Monday, June 13, 2011

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI

BAJETI 2011/2012 ISIYONUFAISHA WALIO PEMBEZONI

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia kikundi kazi cha uchambuzi wa bajeti (Budget Analysis Task Team) wakishirikiana na wanaharakati wengine kutoka ngazi ya jamii wamefanya uchambuzi wa hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012 iliyosomwa bungeni tarehe 8/6/2011 na waziri wa Fedha Mheshimiwa Mustafa Mkulo (Mb).Uchambuzi huu umefanywa kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi, wakiongozwa na kauli mbiu ya “Haki ya Uchumi: Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake walioko Pembezoni”; kama sehemu ya kuchangia na kuendeleza mjadala kuhusu bajeti ya taifa ambayo itaanza kutekelezwa kuanzia Julai mosi 2011na mgawanyo wa rasilimali za nchi kwa ujumla.

Uchambuzi wa bajeti hii umeandaliwa kwa kuzingatia muktadha ambao uchumi wa nchi unazidi kuimarika kidogo baada ya kumalizika kwa zahma ya uchumi duniani na kupelekea kuongezeka kwa pato la taifa kufikia asilimia 7 (2010) ikilinganishwa na asilimia 6 (2009) kutokana na msongo wa uchumi duniani. Nchi yetu vilevile ndio kwanza imetoka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa Rais, wabunge na madiwani pamoja na kuwepo kwa vuguvugu la kudai mabadiliko ya Katiba mpya. Pia nchi yetu inaelekea kwenye sensa ya taifa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 2012. Wakati huo huo, mwaka huu ni wa kwanza wa utekelezaji wa MKUKUTA II (2010/2011-2014/2015). Mwaka huu pia ufadhili wa kibajeti (GBS) umepungua na serikali inakazana kuongeza mapato ya ndani.Hivyo uchambuzi huu umelenga kuchambua muelekeo mzima wa bajeti kuona ni nani anayenufaika zaidi kwa kutazama vipaumbele vyake, utegemezi kwa mikopo na misaada ya wafadhili na masuala mbali mbali ya kisekta.

Baada ya kupitia hotuba hiyo tumeshtushwa na ongezeko la bajeti kutoka 11.6 hadi 13.5 trilioni kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012 licha ya kuwepo pengo la kimapato, ongezeko la madeni, na utegemezi mkubwa wa bajeti kwa wahisani.. Ripoti ya hali halisi ya uchumi imeonesha ukusanyaji wa mapato ya kodi mpaka kufikia Machi 2011 ulikuwa 69% ya malengo ya kukusanya shilingi bilioni 6,176.2 Hii ina maanisha kuna pengo la 31 % ya mapato ambalo ni sawa na bilioni 1,919.9. Kumekuwa na matumizi makubwa ya dola katika rasimu ya bajeti na uchumi kwa ujumla (dollarization of the economy), hii inaonesha kuwa hata serikali inachangia kudumaza thamani ya shilingi. Wakati huo huo ripoti ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali imeonesha kuwa bajeti ya serikali ni tegemezi kwa kiasi kikubwa kwa wahisani na deni la taifa linazidi kukua kutoka Shilingi 7.6 trilioni (2008/2009) hadi Sh10.5 trilioni (2009/2010) ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 38 ya pato la Taifa. Kutokana na ongezeko la deni bado kiasi kikubwa cha bajeti kitaenda kulipa madeni, kwa maana hiyo kutaathiri moja kwa moja kiwango kitakachowafikia wananchi hususani wanawake walioko pembezoni.

Bajeti ya 2011/2012 imeainisha vipaumbele vyake vikiwa ni, mindombinu bilioni 2,781.4 sawa na ongezeko la 85% kwa bajeti ya 2010/2011; Nishati bilioni 539.3 sawa na ongezeko la 65% ; Maji imetengewa bilioni 621.6 sawa na ongezeko la (56%); Kilimo ni bilioni 926.2 sawa na ongezeko la 2.5%; Elimu imetengewa bilioni 2,283 sawa na ongezeko la 12%. Mwisho ni afya bilioni 1,209.1 sawa na ongezeko la 0.3% [62i]. Japo vipaumbele hivi kwa harakaharaka vinaonekana kutoa suluhisho la mahitaji ya jamii kwa wakati huu, kiutekelezaji havina uhalisia na hoja yetu kubwa ni: kwa kiwango gani vipaumble hivi vitatoa nafuu ya maisha kwa wananchi walioko pembezoni hususani wanawake?Je ni kwa kiwango wameshiriki katika kuainisha vipaumbele hivyo?

