Thursday, February 24, 2011

Siri za anayejidai kumiliki Dowans



  • Ni Mzanzibari aliyetorokea Uarabuni

  • Ana mahekalu jirani na vigogo Zanzibar

  • Kuna utata kuhusu deni la Bil.100/- na rehani ya mitambo

WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likielezwa kuanza kuwasha mitambo ya Dowans, mmiliki wa kampuni hiyo aliyezua utata, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, ni Mzanzibari aliyeukana uraia wake baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Raia Mwema limeelezwa.

Habari kutoka Zanzibar alikozaliwa Al Adawi ambaye ni brigedia jenerali mstaafu wa jeshi la Oman, zinaeleza kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa askari polisi wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na alikimbia kama walivyofanya baadhi ya Wazanzibari katika kipindi hicho.

Mtu anayemfahamu kwa karibu Al Adawi, ameliambia Raia Mwema : “Brigedia kimsingi ni Mtanzania maana aliondoka nchini kama Wazanzibari wengi walivyoondoka na wakaukana uraia wao walipofika nje ya nchi ili kupata hifadhi ya kisiasa na kiuchumi.”

Akizungumza kutoka Zanzibar, mtoa habari huyo anasema kwamba baada ya kufika Oman alijiunga na jeshi la nchi hiyo na kubahatika kuwa mmoja wa walinzi wa karibu wa Sultani Qaboos bin Said al Said wa nchi hiyo, ambako alipata wasaa wa kujijenga kabla ya kustaafu na kuamua kuwa mfanyabiashara.

Miongoni mwa watu aliowahi kusoma nao kabla ya kuondoka nchini ni aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Salmin Amour ambaye ndiye anatajwa kumpokea tena Visiwani humo.

“Aliporudi nchini, Dk. Salmin alimsaidia kufanikisha kuuziwa nyumba ya Serikali eneo la Mazizini ambako wanaishi viongozi na watu mashuhuri kisiwani na nyumba yake inapakana na kiongozi mmoja wa juu wa sasa wa SMZ. Ana nyumba mbili pwani ya Mashariki na Pwani ya Magharibi ambazo anafikia anapokuja Tanzania,” anasema.

Taarifa zisizo rasmi zimeeleza kwamba, jana Jumanne, Al Adawi alitarajiwa kukagua mitambo ya Dowans eneo la Ubungo, ambako imeelezwa kuanza kuwashwa kwa majaribio wakati mazungumzo kati yake na Serikali na TANESCO yakiendelea kwa ajili ya kuzalisha umeme kuingiza kwenye gridi ya taifa.

Ilielezwa kwamba mtambo mmoja wa Dowans aina ya LM6000 PD 40MW uliopo viwanja vya TANESCO uliwashwa na kwamba ulikuwa ukizalisha megawati 37 kuchukua nafasi ya mitambo ya Songas iliyokuwa ikizalisha megawati 60 ambayo ilielezwa kupata hitilafu Jumapili.

Ofisa mmoja wa serikali aliliambia Raia Mwema jana kwamba kuna mchezo mchafu unaoendelea kuhusiana na Dowans na akahoji :“Imekuaje tatizo la umeme kuwa kubwa wakati Songas ikizalisha Megawati 60 za umeme na tatizo hilo likaja kupungua ilipowashwa mitambo ya Dowans inayozalisha umeme mdogo wa Megawati 37 tu ? Hii ni kuonyesha kwamba hawa jamaa wamepambana kufa na kupona Dowans iendelee kuvuna fedha zetu.”

Habari zinaeleza kwamba kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wanasiasa kutaka Dowans iwashe mitambo yake na kwamba hivi sasa kumekuwa na vikao vya mara kwa mara kuanzia mwishoni mwa wiki hii kutafuta njia za kutekeleza maelekezo hayo kutoka kwa wanasiasa.

Mitambo ya Dowans ambayo iliwashwa juzi Jumatatu ilizimwa jana asubuhi na ilitarajiwa kuwashwa jana jioni wakati vikao vikiendelea kuhusiana na jinsi ya kuitumia mitambo hiyo kuzalisha umeme na kuuingiza kwenye gridi ya Taifa.

Habari zimeelezwa kwamba mitambo hiyo itawashwa kwa kile kinachoitwa ‘best practice’ kwa shinikizo la Serikali na kwamba zitatumika njia za ‘kuwaziba mdomo’ watu wanaopinga mpango huo wakiwamo wanasiasa na waandishi wa habari.

Kuwashwa kwa mitambo hiyo kumekuja huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, akiendelea kupigia debe kuwashwa kwa mitambo hiyo.

Mitambo hiyo imewashwa siku moja baada ya Al Adawi anayedai kuwa ndiye mmiliki wa kampuni ya Dowans, kuwasili nchini na kuzungumzia sakata la fidia ambayo kampuni yake hiyo inaidai TANESCO kutokana na kukatisha mkataba wake kinyume cha sheria.

Al Adawi aliingia nchini na kukutana na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari, lakini kikao chake hicho kimeibua utata mwingi kutokana na kukataa kupigwa picha, lakini pia kutojibu maswali mengi ya msingi ambayo yanamhusu yeye binafsi na kampuni yake hiyo. Dowans sasa inaidai TANESCO Shilingi bilioni 94 zilizotolewa kama tozo kwa kile kilichoelezwa kukiuka mkataba.

Kwa mara ya kwanza Al Adawi alipozungumza na mwandishi wa habari mmoja nchini Marekani, alikana kuifahamu Dowans kabla ya kukiri baadaye alipozungumza na mwandishi huyo kwa mara ya pili, hali iliyozidi kutia shaka uadilifu wa mwekezaji huyo.

Al Adawi ambaye ni mmmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Services and Trade ya Usultani wa Oman alimtaka mwandishi huyo kutembelea tovuti ya makampuni yake ya (http://www.stcgroups.com) kuona kama kuna kampuni ya Dowans na kwamba wao hawafanyi biashara ya nishati.

Alipoelezwa kwamba mwandishi alikwisha kuitembelea, Al-Adawi alisema, “hatuna kampuni yenye jina hilo. Kama ungetembelea tovuti yetu ungeona kuwa sisi hatujishughulishi na mambo ya nishati; tuko kwenye mambo ya ujenzi”

Katika mahojiano hayo, yaliyofanyika mwaka 2009 na ambayo sauti yake iliwekwa katika mtandao, Al-Adawi, alimpa changamoto mwandishi kwamba kama kuna kampuni ambayo inatajwa kuwa ni yake, na ambayo hajawekeza fedha zake ndani yake, angefurahi sana kama angeweza kupewa kwa bure kampuni ya namna hiyo.

Baada ya Al-Adawi kuelezwa na mwandishi huyo kwamba jina lake limo katika fomu namba 201c za BRELA akitajwa kuwa ni mkurugenzi wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited akiwa ameweka sahihi yake Januari 26, 2007, alibadili msimamo na kukiri kuifahamu kampuni hiyo.

Anuani yake aliyoitumia katika fomu hiyo ni P.O.Box 823, PC 112, Sultanate of Oman, anuani ambayo inatumika pia na kampuni ya Services and Trade ya Oman ambayo aliianzisha na mshirika wake mwingine mwaka 1977 na hivyo kuondoa utata wowote wa kuhusika kwake kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Baada ya kuelezwa kuhusiana na nyaraka za BRELA, Al-Adawi alikiri kuwa kampuni hiyo ni yake na kwamba pekee ndiye mhusika wake na kwamba “aliombwa” kwenda kuleta majenereta nchini wakati ule wa dharura baada ya kampuni ya Richmond kushindwa kufanya hivyo.

“Nimewaletea majenereta mapya kabisa ; sasa kama hawataki mimi nitayaondoa” alisema Bw. Al-Awadi. Alipoulizwa kuhusu kampuni ya Dowans Holding (siyo Dowans Tanzania Limited) imeandikishwa wapi, Al-Adawi hakuwa tayari kujibu na badala yake alianza kutoa vitisho.

Kwa muda mrefu kumekuwa kukitajwa karibu kampuni nne za Dowans ambazo zote zinahusiana na Dowans Tanzania Limited.

Mwanzoni kuna kampuni iliyotajwa kuwa ni Dowans Holdings ya “Falme za Kiarabu” lakini imethibitika kwamba hakuna kampuni yenye jina hilo baada ya Taasisi ya Uwekezaji ya Dubai na Wizara ya Uchumi na Biashara ya Falme za Kiarabu ambayo inatoa leseni za biashara kutokuwa na rekodi za kampuni hiyo wala Idara ya Kanda Huru za Falme za Kiarabu.

Kampuni pekee ya Dowans ambayo inaonekana kuhusiana na Dowans Tanzania Limited ni ile ya Costa Rica ambayo imeonekana ni kampuni hewa huku wamiliki wake nao wakijificha.

Costa Rica ni mojawapo ya nchi ambazo sheria zake za uwekezaji na fedha zinakaribisha sana watu kufungua makampuni feki na zinalinda wawekezaji hao kutokujulikana na ni rahisi kufungua biashara yoyote huko hata kwa mtu mgeni.

Uhalali wa Dowans kisheria nao una utata baada ya usajili wake kuhusisha kampuni ya Portek International kupitia kampuni yake tanzu ya Portek Systems and Equipment Ltd kama mojawapo ya makampuni yenye hisa ya asilimia 39 kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Imethibitika kwamba kampuni hiyo ya Portek kwa mwaka 2007 na 2008 haikuwa na hisa yoyote kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited wala kuonesha kuwa wanaitambua kwa namna yoyote ile kampuni hiyo tata ambayo imekuwa gumzo kwa sasa.

Kwa upande wa Afrika kampuni hiyo ya Portek Systems and Equipment ilikuwa inafanya kazi nchini Algeria kupitia kampuni ya Bejaia Mediterranean Terminals S.p.a. Portek ina hisa za asilimia 15 kwenye kampuni moja tu ya kigeni, nayo iko Phillipines, lakini ni jambo la kushangaza kuona kwamba wameshindwa kuikumbuka kampuni “yao” ambayo wana hisa 39 ndani yake.

Katika mahojiano ya awali ya Al-Adawi inaonekana hakuwa anafahamu kuwa majenereta “yake” yalitumika kuchukulia mkopo wa karibu shilingi bilioni 100 kutoka kwenye mabenki kadhaa nchini. Kwa kadiri alivyokuwa anazungumza inaonekana yeye alikuwa anajua anachodaiwa ni Shilingi bilioni nane tu na habari kuwa kuna mikopo mingine ilichukuliwa huku majenereta yakiwekwa rehani zilikuwa ni habari ngeni kwake.

Alipoulizwa kama yuko tayari kuingia hasara endapo serikali itaamua kuyataifisha majenereta hayo, Al-Adawi alisema : “Unajua kwenye biashara kuna kupata na kukosa; sasa wakiyachukua niko tayari kuyakosa”.

Kati ya Aprili 30 na Novemba 9, 2007, ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuhaulishiwa mkataba kutoka Richmond, Dowans Tanzania Limited ilikopa fedha katika benki mbili tofauti, Barclays na Stanbic, zinazofikia bilioni 97.5/- na kuiweka dhamana mitambo hiyo ya kuzalishia umeme iliyoko Ubungo na mali zote za kampuni hiyo walizonazo sasa na zote ambazo zitapatikana baadaye.

Nyaraka zinaonyesha kuwa Dowans walikopa jumla ya dola za Marekani milioni 55 kutoka Barclays na dola nyingine milioni 20 za Marekani kutoka Stanbic tawi la Tanzania, fedha ambazo zinapaswa kulipwa kwa riba na gharama nyinginezo.

Dowans walipokopa dola za Marekani milioni 20 kutoka Stanbic tawi la Tanzania, dhamana iliyotajwa ni mitambo ya kuzalisha umeme, akaunti yao, mikataba, bima, na amana zote za kampuni hiyo tata.

Katika mawasiliano na kampuni hiyo benki ya Stanbic yenye makao yake makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni, Dar es Salaam, iliwakilishwa na Helen Makanza na Jeff Daly wakati Dowans haionyeshi ni nani aliyewakilisha kampuni hiyo zaidi ya Wakili Samson Russumo, ambaye alikuwa Kamishna wa Kiapo.

Baadaye Juni, 2007, Dowans ilichukua mkopo mwingine wa dola za Marekani milioni 20 kutoka benki ya Barclays ya Mauritius, makubaliano yaliyoelezwa kufuata sheria za Uingereza.

Miezi minne baadaye, Dowans imebainika walichukua tena kiasi cha dola za Marekani milioni tano kutoka Barclays tawi la Tanzania, dhamana ikiwa ni mali zile zile zilizotumika kuchukua mkopo kutoka Stanbic na Barclays ya Mauritius.

Kampuni hiyo inaonekana katika nyaraka nyingine kuweka rehani mali zake na kuchukua dola za Marekani milioni 30, Novemba 9, 2007.

Wakati serikali ikiendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo, haijafahamika kama mitambo hiyo imekwisha kuondoka mikononi mwa taasisi za fedha kutokana na kuchukua fedha hizo.

Wednesday, February 23, 2011

Wanaowatoza fedha watoto, wajawazito na wazee kukiona

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri wabunge au mtu yeyote mwenye majina ya wahusika katika hospitali za Serikali wanaowatoza fedha wazee, akina mama wajawazito na watoto wampelekee ili wahusika washughulikiwe.

Mwanri amesema bungeni mjini Dodoma kuwa, wenye majina ya watu hao wampe ili Serikali ibanane nao.

Mwanri alikuwa anajibu swali la nyongeza la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyedai kuwa watoto na wazee wanatozwa fedha wanapokwenda kupata tiba.

Kwa mujibu wa Mwanri ni sera ya serikali inaagiza kwamba, wazee, akina mama wajawazito na watoto wasitozwe fedha wanapokwenda kupata tiba.

Kwa mujibu wa Lissu, akina mama wanapowapeleka hospitali watoto wanadaiwa sh.5,000 na wazee pia wanatakiwa kutoa kiasi kama hicho ili wapate tiba.

Awali, wakati anajibu swali la msingi la Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema, Mwanri alisema, hospitali mpya ya wilaya ya Moshi iliyotokana na kupandishwa hadhi kwa kituo cha afya cha Mji Mdogo wa Himo inatarajiwa kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wan je Mei mwaka huu.

Mabaki ya mabomu makubwa 2,204 yaokotwa Dar


Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda akiwa na huzuni wakati Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick anamsomea taarifa kuhusu milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Gongo La Mboto. Makinda ametembelea kambi ya waathirika, Mzambarauni jijini humo. (Picha na Fadhili Akida).


JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limebaini mabomu matatu yaliyotua ndani ya choo cha shimo na kwenye tangi la maji, na kwamba hayajulikani kama tayari yamelipuka au la.

Pia Jeshi hilo limesema hadi sasa limekusanya mabaki ya mabomu makubwa 2,204, risasi 303, fyuzi za mabomu 668 na bunduki ndogo nyingi zikiwa zimeteketea na hazifai kwa matumizi.

Akitoa taarifa kwa ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na baadaye kwa Spika wa Bunge Anne Makinda, Mkuu wa Kikosi cha 511 cha Jeshi Gongo la Mboto, Kanali Aloyce Mwanjile, alisema hadi sasa wanashughulikia mabomu hayo na kuona namna ya kuyatoa.

