Friday, December 18, 2009

Mtandao wamuweka Kikwete njia panda

-Lowassa, Sitta, Rostam, Membe watajwa
-Yeye ajipanga kuwatumia vijana kujihami

WAKATI Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikisubiri matokeo ya kamati teule ya rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, habari zinasema kwamba Rais Jakaya Kikwete anajipanga kuingia katika uchaguzi wa mwakani bila ya mtandao 'uliomsaidia' mwaka 2005 kwa vile amegundua unaweza kumponza.

Hiyo inafuatia mtafaruku ndani ya CCM unaoelezwa unachochewa zaidi na Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba kwa upande mmoja, mivutano ya makundi ndani ya mtandao wa 2005 na mfumo wa Rais wa kuchelea kuwaudhi baadhi ya watu, Raia Mwema imeambiwa.

Ingawa kila mara CCM kimedai kwamba hakina makundi, hali halisi inaonyesha kwamba chama hicho kimegawanyika katika makundi zaidi ya matatu, likiwamo kundi linaloongozwa na Rais Kikwete mwenyewe, na mengine yakiwa na wafuasi mchanganyiko.

Kwa mujibu wa habari hizo, sasa Rais Kikwete anachelea kushirikiana na mtandao wa mwaka 2005 lakini pia hataki kulibana sana kundi hilo ambalo kimsingi lilidandia katika mgongo wa umaarufu wake likiweka mazingira ya kuwa ndilo lililomwingiza madarakani, lililojumuisha wanasiasa kama Edward Lowassa, Samuel Sitta, Rostam Aziz, Bernard Membe na Makamba.

Kundi hilo sasa si la watu wamoja tena, miongoni mwao baadhi wamekuwa mahasimu wakubwa na baadhi wamefikia hatua hata ya kufikiria kumpinga Rais Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani, hata kama hadharani hawathibitishi hivyo.

Mbali ya kundi hilo maarufu la mtandao kumeguka na kuwapo mitandao mipya, kundi la wazee wastaafu nalo limeanza kujitokeza kuikosoa Serikali na CCM baada ya kuelezwa kwamba limekwama kutoa mchango wake katika mustakabali wa Taifa kupitia njia za vikao na ushauri.

Taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya watendaji wa karibu na Rais zinaeleza kuwa, hakuna uwezekano wowote kwa Rais Kikwete kubwaga manyanga katika Uchaguzi Mkuu mwakani na ameanza harakati za kujihakikishia kurejea Ikulu, akikwepa rekodi ya kuwa Rais aliyekaa madarakani muda mfupi kuliko masharti ya Katiba.

Katiba inatamka Rais kukaa madarakani kwa miaka 10, lakini akiwa amechaguliwa kwa kura kila baada ya miaka mitano. Ni Mwalimu Julius Nyerere pekee aliyekaa madarakani kwa miaka zaidi ya 20 na baadaye kung’atuka kwa hiari yake.

Taarifa za kiintelijensia zinaeleza kwamba tayari Kikwete amekwisha kuanza kufanya mikakati ya chini kwa chini ikiwa ni pamoja na kuandaa makundi ya vijana ambao wameanza kuahidiwa nafasi kadhaa za kisiasa na kiutendaji baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 kama njia ya kuwafanya wawe watiifu kwake.

Hata hivyo, habari hizo zinaelezwa kupokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wanachama wa CCM, huku baadhi ya vigogo wakibaini uwezekano mdogo wa Kikwete kung’oka si kutokana na kumudu kazi zake barabara bali kutokana na nguvu za madaraka, akiwa Rais na wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM.

“Tunadhani anayo nafasi ya kurudi na hata kama atajitokeza mtu kumpinga, kikubwa ni kwamba watagawana kura za wanachama wa CCM, hawezi kuzipata zote. Hali inaweza kuwa ngumu kama atatokea mtu mwenye maono mapya, akaweza kuwaeleza wana-CCM kwa nini anataka kumpinga Rais,” alieleza mmoja wa viongozi waandamizi serikalini kwa sasa na mwanachama wa muda mrefu wa CCM.

Kiongozi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, anaamini kuwa ripoti ya Kamati ya Mzee Mwinyi ndiyo inayoweza kumjenga Rais Kikwete au kumuharibia mbele ya wana-CCM wenye ushawishi mkubwa katika chama hicho na zaidi itategemea na jinsi uongozi wa juu utakavyoingilia kati maandalizi ya ripoti hiyo kabla ya kutolewa kwake hadharani.

“Kama itaonekana hakuna tija yoyote kutokana na kamati ya Mwinyi na bado, Rais kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa CCM akaonekana kutoeleweka anachokifanya katika kuongoza chama kama taasisi imara kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani, nafasi yake itazidi kuwa finyu,” alisema lakini alipoulizwa na gazeti hili ni kwa nini amzungumzie Kikwete pekee wakati chama kinaongozwa kwa uamuzi wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, alijibu;

“Unajua pamoja na chama kutoa uamuzi wa baadhi ya masuala kupitia vikao vyake bado, Mwenyekiti anayo nafasi kubwa ya kushawishi mwelekeo wa chama. Kwa mfano, tumewahi kutoa matamko ya makundi kufutwa katika chama lakini yamekuwapo kwa muda mrefu, je, Mwenyekiti anaonyesha interest gani? Vitendo vya viongozi wenzake kwenye chama hasa sekretariati wanatenda kwa mtazamo huo au nao wanachochea makundi?

“Kwa hiyo katika utekelezaji wa tamko kama hilo, Mwenyekiti anapimwa kwa kutazama ametumia vipi influence yake kulifanikisha. Inapobainika Mwenyekiti amebaki kimya na wanachama wengi wanaamini influence yake vema maana yake amekwama. Mwenyekiti anapimwa namna anavyojikita kwa dhati katika kuonyesha njia.”

Kigogo huyo ambaye kwa sasa ni miongoni mwa watendaji waandamizi lakini wenye msimamo wa kuenzi Tanzania yenye maadili ya uongozi aliyoiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alikiri kuwapo kwa udhaifu kwa ujumla katika medani ya uongozi nchini na kwamba makundi yameendelea kukuzwa na viongozi wa sasa zaidi.

Wakati hayo yakijitokeza, kumekuwapo na taarifa kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa NEC-CCM kujiandaa kulalamika wazi wazi ndani ya chombo hicho kuhusu mwenendo wa uongozi wa chama chao, ambao wanaamini ni wa kugawa wanachama zaidi kuliko kuwaunganisha, hatua ambayo huenda ikazidisha mpasuko kutokana na staili iliyojitokeza ya viongozi kutopenda kukosolewa.

Inaelezwa kuwa kati ya wanaotarajiwa kuzungumza ni pamoja na watu wenye rekodi makini ya utendaji nchini na ambao kwa kiasi fulani wamekwishaathirika na kauli za viongozi wa sasa wa CCM walioko madarakani.

Miezi michache iliyopita picha halisi ya kugawanyika kwa CCM ilijitokeza mjini Dodoma wakati kamati ya Mwinyi inayowashirikisha Pius Msekwa na Abdulrahaman Kinana, ilipowasilikiza wabunge wa CCM.

Wabunge hao walionyesha kuwapo katika kambi mbili kubwa moja ikitaka kurejeshwa kwa misingi ya kuanzishwa kwa CCM, ikiwa ni pamoja na kuwaengua uongozi wanachama wake watuhumiwa wa vitendo vya rushwa, hususan wale ambao wamekwishajiuzulu serikalini.

Kundi jingine ni lile lilijitokeza kutetea watuhumiwa wa ufisadi kwa madai kuwa hawajafikishwa mahakamani, bila kujali kuwa hata serikalini wamejiuzulu uongozi bila kufikishwa mahakamani.

Hata hivyo, karata ya mwisho sasa inabaki mikononi mwa Kikwete ambaye anakifahamu chama vyema kwa kuwa sehemu kubwa ya maisha yake ameitumia humo tena akiwa katika uongozi ngazi za chini.

Wachunguzi wa mambo wanaeleza kwamba dalili za wazi za kumeguka kwa CCM zimezidi kujitokeza kutokana na uongozi wa juu wa chama hicho kuashiria kuimarisha makundi badala ya kuyavunja.

Kauli ya hivi karibuni ya Makamba na baadaye Kikwete kuhusiana na matamko yaliyotolewa kwenye kongamano la Mwalimu Julius Nyerere, ni moja ya ishara mbaya kwa CCM kuelekea 2010, kutokana na viongozi hao kuonyesha wazi kuwa wanalo kundi wanalolisimamia.

Kauli ya Makamba kubeza na hata kuwakashifu viongozi wastaafu na watu mbalimbali waliotoa kauli za kuikosoa CCM na serikali yake, ilichochewa na kauli ya Kikwete kwamba kuna watu wenye chuki binafsi na kwamba anajiandaa kujibu mapigo, kauli ambazo zimeelezwa kwamba hazikustahili kutolewa na viongozi wa ngazi yao.

Kikwete alikwenda mbali zaidi kwa kutoa takwimu zilizoonyesha kuwakejeli zaidi ya nusu ya wapiga kura kwa kusema kuonyesha kwamba “asilimia 70 ya Watanzania hufuata upepo” huku akisema asilimia 15 ni watu wanaompinga akibakiwa na asilimia 15 tu ya wanaomuunga mkono kwa dhati.

Tathmini hiyo ya Kikwete imezidi kuwachanganya watu baadhi wakisema kwamba imedhihirisha kwamba inawezekana ameanza kuingiwa na wasiwasi badala ya kujifunza na kuchukua hatua kwa kuzingatia maoni na ukosoaji unaotolewa.

Wasomi wa kada mbalimbali wamekwisha kuwahi kutoa maoni yao kwamba hali tete ya uongozi nchini na hasa katika CCM, imechangiwa na Rais Kikwete kutokuyapatia ufumbuzi masuala nyeti ya kitaifa na chama chake kwa wakati.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Ezavel Lwaitama, amewahi kukaririwa na gazeti moja nchini akisema, hatma ya malumbano au mpasuko unaoendelea kujitokeza ndani ya CCM utategemeana Rais ataegemea katika kundi lipi kati ya mawili yaliyopo hivi sasa ndani ya chama hicho.

Makundi hayo mawili ambayo yamekwishaigawa hata serikali, likiwamo Baraza la Mawaziri ni kati ya linalojinadi kupinga ufisadi na jingine likiwa upande wa utetezi likiundwa na majeruhi wa ufisadi.

Kundi linalopinga ufisadi linaundwa na Sitta na wabunge kadhaa, kama Dk. Harrison Mwakyembe, Anne Kilango-Malecela, Christopher ole Sendeka, Fred Mpendazoe, Stella Manyanya, Saidi Mkumba na wengine ambao wamekuwa wakiunga mkono chini kwa chini.

Kundi hili limekuwa na nguvu kubwa mno bungeni kiasi cha kulijengea picha nzuri mbele ya umma, lakini likionekana kuzidiwa nguvu ndani ya CCM, ambako kundi pinzani limejikita, likiongozwa na wabunge, Rostam Aziz na Lowassa, ambao ni wajumbe wa NEC.

Nguvu za kundi hili la Rostam na Lowassa limejiimarisha kuanzia katika sekretariati ya chama hicho, linakoungwa mkono dhahiri na Makamba kama ilivyojitokeza wakati wa mgogoro wa mkataba wa ujenzi wa jengo la eneo la Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM, Dar es Salaam.

Katika sakata hilo, Makamba alitetea wahusika waliotuhumiwa na kada Nape Nnauye ambaye ni mjumbe wa NEC lakini ambaye anatajwa yu katika kundi la Sitta, ambalo pia linahusishwa na vigogo wengine wa CCM, akiwamo John Malecela.

Wengine wanaotajwa kuwamo kwenye kundi la Rostam na Lowassa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake-CCM (UWT), Sophia Simba, Andrew Chenge, ambaye ni mjumbe katika kamati ya maadili ya CCM na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba.

Kuhusu makundi hayo, kwenye maoni yake hayo, Dk. Lwaitama aliweka bayana kuwa kwa sasa CCM inakabiliwa na tatizo kubwa la uadilifu kwa viongozi wake, hali aliyoitaja kuwa ndiyo chanzo cha kuibuka makundi hayo mawili.

“Mustakabali wa Taifa pamoja na urais wa Kikwete katika uchaguzi ujao wa mwaka 2010 utategemeana atajiunga na kundi gani kati ya haya mawili,” alikaririwa akisema Dk Lwaitama na kuongeza; “Haya yote yanayotokea kwa sababu ya kutokuwapo kwa maadili ya uadilifu ndani ya viongozi wetu na hasa wa CCM.

“Haya mambo yanaweza kwisha tu endapo Rais Kikwete atakuwa na ujasiri wa kupigania kurudi kwa misingi ya chama cha TANU ambayo ilikataza kabisa rushwa kuwa ni adui wa haki na kutekeleza kauli hiyo kwa vitendo.”

Source:www.raiamwema.co.tz

Ulaji wa vigogo BoT wahojiwa

MWELEKEO wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kusaidia taifa kuondokana na hatari ya kuzidi kutanuka kwa pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho nchini umeanza kutia shaka, malalamiko yakianza kuibuka miongoni mwa wafanyakazi wake wa ngazi za chini, baada ya menejimenti hiyo kuamua kuongeza kiwango cha mikopo kwa watumishi wake katika hali inayozua maswali zaidi.

Malalamiko ya baadhi ya wafanyakazi wa chini BoT kuhusu kuwapo kwa tofauti kubwa ya kipato kati yao na wakurugenzi, yanaungana na hadhari iliyowahi kutolewa na baadhi ya viongozi wastaafu nchini kuhusu taasisi za serikali kushiriki kutanua pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Menejimenti ya BoT, Desemba 2, mwaka huu imetoa taarifa kwa wafanyakazi wake inayoeleza kuongezeka maradufu kwa viwango vya mikopo katika hali inayotafsiriwa na wafanyakazi wadogo kuwa, inalenga kuwanufaisha zaidi vigogo wa chombo hicho nyeti nchini.

Tofauti hiyo inajitokeza kwenye viwango vya utoaji mikopo, ambapo wakurugenzi, wakurugenzi washiriki, watalaamu washauri waandamizi watakopeshwa Sh milioni 100 ikiwa ni mikopo ya nyumba wakati makarani, madereva, walinzi na wahudumu wa ofisi, zahanati na jikoni wakipewa haki ya kukopa kiasi kisichozidi Sh milioni 30, hali inayozusha malalamiko ya chini chini.

Uchunguzi wa Raia Mwema kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu umebaini kuwa licha ya BoT kuwa na jukumu zito kitaifa la kuisaidia Serikali kupunguza pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho, pia uamuzi wa menejimenti ya benki hiyo umeanza kukabiliwa na malalamiko miongoni mwa wafanyakazi wa ngazi za chini.

“Tulidhani utoaji mikopo utazingatia kupunguza pengo lililopo la kipato miongoni mwa wafanyakazi na kwamba wale ambao mishahara yao midogo wapewe mkopo wa muda mrefu zaidi lakini kwa kiwango kikubwa, mambo yamekuwa kinyume.

“Kiwango cha mikopo muhimu kama ya makazi kimeongezwa mara mbili lakini wale wa juu wamebaki pale pale na wa ngazi ya chini wamebaki chini zaidi, mfano huu unawasilisha hali halisi ya utendaji serikalini, wakubwa wanapata zaidi wakati wadogo wanazidi kubaki chini,” alisema mfanyakazi mmoja wa BoT, katika ngazi ya ofisa mwandamizi (professional I).

Juhudi za Raia Mwema kumpata Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, hazikuzaa matunda, baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa na majibu.

Kumekuwapo na kilio cha muda mrefu kutoka si tu kwa viongozi wastaafu bali hata wanaharakati kuwa pengo la kipato nchini limekuwa likizidi kutanuka na kuibua matabaka yasiyo ya lazima. Moja ya taasisi zilizoko mstari wa mbele kukosoa mwenendo mbovu wa kusimamia mgawanyo sahihi wa rasimali za nchi ni taasisi ya Policy Forum.

Taasisi hiyo imewahi kutoa ripoti inayoeleza namna Tanzania ilivyofanya vibaya ukilinganisha na nchi zingine katika kupunguza umaskini.

Kwa mujibu wa Policy Forum, kwa kulinganishwa na nchi zilizoko kwenye kiwango chake cha uchumi, nchi hizo zimetekeleza vizuri sera za kupunguza umasikini ambazo zimekuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwenye ukanda wa Afrika.

Kati ya nchi zilizoingia kwenye rekodi hiyo ni pamoja na Ghana, Uganda na Asia hususan nchi za Vietnam na India.