Kwa mfano ni kwa kiwango gani ongezeko la 85% katika miundombinu litasaidia kuboresha miundombinu ya vijijini zaidi ambayo itatumika kutoa mazao mashambani kupeleka katika masoko? MKUKUTA II [2.3.2] umeonesha kuwa vifo vya wajawazito husababishwa na umbali mrefu na miundombinu mibovu wakati wanapokwenda kujifungua. Pia imeendelea kuainisha kuwa miundombinu mibovu imefanya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii kuwa ngumu na hivyo kuongeza wimbi la umaskini.

Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, serikali imelenga kukusanya jumla ya shilingi billioni 6,228.8 kama mapato yanayotokana na kodi. Mapato yasiyotokana na kodi yanatazamiwa kuwa shilingi billioni 547.1 na vyanzo vya halmashauri 350.5. Katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato, serikali imelenga kuimarisha utaalamu na mbinu za kuhakiki kodi kutoka kwenye kumbukumbu za biashara; kuimarisha mfumo wa utawala wa kodi kwa kutumia vitalu; kuingiza sekta isiyo rasmi kwenye mfumo wa kodi. Tunauliza sekta isiyo rasmi itachangia asilimia ngapi ya pato la taifa iwapo itaingizwa kwenye mfumo wa ulipaji kodi? Serikali inalenga makundi yapi, wazalishaji na wafanyabiashara wadogodogo kama mama lishe na wamachinga wenye kipato cha chini kabisa au matajiri na wasomi wanaopata kipato kikubwa kila mwezi bila kulipa kodi?

Vile vile serikali itahuisha sheria mbalimbali zinazoruhusu misamaha ya kodi kwa nia ya kudhibiti misamaha hiyo; kwa sasa misamaha hiyo ni 2.5% ya pato la taifa. Hii ni sawa na shilingi 290,000,000,000 kwa bajeti ya mwaka 2010/2011. Nani ananufaika na misamaha hiyo? Kama kiasi hicho cha fedha kingeongezwa kwenye bajeti ya afya kingeweza kuboresha huduma hiyo. Mbinu nyingine ya ukusanyaji wa mapato ni kuendelea kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha kuwa malipo yanafanyika kupitia benki na kuanza kutumia mfumo wa kulipa kodi kwa kutumia njia ya M-Pesa kwa malipo ya kodi yasiyozidi shilingi 500,000 ili kuondoa kero ya walipa kodi kukaa kwenye mstari kwa muda mrefu. Tunahoji hii huduma ya M-Pesa nayo itachangia shilingi ngapi kwenye pato la taifa kwa kuwa nayo ni biashara?

Katika kutekeleza bajeti ya serikali ya 2011/2012, serikali imezingatia misingi ya sera na mikakati iliyojiwekea, mojawapo ya sera/mikakati hiyo ni MKUKUTA II. Hata hivyo utekelezaji wa MKUKUTA II ndani ya miaka mitano yaani 2010/2011- 2015 umeanza kutekelezwa mwaka mmoja kabla ya Mpango wa muda wa kati wa Maendeleo (MTEF) ambao ndio umebeba bajeti ya utekelezaji kwa mwaka mmoja mmoja ndani ya miaka mitano. Serikali inaelezaje mkanganyiko huu?

Katika mapitio ya utekelezaji wa sera za bajeti ya mwaka 2010/2011, waziri wa Fedha alibainisha kuwa gharama za uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba 2010 zilitumika kama zilivyopangwa, bila kutoa maelezo ya kina [14ii].Tunadai ufafanuzi juu yafuatayo: Serikali ilipanga kutumia shilingi ngapi, ilitumia shilingi ngapi, fedha za ndani zilikuwa ngapi na fedha za wahisani zilikuwa ngapi?Pia tunahoji wanwake wa Tanzania wamenufaika vipi kwa fungu hili? hususani tukizingatia kuwa utekeelzaji wa kufikia asilimia 50-50 katika uongozi Nyanja zote bado ni ndoto.