“Tumejiwekea vipaumbele katika kukusanya haya mabomu na kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha yote yaliyoangukia kwenye makazi ya watu tunayaondoa, ila kuna changamoto tunakabiliana nazo ikiwamo hili la mabomu matatu yaliyomo ndani ya shimo la choo na kwenye simtank,” alisema Kanali Mwanjile.

Alisema pia kipaumbele kingine ni kuyafikia mabomu yaliyoruka umbali mrefu ambao wanakadiria kuwa kilometa 14 na kusafisha maghala yote ambayo yameharibiwa na mabomu hayo.

Aliyataja maeneo ambayo mabomu hayo yaliyolipuka Februari 16, yameharibiwa kuwa ni Gongo la Mboto, Pugu, Mbezi, Mnadani na Kinyamwezi.

Naye Makinda alisema Bunge limeshtushwa na taarifa hiyo ya milipuko ya mabomu na ndiyo maana liliahirisha kikao chake kimoja, ili kupisha wabunge waweze kutoa msaada wa karibu kwa ndugu na jamaa.

“Ndiyo maana nilipinga ule mwongozo wa mheshimiwa Mbunge wa kutaka Bunge lijadili suala hili, kwa kuwa msaada wetu si kujadili, bali kusaidia kwa hali na mali kwa vitendo na si maneno,” alisema Makinda.

Aidha, alitoa Sh milioni 37.8 kama msaada kutoka kwa wabunge, mawaziri na wafanyakazi wa chombo hicho cha kutunga sheria, ikiwa ni sehemu ya posho yao ya siku moja.

“Siku ya tukio tulikubaliana kila mmoja wetu achangie posho yake ya siku moja kuwasaidia wenzetu,” alifafanua Mbunge huyo wa Njombe Kusini.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alitoa hadhari kwa timu ya tathmini ya mali zilizoharibiwa na mabomu hayo, kuepukana na udanganyifu unaoweza kuigharimu Serikali fedha nyingi.

“Nina uzoefu na fidia ya mabomu ya Mbagala, tulilazimika kuchelewesha ulipaji fidia zile kutokana na udanganyifu uliofanywa na baadhi ya wananchi kwa kushirikiana na wataalamu wa tathmini,” alisema Lukuvi.

Alisema katika tathmini ya kwanza, ilionesha kuwa Serikali ilitakiwa iwalipe fidia wakazi wa Mbagala ya Sh bilioni 50 na fedha hiyo ilitoka, lakini kwa bahati nzuri kupitia waandishi wa habari, ilibainika kuwa kulikuwa na udanganyifu na katika tathmini ya pili, fedha halisi zilizotakiwa kulipwa zilikuwa ni Sh bilioni nane tu.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick, alisema hadi jana watu waliokufa kutokana na tukio hilo ni 24, na maiti wengine wawili wakiwa na utata unaotokana na wasiwasi kama kweli walitokana na mabomu hayo.

Pia alisema majeruhi katika Hospitali ya Muhimbili wamepungua hadi 34, Amana 17 huku Temeke wakiruhusiwa wote.

“Tatizo lililopo sasa ni watoto wanaotafuta wazazi wao kwani wanazidi kuongezeka, juzi walibaki wanane, lakini leo asubuhi (jana) walifikia 18,” alisema.

Hata hivyo, alibaini kuwa si wote waliopo kwenye kambi hizo za watoto wanatokana na kupoteana na wazazi wao kutokana na milipuko hiyo, bali pia wapo watoto wa mitaani wanaotumia nafasi hiyo kujipatia riziki na wengine wawili wamebainika kuwa wanatafuta kazi za ndani wakitokea Iringa na Dodoma.

Tuesday, February 22, 2011

Semina (GDSS) ya Wiki hii

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII TCIB(Kituo ChaTaarifa Kwa Wananchi Tanzania (Deus Kibamba) WATAWASILISHA

MADA: MATOKEO YA UTAFITI JUU YA - KWA NINI UCHAGUZI WA 2010 ULIKUWA NA IDADI NDOGO YA WAPIGA KURA KULIKO MWAKA WOWOTE TANGU UHURU?
Lini: Jumatano Tarehe 23 Februari, 2011
Muda: Saa 09:00 – 11:00 Alasiri

MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni
WOTE MNAKARIBISHWA

Monday, February 21, 2011

Muungano wa Wanaharakati wa Jinsia na haki za Binadamu FemAct watembelea wahanga wa Mabomu Gongolamboto

Bi Gloria Shechambo kutoka TGNP akichukua maelezo kutoka kwa muuguzi wa wodi ya wahanga wa mabomu katika hospitali ya manispaa ya Temeke

Wana-FemAct wakimpa pole majeruhi wa mabomu ya Gongolamboto


Mtoto aliyetambulika kwa jina moja tu la MWITA ambaye licha ya kuletwa hospitali akiwa hajitambui amepotezana na wazazi wake na bado amepoteza kumbukumbu kuhusu yeye mwenyewe na hata wazazi wake



Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari wakimhoji Mkurugenzi mtendaji wa TGNP Usu Mallya mara baada ya kuwatembelea wahanga wa mabomu.



Mahojiano




Wana-FemAct wakiifariji familia iliyompoteza mpendwa wao mmoja kufuatia kulipuka kwa mabomu





Ndugu wa marehemu wakitoa shukurani zao kwa wana-FemAct kwa kuwatembelea na kuwafariji






FemAct wakipelka msibani maji na juisi kwa familia iliyopoteza watu wanne (Mke na watoto wawili) kufuatia kulipuka kwa mabomu Gongo la mboto







FemAct



Waombolezaji pamoja na Mheshimiwa Meya wa Manispaa ya ILALA Mhe. Jerry Slaa


Mstahiki Meya Jerry Slaa akiwapa pole familia iliyopoteza watu watatu kufuatia milipuko ya mabomu Gongolamboto



Msiba wa watu watatu







FemAct wakipata maelezo kutoka kwa afisa wa serikali mara baada ya kutembelea eneo hili la shule ya msingi mzambarauni ambalo ndiko itakapokuwa kambi ya watoto iliyohamishwa kutoka uwanja wa sabasaba














Thursday, February 17, 2011

Albino walalamikia urasimu hospitalini

MWENYEKITI wa Chama cha Albino mkoa wa Mwanza, Alfred Kapole ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka utaratibu maalumu wa kutoa matibabu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ili kuondokana na usumbufu wanaoupata katika vituo vya afya.

Alisema kuwa kumekuwepo na usumbufu mkubwa ambao albino huupata wanapokwenda katika hospitali mbalimbali mkoani Mwanza kwa ajili ya kupata matibabu .

Miongoni mwa usumbufu ni pamoja na kuamriwa kutoa fedha za kufungulia faili na kulipia gharama za kumwona tabibu.

“Kwa kweli sisi walemavu wa ngozi,tunaiomba Serikali ituangalie katika hili, kwani nasi pia tuliwachagua, pia wakati wa kampeni za uchaguzi walisema kuwa endapo tutawachagua wakaingia madarakani sisi walemavu tutapatiwa matibabu bure.

Lakini ukweli ni kwamba tunapata usumbufu tunapofika katika hospitali kwa ajili ya kutibiwa,"alisema Kapole.

Alisema kuwa utaratibu ambao uliwekwa na Serikali awali kwa ajili ya Albino kupata matibabu, ulikuwa ni kupata barua kutoka kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na baadaye
barua hiyo kuidhinishwa na Mkuu wa Wilaya na mhusika kwenda moja kwa moja hadi hospitali husika kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alisema kuwa pamoja na kupata vibali hivyo, wanapofika hospitalini huwa wanapata usumbufu ambao huwakatisha tamaa ya kupatiwa matibabu.

Alisema, “mimi sioni kama kuna haja ya vibali kwa kuwa sisi ulemavu wetu unaonekana wazi, sasa huwa naona ajabu tunapofika hospitali tunaambiwa tuoneshe kibali ambacho kinatutambulisha kuwa ni walemavu jamani huu si ni urasimu kabisa."

Wanasheria wapinga mkataba mpya na Dowans

WANASHERIA nchini wameonya kuwa kutaifisha mitambo ya kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans, au kuingia nayo mkataba mpya kwa madai ya kulinusuru Taifa na mgawo wa umeme, ni kujitia kitanzi cha kuilipa kampuni hiyo mabilioni mengine ya fedha.

Wameeleza kuwa endapo mpango wa mkataba mpya utawasilishwa bungeni na kupitishwa ili utekelezwe na Serikali, utalisababishia Taifa hasara kubwa, kwa kuwa Dowans haitaupinga kwa kuwa inafanya biashara na kujali maslahi yake zaidi ya Watanzania.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, kwa masharti ya kutotajwa gazetini, wataalamu hao waliishauri Serikali iwe makini na mapendekezo au ushauri inayopewa na wabunge wake, ili kuepuka ‘mitego’ inayoweza kuingia kwa kivuli cha maslahi ya Taifa.

Mtaalamu wa kwanza alihoji uhalali wa Serikali kutumia Sheria ya Uhujumu Uchumi kwa kuuliza kama kampuni hiyo iliwahi kushitakiwa kwa kosa la jinai la kuhujumu uchumi wa Tanzania na kushindwa.

“Ninachofahamu ni kwamba Dowans hawajahujumu uchumi wala kushitakiwa kwa kosa hilo la
jinai, sasa sheria ya kuhujumu uchumi kwa suala lao itaingilia mlango gani?

Unataka kuniambia Serikali itatumia ubabe kuwataifishia mitambo? “Wakati huo sheria itakuwa wapi?

Hamwoni hapo ndipo tutakapoharibu na kudaiwa mabilioni mengi zaidi ya tunayodaiwa sasa na kampuni hiyo? Au ilikwishawahi kuisamehe Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) ili tuseme Serikali ilimalizana nayo?”

Alihoji mtaalamu huyo wa sheria. Mtaalamu mwingine wa masuala ya sheria pia akifafanua kuhusu suala hilo la uhujumu uchumi, alisema wabunge wanapaswa kukumbuka kuwa Dowans ndio walioshinda kesi ya madai iliyoamuliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kuitaka Tanesco iilipe.

“Sasa haya yatakuwa ni maajabu kwa Serikali kushauriwa kuitaifisha Dowans kwa sababu haijahujumu uchumi.

Na kisheria, anayehujumu uchumi ndiye anayepaswa kuwajibishwa kwa sheria hiyo tena kwa kutaifishiwa mali, sasa labda watwambie kama kuna kilichohujumiwa na kampuni hiyo, halafu tukafichwa, ili tusidhani kuwa Serikali inawekewa mtego,” alisema.

Alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria, endapo Serikali itakubali kutumia sheria hiyo,
italazimika kuilipa Dowans fidia ya mitambo yake kulingana na bei inayotumika sokoni, ambayo hata hivyo alisema inaweza kuwa mzigo mkubwa tofauti na inavyofikiriwa na wanaotoa ushauri huo.

Mtaalamu huyo wa sheria, alitaja Ibara ya 24(1) na (2) ya Katiba na kuonya kuwa kipengele hicho kikitafsiriwa vibaya au kuchukuliwa kiholela, kinaweza kuleta matokeo mabaya.

“Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka wazi kwenye ibara niliyoitaja pamoja na ibara zake mbili ndogo kuwa; kila mtu ana haki ya kumiliki mali, na ya kuhifadhi mali aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

“Ibara ndogo ya 2 inasema; bila ya kuathiri masharti ya ibara ndogo (1), ni marufuku kwa mtu yeyote kunyang’anywa mali yake kwa madhumuni ya kuitaifisha au mengineyo bila idhini ya sheria ambayo inaweka masharti ya kutoa fidia inayostahili,” alisema.

Kuhusu wazo la kuingia mkataba mpya na Dowans wa kuwasha umeme japo kwa miezi mitatu ili kunusuru hali ngumu ya umeme iliyopo nchini kwa sasa, wataalamu hao walisema kushauri hivyo ni kuiingiza Serikali kwenye mtego wenye maslahi ya watu binafsi na wala si ya Taifa.

“Nilisikiliza hotuba ya Rais siku fulani na kumsikia akisema kuwa wataalamu wa sheria watatumika kuona watakavyofanya ili Tanesco isilipe deni hilo.

Rais aliitaka isiharakishe malipo hayo na nadhani alifanya hivyo kiuzalendo. “Sasa hawa wanaotaka Dowans ikodishwe tena na kuzalisha umeme wakati shauri la kwanza bado
halijaisha na Mahakama inayolishughulikia haijatoa uamuzi, wanalitakia mema Taifa hili kweli?

Au wanafanya hivyo bila kujua madhara yake baadaye kwa kampuni inayoidai Serikali?” Alihoji mtaalamu huyo.

Alionya kuwa kitendo hicho kitaipa kampuni hiyo nguvu maradufu za kusimamia uhalali wake na kusisitiza juu ya malipo yake ya awali.

“Nashauri busara itumike katika suala hili, kwa sababu linamgusa kila Mtanzania, mambo yachunguzwe kwa kina na mwenye maslahi yake asipewe nafasi ya kutoa ushauri, sidhani
kama Serikali haina namna nyingine zaidi ya Dowans. Nashauri iepukwe ili kutowachanganya wananchi,” alisema.

Vyombo mbalimbali vya habari nchini jana vilimnukuu Mbunge wa Bumbuli na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, akisema kuwa Kamati yake inajadiliana juu ya uwezekano wa kuishauri Serikali iingie mkataba na Dowans wa kuzalisha umeme wa dharura kwa miezi mitatu ili kumaliza tatizo la nishati hiyo.

Pamoja na mambo mengine, alikaririwa akisema itakapobidi, watatumia Sheria ya Kuhujumu Uchumi ili kutaifisha mitambo ya Dowans.

Tuesday, February 15, 2011

Serikali yaeleza mikakati upatikanaji maji

SERIKALI imewasilisha bungeni kauli ikielezea mikakati mbalimbali iliyochukuliwa na inayoendelea kuchukuliwa katika kutekeleza miradi ya maji nchini.

Katika mikakati hiyo, upo ule unaofadhiliwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Mustafa Sabodo wa kutoa fedha ili kuchimba visima 700 nchini kote isipokuwa katika Jiji la Dar es Salaam.

Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, aliliambia Bunge mjini hapa Februari 14 kwamba mikakati hiyo inalenga katika kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo maeneo ya vijijini.

Alisema hivi sasa Serikali ipo katika utekelezaji wa miradi mipya ya maji ambayo itagharimu dola za Marekani milioni 951, zitakazotokana na fedha za Serikali na wafadhili mbalimbali wakiwemo Benki ya Dunia.

Alisema Serikali imesimamia kwa ukaribu utekelezaji wa Programu ya Maji Vijijini ya mwaka 1971 hadi 1991 ambapo miradi 20 ya maji ilijengwa na Serikali.

Alisema ili kuona kama utekelezaji wa miradi ya maji inaleta ufanisi, Serikali ililazimika kuifanyia tathmini Sera ya Maji ya mwaka 1991, tathmini ambayo ilifanyika mwaka 1997 na kufanya Serikali kuunda Sera nyingine ya Maji ya mwaka 2002, ambapo miradi ya maji iliwekewa mikakati bora zaidi ya utekelezaji.

Alisema msukumo mwingine uliwekwa katika programu ya maji ya miaka 25 ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2006 na utaendelea hadi mwaka 2025, ambapo miradi mbalimbali ya maji imeainishwa na kuanza utekelezaji wake ili kuboresha hali ya upatikanaji wa maji.

Alisema hata hivyo msukumo mkubwa umekuwa katika miradi ya maji yenye uwezo wa kutoa matokeo ya haraka ambapo miradi 2024 imeweza kutekelezwa na hivyo kuwafanya wananchi milioni 2 kupata maji.

“Pamoja na miradi mingine ya maji, upo mradi ambao utafadhiliwa na mfanyabiashara Mustafa Sabodo ambaye yeye ataisaidia Serikali kuchimba visima 700, nchini kote isipokuwa Dar es Salaam, hatua ambayo itawezesha wananchi zaidi kupata maji safi na salama," alisema Profesa Mwandosya.

Monday, February 14, 2011

Makinda azuia posho mara mbili kwa wabunge

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amegeuka 'mbogo' na kueleza msimamo wake kwamba hatawavumilia wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, watakaopokea posho mara mbili wanapotembelea taasisi au mashirika yaliyo chini ya kamati hizo.

Uchunguzi wa HabariLeo umebaini kwamba Spika Makinda alitoa onyo hilo alipofanya kikao kwa mara ya kwanza na Kamati ya Uongozi ya Bunge inayoundwa na wenyeviti wa Kamati 18 za Kudumu za Bunge mwishoni mwa wiki mjini hapa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kilieleza kuwa Spika amesema kwake litakuwa ni kosa kubwa kwa wabunge kupokea posho mara mbili wanapofanya ziara kukagua uendeshaji wa mashirika mbalimbali na idara za Serikali.

"Ametuambia wazi kwamba kitendo cha kupokea posho mara mbili kinaathiri kwa kiwango kikubwa usimamizi na ukaguzi katika mashirika haya maana wabunge wakipokea posho za Bunge na zile zinazotolewa na mashirika yanayokaguliwa hushindwa kutimiza wajibu wao
ipasavyo," kilisema chanzo hicho.

Kwa mujibu wa habari hizo, Spika amesema atatumia Kanuni za Bunge zinazozuia wabunge kupokea takrima yoyote wanapotembea mashirika wakati tayari ziara zao zinakuwa zimelipiwa na Bunge.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo Mwenyekiti wake ni Spika na Makamu wake ni Naibu Spika Job Ndugai, January Makamba alikiri Spika kueleza msimamo wake huo juu ya wabunge kupokea posho mara mbili.

January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM) ni Mjumbe wa kamati hiyo kutokana na wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Alisema suala hilo ni mojawapo ya masuala yaliyopewa msisitizo mkubwa na Spika Makinda alipokutana na wajumbe wa Kamati ya Uongozi mwishoni mwa wiki.

"Unashangaa kuona wajumbe wanafanya ziara katika shirika fulani halafu wanapewa bahasha kwa maelezo kwamba ni posho ya chakula, lakini ukiangalia ndani unakuta ni shilingi milioni moja…Sasa sijui ni chakula gani kinachouzwa kwa bei hiyo. Spika amelikemea vikali suala hili," alisema January.

Wajumbe walioshiriki kikao hicho cha Kamati ya Uongozi mbali ya Spika, Naibu Spika na January ni Edward Lowassa (Mwenyekiti Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama); Dk. Abdalah Kigoda (Mwenyekiti Kamati ya Fedha na Uchumi); John Cheyo (Mwenyekiti Kamati ya Hesabu za Serikali); Augustino Mrema (Mwenyekiti Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa); George Simbachawene (Mwenyekiti Kamati ya Sheria Ndogo) na Margaret Sitta (Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii).

Wengine ni Kabwe Zitto (Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma); Jenista Mhagama (Mwenyekiti Kamati ya Maendeleo ya Jamii); James Lembeli (Mwenyekiti Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira); Profesa David Mwakyusa (Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji); Mahmoud Mgimwa (Kamati ya Viwanda na Biashara); Peter Serukamba (Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu); Pindi Chana (Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala); Hassan Ngwilizi (Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge) na Lediana Mng'ong'o (Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Ukimwi).

Sakata la wabunge kulipwa posho mara mbili, liliibuka wakati wa Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta, ambapo wabunge walilalamikiwa kupokea posho mara mbili, hatua ambayo ilisemwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Dk. Edward Hoseah, kwamba ni sawa na kupokea rushwa.

Kauli hiyo ya Dk. Hoseah iliibua mgongano mkubwa baina yake na wabunge kabla ya Spika Sitta kulitolea maelezo kwamba kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ni marufuku kwa wabunge kupokea posho wanapofanya ziara katika mashirika hayo huku tayari ziara hizo zikiwa
zimelipiwa posho na Bunge lenyewe.

Thursday, February 10, 2011

Uandishi wa Katiba mpya na Uhandisi wa mustakabali mpya

Na Jenarali Ulimwengu
Februari 9, 2011

MJADALA kuhusu uandishi wa Katiba mpya ya Tanzania umeanza, na nina imani utaendelea kwa muda mrefu kidogo, na urefu huo wa muda utasababishwa na mambo kadhaa.

Jambo la kwanza linaloweza kusababisha muda wa mjadala huu kuwa mrefu ni kwamba miongoni mwetu kuna watu wasioona umuhimu wake, watu wanaodhani kwamba madai ya Katiba mpya ni wale wenye kile kinachoitwa “uchu wa madaraka.”

Mara nyingi yanapotumika maneno kama haya walengwa wake ni wale walio nje ya madaraka ambao wanadhaniwa kwamba wana “uchu wa madaraka” kwa sababu wanataka kuwang’oa walio madarakani ili waingie wao.

Inawezekana, kweli, kwamba wale walio nje ya madraka wakawa na “uchu wa madaraka”, lakini hiyo haina maana kwamba wale waliomo madarakani hawana huo “uchu wa madaraka.”

Kimantiki tungemwangalia yule aliye madarakani na anayeng’ang’ania kubakia humo kwamba ndiye mwenye uchu wa madaraka (kwa kuendelea kung’ang’nia humo) na yule aliye nje kuwa pia ana uchu wa madaraka (kwa kukazania kumng’oa yule aliye ndani).

Wanasiasa ni watu wanaojulikana kuwa na huo uchu, na kwa kundi moja kuwasema wenzao eti wana uchu wa madaraka na kutaka kusema kwamba hao wanaowasema wenzao hawana uchu wa madaraka. Huo ni uongo na unafiki.

Ni katika jitihada za kusuluhisha na kuratibu aina mbalimbali za uchu wa madarka wa wanasiasa, ndipo Katiba ya nchi inapokuwa na umuhimu, kama kielelezo cha utashi uliobainika na kujengeka miongoni mwa matabaka ya kijamii kuhusu jinsi ya kuendesha utawala, uongozi, uchumi, utamaduni na mambo mengine mengi yanayoihusu jamii husika.

Utashi ninaoujadili hapa una madaraja mengi, na kadri jamii zinavyokomaa na kupevuka, madaraja hayo hunyumbuka na kuchukua sura mpya ambazo awali hazikutambulika hata kama zilikuwa na watetezi wake.

Kwa mfano, Mapinduzi ya Marekani (1776) yalikuwa na dibaji ya Tamko la Uhuru, lililounguruma na kusema, “Tunatambua haya mambo kama yanayojidhihirisha yenyewe, kwamba wanaume wote wameumbwa sawa, na kwamba wamejaliwa na Muumba wao haki sizizoondosheka, na kwamba haki hizi ni pamoja na Maisha, Uhuru na Usasi wa Furaha”

Katika tamko hilo, wanawake hawatambuliki, na nchini Marekani wanawake hawakupata haki ya kupiga kura hadi mwanzoni mwa karne ya 20. Wala tamko hilo halikuwajumlisha wanaume watumwa, na wajukuu zao walikuja kupiga kura kwa mara ya kwanza katika nusu ya pili ya karne hiyo ya 20.

Hiki ni kielelezo kwamba aina na umbo la utashi wa kisiasa hubeba hali halisi ya wale wanaouunda, maslahi yao, uzoefu wao, matumaini yao na hofu zao. Isingekuwa rahisi kwa akina George Washington na Thomas Jefferson, wakombozi wa Marekani dhidi ya ukoloni wa Uingereza, kuwajumuisha wanawake na watumwa katika madai yao. Wakati ule, Uhuru ulikuwa ni kwa ajili ya mabwanyenye wanaume, wenye mali.

Ilichukua muda mrefu kuibadilisha hali hiyo, hadi leo tunashuhudia Mwafrika akiwa rais na amirijeshi mkuu wa Marekani, ukweli ambao hakuna aliyeuota hata miaka 20 tu iliyopita.

Ndiyo kusema, basi, kwamba hakuna hali katika maisha ya binadamu itakayobaki imetulia tuli kwa muda mrefu. Mazingira ya maisha yetu hubadilika siku zote, na juu wa wajuzi wa mambo pamoja na viongozi wa jamii kulitambua hilo ili waweze kuwaongoza wenzao katika kufanya mabadiliko mwafaka na kwa wakati unaofaa. Kutolitambua hilo kunaweza kusabababisha hasara kubwa katika mfumo wa kiutawala na wa kijamii.

Tuesday, February 8, 2011

Bunge kutojadili hoja binafsi ya Dowans

SAKATA la malipo ya kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited, limechukua sura tofauti baada ya Bunge kutupilia mbali hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR) ya kutaka lijadaliwe bungeni.

Wakati Bunge likitoa uamuzi huo Dodoma, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM) amepeleka hoja nyingine, kuitaka Serikali itoe tamko bungeni kuhusu lini hali ya umeme itatengemaa nchini, huku akitaka hoja hiyo itolewe ufafanuzi katika tamko hilo.

Katika hoja hiyo ya January, alisema “jambo hili likibaki bila maelezo, inaweza kujengeka sura kwamba Serikali ilikosa umakini na maadili hayakuzingatiwa.”

Jijini Dar es Salaam nako wanachama wa CUF, wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, waliandamana kupinga malipo ya kampuni hiyo, huku wakitoa mwito wa suala hilo kupelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ili Rais apate ushauri wa chombo mahususi kwa kazi hiyo.

Lakini katika barua ya January, ya Februari 3 mwaka huu kwenda kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja yenye kichwa cha habari ‘Taarifa ya Serikali Bungeni Kuhusu Umeme Nchini’, anaitaka Serikali kutoa taarifa ikibainisha ni lini itapeleka mahakamani pingamizi dhidi ya utekelezaji wa hukumu ya kuilipa Dowans.

Hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) inalitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kuilipa kampuni hiyo Sh bilioni 94.

“Mheshimiwa Waziri, mnamo tarehe 6 Januari 2011 ulizungumza na waandishi wa habari na kueleza kwamba Serikali inajipanga kuilipa Dowans tuzo iliyoamuliwa na ICC, lakini kwa kuwa mzigo huo ni mzito kwa umma, kumekuwa na fikra, likiwamo pendekezo la Kamati ya Wabunge wote wa CCM kwamba ni muhimu kutumia mianya ya sheria iliyopo kupinga rasmi kutekelezwa kwa hukumu hiyo,” alisema.

Aliitaka pia Serikali iueleze umma kupitia Bunge kuwa ni wanasheria gani waliotumiwa na Tanesco kwenye kila hatua katika shauri la Dowans, kuanzia kwenye ushauri kabla ya kuvunjwa mkataba wa kufua umeme, hadi ushauri baada ya kesi kuamuliwa na kiasi cha fedha walizolipwa kwa kila hatua na utaratibu uliotumika kuwalipa.

“Ili kuwaondolea wasiwasi Watanzania ambao wengi wao wanaamini Tanesco ilishindwa kesi ya Dowans kutokana na upungufu wa weledi kwa wanasheria walioiwakilisha kwenye kesi, nashauri taarifa ya Serikali ieleze utaratibu unaotumika kuwapata wanasheria wanaoiwakilisha Serikali na Tanesco kwenye mashauri yake,” alieleza January.

Miongoni mwa mashauri hayo ni pamoja na lile lililofunguliwa na Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) dhidi ya serikali na Tanesco kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kesi za Uwekezaji (ICSID).

Kesi dhidi ya Tanesco ni ya Oktoba mosi mwaka jana na dhidi ya Serikali ni ya Juni 11 mwaka huo huo. January anataka wananchi waelezwe ni nini hasa kinachodaiwa katika kesi hizo.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashillilah akizungumza juu ya ratiba nzima ya vikao vya Bunge hilo alisema hoja ya kampuni hiyo pamoja na kupelekwa kwa maelezo ya Kafulila, haiwezi kujadiliwa kutokana na Bunge hilo kushindwa kuingilia Mahakama.

“Kwa kawaida na kwa mujibu wa kanuni, Bunge haliwezi kujadili hoja ambayo tayari iko mahakamani na hata Mahakama yenyewe huwa haina nguvu kujadili hoja inayojadiliwa bungeni, kifupi hoja hii kwa bahati mbaya haitajadiliwa, kwa sababu tayari iko mahakamani,” alisema.

Kwa upande wa hoja ya kuundwa kwa Katiba mpya, Kashillilah alisema hoja hiyo pia haitawasilishwa bungeni hapo kutokana na kukiuka Katiba hasa baada ya mmoja wa wabunge waliowasilisha makusudio yao kuhusu hoja hiyo, kutaka Katiba ya sasa ifutwe.

Aliwataja baadhi ya wabunge ambao waliwasilisha kusudio lao la kutaka Katiba mpya kuwa ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) na Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (CCM).

Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hoja yeyote ili iweze kupitishwa na kujadiliwa na Bunge, lazima ikidhi vigezo ikiwamo kutokiuka Katiba.

Pamoja na hayo, tayari Serikali imeanza mchakato wa kupeleka hoja bungeni kwa ajili ya kubadili Katiba hivyo hakuna haja ya kuendeleza mjadala huo.

Kuhusu ratiba nzima ya mkutano wa pili wa Bunge hilo la 10 alisema Spika wa Bunge atawasilisha hoja ya kufanya mabadiliko ya kanuni za Bunge baada ya Rais kubadilisha Baraza la Mawaziri.

“Pia kuna baadhi ya wizara ambazo zimebadilishwa na kusababisha baadhi ya idara nazo kuhamishwa hivyo kutokana na mabadiliko hayo inabidi Kanuni zibadilishwe na kusaidia uundwaji wa Kamati za Bunge ambazo nazo zinatakiwa kuendana na mfumo wa wizara zilizopo,” alisema.

Aidha, alisema kwa mujibu wa ratiba hiyo Spika wa Bunge atatangaza Kamati mpya za Bunge hilo, kujadili hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge ambapo alitoa vipaumbele 13 vya kufanyiwa kazi na kusomwa kwa maazimio mawili.

“Hakuna muswada utakaojadiliwa, ila mitatu itasomwa kwa mara ya kwanza na kurejeshwa katika mkutano wa tatu wa Bunge hili la 10 utakaofanyika Aprili,” alisema.

Alisema pia kutafanyika uchaguzi wa wenyeviti watatu watakaomsaidia Spika na Naibu Spika na wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge.

Monday, February 7, 2011

Mfumo wa Bodi ya Mikopo kubadilishwa

RAIS Jakaya Kikwete ameteua tume ya wataalamu 11 kufanya mapitio ya mfumo wa uendeshaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HLSLB) kwa lengo la kuboresha utoaji wa mikopo.