Inaelezwa kuwa wakati Tanzania idadi ya watu masikini ilipungua kwa asilimia 2.4 kati ya mwaka 1991 na 2007, kwa Uganda, Ghana na Vietnam ilipungua karibu mara 10 zaidi, ikiwa kwa wastani wa asilimia 23 hadi 24. India nayo ilifanikiwa kupunguza idadi hiyo kwa kiasi kikubwa takriban asilimia saba kwa kipindi kifupi mno.

Inaelezwa kuwa uchumi wa soko huria Tanzania, kwa sasa umeshindwa katika kupunguza umasikini wa kipato kwa Watanzania wengi, ingawa pia tahadhari ikiwekwa kutambua mafanikio katika nyanja nyingine kama watoto masikini kujiunga shuleni, lakini inaonyesha kuwa kwa Watanzania wengi uwezo wa kujikimu wao wenyewe haujabadilika.

Hali hiyo yote inahusishwa na kuongezeka kwa pengo kati ya masikini na matajiri nchini. Moja ya vyombo vya umma vinavyopaswa kutafakari na kuwa mfano bora katika kuweka mwelekeo wa uchumi unaomkumbuka zaidi masikini ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi.

Mwishoni mwa wiki Raia Mwema, lilipata nakala ya waraka wa kuongezwa kwa viwango vya mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi wa BoT, makao makuu na katika matawi yake kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Zanzibar na katika Chuo cha benki hiyo, jijini Mwanza.

Katika taarifa hiyo, wafanyakazi wa daraja la chini wanakopeshwa Sh milioni 30 kutoka milioni 15 za awali kwa ajili ya mikopo ya nyumba lakini kinachozua hisia za malalamiko ni kwa wakurugenzi kupata donge nono zaidi la Sh milioni 100, kwa kisingizio cha uwezo wa kulipa unaojengewa hoja na kuwa na mishahara minono, ambayo hata hivyo imepangwa na vigogo serikalini.

Mameneja na wataalamu washauri watapata mkopo wa milioni 90, wakati daraja la tatu linawagusa meneja wasaidizi na maofisa wakuu waandamizi wanakopeshwa Sh milioni 70.

Kundi jingine la nne linawahusisha maofisa wakuu (professional I) na maofisa wakuu waandamizi (professional II), wakikopeshwa Sh milioni 60, huku wafanyakazi wenye vyeo vya maofisa waandamizi (professional I) na maofisa wakuu (professional II) watapata mkopo wa Sh milioni 55.

Daraja la sita ni maofisa ngazi ya III-I (professional I), maofisa waandamizi (professinal II) na maofisa- makarani wakuu (cleric officers) watakaoambulia Sh milioni 45.

Maofisa-makarani kuanzia ngazi ya III hadi ngazi ya maofisa-makarani waandamizi (cleric officers), makarani waandamizi na makarani wakuu (clerks) wamepangiwa mkopo wa Sh milioni 40.

Kundi la nane ni ambalo ni la chini ni walinzi, wapishi, madereva, wahudumu wa ofisi na wa zahanati na makarani ngazi ya daraja la III-I ambao watakopeshwa Sh milioni 30.

Hata hivyo, licha ya uamuzi huo kutajwa kuwafurahisha baadhi ya wafanyakazi lakini umezidi kuzua maswali zaidi kwa kuwa msingi wa kutoa mikopo imekuwa ikitokana na kiwango cha mishahara, ambacho hata hivyo ni kikubwa kwa wakurugenzi ikilinganishwa na wafanyakazi wa chini.

Hoja zinazotolewa na baadhi ya wanaoona hatari ya kuzidi kutanuka kwa pengo la wenye nacho na wasio nacho nchini na hususan mfano mbaya ukianzia BoT ni kuwapo kwa pengo kubwa la mishahara, ambalo ndiyo msingi wa pengo kubwa la mikopo.

Uchunguzi zaidi wa Raia Mwema umebaini kuwa hali hiyo ya kuwapo kwa pengo kubwa la mishahara miongoni mwa wafanyakazi wa serikalini nchini kumezidi kukandamiza kimaendeleo wafanyakazi wa kawaida, na kwa kiasi kikubwa kuchangia mmomonyoko wa maadili, na wakati mwingine taarifa nyeti za serikali zikiwafikia matajiri wachache wanaozitumia kwa manufaa yao wakizinunua kutoka kwa wafanyakazi wenye njaa.

Thursday, December 17, 2009

RAIS ANA MAMLAKA KISHERIA

Siku moja baada ya Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe kusema Rais Jakaya Kikwete hawezi kutumia mamlaka yake kuwabana mafisadi, baadhi ya wanasheria nchini, akiwamo Profesa Issa Shivji, wamepinga kauli hiyo kwa kusema sio kweli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam wanasheria hao walisema rais anaweza kuwabana mafisadi kwa kutumia mamlaka yake ndani ya chama na serikali.

Profesa Issa Shivji alisema Rais Kikwete anaweza kupambana na watuhumiwa wa ufisadi kwa kuwavua madaraka walionayo katika chama au serikali.

Gwiji hilo la Sheria na Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, alisema kama watuhumiwa watakuwa watumishi wa serikali au watendaji katika mashirika ya umma, rais anaweza kuwawajibisha kwa kutumia sheria na kanuni za utumishi wa umma.

Kumwajibisha mtuhumiwa sio iwe kumpeleka mahakamani, unaweza kuchukua hatua za awali ikiwemo kumvua nyadhifa zote. Kama ni mwanasiasa au mtumishi katika serikali na mashirika ya umma, unaweza kumwajibisha kwa mujibu wa sheria za umma," alisema Profesa Shivji.

Alisisitiza kusema Rais Kikwete hana uwezo wa kuwabana mafisadi sio kweli na watanzania wanatakiwa kuelewa hivyo kwamba rais anaweza.

Kauli ya Profesa Shivji iliungwa mkono na Profesa Abdallah Safari, aliyetia ngumu akisema sheria za nchi ikiwemo ya utawala, inampa uwezo na mamlaka rais kupambana na vitendo vya ufisadi ndani ya serikali yake na hata katika chama chake.

GAVANA AONGEA KUHUSU MIKOPO BOT

Uongozi wa Benki Kuu (BoT), umetetea mikopo ya mamilioni ya watumishi wake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ukisema mpango huo, unalenga kuwajengea maisha bora watumishi hao.

Kauli hiyo, inakuja kufuatia kuwepo kwa waraka wa baraza la mikopo la nyumba, ambalo limetaja viwango vya mikopo kwa madaraja tofauti katika matawi yake yote ya Mwanza, Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mbeya.

Waraka huo, unaonyesha kila mfanyakazi ataweza kukopa kati ya Sh 100milioni ikiwa ni kiwango cha juu na Sh 30 milioni kiwango cha chini kulingana na wadhifa wa mtumishi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

Akizungumzia waraka huo, Gavana wa BoT Profesa Benno Ndulu, alisema ni utaratibu ambao benki imejiwekea ili kuwawezesha wafanyakazi wake kimaisha.

Profesa Ndulu, alisema BoT, ilijiwekea utaratibu huo baada ya kuangalia mahitaji ya msingi ya makazi kwa watumishi wake.

"Ni utaratibu ambao upo kwa karibu miaka 20 sasa, lakini sasa tumeuboresha kwa kuangalia mahitaji ya mikopo kwa umakini," alifafanua Gavana Ndulu.

Profesa Ndulu ambaye amekuwa katika mchakato wa kuisafisha taasisi hiyo ya fedha, aliweka bayana kwamba mikopo hiyo, imekuwa ikitolewa kwa umakini ili kuhakikisha inarejeshwa.

Alisisitiza kabla benki hiyo, haijatoa mikopo, inatafuta taarifa za wahusika ili kubaini kama wana madeni ndani na nje ya benki hiyo.

Wednesday, December 16, 2009

GTI Waendesha Mafunzo ya Ujenzi wa Vuguvugu la Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi Ngazi ya Jamii Katika Wilaya za Mbeya Vijijini.

Gender Training Insitute –GTI- wafanya mafunzo ya siku tatu juu ya Ujenzi wa Vuguvugu la Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi katika ngazi ya jamii katika vitongoji vya wilaya ya Mbeya vijijini. Mafunzo hayo ya siku tatu yalifanyika katika Manispaa ya jiji la Mbeya kuanzia tarehe 3-5 Novemba 2009 katika Ukumbi wa Mkapa Hall, na yalihudhuriwa na washiriki takribani mia moja kutoka katika vikundi zaidi ya 30 kutoka wilaya ya Mbeya vijijini. Mafunzo hayo yaliwezeshwa na dada Dina Nkya, Rehema Mwaiteba, na Anna Sangai.

