Monday, August 29, 2011

UN Women yatakiwa kusaidia kwa wakati

WABUNGE wanawake wamelitaka shirika la UN-Women kutekeleza nia yake ya kuwasaidia wanawake kwa wakati.

Walitoa mwito huo hivi karibuni mjini Dodoma wakati wa semina iliyoandaliwa kwa ajili ya kuelezea masuala mbalimbali yanayotekelezwa na shirika hilo.

Walisema imebainika kuwa shirika hilo limekuwa likijitokeza kuwasaidia wanawake wanaohitaji msaada dakika za mwisho wakati wakiwa wametatua matatizo yao au kuchukua hatua nyingine.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia alisema licha ya kuomba msaada wa mafunzo kutoka katika shirika hilo mapema kwa ajili ya masuala ya kampeni, halikuwasaidia chochote kutokana na ukweli kuwa lilijitokeza dakika za mwisho wakati wanawake wagombea wakiwa wamemaliza sehemu kubwa ya maandalizi yao.

“Kwa kweli mimi sioni kama UN-women linatusaidia kwa sababu mwaka jana kwa mfano lilikuja kutoa mafunzo mwishoni wakati uchaguzi wa madiwani ulioshirikisha wanawake ukiwa umemalizika. Mafunzo yao kwa kweli hayakuwa na msaada kwa sababu yalitolewa yakiwa yamechelewa,” alisema Ghasia.

Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini, alisema, “Hata msaada wa kifedha nao pia kuupata kutoka kwao ni tatizo sasa sijui labda watueleze wapo kwa ajili ya nani na ni kwa nini wanakuja kutuletea misaada hiyo ikiwa imepitwa na wakati?”

Mbugne wa Viti Maalumu, Regia Mtema (Chadema) alihoji sababu ya shirika kuishia kutoa mafunzo yake kwa wanawake waliokwishapata ufahamu hususan wabunge wakati waliopo vijijini ambao ndio wenye kuhitaji zaidi misaada ya UN Women hawawaoni.

Alisema asilimia kubwa ya wanawake wanaoandamwa na athari za mila mbaya , mfumo dume na unyanyasaji wa aina mbalimbali wa kijinsia wapo vijijini lakini shirika hilo haliwafuati na kudhani linamsaidia mwanamke wa Tanzania kwa kuonana na wachache wa mijini ambao hata hivyo wanauelewa mpana wa namna ya kuepuka au kupambana na unyanyasaji huo.

Akitoa maelezo kwa niaba ya shirika hilo, mwezeshaji wa semina hiyo ambaye pia ni Meneja wa Programu, Anna Falk alisema lengo lao la dhati ni kuwasaidia wanawake.

Alisema huchelewa kujibu maombi yao kwa vitendo kutokana na kucheleweshewa fungu au mahitaji ambayo yanakuwa yanaombwa na wanawake hao kutoka kwa mfadhili wao.

Alisema wao ni shirika dogo na hawana uwezo wa kifedha kiasi cha kutoa misaada inapotakiwa. “Lakini hilo tumeliona sasa tutajaribu kuwahimiza wanaotupatia fungu kufanya hivyo mapema ili nasi tuwe na faida kwenu wanawake wa Tanzania,” alisema.

Alisema UN-Women ina watendaji wachache hivyo ni vigumu kufika hadi vijijini kwenye wanawake wanaoathiriwa na vitendo vya unyanyasaji.

“Tunajua tukiwapa mafunzo wanawake viongozi tunakuwa tumewafundisha wanawake wa vijijini pia, lakini hata hivyo tutaangalia namna ya kulitafutia jibu pendekezo hilo,” alisema wakati akijibu hoja Waziri Ghasia.

Petroli yashuka, Ewura yang’ata

BEI ya bidhaa za petroli imeshuka kuanzia leo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza jana, huku ikifunga biashara ya ghala la kuhifadhi mafuta la Kobil na vituo viwili vya mafuta.

Kushuka kwa bei hiyo kumefanywa na mamlaka hiyo baada ya kupandisha bidhaa hizo wiki mbili zilizopita hali iliyozua manung’uniko makubwa kutoka kwa walaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu alisema Dar es Salaam jana kuwa kuanzia leo, petroli bei ya kikomo kwa Dar es Salaam itauzwa Sh 2,070 kutoka Sh 2,114 iliyokuwa inauzwa hadi jana.

Dizeli itauzwa kwa Sh 1,999 badala ya Sh 2,031 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,980 kutoka Sh 2,005.

Mikoani, bei ya kikomo pia itateremka kuanzia leo kulingana na umbali wa mkoa na bei ya juu ya kikomo itakuwa mkoani Kagera katika Wilaya ya Karagwe na Kigoma katika Wilaya ya Kigoma ambapo petroli lita moja itakuwa Sh 2,301, dizeli Sh 2,230 na mafuta ya taa Sh 2,211.

Bei iliyokuwepo mpaka jana ambayo ilitangazwa na Ewura wiki mbili zilizopita na kulalamikiwa na wananchi ni ya petroli kuuzwa kwa Sh 2,114 kutoka Sh 2,004, dizeli ikauzwa Sh 2,031 kutoka Sh 1,911 huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh 2,005 kutoka Sh 1,860.

Masebu alifafanua kuwa bei hizo zimeshuka kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia. Kwa bei mpya, inaonesha kuwa petroli imeshuka kwa Sh 44. 55, dizeli Sh 31.99 na mafuta ya taa yameshuka kwa Sh 25.62.

Katika soko la dunia, petroli imeshuka kwa dola 43.33 kwa pipa, dizeli imeshuka kwa dola 30.04 na mafuta ya taa yameshuka kwa dola 27.69.

Masebu alisema bei ya mafuta katika soko la ndani zingeshuka zaidi kama thamani ya Shilingi ya Tanzania isingeendelea kuporomoka dhidi ya Dola ya Marekani.

Dola ya Marekani ndio inatumika katika ununuzi ya bidha za mafuta kwenye soko la dunia.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, Dola moja ya Marekani katika soko la rejareja ilikuwa inauzwa kati ya Sh 1,616 na 1,630 hali inayoonesha kuwa sarafu hiyo inazidi kushuka thamani dhidi ya Dola.

Ewura imeendelea kutetea fomula mpya kuwa bado inaleta unafuu mkubwa kwa mlaji.

“Bei za rejareja na jumla zingepanda zaidi endapo fomula ya zamani ingeendelea kutumika,” alisema bosi huyo wa Ewura.

Alisema iwapo fomula za zamani ingeendelea kutumika, petroli kwa bei ya rejareja ingeuzwa Sh 2,249, dizeli Sh 2,179 na mafuta ya taa yangeuzwa kwa Sh 2,161.

Kwa upande wa bei ya jumla kwa kutumia fomula ya zamani, petroli ingeuzwa Sh 2,181, dizeli Sh 1,106 na mafuta ya taa yangeuzwa Sh 2,089.

Katika mazungumzo yake ya jana, Masebu aliishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kwa kutambua mchango wa Ewura wa kupanga bei kwa kuzingatia fomula mpya na mabadiliko inayoyafanya kila baada ya wiki mbili.

Katika maoni ya kamati hiyo yaliyotolewa na Mwenyekiti wake, Dk. Abdalah Kigoda wakati wa kuchangia makadirio ya bajeti ya Wizara ya Fedha, alisema Serikali ilitakiwa ifanye mkakati wa makusudi wa kutoa elimu kwa wananchi juu ya utaratibu wa bei za mafuta katika soko la dunia ambazo Tanzania haizipangi.

“Kwa kweli tunaishukuru kamati hii kwa kutambua juhudi zinazofanywa na mamlaka yetu, hii inaonyesha kuwa tunafanya mambo haya kama timu,” alisema Masebu.

Wakati huo huo, Ewura jana imetangaza kuvifungia vituo viwili kwa sababu mbalimbali pamoja na ghala moja. Ghala la Kampuni ya Kobil lililoko Kigamboni limefungiwa baada ya kubainika kuwa petroli iliyohifadhiwa humo haikidhi ubora uliowekwa na mamlaka hiyo.

Vituo vilivyofungiwa ni pamoja na cha Hass wilayani Magu Mkoa wa Mwanza, ambacho kimefungiwa baada ya kukaidi amri ya Ewura ya kukifungia na kuweka uzio; lakini wamiliki wake wakaondoa uzio huo na kuendelea kufanya biashara.

Pia kituo cha Petro kilichoko Mafinga wilayani Mufindi katika Mkoa wa Iringa kimefungiwa baada ya kuwazuia maofisa wa Ewura kuchukua sampuli za mafuta za kituo hicho.

Tuesday, August 23, 2011

TGNP YASHINDA KESI !

TGNP yashinda kesi ya Jengo
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umeshinda keshi ya madai namba 215/1997 iliyofunguliwa na waliokuwa wapangaji wa Benki ya Uwekezaji (TIB) kabla ya jengo hilo kuuzwa kwa TGNP Juni 1997.
Jengo lenye kesi ni jengo la gorofa moja zilipo ofisi za makao makuu ya shirika Mabibo Dar es salaam,
Chini ya Mheshimiwa Jaji T.B. Mihayo, 15 Oktoba 2009, TGNP Ilishinda kesi hiyo na walalamikaji walidai kuwa TGNP imependelewa. Oktoba 19, 2009, walifungua rufaa katika makahakama kuu ya Rufaa ya Tanzania, wakiipinga hukumu ya kesi ya msngi namba 215/1997 na kukawa na kesi ya rufaa namba 129/2009 ili pia waendelee kukaa kwenye jesngo hilo.
TGNP iliiomba mahakama kufuta ombi la walalamikaji la kuendelea kuwa kwenye jengo ili shirika liweze kufanya shughuli zake, kesi ambayo ilisikilizwa na majaji watatu waheshimiwa jaji Msasali, jaji Msofe, na jaji Rutakanga Julai 22,2011.
Leo tarehe 23. 08.2011, TGNP imeamua kwa mujibu wa sheria kuwatoa kwa nguvu wapangaji hao ambao kwa muda wote wa zaidi ya miaka 10 wamekuwa wakifanya shughuli zao kwenye jengo la TGNP bila kulipa kodi wala ruhusa yetu. Pamoaja na ushindi tulioupata , bado tunaendelea kuheshimu maamuzi ya mahakama kutokana na shauri walilolipeleka mahakamani.
Sote kwa pamoja tunaamini katika haki na na rasilimali lazima zirudi kwa wananachi!
TGNP

Friday, August 19, 2011

Mkurugenzi Wanyamapori asimamishwa kazi

MKURUGENZI wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid Mbangwa amesimamishwa kazi kuanzia jana kupisha uchunguzi kuhusu wanyamapori 120 na ndege 16 waliotoroshwa Novemba mwaka jana kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amelieleza Bunge kuwa, Mbangwa amesimamishwa kazi na watumishi wengine wawili wa Wizara hiyo lakini hakuwataja ili kutoathiri uchunguzi.

Maige amewaeleza wabunge kuwa, Mbangwa ataendelea kulipwa, na wote waliohusika kutorosha wanyama na ndege hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Maige, Wizara hiyo inashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza utoroshaji huo, na kwamba, watu sita tayari wameshitakiwa katika Mahakama mjini Moshi kwa tuhuma za kuhujumu uchumi.

Waziri Maige amewaeleza wabunge kuwa, ndege ya jeshi la Qatar iliyowatorosha wanyama na ndege hao ilikuja nchini kihalali kwa kuwa ilikuwa na kibali cha kumleta mwanadiplomasia nchini kwa safari binafsi.

Amesema, ndege hiyo ilionekana kwenye vyombo vya usalama, lakini haikukaguliwa wakati inaondoka na hadi sasa haijulikani wanyama na ndege hao walipelekwa wapi.

Maige amewaeleza wabunge kuwa, biashara ya kukamata wanyama na kuwasafirisha nje ya nchi ni halali, kampuni 180 zina leseni, na kwamba, waliokamata maliasili zilizotoroshwa walikuwa na vibali vyote muhimu vilivyowaruhusu kukamata na kumiliki wanyama hao lakini ukaguzi ulipofanywa hawakuonekana.

Amesema, Wizara inashirikiana na vyombo vya ulinzi na upelelezi vya kimataifa likiwemo shirika la Interpol ili kufahamu nyaraka zilizotumika kuwasafirisha wanyamapori na ndege, walipelekwa wapi na wapo kwa nani hivi sasa.

Ameomba wabunge wenye taarifa kuhusu utoroshaji huo wampe taarifa na anaamini wanamuamini, wakishindwa wawape mawaziri wengine, na endapo taarifa hizo hazitatumika ipasavyo wamuwajibishe bungeni.

Maige amesema bungeni kuwa, kutoroshwa kwa ndege na wanyama hao kumemkasirisha kuliko jambo lingine lolote katika utumishi wake wa umma.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira jana ilihoji ilichodai kuwa ni kigugumizi cha Serikali kuhakikisha kuwa wanyamapori 116 hai na ndege 16 walioibwa nchini Novemba 24 mwaka jana wanarudishwa nchini.

Kamati hiyo ililieleza Bunge kuwa, wanyama hao wakiwemo twiga wanne na ndege hai ambao wana jumla ya thamani ya Sh. 170,570,500 waliibwa kwa kutumia ndege ya jeshi la Qatar kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

Bunge lilielezwa kuwa, wanyamapori walioibwa wana thamani ya Sh. 163,732,500.00/- na ndege hai wana thamani ya Sh. 6,838,000.00/-

Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli alisema, hadi jana kamati ilikuwa haifahamu wanyama na ndege hao walipelekwa wapi na kama bado wapo hai.

Aliyasema hayo wakati anasoma taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2010/2011 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/2012.

Lembeli alisema, uharamia huo ulifanywa na Watanzania na kwamba, kigugumizi cha Serikali kushughulikia suala hilo kimeisikitisha Kamati kwa kuwa rasilimali iliyoibwa ni adimu na haijulikani itarudishwa lini nchini.

“Kwa hakika kuna dalili kubwa ya uzembe na kulindana ndani ya Wizara hii na ndiyo maana kumekuwa na kigugumizi katika kushughulikia ushauri wa kamati. Ukweli wa mashaka haya unajidhihirisha katika zoezi zima lililofanyika hivi karibuni ndani ya idara husika la kuhamisha maafisa” alisema Lembeli.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amelieleza Bunge kuwa, wanyama hai wa aina mbalimbali 120 na ndege hai 16 walitoroshwa Novemba 26 mwaka 2010 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

Thursday, August 18, 2011

Ewura yajirudi

BAADA ya kubanwa na Baraza la Mawaziri kwa kuyumbisha bei ya mafuta, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imekubali kufanya marekebisho ya fomula ya ukokotoaji, kwa kuzingatia akiba za mafuta zinazokuwa nchini wakati husika.

Uamuzi huo wa Ewura ambao unasubiri baraka za Bodi yake ndipo mchakato huo uanze, umekuja baada ya wananchi kulalamikia hatua ya Mamlaka hiyo kupandisha bei ya petroli kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita, katika kipindi cha saa 48 baada ya bei hizo kushushwa.

Baada ya Ewura kutangaza bei mpya, wananchi wengi walilaani hatua hiyo, kuwa inalenga kunufaisha wafanyabiashara na si wananchi kama ambavyo iliahidiwa na Serikali kuwa ingeshusha bei za mafuta, ili kuleta nafuu ya maisha kwa wananchi.

Mabadiliko hayo ya bei pia yalileta mgongano kati ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu.

Wakati Ngeleja akiliambia Bunge kuwa bei hizo hazihusu akiba ya mafuta iliyopo nchini, Masebu alisema bei hizo zitaanza kutumika mara moja bila kujadili akiba iliyopo sawa na inavyofanyika kwenye kodi.

Ni kutokana na kusigana kwa wakubwa hao, huenda ndiko kuliikera Serikali na kulazimika Mkurugenzi huyo kuitwa mbele ya Baraza la Mawaziri juzi na kuhojiwa juu ya hatua yake ya kupandisha bei ya petroli bila kujali akiba ya mafuta iliyopo nchini.

Gazeti hili jana liliripoti namna Masebu alivyohenyeshwa na mawaziri, kwa namna Mamlaka yake inavyoyumbisha bei za mafuta, hivyo kuwafanya wananchi kutoonja nafuu ya maisha waliyoahidiwa na Serikali wakati wa Bajeti ya mwaka huu.

Katika Bajeti yake, Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, ilitangaza kuondoa baadhi ya tozo kwa asilimia 50 zilizokuwa zinatozwa na taasisi mbalimbali. Hali hiyo ingesaidia kupunguza bei ya mafuta kwa zaidi ya Sh 200 kwa lita.

Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana na kusomwa na Mkuu wake wa Mawasiliano, Titus Kaguo, ilisema imefanya hivyo kwa vile wadau na umma wangependa kuona Mamlaka hiyo ikipitia upya utaratibu wake wa kutangaza bei za mafuta kila baada ya wiki mbili.

“Kwa kuwa Ewura ni taasisi sikivu na yenye kujali maoni ya wadau, itakaa na wadau na kukubaliana haja ya kurekebisha fomula, ili ieleze namna ya kutathmini akiba iliyopo kabla ya kubadilisha bei za mafuta,” alisema Kaguo.

Ewura ilitetea uamuzi wake wa kupandisha bei za mafuta kuwa ulitokana na kupanda kwa bidhaa hizo kwenye soko la dunia na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani.

Juu ya bei kuanza kutumika bila kujali akiba iliyopo ndani ya nchi, Ewura kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake, ilisema suala la bei ya mafuta yaliyomo kwenye maghala lina sura mbili, ambazo ni bei mpya kumrudishia gharama alizowekeza kwenye akiba aliyonayo.

Pili, Masebu alisema bei pia inatakiwa imwezeshe mwekezaji kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwa kwenye soko, wakati anaagiza shehena nyingine ya mafuta, ili kuweka mfumo endelevu wa kuhakikisha kunakuwa na mafuta ya kutosha muda wote.

Katika mkutano wake wa jana, Kaguo alisema Ewura itafuatilia kwa karibu uanzishwaji wa mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja, ambao utawezesha kupata kiasi halisi cha mafuta yatakayokuwa yanaagizwa na kujua bei zake kwa usahihi zaidi.

Alisema bei hizo ndizo zitatumika kukokotoa katika kila kipindi husika. Mfumo huo tangu uanze kuelezwa na Ewura, haijajulikana utaanza lini na Kaguo alipoulizwa alisema ili uanze ni lazima kuwe na Bodi na Menejimenti ya kusimamia kampuni itakayofanya kazi hiyo.

“Bodi inaundwa na waziri, hivyo pindi atakapoiunda, utaratibu wa kupata menejimenti utaanza na ndipo uagizaji mafuta kwa pamoja utaanza,” alisema Kaguo.

Kwa mfumo wa biashara ya mafuta ulivyo sasa, kila kampuni inaagiza kwa vyanzo vyake inavyovijua, huku kampuni zingine kama BP na Engen, zikiagiza kutoka kampuni mama zilizoko Ughaibuni.

Naye Lucy Lyatuu anaripoti kuwa baadhi ya wadau wa usafiri nchini, wameiomba Serikali iifute Ewura kwa kushindwa kusimamia sheria.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (DABOA), Ibrahim Awadh, alisema wanaishangaa Ewura kutokana na kwamba walitarajia bidhaa hiyo iendelee kushuka badala ya kupanda.

Alisema kwa utaratibu huo wa Ewura, imesababisha usumbufu kwao kwa kuwa nao wamekopa fedha benki na kusumbuliwa kunachangia washindwe kulipa mkopo huo kwa muda unaotakiwa.

“Mimi nafikiri katika hili, Serikali ingeifuta kabisa Mamlaka hiyo na kuacha kujiingiza katika biashara huria ya kupanga bei,” alisema Awadh.

Alisema miaka ya nyuma hakukuwa na Ewura, lakini mambo yalikwenda vizuri na hata Serikali ya Awamu ya Tatu ilifanikiwa kuimarisha Shilingi sokoni na kudhibiti bei ya mafuta.

“Kwa mfano wakati wa uongozi wa Mkapa (Benjamin Rais wa Awamu ya Tatu) aliacha mafuta ya dizeli yakiuzwa Sh 800 kwa lita lakini hadi sasa yameongezeka zaidi ya mara tatu, ina maana kwa miaka mingine 10 ijayo wananchi wataishije?” Alihoji Awadh.

Alisema chama hicho kinatarajia kuandika barua kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA) baada ya Mfungo Mtukufu wa Ramadhan, kuelezea kusudio la kupandisha nauli kuliko kuendesha biashara kwa hasara.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama, alisema utaratibu wa Ewura wanauona kama mchezo wa kuigiza: “Yawezekana kuwa Ewura, ni wamiliki wa vituo vya mafuta.”

Alisema kigezo cha mafuta kupanda katika soko la dunia na thamani ya Shilingi kuanguka, ni kiini macho na kuhoji kwa nini katika Awamu ya Tatu hayo yote hayakutokea.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema kutokana na mkanganyiko uliosababishwa na EWURA, aliiomba Mamlaka hiyo kuweka wazi fomula ya ukokotoaji, ili kila mwananchi afahamu kinachofanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji wa Mafuta (TAOMAC), Salum Bisarara, alisema suala la mafuta ni tatizo kubwa la kitaifa na kwa sasa Msemaji Mkuu ni EWURA.

Alifafanua kuwa kitakachosemwa na Mamlaka hiyo watakubaliana nacho.

Wednesday, August 17, 2011

Baraza la Mawaziri laihenyesha Ewura

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Haruna Masebu,amehenyeshwa kwa kuhojiwa kwa undani na Baraza la Mawaziri kuhusu kuyumbisha bei ya mafuta.

Baraza hilo lilitaka kujua kwa nini mamlaka hiyo imekuwa ikiyumbisha nchi na wananchi kuhusu bei za mafuta.

Kwa zaidi ya saa moja, Masebu na wasaidizi wake waliwekwa kiti moto kuhusu bei zilizotangazwa na Ewura mwishoni mwa wiki, ambazo zimepanda kwa asilimia sita kutoka zile zilizotangazwa awali.