Katika hadidu za rejea, tume hiyo imeagizwa kuangalia upya vigezo na sifa zinazozingatiwa katika utoaji wa mkopo endapo vinakidhi haja na mahitaji halisi ya waombaji na taifa kulingana na makusudio ya kuundwa kwa bodi hiyo.

Kabla ya kuangalia vigezo hivyo, tume hiyo imeagizwa kuchambua kwa kina Sheria iliyounda bodi hiyo na kanuni zake na kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya utoaji mkopo.

Akizungumza mkoani hapa jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema tume hiyo imetakiwa kufanya kazi kwa muda wa siku 60 kuanzia Februari 14 mwaka huu na kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo Aprili 15, mwaka huu.

Alisema pia imeagizwa kuangalia kwa kina muundo wa bodi na ufanisi wake katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kutoa mapendekezo.

Mbali na muundo pia imetakiwa kuchunguza kiini cha malalamiko na uhusiano usioridhisha kati ya bodi na wanafunzi, bodi na taasisi ya elimu ya juu na kati ya bodi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na katika mapendekezo, yawepo ya namna ya kurejesha uhusiano mzuri.

Katika kufanya kazi yao wajumbe wa bodi hiyo wameagizwa kuangalia nchi nyingine zenye mazingira kama ya Tanzania zilizofanikiwa kugharimia elimu ya juu kwa mfumo wa mikopo. Lengo lake ni kuwezesha mikopo itolewe kwa wanafunzi wengi wahitaji wa elimu ya juu bila lawama na kuboresha mfumo huo kwa kadiri inavyoonekana inafaa.

Hatua hiyo ya Serikali, imechukuliwa kukiwa na shinikizo kutoka kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wa kuipindua au kuivunja bodi hiyo na kuundwa upya.

Shinikizo hilo la UVCCM, lililotolewa na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la umoja huo wakidai ndio suluhisho la migomo iliyokuwa ikilipuka kutoka katika vyuo vikuu zaidi ya 10 sasa huku kero kuu ikiwa kucheleweshewa mikopo.

Hata hivyo, uundwaji wa tume hiyo, ambao uliahidiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa mara tu alipofanya ziara ya kwanza kutembelea bodi hiyo, umeonekana kutofuata shinikizo hilo la UVCCM.

Mbali na ahadi hiyo, hata tamko la bodi hiyo lililotolewa siku chache baada ya tamko la UVCCM kutaka ipinduliwe, lilieleza kuwa changamoto iko katika mfumo na kwamba hata ikivunjwa, watakaorithi mfumo huo watakumbana na changamoto hiyo hiyo.

Katika tamko hilo la HELSB, ambalo lilitamka wazi kwamba UVCCM walikurupuka, bodi hiyo ililaumu Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na menejimenti za vyuo husika kwa kuchelewesha majina ya wanafunzi wanaopaswa kupewa mikopo.

Hata hivyo, UVCCM katika moja ya malalamiko yaliyokuwepo katika shinikizo hilo, lilikuwepo la mtindo wa bodi hiyo kupeleka fedha za wanafunzi hao kwa uongozi wa vyuo badala ya akaunti binafsi za wanafunzi.

Malalamiko hayo ya kutupiana lawama yameonekana kuzingatiwa, kwani wataalamu wa tume hiyo ya Rais, wamechaguliwa kwa uwakilishi kuunda sura ya Muungano na kutoka menejimenti za vyuo vikuu vya umma na binafsi na TCU zilizolalamikiwa na bodi.

Pia wapo wawakili wa serikali za wanafunzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wahadhiri na wataalamu wa benki na kutoka kwa wadau wengine wa elimu zikiwemo asasi za jamii.

Kati ya wajumbe hao yupo Mwenyekiti ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayehusika na Taaluma, Profesa Makenya Maboko na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Kassim Almas Umba anayehusika na Utawala wa Fedha.

Pia yupo Ofisa Uhusiano wa Kimataifa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Zanzibar, Masoud Mohamed Haji na Mhadhiri Mwandamizi wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha, Dk. Eliawony Meena.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu TCU, Daniel Magwiza, Mkurugenzi Msaidizi (Uandishi Sheria) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Sarah Baharamoka na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Inayopigania Elimu kwa Wanawake tawi la Tanzania, Profesa Penina Mlama.

Wengine ni Ofisa Taaluma Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Deo Daudi ambaye alikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kwa mwaka 2006/2007.

Rais pia amemteua katika bodi hiyo Mkurugenzi wa Mikopo Benki ya CRDB, Anderson Mlambwa, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Wilbert Abel na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania, Rosemary Rulabuka.

Friday, February 4, 2011

Migogoro ya ardhi yakwamisha elimu Kisarawe

Picha hii ni jengo (madarasa na ofisi) la shule ya Msingi Tondoroni iliyopo kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe, picha hii ilipigwa mnamo mwezi Novemba mwaka 2010 wakati wa utafiti uliofanywa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).

  • Serikali yakifuta kijiji ,wananchi watakiwa kondoka
  • Wanafunzi wanatembea kilomita zaidi ya 10 kufuata shule

Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe ni moja ya wilaya zinazokumbwa na tatizo la migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa hapa nchini pamoja na kuwa ina eneo kubwa la ardhi linaloonekana kutokutumika.

Pamoja na kuwepo kwa eneo kubwa la ardhi ambalo halitumiki bado sehemu kubwa inagombaniwa kwaajili ya makazi ya watu binafsi, na shughuli nyingine.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa, eneo kubwa la ardhi ya Kisarawe, hivi sasa linamilikiwa na wafanyabiashara wakubwa, ambao wanamiliki zaidi ya hekta 500 kwa mtu mmoja, taasisi za kiserikali kama vile Jeshi la wananchi(JWTZ),Shirika la Elimu Kibaha, Shirika la Umeme (Tanesco) na Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads).

Kutokana na sehemu ya eneo kubwa la ardhi kuchukuliwa na taasisi hizo, sehemu ndogo inayobaki imeibua migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha vurugu, chuki na uhasama kati ya wananchi na wanajeshi.

Tayari wananchi wa kijiji cha Mloganzila na Tondoroni wameenza kujega uhasama na chuki didhi ya jeshi na serikali, wakidai kuwa wanawanyanyaswa, na kudhulumiwa ardhi yao ikiwemo shule yao ya msingi.

Sekta ya elimu ndiyo inayoadhirika zaidi kwa kiasi kikubwa kutokana na kukosekana kwa maeneo ya kujenga madarasa, shule mpya, na hata nyumba za walimu.
Moja ya kata yenye changamoto kubwa ya ardhi ni kata ya Kiluvya katika vijiji vya Tondoroni, Mloganziala, na Kiluvya A na B.

Vijiji hivi kila kimoja kinakabiliwa na tatizo la ardhi. Moja ya kijiji ambacho kimeadhirika zaidi ni Tondoroni, ambacho shule ya msingi Tondoroni, imelazimika kufutwa kabisa kutokana na tatizo la ardhi. Eneo lote la ardhi ya kijiji cha Tondoroni, limekuwa eneo la jeshi, na kulazimika kuifunga shule hiyo.

Shule ya ya msingi Tondoroni iliyojengwa mwaka 1980 ilikuwa shule ya kwanza kujengwa katika kata hiyo, na kusajiliwa na Wizara ya Elimu kwa namba PW 54-02-42, lakini hivi sasa bado imejengwa kwa miti na kizibwa kwa tope.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Tondoroni Lister Bunzu, anaeleza kuwa shule hiyo ilijengwa kwa nguvu za wananchi lakini, ikasajiliwa ikiwa na walimu wawili tu na madarasa saba wakati huo.
Bunzu anasema wananchi wameshangaa kusikia serikali ikitoa tangazo la kuifuta shule hiyo na kuwahamishia wanafunzi shule za jirani badala ya kuiboresha.

