Tuesday, July 28, 2009

Mjadala kuhusu mgodi wa Kiwira

Hivi juzi tu serikali ilitoa tamko rasmi kuhusu mjadala mkubwa wa mgodi wa kiwira ulioibua hisia na jazba bungeni na wananchi wa kawaida kwa takribani mwaka sasa.

Serikali imetamka rasmi kuwa Mkapa na Yona ambao ndio walionunua mgodi huo kwa bei ya kutupa ya shilingi za kitanzania milioni 70 watarejeshewa gharama zao walizotumia kuukarabati ambazo zimekadiriwa kufikia shilingi bilioni mbili za kitanzania.

Hii ni sawa kwa kiongozi kutumia madaraka yake vibaya na kisha baada ya kugundulika afidiwe gharama?

Viongozi hawa walistahili wachukuliwe hatua za kisheria au warejeshewe gharama zao zinazodaiwa kutumika kwenye kuendesha mgodi huo?

Jadili!!

`Fichueni wauaji wa albino`

JamiiI imeaswa kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuwafichua watu wanaoendesha mila na imani potofu kwa kuwaua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe ili kutokomeza unyama huo.

Aidha jamii imetakiwa imrejee Mwenyezi Mungu kwa kuishi maisha ya kistaarabu ya kupendana, kuheshimiana, kuthaminiana kwani kila kundi lina haki ya kuishi maisha yenye amani na upendo na si kuwindwa kama ndege.

Wito huo ulitolewa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe, kwenye uzinduzi wa albamu ya Tuhurumie iliyotayarishwa na Nzega Disabled Talent (NDT).

Albamu hiyo ilizinduliwa na kwaya ya watu wenye ulemavu, wakiwemo albino na ilifanyika kwenye uwanja wa Parking wilayani Nzega, mkoani Tabora.

Bashe alisema kila jamii nchini ina wajibu wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe kwani wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kuandamwa, hivyo kupoteza imani kama nao wanastahili kuishi kwa amani kama binadamu wengine.

Alisema vita hiyo ni ya kila mwananchi kwani kama ikiachiwa serikali pekee itakuwa ni vigumu wahusika wa unyama huo kubainika kwani wanajificha ndani ya jamii.

Katika uzinduzi huo, Bashe alisema kitendo cha kualikwa kwenye hafla hiyo kimedhihirishia Tanzania haina matabaka wala mipaka ya kidini katika shughuli za maendeleo yanayohusu jamii kwa ujumla.

Awali kwenye risala ya walemavu kwenye uzinduzi huo, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Christian Church of Tanzania (PCCT) na Mwenyekiti wa NDT, Mchungaji Yohana Nghumba, alisema mfuko huo unaendeshwa chini ya kanisa hilo wilayani Nzega.

Source: Nipashe

Friday, July 24, 2009

Kilango na wenzake kudhibitiwa 'kiaina'

KUMEIBUKA upotoshaji wa makusudi wenye malengo ya kuwakatisha tamaa wabunge kutimiza jukumu la msingi, kwa mujibu wa Katiba, la kuishauri na kuisimamia serikali, Raia Mwema limedokezwa.

Upotoshaji huo unaolenga kuwaondoa katika jukumu hilo wabunge wanaohoji ufisadi dhidi ya maliasili za Taifa unatajwa kutumia mbinu mbalimbali.

Moja ya mbinu hizo ni kufanya propaganda ili kugeuza misimamo ya wabunge hao ya kuhoji vitendo vya ufisadi serikalini ili iaminike kwa Watanzania kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa chuki binafsi dhidi ya mawaziri.

Mbali na mbinu hiyo, mbinu nyingine ni kuhusisha suala la udini kwa kulinganisha dini ya mbunge na waziri anayeshambuliwa.

Baadhi ya wabunge walioanza kushughulikiwa na mkakati huo usio na tija kwa Taifa ni pamoja na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango-Malecela, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, Jenista Mhagama na Mbunge wa Ilemela, Antony Diallo.

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao waliwabana baadhi ya mawaziri, wakiwamo Dk. Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia na Shamsha Mwangunga.

Hata hivyo, mbinu hizo zinazotajwa kuwa ni chafu na zisizo na maslahi yoyote kwa Taifa kwa kuwa wabunge hawashambulii mawaziri binafsi, bali wanachoshambulia ni madaraka ya uwaziri kutotumika kulinda maslahi ya nchi, zimeanza kugonga mwamba miongoni mwa wananchi.

Taarifa zaidi zilizotufikia zinaeleza kuwa baadhi ya mawaziri walifikia hatua ya kutaka kuhujumu mpango wa Anne Kilango, kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu wizi wa pembe za ndovu zilizosafirishwa kwenye makontena mawili na kukamatwa nchini Vietnam.

Mawaziri hao wanadaiwa kupiga kampeni kwa wabunge wasio na msimamo wa kutetea raslimali za Taifa ili kama Kilango angewasilisha hoja hiyo siku ya pili ya mjadala wa bajeti wa Wizara ya Maliasili na Utalii, akwamishwe bungeni.

Inadaiwa kuwa usiku wa kuamkia siku ya pili ya mjadala wa bajeti ya wizara hiyo, mawaziri hao walipiga kampeni kwa wabunge hao ili wampigie makofi Waziri wa Maliasili na Utalii, dhidi ya Kilango.

Ingawa mkakati huo unatajwa kufanikiwa kwa kiasi fulani, lakini umezua maswali mengi ikiwa ni pamoja na ufahamu wa wabunge waliofanikisha mpango huo.

Inaelezwa kuwa kutokana na kasi ya Bunge katika kuhoji ufisadi, viongozi waovu serikalini wameanza kujipanga kukabili hali hiyo kwa kutumia mbinu hizo.

“Tunawashangaa wenzetu, wanashawishiwa kwa kampeni ya kupuuzi eti wapige makofi kwa wingi kum-support waziri dhidi ya Kilango, na wanajenga hoja yao katika msingi kwamba wabunge wenye misimamo mikali wana wivu.”

“Hivi ni wivu gani huo mtu anapohoji kuvushwa kwa pembe za ndovu kontena mbili na maofisa wa Tanzania wakitoa nyaraka feki, halafu mbali kontena zinakatamwa nje ya nchi?” alisema mmoja wa wabunge aliyezungumza na Raia Mwema na kuongeza kuwa;

“Mimi niseme tu kwamba ingawa tupo wabunge takriban 300 lakini tija inayotokana na wingi huu ni ndogo kulinganisha na idadi. Wengine ndiyo hao wanashawishiwa kwa hoja za kipuuzi.”

Soma zaidi

Mkataba wa Kanisa na Serikali waanikwa

-Mashehe wataka nao wahusishwe
-Askofu asema ni mkataba usiobagua
-Serikali ya Kikwete njia panda
SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete, imezidi kuingiwa na misukosuko inayogusa waumini wa dini mbalimbali, na sasa kumeibuliwa hati ya makubaliano (MoU) ambayo Serikali iliingia na makanisa nchini. Makubaliano hayo yalikuwa hayafahamiki kwa Watanzania wengi.

Hati hiyo ya makubaliano, ambayo ilisainiwa na Serikali wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, inaelezwa kuzipendelea zaidi taasisi za Kikristo zinazotoa huduma nchini.

Baadhi ya viongozi wa Kiislamu nchini, wameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba mkataba kama huo waliouandaa ulipata kukataliwa na serikali pamoja na kuwa ulifanana kwa kila kitu na huo.

Tayari mjadala wa serikali kujiingiza katika masuala ya dini unazidi kupamba moto ukihusisha uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya Waislamu na kuwapo Waraka wa Kanisa Katoliki unaoelimisha waumini wake kuhusu uchaguzi.

Serikali iliutia saini rasmi hati ya makubaliano kati yake na Baraza la Wakristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (CPT), huku Serikali ikiwakilishwa na Edward Lowassa ambaye wakati huo alikuwa waziri mwandamizi.

Hati hiyo, ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, iliandaliwa na Profesa Costa Mahalu alipokuwa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Katika hati hiyo, iliyotiwa saini Februari 21, mwaka 1992, upande wa serikali uliwakilishwa na mmoja wa mawaziri wake waandamizi wa wakati huo.

Makubaliano hayo yalifanyika kwa kuzingatia mambo kadhaa, ambayo ni pamoja na hali ya uchumi nchini kutomudu kuiwezesha serikali kutoa huduma za elimu na afya kwa kiwango bora.

Msingi mwingine wa makubaliano hayo ni makanisa kuhakikishiwa kuwa serikali itaweka mazingira mazuri kwao kutoa huduma za elimu na afya.

Makubaliano hayo yamegawanywa katika maeneo makubwa mawili, ambayo ni sekta ya elimu na afya na kila sekta ikiwa imetengenezewa bodi yake ndani ya mtandao wa makanisa kupitia CCT na TEC.

Kwa mfano, sehemu ya kwanza ya hati ya makubaliano hayo, kifungu cha kwanza, kinaeleza kuwa makanisa yataanzisha kamisheni ya uratibu wa utoaji huduma hizo.

Katika kifungu hicho cha kwanza, sehemu ‘a’ hati hiyo inaeleza kuwa jukumu la kamisheni hiyo ni kuandaa sera zinazohusiana na huduma za afya na elimu zinazotolewa na makanisa.

Kifungu kidogo cha nne, sehemu hiyo ya kwanza ya hati hiyo, kinaeleza kuwa kamisheni hiyo itakuwa ikiratibu na kusimamia matumizi ya fedha, mikopo kwa ajili ya kuboresha huduma za elimu na afya.

Hati hiyo pia inaeleza kuwa wajumbe wa kamisheni hiyo watatoka katika CCT na TEC na mashirika wafadhili na kwamba ni lazima shughuli zote ziendeshwe kwa mujibu wa sera na sheria za nchi.

Serikali kupitia hati hiyo pia imekubaliana na makanisa kuanzishwa kwa Mfuko wa Huduma za Kijamii ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kupokea mikopo na misaada.

Pia kwa upande wa elimu, serikali ilikubali kutoa nafasi za masomo ya mafunzo wa ualimu kwa wanafunzi wa ualimu.

Soma zaidi

Thursday, July 23, 2009

Bakwata: Waraka wa Kanisa ni safi

WAKATI kukiwa na mjadala kuhusu mashirika ya dini kutoa elimu ya uraia, Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Shehe Suleimani Lolila, amesema elimu hiyo ni haki ya jamii na kwamba itasaidia kupatikana viongozi bora.

Amesema mpaka sasa, Bakwata imeshatoa elimu hiyo katika wilaya zipatazo 16 katika mikoa ya Pwani, Iringa, Dodoma na sasa elimu hiyo itaanza kutolewa mkoani hapa. Shehe Lolila alisema hayo juzi wakati akizungumza na viongozi wa Bakwata kutoka Nachingwea, Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini, Lindi Vijijini na Kilwa.

Awali Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Larry Andre, ambaye alikuwa katika mazungumzo hayo, alisema Marekani imetoa msaada wa Sh milioni 38, kuisaidia Bakwata kutoa elimu hiyo kwa jamii mwaka huu. Balozi Andre alisema fedha hizo zilitolewa na watu wa Marekani ili kudumisha demokrasia ya kweli ambayo italeta amani ndani na nje ya nchi.

Alisema elimu hiyo inahusisha zaidi kufahamu utawala bora, sheria, Katiba, uwajibikaji na haki ya jamii kusikilizwa na kumchagua kiongozi bora atakayeonekana anafaa. Aliongeza kuwa nchi nyingi zinakuwa katika uchaguzi baada ya muda kunatokea vurugu, hali inayosababishwa na uelewa mdogo wa elimu hiyo.

“Mimi nimekaa nchi nyingi za Afrika, utaona mwananchi anakwenda kupiga kura akiwa mnyonge na hana furaha yoyote ile kutokana kutokuwa huru. Hali hiyo inasababishwa na ufahamu mdogo wa elimu ya uraia,” alisema Balozi huyo.

Soma zaidi

Tuesday, July 21, 2009

Wakatoliki waliwaita 'vigogo' kuandaa ilani

-Wamo wa mahakama, wabunge
-CCM ilialikwa lakini haikuhudhuria
-Mafisadi waelezwa hawatapona
WAKATI mjadala mkali ukiibuka kuhusiana na nyaraka zilizotolewa na Kanisa Katoliki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, imefahamika kwamba baadhi ya vigogo ndani ya serikali na vyama vya siasa walishirikishwa katika hatua za awali za maandalizi yake.

Raia Mwema limefahamishwa kwamba maandalizi ya nyaraka hizo ikiwa ni pamoja na Ilani ya Mapendekezo ya Vipaumbele vya Taifa, yalifanyika kwa kuwapo vikao vya pamoja kati ya wanataaluma wa kanisa hilo na wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta nyingine.

Nyaraka hizo ambazo tayari zimekabidhiwa ofisi nyeti nchini, ambazo ni Ikulu, Mahakama, Bunge, Ofisi ya Waziri Mkuu na vyama vya siasa, kwa ajili ya kufanyiwa kazi, zimeibua mjadala zaidi baada ya kuanza kuandikwa na Raia Mwema baadhi wakikerwa na jinsi taarifa kuhusiana na nyaraka hizo zinavyoripotiwa.

Ndani ya nyaraka hizo, pamoja na mambo mengine, kumesisitizwa kwamba kutenda haki ni zaidi ya kufuata sheria na taratibu, na watawala sio mabosi mbele ya watu.

Baadhi ya washiriki katika vikao vya maandalizi wanatajwa kuwa ni pamoja na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, baadhi ya wabunge, maofisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na baadhi ya vyama vya siasa. Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho chama tawala hakikushiriki licha ya kualikwa kama chama tawala.

Mjadala wa kwanza wa maandalizi hayo unaelezwa kufanyika Mei, mwaka huu na kwamba kutakuwapo na muendelezo wa mijadala na vikao katika siku zijazo kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama Cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT), Joseph Ibreck, kati ya Agosti na Septemba, mwaka huu, makundi ya kijamii yatapata fursa ya kujadili juu ya mrejesho (reflection) wa ilani hiyo. CPT ndio waliokuwa waratibu na waandaaji wa nyaraka hizo kwa Baraka zote za Kanisa Katoliki.

"Kalenda inaonyesha kuwapo kwa forum (jukwaa la majadiliano) Agosti au Septemba, mwaka huu kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi, NGOs, wanahabari," alisema Ibreck na kuongeza kuwa;

Soma zaidi

Monday, July 20, 2009

CELEBRATION OF THE LIFE OF PROFESSOR HAROUB MIRAJI OTHMAN AT THE UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM


Tahir, son of Prof. Haroub Othman speaks today during a special commemoration day to celeberate his father's life at the University of Dar es salaam Nkrumah Hall. Tahir amazed the well attended function for turning out to be a good orator, like his father, sending gasps of awe across the famous hall, especially when he declared that like his father, he would like to work as Tanzania's ambassador to Palestine, an ambition he said Prof. Haroub sadly could not live to fulfill as he was a staunch believer of having a Palestine free state.

Wednesday, July 15, 2009

JK ateua majaji wa mahakama kuu wapya 10

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, ameteua Majaji Wapya Kumi (10) wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uteuzi huo ulianza Juni 26, mwaka huu, 2009.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo Jumatatu Ikulu, Dar es Salaam imewataja majaji hao kuwa ni Bwana Ferdinand Leons Katipwa Wambali, aliyekuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani; Bibi Eliamnani Godfrey Mbise, aliyekuwa Msajili Mahakama Kuu na Bibi Sekela Cyril Moshi, aliyekuwa Mkurugenzi Mahakama za Wilaya hadi Rufani.

Wengine ni Bibi Fatuma Hamisi Masengi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Mahakama za Mwanzo, Bwana Sivangilwa Mwangesi, aliyekuwa Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama ya Rufani; Bibi Pellagia Barnabas Khaday, aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani na Bwana Moses Gunga Mzuna, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Iringa.

Taarifa hiyo iliwataja Majaji wengine wapya wa Mahakama Kuu kuwa ni Bibi Hamisa Hamisi Kalombola, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Mbeya; Bibi Fredrica William Mgaya, aliyekuwa Msajili Wilaya Mahakama Kuu, Mwanza na Profesa Ibrahim Hamisi Juma aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

Monday, July 13, 2009

Mwezesheni mwanamke kuleta maendeleo-Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewataka wananchi kuwekeza zaidi katika kulinda uwezo wa kipato kwa mwanamke hasa watoto wa kike kwa kuwapeleka shule na kuwapatia taarifa zinazowawezesha kukua na kumaliza masomo yao katika misingi imara ili wachangie kuondoa umaskini.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati wa maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani yaliyofanyika Kkitaifa Mkoani Shinyanga.

Pinda alisema endapo jamii ikimwezesha mwanamke katika kuleta maendeleo ya jamii hasa kwa wale wenye kipato cha chini kutasaidia kuondoa umaskini na kuleta maendeleo endelevu ya Taifa.

Pinda alisema kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu duniani inayokadiriwa kufikia billioni 6.77 na kwamba katika idadi hiyo inakadiriwa kuwa wanawake ni zaidi ya nusu, ni dhahiri kuwa maendeleo ya dunia yatapata misukosuko zaidi.

Alisema kuwa maadhimisho haya yanatoa tathmini kwa Taifa mafanikio ya juhudi pamoja na mikakati katika kumwekeza mwanamke na kuhakikisha kuwa mwanamke anapewa nafasi inayostahili katika kumwezesha kushiriki katika kujiletea maendeleo.

Waziri Pinda alisema kulingana na kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani kwa mwaka huu inayosema kukabiliana na mtikisiko wa uchumi duniani:kuwekeza katika kuwaendeleza wanawake ni chaguo sahihi, inaelezea umuhimu wa mwanamke katika kumwendeleza kwa lengo la kuinua maendeleo ya jamii.

Mkoa wa Shinyanga una watu milioni 3.6 na ndio mkoa unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu tofauti na mikoa mingine ukifuatiwa na mkoa wa Mwanza.

Friday, July 10, 2009

Ni uwekezaji au ukaribishaji upya ukoloni?

-Hekta milioni 6 za ardhi Afrika zimeshamegwa kwa wageni
MWANZONI mwa Julai mwaka huu, mawaziri wa kilimo barani Afrika watakutana kujadili pamoja na mambo mengine, uwekezaji katika kilimo.

Mkutano huu utafanyika miezi michache tu baada ya Tanzania kushinikizwa na baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuifanya ardhi iwe mali ya kila mwanajamii bila kujali mipaka ya nchi.

Ajenda ya kuifanya ardhi kuwa ya mali stahiki ya kila mwana Afrika ya Mashariki ilikuwa na jambo lililojificha; nalo ni ile dhana ya ukoloni mambo leo.

Baada ya ajenda ya mwaka 1885 iliyoligawa bara la Afrika (kule Berlin, Ujerumani) kwa wakoloni na kufuatiwa na harakati za uchimbaji wa madini (Gold Rush)za miaka ya 1900, sasa ardhi ndiyo lulu na tunu inayokimbiliwa kwa kasi na raia kutoka nje ya nchi katika jina la wawekezaji.

Katika kipindi cha miaka miwili tu iliyopita (2007-09) zaidi ya hekta milioni sita na ushee barani Afrika, zimemegwa na kupewa wanaojiita wawekezaji kutoka Ulaya, China, India, Arabuni na Korea.

Nchi za Uingereza, China, Falme za Kiarabu, India na Korea ya Kusini ndizo nchi zinazoongoza kwa kuingia mikataba ya uwezekaji katika ardhi katika nchi za Afrika.

Lengo kuu la wawekezaji hao ni kuzalisha chakula na nishati ya mafuta itokanayo na mimea (biofuel). Wenye uchungu na Afrika wanawaita “wakoloni mambo leo” ingawa watawala wengi wa Afrika wanawaita “wawekezaji”. Tofauti ya maneno haya inatokana na dhana na nia ya wageni hao wanaokuja Afrika-kama wanakuja kuchuma na kuondoka au ni wadau wa maendeleo wa Waafrika?

Huko Sudan, kwa mujibu wa taasisi ya kimataifa ya mwenendo wa kiuchumi (Economic Bureau) ya Uingereza, kwa mwezi Mei 2009, Korea ya Kusini imepata hekta 690,000 za ardhi kwa ajili ya kilimo cha ngano. Sio ngano ya wana-Sudan; la hasha ni ya Wakorea.

Falme za Kiarabu tayari zinalima hekta 30,000 na majuzi imeongeza hekta 378,000 kulima mtama, nyasi za ng’ombe, ngano, viazi na maharage kwa ajili ya wananchi wake.

China nayo imepewa hekta milioni 2.8 huko Congo (Brazaville) ili kuanzisha shamba kubwa zaidi la michikichi duniani na bado imo mbioni kuitaka Zambia iipe hekta milioni mbili kwa ajili ya kulima mibono (minyonyo).

Hapa Tanzania bado hakuna wawekezaji wakubwa katika kilimo kama ilivyo katika nchi hizo, lakini viwango vya ukubwa wa eneo la kulima vinazidi kukua kila siku.

Mamilioni ya hekta za ardhi nzuri huko Morogororo, Rukwa, Tabora, Lindi, Pwani, Kigoma, Manyara na Ruvuma yameanza kukodolewa macho, na yataendelea kukodolewa na wanaojiita wawekezaji kwa kushirikiana na baadhi ya wenye dhamana hapa nchini.

Tayari bonde la mto Kilombero, mkoani Morogoro, limeanza kunyemelewa kwa kasi na wawekezaji na wananchi wameanza kulionja joto na adha ya uwekezaji wa kilimo cha sukari na mpunga.

Kwa nini wawekezaji hao wanakuja Afrika na sio Asia au Marekani ya Kati au Kusini? Sababu ni kuwa Afrika ndilo bara pekee lililosalia na ardhi nzuri inayoweza kulimwa kila zao kwa gharama ndogo. Ni bara ambalo mwekezaji anahitaji kuja na mkoba mtupu na pesa kiduchu kulala hotelini siku tatu tu na baada ya muda mfupi anakuwa bilionea.

Mataifa ya nje yanataka kupata faida kubwa ya kuuza chakula na mazao ya mafuta (petroli inapanda bei) wakati huu ambapo uhaba wa chakula na mtikisiko wa uchumi ndizo ajenda za kila siku za kimataifa na kitaifa.

Nchi za nje ya Afrika zinakuja kulima Afrika ili kuwalisha watu wao na ziada ikiuze tena kwenye nchi hizo hizo zinazowakaribisha kulima! Hata mafuta ya mitambo na magari yatokanayo na mimea inayolimwa barani Afrika, yatauzwa tena kwa nchi waalika.

Tangu kuanza kushuka kwa uzalishaji wa chakula kati ya 2007/08 na ongezeko la idadi ya watu kwa asilimia tatu tangu 1945, ardhi haijaongezeka kwa eneo. Akiba ya chakula duniani imeshuka kutoka ya siku 116 mwaka 1995 hadi akiba ya siku 57 mwaka 2008, alibainisha Gwynne Dyer mwanahabari wa Economic Bureau.

Ndiyo maana nchi za wenzetu “wenye akili” zimeanza kuja Afrika kulima wakati sisi Waafrika tukiendelea kuimba nyimbo za “kilimo kwanza” na ‘kuruka hewani kwa kutumia ungo’, au kupigana wenyewe kwa wenyewe. Wao watakapokuwa wanavuna sebuleni kwetu, sisi Waafrika tutakuwa tunaugulia njaa, umaskini na kuomba chakula na mafuta! Kweli wajinga ndio tuliwao. Tutaanzishaji Kilimo Kwanza kabla ya kutathmini Siasa ni Kilimo” ?

Kama China itaendelea na sera yake ya kuwatawanya raia wake milioni 5 kila mwaka hasa barani Afrika, ni dhahiri kutakuwa na msukomo wa kupata ardhi kupitia kwa watawala wenye kutafuta ufadhili binafsi na wa familia zao tu - yale yale ya akina Chifu Mangungu wa Mvomero! Lesotho tayari ina raia wa kichina zaidi ya 150,000; huku yenyewe ikiwa na wananchi milioni 1.8 tu.

Kwa upande wa pili, kumekuwa na wawekezaji wachache sana katika kilimo. Haishangazi kuona takwimu za Vituo vya Uwekezaji kama cha Tanzania (TIC) vina taarifa finyu za wawekezaji wanaolima kuliko waliojikita katika fani nyingine za utalii, biashara na madini. Wapo wanaoogopa kuwekeza katika kilimo kwa hofu ya kuogopa yale ya mwaka 1967 yalipotaifishwa mashamba makubwa. Lakini hawataki walime halafu Tanzania ijitosheleze kwa chakula. Watatuhadaa vipi tukishiba?

Lakini kwa jinsi upepo unavyokwenda, utakaposikia Falme za Kiarabu, India, China, Korea na wengine wanataka kupewa mamilioni ya hekta, basi ujue kiama kimekaribia.

Kwa nini kiama? Kwanza, wageni hawafahamu sana aina ya migongano iliyopo kati ya watawala wa nchi na wananchi kuhusu ajira na ardhi kama rasilimali yao kuu hasa kwa vijana. Wageni watakapoanza kununua ardhi kwa wingi, vijana wa kiafrika nao hawatakubali na watafanya mawili: ama kuwavaa wageni au kuwapa wakati mgumu viongozi wao kwa kuwapa wageni ardhi ya mababu zao.

Vijana wao hawatakubali kukosa ajira, elimu, afya bora, na sasa hata ardhi. Wataanzisha mapambano dhidi ya watawala na wageni.

Kabla ya kufikia hatua hiyo, inafaa sasa watawala wa Afrika ikiwemo Tanzania watambue kuwa wawekezaji wa nje katika ardhi wanataka kulima kwa ajili ya chakula chao na kupitia mazao kupata mafuta ya mitambo na magari kwa bei poa. Lakini hawatalima tu, kuna siku watakuja kuishi wao na watoto wao.

Watakapokuwa wanajadili mipango ya uwekezaji katika kilimo mwezi Julai mwaka huu, mawaziri wa Afrika watambue mwelekeo wa dunia na mikakati ya mataifa ya nje ya kurubuni bara la Afrika katika jina la uwekezaji.

Afrika ikae chonjo kweli kweli na mwelekeo huu wa mamilioni ya ardhi yetu kuhodhiwa na wageni huku tukiendelea kuzaa ili tusije kuwa na ulazima wa kukaribisha awamu ya pili ya mapambano mbele ya safari ndani ya nchi kati ya wasio na ardhi na wawekezaji ardhi.

Chanzo: RaiaMwema

Utenzi wa Haroub Othman

Hapa hakuna kulia
Japo ni kali hisia
Janga lilotufikia
Lino limepindukia

Katika za sasa zama
Tumezipata zahama
Mwenzetu anapohama
Kutuachia dunia

Ni wengi walotutoka
Walotambuka mpaka
Na huko walikofika
Tumeshawasabilia

Jeraha lilo moyoni
Na fundo lilo kooni
In’sani hatuoni
Tutavyoyavumilia

Ela tujipe nafasi
Tupunguze zetu kasi
Mola tusije muasi
Kwa chazi lilozidia

Kenda zake kwa Manani
Atakayebisha nani
Ilobaki ni kuhani
Wale waliobakia

Harubu kenda harudi
Ndiyo yetu sote sudi
Kifo kwetu sote budi
Ahadi ikiwadia

Ela tukome kulia
Matama kujishikia
Tuweze kufurahia
Urithi alotwachia

Japo hakuna rufaa
Kaenda ali shujaa
Na nyingi zake shufaa
Rijali alotimia

Harubu alo azizi
Katimiza yake kazi
Bila kufanya ajizi
Sote tumemridhia

Mwanazuoni mahiri
Wanojua wamekiri
Kaacha wake muhuri
Kila alikopitia

Kawafunza wengi wana
Kwa mawazo yenye kina
Bila kufanya hiyana
Na wala kujivunia

Aliwapenda talibu
Naye hakuwapa tabu
Kuwaonyesha vitabu
Vitavyowasaidia

Nje ya lake darasa
Vichwa alivitakasa
Akijadili siasa
Nchini pia dunia

Alipinga ubeberu
Siasa za makaburu
Akitetea uhuru
Wa insani jumuiya

Tulochunguza kwa dhati
Twajua yake sauti
Mashariki ilo Kati
Akitufafanulia

Wahanga wa Palestina
Na Amerika Latina
Walijua lake jina
Kazi alowafanyia

Mzanzibari halisi
Hakupoteza nafasi
Kuwanasihi watesi
Ghadhabu kupunguzia

Upemba na Uunguja
Hakuiona ni hoja
Nyie nyote ni wamoja
Na mimi ni wenu pia

Muhimu tutende haki
Tusitumie bunduki
Wala pinde na mikuki
Hazitufai ghasia

Lino sanduku la kura
Ndiyo njia ya busara
La sivyo twala hasara
Tutaja likumbukia

Masanduku msibebe
Kura hizo msiibe
Acheni wenu ubabe
Harubu kawaambia

Raia wakihamaki
Wakidai zao haki
Mbona mwaleta mikiki
Moto kuwafyatulia

Wakubwa hakuogopa
Ukweli wao kuwapa
Na waliotoka kapa
Hilo wamejitakia

Kituo ameanzisha
Raia kuwakumbusha
Ari zao kuamsha
Waweze jisimamia

Iko siku inakuja
Wapemba na Waunguja
Watapeana faraja
Harubu alinambia

Leo kinachotuzuga
Na akili kuvuruga
Siasa za lugaluga
Bado twazishabikia

Umma utapoamka
Na hekima kucharuka
Dunia itazinduka
Kuja kutushangilia

Kwa upole akinena
Hajawahi kutukana
Alikuwa muungwana
Wote wanashuhudia

Letu si kuomboleza
Bali ni kumpongeza
Ngwe yake kamaliza
Nyingine katuachia

Kazize tuendeleze
Kiporo tusikilaze
Mpaka nchi ipendeze
Alivyokiitakia

Tumshukuru Saida
Kwa alotupa faida
Mume aso kawaida
Umma kuutumikia

Salamu, binti Yahaya
Pokea za jumuiya
Kwa hii kubwa hidaya
Uliyotutunukia

Ya Harubu buriani
Buriani ya Harubu
Ya Harubu buriani
Sote twakushangilia

Utenzi na: Jenerali Ulimwengu

Thursday, July 9, 2009

EWURA yatangaza kupanda bei ya mafuta

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA)imetangaza kupanda kwa bei za rejareja kwa aina zote za mafuta nchini. Taarifa ya Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Haruna Masebu imesema kuwa bei ya Petroli imepanda kwa asilimia 4.00, Dizeli (5000 ppm) asilimia 4.74, Dizeli (500 ppm) asilimia 3.55 na mafuta ya taa asilimia 7.93.

Taarifa hiyo imesema mabadiliko haya ya bei za mafuta yametokana na mabadiliko ya bei katika soko la dunia na kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani. Hata hivyo, amesema kuwa Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo ya asilimia 7.5 ya bei elekezi kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na EWURA hatimaye kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali No. 5 la tarehe 9 Januari 2009.

Mkurugenzi huyo amewataka wanunuzi kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, ambayo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo mteja atauziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.

Monday, July 6, 2009

Mwafaka basi- CUF

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema suala la Mwafaka wa kisiasa kati yake na Chama Cha Mapinduzi (CCM), limekwisha na walikuwa wakijipanga, na sasa wako tayari kuwapa Watanzania fursa ya kuchagua Dira ya Mabadiliko na kuitumia kuongoza harakati za kuing’oa madarakani CCM kupitia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Aidha, chama hicho kimeeleza kushangazwa na hatua ya CCM ‘kuchumpa’ katika suala la kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini, suala ambalo liliwekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala ya mwaka 2005, na katika siku za karibuni, kuzua mjadala nchini.

“Mwafaka ulikwisha. Tulikuwa tumeshafikia makubaliano na wenzetu na kilichobaki ni ceremony (sherehe) za kusaini Mwafaka, lakini wenzetu wakachumpa. Hatuzungumzii tena suala hili. Tutaicheza ngoma kwa kadri itakavyokuwa inadundwa,” ilikuwa kauli ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipozungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ‘Operesheni Zinduka’.