Habari za kuaminika kutoka kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, mjini Dodoma zinasema kuwa waziri mmoja baada ya mwingine walimhoji Masebu na wasaidizi wake kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za mafuta nchini.

Habari zinasema kuwa Masebu ambaye aliingia kwenye ukumbi huo akionesha kujiamini, alianza kupoteza mwelekeo kwa kadri maswali yalivyokuwa yakimiminika kutoka kwa mawaziri.

Hatimaye siyo yeye mwenyewe ama yoyote kati ya wasaidizi wake ambaye alikuwa na majibu ya kutosheleza ama hata ya kuwashawishi mawaziri kuhusu hatua hizo za Ewura na kwa kadri kikao hicho kilivyoendelea, Masebu na wenzake walionekana kukosa hoja.

Habari zinasema kuwa Masebu na wasaidizi wake walitakiwa kujielezea mbele ya Baraza la Mawaziri ili kuliwezesha Baraza hilo, chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, kujiridhisha na mwenendo mzima wa bei mafuta.

Baraza hilo lilitaka ufafanuzi kuhusu bei za petroli, mafuta ya taa na dizeli; nishati ambazo ukosefu wake nusura uiingize nchi katika zahama kubwa wiki iliyopita.

Moja ya maswali ya awali kutoka kwa Baraza la Mawaziri ilikuwa ni kwa nini Masebu na Ewura walitangaza kupanda tena kwa bei za mafuta siku chache baada ya kuzishusha kwa asilimia 9.17 kwa petroli, asilimia 8.31 kwa dizeli na asilimia 8.70 kwa bei ya mafuta ya taa.

Hatua hiyo ya Ewura kupunguza bei ya mafuta ilikuwa inatekeleza uamuzi na maagizo ya Serikali yaliyotangazwa na Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo Juni 22, mwaka huu, bungeni wakati alipowasilisha Bajeti ya Serikali.

Katika bajeti hiyo, Mkullo alisema kuwa Serikali iliamua kuondoa kodi na tozo kadhaa kwenye bei ya mafuta yanayoingizwa nchini kwa nia ya kupunguza bei ya bidhaa hizo ili kumpungumzia makali ya maisha mwananchi.

Hatua hiyo ya Mkullo, pamoja na ile ya Ewura kupunguza bei za mafuta ziliungwa mkono na Bunge na wananchi kwa kiwango kikubwa ambao walikiri kuwa hatua hiyo ilithibitisha jinsi gani Serikali yao inavyowajali.

Hatua ya Ewura kupunguza bei ya mafuta ilipingwa na kampuni karibu zote kubwa za kuingiza mafuta nchini ambazo zilianzisha mgomo kupinga hatua hiyo hasa BP, Engen, Oilcom na Camel Oil.

Baada ya siku moja ya mgomo huo, kampuni zingine nchini zilianza tena kuuza mafuta, lakini kampuni hizo nne zilikataa kufungua vituo vyao kuuza mafuta.

Agosti 9, mwaka huu, Ewura ilitoa amri ya Kimahakama (Compliance Order), kwa kampuni hizo nne kuanza mara moja kutoa huduma katika maghala yao na katika vituo vya rejareja vikiwemo vile vilivyoko chini ya miliki zao.

Katika amri hiyo, kampuni hizo zilitakiwa kuacha mara moja kusababisha upungufu wa makusudi wa mafuta ya petroli katika soko la Tanzania na kujieleza katika saa 24 kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka matakwa ya Sheria ya Mafuta na Utaratibu wa Ewura.

Siku iliyofuata, kampuni tatu zilianza kutoa huduma lakini BP (T) Ltd iliendelea kukaidi amri ya Ewura.

Bodi ya Ewura katika kikao chake cha Agosti 12, ilichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kali kwa kampuni za Oilcom, Camel Oil na Engen, na kuisitishia BP leseni ya biashara ya jumla ya mafuta kwa miezi mitatu na kuamuru Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo na mwenyekiti wake wa bodi wafikishwe kortini.

Lakini katika muda wa saa 48 tu, baada ya hatua hiyo ambayo iliungwa mkono na nchi nzima, Ewura ilibadilisha msimamo na mwelekeo wake na kutangaza kupandisha tena bei ya mafuta hayo ya petroli, dizeli na taa kwa asilimia tano.

Hatua hiyo ya Ewura, ilisababisha hasira ya Serikali yenyewe, Bunge, wabunge na wananchi kwa jumla.

“Ulichofanikiwa kufanya Masebu ni kuharibu kabisa mamlaka na madaraka ya Ewura. Hii ni taasisi ambayo ilikuwa imeanza kujijengea heshima kubwa kwa wananchi kwa kuchukua hatua mwafaka, na sasa mmevuruga kabisa heshima hiyo ya Ewura.

“Kwa kuvuruga heshima ya taasisi hiyo mmezitia doa siasa za nchi yetu,” waziri mmoja alimwambia ana kwa ana Masebu katika mkutano huo.

Masebu alijaribu kujitetea kwa kusema kuwa upandishaji huo wa bei ya mafuta uliofanywa na Ewura kwa mujibu wa Sheria na kwa mujibu wa makubaliano ya kuangalia upya bei kila baada ya wiki mbili kwa sababu mafuta huingizwa nchini kutoka Uarabuni kila baada ya wiki mbili.

Lakini Masebu aliambiwa kuwa hakuna mafuta yoyote yaliyoingizwa nchini tangu mvutano ulipoanza kati ya Ewura na kampuni za mafuta baada ya tangazo la kupunguza bei ya mafuta la Agosti Mosi, mwaka huu.

“Mheshimiwa Mwenyekiti ni mafuta yapi yameingia nchini kutoka Uarabuni katika wiki mbili zilizopita kwa sababu katika muda wote kwanza ulikuwepo mgomo wa kampuni za mafuta uliokolezwa zaidi na kampuni zile kubwa nne.

“Katika kipindi hiki, hakuna mafuta yaliyoingia nchini kwa sababu mafuta yalikuwepo kwenye matangi ya maghala na hayakuuzwa. Sasa Mkurugenzi anatuambia mafuta haya mapya yametoka wapi?” Alihoji waziri mmoja na kuongeza;

“Walichofanya Ewura ni kupandisha bei ya mafuta ambayo yalikuwa yamekwishafika nchini kabla ya mzozo kuanza mwanzoni mwa Agosti mwaka huu,” alisema waziri huyo.

Masebu alipojaribu kujitetea kuwa kwa taratibu za Ewura ni lazima bei za mafuta zipitiwe upya kila baada ya wiki mbili, waziri mwingine aliingia kati na kumwuliza:
“Mnapitia tu hata kama hakuna mafuta mapya yaliyoingizwa nchini kama ilivyotokea katika wiki mbili zilizopita? Mnafanya kazi kama mashine bila kutilia maanani hali halisi?” Alihoji.

Waziri mwingine alionya kuwa vitendo vya Ewura katika wiki mbili zilizopita vililenga kuyumbisha nchi na kuipeleka pabaya bila sababu za msingi.

“Inaelekea nyie Ewura mnahangaika zaidi kutetea maslahi ya wafanyabishara kuliko maslahi ya wananchi wetu,” alisema Waziri huyo.

Tuesday, August 16, 2011

LHRC wataka kusitishwa kwa uchimbaji urani

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeishauri Serikali kusitisha moja kwa moja uchimbaji wa madini ya urani hadi hapo itakapokuwa imewaelimisha wananchi.

Aidha, kwa maeneo ya wilaya za Bahi mkoani Dodoma na Manyoni katika Mkoa wa Singida, kituo kimeshauri uchimbaji wa madini hayo kusitishwa kabisa kutokana na kuwa katikati ya makazi ya watu.

Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Francis Kiwanga alisema hayo jana Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Sera na Maboresho, Harold Sungusia wakati akitoa tamko la LHRC kuhusu uchimbaji wa madini hayo ambayo utekelezaji wake haujaanza.

Alisema tamko hilo linatokana na utafiti uliofanywa na wataalamu wa kituo hicho katika
maeneo ya Bahi, Manyoni na Namtumbo mkoani Ruvuma na kugundua mambo mbalimbali ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kabla utekelezaji wa uchimbaji wa madini katika maeneo hayo.

“Miongoni mwa yaliyogunduliwa ni pamoja na wananchi kutoelimishwa na kuhadharishwa kuhusu taadhira na athari za madini hayo ya urani kwa afya zao, mifugo yao, mazao yao na mazingira kwa ujumla,” alisema Kiwanga.

Hata hivyo, alisema wananchi hawajashirikishwa katika kazi ya utafiti inayoendelea katika maeneo hayo na hata hatma ya maisha yao haijajulikana.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Aloyce Tesha alisema madini ya urani yakiwa katika hali yake ya kawaida bila kuchakachuliwa hayana madhara. Hata hivyo alisema kwa sasa hakuna shughuli za uchimbaji, bali utafiti ambao ni muhimu kwa ajili ya kujua kiasi cha madini kilichopo na ubora wake.

Wabunge walia na Katibu Mkuu Ardhi

WABUNGE wamemtaja Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, kuwa kikwazo cha utatuzi wa masuala ya ardhi hasa migogoro kuhusu uwekezaji na kutaka aondolewe, la sivyo hakuna kitakachofanikiwa.

Wabunge wamesema hayo wakati wa mjadala wa Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2011/12 yaliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Aliyeanza kuchangia hoja alikuwa Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM) ambaye kabla ya kutoa hoja, alijisafisha kuhusu tuhuma za Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC) akisema hahusiki kwa namna yoyote na sakata hilo, hivyo wapiga kura wake wasihofu.

“Kabla ya kuchangia naomba kusema jambo, kutokana na maneno yaliyozagaa, mimi huko kwenye DDC sipo kabisa, kwani mwaka 2009 aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani, aliunda Tume inayofanya shughuli zote za DDC, mimi sipo, hizo ni kelele za mpangaji hazimyimi usingizi mwenye nyumba,” alisema Mtemvu.

Alipomaliza kujisafisha kuhusu DDC, Mtemvu alichangia kuhusu hotuba kwa kubainisha wazi kuwa haungi mkono hoja kwa kuwa hana majibu kuhusu mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, eneo la Kurasini licha ya maagizo kutolewa na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, watu walipwe stahili zao lakini bila mafanikio.

Mtemvu alisema hata Waziri Tibaijuka alitembelea eneo hilo na kuahidi kuwa wanaopisha mradi tangu mwaka 2006 watalipwa, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea na kwa wachache waliolipwa, walilipwa fidia ya Sh 300,000 kwa msingi na kati ya Sh milioni moja hadi 4.5 kwa ardhi na nyumba.

“Waziri wala Naibu Waziri hawana shida, tatizo lipo kwa Katibu Mkuu wa hii wizara na kama ataendelea kukaa katika nafasi hiyo, kazi yote nzuri ya Waziri itakuwa ni bure, kwa kuwa hakuna kitakachofanyika, “Napata hofu kubwa na mradi wa Kigamboni, kama serikali itaweza kwa hali hii, kama hakuna fedha, watu waelezwe ili waendelee kujenga,” alisema Mtemvu huku akishangiliwa hasa na wabunge wa upinzani.

Mbunge wa Mkinga, Dastan Kitandula (CCM), akichangia hoja, alisema suala la uwekezaji limekuwa sumu kwa wazawa, kwa kuwa limewathamini zaidi wageni na inatishia amani kwa kuwa baadhi yao wamepewa maeneo ya mipakani suala ambalo ni la hatari.

Kitandula alitolea mfano jimboni kwake, akisema kuna hekta 25,833 walizopewa wawekezaji mchanganyiko (wazawa na wageni likiwamo Jeshi la Kujenga taifa (JKT), lakini katika kile alichokiita kichekesho na jambo la kusikitisha, hekta nyingine 25,000 zimetolewa kwa mwekezaji mmoja, aliyemtaja kuwa ni Mwitaliano mwenye kampuni ya Arkadia Limited ili alime mibono.

Kitandula alisema wananchi wa wilaya hiyo hawana tatizo na wawekezaji kwa kuwa hao 11 hawajapata tatizo lolote, lakini wamemtaka kutounga mkono hoja hasa kutokana na ukweli kuwa, katika eneo la Mkinga lenye hekta 250,000 mwekezaji mmoja ana hekta 25,000.

Alisema anashangazwa na utendaji kazi wa wizara zinazohusika na ardhi ikiwemo TAMISEMI, lakini hasa Katibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye katika barua yake (tunayo) aliyoiandika Julai 2 na kupokewa Mkinga Julai 4, aliridhia kwamba mwekezaji huyo apewe ardhi hiyo huku Katibu wa TAMISEMI akiandika naye barua ya kuzuia.

“Huu ni mkanganyiko, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi anaidhinisha mwekezaji huyu apewe eneo hilo la hekta 25,000 na barua nyingine kutoka Katibu Mkuu TAMISEMI inazuia uuzwaji huo, hiki ni nini?

Inasikitisha zaidi kwa kuwa wawekezaji wazawa wananyimwa nafasi na kupewa Wazungu,” alisema Kitandula.

Alisema ana wasiwasi kuwa baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wanampotosha Rais Jakaya Kikwete na kumsababisha aonekane mbaya kwa wananchi wa Mkinga kutokana na uzembe wa wachache na kumtaka Waziri Tibaijuka alishughulikie hilo.

Wabunge wengine waliochangia mjadala huo katika kipindi cha asubuhi ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) ambaye alitaka suala la ardhi liwe haki kwa kila Mtanzania hasa wakulima wa pamba wa Shinyanga.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Chatanda (CCM) alitaka maofisa ardhi wawajibishwe kwa kuwa wamekuwa chanzo cha kugawa ardhi na kutaka maeneo yote ya wazi yarejeshwe serikalini.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema), ametaja baadhi ya vigogo nchini kuwa wanamiliki ardhi kinyume cha utaratibu na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi.

Waliotajwa na Msemaji huyo jana bungeni ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, John Malecela.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Awamu ya Tatu.

Akitoa hotuba ya kambi hiyo ya bajeti ya mwaka 2010/11 ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee alisema migogoro mingi ya ardhi imeshindwa kutatuliwa kutokana na nguvu ya wakubwa kama hao.

Alidai vigogo hao wanamiliki mamia kwa maelfu ya hekta katika maeneo yanayotakiwa kupewa wanakijiji wa Wami katika shamba la lililokuwa Shirika la Usimamizi wa Ranchi za Taifa (NARCO) wilayani Mvomero, Morogoro.

“Shamba hili (la NARCO) lina ukubwa wa hekta 49,981 na taarifa zinaonesha hekta 30,007 ilipewa kampuni ya Sukari ya Mtibwa licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa eneo ni kubwa.

“Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa maeneo yaliyokuwa yagawiwe kwa wanakijiji, wamepewa wananchi wafuatao:“Mangula ana hekta 2,000, Malecela hekta 100, Ngwilizi hekta 5,000 zilizosemwa wamepewa wakulima wadogowadogo wa kijiji.

“Mwinyi hekta 2,000, Sumaye hekta 500 na Mkapa hekta 1,000,” alisema Mdee.

Hata hivyo, alimwondoa Mkapa katika tuhuma hizo za shamba namba 299 kwa kuwa ameliendeleza tofauti na viongozi hao wengine aliowataja katika hotuba yake.

Kambi hiyo ya upinzani ilihoji kama vigogo hao ni wanakijiji wa Wami-Dakawa na ni vigezo gani katika utaratibu uliowahusu wanakijiji, vilitumika kuwapa mashamba na kuwanyima wanakijiji wengine.

Pia alihoji kama Serikali haioni mgao huo umejaa dhuluma na upendeleo unaohatarisha maisha ya Watanzania na usalama wa nchi kwa jumla.

Alidai wananchi wana hasira, kwa kuwa walishaelezwa kuwa watapata hekta tano kila mmoja baada ya kutozwa Sh. 20,000 kila mmoja na hivi sasa kwa mujibu wa Mdee, wanaelezwa kuwa maeneo hayo yamekwisha.

Monday, August 15, 2011

Petroli bei juu tena

BEI ya bidhaa ya petroli imepanda tena kwa zaidi ya Sh 100 kwa lita kuanzia Jumatatu, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura) imetangaza Jumapili.

Kwa tangazo hilo la Ewura, katika Jiji la Dar es Salaam lita ya petroli imepanda hadi kufikia Sh 2,114 ambayo ni bei kikomo kutoka Sh 2,004 zilizotangazwa na Ewura Agosti 3, mwaka huu ambazo hata hivyo ziligomewa na wafanyabiashara.

Dizeli kwa bei ya rejareja sasa itauzwa Sh 2,031 kutoka Sh 1,911 huku mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 2,005. Kwa upande wa bei za jumla petroli itauzwa kwa Sh 2,046.62, dizeli itauzwa kwa Sh 1,963.81 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh 1,937.90.

Wiki mbili zilizopita, Ewura ilitangaza bei hizo mpya ambazo ziligomewa na wafanyabiashara wa mafuta hadi Serikali ikatishia kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ndipo baadhi yao wakalegeza msimamo.

Hata hivyo, Kampuni ya BP Tanzania iliendelea na msimamo wa kutouza mafuta kwa bei hiyo ya Serikali na kwa ukaidi huo tayari kampuni hiyo imefungiwa na Ewura kutojihusisha na biashara ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa miezi mitatu.

Hatua hii ya Ewura kupandisha bei tena ya mafuta ni wazi kuwa itazua manung’uniko kwa wananchi ambao walitarajia kuwa ile ahadi ya Serikali iliyoitoa wakati wa bajeti ya kushusha bei za bidhaa hiyo ingedumu kwa muda mrefu.

Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura, Godwin Samwel alitetea uamuzi wa kupandisha bei ya mafuta kuwa umetokana na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani pamoja na kupanda kwa kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

Samwel alisema viwango vya bei zilizotumika katika soko la dunia zimepanda kwa wastani wa asilimia 5.42 na thamani ya Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa shilingi 47.12 kwa Dola moja ya Marekani.

Ewura pia imezidi kujitetea kuwa kanuni mpya ya kukokotoa bei za bidhaa hiyo bado inafanya mafuta kuuzwa kwa bei ya chini ukilinganisha na kanuni ya zamani. Samwel alitoa mfano kuwa iwapo Ewura ingetumia kanuni ya zamani ya kukokotoa bei mpya, petroli ingeuzwa kwa Sh 2,298.33, dizeli ingeuzwa Sh 2,213.36 wakati mafuta ya taa yangeuzwa kwa Sh 2,188.89.

“Bei za rejareja na za jumla zingepanda zaidi endapo furmula ya zamani ingeendelea kutumika,” alisema Meneja Biashara ya Petroli wa Ewura. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Ewura ya mwaka 2008, bei za bidhaa ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na akaongeza kuwa mamlaka yake itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei za bidhaa za mafuta.

Hata hivyo, Samwel alitoa matumaini kwa Watanzania kuwa kuna uwezekano mkubwa baada ya wiki mbili bidhaa ya petroli ikapungua bei kutokana na bei katika soko la dunia kuanza kushuka.

“Bei itashuka iwapo Shilingi haitaporomoka zaidi, ila ikiendelea kuporomoka bei haitashuka sana,” alisema ofisa huyo wa Ewura. Akielezea hali ya biashara ya mafuta kwenye soko la ndani, alisema upatikanaji wa mafuta unaendelea vizuri kwani Ijumaa jumla ya lita milioni 9.5 zimeingizwa kwenye soko la ndani na juzi Jumamosi lita milioni 4.9 za bidhaa hizo ziliingizwa kwenye soko.

Alisema meli za mafuta zinaendelea kuingia nchini na zingine ziko bahari zikisubiri kupakua shehena hiyo. “Hivyo nawahakikishia kuwa upatikanaji wa mafuta utaendelea kuwa mzuri,” alisema. Kuhusu baadhi ya vituo vya Kampuni ya Total na Orxy kuendelea kutotoa huduma kwa wananchi, Ewura imeahidi kutoa tamko leo.

Friday, August 12, 2011

Wabunge kataeni ufadhili huu

TUNAANDIKA kumpongeza mbunge wa Tarime (CCM), Nyambari Nyangwine kwa kitendo chake cha juzi cha kukataa kujumuika na wabunge wengine kwenye ‘lifti’ ya ndege zilizokodishwa na kampuni ya Barrick kwenda kwenye mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.

Lengo la safari hiyo ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ni kwenda kuona iwapo mgodi huo umetekeleza ahadi yake ya kuboresha mazingira kufuatia tukio la mwaka juzi ambapo wanavijiji wengi walidhurika kwa sababu ya sumu kutoka mgodi huo kuingia katika mto Tingite ambao maji yake hutumiwa na vijiji kadhaa.

Kama lengo la safari hiyo ni hilo, haingii akilini kwamba mgodi huo huo ambao wabunge wanakwenda kuuchunguza kama umechukua hatua za kuwalinda wanavijiji wanaouzunguka dhidi ya sumu unaozalisha, ndio huo huo unaowakodishia ndege na kugharimia safari hiyo nzima.

Tuonavyo sisi, jambo hilo halina tafsiri nyingine yoyote mbali ya kwamba ni rushwa itolewayo na mgodi huo kwa wabunge ili warejee Bungeni Dodoma wakiwa na ripoti nzuri kuhusu Barrick; hata kama walichokiona huko hakiridhishi.

Ndiyo maana tumeshawishika kumpongeza Mbunge Nyangwine kwa kukataa ‘lifti’ ya Barrick kwenda Nyamongo; maana hakika angeonekana msaliti kwa wananchi wa jimbo lake hilo; kama ambavyo baadhi yetu tunavyowaona hivi sasa wabunge hao waliokubali kugharimiwa safari hiyo na mgodi wanaokwenda kuuchunguza.

Kwa hakika, tunashangaa na hatuelewi ni vipi Spika Anne Makinda aliruhusu safari hiyo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ifadhiliwe na mgodi huo inaokwenda kuuchunguza. Na hapa, tunaingiwa pia na shaka juu ya ufadhili huo unaanzia wapi na unaishia wapi.

Labda tukumbashane kwamba Bunge lipo kwa ajili ya maslahi ya wananchi, na hivyo safari hiyo ilipaswa igharimiwe yote na Bunge lenyewe; yaani fedha za walipa kodi nchini; badala ya kufadhiliwa na kampuni hiyo ya Barrick ambayo tayari ina migogoro kibao na wanavijiji wanaoishi katika vijiji vinavyoizunguka migodi yao. Kwa walichokifanya wabunge hao, ni kukaribisha migongano ya kimaslahi inayoweza kutia dosari utendaji wao ndani na nje ya Bunge.

Ni matumaini yetu kwamba ufadhili wa aina hiyo hautakubaliwa tena na Bunge letu - uwe unatoka kwa Barrick au kampuni nyingine yoyote.

Chanzo: Raiamwema

Serikali yajitosa biashara ya mafuta

KAMPUNI ya Commercial Petroleum (COPEC) ambayo imepewa leseni na Serikali kuagiza bidhaa ya petroli, imeahidi kuingiza nchini shehena yake ya kwanza ya mafuta mwishoni mwa mwezi ujao.

Tayari kampuni hiyo tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imetangaza zabuni ikialika wafanyabiashara ambao wako tayari kusambaza bidhaa itakayoagizwa nayo.

Copec ilipewa leseni juzi na Serikali baada ya waagizaji binafsi wa petroli kugoma kutokana na Serikali kutangaza bei elekezi chini ya waliyokuwa wanauzia.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Selengia Mlawi, aliliambia gazeti hili jana, kuwa Serikali imekubali kuipa kampuni hiyo dola milioni 38 za Marekani, kwa ajili ya kuagizia shehena yake ya kwanza.

Imetoa fedha hizo kutokana na dharura iliyopo, baada ya wafanyabiashara binafsi kugoma kusambaza mafuta hayo.

TPDC ilikiri kuwa kwenye mipango yake, suala hilo halikuwamo na ndiyo maana Serikali ikaamua kutoa kiasi hicho cha fedha, ambacho kinatosha kununulia, kusafirishia na kulipia bima shehena yake ya kwanza.

Lengo la Serikali kuruhusu kampuni hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na TPDC kujiingiza kwenye biashara ya ushindani, ni kujaribu kupata taarifa sahihi na za uhakika kuhusu uagizaji wa bidhaa hiyo, kutokana na wafanyabiashara binafsi kulalamika kuwa wanapata hasara.

Lingine, ni kuhakikisha kinakuwapo chombo cha uhakika ambacho hakiwezi kupinga wala kutofautiana na maagizo ya Serikali, kama walivyofanya waagizaji binafsi, hadi wakagoma kusambaza bidhaa ya petroli na hivyo kuiingiza nchi kwenye janga la uhaba wa mafuta.

Serikali ina ubia na kampuni ya BP kwa asilimia 50, lakini kampuni hiyo ndiyo inaonekana kushikilia msimamo wa kuendelea na mgomo licha ya agizo la Serikali kukataza mgomo huo.

Hata hivyo, COPEC imeingizwa kwenye biashara hiyo wakati haina watendaji wala bodi, jambo ambalo limeifanya TPDC katika kipindi cha mpito, kuchukua majukumu makubwa ambayo yangeendeshwa na bodi na menejimenti ya Copec.

“Ni kweli, kwa sasa kampuni haina watendaji, kikao cha Bodi cha TPDC kilikaa juzi (Jumanne) na kuamuru wafanyakazi walioko kwenye kitengo cha masoko cha TPDC waendeshe shughuli za kampuni hiyo wakati menejimenti yake ikitafutwa,” alisema Mlawi.

Mlawi alisema pia kwamba Bodi ya TPDC chini ya uenyekiti wa Jenerali (mstaafu) Robert Mboma, ndiyo itakayounda bodi ya COPEC na ilikubaliwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Bodi ya TPDC waingie kwenye bodi hiyo, ili kuipa uhai na kasi ya kuendesha biashara hiyo.

Ndiyo maana hata tangazo la jana la kukaribisha zabuni ya kusambaza shehena ya COPEC lilitolewa na Bodi ya TPDC kwa niaba ya mpuni hiyo.

Katika tangazo hilo, zabuni inawataka wenye sifa za kusambaza tani 9,000 za petroli, 25,000 za dizeli na tani 1,000 za mafuta ya taa. Mwisho wa kuomba zabuni hiyo ni Septemba 12.

“Shehena ya kwanza kuwasili nchini haitazidi mwisho wa Septemba, hivi sasa tunajiandaa kupeleka zabuni kwenye kampuni kubwa ili zituuzie mafuta kwa bei ndogo zaidi kuliko kununua mafuta kutoka meli zinazoelea baharini.

“Sisi tunaingia kwenye mfumo wa zabuni, si kuagiza kwenye kampuni mama kama wanavyofanya BP na Engen, ambao wanapewa bei kabisa na ndiyo maana inakuwa vigumu kwao kubadilisha bei, kwani ni lazima wapate kibali cha kampuni hizo mama,” alisema Mlawi.

Akifafanua kuhusu wafanyakazi, alisema TPDC tangu mwaka 2006 imekuwa na wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya mafuta, kwani tayari Serikali iliwaomba kufanya biashara hiyo na baadaye wakasimamisha suala hilo.

“Tayari tulishaajiri wataalamu kutoka kampuni za mafuta … na uhakikishia kuwa hilo halina shida kwa vile tunao wa kutosha katika kitengo cha masoko,“ alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Maghala Mlawi alikiri kuwa kwa sasa hawana maghala ya kuhifadhia shehena watakayoagiza lakini akasema biashara ya mafuta inaruhusu kampuni kutumia maghala ya kampuni nyingine.

“Kwa kipindi hiki ambacho hatuna maghala, tutaomba kampuni nyingine, kwani sheria inaruhusu kampuni shindani kutupa maghala hayo hata kama tuna ugomvi nao. Kwa hivyo hatuna tatizo na suala hilo,” alisema Mlawi.

Pia alisema wataangalia uwezekano wa kutumia maghala ya kampuni ya kusafisha mafuta ya Tiper, kwani ina maghala ya kutosha kuhifadhia shehena za mafuta.

Alisema kitendo cha COPEC kuingia kwenye biashara hiyo ya ushindani kutawafanya wafanyabiashara binafsi kutoichezea tena Serikali.

Alisema ana uhakika wataendesha biashara hiyo vizuri, licha ya vita vya kutaka kuwakwamisha ili wasiingie katika biashara hiyo.

Vita serikalini Kampuni hiyo licha ya kuanzishwa mwaka 1999, Serikali iligoma kuipa leseni ya biashara hiyo, hali inayoelezwa na baadhi ya vyanzo vya habari kutoka ndani ya TPDC, kuwa ulikuwa ni mpango uliohusisha baadhi ya maofisa wa Wizara ya Nishati na Madini.

Hali hiyo iliifanya TPDC kushindwa kuunda menejimenti yake. Vita dhidi ya COPEC viliifanya Serikali iiamuru TPDC kuachana na biashara ya mafuta badala yake ijielekeze kwenye kutafuta na kutafiti mafuta.

Mwaka 2006 kampuni hiyo ilifufuliwa baada ya kutokea uhaba wa mafuta, lakini baadaye Serikali ikaitaka isiendelee na mpango wake wa kuagiza mafuta.

Baada ya kutokea tena uhaba wa mafuta juzi kutokana na mgomo wa wafanyabiashara binafsi, Serikali katika kikao chake kilichohusisha watendaji wa Ikulu, Wizara ya Nishati na
Madini, TPDC na Ewura, iliamua COPEC iingie rasmi kwenye biashara ya ushindani wa mafuta.

Mpango wa baadaye Kwa mujibu Mlawi, licha ya kupewa kiasi hicho na Serikali, itaendelea sasa na mpango mkakati wake wa kujiimarisha kibiashara, ikiwa ni pamoja na kukopa fedha kutoka vyanzo vya ndani ili iweze kujiingiza kwenye ushindani zaidi.

Alisema pia fedha watakazopata licha ya kuzitumia kuagizia shehena ya mafuta, watazitumia kujenga vituo ya kusambazia mafuta na maghala.

“Tumefanya biashara hii ya mafuta muda mrefu tunaifahamu nakuhakikishia kuwa pamoja na kuungwa mkono na Serikali, lakini tutatoa ushindani wa kutosha,” alisema Mlawi.

Vituoni jana Upatikanaji wa bidhaa ya petroli katika vituo vya mafuta ulikuwa wa kusuasua, kwani vingi havikuwa na bidhaa hiyo, licha ya kampuni kubwa kuruhusu kusambazwa.

Kutokana na mahitaji kuwa makubwa, vituo vingine viliuza nishati hiyo juzi jioni na kujikuta vinaishiwa, hivyo kulazimika kusimamisha huduma na kufanya wananchi waendelee kuhangaika.

Vituo vya BP na Engen pia viliendelea kutotoa huduma hiyo kutokana na maghala ya yake juzi kutoruhusu kusambazwa kwa shehena yake.

Naye Halima Mlacha, anaripoti kwamba wakati hali ya uuzaji mafuta ikiendelea kutengemaa sehemu mbalimbali nchini, bado baadhi ya wasambazaji wa mafuta hayo hasa wa BP walionekana dhahiri kutouza mafuta hayo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye maeneo kadhaa ya Dar es Salaam ulishuhudia vituo kadhaa vya mafuta vya BP na CamelOil vikiwa haviuzi mafuta, huku wafanyakazi wao wakionekana kupiga soga.

Vituo vya BP vya Mwenge, Mikocheni, Sinza Kijiweni, Ocean Road na Kinondoni, vilikuwa tupu, bila dalili zozote za biashara.

Hali ilikuwa vivyo hivyo katika vituo vya CamelOil Afrika Sana, Engen Mikocheni na OilCom. Hata hivyo, gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vituo vya TSN Oil Bamaga, GBP na Big Bon Afrika Sana, vikiendelea na biashara ya mafuta ambapo kwa jana hakukuwa na foleni kubwa ya magari na watu kama ilivyokuwa juzi.

Vituo vingine vilivyokuwa vikiuza mafuta ni Oil Com Mwananyamala, Gapco na Oryx Posta Mpya.

Mfanyabiashara maarufu nchini na msafirishaji mizigo nje ya nchi, Azim Dewji, alitupia
lawama Ewura na Serikali kwa tatizo hilo la ukosefu wa mafuta na kuhadharisha juu ya kurejea enzi za kupanga mistari kununua bidhaa kama sabuni.

“Wanataka kuturejesha enzi za foleni, hii si sahihi kabisa, nchi ilikuwa inakabiliwa na tatizo la umeme, sasa imeibuka la mafuta, ambalo linatokana na kuchanganya siasa na biashara, tunaomba Serikali iliangalie vizuri suala hilo,” alisema Dewji.

Alisema tatizo linaloendelea limetokana na Ewura kulazimisha wafanyabiashara kuuza mafuta chini ya gharama zao za uendeshaji, hali ambayo alidai inatokana na biashara kuchanganywa na siasa.

“Jamani ikumbukwe kuwa bei ya mafuta inadhibitiwa na soko la dunia, hakuna mfanyabiashara mwendawazimu anayenunua mafuta halafu akae nayo,” alisema.

Aliitaka Ewura iweke wazi vipengele ambavyo Serikali imefuta ushuru ili vibainike, kwa kuwa sasa jambo hilo bado ni siri, hali inayosababisha shaka kuwa hakuna punguzo lililofanyika.

