BAJETI ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 imeelezwa kuwa haijazingatia kupanda
kwa hali ya maisha ya wananchi wa hali ya chini na hasa wa vijijini na imewekwa kisiasa zaidi.
Wakichangia maoni yao kwa nyakati tofauti wadau wa vyama vya siasa na wananchi katika Mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012 uliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam walisema bajeti haijamuangalia na haikidhi mahitaji
ya mwananchi wa hali ya chini.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuna
haja ya kuwa na mchakato wa kuandaa bajeti ili wananchi watoe maoni yao kabla bajeti ya Serikali haijatolewa.
Profesa Lipumba alisema katika bajeti ya mwaka huu Sekta ya Kilimo ambayo inaelezwa kuwa ni uti wa mgongo na ndio inaweza kuwainua wananchi wa hali ya chini, haijapewa kipaumbele kinachostahili.
Alisema pia kwa kuangalia bajeti ya afya ya mwaka huu wa fedha 2011/2012 ya Sh bilioni 1,209 (Sh trilioni 1.209) na ya mwaka 2010/2011 ya Sh trilioni 1,205.9 (Sh trilioni 1.206) kwa halisi mwaka huu ni sawa na kuwa imeshuka.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) akichangia katika mjadala huo
alisema kinachokosekana na sera ambazo itamwezesha Mtanzania kuondokana na hali ya umasikini na hiyo ni kutokana na kukosekana utaifa.
Alisema bajeti hiyo imetawaliwa zaidi na wahisani kwa sababu Watanzania wenyewe
wamekosa nafasi ya kukaa na kujadiliana na kuzungumza masuala yao ya msingi wanayotaka kuwekwa ndani ya bajeti yao.
Mkazi wa Dar es Salaam, Kwala Amuli alisema bajeti ya mwaka huu haikuzingatia kupanda hali ya maisha ya wananchi wa hali ya chini na hasa wa vijijini na kwamba ni bajeti iliyopangwa bila kuangalia kundi hilo ambalo ni kubwa zaidi.
Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Nikusela Athanas alisema bajeti
ya mwaka huu inaonesha dhahiri sera ya Serikali ya mwaka 2020/2025 inaweza kuja kukwama siku zijazo kwa kile alichoeleza ina mwelekeo wa kuweka tabaka la walionacho na wasionacho.
No comments:
Post a Comment