Kwa upande wa afya, Serikali imeongeza bajeti kwa 0.3% mabayo ni sawa na taribani asilimia 10.6 ya bajeti nzima. MKUKUTA II na ripoti ya hali halisi ya sekta ya afya (TDHS) zinaonyesha kwamba wanawake 454 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kujifungua. Je, kwa ogezeko la 0.3% serikali itaweza kutekeleza azimio la Abuja ambalo linaelekeza kutengwa 15% ya bajeti ya afya? Na je serikali ina nia ya dhati kuondoa vifo vya uzazi ikiwa ni 51% tu ya wanawake hujifungulia kwenye vituo vya afya (TDHS 2010)? Vipi kuhusu maazimio ya ‘Mpango Mmoja’ (One Plan?)

Kwa upande wa kipaumbele cha nishati, “Serikali inawashauri wananchi kuanza kutumia vyanzo mbadala vya umeme wa jua, upepo na nishati inayotokana na biogesi pamoja na kutumia kwa uangalifu nishati ya umeme iliyopo” [9b]. Je kuna mkakatai ganiwa kuwezesha hili ikizingatiwa gharama ya nishati mbadala wakati wananchi wengi hawawezi kupata hata mlo mmoja kwa siku. Masuala ya nishati yanaendelea kuwa mzigo mkubwa kwa wanawake walioko pembezoni ambao ndio wenye jukumu la kubeba na kuni.

Suala la wafanyakazi kuhitaji kuongezewa mishara na pia kupunguziwa kodi kwenye mishahara ni suala muhimu kwa maisha endelevu lakini halikuzungumziwa na kuwekewa mikakati thabiti katika hotuba ya bajeti ya serikali 2011/2012. Kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa baadhi ya watumishi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka serikalini [77i] itawasaidia wakubwa tu,si wafanyakazi/watumishi wa kima cha chini.. Ajabu serikali inapanga kupunguza kipato cha wananchi waliokuwa wengi wanaofanya biashara ndogo ndogo kwa kutoza ada ya leseni ya biashara mjini na hata vijijini, bila kujali uwezo wao [82]. Je; serikali haioni ukali wa maisha uliopo kwa watumishi wa umma na sekta binafsi na watanzania kwa ujumla? Kwa hali hii watumishi wa umma wataacha kushawishika kutoa na kupokea rushwa?

Miradi mbali mbali ya kilimo ikiwa ni pamoja na Southern Agricultural Growth Corridor imelenga zaidi wakulima na wawekezaji wakubwa huku wakiwafanya watanzania kuendelea kuwa vibarua. Kidhibiti cha kuonyesha kuwa mipango katika sekta ya kilimo inawalenga zaidi wazalishaji wakubwa ni punguzo la kodi zinazowekwa kwenye matrekta, uzalishaji na usafirishaji wa Maua nje ya nchi ambavyo hutumiwa zaidi na wakulima wakubwa. Suala la kilimo pia halijapewa kipaumbele kwa mrengowa kijinsia ukizingatia kuwa wakulima wengi wadogo ni wanawake amabao wamebanwa na mfumo dume katika urithi, maamuzi na mzigo wa kazi.

Kwa mantiki hii tunaona kwamba bajeti ya 2011/2012 haijalenga kumnufaisha mwananchi wa kawaida na hasa wanawake walioko pembezoni. Ni dhahiri kuwa mfumo wa uchumi uliopo ni wa kinyonyaji na unaelekeza zaidi kwenye kukuza mauzo ya nje na kufifisha kipato endelevu kwa wananchi masikini. Tunadai rasilimali kuelekezwa katika mchakato wa katiba, suala ambalo ni nyeti kwa maendeleo ya taifa katika kudai haki na usawa katika jamii. Vile vile tunadai ushiriki zaidi wa wananchi katika kuibua na kupanga vipaumbele vyao vya kibajeti ili kuondokana na dhana ya kuweka msisitizo katika ‘fursa’ badala ya mahitaji halisi ya watu. Pamoja na mipango mingi ya kudhibiti matumizi ya serikali, suala la uwazi na uwajibikaji lipewe kipaumbele hasa katika kusimamia utekelezaji wa matumizi ya rasilimali za taifa.


Imetolewa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)


Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji TGNP

13 June 2011

No comments: