Tuesday, March 22, 2011

Kikwete aizika kasi ya Magufuli

RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Ujenzi, kutotumia ubabe katika ubomoaji wa nyumba za wananchi kwenye hifadhi ya barabara, iweke mbele maslahi ya wananchi hao.

Ameagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, iandae taarifa na kutangaza maeneo yote ya wazi nchi nzima, ili iwaondoe kirahisi waliovamia maeneo hayo.

Ametoa maagizo hayo jana alipofanya ziara katika Wizara hizo kwa nyakati tofauti, na kusisitiza kuwa ubabe na haraka viepukwe katika ubomoaji nyumba za wananchi zilizopo katika hifadhi ya barabara.

“Undeni tume ya kuchunguza kwanza historia ya barabara ndipo mtoe amri ya kubomoa nyumba za wananchi na suala la fidia lazima lizingatiwe,” alisema Rais Kikwete.

Alisema, barabara nyingi zinazojengwa, kihistoria zilikuwa za asili na wananchi wengi walijenga kabla ya kupandishwa hadhi, hivyo si haki kuwabomolea bila kuwalipa fidia au kuwapa muda wa kubomoa wenyewe.

“Jamani hawa ni wananchi ambao wengi ni wanyonge, chochote mtakachowafanyia wao hawana pa kukimbilia, lakini ninyi mna uwezo wa kutotumia ubabe katika suala hili, ingawa mnafuata sheria,” alisema Rais Kikwete.

Aliiasa Wizara ya Ujenzi kutotafuta unafuu kwa kuwatupia mzigo wanyonge na badala yake izingatie zaidi haki za wananchi.

“Huwezi kumpa mtu saa 48 abomoe nyumba yake hata kama yuko kwenye hifadhi ya barabara, naomba katika ile miradi ambayo inachukua muda kuanza, basi wapeni muda angalau hata wa miaka miwili.”

Alisema, wananchi wengi wamejenga katika maeneo hayo miaka mingi iliyopita, wamezaa na watoto wao wamezaa na kuwa na vitukuu, hivyo si haki leo kuwaondoa bila fidia au kuwapa muda mfupi wa kuondoka wakati barabara husika imewafuata.

Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuangalia maeneo ya kuwabomolea wananchi nyumba zao na kupitisha barabara, kwani si maeneo yote yanayopaswa wananchi kuondolewa ili kupisha barabara, akitolea mfano wa maeneo ya milimani kuwa ardhi yake ni ndogo na hata wananchi wakiondolewa barabara husika huenda isiwe na maana.

Kauli ya Rais inaonekana kuiunga mkono ile ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyoitoa siku za karibuni akizuia kasi ya bomoabomoa iliyokuwa inatekelezwa na Waziri Magufuli kwa mujibu wa sheria.

Uamuzi wa Pinda ulizusha malalamiko miongoni mwa wananchi hata kufikia hatua ya kuvumisha kuwa Waziri Magufuli amejiuzulu wadhifa wake kutokana na kitendo hicho, lakini Wizara yake ikakanusha siku moja baada ya uvumi huo kuripotiwa magazetini.

Rais Kikwete jana pia alihimiza wizara hiyo na Mfuko wa Fedha za Barabara kuwa mstari wa mbele kukagua ujenzi wa barabara pale unapokamilika na si kutegemea zaidi taarifa za vitabu ambazo mara nyingi huandikwa vizuri kuliko uhalisia.

Alikiri kuwa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hukagua matumizi ya fedha za miradi, lakini kwa kupitia vitabu na kwamba hali halisi ya barabara husika huwa haiangaliwi, jambo linalosababishwa kuwapo kwa barabara nyingi zisizo na kiwango kinachotakiwa cha kudumu kwa muda wa miaka 15.

“Sitaki tujenge barabara ambazo baada ya miaka mitatu zinabanduka, watu watasema tunaiba, tafuteni wakandarasi na wasimamizi wazuri, msiwe walegevu wala kujivua hili.

“Kagueni barabara, ndiyo maana wakati mwingine msingi unachimbwa, nyumba inajengwa na watu wanahamia kwenye hifadhi ya barabara na ninyi mnapita tu bila taarifa,” alisema.

Alitolea mfano barabara ya Kilwa kuwa imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kuhusu ubora wake, jambo ambalo ni aibu kwa kuwa barabara hiyo iko ndani ya Jiji la Dar es Salaam, ambako wizara na wahandisi wote wapo.

Kuhusu msongamano, alisema, mradi wa mabasi yaendayo kasi utamaliza hali hiyo kwa muda na suluhisho pekee ni kubuni usafiri wa kisasa unaoendana na uwezo wa nchi, akitolea mfano wa matumizi ya reli kwa wakazi wa Kimara, Ubungo hadi katikati ya Jiji - Stesheni.

Kuhusu suala la ardhi, aliitaka Wizara ya Ardhi, kuondoa taswira mbaya ya kukosa uaminifu na kupenda rushwa waliyonayo baadhi ya maofisa wa ardhi kwa wananchi ambapo pia aliwasisitizia maofisa hao kujali zaidi taaluma yao badala ya kujineemesha.

“Haya mambo yanasikitisha, watu wanaweka mbele maslahi yao na kusahau kabisa taaluma yao, sisemi hili kwa kuambiwa, mimi mwenyewe nina mifano halisi iliyonitokea, hata migogoro mingi ya ardhi ukifuatilia chanzo ni hawa maofisa ardhi … wakati mwingine nalazimika hata kuweka saini yangu hadi nihakikishe ukweli wa hati husika,” alisema Rais Kikwete.

Alitoa changamoto kwa wizara hiyo kupitia miradi yake ya kuendeleza miji ya Kigamboni na Kawe, kutowaweka pembeni wenyeji wa maeneo hayo miradi itakapokamilika na badala yake kuwapa kipaumbele kwa kuwarejesha ili kuwalipa fadhila.

Pia alitoa changamoto kwa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), kujenga nyumba ambazo wananchi watamudu gharama kwa kuwa lengo la kuanzishwa kwa shirika hilo ni kusaidia wananchi wenye kipato cha chini na si matajiri.

Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Rais, alitaja miradi ya barabara ambayo ipo katika hatua ya utekelezaji ukiwamo wa magari yaendayo kasi na kwamba kwa sasa kinachokwamisha ni ubomoaji wa nyumba za wananchi walio ndani ya eneo la mradi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema wizara yake ina mpango wa kutumia ramani ya zamani katika kutambua maeneo ya wazi nchini na kuonya hata walioko kwenye maeneo hayo wakiwa na hati halali hazitawasaidia.

Monday, March 21, 2011

UVCCM yajivua gamba

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetangaza kuunda kamati maalumu ili kufanya mageuzi ndani ya umoja huo na kumuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete kwa kujivua gamba na kubadili mtazamo na kukidhi matarajio ya
wengi.

Aidha, umesema utahakikisha viongozi wa chama hicho wanaotoa matamko bila kufuata utaratibu, hawapati nafasi yoyote ya uongozi na chama kisiwateue kugombea nafasi yoyote katika uchaguzi ujao.

Wamekitaka chama hicho kuwaelekeza viongozi wake umuhimu wa kuzingatia maadili na nidhamu kwa kutumia vikao kuwasilisha hoja zao na si kutumia matamko kukidhoofisha na kujijengea umaarufu binafsi.


Aidha, wameitaka CCM kufanya semina elekezi kwa mawaziri na wakuu wa mikoa na wilaya baada ya kuteuliwa ili watambue dhamana na uhusiano wao na chama hicho na malengo na matarajio ya chama kutoka kwa wananchi.

Akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Taifa mjini Dodoma, Kaimu Mwenyekiti wa Umoja huo, Beno Malisa, mbali na kuunga mkono dhamira ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ya kutaka CCM ijivue gamba, vijana hao walisema hata UVCCM inapaswa kujivua gamba.

Katika maazimio hayo, likiwemo la kumpongeza Rais Kikwete kwa kudhamiria kufanya mageuzi katika chama hicho kwa lengo la kukihuisha na kukirudishia mvuto kwa wanachama na wananchi hususani vijana, UVCCM wameona na umoja huo unahitaji kubadilika na kukidhi mahitaji hasa.

Malisa alifafanua kuwa kikao hicho kilichokutana Dodoma, kimeona kuwa umoja huo unahitaji kubadilika katika eneo la uanachama, uongozi, muundo, itikadi, uimarishaji wa uchumi, maadili na utendaji.

Ili kutekeleza dhamira hiyo ya kujivua gamba kama walivyosema, umoja huo umeunda kamati maalumu itakayofanya uchambuzi yakinifu wa namna ya kufanya mageuzi hayo chini ya uenyekiti wa kada wa umoja huo, Mohamed Bashe.

Baada ya kumaliza uchambuzi huo, kamati hiyo yenye wajumbe wengine sita, itawasilisha maoni na mapendekezo hayo katika vikao vya maamuzi, Baraza Kuu la UVCCM.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Riziki Pembe ambaye ni Mjumbe kutoka UVCCM Zanzibar, Fadhili Njagilo Mwenyekiti Vijana Iringa, Rojas Shemwele Mjumbe wa UVCCM Tanga, Daud Ismail kutoka UVCCM Zanzibar, Ashura Shengondo kutoka UVCCM Bara na Anthon Mavunde kutoka UVCCM Bara.

Mbali na kujivua gamba, Baraza hilo pia limelaani maandamano ya Chadema na walichoita kitendo cha viongozi wachovu wa Chadema kuendeleza chuki dhidi ya Serikali halali ya CCM.

Katika maazimio hayo, Baraza hilo limedai kubaini hila na njama zinapangwa dhidi ya Serikali na kuwataka vijana wote wa CCM na Watanzania kwa ujumla kukiogopa chama hicho cha Chadema.

Aidha, limewataka wanachama wote wa UVCCM kuwa tayari kukabiliana na njama hizo. Kuhusu tathimini ya uchaguzi uliopita, Baraza hilo limempongeza Rais Kikwete na Rais wa
Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kushika nafasi hizo, lakini limekishauri chama hicho kutazama upya mfumo wa kura za maoni wa kupata wagombea.

