Wednesday, October 31, 2012

TGNP Yalaani Vitendo Vya Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Muhingo Rweyemamu Vya Kuwakamata Wasichana Waliopata Ujauzito


Taarifa kwa vyombo vya habari


Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Shirika linalofanya kazi za kutetea masuala ya kijinsia, haki za wanawake na wasichana ikiwemo haki ya uzazi salama tumeshtushwa na kusikitishwa na kauli iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Ndugu Muhingo Rweyemamu, kuhusu kukamatwa na kufungwa kwa wasichana waliopata mimba kama njia ya kushinikiza watoe majina ya wanaume waliowapa mimba. Habari hizi zimeandikaa katika gazeti la the Citizen la tarehe 26 Oktoba 2012 na athari zake kwa wasichana kuchambuliwa zaidi na gazeti hilo hilo tarehe 27 Oktoba 2012

Inasemekana kuwa wasichana mashuleni katika Wilaya ya Handeni wanalazimishwa kupimwa ujauzito na wanapokutwa na ujauzito wanafukuzwa shule. Wasichana hawa hupelekwa polisi kwa mahojiano zaidi endapo watakataa kuwataja wanaume waliowapa mimba.

Vitendo hivi vya udhalilishaji vimetolewa taarifa kwenye mikoa mingine ya Tanzania ikiwemo mikoa ya Mbeya na Iringa. Swali la kujiuliza ni kwa nini msichana aadhibiwe vikali namna hiyo?adhabu ya kwanza kupata ujauzito akiwa mwanafunzi/umri mdogo, adhabu ya pili anafukuzwa shule/ nyumbani na dhabu nyingine akamatwe na kupelekwa polisi. Tunaelewa kuwa kuna mazingira mengi hatarishi yanayochangia mtoto wa kike kubakwa na kupata ujauzito, ukiwemo umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni,ukosefu wa mabweni, gharama mbali mbali ikiwemo michango ya shule, mazingira duni ya kujifunzia na kufundishia, ukosefu wa chakula cha mchana, watoto wa kike hushawishiwa kujiingiza kwenye kubakwa na hatimaye kupata ujauzito na kukatishwa masomo.

Mfumo wa elimu yetu ya Tanzania unaendeleza matabaka kwani wasichana wachache wanakwenda kwenye shule nzuri na kwa gharama kubwa na hata wakipata ujauzito wanaweza kutoa hizo mimba!!!bali wasichana walio wengi wanakwenda kwenye shule zisizo na rasilimali za kutosha hasa maeneo ya vijijini na ndiyo wanaofukuzwa wakipata ujauzito. Mfano katika utafiti wa kiraghbishi uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania mwaka huu kwenye vijiji vitatu vya Kata ya Songwa, Mkoa wa Shinyanga wasichana 38 kwa muda wa miaka 2 walikatishwa masomo kutokana na ujauzito.

Kutokana na vitendo hivyo vya udhalilishwaji, sisi kama wanaharakati wa masuala ya usawa wa kijinsia, haki za kibinadamu na demokrasia tumechukizwa sana na tunalaani vikali vitendo na kauli hii ya mkuu wa wilaya na tunakemea na kusema yafuatayo:

Madai yetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni

1. Kuacha mara moja kuwakamata wasichana wanaopata ujauzito na kuwatoa mara moja wale ambao tayari wamepelekwa jela. Pamoja na kuzindua hiyo KAMPENI ya NIACHE NISOME, atuambie kama imeingizwa kwenye mpango mkakati wa wilaya na umetengewe rasilimali kiasi gani na za kufanya nini???

2. Atuweke wazi utaratibu anaotumia kuwawajibisha wahusika kwani kuna taratibu za kisheria zinabidi kufuatwa ili kuwabana na kama hospitali ya Wilaya ya Handeni ina mashine ya kupima DNA itakuwa Hospitali ya Mfano? Je kama haina anapaswa kuwajibika??

Madai yetu kwa Serikali ya Jamhuri ya Tanzania

1.Kumlazimisha msichana kufanya vipimo vya ujauzito ni ukiukwaji wa haki na uhuru wa mwili wa msichana husika na ujauzito unatumiwa kama kigezo cha kumfukuza shule.

2. Elimu juu ya afya ya uzazi, ikiwemo mbinu za uzazi salama lazima ziwekwe wazi na kufikiwa na wasichana wote na zitolewe bila kuwepo na unyanyapaa wowote

3. Lazima kuwepo na ulinzi wa kutosha kwa wasichana na haki ya kufikia elimu bora na nafasi za ajira, maisha endelevu na huduma za afya ya uzazi ambazo zinathamini ustawi wa msichana

4. Sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 lazima irekebishwe na kuwepo kipengele kinachotoa si adhabu kali tu kwa wanaume wanaowapa mimba wasichana, bali kiongezwe kipengele cha kuhakikisha matunzo ya mtoto na huyo binti na liwe ni suala la kikatiba

Kutokana na kauli ya DC tunatoa wito kwa mamlaka ya serikali ya wilaya ya Handeni na sehemu nyingine popote,ya kuweka mazingira endelevu kwa watoto wa kike kulindwa na kufikia malengo yao bila ya kukandamizwa zaidi.

Tunatoa wito kwa wahusika wote na mamlaka za serikali kuchukua hatua za haraka za kutoa elimu ya afya ya uzazi ikiwemo uzazi salama kwa wasichana na jamii nzima na uingizwe kwenye mitaala ya elimu; kusaidia upanuzi wa usalama wa maisha endelevu kwa wasichana na mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa wote wanawake, wanaume, vijana hasa walioko pembezoni.

Tunatoa wito kwa famillia zote, kutoa kipaumbele kwenye mahitaji maalum ya wasichana na kuwapa msaada wanaohitaji katika kufikia elimu bora, afya ya uzazi salama na maisha endelevu na yenye heshima.

Kamwe haki ya msichana haikuzwi kwa kumtupa jela ni kwa kumpa elimu bora ili aweze kufikia ndoto yake ya hapo baadae.

Imetolewa Dar es salaam leo 31/10/2012 na

......................

Lilian Liundi
Kaimu Mkrugenzi Mtendaji TGNP

Rais Kikwete Aridhishwa na Kazi Inayofanywa na Tume ya Katiba

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa anaridhishwa na mwenendo mzima wa kazi ya Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Wananchi Kuhusu Katiba. Aidha, Rais Kikwete amewataka wajumbe wa Tume hiyo kuwakumbusha wananchi kutokutoa maoni kwa kutumwa na watu wengine bali watoe maoni yao wenyewe kwa kadri wanavyotaka Katiba yao mpya iwe.

Rais Kikwete ameyasema hayo Oktoba 30, 2012, kwenye Ikulu Ndogo mjini Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro wakati alipokutana na kuzungumza kwa muda mfupi na baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Profesa Baregu Mwesiga ambao walikwenda kumjulia hali Rais. Rais Kikwete yuko katika ziara ya siku tatu katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Wajumbe hao wanne ambao walikutana na Rais Kikwete ni sehemu ya wajumbe wa Tume ambao wako mkoani Kilimanjaro kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi wa mkoa huo kuhusu Katiba. Watakuwa Kilimanjaro hadi tarehe 6 Novemba, 2012.

Rais Kikwete amewaambia wajumbe hao: “ Kwa maoni yangu nadhani kazi ya Tume inakwenda vizuri na mimi nawatakia kila heri katika shughuli hii muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Zitakuwepo changamoto, lakini hizo hazikosi katika shughuli yoyote ya binadamu.”

Aliongeza Rais Kikwete: “Nawaomba tu muendelee kuwaelimisha wananchi kuwa ni vizuri kwao kutoa maoni yao wenyewe siyo kwa kutumwa na watu wengine. Wahasishwe wasiwe kaseti za kucheza maoni ya watu wengine.”

Profesa Baregu amemwambia Rais Kikwete kuwa kazi ya Tume hiyo inakwenda vizuri na wajumbe wa Tume wanayo matumaini makubwa kuwa kazi hiyo itakamilishwa katika kipindi kilichokubaliwa. “Tunaweza kusema kuwa tunakaribia kumaliza robo tatu ya kazi ya kukusanya maoni ya wananchi.”
Profesa pia amemwambia Rais Kikwete kuwa ni kweli wajumbe wa Tume hiyo wanakumbana na watu ambao wanatumika kama kaseti za watu wengine. “Ni kweli wapo. Mwanzoni walikuwa wengi lakini sasa tunaona kuwa wanaanza kupungua.”

Tuesday, October 30, 2012

Semina: JE, MCHAKATO WA KATIBA MPYA UNAWABEBA WAFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO SOKONI?SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA JUKWAA LA WAZI LA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII MTOA MADA NI GTI/TGNP.

MADA: JE, MCHAKATO WA KATIBA MPYA UNAWABEBA WAFANYA BIASHARA NDOGO NDOGO SOKONI?
Lini: Jumatano Tarehe 31/10/2012

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Tamwa kuzindua mradi wa kutokomeza unyanyasaji kijinsia

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kinatarajia kuzindua mradi wao unaojulikana kama ‘mradi wa kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia.’

Uzinduzi huo utafanyika leo katika ofisi za chama hicho, jijini Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valerie Msoka, malengo ya mradi huo ni kujenga na kuimarisha usawa wa kujinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

Malengo ya mradi huo, ambao utazinduliwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Denmark, yanatarajiwa kutekelezwa kwa ushirikiano na mashirika mengine, kama vile Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Jumuiya ya Wanawake Wanasheria  Zanzibar (Zafela) na Kituo cha Usuluhishi (CRC).

Katika uzinduzi huo, pia elimu kwa wanahabari kuhusu jinsi ya kuibua vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ndani ya jamii ili hatua za kuvikomesha ziweze kuchukuliwa na vyombo husika, itatolewa.

Mradi huo wa miaka miwili, unatarajiwa kuzinuifaisha jumla ya wilaya 10 za Tanzania Bara na visiwani.

Baadhi ya wilaya hizo, ni Wete, Unguja Mjini Magharibi, Unguja Kusini (Zanzibar); Kisarawe, Newala, Mvomero, Lindi Vijijini, Ruangwa, Kinondoni na Ilala (Tanzania Bara).


CHANZO: NIPASHE

Monday, October 29, 2012

Ni Ndoto Kupata Katiba Mpya Ifikapo Mwaka 2014: Hali Halisi ya Ushiriki wa Wanawake katika Mchakato wa Kutoa MaoniNa Kenny Ngomuo - TGNP
Watanzania tumeingia katika historia ya mchakato wa kuandika Katiba mpya ambao ni shirikishi huku  wengi wetu tukiwepo katika  harakati mbalimbali za kimaendeleo hasa zile zakutafuta kipato na kuwakomboa  kutokana na maisha duni yaliyojaa mifumo kandamizi inayotokana na mila na tamaduni zilizowazunguka hasa watanzania walioko pembezoni. 

Pamoja na wanawake kuwa wazalishaji wakuu katika jamii kuanzia ngazi ya familia wanawake wamekuwa waathirika wakubwa na michango yao imekuwa hautambuliki katika pato la taifa. Suala la kwa nini wanawake na wasichana wamebakia pembezoni katika nchi nyingi zinazoendelea ni dhana pana yenye mizizi ya kihistoria, utamaduni, dini na hata saikolojia yenyewe. Matokeo ya utafiti uliofanyika katika nchi za dunia ya tatu na Umoja wa Mataifa, yameonesha kuwa wanawake  walio wengi katika nchi nyingi zinazoendelea bado  wanazidi kuishi maisha duni siku hadi siku ikiongozwa na mifumo kandamizi.. 

Utafiti uliofanyika na Mtandao wa Jinsia Tanzania mwaka 2009  kuhusu kazi  wanazofanya wanawake zisizo na malipo, mfano kuhudumia wagonjwa majumbani, kulea watoto na  wazee ulionesha wazi kuwa wanawake wanatumia nguvu na muda mwingi ambao hautambuliki popote katika pato la taifa. Utafiti uliofanywa na Programu ya Chakula Duniani (World Food Programme)  pia umeonesha kuwa mwanamke anatumia  zaidi ya asilimia 90% ya pato lake kila mwezi  katika familia kwa njia ya aidha kununua  chakula, vitabu na madaftari ya watoto, dawa , neti za kujikinga na mbu kwa ajili ya watoto wao na huduma nyinginezo zinazofanana na hizo.

Pamoja na changamoto nyingi ambazo wanawake wamekumbana nazo katika harakati zao za kujikomboa, wanawake wamekuwa msitari wa mbele katika shughuli zote za kimaendeleo katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya kuandika  Katiba mpya iko katika awamu ya pili .  Zoezi hili limekwenda vizuri hasa kwenye maandalizi na kuwepo kwa vifaa vya kuwezesha wananchi kuendelea kushiriki katika kutoa maoni yao ya masuala ambayo wangependa  yaingie katika Katiba mpya. Pamoja na mambo kadhaa mazuri, bado kumeendelea kujitokeza mapungufu ambayo yanahitaji kurekebishwa ili kuweza kuboresha ufanisi wa ukusanywaji wa maoni katika mikoa ambayo imesalia  ambayo ni takrikbali mikoa 15 sawa na asilimia 50% ya mikoa yote ya Tanzania. Hii ni kutokana na utafiti uliofanyika mwezi  Agosti na Septemba  2012 na Jukwaa la Katiba Tanzania.

Hata hivyo, imebainika kwamba mikutano mingi inafanyika muda wa asubuhi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana na baadaye mchana kuanzia saa 8 hadi 11. Kwa uhalisia mikutano ya asubuhi haijawa rafiki kwa wanawake hasa wale wanaoishi vijijini, ambao  muda mwingi wa asubuhi wako katika  shughuli za uzalishaji mali na kujitafutia kipato, ambapo hata mijini pia muda bado ni changamoto. 

Mfano, Jukwaa la Katiba Tanzania lilipewa taarifa walipotembelea Kata ya Mwakaleli mkoani Mbeya, kuwa mikutano ya asubuhi iliwanyima fursa  ya kutoa maoni wananchi wengi sana waliokuwa katika shughuli za uzalishaji mashambani ambao wengi wao ni wanawake. Katika Mkoa wa Ruvuma, tatizo lilipelekea uwiano wa wanawake na wanaume katika kushiriki mchakato wa utoaji maoni kuwa mbovu sana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana, idadi ya wanawake walioshiriki katika takribani mikutano 21 ya wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma ilikuwa ni 1,949 tu kati ya jumla ya wananchi 8,915 sawa na asilimia 22% tu. Aidha, kutokana na uhamasishaji duni kwa wanawake, hata uchangiaji katika kutoa maoni ulishuhudia wanawake wakichangia kwa idadi ndogo sana ya 198 tu kati ya wananchi wote 2,074 waliotoa maoni kwa Tume, sawa na asilimia 9.5% tu.

Kundi lingine ambalo limesahaulika ni hili lenye mahitaji muhimu hasa watu wanaoishi na ulemavu wa aina mbali mbali. Bado watu wenye ulemavu wa kuona, kusikia na kuongea hawajaweza kupewa fursa kubwa ya kuweza kushiriki vema kutoa maoni yao. Hii ni kutokana na Tume kuendelea kuitisha mikutano hii mbali na makazi ya wananchi walio wengi. Pia Tume haijaweza kuandaa miundombinu kama vyombo maalum kwa wasioona na wakalimani wa lugha za alama kwa wale wasio na uwezo wa kusikia na kuzungumza.
Natoa mapendekezo yafuatayo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya:

1) Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya ihakikishe inawafikia wananchi  walioko pembezoni hasa wanawake ambao kero zao nyingi zimekuwepo kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi kutokana na mifumo, sera na sheria ambazo bado kandamizi na mfumo dume uliokithiri

2) Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni lazima iwasiliane na wataalam wa lugha za alama na wataalam wengine na kuongozana nao mikoani na wilayani ili watanzania wote wakiwemo walemavu waweze kufikiwa na kutoa maoni yao kwa ajili ya Katiba mpya ijayo

3) Tume  ifanye utafiti kwa kila eneo wanalokwenda  ili kubainisha muda ambao ni rafiki kwa kila mwananchi aweze kushiriki  na hili liende sambamba na matangazo ya kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano ya kutoa maoni 

4)  Mchakato wa Katiba Mpya, uendelee kwa kasi ya kawaida na kwa umakini mkubwa bila kukimbizana ili tuweze kupitia hatua zote za kuandika Katiba mpya ambayo ni shirikishi ya kihistoria na ya kidemokrasia.

Vigogo 10 wahusishwa mabilioni ya Uswisi

  • ZITTO ASISITIZA NYARAKA ZIPO, DK HOSEAH NDIYE ANAYEZIZUIA
VIGOGO 10 wametajwa kuhusika katika kashfa ya kuficha Sh303.7 bilioni katika benki mbalimbali nchini Uswisi.

Katika orodha hiyo inadaiwa kuwa yupo kiongozi mmoja mwandamizi mstaafu, maofisa watatu wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mawaziri wastaafu ambao baadhi yao bado ni wabunge na aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Benki Kuu Tanzania (BoT).
Majina hayo ambayo mwandishi wetu amefanikiwa kuyaona, yamo katika orodha ya mchunguzi mmoja wa kimataifa wa masuala ya ufisadi (jina tunalo).

Juzi, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alimshukia Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah akimtuhumu kuandika barua Uswisi akisema Tanzania haina masilahi na mabilioni ya fedha yaliyofichwa katika benki zilizopo nchini humo. Hata hivyo, Dk Hoseah alikanusha madai hayo akisema hajawahi kufanya hivyo.

Akizungumza jana Zitto alisisitiza kauli yake akisema: “Sijawahi kumsema Dk Hoseah kwa lolote, kwa nini leo nimsingizie? Yeye mwenyewe anajua ushirikiano niliompa wakati wabunge wanapinga yeye asichunguze malipo ya posho mara mbili kwa wabunge.”

“Nilisimama kidete kusema Takukuru wapo sahihi na mimi nilikwenda mwenyewe kwao kuhojiwa na kuagiza wajumbe wa kamati yangu (Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma), waende kuhojiwa. Spika aliyestaafu (Samuel Sitta) akaizima kashfa ya wabunge kupokea posho mara mbilimbili. Mwulizeni amesahau? Sasa leo nimzushie ili iwe nini?.”
Alisema orodha ya Watanzania wenye fedha huko Uswisi, ipo na ameiona na nyaraka zinaweza kutolewa kwa taasisi za Serikali tu.

“Dk Hoseah kazuia nyaraka hizo. Akitaka nimwonyeshe mtu anayeweza kutoa nyaraka hizo, nipo tayari isipokuwa aahidi kuiweka wazi,” alisema Zitto.

Alisema katika orodha ambayo Waziri wa Fedha wa Ufaransa anayo, kuna Watanzania lakini akaituhumu Serikali akisema haitaki kufuata njia halali za kupata orodha hiyo kwa kuwa viongozi wengi na wafanyabiashara wakubwa wana akaunti katika benki za Uswisi.

Juni 26, mwaka huu gazeti hili lilichapisha habari kuhusu utoroshwaji wa fedha hizo na kueleza kuwa Polisi wa Kimataifa (Interpol) nchini kwa kushirikiana na Takukuru inachunguza suala hilo.

Kiasi hicho cha fedha kimedaiwa kuingizwa katika akaunti za Watanzania na kampuni moja ya uchimbaji mafuta na kampuni kadhaa za uchimbaji madini ambazo zinafanya kazi Tanzania.
Chanzo hicho kiliongeza kwamba kiasi hicho cha fedha kipo katika akaunti sita tofauti zinazomilikiwa na Watanzania wakiwamo wanasiasa wakubwa.

Hata hivyo, chanzo hicho kilieleza kuwa tangu akaunti hizo zifunguliwe, wamiliki wake halali hawajawahi kuingiza hata shilingi.

“Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa fedha hizo zipo katika akaunti sita tofauti ambazo zinamilikiwa na wanasiasa wakubwa nchini na wenzetu wa Uswisi wameeleza fedha hizo zimeingizwa na kampuni kadhaa ambazo zinahusika na mafuta pamoja na madini hapa nchini,” kilidokeza  chanzo hicho.
Kugundulika kwa kiasi hicho cha fedha katika benki za Uswisi ni kutokana na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) iliyotolewa mwaka huu.

Chanzo: Mwananchi

Thursday, October 25, 2012

MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA SSRA WAOTA MBAWA,WAFANYAKAZI WALIOACHA KAZI AU KUACHISHWA KAZI KUENDELEA KUTESEKAHatimaye  msimamo wa serikali juu ya kupeleka marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii leo umeota mbawa baada ya kuthibitishwa mbele ya kamati ya kudumu ya maendeleo ya jamii ya Bunge iliyokutana na katika ukumbi wa wizara ya maendeleo ya jamii mjini Dar es salaam kwamba wizara ya kazi na ajira haijaandaa muswada huo. Akithibitisha juu ya swala hilo wakati akitoa maelezo ya wizara mbele ya kamati,katibu mkuu wa wizara hiyo ndugu shitindi amedai kwamba wizara imejipanga kupeleka miscellaneous amendments kwa mwanasheria mkuu wa serikali.

Katika amendments hiyo katibu mkuu amesema kwamba kifungu kitakachorekebishwa ni kile Na.44 cha sheria ya PPF ambacho ndo pekee kitaruhusu wanachama wa PPF kuchukua mafao yao.Wanachama wa mifuko mingine kama NSSF fao la kujitoa halitarudishwa katika sheria hivyo kubaki wakisubiri miaka 55 au 60 kuchukua mafao yao.Katika mjadala huo hoja mbalimbali zilijitokeza,mojawapo ni ile iliyoibuliwa na bwana Benjamin Dotto.

Akitoa mchango wake bwana Dotto alitaka kujua kwa nini wizara imekaidi kutekeleza mapendekezo ya bunge la nane,ambalo kupitia kwa mbunge Jaffo liliitaka wizara kurudisha fao la kujitoa kwa wafanyakazi wanaoacha au kuachishwa kazi wakati mchakato wa marekebisho ya sheria ukiendelea.Lakini vilevile alitaka kujua kwa nini wizara imekaidi kuandaa muswada wa sheria badala yake unaleta miscellaneous ammendments.

Akiwasilisha mapendekezo ya wafanyakazi mbele ya kamati,Dotto alisema kwamba rasilimali zote na fedha zilizoko kwenye mifuko ni mali ya wanachama wa mifuko hii.Kwa hiyo ili pesa hizi ziweze kulindwa na kukaa salama,wakati umefika uendeshaji wa mifuko hii usimamiwe na wanachama wenyewe.Hivyo akapendekeza mwenyekiti wa mamlaka ya SSRA,na wenyeviti wa mifuko mingine wasiteuliwe na rais bali wachaguliwe na wanachama wa mifuko ili wakienda kinyume waweze kuwajibishwa na wanachama wenyewe.pendekezo hili lilipingwa vikali na Mustafa mkulo na wabunge wengine kwa sababu linainyima serikali nafasi ya kuteua wenyeviti hao.

Akifafanua Dotto alisema kwamba lengo kubwa la pendekezo hilo ni kuiondolea serikali mamlaka ya kutumia fedha za wanachama jinsi wanavyotaka wao,kwa mfano ujenzi wa Udom,Daraja la kigamboni na njia za mabasi yaendayo kasi ni miradi inayotumia pesa za wanachama kwa sababu wasimamizi wa mifuko hiyo ni wateule wa rais.Kauli hiyo ilimsababishia kasheshe bwana dotto kwani alizuiliwa kuendelea kutoa mapendekezo mengine maana yalionekana kugusa masilahi ya wakubwa.

Hata hivyo baadhi ya mapendekezo aliyozuiliwa kuyataja na kufafanua mbele ya kamati ni pamoja na;

1. FAIDA INAYOPATIKANA KUTOKANA NA UWEKEZAJI WA MIFUKO HIYO IGAWIWE KWA KILA MWANACHAMA KILA MWISHO WA HESABU ZA MWAKA KWA KUWEKWA KATIKA AKAUNTI YA MWANACHAMA.

2. MWANACHAMA ARUHUSIWE KUHAMA MFUKO MMOJA KWENDA MWINGINE KWA KUHAMA NA MAFAO YAKE FAIDA NA HAKI ZINGINE.

3.MFANYAKAZI AKIACHA AU KUACHISHWA KAZI MAFAO YAKE YALIPWE NDANI YA SIKU SABA.

4. KUWEPO NA MIKOPO YA WANACHAMA NA WARUHUSIWE KUCHUKUA HADI NUSU YA MAFAO YAO,DHAMANA YA MKOPO IWE MAFAO YAKE YALIYO KATIKA MFUKO.

Kwa ufupi hayo ndo baadhi ya mambo yaliyojiri.ANGALIZO wafanyakazi bado tuna safari ndefu sana kuweza kufika kwenye nchi ya ahadi na bila MSHIKAMANO DAIMA tutabaki kutendwa na kugeuzwa na serikali kama mafungu ya nyanya kama hali halisi ilivyojidhihirisha leo.

Naomba kuwasilisha.
Mchango wa John Mnyika (Mbunge wa Ubungo)