajili ya maendeleo.

Baadhi ya maswali yaliyomo katika uchambuzi huo ni “Je vipaumbele hivi vimetokana na mpango wa uibuaji wa fursa na vikwazo kwa maendeleo (O&OD) ambao unatoa nafasi kwa walio wengi kuibua vipaumbele vyao wenyewe? Nani ananufaika zaidi, wawekezaji wakubwa au wawekezaji wadogo? Kwa upande wa kuwekeza katika rasilimali watu, ni kwa vipi kila sekta itaongeza ajira kwa watu na ni ajira za namna gani?”.

Kwa takwimu za TGNP, mwongozo wa bajeti uliopangwa na serikali kwa mwaka 2011/2012, unatarajiwa kuwa Sh 11,970,356 ukilinganisha na Sh 11,609,557 mwaka 2010/2011, ambapo bajeti inazidi kuwa kubwa wakati huo huo mapato ya ndani yanazidi kushuka.

Wanaeleza kuwa jambo la kushangaza ni kuona kwamba bado bajeti ya serikali inazidi kuwa tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wafadhili na deni la taifa linazidi kukua kutoka Sh trilioni 7.6 mwaka 2008/2009 hadi Sh trilioni 10.5 kwa mwaka 2009/2010.

Kutokana na hilo, uchambuzi huo uliosainiwa na Usu Mallya, unahoji “je, ni kwa vipi serikali inapanga kuongeza ukubwa wa bajeti wakati deni linazidi kukua na mikopo na misaada ya wafadhili haitabiriki?

Tunadai serikali ipunguze utegemezi wa bajeti kutoka kwa wafadhili kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kupunguza ukubwa wa serikali, yaani wizara, mawaziri na naibu mawaziri kufikia kiasi ambacho hakitaathiri sana ukubwa wa bajeti”.

Kwa mujibu wa uchambuzi huo, mwongozo wa bajeti unasisitiza uimarishaji na uendelezaji wa masuala ya uchumi mpana na siasa, kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuzuia mfumuko wa bei, kuendeleza sekta binafsi, kusimamia usawa katika bei ya mafuta kwa kuwekeza kupitia rasilimali watu.

“Sisi kama wanaharakati tulitarajia kuona muongozo huu wa bajeti unaweka kipaumbele katika kusimamia mgawanyo sawa wa rasilimali katika jamii, kurasimisha kazi zisizo na kipato zinazofanywa na wanawake na wanaume walioko pembezoni,” walisema wanaharakati kupitia uchambuzi huo.

Wanaeleza kuwa pamoja na masuala mengine, suala la ‘mabadiliko ya dhana’ ’ na kuipa ‘fursa’ kipaumbele zaidi kuliko ‘mahitaji ya watu’, inawapa wasiwasi sana kwani wanaona ni bora kuwe na mdahalo mpana wa kitaifa juu ya mawazo haya, maana inaweza kuleta matokeo hasi kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.

Vilevile, wanapinga suala la kuweka kipaumbele katika uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa wawekezaji wakubwa wakati soko la ndani la bidhaa linakufa. Kuhusu kilimo, walisema pamoja na juhudi zote za serikali kuendeleza kilimo na kuwa na mkakati wa mapinduzi ya kijani au “Kilimo Kwanza”, ukuaji wa kilimo unatarajiwa kukua na kufikia wastani wa asilimia 5.5 tu.

Kwa mujibu wa TGNP, ukuaji huo hauendani na umuhimu wa kilimo kwa watanzania wengi. Hali kadhalika pamoja na kilimo kuwekewa kipaumbele, mchango wa kilimo katika pato la taifa unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 21.9 (2010) hadi 18.7 (2011) na hii itakuwa na athari kubwa kwa wakulima wadogo, ambapo wengi wao wanategemea sana kilimo hasa jamii kubwa, ikiwa ni wanawake. Kuhusu umeme, walisema hakuna mkakati wa wazi au chanzo mbadala cha nishati, kama vile gesi, upepo au makaa ya mawe kwa ajili ya kutatua changamoto iliyopo ya umeme.

“ Miaka 50 baada ya Uhuru tunadai kwamba kila Mtanzania ana haki ya umeme akiwa kijijini au mjini. Pia tulitarajia kuona bajeti ya serikali inaliimarisha Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kulijengea uwezo ili kuondokana na tatizo la ukodishaji mitambo ya uzalishaji umeme toka nje ya nchi. Mara kwa mara mitambo hiyo imekuwa ikiligharimu taifa kutokana na kuwepo kwa udanganyifu katika ununuzi na ukodishwaji wake. Tunadai uwajibikaji kuanzia kwa Waziri hadi maafisa wengine wanaohusika na suala la nishati ya umeme hapa nchini,”walisema.

Katika sekta ya elimu, hatua ya serikali kuendelea kuweka bajeti ya wastani wa Sh 1,500 kwa kila mwanafunzi kwa siku kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, haiendani na hali halisi ya mahitaji ya lishe na kupanda kwa maisha.

Asilimia 40 ya ruzuku maalum kwa wanafunzi, hutolewa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu, lakini hali halisi iliyopo inaonyesha kwamba shule nyingi za msingi kufikia mwezi Disemba 2010, zilikuwa zimepokea kiasi kisichozidi jumla ya Sh 60, 000 hadi 300,000 tu kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada na ziada kwa mwaka 2009/2010.

Hali hiyo ndiyo iliosababisha shule nyingi kukosa vitabu na kila mtoto kuambiwa ajinunulie vitabu. Katika Sekta ya Afya, mwongozo haukueleza ni jinsi gani serikali itakabiliana na changamoto za uzazi salama.

Uchambuzi unasema walitarajia kuona mwongozo unaelekeza kutengwa kwa bajeti ya Afya inayoanzia asilimia 15, kama ilivoelekezwa katika azimio la Abuja pamoja na mikakati mahususi ya kuhakikisha sekta ya afya linaboreshwa.

Kutokana na yaliyojitokeza katika mwongozo wa bajeti, wanaharakati hao wanataka mikakati ya kuimarisha soko la bidhaa za ndani, kwa kuimarisha barabara za vijijini zitakazosaidia kuchukua mazao ya wakulima wadogo, ambao wengi wao ni wanawake.

Katika utekelezaji wa malengo ya MKUKUTA II, lazima mwongozo uzingatie masuala ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi, hasa wanawake walioko pembezoni; na si kuangalia masuala ambayo yatawafanya wananchi kuwa watumwa katika nchi yao.

Chanzo: Habari Leo 6.6.2011

No comments: