Thursday, April 30, 2009

TANESCO yaingizwa katika kashfa mpya


-CAG abaini malipo tata ya mabilioni

-Ni yanayolipwa kampuni ya Songas

-Sasa Bunge kuwasha moto mpya

UTATA mpya umeibuka katika mkataba wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ukihusu shirika hilo la umma na kampuni ya kuzalisha umeme ya Songas Limited, iliyolipwa kila mwezi zaidi Sh Bilioni tano katika mazingira yanayotia shaka, imefahamika.

Fedha hizo ni zile zilizolipwa na TANESCO kila mwezi kwa ajili ya kununua umeme kutoka kampuni ya Songas Ltd ya Dar es Salaam, ikiwa ni malipo ya ‘capacity charges’ zinazoelezwa kwamba si sahihi, na zimelipwa katika mazingira tata.

Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amependekeza kupitiwa upya kwa mkataba huo unaotajwa kumalizika muda wake miaka 25 ijayo, yaani mwaka 2024. Bunge linatarajiwa kuazimia kumuunga mkono CAG kuhusu suala hilo.

Hatua hiyo ya Bunge inatokana na taarifa ya CAG ya ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa fedha 2007/2008 ndani ya TANESCO, shirika ambalo linaaminika kuwa katika matatizo makubwa ya kifedha lakini likiwa na mianya mingi ya kupoteza fedha, hususan katika ununuzi wa umeme kutoka kampuni binafsi au zenye ubia na Serikali.

Soma zaidi

Mwakyembe kulipua bomu la Kiwira bungeni



-Ben Mkapa kuguswa

WAKATI wowote kuanzia leo, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe atawasilisha hoja binafsi kuhusu mgodi wa Kiwira ili kuwatetea wafanyakazi wa mgodi huo ambao hawajalipwa mishahara yao kwa zaidi ya miezi 10, hali inayowafanya kushindwa kumudu gharama za maisha.

Dk. Mwakyembe amelazimika kuchukua hatua hiyo ambayo imekubaliwa na uongozi wa Bunge hususan Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah kutokana na kile kinachoelezwa kuwa shinikizo la wafanyakazi hao kwa mbunge wa eneo ulipo mgodi huo.

Wafanyakazi wa mgodi huo ambao wamepunjwa malipo ya mafao yao na kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi 10 sasa, wanadai wamefikia hatua hiyo kutokana na ukimya wa Serikali katika kushughulia matatizo hayo.

Soma zaidi

Tuesday, April 28, 2009

A to Z Kugawa Vyandarua kwa Watoto.

Tarehe 25/04/2009 ilikuwa ni siku ya maralia duniani. Siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka kukumbuka madhara yanayosababishwa na maralia, huambatana na shughuli mbalimbali kutoka kwa wadau wanaopambana na ugonjwa huu. Hapa nchini, kampuni ya kutengeneza vyandarua ya A to Z ya mjini Arusha inatarajiwa kugawa vyandarua vya mbu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano nchi nzima. Tunapongeza harakati kama hizi zenye lengo la kutoa nafuu kwa wananchi walio wengi.
Soma zaidi habari hii kwa kubofya hapa.

Habari zaidi kuhusiana na Siku ya Malaria duniani bofya hapa
www.worldmalariaday.org
http://www.rbm.who.int/worldmalariaday/index.html

Friday, April 24, 2009

Kigoda cha Mwalimu: Ni wakati wa umma kuongoza

TAMASHA la Kigoda cha Mwalimu Nyerere, limemalizika kwa mafanikio makubwa. Chuo kikuu cha Dar es Salaam, kimeweka historia isiyofutika.

Heshima ya chuo hicho iliyovuma miaka ya sabini na wakati wa mapambano ya ukombozi wa nchi za Afrika zilizokuwa zikikaliwa na wakoloni na Makaburu, imerudi kwa kasi mpya.

Vijana wanauliza: Leo hii tunawaimbia sifa za Mwalimu; tunawaimbia fikra za Mwalimu na mchango wa Mwalimu wa kuikomboa Tanzania na kuzikomboa nchi nyingine za Afrika; tunawaimba wimbo wa Nkrumah na wanamapinduzi wengine wa Afrika; wimbo wa utumwa na Ukoloni: Je wao watawaimbia wimbo gani watoto wao na wajukuu wao?

Kwa lugha nyepesi, swali la vijana ni je, sisi kizazi chetu kimefanya nini? Kigoda cha Mwalimu, ambacho hapo baadaye kitaratibu masomo ya Umajumuhi wa Afrika, ni jibu la swali la vijana wa Tanzania na vijana wa Afrika!

Tamasha hili lilikuwa na matukio mengi; mengine ya kuburudisha, kufurahisha, kufundisha na kutafakarisha, lakini mengine ya kusikitisha. Ni vigumu kuyaandika yote hapa. Ni imani yangu kwamba mengine yataandikwa au yameandikwa tayari na kuchambuliwa na wengine. Mimi nitaongelea machache ambayo yaliugusa moyo wangu na niliyaona kama changamoto kubwa:

Soma zaidi

Thursday, April 23, 2009

Elimu kwa Vijana na Watu Wazima Tanzania: Je, Imepewa Kipaumbele?

Katika mfululizo wa semina za GDSS, jumatano ya tarehe 22/04/2009 mada ilikuwa ni “Elimu kwa Vijana na Watu Wazima Tanzania; Je, Imepewa Kipaumbele? Watoa mada walikuwa ni Profesa mshiriki kutoka UDSM dada E.P Bhalalusesa na Anthony Itelema afisa elimu kutoka wizara ya Elimu kitengo cha elimu kwa watu wazima, na mwezeshaji alikuwa ni dada Shekilango.

Dada Bhalalusesa alieleza maana ya kuelimika kama ilivyotafsiriwa na UNESCO; ni uwezo wa mtu kusoma na kuandika katika maisha yake ya kila siku. Mtu wazima ni mtu yeyote anayekubali majukumu katika jamii na anayejitegemea na vijana walitafsiriwa kuanzia umri wa miaka 14-35.
Aprili 2000, wawakilishi kutoka nchi 164 walikutana Dakar senegal na kukubalina juu ya Azimio la elimu kwa wote duniani (World Declaration on Education For All- EFA), miaka saba baadae(2007), kuna zaidi ya watu wazima milioni 774 wasiojua kusoma wala kuandika duniani, wanawake wakiwa 64% ya watu wote wasiojua kusoma. Nchini Tanzania EWW ilikuwa na msukumo sana baada ya uhuru mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1980 ilipoanza kushuka kutokana na sera mpya za SAPs. Juhudi za serikali za kutaka kufikia usawa kupitia elimu ziliisha na nguvu kuelekezwa katika shughuli za kiuchumi, hivyo EWW haikuwa tena ajenda kuu katika maendeleo ya nchi. Vituo vingi vya EWW vilifungwa kutokana na utoro, pia serikali iliacha kutoa fedha kwa ajili ya EWW. Kwa sasa idadi ya watu wasiojua kusoma nchini Tanzania inakadiriwa kufikia 69.4% ya wananchi wote.

Mwaka 2000+ juhudi za kutokomeza ujinga kwa watu wazima zikaanza upya, serikali kupitia wizara ya elimu ikandaa na kutekeleza sera na mipango kadhaa yenye lengo la kuurithi mpango wa EWW. Mipango kama MKUKUTA, MEMKWA, MUKEJA, ilibuniwa na kutekelezwa ili kuhakikisha dira ya taifa ya mwaka 2025 yenye lengo la kuwa na jamii iliyoelemika ikifikiwa. Lakini pamoja na juhudi hizi bado kuna changamoto nyingi ambazo serikali inakutana nazo ambazo ni pamoja na; tafsiri mbaya ya dhana ya elimu ya watu wazima, ukosefu wa sera na mipango thabiti ya kuinua EWW, upungufu wa rasilimali, kukosekana kwa utashi wa kisiasa, na wananchi kukosa utashi wa kushiriki katika mipango hii.

Pia washiriki waliainisha changamoto zingine katika sekta ya elimu nchini ambazo ni; kukosekana kwa sera ya wazi ya EWW, umasikini unasababisha wananchi wengi kushindwa kushiriki katika maswala ya elimu, kukosekana kwa uzalendo kwa wananchi na viongozi kunakosababisha jamii ikose upendo, serikali haijatoa kipaumbele kwa mpango wa EWW, hivyo mpango huu hauna malengo, mipango na rasilimali za kutosha kuutekeleza.

Nini kifanyike?
Katika nini kifanyike, washiriki walipendekeza maoni yafuatayo;

• Wananchi wawashinikize viongozi wao wanaoomba kura wawaeleze mipango yao ya kuboresha EWW kabla ya kuwapigia kura, na wanasiasa waahidi kutekeleza ahadi hizo.
• Serikali iianzishe vituo vya EWW kuanzia ngazi ya Kata na kutoa ruzuku ya kutosha kwa vituo hivi ili viweze kutoa huduma.
• CBOs zishirikiane na serikali katika kuboresha EWW nchini kote.
• Wizara ipitishe mpango wa kuwatumia walimu waliopo kufundisha katika vituo vya EWW kama overtime, hii inaweza kupunguza upungufu wa walimu wa EWW.
• Turudishe moyo wa zamani wa uzalendo ambao ulitusaidia kulitumikia taifa letu, tofauti na sasa ambapo viongozi wengi wapo kwa ajili ya maslahi binafsi.
• Tutafute falasfa ya kutungoza katika swala la elimu. Enzi za mwalimu, falsafsa yetu ya Elimu ya Kujitegemea ilisaidia sana kujenga jamii ambayo iliweka mbele maslahi ya taifa na hivyo elimu ilipewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ujinga.
• Serikali iwe na sera thabiti ya EWW, tofauti na sasa ambapo kuna mipango kadhaa ambayo inatumiwa kama dira ya kufikia malengo ya EWW kwa wote.

Kama Mwananchi wa kawaida unafanya nini kuhakikisha Elimu ya Watu Wazima Inaboreshwa Nchini Tanzania?

Tuesday, April 21, 2009

Tunaungana na Prof Soyinka juu ya Kuwakosoa Viongozi wetu

Wiki iliyopita katika 'Wiki ya kazi za Kitaaluma za Nyerere' pale UDSM mambo mengi yalizungumzwa na kuazimiwa kutekelezwa katika kuelekea Afrika moja yenye maendeleo ya kweli kwa wananchi wake. Jambo moja muhimu ambalo sisi kama wanaharakati hatuna budi kuliwekea mkazo ambalo Prof. Wole Soyinka aliligusia ni pamoja ule uwezo wa wananchi kuwakosoa viongozi wao na viongozi kukubali kukosolewa kama njia ya kujirekebisha na kufanya vizuri zaidi katika siku za usoni. Katika Afrika yetu ya leo yenye matatizo mengi- ukosefu wa huduma za msingi za afya, barabara, maji, umeme, shule, rushwa iliyokithiri, uongozi mbovu, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukatili wa kijinsia na n.k Kwa nini Viongozi wetu wakatae Kukosolewa? soma zaidi.

Monday, April 20, 2009

Wangekuwa na Robo tu ya Sifa za Nyerere…

Wiki jana muhimu na ya aina yake si tu kwa sisi tunaosisimshwa na kuhamasishwa na maisha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere; bali Watanzania wote kwa ujumla. Ni wiki ya tamasha la kumuenzi Mwalimu Nyerere.

Miongoni mwa wanazuoni maarufu duniani ambao wamekuja Dar es Salaam kushiriki tamasha hili linaloendelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni mshindi wa tuzo ya Nobel, Profesa Wole Soyinka, mtoto wa Nkwame Nkrumah anayeitwa Gamal Nkrumah na mtoto wa Frantz Fanon (mtunzi wa The Wretched of the Earth) anayeitwa Olivier Fanon, kwa kuwataja wachache.

Kwamba miaka kumi baada ya kifo chake wanazuoni mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani wanasafiri na kuja nchini kujiunga na wenzao (kina Shivji) kuhudhuria tamasha hili la kumuenzi, ni ushahidi wa wazi kwamba Nyerere alikuwa zawadi ya pekee ya Mungu kwa Watanzania, na kamwe fikra zake hazitakufa kabisa kwa wapenda haki na amani duniani. soma zaidi.

Sunday, April 19, 2009

Mrejesho wa GDSS: Kampeni ya Utafiti wa Ugonjwa wa Fistula – Manyoni Singida.

Jumatano ya tarehe 15/04/2009 katika mfululizo wa semina za jinsia na maendeleo mada
ilikuwa ni Muendelezo wa Kampeni dhidi ya Fistula, ambapo ulitolewa Mrejesho wa Utafiti wa ugonjwa wa Fistula uliofanywa na Utu Mwanamke katika kata kumi na moja (11) za wilaya ya Manyoni mkoani Singida. Waongoza mada walikuwa ni Anna Sangai (TGNP) na Modestus Kamonga (Daktari Mwanafunzi -Muhimbili University).

Kampeni hii ilifanywa na timu ya watu kumi na moja, na wilaya ya Manyoni ilichaguliwa kwa sababu ni eneo ambalo limeathirika sana na ugonjwa huu. Wagonjwa 19 walipatiwa huduma na 11 kati yao waliletwa Dar es salaam kwa matibabu zaidi. Katika kampeni hii wananchi walifundishwa kuhusu Ukweli kuhusu Fistula, chanzo chake, madhara, jinsi ya kujikinga na fistula, na tiba zake.

Vyanzo ambavyo vinasababisha mwanamke apate fistula ni pamoja na; mtoto kuwa mkubwa kuliko viungo vya uzazi; mtoto kukaa vibaya tumboni; kupata ujauzito katika umri mdogo (wataalamu wanashauri kuanzia miaka 18); kupata ujazito katika kipindi kifupi (mama anashauriwa apumzike angalau miaka mitatu kabla ya kujifungua tena); sababu zinazosababishwa na wataalamu wa afya katika kuokoa maisha ya mama wakati wa kujifungua; mila potufu za ukeketaji na kujifungulia nyumbani kwa kuamini ni ujasiri; na matatizo ya ujauzito wa mara ya kwanza na kukosa msaada wakati wa kujifungua.

Fistula inaweza kuzuilika kama mama atapata huduma za mwanzo za kliniki hivyo ataweza kufahamu ni lini atajifungua, uweze na hali ya mtoto tumboni, kupata ushauri mbalimbali kutoka kwa wataalamu na pia mama akijiepusha na vihatarishi vilivyotajwa. Hospitali zinazotibu fistula ni pamoja na; Kituo teule CCBRT, Muhimbili, Bugando, Kambi Maalumu Dodoma, na KCMC-Moshi.

Hamasa ya kampeni.
Katika kampeni hii ya fistula mashirika kadhaa yalishirikiana kufanikisha zoezi hili, mshirika hayo ni; TGNP -Utetezi na Ushawishi, Utu mwanamke kutoa taarifa na takwimu mbalimbali, hospitali ya CCBRT kutoa bure huduma kwa wagonjwa waliopatikana, na habari zilisambazwa na kituo cha TBC 1.

Yaliyojiri katika kampeni.
Mambo matatu yaliyojiri ni; Tatizo la mfumo dume limechangia kwa kiasi kikubwa ugonjwa huu kuendelea kuwepo, kwa mfano baadhi ya wanaume wameshindwa kuwapeleka wake zao kliniki hivyo kukosa taarifa muhimu za maendeleo ya afya za wake zao; mila potofu ambazo zinalelewa na mfumo dume kwa mfano ukeketaji; wanawake kukosa sauti na maamuzi juu ya afya ya uzazi na kupelekea kuzaa bila mpangilio pamoja na kukosa huduma muhimu wakati wa kipindi cha ujauzito. Ukatili na ukali wa baadhi ya wahudumu wa afya ni chanzo kimojawapo cha fistula kilichotajwa katika utafiti huu (kwa mfano wahudumu wengine kutowahudumia wajawazito mpaka wapewe chochote kitu). Umbali wa vituo vya afya na makazi ya wanakijiji huchangia kwa kiasi kikubwa akinamama kupata fistula (kwa mfano katika baadhi ya vijiji vituo vya afya vya karibu vipo umbali wa kilomita 50, na mara nyingi vituo hivi havina madawa muhimu wala wataalamu wa kutosha, pia barabara hazipitiki na vituo hivi havina magari ya wagonjwa).

Nini Kifanyike?
* Kuwapa nguvu wanawake ili wajitambue na kuweza kupambana na mfumo dume ambao umechangia kuwakandamiza na kusababisha wakose fursa ya kupata huduma bora za afya ya uzazi kwa wakati muafaka na hatimaye kupelekea kupatwa na magonjwa kama fistula.
* Kutoa elimu zaidi kwa akina mama li waweze kutumia vituo vya afya vilivyopo karibu na maeneo yao na kujiepusha na mila potofu zinawagandamiza.
* Kupinga mila na desturi zote potofu ambazo zinazuia akinamama kujifungilia katika vituo vya afya na badala yake kushawishi wajifungilie
* Kuhimiza serikali kuandaa vifaa na wataalamu wa kutosha wa maswala ya afya ya uzazi kwani ni jukumu la serikali kuandaa vitu hivyo na vitasaidia kupunguza wanawake kupata fistula na vifo vya uzazi.
* Kuandaa ajenda ya kitaifa ili kuuelimisha na kuhamasisha umma juu ya ugonjwa huu wa fistula na umuhimu wa kuutokomeza ugonjwa kwani inawezekana.
* Ushirikishwaji wa wanaume katika huduma ya afya ya mama na mtoto ni muhimu uwe wa pande mbili badala ya kuachiwa akina mama peke yao, hivyo kuweka msukumo kwa akina baba kwenda kliniki na wake zao ili kuweza kuwa na taarifa za afya za wake zao.


Kama Mwanaharakati unafanya nini kuhakikisha Fistula inatokemezwa nchini Tanzania? Je, Unashiriki vipi katika kukomesha Fistula?

Kwa maelezo zaidi tembelea; www.womensdignity.org

Friday, April 17, 2009

Wanazuoni katika wiki ya Mwalimu Nyerere


Kushoto ni Prof.Saida Othman, katikati ni Prof.Marjorie Mbilinyi na kulia ni Prof.Amandina Lihamba. Nao walijumuika pamoja na halaiki ya wanazuoni katika wiki ya Mwalimu Nyerere ukumbi wa Nkrumah Chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Thursday, April 16, 2009

Filamu ya Nyerere kuonyeshwa DStv

Filamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, inatarajiwa kuonyeshwa Jumapili ijayo katika chanel ya M-net kupitia DStv. Akizungumza na waandishi wa habari jana, mtayarishaji wa sinema hiyo kutoka Kampuni ya utengenezaji sinema, Savannah, Imruh Bakari alisema filamu hiyo ni ya dakika 51.

Alisema filamu ya Mwalimu Nyerere ni moja kati ya filamu sita zitakazoonyeshwa katika chanel hiyo zinazowazungumzia viongozi wengine mahiri wa Afrika. Bakari alisema sinema hiyo imetumia miaka miwili kuitengeneza na imeshirikisha wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Naye mwongozaji wa filamu hiyo, Lekoko Ole Levilal, alisema katika utengenezaji wake walikumbana na changamoto mbalimbali. Alisema changamoto kubwa mojawapo ni ugumu wa kutengeneza filamu kuhusiana na maisha ya mtu ambaye amefariki dunia. Filamu hiyo ilizinduliwa rasmi juzi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Tamasha la Kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere, linaloendelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tumpambe Mwalimu Nyerere kwa kuunganisha Afrika

KAULIMBIU ya Tamasha la Kigoda cha Mwalimu ni: Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni lazima iungane.

Sina uhakika kama walioandaa tamasha hili, wanaichukulia kaulimbiu hii kama “wimbo” wa kuburudisha na kuchangamsha na baadaye maisha yanaendelea kama kawaida; au wanaichukulia kaulimbiu hii kama mvinyo; kuna msemo kwamba penye mvinyo pana ukweli!

Mvinyo ukitoka kichwani, ukweli unageuka uongo? Je, kaulimbiu hii ni kama tulizozizoea za wanasiasa? Wasomi wetu wanaamini kaulimbiu hii? Tamasha litaendeshwa kwa lugha gani? Kiswahili, Kiyoruba, Kinyarwanda na Kiganda, au Kiingereza na Kifaransa?

Kwa nini zisitumike lugha za Afrika, wakawapo “wasomi” wakatafsiri? Usomi, ni pamoja na kuzifahamu vizuri lugha zetu; kuzitumia lugha zetu kuelimishana na kuunda mshikamano. Bila hivyo tutagawanywa makundi makundi kwa kutumia lugha za kigeni na kuendeleza ukoloni mamboleo. Afrika haiwezi kuungana bila kuwa na lugha zake, fikra zake na falsafa yake. Afrika haiwezi kuungana kama tunaendelea kuimba wimbo bila matendo.

Ni wazi kwenye tamasha tutaimba mashairi na nyimbo, tutacheza ngoma na kuimba ngonjera. Tutakunywa mvinyo na kutema cheche za ukweli wote! La msingi na ambalo ni muhimu, ni kwamba nyimbo hizo, mashairi hayo na ngojera hizo zisipite kama mvua za masika. Zipande mbegu ya kuota, mbegu ya kuendeleza mawazo ya Mwalimu Nyerere, ya Umoja wa Afrika. Mvinyo tukaokunywa, utusukume kutema cheche cha ukweli usiogeukwa, ukweli wa kudumu, ukweli wa kujenga Umoja wa Afrika.

Mwalimu Nyerere, hakuimba wimbo wa Binadamu wote ni sawa, Afrika ni moja na Afrika ni Lazima iungane; hakutumia mvinyo ili aseme ukweli. Alitekeleza kwa matendo! Ndiyo maana wakati wa uongozi wake, Tanzania, ilikuwa kimbilio la kila mwanadamu. Wapigania uhuru walikaribishwa Tanzania na kuishi kama nyumbani kwao; walipotaka kutembelea nchi za nje kama Ulaya na kwingineko, walitumia pasi za Tanzania; walianzisha makambi ya mapambano hapa hapa Tanzania. Uganda, ilipopinduliwa na kutawaliwa na Iddi Amin, Mwalimu, alikataa kukaa kimya, alifanya uamuzi mgumu wa kuingilia kwenye mapambano ya vita vya Kagera. Hatukusikia lugha ya wahamiaji haramu wakati wa uongozi wa Mwalimu.

Sasa hivi ni kinyume. Watanzania tumeanza kujenga utamaduni wa ubaguzi, tena ubaguzi mbaya kabisa. Hivi karibuni Tanzania, tumekuwa na zoezi la kuwafukuza wahamiaji haramu kutoka Rwanda, Burundi na Uganda. Hawa tunaunganishwa na damu, na wengine tunazungumza lugha moja na utamaduni unaofanana, lakini tunateganishwa na mipaka ya kikoloni.

Hata hivyo, kwa nini tufukuzane, badala ya kushirikiana? Kwa nini tufukuzane wakati tunaimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki? Wakati tunaimba wimbo wa Umoja wa Afrika? Tutaungana bila kuishi pamoja?

Kwanini wahamiaji haramu, wasishawishiwe kuishi kwa vibali na kama wanafanya biashara au uwekezaji kwenye mifugo na viwanda, watozwe kodi na kuchangia pato la taifa? Kama mtu anaweza kuwekeza kutoka Marekani, kwa nini Warundi, Wanyarwanda na Waganda wasiwekeze? Kwa nini tusijenge daraja la kuunganisha Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda na Uganda na daraja hili likaendelea kutuunganisha na nchi za kuzini, kaskazini na magharibi mwa Afrika?

Tanzania haikuwa na ubaguzi. Serikali ya awamu ya kwanza hadi awamu ya pili haikuwa na dalili za ubaguzi. Msamiati wa “Wahamiaji haramu” hatukuufahamu! Mbegu ya ubaguzi imepandwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu.

Mwaka 1997 Tanzania iliamuwa kuwarudisha kwa nguvu nyumbani wakimbizi wa Kihutu kutoka Rwanda. Hili lilikuwa ni zoezi la kikatili ambalo nililishuhudia. Kuna wakimbizi ambao walitembea zaidi ya kilomita 100 kwa miguu kuufikia mpaka wa Tanzania na Rwanda wakisindikizwa na wanajeshi.

Baada ya zoezi hili la kikatili, tulianza kusikia watu wakinyang’anywa uraia kwa vigezo vya kuangalia pua zao za Kitutsi na historia yao. Wale wenye asili ya Rwanda, Burundi na Uganda, walibaguliwa! Wengine walisombwa na kupelekwa kwenye nchi hizi bila utashi wao. Baadhi walikuwa wameishi Tanzania maisha yao yote tokea vizazi vya mababu kutokana na mipaka ya kikoloni.

Zoezi hili la wahamiaji haramu limeendelea hadi kwenye serikali ya awamu ya nne. Tanzania nchi iliyokuwa ikuuchukia ubaguzi, sasa inaongoza kwa vitendo vya kibaguzi.

Wakati ubaguzi huu unaota mizizi, wasomi wetu wanaopigia debe Umoja wa Afrika wako wapi? Ni kweli kwamba kuna baadhi ya wasomi wanaunga mkono Shirikisho la Afrika ya Mashariki; wangependa twende haraka kuuda shirikisho. Lakini pia kuna wasomi wanopinga kwa nguvu zote kuanzishwa kwa shirikisho na wengine wanakwenda mbali hata kuupinga Muungano wa Tanzania. Wangependa zirudi tena Tanganyika na Zanzibar!

La kushangaza ni kwamba baadhi ya wasomi hawa wanaopinga shirikisho na Muungano wetu, ni waumini wa Umoja wa Afrika! Wakisimama kuzungumza wanatetea umoja wa Afrika kwa nguvu zote. Ikifika wakati wa matendo, wanajionyesha walivyo! Wanahubiri wasiyoyaishi, wanahubiri wasiyoyapenda! Wanafiki!

Hivyo kuna haja wakati tunamkumbuka Mwalimu, na hasa tunapomkumbuka katika anga za kisomi, kuelezea jinsi wasomi, wa hapa na wa nje wanavyosaliti jitihada zilizoanzishwa na wasomi waliotangulia za kutetea na kuelezea umuhimu wa Umoja wa Afrika. Hapa Tanzania, tumemsaliti Mwalimu Nyerere; tumesaliti jitihada zake za kuwaruhusu Waafrika wote kuja na kuishi Tanzania, tumesaliti jitihada zake za kupigania ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, tumesaliti jihudi zake za South-South Commission, tumesaliti juhudi zake za upatanishi wa mgogoro wa Burundi.

Kuna mwamko wa nchi za Afrika kupeleka askari wa kulinda amani kwenye nchi za Afrika zenye mapigano. Majeshi yamepelekwa DRC, Darfur, Somalia na kwingineko. Hata majeshi yetu yanashiriki. Hizi ni dalili nzuri, lakini haziondoi matatizo ya nchi husika. Haziondoi umasikini, haziondoi ujinga, hazijengi demokrasia na utawala bora. Kuna haja ya nchi hizi masikini, nchi hizi ambazo zina rasilimali nyingi kuungana ili ziwe na nguvu ya kupambana kwa pamoja.

Kama anavyosema Profesa Mwesiga Baregu: “ Kinachojitokeza baada ya kuchambua makubaliano na taratibu zilizopo ni kwamba mpaka sasa amani, ulinzi na usalama katika Afrika Mashariki unatawaliwa na maana finyu inayozingatia zaidi vyombo vya ulinzi na usalama.

Kwa kuwa mashambulizi ya nchi hizi kutoka nje hayatazamiwi, majeshi yataendelea kuelekeza nguvu zake katika kuthibiti migogoro na kukabiliana na maafa pale yanapojitokeza. Majukumu haya yatayasogeza majeshi ya ulinzi karibu sana na raia kuliko tulivyozoea.

Hili linaweza kuwa jambo zuri la kuleta amani ndani ya raia. Lakini vile vile linaweza kuleta madhara hasa pale ambapo majeshi haya hayajaandaliwa vizuri kwa majukumu haya mapya. Athari moja inaweza kuwa migongano kati ya raia na wanajeshi pale ambapo maslahi ya raia yanakinzana na ya wanajeshi. Athari ya pili inawezekana ikawa mgongano kati ya wanajeshi na askari hasa pale ambapo mipaka ya mamlaka inaingiliwa bila mwongozo maalum. Athari nyingine na kubwa zaidi inaweza kuwa kuingiza hofu ndani ya jamii na kujenga misingi ya udikteta au utawala wa kijeshi. Hili linaweza kuathiri sana haki za binadamu na raia na kurudisha nyuma mipaka ya demokrasia kwa kujenga jamii yenye woga wa ki-siasa.

“Katika hali kama hii kuna haja ya kutambua kimsingi kwamba hiki ni kipindi cha mpito na kwamba ni muhimu kufanya maadalizi ya kukabili mipito hii kwa wakati mmoja. Mchakato wa kutoka kwenye dola ndogo ndogo na hafifu kuelekea shirikisho la Afrika tukipitia shirikisho za kanda kama Afrika ya Mashariki.

Kuna ulazima wa kuelewa ki-msingi na kutangaza kwa uwazi kwamba suala la nchi za Afrika kufanya juhudi pevu za kuugana si la hiari lakini la ulazima kama Afrika na Waafrika wataendelea kuwapo, kujilinda, kulinda mali zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya ulimwengu.

Hatua hii itahitaji upeo, ujasiri na uwezo wa kuthubutu kubadilisha historia ya Afrika.”

Tunahitaji kuunganisha nguvu, tunahitaji mifumo ya kulifanya Bara la Afrika kuwa bara lenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kielimu. Tunahitaji mifumo ya kulifanya Bara la Afika kuwa na watu wenye afya njema na wanaoishi kwa miaka mingi. Tunahitaji mifuno ya kulifanya Bara la Afrika kuwa na imani iliyojengwa na kusimikwa juu ya udongo wa Afrika. Mungu, aliyeiumba Afrika, ndiye huyo huyo aiyeshusha imani yake kwake. Haiwezekani Mungu, akaiumba Afrika na kuicha yatima hadi zilipokuja dini za kigeni.

Tunahitaji kuwa na vyuo vikuu vya Afrika, vinavyofundisha kwa kutumia lugha za Afrika, na kufundisha falsafa ya Afrika. Tunahitaji kujijengea uwezo wa kuweza kupamba na utandawazi. Tishio kubwa la Afrika ni utandawazi, kama anavyosema, amini na kufundisha Profesa Baregu.

Kwa maoni yake silaha ya kupambana na utandawazi ni umoja. Anakataa yale mawazo kwamba utandawazi ni kijiji. Kwa maoni yake, kijiji daima ni maeneo yenye usalama. Mtu ukifika kijijini unakuwa unatarajia kupata malazi, chakula na maji ya kunywa. Utandawazi hauna undugu wa kijiji, na hasa kijiji cha Afrika.

Kwake yeye utandawazi ni pori! Na ili mtu upite salama kwenye pori ni lazima uwe na silaha, vinginevyo unakuwa kitoweo cha simba! Profesa Baregu, anatupatia mtizamo mpya kabisa wa kufananisha utandawazi na pori.

Hivyo tusiimbe wimbo wa Umoja wa Afrika, tusiimbe wimbo wa Binadamu wote ni sawa, bali tutekeleze falsafa hii. Tusimkumbuke Mwalimu Nyerere, kwa mihadhara mizuri ya kupendeza, bali tuunde mifumo ya kutuwezesha kutekeleza falsafa hii ambayo ni urithi wetu mkubwa.

Mwalimu aliwaheshimu binadamu wote na alifanya jambo hilo kwa matendo! Mwalimu aliamini kwamba Afrika ni lazima iungane; na alifanya hivyo kwa matendo kwa kufungua milango ya Tanzania kwa kila Mwafrika. Kigoda cha Mwalimu kiwe taa ya kutuongoza hadi kufikia Umoja wa Afrika. Mungu Ibariki Afrika! Mungu wabariki watoto wa Afrika.

Thursday, April 9, 2009

Mrejesho wa GDSS: Mrejesho wa Utafiti wa 'Hatuna Chaguo'

Katika mfululizo wa semina za GDSS wiki hii ya tarehe 08/04/2009 mada ilikuwa ni "Mitizamo na Uzoefu wa Wanawake wa Kitanzania, Wahudumu wa Afya na Wakunga wa Jadi" Lengo la semina ni kuangalia na kujadili mrejesho wa utafiti uliofanywa na Utu Mwanamke, Care TZ, Chama cha wakunga wa jadi Tanzania(TAMA)na GRAFCA, katika wilaya tatu za Tunduru, Mpwapwa, na Kwimba. Utafiti huu uliobeba jina la 'Hatuna Chaguo'(We have no Choice), ulilenga kuelewa vikwazo vikuu ambavyo wanawake wanakumbana navyo katika upatikanaji na utumiaji wa huduma za kujifungua, na vikwazo ambavyo watoa huduma wanakumbana navyo katika utoaji wa huduma bora za kujifungua.

Mtoa mada dada Festa Andrew kutoka Utu Mwanamke, alitoa mrejesho wa utafiti huo na kutoa nafasi kwa washiriki kujadili ripoti ya tafiti hiyo. Tafiti imeonyesha wanawake waliohojiwa wanapenda kujifungulia katika vituo vya afya, isipokuwa hali ya umasikini waliyonayo na ubora hafifu wa huduma hizi katika vituo vya serikali inawapelekea wajifungulie nyumbani ama kwa wakunga wa jadi. Vikwazo vingine ambavyo vinavyochangia wanawake kutokwenda kujifungulia katika vituo vya afya ni pamoja na; Umbali kufikia katika vituo vya huduma- kwa mfano, Tunduru kituo cha karibu ni kilomita 32; Mpwapwa ni kilomita 58-, Ukosefu wa usafiri wakati wa uchungu, gharama zilizo rasmi na zisizo rasmi. Shuhuda zinaonyesha kwamba sera ya serikali ya kutoa huduma za uzazi bila malipo haijatosheleza au haitekelezwi kikamilifu.

Utafiti pia ulitoa Mapendekezo kwa ajili ya koboresha Upatikanaji, Utumiaji, na Utoaji wa Huduma za kujifungua ni pamoja na:

• Kueneza, kutekeleza, na kusimamia kitaifa sera ya serikali inayowaondolea wanawake malipo kwa ajili ya huduma ya uzazi.
• Kupanua huduma kabambe za dharura za uzazi –ikiwemo upasuaji- kwa hospitali zote za wilaya na asilimia 50 ya vituo vya afya ifikapo 2015. Kipaumbele zaidi kwa maeneo ya pembezoni.
• Kuanzishwa kwa mfumo imara wa afya ili kuhakikisha uwajibikaji katika utoaji wa huduma bora za afya.
• Kusambaza kitaifa ‘Mkataba wa huduma kwa Mteja’ ili watumiaji huduma wajue haki zao.
• Kuanzishwa utaratibu imara wa wazi wa kushughukia malalamiko, utakaoshughulikia maoni ya watumiaji wa huduma na watoa huduma.
• Kuajiri na kusambaza watumishi wa afya wenye ujuzi ili kupanua magawanyo wa wakunga wenye ujuzi kwenye maeneo ya pembezoni.
• Kuhakikisha maji, usafi, huduma za utupaji taka, na umeme wa kuaminika vinapatikana katika vituo vyote vya afya.
• Kuwa na usambazaji mfufulizo kwa madawa muhimu kwa ajili ya kujifungulia.

Katika kuhitimisha mtoa mada aliwapa nafasi washiriki waweze kuchangia juu ya utafiti na kuangalia jinsi ya kupeleka taarifa hizi kwa wananchi na kuandaa na mpango wa pamoja katika kufanikisha mapendekezo haya yanafanyiwa kazi na serikali.

Washiriki waliona vifo hivi vinavyotokana na uzazi (wanawake 24 wanakufa kwa siku, 8000 kwa mwaka) bado ni changamaoto kubwa ambayo wanaharakati wanaweza kuwahoji wanasiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mtaa na uchaguzi mkuu mwakani, je wamefanya nini ama wamejipanga vipi kuhakikishga vifo hivi vinapungua?

Pia ni muhimu kwa wanaharakati kuandaa mkakati maalumu wa 'kuichallange' serikali ili iboreshe sekta ya afya, ukiangalia kwa makini guideline za bajeti kwa mwaka huu 2009/10 inaonyesha wazi kwamba bado sekta ya afya haijapewa kipaumbele sana na serikali yetu(Afya, Maji, na elimu imepewa 29.2% ya bajeti yote), ingawa serikali yetu ilisaini makubaliano ya Abuja juu ya afya ya mwaka 2001. Je serikali inatekeleza mkataba huu wa Abuja na mikataba mingine inayoitaka kuongeza bajeti ya sekta ya afya?

Wanaharakati walibainisha ukosefu wa rasilimali ni changamoto mojawapo ambayo inakwamisha kupeleka elimu kama hii kwa wananchi walio wengi maeneo ya vijijini ambao ndio wenye matatizo makubwa ya kupata huduma hizi za uzazi na afya kwa ujumla.

Pia washiriki walipendekeza iandaliwe mijadala ya kitaifa ambayo itajadili hali hii ya vifo vinavyotokana na uzazi kote nchini, ikianzia katika ngazi ya serikali za mitaa na kata, kupitia katika kamati za afya za mitaa, vijiji na kata.

Jamii inapaswa kuelimishwa kwamba vifo hivi vinavyotokana na uzazi havitokani na mipango ya Mungu na wala si hali ya kawaida, bali ni hali ambayo inawezwa kuzuilika kabisa ikiwa wanajamii watasimama pamoja na kuifanyia kazi kuitokomeza.

Kwa utashi imara wa kisiasa na mikakati ya kutoa maamuzi katika ngazi zote, vifo vitokanavyo na uzazi nchini Tanzania vinaweza kupunguzwa kwa haraka. Kama mwananchi unashiriki vipi katika kufanikisha vifo hivi vya uzazi vinatokemea?

Hatufiki popote bila kuwekeza kwenye elimu ya taifa

NIMESHAWISHIKA kuchangia katika mjadala unaoendelea kuhusu sekta ya elimu nchini. Katika hoja zangu nitaongozwa na dhana niipendayo ya maslahi ya umma (public good au the greater good).

Katika hitimisho nitajaribu kueleza ni kwa vipi mfumo wa mikopo ya elimu ya juu nchini unaweza kuchochea hulka za ufisadi miongoni mwa wasomi na wataalamu.

Kwa bahati nzuri, Tanzania imejitahidi kujenga na kuendeleza misingi ya elimu. Hadi sasa tuna idadi kubwa ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu. Kwa maana hiyo, maendeleo ya elimu peke yake si kigezo tosha cha kuleta maendeleo ya taifa.

Mwaka 2002 Rais Jacques Chirac wa Ufaransa alisema: “Hatuwezi kupata maendeleo ya jamii bila kuzalisha mali, na mali haiwezi kuzalishwa bila elimu na uwekezaji.”

Rais Chirac hakusema tuhangaikie kupata elimu peke yake, bali alituasa kuhusu kigezo kingine muhimu ambacho ni uwekezaji. Na hapa ndipo tunastahili kujiuliza na kutafakari kikamilifu iwapo elimu yetu inafuata misingi ya uwekezaji.

Inawezekana tukapata jibu la haraka kwamba upo uwekezaji wa kutosha, kwa maana kwamba tunaingiza fedha na rasilimali katika miradi ya elimu, tunazalisha wataalamu wengi, tunafanya utafiti mwingi, na pia tunarejesha fedha zinazokopeshwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Lakini pamoja na yote hayo, bado hatujapata maendeleo. Rasilimali zetu bado hazitumiki kikamilifu, na elimu yetu bado ina matatatizo. Wakati tunajiuliza, tunaweza kujifunza kutoka kwa majirani zetu kama Uganda.

Mwaka 2007, Rais Museveni wa Uganda alisema: “Japokuwa serikali yetu imewekeza sana katika elimu ya msingi, na sasa katika elimu ya sekondari, tunahitaji jitihada zaidi katika kuongeza ubora. Nimeelezwa kuwa tatizo letu katika sekta ya elimu si fedha, bali ni ukosefu wa ufanisi katika kutengeneza mazao ya akili, ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko mazao ya kawaida”.

Kulingana na maoni hayo ya Rais Museveni, umasikini wa taifa unakomaa kutokana na uwekezaji hafifu katika elimu au taaluma. Kiini cha tatizo hili ni hulka za ubinafsi au fikra finyu katika taaluma.

Undani wa jambo hili unapatikana pia toka kwa Rais wa zamani wa Marekani, Theodore Roosevelt ambaye mwaka 1910 alisema: “Endapo elimu ya mtu yeyote haiongozwi na kurekebishwa na maadili thabiti, basi kadri mtu huyo atakavyoendelea kuongeza elimu yake ndivyo atakavyozidi kuwa mbovu, na ndivyo atakavyoendelea kuwa hatari zaidi katika jamii.

Roosevelt anaongeza: “Juhudi, elimu, au sifa zozote humfanya binadamu awe fedhuli mbaya zaidi iwapo zitalenga tu kutimiza haja zake binafsi za maendeleo katika mazingira ya uadui yanayopuuza maendeleo ya jamii nzima.”

Ufedhuli wa kukosa mwamko wa elimu ya taifa tunauona bayana katika kilio cha Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambaye mwaka 1999 alisema kwamba: “Ilifika wakati ambapo maafisa wa serikali walizama kabisa katika hulka ya ufisadi na kutothamini maadili ya uongozi, na walionyesha mwamko hafifu sana katika kushughulikia maendeleo ya jamii na maslahi ya umma.”

Miaka mitano baadaye kilio kama hicho kilisikika tena huko Guyana ambako Rais Bharrat Jagdeo alisema: “Watu waliokabidhiwa majukumu ya kuongoza nyanja mbalimbali za maendeleo wangeweza kuleta mafanikio makubwa zaidi kama wangejitahidi kuonyesha upendo kwa umma na kujali zaidi maslahi ya jamii nzima.”

Katika siku za karibuni wanasiasa, wabunge, wasomi, na wananchi wengi hapa Tanzania wametafakari matatizo ya ufisadi katika nchi yetu. Hata hivyo zipo athari kubwa zaidi za kifikra na kitaaluma ambazo bado hatujazibaini; ingawaja tayari zimejitokeza bayana.

Rais Barrack Obama wa Marekani, mwaka 2006, akiwa seneta, alisema: “Ufisadi unayo tabia ya kuchochea usugu wa matatizo makuu katika maisha ya jamii, kwani huvuruga upeo wa kufikiri na kutafakari jinsi ya kushughulikia majanga mbali mbali”.

Kadhalika, Obama alibaini kuwa “ufisadi hudiriki kupandisha juu zaidi ngazi au kamba ya kutokea katika dimbwi la umasikini, kiasi kwamba jitihada za kujinasua miongoni mwa wanyonge waliozama katika dimbwi hilo hulazimishwa daima kuwa ndoto zisizotekelezeka”.

Kama alivyobashiri Obama, hapa Tanzania tumeona bayana kwamba ufisadi umefanikiwa kudhoofisha mifumo yetu ya kufikiri, kujadili, kukubaliana, kuamua, na kutekeleza mikakati ya kutatua matatizo makubwa ya kitaifa, hasa katika eneo la nishati.

Hii ina maana kuwa hata kama fedha zote zilizochotwa na mafisadi zingerudishwa ghafla, au kama tukiamua kusamehe fedha hizo, bado tutabaki na ulegevu ulioletwa na sumu ya ufisadi katika kufikiri na kutatua matatizo.

Matokeo ya udhaifu huu ni kwamba tumefikishwa mahali ambapo tunaambiwa kuchagua kati ya kukumbatia ufisadi au kuzama katika giza totoro.

Kama tunakubaliana kwamba hatutaki ufisadi na pia hatutaki kuingia katika giza totoro, au matatizo mengineyo kama hayo, tutakuwa tumejenga imani kwamba ipo njia ya tatu ya kutokea, inayoweza kutupeleka katika hali ya afueni zaidi. Na njia hiyo ya tatu haiwezi kupatikana katika mazingira yoyote zaidi ya kuwekeza katika elimu ya taifa, ili kuifanya taaluma iwe rasilimali na mwongozo kwa ajili ya maendeleo ya taifa zima.

Mara nyingi sana tumejiuliza swali la kwa nini tunabaki masikini wakati tunazo rasilimali za kutosha bila kupata majibu ya uhakika. Nadiriki kusema kuwa jibu pekee ni kuwa bado nchi yetu haina ubunifu wa kitaaluma unaoweza kujenga mahusiano bora zaidi baina ya misingi ya maendeleo.

Mwalimu Nyerere alituasa vizuri sana kuhusu misingi ya maendeleo na umuhimu wa taaluma katika taifa. Lakini kwa bahati mbaya, Nyerere hakusema tangia mwanzo kuwa elimu ni mojawapo kati ya misingi mikuu ya maendeleo.

Hata hivyo, ni dhahiri kabisa kuwa Nyerere alitambua na kueleza bayana umuhimu wa elimu, na alitumia rasilimali nyingi za taifa kuimarisha elimu kama msingi wa maendeleo.

Naamini kuwa Mwalimu Nyerere asingeweza kamwe kusahau kutaja elimu miongoni mwa misingi mikuu ya maendeleo, na hii inanifanya niamini kuwa alichotaka tuelewe ni kwamba elimu ndiyo mama wa misingi yote ya maendeleo.

Hata hivyo, hatuwezi kuliacha jambo hili libaki katika ngazi ya hisia kwa muda wote. Tunayo nafasi na jukumu la kutafakari fikra za Mwalimu Nyerere katika mazingira ya sasa, na naamini kwamba Rais Kikwete tayari ameonyesha nia ya kutuongoza kuona kwamba elimu lazima ichukue nafasi ya kipekee katika harakati za maendeleo ya taifa.

Ili tuweze kuinua uchumi na maendeleo ya taifa ni lazima tuwekeze katika elimu kwa mtazamo wa kuunganisha nguvu za taaluma na utafiti katika kukuza na kuendeleza rasilimali na kila raia lazima achangie na afaidike.

Kuchangia gharama za elimu, kupatikana mikopo ya elimu ya juu toka serikalini, na kupanua miundombinu au taasisi za elimu ni baadhi ya mikakati inayoweza kulifanya taifa liwe na watu wengi wenye elimu na ajira, ambalo ni jambo lenye manufaa mengi.

Hata hivyo, haya yote bado hayatoshi kukamilisha lengo kuu la elimu katika maslahi ya taifa. Maendeleo ya taifa hayapatikani kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wenye ujuzi au wenye ajira, bali ni kutokana na michango ya ubunifu toka kwa watu ambao hudhamiria na kuwezeshwa kufika katika kilele cha malengo ya elimu.

Ni rahisi zaidi kufika katika kilele cha elimu, na ni rahisi zaidi kuyajua yale ambayo waliofika kileleni huonekana kuyafanya, kuyasema, au kuyaandika. Ni rahisi pia kupata vyeti na vyeo vinavyohusiana na sifa za elimu ya juu.

Jambo gumu ni jinsi gani mafanikio au malengo hayo yanaweza kupitishwa katikati ya maslahi binafsi, hadi kufikia upeo wa fikra na ubunifu wenye maslahi ya taifa.

Elimu ya juu nchini inaelekea kuongozwa na mikakati iliyo chini ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu, yaani HESLB. Hata hivyo, hatuna budi kubaini kwamba mfumo huu wa mikopo unaathiri sana mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa.

Hii ni kwa sababu mfumo huu unajenga hisia potofu kwamba wanafunzi katika vyuo vikuu wanagharamia au kulipia elimu yao, na kwa hiyo wanao uhuru wa kukidhi maslahi yao binafsi. Lakini ukweli ni kwamba HESLB haitoi mikopo kwa wanafunzi, na wala wanafunzi hawagharamii elimu yao. Kinachotokea ni kichekesho chenye hasara, ambacho ni kwamba serikali inatoa ruzuku ya elimu kwa wanafunzi, wanafunzi wanagharamia kuwapo kwa HESLB, na HESLB inasababisha wanafunzi wakosane na serikali na wakose mwamko wa kuchangia katika elimu ya taifa na maendeleo ya jamii.

Ili kuwekeza kikamilifu katika elimu, ni bora serikali iondokane na dhana ya mikopo ya elimu ya juu, na badala yake irudi katika mfumo wa ruzuku toka wizarani. Katika kukamilisha uwekezaji huo, serikali ianzishe utaratibu bora zaidi wa kutambua na kugharamia wanafunzi wenye mwelekeo wa kuendeleza elimu ya taifa kupitia mfumo wa ruzuku.

Kwa maana hii ni lazima serikali iwe tayari kutumia fedha za umma kuendeleza wasomi wanaoweza kuishauri katika jitihada za kendeleza rasilimali, kuokoa fedha, kujenga imani ya wananchi, kudumisha amani na kulinda maslahi ya vizazi vijavyo.

Kupitia mfumo wa ruzuku, serikali inaweza kutumia fedha zinazoitwa mikopo bila kuwa na migomo katika vyuo vikuu.

Hapo itawezekana kukusanya fedha zaidi kupitia ubunifu na usimamizi wa wataalamu wanaopata elimu. Badala ya kumdai mtaalamu arejeshe mkopo kwa miaka 20, mfumo wa ruzuku unaweza kumfanya asimamie vizuri uzalishaji au uokoaji wa fedha za umma kiasi cha kurejesha fedha hizo ndani ya mwaka mmoja, hasa katika sekta za madini, uvuvi na ukusanyaji wa kodi.

Licha ya kusimamia uzalishaji na kubuni mbinu za kuendeleza rasilimali za taifa, wataalamu hao na raia wote bado watawajibika kulipa kodi, na ambayo bado inaweza kujumuisha makisio ya marejesho ya ruzuku au mikopo hiyo inayotumika katika elimu ya juu.

Jambo la msingi hapa ni kwamba elimu ya taifa ni ubunifu wa ziada, ambao mtu anaweza akauficha iwapo amechukizwa na mfumo uliopo. Ili kuweka uwazi unaofaa, watu wenye vipaji lazima wagharamiwe na umma na kisha wahudumie umma.

Utaratibu wa sasa wa kupima utajiri wa kila mzazi na kumtaka alipie gharama za mtoto wake hautusaidii kujenga misingi ya elimu ya taifa. Badala yake, wananchi wenye uwezo kifedha wanastahili kuchangia zaidi katika elimu kupitia malipo ya kodi ya kila mwaka.

Iwapo hao wenye uwezo kifedha watalipa kodi kikamilifu, serikali itaweza kutoa ruzuku kubwa zaidi kugharamia elimu. Kadhalika mfumo huu wa kodi na ruzuku utawafanya matajiri wote wachangie elimu kila wakati, badala ya kusubiri waingize watoto wao katika vyuo vikuu.

Miongoni mwa matatizo makuu ambayo nahisi yameanza kujitokeza kutokana na sera za HESLB ni mfumuko wa kugushi vyeti vya kidato cha sita. Baada ya kutangazwa utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu, inaelekea hata wizi wa mitihani umepitwa na wakati. Badala yake, upo uwezekano kuwa tayari kuna wimbi baya zaidi la kugushi na kununua vyeti vya daraja la kwanza vya kidato cha sita, kama sehemu ya kutafuta mikopo ya HESLB.

Inawezekana tukawa na idadi kubwa ya wanafunzi walio mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu ambao wamechaguliwa kwa kutumia vyeti vya aina hii. Sasa hivi wapo wanafunzi wengi sana ambao baada ya kupata daraja la nne katika kidato cha nne, wamebadilika ghafla na kupata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha sita!

Uzoefu wangu unanilazimisha nifikiri kuwa jambo hili haliwezekani bila kugushi vyeti kwa mbinu kali, na wala si wizi wa mitihani.

Kwa hiyo, basi, bila kuwa na mfumo bora wa elimu na kuwekeza katika elimu, tutaendelea kutoa mikopo kwa watu ambao hata kidato cha nne hawajafika, mradi tu wamekaa mjini na kujua wapi vinatengenezwa vyeti vinavyoonekana kuwa halisi, nje ya taratibu za Baraza la Mitihani la Taifa.

Wilfred Kahumuza ni mdau wa sekta ya elimu nchini wa muda mrefu.

Hatufiki popote bila kuwekeza kwenye elimu ya taifa

NIMESHAWISHIKA kuchangia katika mjadala unaoendelea kuhusu sekta ya elimu nchini. Katika hoja zangu nitaongozwa na dhana niipendayo ya maslahi ya umma (public good au the greater good).

Katika hitimisho nitajaribu kueleza ni kwa vipi mfumo wa mikopo ya elimu ya juu nchini unaweza kuchochea hulka za ufisadi miongoni mwa wasomi na wataalamu.

Kwa bahati nzuri, Tanzania imejitahidi kujenga na kuendeleza misingi ya elimu. Hadi sasa tuna idadi kubwa ya shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu. Kwa maana hiyo, maendeleo ya elimu peke yake si kigezo tosha cha kuleta maendeleo ya taifa.

Mwaka 2002 Rais Jacques Chirac wa Ufaransa alisema: “Hatuwezi kupata maendeleo ya jamii bila kuzalisha mali, na mali haiwezi kuzalishwa bila elimu na uwekezaji.”

Rais Chirac hakusema tuhangaikie kupata elimu peke yake, bali alituasa kuhusu kigezo kingine muhimu ambacho ni uwekezaji. Na hapa ndipo tunastahili kujiuliza na kutafakari kikamilifu iwapo elimu yetu inafuata misingi ya uwekezaji.

Inawezekana tukapata jibu la haraka kwamba upo uwekezaji wa kutosha, kwa maana kwamba tunaingiza fedha na rasilimali katika miradi ya elimu, tunazalisha wataalamu wengi, tunafanya utafiti mwingi, na pia tunarejesha fedha zinazokopeshwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Lakini pamoja na yote hayo, bado hatujapata maendeleo. Rasilimali zetu bado hazitumiki kikamilifu, na elimu yetu bado ina matatatizo. Wakati tunajiuliza, tunaweza kujifunza kutoka kwa majirani zetu kama Uganda.

Mwaka 2007, Rais Museveni wa Uganda alisema: “Japokuwa serikali yetu imewekeza sana katika elimu ya msingi, na sasa katika elimu ya sekondari, tunahitaji jitihada zaidi katika kuongeza ubora. Nimeelezwa kuwa tatizo letu katika sekta ya elimu si fedha, bali ni ukosefu wa ufanisi katika kutengeneza mazao ya akili, ambayo yana thamani kubwa zaidi kuliko mazao ya kawaida”.

Kulingana na maoni hayo ya Rais Museveni, umasikini wa taifa unakomaa kutokana na uwekezaji hafifu katika elimu au taaluma. Kiini cha tatizo hili ni hulka za ubinafsi au fikra finyu katika taaluma.

Undani wa jambo hili unapatikana pia toka kwa Rais wa zamani wa Marekani, Theodore Roosevelt ambaye mwaka 1910 alisema: “Endapo elimu ya mtu yeyote haiongozwi na kurekebishwa na maadili thabiti, basi kadri mtu huyo atakavyoendelea kuongeza elimu yake ndivyo atakavyozidi kuwa mbovu, na ndivyo atakavyoendelea kuwa hatari zaidi katika jamii.

Roosevelt anaongeza: “Juhudi, elimu, au sifa zozote humfanya binadamu awe fedhuli mbaya zaidi iwapo zitalenga tu kutimiza haja zake binafsi za maendeleo katika mazingira ya uadui yanayopuuza maendeleo ya jamii nzima.”

Ufedhuli wa kukosa mwamko wa elimu ya taifa tunauona bayana katika kilio cha Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambaye mwaka 1999 alisema kwamba: “Ilifika wakati ambapo maafisa wa serikali walizama kabisa katika hulka ya ufisadi na kutothamini maadili ya uongozi, na walionyesha mwamko hafifu sana katika kushughulikia maendeleo ya jamii na maslahi ya umma.”

Miaka mitano baadaye kilio kama hicho kilisikika tena huko Guyana ambako Rais Bharrat Jagdeo alisema: “Watu waliokabidhiwa majukumu ya kuongoza nyanja mbalimbali za maendeleo wangeweza kuleta mafanikio makubwa zaidi kama wangejitahidi kuonyesha upendo kwa umma na kujali zaidi maslahi ya jamii nzima.”

Katika siku za karibuni wanasiasa, wabunge, wasomi, na wananchi wengi hapa Tanzania wametafakari matatizo ya ufisadi katika nchi yetu. Hata hivyo zipo athari kubwa zaidi za kifikra na kitaaluma ambazo bado hatujazibaini; ingawaja tayari zimejitokeza bayana.

Rais Barrack Obama wa Marekani, mwaka 2006, akiwa seneta, alisema: “Ufisadi unayo tabia ya kuchochea usugu wa matatizo makuu katika maisha ya jamii, kwani huvuruga upeo wa kufikiri na kutafakari jinsi ya kushughulikia majanga mbali mbali”.

Kadhalika, Obama alibaini kuwa “ufisadi hudiriki kupandisha juu zaidi ngazi au kamba ya kutokea katika dimbwi la umasikini, kiasi kwamba jitihada za kujinasua miongoni mwa wanyonge waliozama katika dimbwi hilo hulazimishwa daima kuwa ndoto zisizotekelezeka”.

Kama alivyobashiri Obama, hapa Tanzania tumeona bayana kwamba ufisadi umefanikiwa kudhoofisha mifumo yetu ya kufikiri, kujadili, kukubaliana, kuamua, na kutekeleza mikakati ya kutatua matatizo makubwa ya kitaifa, hasa katika eneo la nishati.

Hii ina maana kuwa hata kama fedha zote zilizochotwa na mafisadi zingerudishwa ghafla, au kama tukiamua kusamehe fedha hizo, bado tutabaki na ulegevu ulioletwa na sumu ya ufisadi katika kufikiri na kutatua matatizo.

Matokeo ya udhaifu huu ni kwamba tumefikishwa mahali ambapo tunaambiwa kuchagua kati ya kukumbatia ufisadi au kuzama katika giza totoro.

Kama tunakubaliana kwamba hatutaki ufisadi na pia hatutaki kuingia katika giza totoro, au matatizo mengineyo kama hayo, tutakuwa tumejenga imani kwamba ipo njia ya tatu ya kutokea, inayoweza kutupeleka katika hali ya afueni zaidi. Na njia hiyo ya tatu haiwezi kupatikana katika mazingira yoyote zaidi ya kuwekeza katika elimu ya taifa, ili kuifanya taaluma iwe rasilimali na mwongozo kwa ajili ya maendeleo ya taifa zima.

Mara nyingi sana tumejiuliza swali la kwa nini tunabaki masikini wakati tunazo rasilimali za kutosha bila kupata majibu ya uhakika. Nadiriki kusema kuwa jibu pekee ni kuwa bado nchi yetu haina ubunifu wa kitaaluma unaoweza kujenga mahusiano bora zaidi baina ya misingi ya maendeleo.

Mwalimu Nyerere alituasa vizuri sana kuhusu misingi ya maendeleo na umuhimu wa taaluma katika taifa. Lakini kwa bahati mbaya, Nyerere hakusema tangia mwanzo kuwa elimu ni mojawapo kati ya misingi mikuu ya maendeleo.

Hata hivyo, ni dhahiri kabisa kuwa Nyerere alitambua na kueleza bayana umuhimu wa elimu, na alitumia rasilimali nyingi za taifa kuimarisha elimu kama msingi wa maendeleo.

Naamini kuwa Mwalimu Nyerere asingeweza kamwe kusahau kutaja elimu miongoni mwa misingi mikuu ya maendeleo, na hii inanifanya niamini kuwa alichotaka tuelewe ni kwamba elimu ndiyo mama wa misingi yote ya maendeleo.

Hata hivyo, hatuwezi kuliacha jambo hili libaki katika ngazi ya hisia kwa muda wote. Tunayo nafasi na jukumu la kutafakari fikra za Mwalimu Nyerere katika mazingira ya sasa, na naamini kwamba Rais Kikwete tayari ameonyesha nia ya kutuongoza kuona kwamba elimu lazima ichukue nafasi ya kipekee katika harakati za maendeleo ya taifa.

Ili tuweze kuinua uchumi na maendeleo ya taifa ni lazima tuwekeze katika elimu kwa mtazamo wa kuunganisha nguvu za taaluma na utafiti katika kukuza na kuendeleza rasilimali na kila raia lazima achangie na afaidike.

Kuchangia gharama za elimu, kupatikana mikopo ya elimu ya juu toka serikalini, na kupanua miundombinu au taasisi za elimu ni baadhi ya mikakati inayoweza kulifanya taifa liwe na watu wengi wenye elimu na ajira, ambalo ni jambo lenye manufaa mengi.

Hata hivyo, haya yote bado hayatoshi kukamilisha lengo kuu la elimu katika maslahi ya taifa. Maendeleo ya taifa hayapatikani kutokana na kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wenye ujuzi au wenye ajira, bali ni kutokana na michango ya ubunifu toka kwa watu ambao hudhamiria na kuwezeshwa kufika katika kilele cha malengo ya elimu.

Ni rahisi zaidi kufika katika kilele cha elimu, na ni rahisi zaidi kuyajua yale ambayo waliofika kileleni huonekana kuyafanya, kuyasema, au kuyaandika. Ni rahisi pia kupata vyeti na vyeo vinavyohusiana na sifa za elimu ya juu.

Jambo gumu ni jinsi gani mafanikio au malengo hayo yanaweza kupitishwa katikati ya maslahi binafsi, hadi kufikia upeo wa fikra na ubunifu wenye maslahi ya taifa.

Elimu ya juu nchini inaelekea kuongozwa na mikakati iliyo chini ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu, yaani HESLB. Hata hivyo, hatuna budi kubaini kwamba mfumo huu wa mikopo unaathiri sana mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa.

Hii ni kwa sababu mfumo huu unajenga hisia potofu kwamba wanafunzi katika vyuo vikuu wanagharamia au kulipia elimu yao, na kwa hiyo wanao uhuru wa kukidhi maslahi yao binafsi. Lakini ukweli ni kwamba HESLB haitoi mikopo kwa wanafunzi, na wala wanafunzi hawagharamii elimu yao. Kinachotokea ni kichekesho chenye hasara, ambacho ni kwamba serikali inatoa ruzuku ya elimu kwa wanafunzi, wanafunzi wanagharamia kuwapo kwa HESLB, na HESLB inasababisha wanafunzi wakosane na serikali na wakose mwamko wa kuchangia katika elimu ya taifa na maendeleo ya jamii.

Ili kuwekeza kikamilifu katika elimu, ni bora serikali iondokane na dhana ya mikopo ya elimu ya juu, na badala yake irudi katika mfumo wa ruzuku toka wizarani. Katika kukamilisha uwekezaji huo, serikali ianzishe utaratibu bora zaidi wa kutambua na kugharamia wanafunzi wenye mwelekeo wa kuendeleza elimu ya taifa kupitia mfumo wa ruzuku.

Kwa maana hii ni lazima serikali iwe tayari kutumia fedha za umma kuendeleza wasomi wanaoweza kuishauri katika jitihada za kendeleza rasilimali, kuokoa fedha, kujenga imani ya wananchi, kudumisha amani na kulinda maslahi ya vizazi vijavyo.

Kupitia mfumo wa ruzuku, serikali inaweza kutumia fedha zinazoitwa mikopo bila kuwa na migomo katika vyuo vikuu.

Hapo itawezekana kukusanya fedha zaidi kupitia ubunifu na usimamizi wa wataalamu wanaopata elimu. Badala ya kumdai mtaalamu arejeshe mkopo kwa miaka 20, mfumo wa ruzuku unaweza kumfanya asimamie vizuri uzalishaji au uokoaji wa fedha za umma kiasi cha kurejesha fedha hizo ndani ya mwaka mmoja, hasa katika sekta za madini, uvuvi na ukusanyaji wa kodi.

Licha ya kusimamia uzalishaji na kubuni mbinu za kuendeleza rasilimali za taifa, wataalamu hao na raia wote bado watawajibika kulipa kodi, na ambayo bado inaweza kujumuisha makisio ya marejesho ya ruzuku au mikopo hiyo inayotumika katika elimu ya juu.

Jambo la msingi hapa ni kwamba elimu ya taifa ni ubunifu wa ziada, ambao mtu anaweza akauficha iwapo amechukizwa na mfumo uliopo. Ili kuweka uwazi unaofaa, watu wenye vipaji lazima wagharamiwe na umma na kisha wahudumie umma.

Utaratibu wa sasa wa kupima utajiri wa kila mzazi na kumtaka alipie gharama za mtoto wake hautusaidii kujenga misingi ya elimu ya taifa. Badala yake, wananchi wenye uwezo kifedha wanastahili kuchangia zaidi katika elimu kupitia malipo ya kodi ya kila mwaka.

Iwapo hao wenye uwezo kifedha watalipa kodi kikamilifu, serikali itaweza kutoa ruzuku kubwa zaidi kugharamia elimu. Kadhalika mfumo huu wa kodi na ruzuku utawafanya matajiri wote wachangie elimu kila wakati, badala ya kusubiri waingize watoto wao katika vyuo vikuu.

Miongoni mwa matatizo makuu ambayo nahisi yameanza kujitokeza kutokana na sera za HESLB ni mfumuko wa kugushi vyeti vya kidato cha sita. Baada ya kutangazwa utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaopata daraja la kwanza na la pili tu, inaelekea hata wizi wa mitihani umepitwa na wakati. Badala yake, upo uwezekano kuwa tayari kuna wimbi baya zaidi la kugushi na kununua vyeti vya daraja la kwanza vya kidato cha sita, kama sehemu ya kutafuta mikopo ya HESLB.

Inawezekana tukawa na idadi kubwa ya wanafunzi walio mwaka wa kwanza katika vyuo vikuu ambao wamechaguliwa kwa kutumia vyeti vya aina hii. Sasa hivi wapo wanafunzi wengi sana ambao baada ya kupata daraja la nne katika kidato cha nne, wamebadilika ghafla na kupata daraja la kwanza katika mitihani ya kidato cha sita!

Uzoefu wangu unanilazimisha nifikiri kuwa jambo hili haliwezekani bila kugushi vyeti kwa mbinu kali, na wala si wizi wa mitihani.

Kwa hiyo, basi, bila kuwa na mfumo bora wa elimu na kuwekeza katika elimu, tutaendelea kutoa mikopo kwa watu ambao hata kidato cha nne hawajafika, mradi tu wamekaa mjini na kujua wapi vinatengenezwa vyeti vinavyoonekana kuwa halisi, nje ya taratibu za Baraza la Mitihani la Taifa.

Wilfred Kahumuza ni mdau wa sekta ya elimu nchini wa muda mrefu.

Wednesday, April 8, 2009

Kwa staili hii, vita dhidi ya rushwa na ufisadi imetushinda…!

KATIKA kipindi hiki ambacho jamii imelemewa na ugumu wa maisha kisiasa, kiuchumi na kijamii, na kwa maumivu na huzuni ikipiga kite,wasomi wameamua kutokuwa upande wowote, na wengine wameamua kuungana na wanaosababisha hali hii.

Kwa kifupi na kwa ujumla, msomi wetu ambaye kwa elimu yake na nafasi yake katika jamii, anapaswa kuwa mlinzi na kisima cha busara, hekima, uhuru na haki; ni mvivu, mwoga, muasi, asiye radhi kupambana dhidi ya maovu katika jamii yake.

Matokeo yake ni nchi kugubikwa na majanga ya rushwa, ufisadi, demokrasia duni, na uporaji wa rasilimali za Taifa unaofanywa na wageni kwa kushirikiana na baadhi ya wzawa kwa nchi isiyo na mlinzi.

Tafsiri ya neno “momi”, ni mtu mwenye uelewa mzuri juu ya mambo; mtu mwenye akili, uwezo wa kufikiri na mmaizi wa mambo. Mmaizi huyu, kwa nafasi yake katika jamii, anatarajiwa kujihusisha na kuhusika na yote katika mazingira yake, ikiwa ni pamoja na jinsi anavyoshiriki na kujishirikisha na wanaomtawala.

Msomi hapaswi kuambiwa tu jinsi mambo yalivyo na yanavyotakia kuwa, bali anapaswa kujihusisha katika kuleta mabadiliko yanayotakiwa na mchakato mzima wenye kuleta mabadiliko hayo. Huo ni wajibu wake usiokwepeka, kwa sababu jamii na nchi kwa ujumla ilikwishajitolea kwa kutoa sadaka ya kile kidogo ilicho nacho, aweze kupata elimu, ili hatimaye aitumikie kwa wema na kwa maendeleo ya wote. Asipofanya hivyo ni mwasi kwa jamii na Taifa lake.

Moto wa majanga yote tuliyoyataja hapo mwanzo unaoendelea kulitafuna Taifa si tu unaongezeka na wasomi wetu wakiangalia, bali wakati mwingine wao ni washiriki katika kuchochea kuni kwa sababu wanazozijua.

Ni kwa sababu hii ipo siku ambay umma wa Kitanzania utachoshwa na uasi huu na kuamua kumsukuma msomi kizimbani kujibu mlolongo wa tuhuma, zikiwamo, kushindwa kutenda na kuwajibika katika kuiokoa jamii nyakati za hatari na migogoro, kuhatarisha ustawi wa Taifa na raia wake; kula njama na ubepari wa kimataifa na mashirika ya nje ya kuhodhi (transnationals), kudumaza, kuua sera sahihi za uchumi za nchi; kuasi mstakabali wa kitaifa (national cause) kwa kujishirikisha na rushwa na ufisadi; na shitaka la mwisho, kuiuza nchi kwa “mbwa mwitu”.

Pale kizimbani, msomi huyu inawezekana akauliza: Kwa nini niandamwe mimi pekee, wakati kuna washiriki (accomplices) wengi tu katika jinai hii? Chochote na kiulizwe; lakini ushahidi wote utamlemea msomi kwa sababu ya jukumu na wajibu wake katika jamii, kama tulivyoeleza hapo mwanzo. Nani asiyejua, asiyeona jinsi wasomi wetu walivyoshindwa kutoa mchango katika kuboresha mchakato wa demokrasia ya kweli katika nyanja za siasa na uchumi; kwamba utawala wa sheria unabezwa, Katiba inakanyagwa kwa kisigino, huku uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja (isipokuwa kwa wateule) ukiporomoka kwa kasi ya kutisha?

Je, msomi huyu anaelewa nini, na ametendaje juu ya changamoto mpya kufuatia mfumo huria wa siasa na uchumi wa soko na madhara yake kwa jamii? Chukua mfano wa rushwa: ugonjwa huu si tu kwamba unaangamiza maadili ya kijamii, bali pia unadumaza na kudhoofisha taasisi zote za kidemokrasia nchini. Je, ni kweli hajui, au anajifanya kutojua, kwamba sababu kuu ya rushwa katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kisiasa ni matokeo ya kutozingatiwa kwa misingi ya utawala bora, uwanja ambao yeye ni mshiriki na mchezaji?. Atueleze, ameipeleka wapi, au ameifanyia nini Taarifa ya Tume ya Jaji Joseph Warioba juu ya Mianya ya Rushwa nchini?

Uchumi wetu umeshindwa kuchanganya, huku msomi akipiga kelele juu ya paa kwamba “ndege ya uchumi wa nchi inapaa”, wakati ukweli ni kuwa ndege hiyo iko chini, gurudumu zake zimetoboka. Ni nani aliye nyuma ya kashfa za EPA, IPTL, Deep Green, Richmond / Dowans, Mfuko wa “Import Support, Mikataba ya uwekezaji ya kiporaji, kama si msomi mwenyewe?

Nani anayeunda Bunge butu la nchi, lisiloweza kumtetea na kumsemea mwananchi wa chini, lililogubikwa na minyukano ya kugombea maslahi badala ya kupigania maendeleo kwa wote, kama si msomi huyu? Nani anayewauza wananchi kwa “mbwa mwitu”, kwa mashirika mumiani kama Benki ya Dunia (WB), Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), na kwa nchi tajiri zenye kupora na kukomba rasilimali zetu, kama si msomi huyu?

Heri waasisi wa uhuru wetu, wengi hawakuwa wasomi sana kama watawala wa leo, lakini walijali maslahi ya walio wengi, walijitoa mhanga, bila hivyo tusingepata Uhuru. Je, tuelewe kwamba usomi siku hizi maana yake ni umamluki wa mitaji na ubeberu wa kimataifa?.

Je, ushahidi wote huu, hautoshi kumpeleka lupango kwa tuhuma zinazomkabili? Umma utamke hukumu na adhabu yake. Lakini subiri kidogo. Ni msingi wa kisheria, kwamba mtu hawezi kuhukumiwa bila kusikilizwa. Tumpe nafasi hiyo, ambayo ni haki yake ya kikatiba pia.

Atafungua utetezi wake kwa kukana na kukanusha kwa nguvu zote tuhuma dhidi yake akisema tatizo si yeye , bali tatizo ni sera za uchumi, wanasiasa na mfumo wa siasa unaopaswa kulaumiwa.

Atacharuka na kuhoji: “Ni nani anayeamua juu ya mahitaji ya jamii? Ni msomi, watu au wanasiasa”. Atasema, kama angeruhusiwa kupitia maktaba yake vizuri, angeweza kuandika vitabu vingi kuonyesha kwamba, ni wanasiasa (iwe hao ni wasomi au la), ndio wanaoamua juu ya mahitaji ya kiuchumi na kisiasa ya jamii na yeye kuwekwa pembeni.

Atasema, Sera kama zile za elimu ya kujitegemea, maendeleo vijijini, mashirika ya umma na vyama vya ushirika, vijiji vya ujamaa, madaraka mikoani, sera za nje, mfumo wa chama kimoja na nyingine zote zilizoifikisha nchi hapa, hazikutungwa na kusimamiwa na wasomi kama yeye, bali wanasiasa, chini ya chama na Bunge lililodhibitiwa.

Atakumbusha juu ya maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya mwaka 1966, dhidi ya maamuzi ya wanasiasa ya kujiongezea marupurupu kwa gharama ya wanyonge, kwamba ulikuwa mfano hai jinsi wasomi wasivyoiva chungu kimoja na wanasiasa, lakini wakanyukwa nyundo na kufukuzwa chuoni kama njia ya kuwanyamazisha.

Ataeleza chimbuko la mifaraikano, kati ya wasomi na wanasiasa, kwamba linaanzia enzi baada ya Uhuru. Kwamba, mwanzoni wasomi na wanasiasa walishirikiana vizuri katika harakati za kutafuta uhuru na demokrasia ya kitaifa. Baadaye, wakati wasomi wakiendelea kuimarisha dhana ya demokrasia ya kitaifa (nationalist democracy) kwa njia ya mijadala, midahalo na machapisho miaka ya 1960, wanasiasa kwa upande wao, walijikita katika kuhamasisha umma kufikia lengo hili. Hii ilikuwa ndoa ya maridhiano, kati ya wasomi na wanasiasa, walipoweza kuunda timu moja.

Lakini miaka ya 1970 mambo yalibadilika, wakati ukinzani ulipoanza. Wakati wasomi waliendelea kuimarisha na kukomaza demokrasia na matunda ya uhuru, wanasiasa walichoropoka kutaka kuibadili dhamira ya kitaifa (nationalistic consciousness) kuwa itikadi ya kimaendeleo (ideology of developmentalism), na ndiyo iliyokuja kuwa itikadi ya tabaka la watawala waliyoitumia kuendeleza ubinafsi.

Itikadi hii ilisisitiza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa gharama ya demokrasia, kiasi kwamba aliyelilia demokrasia hakuwa “mwenzetu”, wengi wao wakiwa wasomi. Itikadi hii ilibeza kiungo kati ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa kudai kwamba, ukuu wa siasa, na si ukuu wa demokrasia, ulikuwa mhimili wa maendeleo ya kiuchumi.

Pengine hii ilikuwa ni kuitika wito wa Kwame Nkrumah bila kuuelewa vizuri kwamba, “utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa, na mengine yote mtazidishiwa”. Kweli nchi iliutafuta ufalme huo badala ya ufalme wa kiuchumi na demokrasia, lakini hadi leo, si ufalme wa kisiasa wala wa kiuchumi tuliopata, kwani tunaendelea kuwa tegemezi kwa vyote kutoka nje.

Kuvunjika kwa ndoa kati ya wasomi na wanasiasa kulizaa uhasama wa kuitana majina mabaya mabaya – “mpinga maendeleo” “mpinga mapinduzi” na majina mengine kwa sababu tu mtu ameamua kutofautiana kimawazo na baadhi ya wanasiasa. Kuanzia hapo, msomi alipata baridi kwa kunyimwa nafasi ya kushiriki katika kuleta mabadiliko ya kijamii; ubunifu ukafifia, akaamua kuziba mdomo kwa hofu ya kuishia kizuizini.

Ni miaka ya 1980 tu wakati mfumo wa chama kimoja ulipobainika kushindwa na migogoro ya kiuchumi kukithiri, ndipo umuhimu wa demokrasia katika maendeleo ulipoanza kujidhihirisha.

Mabadiliko haya, ya demokrasia inavyoonekana sasa ni msingi muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, amani na utulivu na si kinyume chake. Lakini atasema, katika mazingira haya mapya, ya siasa kununua utajiri, na utajiri kununua siasa, msomi asiye na fedha au asiye fisadi, ana nafasi gani ya kusikilizwa? Je, wanasiasa watamwelewa na kumkubali?

Kama Bunge limesheheni wafanyabiashara, kiasi kwamba maslahi binafsi ndiyo yenye kutawala mijadila Bungeni na sheria zinazotungwa, msomi afanye nini katika mazingira kama hayo?, atauliza.

Atasema, msomi anashindwa kuitumikia jamii yake ipasavyo kwa sababu anabezwa, hapewi nafasi kushughulisha elimu yake kikamilifu. Na kwa sababu hiyo ndiyo maana wasomi wengi wanakimbilia siasa na kutelekeza taaluma zao, kwa sababu wanasiasa wamejitengenezea “pepo” na kuwatupa wasomi jehanamu.

Atamaliza kwa kumnukuu Profesa Alvin Toffler, katika kitabu chake “Powershift”, kwamba “kama elimu ndiyo chanzo cha madaraka ya kidemokrasia, basi hakika mchakato wa kisomi, lazima utilie mkazo uhuru wa mawazo, kutofautiana na kupiga vita aina zote za udikteta, kauli-tabia (dogma), utii na unyenyekevu potofu”.

Mwisho atahoji, “msomi atatekelezaje wajibu wake katika jamii kwa kuitwa “mpinzani”, “mpinga maendeleo”, “si mwenzetu”, “kipofu” au “mvivu wa kufikiri”?. Msomaji, kwa maoni yako, je unafikiri ana kesi ya kujibu? Kwa lipi?

Monday, April 6, 2009

Nchi inavyotafunwa

Tanzania inaendelea kupoteza mamilioni ya fedha kutokana na serikali kusuasua kupeleka bungeni muswada wa sheria itakayoongoza sekta hiyo nchini.

Inaelezwa kuwa kutokuwepo kwa sheria ya madini nchini kumesababisha sekta hiyo kuendeshwa kiholela na kutokuwepo kwa udhibiti wa kutosha, hali ambayo inawanufaisha zaidi wawekezaji wa nje wanaotumia mwanya huo kuhamishia nchi za nje fedha zinazotokana na biashara hiyo.

Madini moja ya sekta inayoelezwa kuzalisha mabilioni ya fedha kila mwaka, imekuwa ikichangia kwa kiasi kidogo tu katika pato la taifa, hali ambayo imekuwa ikiwashangaza watu wengi wakiwemo wachumi kiasi cha kuzusha malalamiko kutoka kwa wananchi.

Wataalam mbalimbali, wachumi na wabunge mara kwa mara wamekuwa wakipiga kilele kuitaka serikali ifumbue macho na kutazama jinsi taifa linavyoibiwa mamiloni ya fedha katika sekta hiyo, lakini kasi imekuwa ndogo katika utekelezaji.

Pamoja na kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na madini mengi na ya kila aina, vikiwemo vito vya thamani ambavyo baadhi yake havipatikani mahali popote duniani, bado haijaweza kunufaika na sekta hiyo kutokana na kuwepo kwa utaratibu mbovu katika kuisimamia.

Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete, baada ya kuingia madarakani, aliliona tatizo hili na kuchukua hatua ya kuunda tume ya kufuatalia sekta ya madini na kisha tume hiyo itoe mapendekezo yake ili taifa liweze kunufaika na sekta hiyo kuliko ilivyosasa.

Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mark Bomani, kwa bahati nzuri ilishakamilisha kazi na kukabidhi ripoti yake kwa Rais Kikwete.

Baadhi ya mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo ni kutaka itungwe sheria mpya ya madini na kufanyiwa marekebisho sera inayoongoza sekta hiyo.

Inaelezwa kuwa endapo serikali itakubaliana na mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti ya Tume ya Jaji Mark Bomani, taifa litaanza kunufaika kwa kiasi kikubwa na madini yake kuliko ilivyo sasa ambapo pamoja na kukua kwa sekta hiyo hadi kufikia kuchangia asilimia 40 ya mapato yatikanayo na mauzo nje ya nchi, lakini inachangia asilimia 3 tu ya Pato la Taifa.

Katika kikao cha Bunge cha Novemba mwaka jana, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alisema kulingana na ripoti ya Jaji Mark Bomani, sekta ya madini inakabiliwa na changamoto, ikiwemo mchango wake mdogo katika pato la taifa, madini kuendelea kuuzwa yakiwa ghafi na uchimbaji duni wa wachimbaji wadogo na kupendekeza kufanyiwa marekebisho kwa sheria na sera hizo.

Alisema kutokana na kutolewa kwa taarifa hiyo, tayari kikosi kazi kimeundwa ili kuangalia namna bora ya kutekeleza mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo ya Tume ya Rais.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wanalalamikia kasi ndogo ya serikali kupeleka muswada wa sheria hiyo bungeni ili uweze kujadiliwa na kisha kupitishwa ili uweze kutumika kuongoza sekta hiyo muhimu.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa Tume ya Jaji Bomani, jana aliliambia gazeti hili, kuwa wakati tume hiyo ilipokuwa ikifanya kazi zake, ilibaini mapungufu mengi kwenye sekta ya madini, mapungufu ambayo yamesababisha serikali kukosa mabilioni ya fedha.

Alifichua kuwa makampuni ya madini yamekuwa yakiinyonya Tanzania kwa kutumia njia mbali mbali, ya kwanza ikiwa ni kulipa mrahaba mdogo kuliko hali halisi na pili ni kupitia msamaha wa kodi ya mafuta ambao makampuni hayo yamepewa na serikali.

Alifafanua kuwa kwa utaratibu wa sasa makampuni ya madini yanalipa mrahaba kwa kiwango cha asilimia 3 tu tena baada ya kuondoa gharama zote za uzalishaji na nyinginezo.

Alisema utaratibu huo umekuwa ukiisababishia serikali kupata mapato kiduchu ikilinganishwa na faida kubwa ambayo makampuni ya uchimbaji madini yamekuwa yakipata.

Zitto alisema kutokana na kutumika utaratibu huo wa kinyonyaji, katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 1998 hadi 2008, serikali ilipoteza zaidi ya sh. 883, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko hata misaada inayotolewa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa Tanzania.

Kuhusu jinsi msamaha wa kodi ya mafuta kwa makampuni ya uchimbaji wa madini unavyolikosesha taifa mapato mengi, Zitto, alisema kwa kipindi cha mwaka 2005/2006, zaidi ya sh. 32 bilioni zilipotea kutokana na msamaha huo, huku makampuni hayo katika kipindi hicho yakilipa sh 23 bilioni tu kama mrahaba.

Aliongeza kusema kuwa katika kipindi cha mwaka 2006/2007 serikali ilikosa zaidi ya sh. bilioni 59 kutokana na msamaha huo, huku makampuni hayo yakilipa sh. bilioni 25 tu kama mrahaba katika kipindi hicho.

Mbunge huyo, alisema kwa kipindi cha mwaka 2007/2008 serikali ilikosa tena zaidi ya sh bilioni 91, huku makampuni hayo yakilipa sh bilioni 28 tu kama mrahaba.

``Ukiangalia takwimu hizi utaona kwamba makampuni hayo yamesamehewa kiasi kikubwa cha kodi huku yenyewe yakiilipa serikali kiasi kidogo tu cha fedha kama mrahaba, hivyo utaona serikali inapoteza mabilioni ya fedha kutokana na msamaha, huku makampuni yakitengeneza faida kubwa`` alifafanua.

Alieleza kuwa serikali kuyaachia makampuni ya uchimbaji wa madini kutumia umeme wao, pia kunalikosesha Shirika la Umeme nchini (Tanesco) mabilioni ya fedha kutokana na kushindwa kuyauzia umeme makampuni hayo.

Zitto, alieleza kuwa Tume ya Jaji Mark Bomani baada ya kubaini mapungufu mengi katika sekta ya madini, katika ripoti yake iliyoitoa baada ya kukamilisha kazi yake, ilitoa mapendekezi kadhaa ya kufanyiwa kazi na serikali haraka.

Aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni kubadilisha kiwango cha mrahaba kutoka asilimia 3 hadi 5 na kiwango hicho kitozwe kabla ya makampuni kuondoa gharama za uzalishaji na kufutwa kwa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa wawekezaji.

Pendekezo jingine ni kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Madini ambao utasaidia maendeleo ya sekta hiyo na jingine ni kutaka kiasi cha fedha za mrahaba ziende moja kwa moja kusaidia maendeleo ya vijiji vyenye migodi.

Jingine ni kutungwa kwa sheria mpya ya madini na kuifanyia marekebisho sera ya madini nchini na pia uwekwe mkakati wa kuhakikisha sekta ya umeme nchini inasaidia maendeleo ya sekta ya madini.

Hata hivyo, mbunge huyo, alionyesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya madini, akisema kuwa hali hiyo inaligharimu taifa kuendelea kupoteza fedha nyingi bila ya sababu za msingi.

``Muswada wa sheria hii kwanza ulikuwa uletwe na serikali bungeni Februari mwaka huu lakini haukuja, sasa tumeambiwa utaletwa kikao kijacho cha bunge, hata hivyo tunatarajia kikao kijacho cha bajeti serikali itatangaza mabadiliko makubwa kwenye sekta ya madini`` alisema.

Alitoa wito kwa wananchi na wadau mbalimbali kuishinikiza serikali iharakishe kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Jaji Bomani ili taifa lisiendelee kupoteza fedha zaidi.

Sheria ya madini iliyopo sasa ambayo ilipitishwa na bunge mwaka 1997 inaelezwa imechangia kwa kiasi kikubwa kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya dola za Marekani milioni 883kutokana na mapungufu yake.

Katika kipindi hicho, bunge lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali za Fedha, ambayo ndiyo iliyoweka msingi wa sheria za kodi za madini, ambazo hazikujali maslahi ya taifa na badala yake kuwanufaisha zaidi wawekezaji.

Kwenye sheria hii kuna kipengele cha asilima 15 kinachosema baada ya kampuni ya uchimbaji madini kutoa gharama zake za uzalishaji, inaruhusiwa kuongeza asilimia nyingine 15 ya gharama hizo na kutokana na sheria hiyo toka mwaka 1997 hadi 2007 kikiwa ni kipindi cha miaka 10 imeiingizia hasara serikali ya dola za Marekani milioni 883 sawa na sh trilioni 1 za Tanzania kwa kiwango cha sasa cha kubadilisha fedha, endapo fedha hizo zingekusanya zingesaidia mambo mbalimbali ya maendeleo.

Hatua hiyo ilimfanya, Basil Mramba, wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, apeleke bungeni muswada wa sheria wa kuifuta na baadaye kuridhiwa na bunge, lakini mwaka mmoja baadaye 2002, Mramba huyo huyo alipeleka tena muswada wa sheria wa kutaka sheria hiyo irudishwe na wabunge waliokuwa bungeni kipindi hicho wakaipitisha.

Kupitishwa kwa sheria kuliyafanya makampuni ya uchimbaji madini kuchelewa kulipa kodi kutokana na kupewa muda mrefu wa kufanya hivyo.

Kwa mfano kampuni ya uchimbaji madini ya Bulyanhulu iliyoanza uchimbaji mwaka 1999, itaanza kulipa kodi mwaka 2019, hii ina maana kuwa itaanza kulipa kodi mwaka wa mwisho wa urais wa awamu ya tano, kampuni nyingine ni ya Anglo-Gold iliyoanza kuchimba mwaka 2002 lakini itaanza kulipa kodi mwaka 2012 na kampuni ya madini ya Resolute ya Nzega inaweza isilipe kabisa kodi kwani madini ya dhahabu iliyokuwa ikichimba katika eneo hilo yamemalizika kabla ya kipindi chake cha kuanza kulipa kodi hakijafika.

* SOURCE: Nipashe

Mila potofu yakwaza maendeleo ya wanawake

Ukosefu wa elimu, mila potofu pamoja na mfumo dume vinachangia baadhi ya wanawake kushindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na baadhi ya jamii kuamini hawawezi kuongoza mambo mbalimbali.

Hayo yalisemwa juzi jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Mtandao wa Wanawake Barani Afrika (WiLDAF), Judith Odunga, wakati wa mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari kuhusu Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia.

Alisema ingawa sera hiyo imelenga kumkomboa mwanamke katika nyanja za siasa na uchumi lakini haijaweza kumsaidia kutokana na jamii hususan wanawake wenyewe kuwa na dhana potofu kwamba mwanamke mwenzao hawezi kuwaongoza.

“Nawasihi wanawake wenzangu wawachague wanawake wanaojitokeza kugombea uongozi katika ngazi mbalimbali, msiwakebehi pia ondoeni mfumo dume kwa kuwasomesha watoto wenu ili waweze kuwasaidia,” alisema.

Naye mwezeshaji kutoka Kituo cha Mafunzo na Maendeleo (TWIFUNDE), Yasin Ally, aliiasa jamii kuondoka na mila potofu zinazomkandamiza mwanamke na kuwasihi wanawake kujishughulisha na biashara mbalimbali zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Imeandikwa na Veronica Mheta; Tarehe: 5th April 2009
HabariLeo

Friday, April 3, 2009

Mrejesho wa GDSS: Je, Bajeti Mpya Itawanufaisha Wanawake? Uchambuzi wa Muongozo wa Bajeti 2009-12 Kwa Mtizamo wa Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi.

Mfululizo wa semina za GDSS, jumatano ya tarehe 1/04/2009, mada ilikuwa ni Uchambuzi wa Muungozo wa bajeti kwa mwaka wa fedha 09/12 uliotolewa na serikali kwa mtizamo wa Ukombozi wa wanawake kimapinduzi. Mada hii iliwakilishwa na Glory Shechambo na Marjorie Mbilinyi (TGNP)

Mada ililenga kuchambua mambo makuu mawili; kwanza, Mgawanyo wa fedha kulingana na vipaumbele vya Serikali na Mtarajio ya wananchi walio wengi; pili, Nafasi ya wananchi katika utayarishaji wa bajeti.
Katika uchambuzi mambo makuu yaliyoangaliwa ni pamoja na; Kukua na Kuyumba kwa Uchumi wa nchi, Maendeleo ya sekta kulingana na Malengo Matatu ya MKUKUTA- Kupunguza umasikini wa kipato, Ustawi wa jamii, na Utawala bora, nk. Mambo yaliyojitokeza katika uchambuzi;-
• Uchumi wa Nchi unaonekana umekuwa kwa 7% kwa mwaka 2001-07
• Mfumuko wa Bei umekua kwa 3%-10% kwa mwaka 2007-08
• Matumizi ya serikali yamezidi kutoka tilioni 7.2 (08/09) hadi tlioni 8.1 (09/10)
• Kushuka kwa thamani ya shilingi kwa 13.2%

Vipaumbele vya serikali kwa mwaka huu wa fedha ni; Miundombinu-barabara na mawasiliano-, ajira, Kilimo cha Umwagiliaji, Madini na Nishati. Na vipaumbele vya wanaharakati ni Maji, Afya, Elimu, Ukatili wa Kijinsia na HIV. Mgawanyo wa Fedha kulingana na malengo matatu ya MKUKUTA kwa mwaka wa fedha 09/10 ni kama ifuatavyo; Kupunguza Umasikini 51.2% pungufu kwa 2.9%,Ustawi wa Jamii 29.2% pungufu kwa 4.9%, na Utawala Bora 19.5%.

Muongozo huu wa bajeti umeacha maswali kadhaa bila kujibiwa; Mfano; Kwa nini bado kuna upungufu wa chakula nchini? Ni ajira gani zilizoongezeka? Na njia zilizotumika kuongeza ajira hizo? Katika elimu hakielezwi ni kiasi gani cha fedha kilichotengwa katika kuendeleza elimu? Kulipa madai ya walimu? Kununua vitabu? na kujenga nyumba za walimu? Katika afya, hakielezwi kiasi kilichotengwa kulipia wauguzi wa afya? Kuongeza watumishi? Kupunguza vifo vya akina mama na watoto?

Mambo kama Maji, Rushwa na Ufisadi, Kuuguza wagonjwa wa UKIMWI, Usalama wa Walemavu-albino-, asilimia ya wanawake katika ngazi za maamuzi na Uimarishaji wa ushirikishaji wa jamii katika Utayarishaji wa bajeti hayakuchambuliwa katika muungozo huu wa bajeti.

Changamato Zilizopo.
1. Swala la Uwazi katika maandalizi ya bajeti, raia wa kawaida wameshindwa kushiriki katika maandalizi ya bajeti. Pia Muungozo wa Bajeti umeandaliwa kwa Lugha ya Kiingereza na Kuchelewa kusambazwa, vitu ambavyo vimepelekea wananchi wengi wa kawaida kushindwa kushiriki katika uandalizi huo. Wananchi wanaweza kushiriki katika mchakato wa bajeti katika Nyanja mbili; kuandaa budget na kufuatilia matumizi ya bajeti.

2. Ongezeko la bei (Inflation) limetumika kama kigezo kikuu cha kuendelea kuomba misaada na kushuka kwa thamani ya shilingi. Utegemezi kwa nchi wahisani kwa mwaka wa huu 09/10 ni 34.5%, kitu amabacho kinatishia uhuru wetu wa maamuzi, misaada hii huambatana na masharti mengi.

3. Maswala kama mgawo wa umeme, mishahara ya wabunge, udhibiti wa maliasili, Ufisadi, mapato ya madini na swala la wachimbaji wadogo hayajagusiwa sana katika muungozo huu wa bajeti

4. Serikali imeendelea kushindwa kuandaa mazingira ya kuwawezesha wananchi wa kawaida kuwekeza na kuzalisha, badala yake imekuwa ikiendelea kuwanyanyasa kwa mfano kuwasumbua wafanyabiashara wadogo.

Nini Kifanyike?
Wanaharakatia waliweza kukubaliana Mambo Makuu Matatu;
1. Tunahitaji kuwa na Muungozo Mbadala wa Bajeti, ambao utakuwa wazi na kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika maandalizi ya bajeti, na kohoji na kusimamia matumizi ya fedha hizo.
2. Wananchi watumie fursa ya Uchaguzi iliyopo mwaka huu wa 2009 na 2010 kuchagua viongozi wa serikali wa mitaa, wabunge, na Rais kuchagua viongozi amabo wataweza kuwajibika kwa maslahi ya wengi.
3. Wanaharakati wafuatilie Maazimio wanayofikia mara kwa mara katika vikao na semina mbalimbali.

Ukiwa kama mwanaharakati unashiriki vipi katika kuandaa bajeti mbadala inayowajali wanawake?

Wizara ya ardhi inawafanya wanyonge kuwa maskini zaidi

MWAKA 2009 umewadia, na hivi karibuni tutaanza kusikia tambo za wanasiasa mbali mbali wakijinadi kwa wananchi ili waweze kupigiwa kura katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na hatimaye Uchaguzi Mkuu mwakani.

Moja ya silaha za wanasiasa katika kipindi hiki ni sera za vyama vyao ambazo wamezibuni ili kuwaletea wananchi maendeleo; na ndizo ambazo watakuwa wakizinadi ili kupata ridhaa ya wananchi katika maeneo husika kuongoza ili watekeleze sera walizozinadi na hatimaye wananchi wapate maendeleo. Kama wananchi watapata maendeleo au la, hilo hubaki kitendawili.

Ni katika kipindi hiki ambacho utasikia wanasiasa wa kambi moja wakiwaambia wenzao wa kambi nyingine kuwa hawana sera. Ni kauli hizi ndio zimenifanya nijiulize kuna tofauti gani kati ya wanasiasa wasiokuwa na sera na wale wenye sera lakini wakisha kuchaguliwa na kushika hatamu za uongozi hawatekelezi sera walizozinadi kwa wananchi?

Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ilitolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2004. Katika suala la Ardhi Sera hiyo inatamka bayana: “Serikali itatumia ardhi kama njia ya kuwawezesha wananchi wake kushiriki kikamilifu kiuchumi. Lengo ni kusaidia wananchi watumie ardhi waliyo nayo ama kwa kujipatia hisa katika shughuli za uwekezaji huo au pato lenye kuwanufaisha kushiriki kikamilifu katika shughuli nyingine za kiuchumi”.

Unasema mkakati wa utekelezaji wa tamko hilo ibara ya 4.9.3.(ii): “Kutoa ardhi kwa wawekezaji wakubwa kwa shughuli mbali mbali za kiuchumi. Pale ambapo itabidi Wananchi wahamishwe ili kuwapisha wawekezaji wakubwa. Serikali itawasidia utaalamu wa kuingia katika makubaliano muafaka na wawekezaji kwa nia ya kuwanufaisha”.

Sera hii ni kati ya mihimili iliyotumika kutunga Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, katika Ibara ya 48 ya Ilani ya CCM ya 2005 inatamkwa: “utekelezaji wa dhati wa Sera ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi itatuepusha na balaa la kuwa na jamii ambayo ina matajiri wachache walionacho na wananchi wengi wasio nacho”.

Katika miaka ya hivi karibuni limekuwapo ongezeko kubwa la migogoro ya ardhi kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wananchi. Wananchi wakipinga viwango vidogo vya fidia wanayolipwa ili kupisha miradi mbali mbali ya maendeleo inayopendekezwa na Wizara ya Ardhi.

Kibaya zaidi Wizara ya Ardhi inatumia kutokuelewa kwa wananchi kuhusu thamani halisi ya ardhi na nyumba zao kukiuka kwa makusudi Sheria za Ardhi namba 4 na 5 za mwaka 1999 zinazotamka bayana kuwa “fidia itakuwa ni kwa bei ya soko”; na pia zinaelekeza utaratibu wa kufikia bei ya soko “kuwa itakuwa ni kwa kulinganisha na mauzo ya hivi karibuni ya ardhi au nyumba katika eneo husika”.

Madhumuni ya Wizara ya Ardhi kukiuka Sheria za Ardhi ni kujipatia faida kubwa ya zaidi ya asilimia 1000 kwa kuuza ardhi ilizozipoka kutoka mikononi mwa wananchi wanyonge, ilihali wananchi wanaohamishwa wakipata malipo ya fidia hafifu wakishindwa kujirejeshea viwango vya makazi na maisha waliyokuwa nayo awali kabla ya kuhamishwa kwao. Wengi wao hushindwa kujijengea nyumba bora kama walizokuwa nazo, kujirejeshea huduma za umeme, maji, barabara, ajira n.k na hivyo kurudisha nyuma jitihada za kufikia malengo ya milenia.

Tuchukue mfano wa mradi wa mji wa mfano wa Luguruni ulioanza kutekelezwa na Wizara ya Ardhi Januari mwaka 2007. Tokea mwaka 2005 viwanja katika eneo la Kata ya Kibamba vilikuwa vikiuzwa kwa bei ya sh. milioni sita kwa kiwanja cha meta 20 x 20. Kiwanja cha meta 20 x 20 kina meta mraba 20 x 20= 400.

Ukikokotoa utagundua kuwa ardhi katika Kata ya Kibamba inauzwa kwa bei ya Shs 15,000/= kwa meta mraba tokea mwaka 2005. Cha kushangaza Wizara ya Ardhi, pasipo utu wala ubinadamu, Desemba 2007, iliwalipa fidia wakazi 259 wa eneo la Luguruni waliotakiwa kuhama kupisha mradi huo sh. 300 tu kwa meta ya mraba, sawa na sh. 120,000/= kwa kiwanja cha Mita 20 x 20. Iliwabidi wananchi walioathriwa na mradi huo kuikaba koo Wizara ya Ardhi ndipo ikapandisha kiwango hicho kufikia sh. 1977 tu kwa meta moja ya mraba sawa na fidia ya sh. 790,800 kwa kiwanja cha meta 20 x 20.

Iliwalazimu wananchi waliohamishwa kutoka katika eneo hilo wanunue viwanja kwa bei ya sh. milioni 6 hadi 8, ikimaanisha kuwa walilazimika kuchota fidia za nyumba ili kupata viwanja kwa kuwa fidia ya ardhi haikuweza kuwawezesha kununua viwanja mbadala.

Mara tu baada ya kukamilisha kuwahamisha wananchi kutoka eneo hilo, Wizara ya Ardhi ilitangaza tenda kuuza mapori hayo (pasipo uendelezaji wowote). Nyaraka za tenda zinagharimu sh. 300,000, na bei ya meta moja ya mraba ni sh. 30,000.

Mnunuzi yoyote anayetuma ombi chini ya kiwango hicho hukataliwa kwa kutofikia bei iliyopangwa. Kutokana na bei hiyo, Wizara ya Ardhi inauza kiwanja cha 20 x 20 chenye meta mraba 400 kwa sh. milioni 12, ilihali yenyewe ilimfidia mwananchi sh. 790,800 tu; na hivyo kujipatia faida ya asilimia 1500 (1500%).

Hii ni hali inayothibitisha kuwa maadili ya kitaifa yameporomoka kwa kiwango cha kutisha sana kama taasisi ya Serikali inabuni mpango wa kujipatia faida kubwa sana kiasi hicho kwa kuwanyonya wananchi kwa kukiuka sheria zilizopo kwa makusudi.