Mbali na mfumo huo, Baraza hilo pia limetaka chama hicho kitazame upya mfumo wa utoaji kadi za wanachama wakati wa uchaguzi wa wagombea na kuepuka makosa yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Kutokana na ushindi huo wa 2010, baraza hilo limeandaa mkakati wa kwenda kuwashukuru wananchi na vijana kwa kukipigia kura na limeagiza viongozi wote wa UVCCM kuhakikisha wanafanya mikutano na ikibidi maandamano ya kuwashukuru Watanzania kwa kukichagua CCM.

Baraza hilo pia lilijadili changamoto zinazojitokeza serikalini na zinazojitokeza kwa vijana na kutoa baadhi ya maagizo ya kufanyiwa kazi na Serikali.

Katika maagizo hayo, lipo la kutaka Serikali kuchunguza sababu za kupungua kwa ari ya baadhi ya watendaji wa Serikali katika kutimiza wajibu wao.

Hali waliyosema imeendelea kuwakatisha tamaa wananchi na hata wanaCCM na hivyo kujenga chuki dhidi ya Serikali halali ya CCM.

Friday, March 18, 2011

Mkulo ataja vipaumbele 12 vya bajeti ijayo

WIZARA ya Fedha imetaja vipaumbele 12 katika Bajeti ijayo ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha inayokadiriwa kufikia Sh. trilioni 11.9.

Wabunge wameitaka Serikali ivipungeze hadi vitano ili vitekelezwe kwa ufanisi kulingana na hali ya uchumi wa Taifa.

Vipaumbele hivyo kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ni elimu, kilimo, nishati, miundombinu, viwanda, afya, maji, ardhi, raslimaliwatu, sayansi na teknolojia, huduma za fedha na masuala mtambuka.

Akizungumza Dar es Salaam jana na wabunge, Waziri Mkulo alisema makadirio ya awali ya mapato katika mwaka ujao wa fedha ni Sh. trilioni 12 ikilinganishwa na matarajio ya Sh. bilioni 11.1 mwaka huu wa fedha na zinatokana na mapato ya ndani, mapato ya Serikali za mitaa, mikopo na misaada ya wahisani.

Wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo ya Mkulo, walisema hali ya uchumi hairuhusu kutekelezwa kwa vipaumbele vyote hivyo na badala yake wakataka vipunguzwe hadi vitano au sita ambavyo ni elimu, nishati, miundombinu, kilimo, afya na maji.

Wabunge hao pia waliitaka Serikali ichukue hatua za haraka kupunguza mfumuko wa bei ambao waliuelezea kuwa umewafanya wananchi waishi maisha ya shida kutokana na gharama kupanda kila siku.

Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), alisema amekuwa serikalini kwa muda mrefu, na anajua ujanja wa watumishi kujiwekea vipaumbele vingi kama njia ya kujitengenezea mambo yao.

“Vipaumbele vikiwa vichache na kutengewa fedha za kutosha, uchumi wa nchi utasonga mbele, la sivyo itakuwa kama kawaida … hayo mengine msiyaendekeze, najua kwa nini wanayasukumia humo,” alisema Chenge.

Mbunge wa Ilala, Musa Azzan Zungu (CCM) alisema, tatizo la Tanzania si mipango bali ni utekelezaji. Na tatizo hilo linatokana na watumishi wengi kutanguliza ubinafsi, roho mbaya na kutochukua uamuzi matokeo yake uchumi wa nchi haupigi hatua.

“Hapa tunaletewa mipango mingi na mizuri, lakini hakuna mkakati wa utekelezaji,” alisema Zungu na kutoa mfano kuwa Kilimo Kwanza licha ya kuwa ni kipaumbele cha Serikali, hakuna mipango ya uzalishaji mazao unaoonekana.

“Leo hii Kilimo Kwanza kimekuwa ni Power Tiller (matrekta madogo) kwa sababu tu ni mipango ya watu na ndiyo maana inapigiwa debe kila kona … usishangae hata Muhimbili tukaambiwa wanapelekewa Power Tiller,” alisema Zungu na kusababisha kicheko kutoka kwa wabunge.

Mbunge wa Magu, Festus Limbu (CCM), alipendekeza kuwepo bajeti ya miaka miwili itakayotumika kurekebisha matatizo ya kiuchumi na vipaumbele vya Taifa vianze kutekelezwa baada ya bajeti hiyo ya miaka miwili.

Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM), aliponda Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta) kwa madai kwamba umeshindwa kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi, lakini pia umeshindwa kukuza uchumi wa Taifa.

Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliunga mkono kupunguzwa kwa vipaumbele, lakini akaitaka Wizara kuhakikisha vipaumbele vyake vinafanana na ahadi za Rais Jakaya Kikwete ambazo alizitoa wakati akiomba kura za Watanzania.

Kuhusu mfumuko wa bei, Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), alisema bei za vyakula ziko juu na akataka Serikali ieleze mkakati wake wa kukomesha mfumuko huo, kwa sababu hawana uwezo tena wa kununua.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), alihoji iweje takwimu za Serikali zinaonesha mfumuko mdogo wa bei, asilimia 5.6 Desemba mwaka jana, wakati gharama za maisha zinazidi kuongezeka kila kukicha. “Wachumi twambieni ukweli nasi tuwaambie wananchi, kuwa hali ya uchumi ni mbaya.”

Wabunge wengine pia walihoji kuongezeka kwa deni la Taifa kutoka dola milioni 9.3 za Marekani hadi dola milioni 11 sawa na asilimia 18, lakini Waziri Mkulo alisema deni hilo linahimilika.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alitaka kujua sababu ya Tanzania iliyokuwa kwenye Mpango wa Kupunguziwa Madeni kwa Nchi Masikini (HIPC) deni lake lizidi kuongezeka kila mwaka.

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alisema deni la nje linaongezeka kwa vile Serikali inakopa fedha hata kwa matumizi ya kawaida, badala ya kukopa fedha kwa matumizi ya miradi ya maendeleo. “Hii ni hatari kwa Taifa,” aling’aka.

Thursday, March 17, 2011

Hali ya nchi tete



-Dk. Slaa:Watanzania hawahitaji kufundishwa ya Misri
-Asema kama si CHADEMA kuwapoza “hali ingelikuwa tayari”
-Azungumzia pia CCM inafadhiliwa kutoka nje


WAKATI Kanisa Katoliki likionyesha kukerwa na mwenendo wa Serikali katika kutumikia umma, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umejitosa kupooza joto la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwavaa wazee ndani ya chama hicho tawala, Raia Mwema limebaini.

Uchunguzi wa Raia Mwema kwa wiki kadhaa sasa umebaini kwamba UVCCM imekuwa katika mikakati mizito ya kufanya mageuzi makubwa ndani ya CCM kivitendo kwa kufanya mambo ambayo yamekuwa yakifanywa na CHADEMA yakiwavuta vijana wengi.

“Vijana sasa wameamua kufanya siasa za ukombozi maana tumechoka kuchekwa na kuwafanya wananchi wapoteze imani na CCM kwa sababu tu haiwatetei. Vijana wa CCM nao wameamua ‘kufanya kweli’ kuwatetea wananchi bila kujali kama Serikali ni ya CCM.

“Kama tutakosea mahali basi kazi ya wazee itakuwa kutuombea radhi maana wao ndio wamechelewa kufanya siasa. Walijisahau sana na wengine badala ya kutetea wamekuwa wakitumaliza,” anasema mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya UVCCM.

Tayari kuna habari kwamba mbali ya kutoa matamko mazito, UVCCM wanapanga kufanya maandamano nchi nzima huku baadhi wakipendekeza hata kuiteka Ofisi Ndogo ya CCM-Lumumba Dar es Salaam.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinabainisha kuwa vijana wa CCM wamepanga ‘kuiteka’ ofisi ndogo ya CCM-Lumumba inayotumiwa na Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa; Katibu Mkuu, Yusuf Makamba; Naibu Katibu Mkuu, George Mkuchika; Katibu wa Uenezi, John Chiligati na Mweka Hazina Amos Makalla.

Ukimtoa Msekwa, wanaobaki katika orodha hii ni wajumbe wa sekretariati ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikituhumiwa kwa kushindwa kuongoza vyema chama huku ikipendekezwa kwamba wajumbe wake hao wapime wenyewe kama bado wanahitajika katika nafasi walizonazo.

Inadaiwa kuwa vijana hao wamechoshwa na namna chama chao kinavyoendeshwa na kwamba sekretariati ya sasa ya chama hicho haina uwezo tena wa kukistawisha chama.

“Tunadhani muda unazidi kupotea kwa kuendelea kuicha sekretariati hii madarakani. Vijana wanajipanga kwenda kuwaondoa ofisini kwa nguvu,” alisema mmoja wa wajumbe wa Baraza la Utendaji la UVCCM.

Lakini wakati taarifa hizo za ‘mapinduzi’ zikivuja Katibu wa UVCCM, Martin Shigela, amekanusha kuwapo kwa mpango huo na akasisitiza kuwa huo si utaratibu wa CCM.

“Ndani ya CCM hatuna utaratibu wa kuteka ofisi. Isipokuwa kiongozi anaweza kujiondoa ofisini au katika madaraka aliyonayo kwa kujiuzulu au kuondolewa. Utaratibu wetu ni kwamba mtu anakabidhiwa madaraka kwa kuchaguliwa au kuteuliwa na si kuteka ofisi.

“Ni kweli vijana wameanza kutoa maoni ya kutoridhishwa na baadhi ya watendaji ndani ya chama ngazi ya Taifa. Lakini naamini wanajua taratibu za chama na moja ya taratibu hizo ni kutoa maoni yao kwenye vikao vyao kama walivyofanya,” alisema Shigela.

Katika hatua nyingine, vijana ndani ya CCM wamepanga kukutana mwishoni mwa wiki mjini Dodoma kupitia Baraza la Utendaji la Taifa, ambako watatoa tamko kuhusu mwenendo wa chama chao.

Kikao hicho cha UVCCM kinafanyika katika mazingira ya kuzidisha shinikizo dhidi ya sekretariati ya CCM kung’olewa na kukemea baadhi ya waliopata kuwa vigogo wa serikali ambao wanadaiwa kushambulia serikali.

Shigela, amelithibitishia gazeti hili kuwa kikao cha Baraza la Utendaji UVCCM Taifa kitafanyika mwishoni mwa wiki hii mjini Dodoma na kwamba maazimio yatatolewa kuhusu msimamo wa umoja huo.

Mkutano huo utafanyika ukiwa umetanguliwa na vikao vya UVCCM ngazi ya mkoa, na baadhi ya mikoa imetoa kauli zilizotikisa sekretariati ya CCM.

Hivi karibuni, mkoani Pwani, katika hali inayoonyesha kukosa uvumilivu, UVCCM mkoani humo ulikemea kauli zilizotolewa na baadhi ya wana CCM maarufu na pia udhaifu wa baadhi ya watendaji ambao umoja huo unaamini sasa wameshindwa kumshauri Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kustawisha chama hicho.

UVCCM mkoa wa Pwani, waliwataja kwa majina Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisaidia kukielekeza chama jinsi ya kukabiliana na mapigo ya CHADEMA.

Lowassa yeye alikwenda mbali zaidi kwa kuikosoa Serikali akitaka iongeze kima cha chini cha mishahara kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, kauli ambayo vijana wameiona ina malengo ya kujikweza kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Akizungumzia hali hiyo, Katibu Shigela alilieleza gazeti hili kuwa vijana hao wanao uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni kama ambavyo wamefanya na anasubiri taarifa yao rasmi.

“Kwa sasa nami nimepata taarifa hizo kupitia magazeti tu bado taarifa rasmi naisubiri kutoka kwa Katibu. Kwa kawaida, vikao kama hivyo vinapofanyika tunaandikiwa muhtasari ngazi ya Taifa,” alisema Shigela akizungumzia kauli ya vijana wa Pwani.

Aliunga mkono vijana wa chama hicho kushangazwa na waliopata kuwa viongozi wakuu wa serikali ambao sasa wanaishambulia Serikali iliyopo madarakani hata katika mambo ambayo alisema wakati wao walishindwa kuyatekeleza kwa ufanisi.

“Vijana pia wametoa maoni yao kuhusu mwenendo wa baadhi ya viongozi waliowahi kushika nafasi za juu serikalini hasa wanaokosoa kupitia vyombo vya habari wakati huo si utaratibu wa chama.

“Ni muhimu kwa viongozi hao wakatumia taratibu za chama kutoa maoni yao. Baadhi ni viongozi bado ndani ya chama hasa vikao nyeti kama Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini ni kama hawajui tena kanuni za chama zinasemaje. Ni kweli kuna uhuru wa kutoa maoni, lakini ndani ya vikao,” anasema Shigela.


Wakati hayo yakiendelea ndani ya CCM, vyama vya NCCR-Mageuzi na CUF kupitia wenyeviti wa vyama hivyo, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza wakiendesha mikutano ya hadhara wakishambulia mwenendo wa viongozi wa CHADEMA kuitisha maandamano na mikutano.

Kwa mujibu wa Mbatia na Lipumba, viongozi hao wa CHADEMA wamekuwa wakihimiza uvunjifu wa amani kwa lengo la kutaka kuing’oa madarakani Serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

Mikutano hiyo imekuwa ikifanyika kwa siku kadhaa sasa katika maeneo mbalimbali mkoani Kigoma. Katika mwelekeo huo, CUF na NCCR-Mageuzi ni kama vimeungana na CCM na Serikali katika kukikosoa CHADEMA.

Katika ziara hizo, Mbatia ambaye hana wadhifa serikalini ametembelea miradi na maeneo mbalimbali ikiwamo uwekezaji katika Shirika la Reli (TRL), alikotoa kauli ya kutaka kukarabatiwa kwa miundombinu.

Mbali na joto hilo la kisiasa, hali ya uhusiano kati ya dola na baadhi ya viongozi wa dini nchini si shwari huku baadhi ya viongozi wa dini wakianza kutoa kauli zinazoashiria kuandamwa na hata kuwapo kwa kusudio la kuuawa.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ni kati ya viongozi walioweka bayana kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Serikali hawafurahishwi na viongozi wa dini kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mustakabali wa nchi yao.

Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, baadhi ya viongozi serikalini wamekuwa hodari kuficha uozo wanaowatendea wananchi kwa gharama yoyote.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo wakati wa Misa ya kuwaombea watu waliopoteza maisha kwenye milipuko ya mwezi uliopita ya mabomu Gongolamboto, jijini Dar es Salaam.

Alitaja baadhi ya uozo unaofanywa na viongozi hao kuwa ni pamoja na ufisadi wa mali za umma, akitolea mfano utayari wa ghafla wa baadhi ya viongozi kutaka serikali ilipe bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans.

Kwa mujibu wa Pengo, hali ni mbaya kiasi cha baadhi ya watu kutenda maovu na kufunga midomo watu na baadhi ya vyombo vya habari kuzungumzia uovu huo. Alisisitiza kuwa viongozi hao mafisadi wako tayari kutoa uhai wa watu wanaodhani ni kikwazo kwao.

Pengo alisema Nabii Yeremia alitaka kuuliwa kwa sababu tu alitoa unabii ambao si mzuri kwa taifa lake.

“Viongozi wanapenda tu habari za kuwafurahisha wao na wapambe wao. Wanapenda kusikia tu mambo mazuri hata kama ni ya kipumbavu. Yeremia alivyowaambia ukweli walifanya kila liwezekanalo kumuu, mpaka wakaenda kumtupa kwenye kisima kilichokuwa na matope,” alieleza Kardinali Pengo na kuongeza:



“Mimi nimesema haya leo. Maisha yangu yapo mikononi mwenu, lakini kwa kuwa ni Mungu kanituma nitasema. Mkiniua leo au kesho sijali. Mkisikia, msiposikia shauri yenu.”

Alifafanua: “Mkiniuwa damu yangu iko mikononi mwenu, kwa sababu mtakuwa mmemwaga damu isiyokuwa na hatia. Nasema hivi si kuwa naropoka. Najua ninachokisema. Kwanini nifungwe mdomo? Nasema haya leo na nyie mkiwa hapa, kama kuna chombo kitakacho kuwa na ujasiri wa kuandika mtaona yatakayotokea.”

Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amerejea kutoka safari ya Monrovia, Liberia na kutoa kauli nzito kuhusu hali ya kisiasa akijibu shutuma zilizotolewa dhidi ya chama chake kufadhiliwa na mataifa ya nje.

Katika maelezo yake katika mtandao wa Jamiiforums.com na katika mahojiano maalumu na Raia Mwema jana, Dk. Slaa alisema kuihusisha CHADEMA na vurugu ni ufinyu wa fikra kutokana na chama chake kujitahidi kuwasihi wananchi watulie:

“Ni upofu kujifanya huoni hali tete ya Tanzania. Watanzania huhitaji kuwafundisha kuwa ‘kama Tunisia, Misri nk…. Wanaona kwa macho yao wenyewe. Watanzania saa hizi wako mbele kuliko sisi, na kama si kuwapoza sisi hali ingelikuwa tayari. Asiyetaka kuona hilo ni ‘kipofu’ bila sababu (siyo wasioona kuna tofauti ya msingi sana).

“Unahitaji tu (kuangalia) kwenye mikutano mabango yanayoandikwa. Nani kawafundisha.Wakati wa kufanya ‘mchezo wa bundi’ umeisha. Tuwe wakweli tutoke tunduni, tutaokoa Taifa letu. Taifa haliokolewi kwa kujenga hofu bali kwa kuondoa kero, kufanyia kazi kero za watu, kujibu hoja zilizoko kwa hoja. Mbinu za mwaka 47 hazina nafasi tena”.

Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema muda mfupi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dk. Slaa alizungumzia shutuma za CHADEMA kufadhiliwa na mataifa ya nje ikiwamo Ujerumani akisema kwamba vyama vyote kikiwamo CCM vinashirikiana na mashirika na vyama marafiki na hakuna usiri katika hilo.

“Kwa wale wasiofahamu, ni vema wakafahamu kuwa kama ambavyo CHADEMA inashirikiana na Konrad Adenauer Stiftung (Foundation) NGO ya Kijerumani yenye Itikadi ya Mrengo wa Centre- Right kama ilivyo CHADEMA, CCM ina ushirikiano kama huo huo na Friedrich Ebert Stiftung, ambayo kwa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwakilishi wake ni Dk.Stefan Chrobat, aliyeko Plot 397, barabara ya Kawawa,” alisema.

Dk. Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walikuwa nchini Liberia kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Democratic Union of Africa (DUA) ambayo hadi mwaka 2009 CHADEMA ilikuwa sekretarieti na NPP ya Ghana ilikuwa mwenyekiti. Mbowe alitoa mada katika mkutano huo.

Wednesday, March 16, 2011

Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) yafungua kesi kupinga Mfuko wa Jimbo

MASHIRIKA sita yasiyo ya Serikali yamefungua shauri la kikatiba Mahakama Kuu kutaka ibatilishe Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo, kwa yanachodai kuwa inapingana na Katiba ya nchi.

Katika madai hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanayohoji uhalali wa kikatiba wa Sheria hiyo namba 16 ya mwaka 2009, mashirika hayo yanadai kwamba ina athari kutokana na kudhoofisha majukumu ya wabunge na kukinzana na dhana ya kikatiba ya mgawanyo wa madaraka.

Mashirika husika ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), The Leadership Forum, Ulanga West Development Organisation, Haki Development Organisation, Uchungu wa Mwana na Mtandao wa Policy Forum.

“Tunapenda kusisitiza kuwa japo Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo unaweza kuonekana kama jambo zuri, tumebaini kuwa utekelezaji na usimamiaji wa Mfuko huo utakuwa na kasoro nyingi na hasa nafasi wanayopewa wabunge kuwa wasimamizi wake wakuu,” alisema Israel Ilunda wa Policy Forum.

Ilunda ambaye alisoma taarifa ya mashirika hayo jana Dar es Salaam kabla ya kwenda Mahakama Kuu kuwasilisha shauri lao, alisema sheria hiyo ikiendelea kutumika, itadhoofisha nguvu ya wabunge bungeni katika kuisimamia Serikali.

Alifafanua: “Na endapo wabunge watajiingiza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo wenyewe badala ya kuziachia Serikali na halmashauri za wilaya, watakuwa wamedhoofisha uhuru na nguvu yao ya kuihoji Serikali kwenye masuala ya utekelezaji wa bajeti.”

Pamoja na kufungua shauri hilo, mashirika hayo yameishauri Serikali iwawezeshe wabunge kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha wanapata ofisi majimboni, wanaboresha mfumo wa mawasiliano kati ya wabunge na wananchi majimboni na iwezeshe kila mbunge kuwa na wasaidizi rasmi wanaoweza kufanya utafiti, kufuatilia masuala na kutekeleza majukumu yao.

Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ilitungwa Julai mwaka juzi na kusainiwa na Rais, Agosti 21 mwaka huo kwa lengo la kuchochea maendeleo jimboni.

Hata hivyo, tangu sheria hiyo ilipokuwa kwenye mchakato wa kutungwa, wanaharakati waliipinga wakidai inakiuka Ibara za 63 na 64 za Katiba zinazobainisha kazi za wabunge. Pia wanadai inapingana na Ibara ya 4 ya Katiba kuhusu mgawanyo wa madaraka.

Shida ya maji Dar es Salaam mwisho 2013

SERIKALI itatumia Sh bilioni 654 katika programu maalumu ya maji jijini Dar es Salaam ili kuongeza usambazaji wa maji pamoja na kupunguza idadi ya maji yanayopotea kutoka asilimia 50 hadi asilimia 30.

Chini ya programu hiyo inayotarajia kukamilika mwaka 2013, Serikali itachangia asilimia 80 ya mradi huo ambazo ni Sh bilioni 526 , wadau wengine wa maendeleo watachangia asilimia 20 (Sh bilioni 128).

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya alisema, programu hiyo ni kubwa inaofanywa na Serikali ukifuatiwa na mradi wa maji wa Kahama-Ziwa Victoria uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 220.

Profesa Mwandosya alisema, programu hiyo pia itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafisha maji katika Bonde la mto Msimbazi, Mbezi Beach na baadaye katika maeneo ya Kurasini.

“Programu hiyo itahusisha ujezi wa visima virefu katika maeneo ya Kimbiji (Kisarawe) na Mpera katika Wilaya ya Mkuranga ili kutoa huduma ya maji kusini mwa Dar es Salaam,” alisema.

Profesa Mwandosya alifafanua kuwa, upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda huko Morogoro utamalizika Juni mwaka huu; bwawa hilo la kuhifadhi maji litakuwa chanzo cha maji jijini Dar es Salaam itakayoongeza katika mto Ruvu ambao iliarifiwa kiwango cha maji kilipungua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotokana na uharibifu wa mazingira.

“Kwa sasa tunatafuta mkandarasi kupanua mtambo wa maji wa Ruvu Juu utakaowezesha kusambaza maji lita milioni 142 kutoka za sasa ambazo ni lita milioni 82 ikiwa ni ongezeko la lita milioni 60 kwa siku.

Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini tayari unaendelea chini ya makampuni kutoka Ufaransa na Kenya ambapo uzalishaji wa maji utaongezeka kutoka lita milioni 182 hadi lita milioni 272 kwa siku ikiwa ni ongezeko la lita milioni 90 kwa siku, alieleza Waziri huyo wa Maji.

Alisema, mabomba makubwa mawili yatajengwa kutoka Ruvu Juu hadi Segerea ili kutoa huduma kwa wakazi wa Kimara, Ubungo, Kinyerezi na Segerea na bomba lingine litajengwa Ruvu Chini.

Alisema, fedha kutoka wadau wa maendeleo zitapatikana kwa kuwa , kati ya hizo zinatoka katika Akaunti ya Changamoto za Milenia na kwa kuwa programu hiyo ni ya miaka minne, Serikali imejiandaa kuhakikisha fedha zote zinapatikana.

Ingawa programu hiyo itakamilika Desemba 2013, imeanza katika Bajeti ya Serikali ya 2010/11 hadi 2013/14, na kwa zaidi ya miaka 30, Dar es Salaam haikuwa na mradi wowote wa usambazaji wa maji ambapo ule wa Mtoni ulijengwa mwaka 1949, Ruvu Juu 1959 na Ruvu Chini ilijengwa mwaka 1976.

Tuesday, March 15, 2011

Wanawake wasioona kufundishwa haki zao

IDARA ya Wanawake ya Chama cha Wasioona Tanzania, imezindua rasmi mafunzo ya kuwajengea wanawake wasioona uwezo wa kutambua haki zao na kupambana na kero mbalimbali za maisha.

Mafunzo hayo kwa viongozi wanawake wasioona yataendeshwa kwa awamu katika kipindi cha miezi tisa kuanzia mwezi huu, yakihusisha eneo la majaribio la awali la mradi huo lenye wilaya 12 katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Iringa.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka makao makuu ya Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), Doroth Kaihuzi aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kutoka wilaya za Bahi, Mpwapwa, Chamwino na Dodoma mjini jana kuwa, mpango huo umegharimiwa na Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS) kwa gharama ya Sh milioni 45.

Amesema, wanawake wasioona wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu bila kutambua haki zao za msingi, ambapo mradi huo utawasaidia kutambua na kudai haki zao bila kujali mtazamo hasi wa jamii na familia zao.

“Mradi unalenga kuwajengea uwezo wa kujitegemea, kujitetea wenyewe na kujisemea bila kutegemea uwakilishi wa watu wasio na ulemavu ambao hawana uchungu na hali yetu kwa vile haiwagusi.”

“Tunataka kila mwanamke asiyeona ajiamini na kwenda kwenye vyombo vya uamuzi kudai haki,” alisisitiza Kaihuzi ambaye ni mlemavu asiyeona na Katibu wa Idara ya Wanawake ya TLB.

Katika mafunzo hayo wanawake wasioona watajifunza mbinu za ushawishi na utetezi, ujasiriamali, sheria mbalimbali, haki za binadamu na sera zinazogusa huduma za kijamii wanazokoseshwa kutokana na ulemavu wao.

Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake Wasiiona, Dorice Kulanga akizungumzia historia fupi ya idara hiyo iliyoundwa 1989, alisema ililenga kuwaunganisha walemavu wasioona Tanzania Bara na kushughulikia masuala ya kuinua uchumi kwa kuwahimiza kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali.

Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa TLB, tawi la Mkoa wa Dodoma, Omari Lubuva alitoa changamoto kwa Serikali na wadau kuwekeza katika elimu ya watu wenye ulemavu na kubainisha kuwa idadi yao siyo kubwa hasa wanawake wasioona.

Monday, March 14, 2011

Weza yanufaisha wanawake 7,686 Zanzibar

Wanawake 7,686 wanaonufaika na mradi wa kuwawezesha Wanawake Zanzibar(Weza) wameanza kuchukua hatua za pamoja katika kutatua matatizo yao yakiwemo ukatili wa kijinsia na upatikanaji wa huduma muhimu.

Wanawake kutoka Shehia ya Mgogoni walisema wamechanga Sh. 480,000 na kuchimba kisima ambacho hivi sasa ndicho kinachotumiwa Shehia nzima kupata maji safi.

Wanawake hao waliyabainisha hayo walipotembelewa na wataalamu wa jinsia na maendeleo kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Care Austria hivi karibuni.

Wanawake hao kutoka Shehia za Mchangani Unguja Kusini, Mtambwe Kaskazini, Mgogoni na Kisiwani Kaskazini Pemba wamesema wenyewe wameweza kufuatilia kesi za udhalilishaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika ngazi tofauti ambapo baadhi zimefanikiwa kuchukuliwa hatua zinazostahili.

Fatma Said (29) wa Shehia ya Mgogoni alisema yeye alijenga nyumba yake aliyoishi na mumewe, lakini baadaye mume wake alimuacha na kumfukuza ndani ya nyumba hiyo.

Amesema kwa kusaidiana na wanawake wenzake walifuata taratibu za kisheria na iliposhindikana kupata haki ya nyumba yake mahakamani walikwenda Wizara ya Wanawake na Watoto Pemba ambapo iliamuliwa arejeshewe nyumba yake.

Alisema hata hivyo baadaye alimuomba kumrejea na hivi sasa wameoana tena na wanaishi pamoja.

Naye Mratibu wa Shehia ya Mchangani, Nawaje Mussa, alisema hivi karibuni wamesimamia kesi ya msichana ambaye alipewa ujauzito kuhakikisha kuwa anarejea shuleni badala ya kuolewa kama baadhi ya wazee wake walivyopanga kufanya.

Wanawake wa Mtambwe kaskazini wamesema wameweza kushughulikia kesi sita zinazohusiana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambazo baadhi ziko mahakamani.

Mmoja wa wanaharakati wanaotetea haki za wanawake na watoto Pemba, Jaria Hamad amesema kesi hizo zinahusu wanawake kupigwa, ubakaji na mimba za utotoni.

Thursday, March 10, 2011

Mfanyabiashara adaiwa kumnajisi mtoto

MFANYABIASHARA Joseph Mathew (40), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam akidaiwa kumnajisi mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 10.

Mbele ya Hakimu Wilberforce Luhwago, Mwendesha Mashitaka Sakina Sinda alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 3 mwaka huu, saa 2 usiku katika mtaa wa Narung’ombe wilayani Ilala.

Alidai kuwa kwa makusudi mshitakiwa alimuingilia kinyume na maumbile mtoto huyo (jina limehifadhiwa) na kumsababishia maumivu.

Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande hadi Machi 24 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. Katika hatua nyingine, watu watano wamefikishwa katika Mahakama hiyo kwa tuhuma za kuiba vifaa vya umeme vyenye thamani ya Sh 694,000 zikiwemo nyaya.

Washitakiwa hao ni Omary Issa (23) mkazi wa Kiwalani, Nuhu Idrisa (23) mkazi wa Kariakoo, Christopher Mwaitobe (36) mkazi wa Yombo, Juma Ally (20) mkazi wa Jangwani na Hamis Salim (20) mkazi wa Tandika.

Ilidaiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Luhwago kuwa Machi 4 mwaka huu saa 10 jioni katika mtaa wa Lindi, washitakiwa hao walipanga njama na kuiba mali hizo.

Washitakiwa hao walikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini, na kesi hiyo itatajwa tena Machi 24 mwaka huu.

Hivi karibuni kumezuka tabia ya watoto wadogo kufanyiwa ukatili wa namna
mbalimbali ikiwemo kubakwa, kama jamii unaliongeleaje hili?

Tuesday, March 8, 2011

Wanawake, tujikwamue na changamoto zinazotukabili

LEO duniani kote wanaadhimisha Siku ya Wanawake, lakini pia ni siku muhimu kwa kuwa siku hiyo pia inatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.

Kwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine, leo wanaungana na wenzao kuadhimisha siku hiyo ambayo hutumiwa kwa ajili ya kuhamasisha juu ya haki za mwanamke lakini pia kuamsha hamasa kwa wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na hata kijamii.

Ukweli ni kwamba siku hiyo ni maalumu ambayo wanawake wengi wanaokosa nafasi ya kusikika hutumia fursa hiyo angalau kutoa kilio chao au kuonyesha mfano kwa wanawake wengine ambao bado wana uoga wa kujaribu.

Ni siku ambayo pia hutumika kutathmini jitihada zinazofanywa na taasisi na vyama mbalimbali vya wanawake pamoja na harakati za wanawake kuona kama jitihada hizo ama zimefanikiwa, kupunguza au zimeshindwa kutatua matatizo ya wanawake.

Kihistoria siku hiyo ilianza kuadhimishwa tangu mwaka 1911 wakati makundi ya wanawake nchini Marekani yalipokusanyika na kupinga udhalilishaji, ukandamizaji, uonevu na ubaguzi wa kijinsia hususani sehemu za kazi.

Kutokana na hamasa ya wanawake hao na matatizo mengi yaliyokuwa yakiwakabili wanawake
katika mataifa mbalimbali duniani, nchi nyingi nazo zilijiunga na kuteua siku moja ambayo ni Machi 8 ya kila mwaka kuadhimisha siku hiyo.

Na hiyo ilitokana na ukweli kuwa matatizo mengi yanayohusu wanawake katika nchi nyingi yalikuwa ama yakifanana au baadhi ya maeneo yalizidiana.

Hivyo hadi leo, maadhimisho hayo sasa yanatimiza miaka 100, huku bado wanawake wakiendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo bado zimelalia katika tatizo sugu la mfumo dume, bila kusahau matatizo ya uzazi ambayo yanaondoa duniani wanawake wengi huku wengine wakiachwa na magonjwa sugu.

Sasa wakati umefika kwa wanaharakati nchini lakini pia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, kuziangalia kwa karibu changamoto hizo na kuzichukulia hatua kwa vitendo na si kubaki na maneno jukwaani.

Tumekuwa tukisikia kila kukicha maneno ya kukemea vitendo vya kikatili kama vile unyanyasaji wa wanawake, ukeketaji kwa wanawake, vitendo vya kubakwa na ndoa za utotoni
na hata kufikia kuomba sheria ya ndoa kufanyiwa marekebisho huku bado matatizo hayo yakizidi kuendelea katika baadhi ya maeneo.

Sisemi kwamba hakuna mafanikio yoyote mpaka sasa, lakini ninachosisitiza ni hatua thabiti zinazoonekana kuchukuliwa dhidi ya matatizo hayo sugu hususani hilo la vifo vya akinamama
wajawazio ambalo bado ni mzigo.

Tuadhimishe siku hii, kwa wanawake wenyewe kuwa mstari wa mbele na kushirikiana kukabiliana na changamoto hizo, na jambo la msingi ni kuacha ubinafsi na kutopendana na
kuungana pale inapodi ndipo mafanikio yataonekana.

Katika kutatua matatizo makubwa na sugu yanayowakabili wanawake duniani kote na si Tanzania pekee, ushirikiano, umoja na upendo na kujituma kunatakiwa na si kuingiza siasa.

Imeandikwa na Halima Mlacha

Monday, March 7, 2011

Maadhimisho Siku Ya Wanawake Duniani Machi 8

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kila mwaka tarehe 8 Machi. Madhumuni ya Maadhimisho haya ni kupima utekelezaji wa maazimio, matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusu masuala ya wanawake. Aidha, madhumuni mahususi ni pamoja na:

• Kujenga mshikamano wa wanawake wote duniani.
• Kuweka msisitizo na kuhamasisha jamii kuhusu kaulimbiu ya kimataifa wakati wa
Maadhimisho ya kila mwaka
• Kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali, asasi mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kuwaendeleza wanawake.
• Kuhamasisha jamii kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na ahadi mbalimbali za kudumisha “Amani, Usawa na Maendeleo”.

Vilevile, Maadhimisho haya hutoa fursa maalum kwa Taifa, Mikoa, Wilaya mashirika ya dini, vyama vya siasa, mashirika ya hiari, jamii na wanawake, kupima mafanikio yaliyofikiwa kimaendeleo na kubainisha changamoto zilizojitokeza katika kufikia azma ya ukombozi na maendeleo ya wanawake na hivyo kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.

Hapa nchini maadhimisho haya yalifanyika Kitaifa kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 2005 na baada ya hapo Serikali ilipitisha uamuzi kuwa yafanyike kila baada ya miaka mitano. Uamuzi huu ulipitishwa ili kutoa muda wa kutosha wa utekelezaji wa maazimio mbalimbali na kuweza kupima mafanikio ya utekelezaji wa shughuli hizo za kila baada ya miaka mitano.

Madhumuni ya kufanya maadhimisho hayo kila baada ya miaka mitano:-

1. Kutoa fursa kwa Serikali, vyama vya siasa, jamii na wadau wengine kuweza kupima mafanikio ya utekelezaji wa sera, mikakati na programu mbalimbali za kitaifa na kisekta.

2. Kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazojitokeza.

Kwa kuzingatia uamuzi huo maadhimisho ngazi ya Kitaifa yalifanyika mwaka 2010, sambamba na maadhimisho ya miaka 15 ya utekelezaji wa Azimio na Ulingo wa Beijing, 1995. Maadhimisho haya yalifanyika Mkoani Tabora, na Mgeni rasmi akikuwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo maadhimisho haya kwa mwaka 2011 yataandaliwa katika ngazi ya mkoa, na kila mkoa umejiwekea utaratibu wa maadhimisho haya kwa kuzingatia ujumbe wa Kaulimbiu ya mwaka 2011.

Kaulimbiu ya Mwaka 2011
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2011 ni ‘Fursa sawa katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia: Njia ya Wanawake kupata ajira bora” na katika lugha ya kingereza ni ‘Equal access to education, training, science and technology: Pathway to decent work for women”.
Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuwapatia wanawake na wanaume fursa sawa katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia ili nao waweze kupata ajira bora kama ilivyo kwa wanaume. Kaulimbiu hii inaenda sambamba na utekelezaji wa Ulingo wa Beijing, kwa kuzingatia kuwa mojawapo ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Ulingo wa Beijing ni kuwapatia wanawake elimu mafunzo na Ajira.

Kaulimbiu ya mwaka 2011 inahamasisha Serikali katika kutoa fursa sawa kwa watanzania wote bila kujali jinsi zao.
Katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na fursa sawa kwa wanawake na wanaume, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kurekebisha baadhi ya sheria na inapobidi kutunga mpya ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na fursa sawa kati ya wanawake na wanaume katika elimu, mafunzo sayansi na teknolojia.

Katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Serikali imeandaa mpango wa uboreshaji wa mfumo wa sayansi na teknolojia na ubunifu hapa nchini. Aidha, imeendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari kuhusu matumizi ya vyombo vya sayansi na teknolojia.

Friday, March 4, 2011

Rais Kikwete hasomi alama za nyakati - Slaa

-Asema Katiba inawapa nguvu wananchi
-Wavuta watu Mwanza, Mara na Shinyanga

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kusoma alama za nyakati badala ya kulaumu wapinzani kwa mawimbi ya kisiasa nchini kwa vile mazingira ya sasa yanasukumwa na nguvu ya wananchi wanaotaka kupata maisha bora waliyoahidiwa.

Akizungumza na Raia Mwema kwa simu akiwa njiani kuelekea Maswa mkoani Shinyanga, jana Jumanne, Dk. Slaa alisema wimbi la mageuzi la sasa katika Tanzania na duniani halitokani na CHADEMA bali linasababishwa na wanasiasa walioshindwa kuusikiliza umma, kwamba Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) vimewachosha wananchi na wao kama chama cha siasa kilichobaini mapungufu hayo, hawatasitisha vuguvugu la sasa.

Alisema Rais Kikwete ana haki ya kuwa na hofu kuhusu hali ya sasa lakini kwamba anapaswa kusikiliza kilio cha wananchi walio wengi kwani “ndiyo salama yake, vinginevyo hatakuwa salama”.

Akihutubia Watanzania kupitia vyombo vya habari Juzi Jumatatu, Rais Kikwete alielekeza lawama zake kwa CHADEMA kuwa ni chama kinachotaka kuleta vurugu nchini kwa nia ya kuiondoa Serikali halali madarakani kwa kuhamasisha wananchi nchi nzima wakati uchaguzi ukiwa umemalizika.

“Siyo sawa hata kidogo kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani. Ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,” alisema Kikwete katika sehemu ya hotuba yake hiyo.

“Nadhani Bwana Mkubwa (Rais Kikwete) kateleza juu ya Katiba aliyoapa kuilinda na kuitetea. Anaanza kusema kwamba uchaguzi umeisha na CHADEMA inafanya vurugu; anasahau uchaguzi mmoja ukiisha unaanza mwingine na kazi yetu si kumpigia makofi tu bali kazi yetu ni kuikosoa Serikali.

“Nadhani anajenga hofu, ambayo ni hofu ya hakika na ni halali kwa sababu ya udhaifu wa Serikali yake na udhaifu wa wanaomshauri. Sisi CHADEMA hatuna namna ya kumsaidia. Serikali imara ni ile ambayo haihitaji kunyooshewa vidole bali inachukua hatua kwa kila jambo linalohusu maslahi ya watu wake,” anasema Dk. Slaa.

Dk. Slaa ambaye alikuwa mgombea Urais mwaka 2010, katika uchaguzi ambao Kikwete aliibuka mshindi, anasema Serikali ijue kwamba mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa mwingine na kwamba hiyo ndiyo kazi inayofanywa na CHADEMA sasa nchi nzima.

“Kikwete anaona tunasababisha vurugu, lakini walipokuwa wakichezea uchaguzi hawakugundua kwamba wanaanzisha vurugu? Hawakujua ndiyo matokeo yake? Akumbuke sisi hakuna mwenye uchu wa madaraka wala kukimbilia Ikulu na ajue tokea zamani hatujaikimbilia Ikulu ila ajue maisha ya umma wa Watanzania ndiyo yanatusukuma tuwafuate wananchi na kuwasikiliza.

“Wananchi wale hakuna anayebebwa na magari, hakuna maduka yanayolazimishwa kufungwa wala hakuna polisi wanaowafukuza mitaani wahudhurie mikutano yetu, bali wanatufuata kwa mapenzi yao na kwa kuchoshwa na Serikali yao. Akitaka asikilize kilio cha wananchi kwa kutekeleza matakwa yao,” anasema Dk. Slaa.

Akitoa mfano wa hatua zilizochukuliwa na Serikali baada ya kuanza kwa maandamano, Dk. Slaa amesema Serikali imechukua hatua ya kudhibiti bei ya sukari baada ya CHADEMA kutoa siku tisa kwa Serikali, wakati ilishindwa kufanya hivyo wakati wabunge walipolipigia kelele suala hilo ndani ya Bunge.

“Kama bungeni hawakusikiliza kuhusu sukari, tumempa siku tisa amesikiliza. Ajue hakuna mwenye nia ya kumuondoa ila ajue akishindwa hatuna ndoa yoyote na yeye wala CCM. Kama atashindwa kuondolewa kwa kura na kama akichakachua tena ataondolewa kwa nguvu ya umma uliochoka,” alisema Slaa ambaye alikuwa wa pili baada ya Kikwete katika uchaguzi uliomalizika Oktoba mwaka jana.

Akizungumzia hali ya maisha inayowasukuma wananchi kuichukia serikali, Dk. Slaa amesema; “Bei za bidhaa zimepanda kwa kasi zaidi, hatuwezi kufumba macho, hatuwezi kusuburi… Tunasema kwa miaka mitano iliyopita watawala watuambie wamejenga majumba mangapi wao na familia zao. Wamepata wapi ukwasi wote huo katika dimbwi la umasikini wa Watanzania?”

Anasema kwa zaidi ya miaka mitano ni suala moja tu ambalo serikali imelifanyia kazi nusu nusu na kuacha mambo mengine mengi yakielea bila kufanyiwa kazi.

“Wamezima sakata la ufisadi wa Meremeta, Kagoda na EPA, tena tuliyazungumza bungeni; Suala la EPA ameonyesha kidogo lakini hakuna alichofanya na badala yake serikali imeapa bungeni kwmaba haitajibu suala la Meremeta.

“Sasa yeye anatuambia turudi bungeni akijua wao wako wengi na watamtumia Spika kuzima hoja zetu, tunakataa na tunaamua kutumia Ibara ya 8 (a) ya Katiba ambayo inatoa mamlaka ya juu kwa wananchi ambao ndio wanaoliweka Bunge na serikali,” anasema.

Ibara ya 8 (a) ya Katiba inasema, “Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii.”

CHADEMA wameanza kampeni kali wakianzia na mikoa ya kanda ya Ziwa ya Mwanza, Mara na Shinyanga, kampeni ambazo zimepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, hali inayotishia watawala akiwamo Rais Kikwete aliyejikuta akishindwa kujizuia kuonyesha hofu yake katika hotuba yake ya Juzi Jumatatu.

Akizungumza na jarida la mtandao la FikraPevu, Dk. Slaa alisema maandamano na mikutano ambayo chama hicho kimefanya na kinaendelea kufanya ni mwanzo tu wa shinikizo la umma dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete kuitaka serikali hiyo kuchukua hatua mara moja na kali dhidi ya ufisadi, mfumuko wa bei, na kuweka ratiba wazi ya mchakato utakaohakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao wa 2015 unafanyika chini ya Katiba mpya.

Dk. Slaa amesema kuwa chama chake kimefikia uamuzi wa kutumia nguvu ya umma kuongeza shinikizo hilo hasa baada ya kuona kuwa serikali ya CCM haichukulii kwa uzito unaostahili madai na malalamiko ya wananchi.

Akijibu swali ya kwanini wanafanya maandamano hayo sasa badala ya kusubiri uchaguzi mkuu ujao kwani nchi imetoka tu kwenye uchaguzi mwingine Dk. Slaa alisema kuwa “uchaguzi siyo mwisho; mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi ya mwingine na shughuli za kisiasa hazikomi kwa sababu uchaguzi umefanyika.”

Kiongozi huyo wa CHADEMA ambaye katika ziara hizi za maandamano ameungana na Mwenyekiti wa Chama hicho na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe pamoja na baadhi ya wabunge, amesema kuwa hoja ambazo wanazijenga sasa hivi zinahitaji maamuzi ya haraka.

Dk. Slaa alizungumzia pia suala la malipo ya Dowans na kwanini chama chake kimechukua msimamo wa kutaka majenereta ya kampuni hiyo yakamatwe mara moja. “Hili linaendana na ukweli kuwa suala la Dowans limefungamana na kuingia kwa kampuni ya Richmond nchini na vile vile hoja nzima ya jinsi gani kampuni ya Dowans iliweza kuchukua kiulaghai mkataba wa Richmond na TANESCO”. Dk. Slaa alisema pia kuwa “serikali ina jukumu la kukamata mitambo hiyo na hakuna sababu ya kuilipa kampuni hiyo”

Akifafanua kama itakuwa vizuri kukamata mitambo hiyo wakati kuna tozo iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa kibiashara Dk. Slaa alisema kuwa “kwa vile Dowans ilitumia ulaghai kushinda kesi hiyo serikali haitakiwi kufungwa na hukumu hiyo”. “Ni bora kuzuia malipo hayo sasa badala ya kusubiri miezi sita au saba baadaye ndipo tuje kugundua tumefanya makosa kuwalipa. Fedha hizo zingeweza kutumiwa katika kuboresha maisha ya watu wetu, wanafunzi, wafanyakazi na wakulima wa nchi yetu”.

Vile vile, Dk. Slaa alizungumzia suala la haraka ya kuwasha mitambo ya Dowans hata ikibidi kwa mkataba wa muda mfupi kama inavyopendekezwa na baadhia ya watu ili kupunguza ukali wa tatizo la ukosefu wa nishati kwa maisha ya watu na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Dk. Slaa hata hivyo alitupilia mbali pendekezo hilo.

“Ni lazima kuelewa kwanza maudhui ya mambo yanayoendelea kabla ya kufikia hitimisho hilo. Tayari nchi inapoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa kulipia gharama ya kutumia mitambo ya IPTL. Serikali ilishauriwa karibu miaka mitano iliyopita inunue moja kwa moja mitambo ya IPTL lakini haikufanya hivyo. Mwaka 2007 serikali iliambiwa kuwa mitambo ipo na kuwa ifanye ununuzi wa kimataifa lakini serikali haikufanya lolote vile vile.”

Dr. Slaa aliendelea kusema kuwa “tunaamini kabisa kuwa juhudi za kutaka mitambo ya Dowans iwashwe na mkataba mwingine uingie ni sehemu ya ufisadi ule ule unaondelea nchini. Tukumbuke kuwa mwezi wa Machi umeshafika na ndio kipindi cha kuanza kwa mvua za masika nchini na hivyo ni wazi baada ya muda si mrefu mabwawa yetu ya kufua umeme yatakuwa yamejaa maji. Sasa kwanini tuingie mkataba wakati huu?” aliendelea “tukumbuke pia kuwa wakati majenereta haya hatimaye yanaanza kufanya kazi mwezi Machi mwaka 2007 mvua zilikuwa zimeanza na mabwawa yalikuwa yamejaa maji lakini tulikuwa tumefungwa na mkataba. Fedha ambazo tungetumia kuingia mkataba na Dowans wakati huu zingeweza kabisa kutumika kununua mitambo mipya tena ya kwetu bila ya kuja kulazimika kulipia gharama ya matumizi ya mitambo hiyo”.

Ameendelea kwa kusema “tayari nchi inapoteza umeme sasa hivi, ni bora basi kupoteza umeme huo kwa wiki mbili zijazo na kupata suluhisho la kudumu kuliko kujiingiza katika mkataba mwingine utakaotugharimu kwa muda mrefu ujao.”

Akizungumzia suala la Katiba Mpya Dk. Slaa alisema kuwa chama chake kiliandika katika ilani yake ya uchaguzi suala la Katiba mpya na kiliweka ahadi ya kuwa uchaguzi ujao ungefanyika chini ya Katiba mpya endapo chama hicho kingeshika madaraka. “Sasa kwa vile serikali imekubali kimsingi suala la Katiba Mpya hakuna jinsi nyingine isipokuwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na Katiba mpya ambayo itaweka vyombo na taratibu ambazo zitazuia kabisa uwezekano wa kutokea machafuko na umwagikaji damu nchini”.

Dk. Slaa alizungumzia hekima na umakini mkubwa uliotumika kuzuia munkari wa vijana wengi baada ya uchaguzi ambao walikuwa wanataka kuingia mitaani kupinga kile ambacho waliamini kuwa kilikuwa ni uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi hafifu Rais Kikwete kulinganisha na ushindi wake wa 2005. “Watu walikuwa wanasubiri kabisa wasikie nitasema nini, lakini sikuwa tayari kusukumiza watu katika kudai kwa nguvu haki yao. Sasa kama hatukufanya hivyo wakati ule hatuna sababu ya kutumia nguvu sasa hivi” alisema Dk. Slaa.

Akizungumzia kile ambacho serikali inaonekana kukihofisa sasa hivi hasa baada ya matukio ya Misri na Tunisia ambapo viongozi wa muda mrefu wa nchi hizo walijikuta wanaondolewa madarakani kwa nguvu za umma Dk. Slaa alisema kuwa wakati wowote wananchi wanaona kuwa haki zao zinapuuzwa wanaweza kujikuta wanalazimika kuzidai kwa nguvu.

“Kile kilichotokea Misri ndicho kilichotokea Arusha vile vile, na ndicho kilichotokea Geita na sehemu nyingine nchini mara baada ya uchaguzi mwaka jana na katika maeneo mbalimbali wananchi walikuwa tayari kwenda kudai haki zao na kama siyo hekima tuliyotumia kwa kweli hali ingekuwa mbaya kwani hata watu waliotaka tuitishe maandamano makubwa tuliwakatalia kwa sababu hatukuwa tayari kufanya hivyo wakati huo”.

Dk. Slaa alisema kuwa “ili kuepusha yanayotokea huko Libya, Misri, Tunisia, Bahrain, Yemeni na nchi nyingine za Kiarabu ni lazima serikali na chama tawala wasikilize kilio cha wananchi na mara moja waanze kutenda kufuatana na madai tunayoyatoa kwani hatutoi madai ya kibinafsi bali madai ambayo ni maslahi ya taifa. Sisi sote ni wadau katika maslahi ya taifa hili; tunataka kuona amani na utulivu lakini wakati huo huo hatuwezi kuwaacha watu wachache waendelee kuliharibu taifa letu”.

Pamoja na hayo Dk. Slaa amesema kuwa wamejaribu mara kadhaa kuanzisha mawasiliano na serikali ya Kikwete ili kusaidia kutoa ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Dk. Slaa na timu nzima ya viongozi wa CHADEMA wameendelea na maandamano na mikutano huko Shinyanga na baadaye wanaendelea na mikutano hiyo huko Kagera kabla ya kurudi Dar-es-Salaam kwa mapumziko mafupi siku chache zijazo.

Chanzo: Raia Mwema

Chadema wasakamwa, wadaiwa wahaini

WANASIASA na taasisi mbalimbali nchini wamepinga maandamano yanayoendeshwa na Chadema kuhamasisha wananchi kuipinga Serikali na kuiondoa madarakani kuwa ni uhaini na inapaswa kushitakiwa.

Aidha, wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, kuangalia uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho kwa usalama wa Taifa na kudai kuwa maandamano hayo ni chanzo cha vurugu na kuvunjika kwa amani, ambazo ni dalili zinazopaswa kuchukuliwa hatua za kiusalama haraka ili Taifa lisiingie katika machafuko ya kisiasa.

Katika siku za karibuni Chadema imekuwa ikifanya maandamano na mikutano ya hadhara kwa lengo la kupinga ufisadi serikalini, hali ngumu ya maisha inayotokana na kupanda kwa bei ya vyakula, malipo kwa Kampuni ya Dowans na tatizo la umeme.

Wakizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Wanaharakati wa Haki za Watu Wenye Ulemavu nchini, walisema kinachofanywa hivi sasa na vyama vya siasa na wanasiasa kuzunguka nchini kuhamasisha wananchi wakubali kuondoa Serikali halali madarakani, kinaweza kusababisha madhara makubwa.

Walipongeza hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wiki iliyopita na kupinga maandamano yanayoendelea katika mikoa tofauti na kusema madhara hayo waathirika wake ni jamii ya watu wenye ulemavu.

Msemaji wa wanaharakati hao, Abubakar Rakesh, alisema wanampongeza Rais kwa kuona kwamba amani ya Watanzania ambayo ni tunu inaanza kutoweka kwa kusema kwake na kuwaondoa hofu Watanzania, imeonesha jinsi anavyowajali wananchi wake.

“Uzoefu na ushahidi unatuonesha, kwamba nchi nyingi duniani zilizokabiliwa na migogoro na uvunjifu wa amani, wahanga wakubwa wa kupoteza maisha ni watu wa jamii ya walemavu, hivyo tunamwomba Rais aendelee kukemea lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi yetu,“ alisema Rakesh.

Walimtaka Rais Kikwete pamoja na kuendelea kukemea hali hiyo, lakini pia asiyumbe katika kulinda amani ya nchi na kuhakikisha kuwa Katiba iliyopo inaheshimiwa na kila mmoja, kwani Katiba ya nchi si ya chama.

Katibu wa Kamati ya Amani Umoja na Mshikamano wa Kitaifa (UPF), Risasi Mwaulanga, alisema wanachofanya Chadema ni uhaini wa wazi, kwani umma utakapokasirika utapata hamasa na kugomea sera ya chama tawala na kuacha kushiriki shughuli za maendeleo.

“Vyombo vya usalama vinatakiwa kuchukua hatua dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema na Katibu Mkuu wake wakamatwe na kufunguliwa mashitaka ya uhaini, ikiwa ni pamoja na Bunge kutoa onyo kwa wabunge wake na Msajili kuangalia vifungu vya Katiba kuona uwezekano wa kukisimamisha au kukifuta chama hicho,” alisema Mwaulanga.

Pia aliwataka wananchi kupuuza mikutano yao ya hadhara bila kujali itikadi, kujenga ushawishi wa kutengwa na taasisi mbalimbali hadi watakaporekebisha mustakabali wa siasa zao za uchochezi nchini .

Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema maandamano hayo yanahamasisha wananchi kuiga mifano ya nchi za Kaskazini mwa Afrika, ambazo chanzo cha maandamano na hatimaye vifo yametokana na vyama vya upinzani.

“Maandamano hayawezi kutuondolea matatizo tuliyonayo, bali yatasababisha maafa makubwa yasiyoweza kulipika, kama ilivyotokea kwenye nchi nyingine duniani, ni wazi tunaweza kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa kutumia njia za kikatiba na kisheria kwa ridhaa ya wananchi kwa kura zao,” alisema Mrema.

Aliwasihi wapinzani wenzake kuwa kwa kutumia njia sahihi wana uwezo wa kuingia madarakani, ndiyo maana walipata asilimia 40 ya kura za urais na wana wabunge na madiwani.

“Wapinzani tuko bungeni, kwenye halmashauri za miji, serikali za vijiji na vitongoji, kwa nini tusitumie fursa hizo? Baada ya uchaguzi siasa zihamie bungeni na kwenye mabaraza ya halmashauri na miji na si kuishia maandamano na mikutano tu,” alisema Mrema.

Alisema wapinzani wana wenyeviti katika kamati mbalimbali za Bunge, hivyo wanaweza kupambana na ufisadi na wakishindwa ni uzembe wao, kwani hawana kikwazo, aliwataka kukamata mafisadi na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria kwani ufisadi hauwezi kuondolewa kwa maandamano.

“Kwa mfano mimi nilishakabidhiwa vitabu vya ukaguzi kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali vinavyoonesha kwenye halmashauri za miji kuna ubadhirifu wa kutisha, kuliko hata ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na Dowans,” alisisitiza Mrema.

Aliwataka Watanzania wasidanganywe na kufananisha Tanzania na nchi nyingine kama Libya na Misri, kwani matatizo hayafanani na nchini tatizo ni umasikini, hali ngumu ya maisha, umeme na ufisadi, wakati nchi hizo zingine, matatizo yao ni mfumo mbaya wa kiutawala tofauti Tanzania.

Wednesday, March 2, 2011

TGNP YAADHIMISHA WIKI YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA MIAKA 50 BAADA YA UHURU

Mmoja wa jopo la watoa mada akiwasilisha mada yake

Mwenyekiti wa TGNP Bi. Mary Rusimbi akitoa muktadha na kuwakaribisha watu waliofika katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani


Wanaharakati wakiserebuka baada ya kuvutiwa na burudani ya kikundi cha sanaa cha Parapanda


Mtoa mada Bi. Anna Mushi kutoka TGNP akiwasilisha mada yake


Bi. Asseny Muro ambaye ni mwanachama mwanzilishi wa TGNP akimkaribisha mwenyekiti wa TGNP Bi. Mary Rusimbi kufungua maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa niaba ya Mkurugenzi wa TGNP

Wanaharakati wakifuatilia mada kwa makini


Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Mary Rusimbi akiongea na waandishi wa habari wa kutoka vyombo mbalimbali kuhusu kuelekea kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani na miaka 50 baada ya uhuru na pia kutafakari juu ya maisha ya wanawake kwa kuzingatia elimu bora na kipato endelevu. Mary Rusimbi amebainisha kuwa siku ya wanawake duniani ni kutafakari miaka 100 ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani katika ustawi wa mwanamke wa kitanzania kiuchumi na kijamii, kuainisha michango, mapambano ya wanawake miaka 50 baada ya uhuru na kubainisha changamoto zinazowakabili kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na kupanga mikakati ya baadae, kutandaa na kupashana habari.












Tuesday, March 1, 2011

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI MACHI 2, 2011

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO



UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII



TGNP WAKISHIRIKIANA NA FEMACT WAMEANDAA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI.

KAULI MBIU: “Miaka 50 baada ya uhuru: Tafakari ya hali halisi ya maisha ya wanawake kwa kuzingatia Elimu bora na kipato endelevu”.



Lini: Jumatano Tarehe 02 Machi, 2011

Muda: Saa 09:00Asubuhi – 08:00 Mchana

MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni




WOTE MNAKARIBISHWA

Kikwete aionya Chadema

RAIS Jakaya Kikwete amekionya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuacha vitendo na kauli za kuwajengea wananchi hofu kuhusu usalama wa nchi yao.

Amesema, vitendo hivyo vya Chadema vina dhamira ya kutaka kuleta machafuko makubwa na uvunjifu wa amani nchini.

“Kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia. Lakini, kuigeuza fursa hiyo kuwa jukwaa la kuchochea ghasia kwa nia ya kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa mabavu, ni matumizi mabaya ya fursa hiyo,” amesema Rais.

Rais Kikwete alikuwa akilihutubia Taifa jana katika utaratibu wake wa kuzungumza na wananchi kwa njia ya televisheni na redio.

Alisema, Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na kila miaka mitano uchaguzi wa viongozi unafanyika na wa mwisho ukiwa ni uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana.

“Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi miwili na nusu. Kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo ya wananchi wa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa.

“Iweje leo, miezi mitatu baadaye kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni? Si sawa hata kidogo. Kuchochea ghasia eti kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima. Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi,” alihadharisha Rais.

Aliwaasa Chadema kutumia Bunge na halmashauri za wilaya kuboresha sera na hoja zao na kuziwasilisha kwa watu badala ya kuzunguka nchi nzima kuchochea ghasia kwa lengo la kuingia madarakani.