Profesa Lipumba akiwa na viongozi wengine wakuu wa CUF, alisema suala la Mwafaka halina nafasi tena, bali chama hicho kitakabiliana na mambo kwa kadri yatakavyokuwa yakitokeza, lakini muhimu kwa sasa ni kuwapelekea wananchi Dira ya Mabadiliko ambayo inatilia mkazo mambo 13.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kila raia popote alipo kuwa na haki ya kuchagua na kuchaguliwa kuwa kiongozi; kujenga umoja wa kitaifa wa kweli; kuhakikisha kuwa kila mwananchi ana uwezo na anawezeshwa kupata milo mitatu kwa siku; kuhakikisha kuwa kila raia ana haki na anapata huduma za msingi za afya; kujenga maadili ya kuwaheshimu na kuwaenzi wazee na watoto wote wa Tanzania wawe na haki ya kupata elimu bora ya msingi na ya sekondari.

Mambo mengine ni motisha maalumu utolewe kwa wasichana na familia zao ili wamalize elimu ya msingi na waendelee na sekondari; kuwaelimisha wasichana na wanawake washiriki katika soko la ajira; Taifa litoe kipaumbele maalumu katika kuendeleza elimu ya sayansi na teknolojia.

“Kujenga uchumi wa kisasa wenye ushindani wa kimataifa na utakaohimili misukosuko ya utandawazi; wananchi wahisi na waone kuwa uchumi wa Taifa unatoa fursa kwa wananchi wote; kukuza uchumi na kuongeza ajira na kuwapo kwa uongozi imara na utawala bora katika kukuza uchumi,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza kuwa CUF imeandaa dira huyo ya kuleta mabadiliko kupitia mijadala.

Alisema kwa kuanzia, CUF itazindua ‘Operesheni Zinduka’ Julai 11, mwaka huu katika Jiji la Mwanza, na itafanya kampeni hiyo kwa awamu ya kwanza katika mikoa 11 ya Bara itakayohusisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Tabora na Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Mbeya na Morogoro.

Alisema CUF itaongoza kampeni hiyo ya mabadiliko kwa sababu ndicho chama kikuu cha upinzani Tanzania, kiko imara na kina viongozi makini. “Vyama vingine vya siasa vimejionyesha kuwa ni vyama vilivyopo kwa maslahi ya viongozi wake wachache wanaovifanya kama ni miliki yao na ambao hawawezi kuhojiwa na hivyo kupelekea vyenyewe kuzama katika ufisadi na kushindwa kujiendesha.

Vingine ni dhaifu na visivyo na mtandao wa kitaifa wa kuweza kuleta mabadiliko ya maana yatakayoleta tija,” alisema Lipumba na kuongeza: “Kwa chama makini cha siasa kinachopigania mabadiliko, kufichua maovu na ufisadi au kwa lugha ya mtaani ‘kulipua mabomu’ pekee hakutoshi kuleta ukombozi wa kweli wa Mtanzania. Kauli za hamasa na jazba ni muhimu kuwapa wananchi ari ya kujiletea mabadiliko katika maisha yao.”

Alisema mabadiliko wanayotaka Watanzania hayawezi kuja kwa njia za kushitukiza na kuongeza kuwa “Watanzania wanastahili kuwa na Dira ya Taifa ya kujenga nchini inayoheshimu haki za binadamu, yenye misingi mizuri ya demokrasia ambapo raia wote watu wazima wenye akili timamu wana haki ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa masuala yanayohusu maisha yao na hatma ya nchi yao.”

Akijibu maswali mbalimbali ya wahariri, Profesa Lipumba alisema CUF itaendelea kudai Katiba na Tume huru ya uchaguzi, huku akimtupia lawama Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Lewis Makame akidai ni ‘goigoi’ ambaye atastaafu wadhifa huo akiwa hana la kukumbukwa.

Aligusia suala la Mahakama ya Kadhi, akisema, “Hili limewekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM, na wenzetu, tena wasomi baada ya kuisoma wakasifu sana, lakini sasa wanachumpa. Hili litaleta vurumai.”

Aidha, Profesa Lipumba pia alimsifu Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM) kwa hoja yake bungeni kuhusu mgawanyo wa fedha za barabara, ingawa alisema kumekuwa na vituko vingi bungeni kutoka kwa wabunge wa chama tawala katika michango yao hivi sasa.

Kuhusu Operesheni Zinduka na pigo la hivi karibuni la CUF kuondokewa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, Wilfred Lwakatare aliyehamia Chadema, Profesa Lipumba alisema muhimu ni kujenga chama kama taasisi na siyo kutegemea sifa ya mtu binafsi.

“CUF inaamini katika kujenga chama kama taasisi, chama ni demokrasia, personality ni muhimu katika siasa, lakini chama kijengwe kama taasisi, ili anapoondoka mtu hakiathiriki. Hili la kuondoka kwa watu tunaowajenga, linasikitisha, linanifedhehesha, lakini huwezi kulikwepa,” alisema mchumi huyo.

Thursday, July 2, 2009

Washitakiwa mauaji ya albino kuanza kujitetea

Upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji ya albino inayoendelea Mahakama Kuu inayoketi mjini Kahama imefunga ushahidi wake baada ya shahidi wa 15 kutoa ushahidi na kielelezo cha ungamo la mshitakiwa wa tatu, Charles Kalamuji (42) na leo unaanza kusikiliza upande wa utetezi.

Akitoa taarifa ya kufunga ushahidi huo mbele ya Jaji Gabriel Rwakibalila, wakili mwandamizi wa serikali, Neema Ringo, alisema upande wa Jamhuri sasa hauna shahidi mwingine.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Masumbuko Madata wa kijiji cha Ituga na wenzake Emmanuel Masangwa wa kijiji cha Bunyihuna na Charles Kalamuji wa kijiji cha Nand Wilayani Bukombe kwa kumuua kwa makusudi mtoto albino, Matatizo Dunia (13) katika kijiji cha Bunyihuna.

Shahidi wa 15 katika kesi hiyo, F296 Sajenti Nasibu, aliwasilisha maelezo ya mshitakiwa wa tatu, Charles Kalamuji aliyoyatoa polisi kama kielelezo cha 15 na mahakama ilikubali kuyapokea licha upande wa utetezi kutoa pingamizi ambalo hata hivyo lilitupiliwa mbali. Mbali na washitakiwa kujitetea, mashahidi wengi wanatazamiwa kuwa ndugu zao.

CHANZO: NIPASHE

‘Jeneza’ la Tarime, Rorya lachongwa

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametangaza azma yake kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuzifuta wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara, kutokana na viongozi wa wilaya hizo kushindwa kusimamia amani.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati akihutubia maelfu ya wananchi na viongozi wa wilaya, mikoa, halmashauri na manispaa nchini, walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Sherehe za Serikali za Mitaa kitaifa ambazo zilifanyikia mkoani Mara.

Waziri Pinda ambaye alionesha kukasirishwa na mapigano ya koo na makabila mkoani humo, alisema serikali imechoka kuona maisha ya watu yanapotea na mali zao kuharibiwa huku viongozi wakiwapo, lakini wameshindwa kusimamia wananchi wao kwa kuwakalisha chini na kumaliza tofauti zao na kuishi kwa amani na utulivu kama ilivyo mikoa mingine.

Sambamba na kutishia kuzifuta wilaya hizo na kuteua wanajeshi kuziongoza, alitoa miezi sita ya huruma kwa wakuu wa wilaya hizo na wa halmashauri, kuhakikisha wanaandaa taarifa za mikakati yao ya kukomesha mapigano ya koo chini ya uratibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Enos Mfuru, vinginevyo hawatakuwa na kazi.

Pinda alisema kwa mwaka jana pekee yalikuwapo matukio 66 ya mapigano ya koo ambapo ng’ombe 601 waliporwa na watu wengi kupoteza maisha.Na katika mapigano ya sasa baina ya watu kutoka Tarime na Rorya, alisema watu 32 wamekufa, zaidi ya nyumba 400 zimechomwa moto na watu zaidi ya 3,000 hawana makazi kutokana na upuuzi wa wizi wa ng’ombe watano ambao kati yao watatu walipatikana na kuzua balaa la vita.

Alieleza mikakati ya kukomesha uhalifu katika wilaya hizo kuwa ni kuanza utekelezaji wa kuzifanya Tarime na Rorya kuwa mikoa ya kipolisi, kuanzisha kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Tarime, kudhibiti fujo na wizi wa mifugo.

Mikakati mingine ni ya kuimarisha barabara za mipakani na kuwasisitizia viongozi wasikwepe majukumu ya kufanya wilaya hizo zikalike. “Nasema suala hili si la kuchezea hata kidogo, Rorya Rais kamweka mwanajeshi mstaafu na Tarime tumempeleka kada wa CCM, kama anapwaya tutambadilishia kituo cha kazi apelekwe mwanajeshi,” alisema Pinda.

Wednesday, July 1, 2009

HITMA ZA KUMUOMBEA PROFESA HAROUB OTHMAN KUSOMWA DAR KESHO


Marehemu Profesa Haroub Othman

HITMA MBILI KUMUOMBEA MAREHEMU PROFESA HAROUB OTHMAN ALIYEFARIKI MAJUZI NA KUZIKWA HUKO ZANZIBAR ZITAFANYIKA KATIKA MISIKITI MIWILI TOFAUTI JIJINI DAR KESHO ALHAMISI. NDUGU, JAMAA NA MARAFIKI MNAALIKWA KUHUDHURIA.

KWA MUJIBU WA MWANA WA MAREHEMU, TAHIR OTHMAN, HITMA YA KWANZA ITAFANYIKA KESHO ALHAMISI SAA KUMI NA MOJA JIONI KATIKA MSIKITI WA NGAZIJA ULIOPO MTAA WA MAKJUNGANYA KATIKATI YA JIJI LA DAR.

TAHIR AMESEMA HITMA INGINE ITAFANYIKA HIYO HIYO KESHO ALHAMISI BAADA YA SALA YA I'SHA (BAADA YA SAA MBILI USIKU) KATIKA MSIKITI WA MASJID MA'AMOUR ULIOPO UPANGA JIJINI DAR.

FAMILIA YA MAREHEMU PROFESA HAROUB OTHMAN INATOA SHUKRANI NYINGI SANA KWA NDUGU, JAMAA NA MARAFIKI KWA MSAADA MKUBWA MLIOTOA WAKATI HUU WA MAJONZI.

NI VIGUMU KUMSHUKURU MMOJA MMOJA NA SI RAHISI KUFANYA AMA KUSEMA LOLOTE ZAIDI YA KUMUOMBA MOLA AWAONGEZEE, MAANA YEYE NDIYE MPANGAJI WA YOTE.