Pamoja na malengo mengine mafunzo hayo yalikuwa na malengo yafuatayo: Kujenga Uelewa wa pamoja wa vuguvugu la Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi; Kujenga msingi wa uanzishwaji wa semina za GDSS katika ngazi ya jamii; Kueneza itikadi ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi; Kujenga uwezo kwa washiriki kufuatilia bajeti kwa mrengo wa kijinsia; Kuandaa mpango kazi wa pamoja; na Kuendendeleza vuguvugu la Ukombozi wa wanawake kimapinduzi.

Katika mafunzo hayo wawezeshaji walitumia mbinu mbalimbali ili kuweza kufikisha ujumbe kwa washiriki kwa urahisi zaidi, ambapo wawezeshaji waliweza kutumia mbinu za nyimbo, maigizo maafupi, visa mkasa, na michoro ambavyo viliandaliwa na washiriki wenyewe. Pia wawezeshaji walitumia mbinu shirikishi ambayo iliweza kuibua visa mkasa vingi kutoka kwa washiriki wenyewe. Mafunzo yalifundishwa ni pamoja na jenda na jinsia, Teknohama na ujenzi wa vuguvugu la maendeleo, itikadi za ukombozi wa wanawake, na ujenzi wa nguvu za pamoja katika harakati za ukombozi wa wanawake.

Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa GTI ya kuibua vuguvugu la Ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi ya jamii, ambayo yanatarajiwa kufanyika kote nchi nzima hapo mwakani.

Habari zaidi, visa mkasa na picha za mafunzo haya zitaendelea kuchapishwa katika blog hii mapema.

Monday, December 14, 2009

'Masoko ya usiku yanaongeza kasi ya ukimwi'

MKUU wa wilaya ya Kasulu, Zainab Kwikwega, amepiga marafuku
masoko ya usiku wilayani humo yanayodaiwa kuwa chanzo cha ngono.

Inadaiwa kwamba masoko hayo yanachochea maambukizi mapya ya Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU) wilayani humo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Msambara wilayani humo, Kikwega alisema, utafiti wa wataalamu unaonyesha kuwa masoko hayo yamekuwa chanzo kikuu cha ngono zisizo salama zinazochangia maambukizi mapya ya Ukimwi.

Alisema, kuanzia sasa masoko yote yatafanya kazi hadi saa 12:30 jioni na pia vilabu vya pombe za kienyeji vitafungwa muda huo huo.

Kikwega amesema, lengo la kupiga marufuku masoko hayo ya usiku ni kurudisha maadili katika jamii.

Kwikwega alisema, masoko ya usiku na vilabu vya pombe vimesababisha wanajamii wasikae pamoja kujadili mambo yenye manufaa kwa familia hivyo kusababisha mmomonyoko wa maadili.

Makamba hajatulia ! Jaji Warioba

WAZIRI Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais (mstaafu), Jaji Joseph Warioba, amesema matusi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba kwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na washiriki wa kongamano la miaka 10 kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, hayawanyimi usingizi na kwamba, kiongozi huyo ndiye kinara wa kundi la chuki CCM.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hoja zilizojadiliwa kwenye kongamano hilo jijini Dar es Salaam, zinahusu Taifa na si watu binafsi, akitolea mfano, kuporomoka kwa maadili na viashiria vya kusambaratisha umoja wa kitaifa.

“Rais Kikwete akisema nchi inakabiliwa na matatizo ya kuporomoka kwa maadili, ubaguzi, rushwa na ufisadi ni sawa. Salim na Warioba wakisema hayo hayo wanaitwa watu wenye chuki na wivu.

“Waziri Mkuu Pinda akisema kwamba tofauti ya kipato kati ya matabaka ni hatari kwa usalama wa taifa Makamba anaona ni sawa. Lakini maneno hayo hayo yakisemwa na Salim na Warioba wanaonekana ni wehu na wahuni.

“Maneno hayo hayo yamesemwa kwenye makongamano na semina nyingi, bungeni na mahali pengine lakini Mh. Makamba hakuita waandishi wa habari. Lakini yaliposemwa kwenye kongamano la Taasisi ya Mwalimu Nyerere ameita waandishi wa habari na kutukana.

“Makamba alikuwa anawasifu sana viongozi waliopita. Sasa anawalaumu. Hivi Makamba anamsifu kiongozi kutoka moyoni kwake au ni kutekeleza ajenda binafsi. Kumsaidia kiongozi wako siyo lazima kumsifu wakati wote bali pia kutoa ushauri mgumu.”

Alisema Warioba wakati akizungumza na Raia Mwema jijini Dar es Salaam mapema wiki hii.

Ameelezea kushangazwa na Makamba kutoa matusi bila kugusia hoja zilizopo na wala kupata muhtasari wa yaliyojadiliwa kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, George Mkuchika, ambaye alihudhuria kongamano hilo.

Siku chache baada ya kongamano hilo kumalizika, Makamba alizungumza na waandishi wa habari na kuwaita baadhi ya washiriki wehu kutokana na hoja walizotoa na hasa kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua uamuzi mgumu ili kudhibiti mwenendo wa mambo yanaonekana kuwa ya ovyo na akishindwa astaafu.

“Sisi tumesikia matusi aliyotoa Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Makamba, lakini hayatunyimi usingizi. Mheshimiwa Makamba siyo Waziri Mkuu wa Rais Kikwete lakini inaonekana anatumia muda mrefu sana kuzungumzia mambo ya serikali badala ya kujishughulisha na mambo ya chama.

“Kwa muda sasa, kumetokea maneno ya kubeza, kukejeli, matusi kila baadhi yetu tunapozungumzia mambo ya msingi ya kitaifa na hayo yamesemwa kutoka Makao Makuu ya Chama, siyo kutoka serikalini.

“Oktoba (mwaka huu), nyinyi waandishi wa habari mlituhoji mimi na Salim (DK. Salim Ahmed Salim) ili tutoe maoni yetu kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 10 tangu Mwalimu alipotutoka.

“Baada ya kusema tuliyosema alitokea mtu makao makuu ya chama akatutukana. Hakushughulika na hoja tulizotoa, sisi tulizungumzia mambo mawili makubwa.

“Moja, ni kuporomoka kwa maadili katika taifa letu, la pili mmomonyoko kwenye umoja wa taifa lakini tulitukanwa kwamba sisi ni watu tunaomwandama Rais Kikwete.

“Lakini mwezi huo huo, Rais Kikwete akahutubia taifa kutokea Butiama akazungumzia mambo yale tuliyozungumza tena kwa ufasaha zaidi kuonyesha kwamba ni matatizo kwenye nchi.

Alizungumzia kuporomoka kwa maadili, hatari inayooneka kwenye kusambaratika kwa umoja wetu, alizungumzia rushwa akazungumzia ufisadi. Ni yale yale tuliyokuwa tumeyasema na sisi tulifarijika, tukapumua tukaona kumbe Rais wetu anaelewa haya matatizo,” alisema Warioba na kuongeza kuwa:

“Sasa wakati ule tumetukanwa kulikuwa na reaction ya watu mbalimbali baadhi walituambia kwamba yule kijana aliyesema alikuwa ametumwa na Makamba ili atutukane, sisi hatukuamini.

“Kongamano limetambua juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya madini lakini wametoa ushauri namna ya kuboresha zaidi, wametambua juhudi za serikali kuhusu umiliki wa ardhi lakini wamesema juhudi zaidi zinahitajika, wametambua juhudi za serikali katika kuboresha elimu lakini wanasema juhudi zaidi zinahitajika.

“Lakini kubwa zaidi walizungumza sana kuhusu kuporomoka kwa maadili, dalili za kusambaratisha umoja wetu, sasa haya ni mambo ya msingi na kama nilivyosema Rais mwenyewe alikwishayatambua.”

Jaji Warioba alisema hawaoni kosa walilofanya kuzungumzia masuala ya kitaifa kiasi cha kumfanya Makamba atukane na kwamba msimamo wa Makamba ni tofauti na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alitoa mfano kwa kurejea hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumzia hatari ya kuongezeka pengo kati ya masikini na matajiri nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwenya kumbukumbu ya miaka 75 ya Kanisa Anglikana, Dar es Salaam.

“Mgeni rasmi ilikuwa awe Waziri Mkuu lakini kwa bahati mbaya akawa amesafiri kwenda Vienna kwa hiyo akamtuma Waziri Marmo (Philip Marmo) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-(Bunge) kusoma hotuba yake, ilikuwa ni hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa na Waziri Marmo.

Na sehemu ya hotuba hiyo inasema ifuatavyo; “Kama nilivyoeleza Tanzania ina watu wapatao milioni 40. watu hawa wana viwango tofauti vya mapato na hili linaeleweka. Hatuwezi kuwa na mapato sawa.

“Tatizo linakuja pale ambapo tofauti ya kipato inapokuwa kubwa miongoni mwa makundi katika jamii. Lakini tatizo hili linazidi kuwa kubwa pale ambapo tofauti ya kipato inapokuwa kubwa miongoni mwa makundi katika jamii.

“Lakini tatizo hili linazidi kuwa kubwa pale ambapo ukubwa wa tofauti hiyo unapoongezeka. Madhara ya ongezeko hilo mnayafahamu kwani kuna hatari ya matajiri wachache kuendesha maisha ya maskini walio wengi kwa njia ambayo itazidi kuwaongezea utajiri huku ikiwadidimiza zaidi maskini.

“Si ajabu matajiri hao wachache wakawa ndio wanaoendesha vyama vya siasa, Serikali, Mahakama, Bunge, Makanisa, Misikiti n.k. Katika hali hiyo Taifa halina usalama.

“Hivyo hatuna budi kuwa na misingi inayopunguza tofauti kati ya masikini na tajiri. Kama Serikali tunazo njia mbalimbali tunazotumia kupunguza tofauti hiyo. Lakini ninaamini madhehebu ya dini nayo yana jukumu la kufanya.

“Licha ya kuchukua tahadhari yasiendeshwe kwa matakwa ya matajiri hao, wanalo jukumu la kuona na kuhakikisha kuwa vyanzo vya utajiri wa waumini wao ni vya haki na havitokani na mapato haramu au kuvunja amri za Mungu.

“Hivyo, ningependa kuwaomba viongozi wa dini kushirikiana na mihimili yote ya dola ili kupunguza kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya matajiri na maskini kwa kuwa mwisho wake si mwema,” alihitimisha kunukuu hotuba ya Waziri Mkuu na kuendelea kusema:

“Sasa haya maneno hayana tofauti kabisa na yale yaliyozungumzwa katika kongamano. Tulichoona hapa ni kwamba Serikali kama serikali inasikiliza ushauri. Rais amewahi kuyasema na Waziri Mkuu anayasema.

“Na kongamano lilikuwa linaishauri Serikali, kama Serikali haina tatizo na hayo yaliyosema huko, mheshimiwa Makamba ana matatizo gani mpaka atutukane kwamba sisi ni wehu na wahuni.

“Uongozi ni kuonyesha njia, mheshimiwa Makamba ni kiongozi wa ngazi ya juu katika chama ndiye mtendaji mkuu na ukiwa kiongozi mwenye madaraka lazima uchunge lugha yako.

“Rais pamoja na cheo chake anaheshimu sana watu, anatuheshimu sana sisi wazee hatutukani, hatubezi hata pale ambapo tunatofautiana mawazo, Rais anatuheshimu sana nasi tunamheshimu.”

Source:www.raiamwema.co.tz

Thursday, December 10, 2009

Zuma kumvisha nishani Anna Abdallah

MBUNGE wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) ameteuliwa kupokea nishani ya Kitaifa ya Uongozi inayotolewa na Afrika Kusini.

Atakabidhiwa nishani hiyo ijulikanayo kama Order of the Grand Companions of O.R. Tambo, Silver.

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma ndiye atakayemvisha nishani hiyo ya juu nchini humo; kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam.

Ilieleza kuwa barua ya uteuzi inaonesha kwamba hafla ya kutunukiwa tuzo itafanyika kesho katika Ikulu ya Afrika Kusini mjini Pretoria.

Mbunge huyo anaondoka nchini leo kwenda Afrika Kusini kupokea nishani hiyo.

Katika msafara wake, Mbunge huyo aliyewahi kuwa Waziri na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT), atafuatana na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo (CCM) na maofisa wawili wa Bunge, Justina Shauri na Ernest Zulu.

Tafakuri Jadidi!

je, unafikiri katika miaka minne ya utawala wa Rais Kikwete ameweza kukidhi matarajio na yako au kuleta maisha bora kwa mtanzania?

Na pia unazungumziaje kauli mbiu ya kilimo kwanza? Unafikiri itaweza kuinua hali ya maisha ya mkulima mdogo?

J

Monday, December 7, 2009

Magazeti ya udaku na Jinsia

Na Privatus Karugendo

MAGAZETI ya udaku, ama magazeti pendwa kama wenyewe wanavyotaka yaitwe duniani kote, yana sifa mbalimbali, ikiwamo kutangaza uongo na hata umbeya. Pamoja na ukweli kwamba magazeti ya aina hii nchini yanasomwa na wengi, bado tunayadharau na kufikiri kwamba yanasomwa na watu wasiokuwa makini.

Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno udaku kama tabia ya kutafuta na kutaka kujua habari za watu; kilimilimi na umbea. Kuyabatiza magazeti haya kuwa ya udaku ni lengo zima la kutoa ujumbe kwamba haya ni magazeti ya umbea na uzushi.

Je, ni kweli kwamba magazeti haya ni ya umbea na uzushi? Je, watu wengi, na hasa vijana wanapenda kusoma umbea na uzushi? Kila mahali magazeti haya yanauzwa sana. Ukweli ni kwamba magazeti ya udaku yanasomwa sana. Lakini kwa nini watu wapende kusoma umbea na uzushi?

Hoja ninayoijenga katika makala hii si kununuliwa kwa magazeti au kutonunuliwa; bali ni kutaka kumshirikisha msomaji ufunuo nilioupata juu ya magazeti ya udaku. Mimi pia nilikuwa kati ya watu waliokuwa wakiyapiga vita magazeti ya udaku. Nimeandika makala nyingi nikipinga utamaduni wa watu kuacha kusoma vitabu na magazeti makini na kukimbilia magazeti ya udaku. Niliamini kabisa kwamba wale wote wanaoyasoma magazeti ya udaku si watu makini.

Inawezekana kabisa nikawa sijafanikiwa kufahamu vizuri sababu inayowasukuma watu kusoma magazeti ya udaku; na inawezekana pia kwamba wale wanaoyaandika magazeti ya udaku wana malengo na nia tofauti na ile niliyofunuliwa. Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba magazeti ya udaku yanaandika maswala ya jinsia kuliko magazeti tunayoyaita ni makini.

Karibia magazeti yote ya udaku kurasa zake za mbele zinapambwa na masuala ya jinsia. Mifano ya magazeti haya na habari zinayoandika ni mingi. Inahusu wanasiasa kushiriki ngono; mafumanizi, ufusika wa kupindukia na nyingine nyingi. Ingawa hapa ninatoa mfano wa habari katika magazeti machache tu, ukweli ni kwamba karibia magazeti yote ya udaku yanaandika mambo ya jinsia na yaliyo tofauti. Hakuna gazeti linalorudia yale yaliyoandikwa na gazeti jingine. Kila gazeti linajitahidi kuibua kitu kipya. Ukitaka kufahamu hali ya jinsia ilivyo katika taifa letu la Tanzania, soma magazeti ya udaku.

Wanaharakati wa kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi, wanaharakati wa haki za binadamu na wanaharakati wote wanaotetea usawa wa kijinsia, watakubaliana na mimi kwamba niliyoyataja hapo juu ni masuala ya jinsia. Ni nadra sana kuona magazeti makini yakibeba maswala ya jinsia kwenye kurasa za mbele. Ikitokea yakawemo ni katikati na yanapewa nafasi ndogo kinyume na yanavyofanya magazeti ya udaku.

Inawezekana kwamba habari hizo zinakuwa zimehakikiwa na kuchujwa na wamiliki au na hata Serikali. Habari nyingine zinachujwa na viongozi wa dini na zile ambazo ni nyeti zaidi zinafunikwa na kufichwa kabisa hadi Kristo atakaporudi mara ya pili! Kwa njia hii hatuwezi kujisahihisha, kwa njia hii hatuwezi kuendelea. Nchi nyingi zilizoendelea zimeheshimu na kukumbatia usawa wa kijinsia.

Magazeti tunayoyaita makini yanaandika habari za siasa, za wanasiasa na matukio yanayowahusu wanasiasa hasa katika kurasa zile za mbele. Haina maana kwamba haya nayo si muhimu katika jamii. Ila ni kwamba magazeti yale tunayoyaita makini hayazingatii habari za jinsia.

Pia waandishi wa magazeti haya tofauti na ilivyo kwa magazeti ya udaku, hawaitumi kutafuta habari kwenye vyanzo mbali mbali. Mara nyingi wanajikita kwenye vyanzo vya kiserikali; kusubiri pale Maelezo au kusubiri mikutano ya viongozi wakuu na waandishi wa habari. Pia wamejenga utamaduni wa kutafuta habari za matukio mbali mbali kama vile vifo, kupigwa, kubakwa kutoka kwa makamanda wa polisi wa wilaya na mikoa.

Matokeo yake ni kwamba, haya magazeti yetu makini, ukisoma mmoja huna haja ya kusoma jingine. Wakati mwingine unakuta karibia magazeti yote yana habari ile ile kwenye kurasa za mbele.

Hata ukisoma kurasa za ndani unakuta habari zinafanana. Kwa wale wanaosikiliza mapitio ya magazeti kwenye runinga watakubaliana na hoja yangu maana anayeyapitia magazeti akishasoma habari za gazeti linalotangulia, anabaki kusema; “ habari hii imejirudia karibia katika magazeti yote”. Jambo hili linaeleweka vizuri, maana magazeti haya vyanzo vyao vya habari ni vilevile. Hawatafuti habari, wanasubiri kuletewa habari. Wanasubiri kuambiwa ni lipi la kuandika na ni lipi la kuacha. Kwa njia hii wanajikuta wanayaweka maswala ya jinsia pembeni.

Magazeti ya udaku hata yote yakitoka siku mmoja, ni vigumu yawe na habari zinazofanana. Waandishi wao wanatafuta habari. Hawategemei kupata habari kutoka maelezo au kusubiri mikutano ya waandishi wa habari na viongozi au watu maarufu katika taifa letu. Wanaingia ndani ya jamii na kutafuta habari zinazogusa maisha ya watu. Wanaibua mambo mengi ya jinsia. Wanaibua ukatili majumbani, wanaibua vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake na watoto, wanaibua matendo ya udanganyifu katika ndoa, wanaibua rushwa ya ngono, kwa ufupi wanaibua mambo yote yanayokwenda kinyume na maadili.

Ni kiasi gani yale yote yanayoibuliwa na magazeti ya udaku yanafanyiwa kazi ni swali la kujiuliza. Ni kiasi gani yanayoibuliwa yana ukweli pia ni swali la kujiuliza. Je, mashirika ya kutetea haki za binadamu, mashirika ya harakati za kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi ni kiasi gani wanatumia habari za udaku kuimarisha mapambano yao na mfumo dume? Je, na wanaharakati wanayanyanyapaa magazeti ya udaku? Wanayanyanyapaa magazeti yanayoandika na kuibua maswala ya jinsia?

Swali jingine, ambalo nimeligusia mwanzo mwa makala hii ni kiasi gani wamiliki na wahariri wa magazeti ya udaku wanafahamu umuhimu wa habari wanazoziandika? Ni kweli kwamba wanaandika habari hizi kuibua maswala ya kijinsia au imetokea tu bahati mbaya wakati wakiwa kwenye harakati za kutafuta fedha? Au walifanya utafiti na kudungua kwamba vijana wengi wanapenda kusoma habari zinazoelezea mahusiano ya mwanamke na mwanaume? Habari za mapenzi, habari za ngono na mambo yote yanayofanana na hayo? Vijana ni wengi – hivyo soko ni kubwa?

Je, wanaadika kuuza magazeti yao? Ili wapate fedha na kuwa matajiri? Kuwa matajiri kuisaidia jamii au kuwa matajiri kwa faida yao na familia zao? Au wanaandika kufundisha jamii? Wanaandika kuibua maswala ya jinsia kwa lengo la kusambaratisha mfumo dume ili kuleta usawa wa kijinsia? Wanaandika kwa vile wao ni wanaharakati? Au nao pamoja na kuandika majumbani kwao wanaendeleza mfumo dume?

Kuna haja ya kuyaangalia magazeti ya udaku kwa mtizamo mpya! Hata kama wanaoyaandaa wana malengo mengine, lakini yale wanayoyaibua kuna haja ya kuyafuatilia; kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii tunaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu na kuzingatia usawa wa jinsia.

Wakiandika juu ya fumanizi, tukio hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya ukatili majumbani, kwa vile wanatoa majina ya watu na wakati mwingine maeneo ya tukio, ni vyema matuko haya yafuatiliwe kwa karibu. Wakiandika juu ya rushwa ya ngono, jambo hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya wabunge wetu kuwa na nyumba ndogo kule Dodoma, kuwasafirisha watoto wadogo hadi Dodoma ili kufanya nao vitendo vya ngono , jambo hili lifuatiliwe ili waheshimiwa wetu wawajibishwe na kusaidiwa kuyabadilisha maisha yao.

Wakiandika juu ya waheshimiwa wabunge kununua dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wingi wakati wa vikao vya Bunge, jambo hili lifuatiliwe – kwa nini wabunge wetu wahitaji nguvu za ziada kufanya tendo la ngono wakati wako mbali na familia zao? Bungeni wanahitaji nguvu za kufanya ngono au nguvu za kufikiri na kufanya kazi? Lolote litakalo andikwa na udaku lifuatiliwe, hsasa kama linaibua habari za jinsia.



Simu:
0754 633122

Mwalimu Nyerere wamlipua Kikwete

-Siri za uteuzi wa mgombea urais CCM zaanikwa
-Butiku asema wafanyabiashara wamembana Rais
-Kilaini asema nchi 'inatembea bila nguo'

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ambacho hivi karibuni kupitia Halmashauri Kuu (NEC) yake kiliunda kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, kutafuta suluhu ya mpasuko miongoni mwa wabunge wake, kimeongezewa ukurasa mpya kwa kutangazwa kwa siri za kikao cha Halmashauri kuu (NEC) cha mwaka 1995, kilichopitisha wagombea watatu wa urais.

Siri hiyo ilitangazwa juzi Jumatatu, kwenye kongamano la Miaka 10 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam lililowashirikisha viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na baadhi ya wahadhiri waliotoa kauli kali ambazo zinamgusa moja kwa moja Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, aliyeanza mbio za urais mwaka 1995.

Kwa mujibu wa siri za kikao hicho (NEC-CCM) kilichopitisha majina ya Benjamin Mkapa, Cleopa Msuya na Kikwete ili mmojawapo achaguliwe kuwa mgombea urais wa chama hicho, Mwenyekiti wa kikao, wakati huo Rais Ali Hassan Mwinyi, alizidiwa nguvu kikaoni, akazomewa katika kitendo cha utovu wa maadili kwa baadhi ya wajumbe ambao inadaiwa walikuwa wamehongwa fedha.

Kutokana na Mwinyi kuzidiwa kikaoni baada ya kuibuka zogo wakati akielezea sababu za baadhi ya wagombea kukatwa majina yao, Mwalimu Julius Nyerere alilazimika kuingilia kati, akitoa vitisho dhidi ya waliokuwa na jazba zinazodaiwa kuchochewa na kuhongwa fedha na kuwapo kwa mtandao mahsusi wa vijana.

Siri hizi zilivujishwa Jumatatu na aliyekuwa mjumbe katika NEC hiyo, Joseph Butiku, ambaye sasa ameweka bayana kuwa tatizo la msingi CCM na serikalini ni mtandao ambao amedai umekuwa pingamizi kwa baadhi ya viongozi waadilifu kupewa madaraka.

“Mwaka 1995 wakati wa uchaguzi Nyerere hakuwa Rais wala Mwenyekiti wa CCM, alikuwa ni Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi). Mtandao umeanzia pale, wengi waliokuwamo serikalini sasa ni sehemu ya mtandao. Wakati ule, niliwafuata wana-CCM wawili mmoja mgombea na mwingine mgawa fedha.

“Nilimfuata huyu mgawa fedha nikamuuliza akakataa kukiri lakini nikamwambia hizi fedha unazogawa kwa nini usiwawezeshe tu vijana kwenye miradi yao na badala yake mnazitumia kupata uongozi…hakuwa na jibu na hadi leo ananikwepa. Mwenzake alikuwa mgombea urais.