Katika lengo hili hilo la kujipatia faida kubwa zaidi Wizara ya Ardhi imewavamia wananchi wa eneo la Kwembe walioko jirani na kituo cha mji wa Luguruni na kupima viwanja vidogo vidogo ndani ya ua wa makazi yao.

Makaro ya maji machafu, matanki ya maji, nyumba za watumishi na mabanda vimemegwa na kuingizwa katika viwanja vipya vilivyotengenezwa kwa ajili ya kuuzwa pasipo kujali hawa binadamu wataishi vipi kuanzia sasa. Wakazi waliokuwa wakipakana na barabara ardhi zao zimemegwa kwa mbele kutengeneza viwanja vya kibiashara kwa ajili ya kuuzwa kwa faida kubwa. Haki za kibanadamu wala utu havijaliwi kabisa, kinachozingatiwa ni idadi ya viwanja vinavyoweza kuzalishwa ili Wizara ya Ardhi iweze kutengeneza fedha zaidi kutokana na mauzo ya viwanja hivyo.

Wakati haya yakitendwa na taasisi ya kiserikali, sera za uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia ardhi zilizonadiwa kwa wananchi mwaka 2005 ziko wapi? Je, wanaopaswa kutekeleza sera hizi wako wapi? Hawaoni yanayotendeka? Wengine ni viongozi waandamizi katika chama tawala. Ni nini kinawafanya wakae kimya kuhusu hali hii ya kinyonyaji? Wanaopaswa kusimamia utekelezaji wa sera hizi wako wapi? Ina maana hawasikii malalamiko ya wananchi katika maeneo yao na katika vyombo vya habari? Kama huu ndio mwendo wenyewe ni afadhali ya kukosa sera kuliko kuwa na sera za kuwadanganyia wananchi na kisha kushindwa kuzitekeleza.


Mwandishi wa makala hii Chrizant Kibogoyo ni mwanaharakatai wa masuala ya ardhi, aliwasaidia sana waathrika wa mradi wa Luguruni kudai haki yao, na sasa yuko bega kwa bega na wakazi wa Kwembe kuhakikisha kuwa unyonyaji unaoendeshwa na watumishi wa Wizara ya Ardhi unakomeshwa ili ardhi waliyo nayo wananchi itumiwe kuwaendeleza kiuchumi. Anapatikana kwa simu 0787-125599/0719-126575 au chrizant.k@gmail.com

Thursday, April 2, 2009

Masharti ya mikopo yananeemesha nchi tajiri na kuzikwaza nchi masikini

UCHUMI wa dunia unaendeshwa na nchi tajiri chini ya kivuli cha masharti yatolewayo na taasisi za ukopeshaji za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Taasisi hizi mbili hushirikiana kwa karibu na Jumuia ya Biashara Duniani (WTO) na Jumuia ya Makubaliano ya Jumla katika Ushuru wa Forodha na Biashara (GATT).

Kuna sababu kubwa mbili zitolewazo na taasisi za Bretton Woods kuhalalisha mikopo inayoambatana na masharti. Kwanza, ni kuhakikisha mkopaji anauwezo wa kulipa deni na riba. Pili, eti nchi inaomba mkopo au msaada kwa sababu sera zake zilishindwa kuzaa matunda. Kwa hiyo taasisi hulazimika kutoa sera mpya ili kulinda mkopo unaotolewa.

Waswahili husema; mwenye njaa hana miiko. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Tanzania ilitupilia mbali misingi iliyoijenga kwa muda mrefu na kukubali masharti ya taasisi za Bretton Woods, yaliyopewa kaulimbiu ya SAP (Structural Adjustment Program). Mosi, Serikali ilitakiwa kuondoa ukiritimba wa kulinda bidhaa za ndani kwa kuruhusu bidhaa kutoka nje bila masharti yoyote.

Pili, ilitakiwa kushusha thamani ya shilingi ili kukatisha tamaa manunuzi ya bidhaa kutoka nje (imports), na kuongeza bidhaa zilizouzwa nje (exports). Tatu, fedha za mikopo na misaada zisingetumika kuwapa ruzuku wakulima ili kupunguza makali ya uzalishaji. Na nne, serikali ilishauriwa kubana matumizi katika sekta zote.

Sera za SAP zilivizika kabisa viwanda vichanga vilivyokuwa vimeanzishwa Tanzania. Viwango vya uzalishaji Tanzania vilikuwa ni vya chini sana. Fedha za kigeni zilitumika kununua malighafi kutoka nje, mfano, mafuta, vitabu, madawa na mbolea. Shilingi iliposhushwa thamani na fedha za kigeni kupanda, gharama za uzalishaji zilipanda na kusababisha mfumuko wa bei kwa bidhaa zilizozalishwa na viwanda vya Tanzania.

Mikopo iliyotolewa mwanzoni mwa miaka ya 1990, iliambatana na masharti yaliyoitaka serikali kubinafsisha mashirika ya umma, kuvutia wawekezaji na kuweka mazingira ya kukuza sekta binafsi. Juni 2000 serikali ya Tanzania ilitia saini makubaliano ya sera na IMF. Hata hivyo, Tanzania iliendelea kuelemewa na msalaba wa madeni.

Risala iliyosomwa Februari 2006 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Salome Mbatia, wakati akifungua warsha ya Mpango wa Milenia, ilitoa mwanga.

Alisema; “deni la nje ni kikwazo kikubwa dhidi ya jitihada za maendeleo na kukua kwa uchumi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania. Hadi kufikia Novemba 2005, deni la nje kwa Tanzania lilikuwa dola bilioni 7.88 na serikali ilikuwa inalipa wastani wa dola milioni 150 kila mwaka”.

Akichangia hoja katika mkutano wa uchumi duniani uliofanyika Davos, Januari 2005, Rais Benjamin Mkapa alisema mapato ya serikali yalitumika kulipa madeni mapya na kuhudumia ya zamani. Aliomba madeni yafutwe ili mapato ya serikali yatumike katika huduma muhimu za jamii kama elimu na afya. Kilio kilisikika na Tanzania ilifutiwa madeni katika mkutano wa mataifa yenye maendeleo ya viwanda G8 uliofanyika Gleneagles, Julai 2005. Hata kabla ya kufutiwa madeni, bodi ya Benki ya Dunia ilikwisha kuanzisha mpango kabambe wa kuikopesha Tanzania (CAS).

Kuanzia Julai 2005 mpaka Machi 2009, Benki ya Dunia imekwisha kuikopesha Tanzania zaidi ya dola bilioni 2. Asilimia 85 ya mikopo hiyo imewekezwa katika miradi isiyopashwa kupewa kipaumbele na isiyozalisha fedha taslimu.

Mifano michache ni mkopo wa dola milioni 3.5 kwa ajili ya mradi wa Kihansi wa kutunza vyura (Kihansi Spray Toads). Na dola milioni 40 kwa ajili ya kutoa mafunzo, motisha, vivutio na zawadi kwa wizara, idara na asasi za serikali ili kuhimiza tija, utendaji na uwajibikaji.

Kutumia fedha za mikopo kutunza vyura, kutoa motisha, zawadi na miradi mingine isiyozalisha fedha taslimu ni kuwatumbukiza raia katika lindi la umasikini kinyume na Malengo ya Milenia.

June 2008 Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo, aliliambia Bunge kwamba Bajeti ya Serikali ya 2008/2009 ni shilingi bilioni 7216. Takriban asilimia 34 ya fedha hizo inatokana na mikopo au zawadi kutoka nje na asilimia 65 inatokana na mapato ya ndani. Alisema mpaka Desemba 2007, deni la taifa lilifika dola bilioni 7. Katika kipindi cha miaka miwili tu, 2005 mpaka 2007, deni la taifa lilirudi karibia lilipokuwa kabla ya kufutiwa madeni.

Kuna mifano mingi, lakini kwa sababu ya mgao wa umeme unaoendelea, mfano muafaka ni mradi wa kuzalisha umeme wa Songosongo. Mradi unaotoa taswira ya jinsi nchi tajiri zinavyonufaika na masharti yanayoambatana na mikopo kutoka katika taasisi za ukopeshaji.

Ghrama za miundombinu ya mradi wa Songosongo zimegawanywa katika sehemu nne. Mosi, kukarabati na kufufua visima vya gesi kisiwani Songosongo. Pili, kujenga karakana na kufunga mitambo ya uchakataji ili kuchuja, kusafisha na kuondoa maji na kemikali chafu ndani ya gesi.

Tatu, kujenga bomba la kilomita 232 kutoka kisiwani mpaka kituo cha Ubungo Dar es Salaam, na bomba la kilomita 16 kutoka Ubongo mpaka kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill. Na nne, Kuboresha mitambo minne ya zamani katika kituo cha Ubungo ili izalishe umeme kwa kutumia gesi badala ya mafuta, na kununua mitambo miwili mipya ya kuzalisha umeme.

Gharama za miundombinu zinakadiriwa kuwa takriban dola milioni 320. Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola milioni 183 kutoka Benki ya Dunia (WB), dola milioni 40 kutoka Benki ya Rasirimali ya Ulaya (EIB) na dola milioni 175 kutoka Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB).

Masharti ya mikopo yalikuwa mawili; mosi, kuishirikisha sekta binafsi kwa kuunda kampuni ya kusimamia mradi wa Songosongo. Pili, serikali kuhifadhi hiyo mikopo ili kuikopesha tena kampuni itakayoundwa kusimamia mradi. Iliundwa kampuni ya Songas na serikali iliikopesha tena hiyo mikopo kwa riba ya asilimia 7.1.

Julai 2004 kampuni ya Songas inayomiliki miundombinu yote, iliingia mkataba wa miaka 20 wa kuiuzia umeme TANESCO. Malipo ya TANESCO kwa Songas yamegawanywa katika sehemu mbili; kwanza ni manunuzi ya umeme unaozalishwa. Mitambo ya Songas inazalisha megawati 115 ambazo zinaweza kuigharimu TANESCO dola milioni 4 kwa mwezi.

Pili ni gharama za miundombinu (capacity charge) ambazo zimegawanywa katika sehemu tatu. Mosi, mtaji uliowekezwa na wabia wa Songas wa dola milioni 60 na riba ya asilimia 22. Pili, mkopo wa dola milioni 320 na riba ya asilimia 7.1, ambao ulitolewa na Tanzania kwa Songas. Tatu, gharama za kuhudumia miundombinu na kuzalisha umeme.

Ili kupunguza makali ya gharama za miundombinu, Oktoba 11, 2001 serikali ilikubaliana na Songas kwamba, kama TANESCO haitailipa Songas mkopo wa dola milioni 320 na riba ya asilimia 7.1, basi Songas itasamehewa deni hilo. Mpaka sasa TANESCO imeshindwa kulipa hilo deni, hivyo serikali imeliahilisha mpaka TANESCO itakapoweza kulilipa.

Pamoja na msamaha huo, gharama za miundombinu zilizosalia peke yake, bila ununuzi wa umeme, zinaigharimu TANESCO takriban dola milioni 6 kwa mwezi. Kuzimudu inabidi, ama; TANESCO ipate ruzuku kutoka serikalini au ipandishe bei ya umeme kwa wateja.

Mpenzi msomaji fikiria, serikali ilipewa mikopo kwa masharti ya kuikopesha tena kampuni binafsi ya Songas ili iweze kusimamia ujenzi na uendeshaji wa mradi. Lakini Songas iliingia mkataba na TANESCO (inayomilikiwa na kupata ruzuku kutoka serikali) unaosema, si Songas bali ni TANESCO inayopaswa kuilipa serikali huo mkopo na riba.

Kadri ya mkataba, TANESCO isipolipa, Songas inasamehewa deni. Songas inaweza kusamehewa deni na serikali kwa sababu TANESCO haiwezi kulilipa, lakini serikali inalazimika kulipa hilo deni katika mabenki ya WB, EIB na ADB.

Kwa nini mkopo wa mradi wa Songosongo haukutolewa moja kwa moja kwa kampuni ya Songas badala ya serikali? Au kwa nini serikali haikukopa kwa niaba ya TANESCO ili kuliwezesha shirika kuingia katika ubia na Songas bila kulazimika kulipia gharama za miundombinu?

Kwa nini Songas wasiuze umeme moja kwa moja kwa wateja badala ya kuiuzia TANESCO? Mbona kampuni ya Orca inauza gesi katika viwanda vya Kioo, TBL, Urafiki, na Aluminium Afrika bila kulipia gharama za miundombinu?

Wabia wa Songas ni Globeleq (mtaji wa dola milioni 33.8 na hisa asilimia 56). Globeleq iliundwa mwaka 2002 na kitengo cha maendeleo ya kimataifa (DFID) cha serikali ya Uingereza. Ni shirika la umma linalomilikiwa na serikali ya Uingereza kwa asilimia 100.

Kampuni ya Maendeleo ya Uholanzi (FMO) - (mtaji wa dola milioni 14.6 na hisa asilimia 24). FMO iliundwa mwaka 1970 na serikali ya Uholanzi, ambayo inamiliki asilimia 51 ya hisa za kampuni hiyo. CDC (mtaji wa dola milioni 3.6 na hisa asilimia 6). CDC iliundwa mwaka 1948 na serikali ya Uingereza, ambayo inaimiliki kwa asilimia 100.

Wengine ni TDFL (mtaji wa dola milioni 4 na hisa asilimia 7). TDFL inamilikiwa na tawi la benki ya Uingereza la African Banking Corporation kwa asilimia 68 na serikali ya Tanzania kwa asilimia 32. Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) - (mtaji wa dola milioni 3 na hisa asilimia 5). Shirika la Umeme (TANESCO) - (mtaji wa dola milioni moja na hisa asilimia 2).

Kwa nini nchi tajiri zinashabikia mikopo kwa nchi masikini inayoambatana na masharti ya kuinua sekta binafsi, lakini katika mradi huu, Uingereza imeleta kampuni ya Globeleq inayomilikiwa na umma? Sekta binafsi ya Tanzania itakua vipi kama asilimia 76.6 ya hisa za Songas zinamilikiwa na serikali za nchi tajiri za Uingereza na Uholanzi?

Ni watanzania peke yao kupitia TANESCO na serikalini wanaogharamia mtaji wa wabia wa Songas wa dola milioni 60, mikopo ya dola milioni 320 iliyogharamia miundombinu, gharama za kuendesha mitambo, ambayo awali ilimilikiwa na TANESCO na gesi inayotumika kuendesha mitambo, ambayo ni mali ya Watanzania. Pia wananunua Umeme unaozalishwa.

Baada ya miaka 20 ya mkataba, Shirika la umma la Uingereza (Globeleq) litaondoka na faida, na shirika la umma la Tanzania (TANESCO) litarithi madeni yasiyolipika.