Akizungumza na HABARILEO, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema kuhusu baadhi ya vituo kutouza mafuta Bodi ya Mamlaka hiyo inatarajiwa kukutana leo, pamoja na mambo mengine, kujadili suala hilo na hatua za kuchukuliwa.

Kuhusu kutoweka wazi vipengele vya ushuru uliopunguzwa na Serikali, alisema suala hilo si la kweli na kwamba hata katika ukokotoaji wa bei hizo mpya, kila kipengele kilioneshwa na kampuni zote za biashara kupewa nakala.

Wednesday, August 3, 2011

Kwa nini tupoteze fedha nyingi kujadili “ndiyo” bungeni?

Na Privatus Karugendo

“UKISEMA, ‘ndiyo’, basi, iwe ‘ndiyo’, ukisema ‘siyo’, basi iwe kweli ‘siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu” (Mathayo 5:37).

Haya ni maneno ya Yesu Kristu wa Nazareti wakati akiwafundisha wafuasi wake. Somo lenyewe lilikuwa juu ya mtu kuwa na msimamo, uadilifu na uaminifu. Kwamba mtu ukiamua kuisimamia “ndiyo”, basi aisimamie bila kutetereka, na akiamua kuisimamia “siyo” vile vile aisimamie bila kuyumba. Na kwamba mtu akiisimamia “ndiyo” ukijua kwamba ni “siyo” ni unafiki na uovu. Vilevile akiisimamia “siyo” ukijua kwamba ni “ndiyo” ni unafiki na uovu!

Kwa maneno mengine, mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu hawezi kujiwekea kikao cha kujadili “ndiyo” anayoijua ni “ndiyo” na “siyo” anayoijua ni “siyo”. Mtu mwenye msimamo, uadilifu na uaminifu daima anakuwa mbali na unafiki na uovu.

Hii ni falsafa ya Yesu wa Nazareti aliyowafundisha wafuasi wake. Bila kuingilia masuala ya imani, mtu yeyote anaweza kuitumia falsafa hii katika maisha yake; maana ina msingi chanya wa kuendesha maisha katika jamii yoyote ile.

Wakati Yesu wa Nazareti akifundisha falsafa hii ya msimamo, uadilifu na uaminifu katika jamii ya Wayahudi; jamii yenyewe ya Wayahudi ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha mabadiliko. Watawala waliabudu madaraka na mali; walipinduana katika utawala, walisalitiana na wakati mwingine waliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Unafiki na uovu viliongoza maisha yao ya siku kwa siku. Kuna wanaojenga hoja kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa mwanasiasa aliyeguswa na hali ya maisha ya watu katika jamii yake ya Wayahudi. Kwa wale wanaoipokea imani ya Kikristu bila kuchimba kwa kina historia, theolojia na elimu ya Biblia, watasema mimi ni mzushi; lakini ukweli utabaki pale pale kwamba Yesu wa Nazareti alizaliwa katika jamii fulani na kuishi akizungukwa na historia, utamaduni na desturi za watu wake.

Ingawa sisi hapa Tanzania hatujafikia hatua ya kupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, hatujabaguana na kushindana kama walivyokuwa wana wa Israeli, unaweza ukafananisha hali ya Uyahudi ya wakati ule na hali ambayo taifa letu la Tanzania linapitia hivi leo.

Unafiki na uovu vinawaongoza watawala wetu; hivyo tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Tunahitaji viongozi watakaosema “ndiyo” wakimaanisha “ndiyo” na watakaosema “siyo” wakimaanisha “siyo”. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba viongozi wetu wanasema “ndiyo” wakimaanisha “siyo” na wanasema “siyo” wakimaanisha “ndiyo”.

Tuna viongozi ambao wanacheka kumbe wanalia, na ambao wanalia kumbe wanacheka! Tuna wabunge wanaosinzia Bungeni wakisingizia kutafakari. Wakibanwa zaidi wanasema huo ni uchochezi wa waandishi wa habari! Wabunge wetu walipambana kufa na kupona waitwe “Waheshimiwa” na kusahau kabisa kwamba waheshimiwa ni wananchi waliowatuma Bungeni.

Katika familia zetu, katika jamii zetu na katika taifa letu, tunahitaji msimamo, uadilifu na uaminifu. Hatuwezi kujenga familia, jamii na taifa imara bila kuwa mbali na unafiki na uovu. Bila kujenga utamaduni wa “ndiyo” kuwa ni “ndiyo na “siyo” kuwa ni “siyo”, hatuwezi kupiga hatua ya maendeleo bila kuizingatia falsafa hii.

Jambo hili ni muhimu; maana jinsi mambo yanavyokwenda ni kama vile sisi (kama taifa) hatujakubaliana “ndiyo” ni nini na “siyo” ni nini. Na kama makubaliano haya yapo, kitu ambacho sina imani kubwa nacho, basi ni lazima tukubaliane kwamba msimamo, uadilifu na uaminifu vimezikwa kaburi moja na Azimio la Arusha!

Huu ni mjadala mrefu ambao ninafikiri unahitaji makala inayojitegemea. Ni mjadala ambao ni lazima kuendeshwa kwa uangalifu mkubwa ili kukwepa ushawishi wa kuichukulia falsafa yenyewe kama kichocheo cha udini.

Watanzania wakitaka kupindisha ukweli wanauweka udini mbele. Wakati mwingine udini ni silaha ya kuifumba midomo ya watu na kulenga kuwatenga Watanzania kwenye makundi ili wasishirikiane kudai haki zao kutoka kwa watawala. Hivyo falsafa hii ya “ndiyo” na “siyo” nitaijadili wakati muafaka ukifika.

Hata hivyo, hoja ninayoijenga leo kwenye makala hii ni kule kupoteza muda mwingi na fedha nyingi kuijadili “ndiyo” ambayo hata kama watu wengi wanajua na kuamini kwamba ni “siyo” lakini watawala na mfumo uliopo unaamua kwamba ni “ndiyo”.

Tunahitaji muda kuyashughulikia mambo mengine mengi; maana taifa letu bado ni masikini. Tunahitaji fedha kutekeleza mipango mingi ya maendeleo. Kwa nini basi muda huu unaohitajika hivyo na fedha hizi za maendeleo vitumike kujadili “ndiyo”?

Tunalalamikia ufinyo wa bajeti. Kila wizara inalalamika kupata mgawo kidogo kutoka kwenye mfuko wa taifa letu. Watanzania walio wengi wanashauri wizara zote bajeti zao zipanuliwe na kuongezewa fedha nyingi, na hasa fedha inayowalenga Watanzania wanaoishi pembezoni.; badala yake tunawaweka wabunge pale Dodoma kwa kipindi cha miezi miwili, wakitumia fedha za Watanzania.

Siku za kuishi Dodoma zikipunguzwa, ni wazi fedha nyingi zitapatikana ili ziongezewe kwenye bajeti za wizara mbalimbali. Ingawa sina takwimu za fedha wanazolipwa wabunge wetu, ni wazi siku zaidi ya 30 zikipunguzwa kwenye siku ambazo wabunge wanalazimika kuishi Dodoma, tutapata fedha ya kutosha kufanya miradi mingine ya maendeleo.

Bajeti yetu ya taifa inayojadiliwa kila baada ya mwaka mmoja kwa utawala na mfumo uliopo sasa ni “ndiyo”. Ijadiliwe isijadiliwe ni lazima ipitishwe. Hata pale inapoonekana wazi wazi kwamba kuna ulazima wa kubadilisha kama inavyojionyesha kwenye bajeti ya mwaka huu ya Nishati na Madini, bado bajeti inapitishwa hivyo hivyo; maana wabunge wa chama tawala ni wengi kuliko wa upinzani.

Wakati mwingine inasikitisha zaidi bajeti inapopitishwa hata bila kujadili vifungu vyote kwa kisingizio cha kukimbizana na muda. Hoja ni kwamba kwa nini wabunge wakae Dodoma miezi miwili wakijadili “ndiyo”. Ni busara gani inayotumika? Kama lengo ni wabunge kuibariki bajeti, kwa nini bajeti isisomwe kwa siku mbili au tatu na kupitishwa ili kuokoa muda na fedha?

Bunge letu lina utamaduni wa kupitisha mambo kwa swali: Wanaokubali waseme “ndiyo” na wasiokubali waseme “siyo”. Kufuatana na utawala na mfumo tulio nao kwa sasa hivi, jibu ni “ndiyo” hata pale ambapo na watoto wadogo wanaweza kutambua kwamba “ndiyo” ni “siyo”, na wakati mwingine sauti za wabunge wanaosema “siyo” ni nyingi zaidi ya wale wanaosema “ndiyo”, Spika na wasaidizi wake watasema wa “ndiyo” wameshinda; maana vichwani mwao hakuna kitu kingine zaidi ya “ndiyo”.

Soma zaidi

Bei petroli yashuka, atakayepandisha faini mil.3/-

BEI ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa imepunguzwa kwa kiasi na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA). Kwa mujibu wa tangazo la Ewura jana kwa waandishi wa habari mjini hapa, bei hizo mpya zitaanza kutumika leo nchini kote.

Bei hizo zinaonesha kwamba, bei ya petroli imepungua kwa Sh 202.37, sawa na asilimia 9.17, dizeli kwa Sh 173.49(8.31%) wakati mafuta ya taa, yameshuka kwa Sh 181.37 (8.70%). Mabadiliko hayo yalitangazwa jana mjini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, aliyesema bei mpya zimezingatia mapendekezo ya marekebisho ya vipengele vya kanuni ya kukokotoa bei za mafuta na hivyo kufanya punguzo kubwa la tozo katika biadhaa za mafuta.

Kwa mujibu wa Masebu, tozo katika petroli imepunguzwa kutoka Sh 54.03 kwa lita hadi Sh 27.27 (asilimia 49.53); dizeli kutoka Sh 55 hadi Sh 28.15 kwa lita (asilimia 48.80); mafuta ya taa kutoka Sh 55.66 hadi Sh 24.50 (asilimia 55.98). Kwa wastani, tozo za taasisi zimepungua kwa asilimia 51.44.

Kutokana na hatua hiyo, Ewura iliagiza, kwamba hakuna muuzaji wa rejareja atakayeruhusiwa kuuza petroli kwa zaidi ya Sh 2,004. Awali, bei ya juu kabisa ilikuwa Sh 2,206. Hali kadhalika, bei ya juu ya dizeli sasa ni Sh 1,910.84 ikilinganishwa na Sh 2,084 iliyokuwa ya kikomo mwezi jana.

Aidha, bei ya juu ya mafuta ya taa sasa itakuwa Sh 1,904.53 ikilinganishwa na ya awali Sh 2,085.90. Kutokana na bei mpya za bidhaa za mafuta, Masebu alisisitiza kwamba mfanyabiashara atakayeongeza hata senti moja, kosa hilo litamgharimu Sh milioni 3.

Hata hivyo, alisema katika kukabiliana na ushindani wa biashara, wafanyabiashara wanaweza kupunguza bei za bidhaa zao kiasi wanachopenda, ili kuvutia wateja, lakini si kuongeza bei.

“Nasisitiza, kuwa ni kinyume cha sheria kwa wauzaji bidhaa za mafuta kuuza kwa bei ya juu, tofauti na iliyopangwa na Mamlaka. Hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya watakaokwenda kinyume na haya,” alisema Masebu aliyeahidi kufuatilia kwa karibu ukiukwaji wowote utakaofanywa na wafanyabiashara.

Mkurugenzi huyo pia alionya wafanyabiashara watakaokwepa kuanza kutumia bei hiyo kuanzia leo, akisisitiza lazima zitumike, bila kujali mfanyabiashara ameingiza lini sokoni bidhaa yake na kwa bei ya wakati gani.

Aliongeza kwamba, Ewura ingependa kushusha zaidi bei ili kumpa nafuu mtumiaji wa kawaida, lakini kwa bahati mbaya kwa kiasi kikubwa bei ya bidhaa hizo inategemea na kupanda kwa bei katika soko la dunia na pia kuyumba kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

“Pamoja na kupungua kwa bei ya mafuta nchini, bado tuna changamoto, ikiwa ni pamoja na hii ya soko la dunia. Hata hivyo, Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta,” alisema.

Aliongeza kwamba viwango vya gharama za kibiashara vimezingatiwa ili kuhakikisha wafanyabiashara wanarejesha gharama zao za uwekezaji, uendeshaji na faida stahiki, huku mlaji naye akipata unafuu wa bei za bidhaa kwa ubora na ujazo unaostahili.

Ewura pia ilivitaka vituo vyote kuweka bei za mafuta katika mabango ya wazi yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na kwamba kinyume chake, adhabu kali zitamwangukia mmiliki wa kituo.

Aidha, wanunuzi wameshauriwa kuhakikisha wanapata stakabadhi za malipo zikionesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita, ili stakabadhi hizo ziweze kutumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutatokea malalamiko ama ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au atakuwa ameuziwa mafuta yasiyo na ubora stahiki.

Akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2011/12 Juni, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, alibainisha kwamba kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma nchini pamoja na mambo mengine, inasababishwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia Alifafanua kuwa ongezeko hilo linatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuongezeka kwa bei katika soko la dunia.

“Kwa mfano baada ya msukosuko wa uchumi duniani, bei ya mafuta ilishuka hadi dola za Marekani 40 kwa pipa. Kwa sasa bei ya mafuta katika soko la dunia imefikia takribani dola 120 kwa pipa, ambayo ni mara tatu ya bei iliyokuwapo awali.

“Aidha, ongezeko la bei linachangiwa pia na kuongezeka kwa gharama za bima ya mizigo kwa meli zinazoleta mizigo nchini, kutokana na tishio la maharamia baharini, uagizaji wa mafuta wa kampuni moja moja na migogoro ya kisiasa katika nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika,” alisema Mkulo.

Pia alibainisha kwamba pamoja na sababu zilizotajwa, bidhaa ya mafuta ya petroli inapoingia hapa nchini hutozwa ushuru wa bidhaa na wa mafuta. Zipo pia tozo zinazotozwa na mamlaka zinazotoa huduma katika mfumo wa uagizaji na upokeaji wa mafuta ambazo ni pamoja na EWURA, SUMATRA, Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Kiwanda cha TIPER, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Bandari na kampuni zinazoagiza mafuta.

“Pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani na kuweka viwango maalumu vya ushuru wa bidhaa kwenye mafuta, bado bei ya mafuta imeendelea kuwa kubwa na kuongeza gharama za maisha,” alifafanua Mkulo.

Hata hivyo, hatua ya jana, inatarajiwa kupunguza kwa kiwango kidogo mzigo huo wa maisha kutokana na punguzo kuwa la asilimia ndogo, tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, ingawa sababu za kupanda kwa bei ya mafuta ni za kimataifa.

Tuesday, August 2, 2011

BAJETI YA ELIMU 2011/2012: JE ELIMU NI SUALA LA HAKI AU UPENDELEO?

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII HAKIELIMU WATAWASILISHA:

MADA: BAJETI YA ELIMU 2011/2012: JE ELIMU NI SUALA LA HAKI AU UPENDELEO?

Lini: Jumatano Tarehe 02 Agosti, 2011

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo


WOTE MNAKARIBISHWA

Mbunge wa Igunga Rostam Aziz alipotangaza kujiuzulu

MAJIBU YA DR. MWAKYEMBE KUHUSU LOWASSA YALIKUWA HIVI

Tujikumbushe: Edward Lowassa Akijieleza TVT baada ya kujiuzulu Uwaziri Mkuu

CCM: Bei mafuta ya taa ishushwe

KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiagiza Serikali kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa na kuhakikisha mafuta yote yanayoingia nchini yana ubora unaotakiwa.

Pia Kamati hiyo imeitaka Serikali kutafuta suluhu ya uchakachuaji wa mafuta, kwani uwezo wa kufanya hivyo inao.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema Kamati Kuu ya Chama hicho iliyokutana juzi pamoja na kujadili mambo mbalimbali ya chama, haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa.

Alisema nishati hiyo ndiyo inayotumiwa na wananchi wengi wa kipato cha chini nchini, na kwamba kupandishwa bei kwa kisingizio cha kupunguza uchakachuaji, si sahihi.

Aliongeza kwamba, kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta hayo Serikali inapaswa kukaa na kutafuta njia zitakazoshusha bei hiyo na kuvitaka vyombo husika kuhakikisha ubora wa mafuta yanayoingia nchini.

“Tunaitaka Serikali itafute njia ya kushusha bei ya matufa ya taa na pia kutafuta suluhisho la uchakachuaji na si kupandisha bei,“ alisema Nape.

Aidha, alisema suala la umeme ni nyeti na kwa hali ilivyo sasa si nzuri na kuishauri Serikali kuja na njia za kunusuru hali hiyo.

“Athari ya kukosekana kwa umeme nchini ni kubwa, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, itumie muda iliopewa kurekebisha bajeti yao vizuri na kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hili na pia kuja na majibu ya suluhu ya tatizo hili,” alisema Nape

Aliongeza kwamba madhara yanayoipata nchi na mtu mmoja mmoja ni makubwa na inasikitisha kwa hali ilivyo na kwamba lazima Serikali ije na suluhu ya jambo hilo.

Aidha, Nape alisema Kamati Kuu pia ilijadili masuala yanayogusa wananchi likiwamo la migogoro ya ardhi, madini bei ya pamba na kuagiza Serikali iyashughulikie kabla migogoro hiyo haijawa mikubwa.

Hivi sasa mafuta ya taa yanauzwa bei kubwa kuliko dizeli na petroli ambapo katika baadhi ya vituo bei elekezi ni Sh 1,940 na kikomo ni Sh 2,086 kwa Dar es Salaam wakati kigoma elekezi ni Sh 2,117 na kikomo ni Sh 2,334 kwa lita.

Kwa hali hiyo hiyo, bei elekezi ya dizeli kwa Dar es Salaam ni Sh 1,939 na kikomo ni Sh 2084 huku kwa Kigoma elekezi ni Sh 2170 na kikomo ni Sh 2,333.

Hatua ya kupandishwa kwa bei hiyo ya mafuta ilifikiwa bungeni katika Bajeti ya Mwaka huu wa Fedha, kwa lengo la kuhakikisha kwamba kodi ya mafuta ya taa haizidiani sana na ya dizeli na hivyo kuondokana na uchakachuaji.

Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya uchumi wanadai kwamba wachakachuaji wanafahamika na hivyo ni wajibu wa Serikali kuwabana kuliko kumwumiza Mtanzania masikini anayeishi kwa kutegemea mafuta ya taa.

Lakini pia wanasema tatizo linalosababisha yote haya ni kwamba mafuta yote yanaagizwa kutoka nje ya nchi ambako bei inatoka huko huko lakini pia kodi ya mafuta nchini ni kubwa.
Wanatoa mfano kwamba lita moja ya mafuta ya taa huitozwa kodi ya Sh 400.30, ya petrioli ni Sh 534 na dizeli ni Sh 415.

Wachambuzi hao wanasema pia kwamba hata thamani ya sarafu kulinganisha na dola ya Marekani ni tatizo, “angalia Machi kiwango kilikuwa dola moja kwa Sh 1,400 leo ni Sh 1,600,” alisema mchambuzi ambaye hakuta kutajwa jina.

Asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia umeme huku asilimia iliyosalia ambayo wengi ni wananchi masikini waishio vijijini, wanatumia mafuta ya taa kumulikia na hata kupikia, hivyo bei ya nishati hiyo inapopanda inawaumiza.

Wakati huo huo, habari zilizopatikana jana jioni Dodoma, zilisema leo Serikali inatarajiwa kutangaza bei mpya ya mafuta nchini, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kukokotoa kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali

MKUU WA SHULE NA MAKAMU WAKE WAPOKEZANA KUFUNDISHA SHULE NZIMA YA MSINGI MCHUCHUMA LUDEWA

Mwalimu mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Mchuchuma wilaya ya Ludewa mkoani Iringa Bw.Joseph Thomas Lugome (58) akionyesha darasa la saba ambalo limekuwa likisomewa pia na wanafunzi wa darasa la sita kwa kupokezana na darasa la saba kutokana na shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 200 kuwa na walimu wawili pekee

SHULE ya msingi Mchuchuma katika wilaya ya Ludewa mkoani Iringa yenye wanafunzi 208 wakiwemo wanafunzi wasichana 90 na wavulana 118 imekuwa ikifundishwa na mkuu wa shule na makamu mkuu wa shule pekee ambao wote ni wanaume .

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari za mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP ) mkoani Iringa umebaini kuwepo kwa hali hiyo ambayo pia imekuwa ikiwapa wakati mgumu walimu hao hasa pindi wanafunzi wa kike wanapougua na kuhitaji msaada wa kupelekwa katika matibabu .

Hata hivyo kutokana na upungufu mkubwa wa walimu katika shule hiyo ambayo inaelezwa kujengwa juu ya madini ya mchuchuma na linganga ,umekuwa ukikwamisha kwa kiasi kikubwa ufaulu wa wanafunzi katika shule hiyo na kupelekea baadhi ya watoto kuacha shule kwa kutokana na kukosa walimu wa kuwafundisha .

Mmoja kati ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo Augustino Haule alisema kuwa kwa upande wake alikuwa na watoto wawili waliokuwa wakisoma katika shule hiyo ila mmoja wa kike ambaye alikuwa darasa la saba amelazimika kumwachisha shule baada ya muda mwingi kushida mitaani baada ya walimu kutofundisha mara kwa mara.

Haule alisema kuwa mbali ya walimu kuwa wachache katika shule hiyo ila bado mazingira ya shule hiyo yamekuwa yakichangia watoto kuacha shule kutokana na muda mwingi kufanya kazi za kupika na kuchota maji ya walimu umbali wa zaidi ya kilomita 2 kutoka katika shule hiyo.

Pia alisema kuwa ni vema serikali kuifunga kabisa shule hiyo hadi pale itakapolipatia ufumbuzi tatizo la upungufu wa walimu kuliko serikali kuendelea kuwaacha wanafunzi zaidi ya 200 kufundishwa na walimu wawili pekee tena wote wakiwa ni wanaume.

Mwalimu mkuu mssaidizi wa shule hiyo Joseph Lugome alithibitisha uhaba huo wa walimu katika shule hiyo na kuwa hadi sasa kwa zaidi ya wiki mbili mwalimu amebaki peke yake baada ya mwenzake kupata matatizo ya kiafya.

Alisema kuwa katika shule hiyo wanafunzi 47 ni darasa la saba ambao wanangoja kufanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi na kati ya wanafunzi hao wasichana ni 24 na wavulana ni 25 huku wanafunzi wa darasa la nne katika shule hiyo ni 10 pekee wasichana wakiwa 11 na wavulana 8.

Hata hivyo alisema kuwa kutokana na shule hiyo kutokuwa na maji wanafunzi wamekuwa wakipagiwa zamu ya kuchota maji ya walimu umbali wa kilomita zaidi ya 2 kutoka katika shule hiyo ili kutoka nafasi ya walimu kufundisha wanafunzi wengine .

Kwani alisema kuwa iwapo walimu wataondoka na kwenda kutafuta maji basi upo uwezekano wa wanafunzi kuendelea kukosa vipindi .

Lugome alisema kuwa wakati mwingine shule hiyo imekuwa ikifungwa kwa muda iwapo wanafunzi zaidi ya mmoja wataugua na walimu hao kufanya kazi ya kuwabeba mgongoni wanafunzi hao wagonjwa na kuwapeleka zahanati iliyopo kijiji cha jirani kilichopo umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya 12 kijiji cha Nkomang'ombe.

Pamoja na mazingira hayo ya kufundisha yakiwa magumu bado mwaka jana shule hiyo darasa la saba ambalo lilikuwa na wanafunzi 36 wanafunzi 8 walifaulu kujiunga na elimu ya sekondari.

Aidha alisema kuwa mbinu za ufundishaji ambazo zimekuwa zikitumiwa katika shule hiyo yenye walimu wawili ni pamoja na kuunganisha madarasa kwa kufanya darasa la kwanza na la pili ndani ya chumba kimoja na darasa la tatu na la nne kuwa ndani ya darasa moja na darasa la sita wamekuwa wakisoma kwa kupokezana na wale wa darasa la saba.

Mwalimu Lugome alisema kuwa tatizo la utoro kwa wanafunzi limekuwa ni sugu kwa kipindi cha masika zaidi kutokana na wanafunzi kutoka mbali na shule hiyo umbali wa zaidi ya kilomita 2 na kuwa kutokana na mvua na mito kujaa maji wa wanafunzi ambao wamekuwa wakifika shule ni 100 ama 90 pekee na sehemu kubwa hushindwa kufika shule.

Afisa elimu wa wilaya ya Ludewa Robart Hyella amethibitisha kuwepo kwa tatizo la uhaba wa walimu katika shule za msingi ndani ya wilaya hiyo na kuwa shule zinazoongoza kwa upungufu wa walimu ni zile za pembezoni mwa wilaya hiyo .

Monday, August 1, 2011

Wanasiasa walichoka Bunge

WANASIASA wakiwemo viongozi wastaafu pamoja na wazee, jana waliungana na Watanzania wengine kuelezea kukerwa na tabia ya baadhi ya wabunge kutokuwa na uadilifu na kukidharua kiti cha Spika wa Bunge.

Wengi wamesema, Bunge sasa ni la vichekesho, la mzaha, vurugu, kupiga zeze, la shuleni na la watu wanaokesha katika baa; baadhi wakiwataka waasisi wa taifa kunusuru hali hiyo huku wengine wakisema hakuna imani kwa Cha Cha Mapinduzi (CCM) wala upinzani.

Baadhi ya wanasiasa hao wameelezea hofu yao ya kubadilika kwa dhamira za wanaogombea ubunge; badala ya uwakilishi, wanafuata ajira na kuonya hali ikiendelea hivyo, hata wagombea urais wajao, watafuata maslahi binafsi Ikulu.

Aliyekuwa Mbunge wa Kwela mkoani Rukwa, Dk. Chrisant Mzindakaya alisema Bunge la sasa limekuwa linaendeshwa kama ‘kupiga zeze’ na wabunge wanajua Kanuni moja tu ya 68 ya kuomba Mwongozo wa Spika.

Aliwaasa wabunge wa CCM kutotumbukia katika malumbano hayo na badala yake wajibu hoja za upinzani kistaarabu.

Akilichambua Bunge hilo la 10, Mzindakaya aliyekaa bungeni kwa zaidi ya miaka 35, alisema ni tofauti na Bunge lililohusisha wapinzani kati ya mwaka 1995 na 2005 ambapo kulikuwa na umoja wa kitaifa, uadilifu na kuheshimu Kanuni, lakini hili la sasa limekuwa linaendeshwa kama ‘kupiga zeze’.

“Kutoa mawazo ni jambo zuri ingawa si lazima kukubaliana… wabunge sasa hawana utaifa wameweka mbele itikadi za kisiasa, hii si nzuri.

“Mfano katika Bunge la zamani tuliwahi kwenda Uingereza na tukaulizwa jinsi tutakavyotatua tofauti za kisiasa Zanzibar wakati huo mwafaka haukuwepo, lakini Mbunge wa CUF (hakumtaja jina) alijibu kizalendo kwamba lengo la vyama vyote ni kuijenga Zanzibar.

“Ukiangalia televisheni leo unaona Bunge limekuwa la vichekesho, lina wasomi wengi na vijana wasio na uadilifu, hawaheshimu Kanuni wala kiti cha Spika na kila anayesimama anajua Kanuni ya 68 tu; ya kuomba Mwongozo wa Spika,” alisema Dk. Mzindakaya na kuongeza:

“Haitakiwi kanuni kumuachia Spika peke yake, wote wanapaswa wazisome… wabunge wabadilike wajue ukishakuwa kiongozi unaacha kwenda baa kukaa kwenye kiti kirefu na mambo yasiyo na maadili na raha unaachana nazo.”

Alisema Mbunge mwadilifu hawezi kula rushwa, lakini wabunge wa sasa wameanza kupoteza uadilifu na sababu kuu ni kubadilika kwa malengo ya kuingia bungeni ambapo wapo wanaotaka uwaziri na wanakuwa wabunge bila wito, bali ajira.

Alieleza hofu yake katika miaka ijayo pia watakaogombea urais watakuwa wanatafuta ajira na maslahi yao na si wito wa kuwatumikia wananchi. Aliwataka wabunge wa CCM waisaidie Serikali yao kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kujibu hoja.

“Upinzani wanafanya makusudi kuharibu system (mfumo)…nao CCM wasipoangalia miaka mitano itaisha kwa malumbano ya kisiasa na hawatarudi bungeni maana hawatakuwa na kitu walichofanya cha kuwasaidia wananchi,” alieleza mwanasiasa huyo mkongwe.

Pia alizungumzia tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaojisifu kuwa na urafiki na Rais Jakaya Kikwete, alisema; “Rais akikupa uongozi, urafiki unakufa, unatakiwa ufanye kazi zaidi tena kwa uadilifu ili usimfedheheshe na ukimsikia mtu anajisifu Rais rafiki yake ujue hana akili.”

Chama Cha Kijamii (CCK), pamoja na kutokuwa na mwakilishi bungeni, jana kililaani tabia hizo za baadhi ya wabunge kuwa zinalifanya Bunge liwe eneo la mzaha na vurugu.

Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muhabi aliwataka waasisi wa Taifa waliobaki au viongozi wengine wenye utashi na ushawishi wa kubadili mwenendo huo potofu wa Bunge la sasa kutumia busara zao kulinusuru.

Muhabi alisema hali hiyo ikiachwa, inaashiria hatari ya kulifanya Bunge lipoteze umuhimu wake kwa kuwa kinachoendelea ndani ya mhimili huo muhimu ni matokeo ya kuwepo na viongozi wabinafsi na wenye kujali maslahi yao.

“Wabunge hawaheshimu kanuni …wala kufanya kazi waliyotumwa na waliowachagua, wenye kulala haya, wenye kuonyesha hasira zao… wanajiropokea na wenye kuonyesha umahiri wa kuvunja kanuni na kutomheshimu Spika nao wanajipa nafasi bila aibu.

“Endapo viongozi wengine waliobahatika kuasisi Taifa hili na Hayati Mwalimu Julius Nyerere au waliobahatika kuzishika busara na kuiga maadili yake wataendelea kujifungia kwenye mageti nyumbani mwao… hali itakuwa ya hatari,” alisema Muhabi.

Alisifu uongozi wa Bunge hilo kwa kuwachukulia hatua wanaovunja kanuni kwa kuwatoa nje ya ukumbi na kupendekeza kuandaliwe utaratibu maalumu wa viongozi wenye busara akiwemo Rais Kikwete kuwahutubia wabunge kuhusu maadili na nidhamu binafsi mara kwa mara. *Mbatia alia ni Bunge la kishule-shule

Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia alisema malumbano hayo yanatokana na mfumo wa elimu uliopo na kukosekana kwa Chuo cha Uongozi uliosababisha bunge liwe la kishule.

Mbatia alisema kutokuwepo kwa chuo hicho kumesababisha wabunge wengi wachaguliwe bila kujua maana ya uongozi na hivyo kujikuta wanafanya mambo yasiyo ya kawaida na kutumia vipaza sauti kwa jazba bila mpangilio.

“Zamani watu wote wanaoongoza walipita Kivukoni na kujifunza maadili ya uongozi lakini leo hii vijana wanatoka shuleni moja kwa moja wanaingia bungeni na kufanya mambo yao ya kishule- shule.

“Tuachane na siasa nyepesi, maana tukitaka kuonyeshana mbabe kuliko mwingine, tutaliangamiza Taifa na tutaharibu kizazi chetu, tunatakiwa sote tukae kwenye meza moja ya mazungumzo na tuangalie matatizo yanayoikabili nchi kwa sasa,” alisema Mbatia.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Idd Simba alisema Bunge sasa halina maadili wala uzalendo, bali mvurugano.

Samba alisema anachokiona ni kundi la watu wachache waliodhamiria kugawa na kumaliza nguvu ya CCM kwa uchu wa kutaka kuingia Ikulu kwa lazima na kuonya wazee wa chama hicho wamejipanga nchi nzima kupambana nalo.

Simba akizungumza jana, Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na baadhi ya magazeti, alidai hali ni mbaya na tete, haivumiliki kwa kuwa inahatarisha amani iliyodumu kwa zaidi ya miaka hamsini.

“Hali ya siasa ni mbaya, watu wachache wanafanya mambo kwa maslahi yao huku wakidai wanamuenzi Mwalimu Nyerere, Mwalimu hakuwa hivyo.

“Angalia Bunge vyama vinagombana si kutoa huduma kama elimu, maji na afya, bali vyeo, wananchi hawana imani na chama tawala, wala upinzani wala mfumo wenyewe wa vyama vingi,” alisema Simba. Simba aliyewahi kuwa Mbunge wa Ilala na Waziri wa Viwanda na Biashara, alisema wazee wanajipanga kuwashikisha adabu wanasiasa wasio na nidhamu na kuhakikisha kuwa, CCM inarejesha imani, heshima na kuondoa udhaifu uliopo katika chama na siasa za nchi.