“Tutajenga misingi ya hovyo na nchi yetu itakosa amani na utulivu daima. Hebu fikirieni, kama kila atakayeshindwa uchaguzi anafanya hivyo tutakuwa nchi ya namna gani? Tanzania yetu hii yenye sifa na heshima ya kuwa nchi ya amani na utulivu itapoteza kabisa sifa hiyo, na badala yake umwagaji damu na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia vitageuka kuwa maisha ya kawaida,” alisema Rais.

Alikiri kuwa hali ya maisha ni ngumu na kukabiliana nayo ndiyo kazi inayofanywa kila siku na Serikali na ndiko ilikoelekeza nguvu zake na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali.

“Kikwazo si upungufu wa sera wala dhamira, bali kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu na hivyo uwezo wetu si mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo tunapenda iwe.

“Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii. Na wale wa umri wangu au kunizidi, wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri.

“Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa naye miaka 10 hakuyamaliza.

Miye nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote. Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo,” alisema.

Viongozi wa Chadema wanazunguka mikoani wakifanya mikutano ya kuhamasisha wananchi kuichukia Serikali iliyoko madarakani kwa madai kuwa imeshindwa kumaliza matatizo ya wananchi na hata kufikia kumwekea Rais muda wa kutatua matatizo hayo.

Rais Kikwete alisema ni kweli kuna hali ngumu ya maisha, na kwamba kukabiliana nayo ndiyo kazi wanayoendelea nayo kufanya kila siku.

"Tumeelekeza nguvu zetu na rasilimali zetu huko na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali. Kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, kikwazo kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu na hivyo uwezo wetu siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo tunapenda iwe.

Lakini, pia ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wetu ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana na yale yanayotokea katika uchumi wa dunia. Unapoyumba na sisi tunayumba. Bei za mafuta katika soko la dunia zikipanda na kwetu kupitia gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda," alieleza Rais.

"Mfumuko wa bei ukipanda China, nguo na bidhaa tunazonunua kutoka China hupanda bei. Hivi sasa mataifa yote makubwa tunakonunua bidhaa mfumuko wa bei umepanda na sisi tunaathirika. Mvua ikikosekana kunakuwa na uhaba wa chakula, bei za vyakula hupanda na watu wengine hukosa chakula

"Lawama kwa Serikali au Rais Kikwete inaanzia wapi? Hata kwa matatizo yote hayo na mengine tumekuwa tunatafuta nafuu kwa kiwango tunachoweza. Aghalabu, hutoa nafuu ya kodi kama tulivyofanya kwa sukari na tulivyowahi kufanya kwa saruji na kadhalika. Tutaendelea kufanya hivyo inapobidi."

Kuhusu umeme, Rais alisema imekubalika kukodi mitambo ya megawati 260, lakini ikasisitizwa kuwa pamoja na udharura uliopo, sheria na taratibu za ununuzi wa umma vizingatiwe. Pia, ihakikishwe kuwa mikataba inayoingiwa iwe ni yenye maslahi kwa Taifa.

Vilevile, watoa huduma wawe ni kampuni zinazofahamika na zenye sifa stahiki na kuaminika.

“Bahati mbaya sana tatizo la ukame limetukuta tena wakati mipango mingi ya umeme imeanza lakini haijakamilika. Miaka miwili ijayo, hali itakuwa tofauti sana, kwani miradi hii na mingine kadhaa itakuwa imekamilika na kulihakikishia Taifa uhakika wa umeme,” alisema.

Alisema miradi hiyo ya umeme huchukua muda kukamilika. Mitambo huchukua muda kutengenezwa na ujenzi wa vituo pia. “Ingekuwa ni mitambo ya kununua tu dukani tungefanya hivyo na kulimaliza mara moja tatizo hili. Tena lingeisha zamani na wala sisi tusingelikuta,” alisema.

Akizungumzia chakula, Rais alisema hali ya upatikanaji wa chakula nchini katika maeneo mengi ni ya kuridhisha isipokuwa katika maeneo machache. Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, inaonesha kwamba kuna akiba ya kutosha ya chakula katika maghala ya Serikali, ya wafanyabiashara wakubwa na ya wakulima mashambani.

“Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yana tani 216,012 za mahindi na mpunga, nafaka ambazo zinatuhakikishia kuwa upungufu wowote wa chakula tutaukabili bila matatizo. Kiasi hicho ndicho kikubwa kuliko chote kilichowahi kuhifadhiwa tangu hifadhi hiyo ianzishwe na shabaha yetu ni kufikia tani 400,000 mwaka 2015,” alisema.

Kuhusu waathirika wa mabomu, Rais alisema maiti wote 25 wameshazikwa kwa gharama ya Serikali kule ambako ndugu waliamua wakazikwe. Kwa ajili hiyo maiti 10 wamezikwa Dar es Salaam na wengineo mikoani kama ifuatavyo.

Mara walizikwa wanne, Pwani watatu, Tanga wawili, Lindi mmoja, Kagera mmoja, Kilimanjaro mmoja, Mbeya mmoja na Mtwara mmoja. Majeruhi wameendelea kupatiwa matibabu na huduma stahili.

Mpaka sasa alisema kuna majeruhi 36 ambao bado wamelazwa katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili.

Watoto 857 waliopotezana na wazazi wao wameshaunganishwa na familia zao. Hata hivyo, 15 bado hawajatambuliwa na wazazi au walezi wao. Kwa sasa watoto hao wamepelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto cha Kurasini.

Kuhusu nyumba zilizobomoka kutokana na milipuko hiyo ya Februari 16, Rais Kikwete alisema utekelezaji wa agizo la kutambua na kufanya tathmini ya nyumba zilizoharibiwa unaendelea kwa nia ya kuwafidia ipasavyo.

“Kwa upande wa fidia, tumeamua kuwa Serikali ibebe jukumu la kujenga upya nyumba hizo kwa mujibu wa kiwango cha uharibifu. Nimeagiza Jeshi la Kujenga Taifa lifanye kazi hiyo kupitia Shirika lake la Uchumi. Nimeamua hivyo ili kuhakikisha kuwa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na maafa haya, yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo, aliwasihi Watanzania kuwa na subira na kuacha tabia za kueneza uvumi kwenye vijiwe vya kahawa na kwenye vikao vya kinywaji, kuhusu chanzo cha milipuko hiyo.

“Wakati mwingine watu wanageuza dhana zao kuwa ndiyo ukweli na kupotosha au hata kuwatia watu hofu. Wataalamu wamekwishafika, ukweli wenyewe utajulikana baada ya muda si mrefu,” alisema

Lowassa awataka viongozi waseme ukweli

WAZIRI Mkuu wa zamani Edward Lowassa amewataka viongozi wa Serikali na siasa wajitokeze hadharani na kusema ukweli kuhusu hali mbaya ya uchumi nchini.

Lowassa amesema, hali hiyo kwa sasa lazima iendane na kupanda kwa mishahara kwa wafanyakazi wa umma kote nchini.

Lowassa alizungumzia pia mgogoro wa dini ulioibuka katika mji wa Mto wa Mbu wilayani Monduli mkoani hapa na kuwataka wananchi kutulia kwani suala hilo linashughulikiwa na waendelee na kazi zao bila bughudha.

Mbunge huyo wa Monduli alisema hayo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), muda mfupi alipotua hapo akienda jimboni mwake kuhudhuria mazishi ya Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Magdalena Shoo aliyefariki ghafla juzi nyumbani kwake na anatarajia kuzikwa kesho mjini Moshi.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa hali iliyopo sasa ya uchumi kuyumba nchini ni hali iliyopo kote duniani, hivyo viongozi wa Serikali na siasa wanapaswa kujitoa hadharani kwa kusema ukweli bila ya woga.

Alisema bei ya nafaka katika soko la dunia imepanda kwa asilimia kubwa na pia mafuta yatapanda vivyo hivyo, “hivyo basi viongozi hatuna budi kupandisha mishahara ya wafanyakazi kutokana na hali iliyopo kuliko kuwalipa mishahara ya zamani ambayo haikidhi mahitaji kwa asilimia kubwa.”

Alisema, itakuwa sio jambo la busara kuona hali ya maisha inazidi kuwa mbaya na ngumu, lakini mishahara ibaki pale pale akiongeza kuwa “hapo hatutawatendea haki wafanyakazi na malalamiko yataendelea kote nchini wakati sababu za msingi zipo.”

Alisema kuacha kupandisha mishahara kwa sasa ni suala lisilowezekana na kiongozi yeyote awe wa Serikali na wa siasa atayepingana na hilo, anapaswa kuwa na takwimu za ukweli kwani hali hiyo iko kote duniani.

Alishauri kuundwa kwa tume huru juu ya kutafuta namna gani mishahara itapandishwa na tume hiyo inapaswa kuundwa kwa kushirikisha wataalamu waliobobea wa uchumi, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na Serikali kwa ujumla.

Alisema tume hiyo pia itaangalia vyanzo vyote vya mapato vya Serikali ikiwa ni njia mojawapo ya kutaka kupanga mshahara wa dhati wa mfanyakazi kwa hali iliyopo kwa sasa ya uchumi.

“Tujitoe na kusema ukweli juu ya hali mbaya ya kupanda kwa maisha iliyopo sasa na dawa ya hiyo kwa sasa ni kupandishwa kwa mishahara tu ili twende na hali vinginevyo tunajidanganya na hilo linaweza kuwa na athari hapo baadaye,” alisema Lowassa ambaye katika Mkutano wa Pili wa Bunge la 10 uliomalizika hivi karibuni, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Akizungumzia ugomvi wa kidini katika mji wa Mto wa Mbu, alisema amesikitishwa na hali iliyojitokeza na kuwataka wananchi kutulia na kutafakari kwa kina ni shetani gani amewafikia na kuchukua hatua hiyo.

Aliahidi kwenda kukutana na wazee wa mji huo na kukaa nao ili kutatua suala hilo ili lisijirudie kwani waumini kupigana na kufikia hatua ya kutoana damu ni hatari kwa sababu Watanzania hawana tabia hiyo.

Alisema mji wa Mto wa Mbu wenye makabila zaidi ya 120, ni mji wa kitalii hivyo amani inapaswa kuwepo kwa asilimia 100, hivyo aliwataka wananchi hao kutulia na kuendelea kufanya kazi zao.