“Huyu nilimfuata nikamwambia wenzako wanataka uwe rais lakini tatizo lako unafukuzana sana na mali. Akasema kweli. Alikuwa na fedha nyingi zilizobainika ni kutoka nchi moja. Nikamuuliza hizi fedha zako umemwambia Waziri Mkuu (alikuwa David Msuya). Akasema sikumwambia. Nikamweleza kamwambie na ikibidi uzirejeshe…sijui kama alifanya hivyo.

“Sasa kikaja kikao cha NEC; Rais Mwinyi ndiye anaongoza kikao akiwa Mwenyekiti wa CCM. Akaanza kutaja majina fulani yamekatwa, alitajwa mtu fulani nusu ya kikao wakakataa, wakaanza kuimba jina fulani, kama genge hivi. Mwalimu Nyerere ambaye alialikwa kwenye kikao hicho akaomba kuzungumza.

“Alipokubaliwa akaanza kwa kuuliza maswali matatu kutokana na zogo hilo, kwanza akauliza, ninyi ni wahuni au viongozi? Pili, je, hivi ndivyo mnavyochagua Rais? Tatu, Watanzania kama wangewaona, je, wangeamini kuwa ninyi ni viongozi wao?

“Baada ya maswali hayo, ndipo hali ikatulia. Ilifikia hatua ikawa ni uchaguzi kati ya uchafu unaoshabikiwa na wema, akaonya kama ni hivyo (wanashikilia msimamo) twendeni kwa wananchi. Ninyi piteni huko, nasi tupite huku tuone,” alifichua Butiku huku akipewa ishara na viongozi wenzake wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Dk. Salim Ahmed Salim na Jaji Warioba pamoja na Brigedia Jenerali mstaafu Hashim Mbita, kuacha kuyarejea matukio hayo bila mafanikio.

“Mniache niseme. Maana huu ndio wakati wake. Siwezi kukaa nayo moyoni na kufa nayo haya,” alisema Butiku na kuendelea; “Sasa haya yaliyojengwa yameanza kuibuka hadharani, Umoja wa Vijana CCM wanagombea majengo (mkataba wa kinyonyaji wa ujenzi, eneo la makao makuu UVCCM Dar es Salaam).

“Nyerere aliacha nchi ikiwa moja. Leo imekuwa nchi ya vipande. Nasema hatuwezi kuishi ndani ya takataka kwa muda mrefu. Wengine wakisema wanafukuzwa kazi. Wengine wanaambiwa walitaka urais. Mtandao katika CCM uondolewe. Mliuleta wenyewe. Mkauondoe, hasa vijana, hamna mzee humo labda Kikwete.

“Mtandao unasema fulani asipate kazi, cheo. Salim (Dk. Salim Ahmed Salim) wewe uko NEC mkaondoe mtandao. Mkishindwa kuuondoa ili sisi tuwe na uhakika wa maisha ya wajukuu zetu, tutavaa migolole na mikwaju mje mtuondoe barabarani.

“Tujitambue kwanza sisi ni Watanzania. Haya makundi…mitandao haina maana. Msaidieni Rais (wanamtandao) acheni majungu. Wezi waliomzunguka kama wapo msaidieni awaondoe. Hatuwezi kuwa na Rais compromised, tutamsaidia kuondokana na majungu. Hatukumchagua Rais awe mtumwa wa wafanyabiashara, wafanyabiashara wamemfanya Rais mtumwa,” alisema Butiku.

Katika mjadala huo, kutokana na wazungumzaji wengi kuonyesha hatari inayozidi kulikabili taifa kwa kutokuwa na miiko ya uongozi, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki Dar es Salaam, Methodius Kilaini, alisema; “Nashukuru kama Taifa tumeanza kutambua kuwa tunatembea bila nguo.” Akimaanisha udhaifu umeanza kuzungumzwa wazi na kutafutiwa ufumbuzi na Watanzania wenyewe.

“Tumeanza kutambua tunatembea bila nguo, mwanzo ilikuwa vigumu kuambiana. Tulikuwa tunatembea bila nguo lakini hatuambiani…vijana endeleeni kupiga kelele (dhidi ya rushwa, ufisadi na dhuluma) zitasikika kuliko hata wazee.

“Nashukuru kusikia mapendekezo ya kurejeshwa Azimio la Arusha hata kama likiwa limekarabatiwa…hatuwezi kubaki kutokuwa na chombo kinachotoa mwongozo kwa viongozi. Siku hizi watu wenye maadili mabovu wanakuwa viongozi na wanaendeleza uchafu wao huo.

“Nyerere alikuwa pia na viongozi wasio na maadili lakini alijaribu kuwarekebisha japokuwa si wote walirekebishika. Alikuwa na wanafunzi wake kwenye uongozi ingawa wengine wamekuwa wanafunzi wabaya.

“Siku hizi, unakuwa na viongozi wabovu serikalini, ukijaribu kuwarekebisha hata hawarekebishiki. Kama fisadi anaingia na ufisadi wake kwenye uongozi basi anauendeleza,” alisema Askofu Kilaini, ambaye mantiki kwenye kauli zake hizo zilidhihirika kuzidisha utulivu wa washiriki kumsikiliza kwa makini zaidi, na kuongeza kuwa; “Tanzania ya leo ndiyo nchi pekee mtu anaingia kama mwekezaji akiwa na dola moja lakini anaondoka na dola milioni moja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CCM mstaafu, Philip Mangula alishauri Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuanza kutoa mafunzo kwa viongozi kama ilivyo nchini China ambako viongozi wanaoteuliwa au kuchaguliwa hupewa mafunzo ya miezi mitatu ili kujua wajibu wao kwa umma, akisema hiyo ndiyo sehemu muafaka ya kupokezana kile alichoita ‘vijiti.’

Rose-Mary Nyerere mtoto wa Mwalimu Nyerere na aliyewahi kuwa Mbunge alionyeshwa kukerwa na msamiati aliouita wa sasa hivi wa upendeleo kwa tiketi aliyoiita kuwa ni “watoto wa wakubwa” akisema wao walishiriki kukata kuni Jeshi la Kujenga Taifa na shughuli nyingine ngumu akitolea mfano licha ya kuwa na kilo 47 kwa wakati huo, aliweza kubeba mzigo wa kilo 57 akiwa JKT.

Naye, Mwanasheria mahiri Tundu Lisu alisema viongozi wengi wanashindwa kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kipengele cha ujasiri, akitoa mifano maeneo ambayo Nyerere alionyesha ujasiri ambayo ni kumkosoa wazi wazi Rais aliyeko madarakani, kumwita Waziri Mkuu aliyeko madarakani muhuni, kupingana na wakoloni kiasi cha kufunguliwa kesi ya uchochezi.

“Siku hizi viongozi wanaogopa gharama za ujasiri tofauti na ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere,” alisema Lisu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya bia Tanzania (TBL) Arnold Kileo alisema: “ CCM imekosa maadili kiasi cha kushindwa kuwanyoshea kidole viongozi wa Serikali wasio na maadili na akashauri haja ya kutathmini mfumo wa elimu nchini na hasa mitaala ambayo hubadilika kulingana na matakwa ya kiongozi aliyepo madarakani.

Mkutano huo wa Mwalimu Nyerere, umekuja wakati hali ya kisiasa nchini ikiwa tete kiasi cha miezi tisa tu kabla ya Uchaguzi Mguu wa mwaka 2010. Maoni ya wengi ni kwamba kuna ombwe katika uongozi wa nchi na ndani ya vyama vya siasa.

Hali hiyo imechochewa zaidi na kuwapo kwa makundi ya wazi wazi ndani ya mfumo yaliyotokana na kuwapo kwa mfululizo wa tuhuma za ufisadi dhidi ya wanasiasa, watendaji serikalini na wafanyabiashara wengine ambao ni viongozi wa juu ndani ya chama tawala. Kipindi hiki pia kimeshuhudia viongozi wa dini wakijitokeza kuikosoa Serikali.

Source:www.raiamwema.co.tz

Thursday, December 3, 2009

TCRA kumbana mwekezaji Loliondo

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imebaini kuwa kampuni ya simu za mkononi yenye makao yake katika Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE), inaendesha shughuli zake za kutoa huduma ya mawasiliano ya simu bila leseni.

Kwa mujibu wa TCRA, kampuni hiyo inatoa huduma hiyo katika eneo la uwindaji liliopo Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Profesa John Nkoma, amekataa kutaja jina la kampuni hiyo ya simu.

Kwa mujibu wa Profesa Nkoma, wataalamu wa TCRA wamebaini hilo baada ya kwenda kwenye eneo hilo kuchunguza.

Eneo hilo lipo chini ya kampuni ya uwindaji ya Otterlo Business Corporation Limited (OBC) inayodaiwa kumilikiwa na mwanajeshi wa cheo cha juu kutoka familia ya kifalme,UAE.

OBC ilipewa eneo hilo mwaka 1992 na tangu wakati huo imekuwa ikiongezewa muda kila baada ya miaka mitano.

Bunge limeiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa upya vitalu vya uwindaji ifikapo mwaka 2011 kwa kufuata taratibu mpya.

Wananchi wa eneo hilo wamewahi kulalamika kuwa wanapoingia kwenye eneo hilo simu zao zinabadilika na kuonyesha wanaingia eneo la Uarabuni.

Kwa mujibu wa madai hayo, simu zinakuwa chini ya kampuni ya Etisalat na wanatozwa fedha nyingi wanapopiga simu.

Mkurugenzi Mtendaji wa OBS, Isaack Mollel, aliwahi kukaririwa akisema kuwa, eneo hilo lipo chini ya Etisalat kwa sababu familia ya kifalme ya UAE inahitaji mawasiliano ya uhakika inapotembelea eneo hilo.

Mollel alisema, kwa kuwa Etisalat ni mwanahisa mkuu katika kampuni ya Zantel, hakuna haja ya kuomba leseni TCRA.

"Ni kweli nyumba za wafugaji zimechomwa Loliondo'

MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Job Ndugai amekiri kuwa, kamati hiyo imeyaona maboma ya wafugaji wa jamii ya wamasai yaliyochomwa wakati wa operesheni ya kuwahamisha kutoka eneo la uwindaji, Loliondo mkoani Arusha.

Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea vijiji ambavyo vimeathirika wakati wa operesheni hiyo Ndugai, amesema, maboma yaliyochomwa baadhi ni ya muda na mengine ni ya kudumu na kwamba wafugaji walikuwa wakiishi humo.

“Kwa kweli hilo halina ubishi,tumeshuhudia kuchomwa kwa maboma jambo ambalo si zuri,“ amesema Ndugai.

Mbunge huyo wa Kongwa (CCM) ameyasema hayo wakati anazungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Sointsambu ambacho kilikuwa cha mwisho kutembelewa na kamati hiyo.

Bunge liliipa kamati hiyo jukumu la kuchunguza mgogoro wa Loliondo baada ya Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM) kutoa maelezo binafsi bungeni kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliodaiwa kufanywa na Polisi wa kutuliza ghasia(FFU).

Wafugaji walihamishwa katika eneo hilo linalodaiwa kukodishwa kwa kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC) kwa ajili ya uwindaji.

Ndugai amesema,wabunge walipotembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji, viongozi wa mkoa na wilaya wamegundua kuwepo kwa upungufu kwenye sheria za vijiji na sheria za wanyama pori.

“Hii sheria ya wanyama pori ya ina mapungufu makubwa haielezi mpaka wa pori tengefu katika eneo hili ni ipi, kwani sheria ya vijiji inatambua kuwa maeneo yanayopigiwa kelele ni maeneo halali ya vijiji hadi mpakani na mbuga ya Serengeti,” amesema Ndugai.

Ndugai amesema, Rais Jakaya Kikwete amesaini sheria mpya ya wanyama pori hivyo inaweza kutumika Loliondo kuepusha matatizo hayo kwani inaeleza mipaka ya hifadhi za taifa, pori tengefu.

Amewasihi wananchi wa Loliondo wawe na subira na matumaini kwa kamati hiyo ya Bunge iliyotembelea vijiji saba. “Nawahakikishia kuwa tutakuja na ushauri mzuri kwa Serikali kuhusu tatizo hili la Loliondo.”

Kamati hiyo ilitembelea vijiji vya Oloipiri, Oleirien Magaiduru, Losoito Maalon, Arash, Piyaya, Ololosokwan, na Soint Sambu.

Wednesday, December 2, 2009

ATCL yapunguza wafanyakazi 155

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa barua za kuwapunguza kazi wafanyakazi wake takribani 155 kati ya 333.

Inadaiwa kuwa uamuzi huo una lengo la kuiwezesha kampuni hiyo kutekeleza majukumu ya uendeshaji yaliyokuwa yameshindikana kutokana na kuzidiwa na idadi kubwa ya wafanyakazi.

Chama cha Wafanyakazi wa Mawasiliano na Uchukuzi (COTWU), kimeridhia vigezo vya awali vya serikali na kuachana na azma yao ya awali ya kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda aingilie kati suala hilo.

Hatua nyingine ni ya serikali kuingia ubia na Kampuni ya China iitwayo China Sonangol International Ltd (CSIL) ambayo mbia huyo ameshaonesha nia.

Awali, COTWU ilisema imegomea hatua ya serikali ya kutaka kuwalipa wafanyakazi kwa kigezo cha nusu mshahara (mshahara wa wiki mbili) unatakaozidishwa katika miaka ya utumishi wa mfanyakazi isiyozidi 10.

Wafanyakazi wanataka pamoja na stahili nyingine, anayepunguzwa alipwe mshahara wa miezi miwili utakaozidishwa katika miaka isiyopungua 10 ya kazi.

Jana, gazeti hili lilifika Makao Makuu ya ATCL Dar es Salaam jana na kukuta wafanyakazi wakipishana huku na huko wengine wakiingia katika chumba cha wahasibu kulikoelezwa kutolewa barua na hundi.

“Yaani hapa leo hakukaliki kwa kweli viongozi wote karibu hawapo ofisini, walioko ni wale wanaotekeleza hatua hii ya kutoa barua, hivyo shughuli za kiofisi pengine kesho,” alisikika mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Mfanyakazi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema,imemlazimu kupokea barua na fedha iliyopo kwa matakwa ya serikali na kubainisha kuwa COTWU walikubaliana na serikali kwa sababu hata hicho kidogo kama wakiendelea kukikataa,watakikosa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu, Omari Chambo na Kaimu Ofisa Mkuu wa ATCL, William Hajji, kwa nyakati tofauti walithibitisha kuendelea kwa hatua hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Balozi Mustafa Nyang’anyi, amesema, malipo (bila kubainisha kiasi) yanafanywa na Shirika la Kusimamia Mali za Mashirika ya Serikali yanayouzwa au kubinafsishwa (CHC).

Tuesday, December 1, 2009

Leo ni siku ya ukimwi duniani: Tafakari!!!

Leo ni siku ya ukimwi Duniani,
Nimeona nitumie opportunity hii ili tukumbushane na Watanzania wenzangu na hata walio sio watanzania kwani hili ni tatizo kwa kila nchi na kila jamii hapa Duniani.
Hili tatizo la Ugonjwa huu wa ukimwi(AIDS)Lemetukabili na inabidi tulichukulie serious na tulipe umuhimu sana kwani limetuathiri sana na linaendelea kutuathiri kuanzia wazee, vijana na hata watoto katika jamii.

Naomba tuwe mstari wa mbele katika kwenda kupima na kujua msimamo wetu na vilevile kuwakumbusha watu wengine kwenda kupima na bila kuogopana.
kwa mfano mtu anapopata mchumba basi asisahau kumkumbusha mwenzake kwenda kupima kwani kufanya hivyo kutaokoa maisha ya wengi hasa ukizingatia wengi wanaoambukizwa katika jamii yetu wameambukizwa na waume au wake zao kwa kuogopa kukumbushana kwenda kupima.
Na baada ya kupima utapata ushauri mzuri toka kwa daktari wako katika jinsi gani ya kujiepusha zaidi hata kama uwe unao ugonjwa au huna.
Katika siku hii ya ukimwi duniani kama wewe ni mtanzania basi tumia fursa hii kumkubusha mwenzio kuhusu hili suala hata kama hataki kusikia lakini yatakuwa yamemuingia akilini.

Naomba kwa mwenye kutaka ushauri zaidi kuhusiana na ugonjwa huu basi awasiliane nami kupitia.......
aljabry@comcast.net
Kumbuka sio lazima ujitambulishe kwa jina unaweza kutumia jina lolote ili kuondoa wasiwasi.