“Sisi tulifikiri kuwa serikali ingechukua jukumu la kuijenga upya hii shule, lakini imeamua kuifuta kwa sababu kuwa eneo hili limepewa jeshi, yaani sisi wananchi hatuna haki tena na shule yetu tuliyoijenga, ardhi anapewa mtu na shule yetu inafutwa,”anasema Bunzu.
“Hatukatai serikali kulipa jeshi ardhi, sisi tunataka utaratibu ufuatwe na wananchi wanaokutwa wakimikili ardhi wapewe haki zao stahili. Shule yetu iliyopo hapa iendelee, siyo kufutwa,”anaongeza Mtendaji huyo.

Wanafunzi zaidi ya 250 waliokuwa wakisoma katika shule ya Tondoroni kwa sasa wamehamishiwa shule za msingi, Visegese,Chanziga,Kiluivya A na B, na Mloganzila.
Kwa sasa baadhi ya wanafunzi kuanzia wa darasa la kwanza hadi la saba wanaohamishwa kutoka katika shule hiyo watapaswa kutembea umbali wa kilomita zaidi ya saba hadi 18 kwa siku ili kufika shuleni.

Tatizo kubwa ambalo linaonekana na ni changamoto kwa watoto wadogo wanaokwenda shule ni suala la umbali kwasababu mazingira ya vijiji hivyo ni pori, watoto hao wanapaswa kukatiza maeneo ya porini, kuzifikia shule.
Bunzu anasema: “hapa watoto wetu wenye umri mdogo wamekwama, wale wenye umri wa miaka saba hadi 10. wanasubiri nyumbani, wakifika miaka 11 hadi 14, ndiyo wanaoweza kumudu umbali na kukatiza porini ili kwenda shuleni,”

Kwa mujibu wa Barua ya Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ya iliyoandikwa kwa wananchi wa Tondoroni Machi 10,2009, ya kuifunga shule hiyo, imeeleza kuwa shule hiyo imefutwa kutokana na tatizo la ubovu wa majengo yake.
Mwanaisha Kassimu (7), ni mmoja wa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi Visegese, anatembea kilomita nne kwenda shule tu akikatiza katika eneo la kijiji cha jirani, kutokana na shule yake ya awali ya Tondoroni kufutwa.
“Shule yangu ipo katika kijijni cha jirani, ninatembea saa mbili kuitafuta shule, wakati mwingine siendi kwasababu kuna nyoka, na unatemebea porini mwenyewe,”anasema Mwanaisha.
Adelina Mathias Mbowetu, ni mwalimu wa kwanza wa shule hii, aliyeanza kazi shuleni hapo mwaka 1980, yeye anaelezea jinsi walivyoianzisha shule hiyo na ilivyokuwa muhimu wakati huo.
Anasema kuwa wakati huo walikuwa walimu wawili, yeye na mwingine ambaye alimtaja kwa jina moja la marehemu Mwamvita, na shule ilikuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Kiluvya kutokana na kuwa shule pekee katika kata hiyo.

“Nimeingia katika kijiji hiki mwaka 1980, nikiwa nimehitimu masomo, nikaamua kufanya kazi hapa mazingira yalikuwa ya kujitolea zaidi, tulikuwa walimu wawili tu, lakini hatukukata tamaa, tumefundisha, tukitegemea kuwa shule hii ingeboreshwa lakini hadi nimehama na hata kufikia kustaafu miaka 30 baadaye shule imebakia vilevile,”anasema Mwalimu Adelina ambaye amestaafu sasa.

Afisa Mtendaji wa kata ya Kiluvya, Godfrey Lamecky, anasema kuwa eneo yeye hana taarifa kama kijiji cha Tondoroni kimefutwa na na kama hakijafutwa rasmi shule hiypo ingepaswa kuendelea kuwepo.
Lamecky anasema kuwa kata yake imekuwa na kesi nyingi za ardhi ikiwepo migogoro inayotokana na ukosefu wa ardhi kwasababu watu wachache au taasisi kujichukulia maeneo ya wananchi.

“Hapa kuna migogoro mingi, badhi ya kesi zipo kwenye baraza la ardhi la kata, na nyingine mahakama kuu kitengo cha ardhi, hii inatokana ana mgawanyo wa ardhi ambao kwa baadhi ya maeneo haukuzingatia sheria na taratibu,”anasema.

Kauli ya Mtendaji huyo, inaungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauiri ya Kisarawe, Isaya Moses, anayesema kuwa mgawanyo wa ardhi katika wilaya yake haukuzingatia taratibu na sasa anaanza operesheni ya kupitia upya taratibu zinazotumika.
Kuhusu Shule hiyo ya Tondoroni, Moses anasema serikali imeifuta shule hiyo na wanafunzi watapaswa kufuata maagizo ya serikali kwa kuhamia katika shule walizohamishiwa.
“Nikueleze ukweli, shule hii imefutwa, haruhusiwi mtu yoyote kutumia majengo ya shulke hiyo, akikutwa mtu pale sisi tutamkamata,”anasema Isaya.
Migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa inakwamisha ari ya wananchi ya kuchangia elimu kwasababu wanaona kuwa hakuna haja ya kujenga shule ambazo zipo mbali na makazi yao na watoto wao hawataweza kusoma kutokana na umbali.

Kutokana na kufutwa kwa kujiji hicho kinyemela wananchi wa Tondoroni hivi sasa hawana huduma za msingi za kijamii, kama vile afya, maji, elimu, chakula kutokana na kukatazwa kuliendeleza eneo hilo.

Akizungumza kwa uchungu, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Lister Bunzu, alisema anashangaa kuambiwa kuwa kijiji hicho kimefutwa wakati yeye na wananchi wake hawajawahi kupewa barua ya kufutwa kwa kijiji.
“Tondoroni ni kijiji cha siku nyingi, tulijenga shule yetu ya msingi hapa mwaka 1980, na mwaka 1986 kijiji hiki kiliandikishwa na serikali. Mwaka 1992 kijiji chetu kilipewa hati ya usajili kutoka serikalini, na hati hiyo tunayo hadi leo, haijafutwa,”alisema Bunzu.

Bunzu amesema mgogoro huo umesababishwa na serikali ya Wilaya kushindwa kuwatetea wananchi wake wakati Jeshi linapotaka kukichukua kijiji hicho, kwani wananchi wanishi hapo kihalali, na walipaswa kupewa eneo lingine la kuishi na kulipwa fidia ikiwepo kupewa barua rasmi ya kukifuta kijiji hicho.

Kwa Mujibu wa hati ya Usajili wa kijiji hicho, Kijiji kiliandikishwa kwa hati namba PW/KIJ/539. Chini ya sheria namba 7 ya mwaka 1982 chini ya kifungu namba 22(sheria ya serikali za mitaa na mamlaka ya Wilaya) na kutolewa septemba 14,1993.
Akizungumzia saula hilo, Mtandaji wa kata ya Kiluvya, Godfrey Lamecky, alisema yeye hana taarifa za kufutwa kwa kijiji hicho kwani hajawahi kuona barua kutoka serikalini ya kukifuta kijiji licha ya kuona hati ya usajili wa kijiji.
“Mimi ninashangaa ninaposikia kuwa kijiji kimefutwa, kwasababu nimeingia katika ofisi hii sikukukuta barua, na sijawahi kupewa, sasa mimi mnataka niseme uongo kuwa kijiji kimefutwa wakati sina ushahidi?

“Nimeuliza katika vikao vya halmashauri juu ya kijiji hicho, tena cha kushangaza bado tunapeleka huduma pale, kama vile vyandarua vya mbu tumegawa pale juzi, kuna afisa kilimo na mifugo ambaye analipwa na halmashauri, na kuna tawi la Chama cha Mapinduzi(CCM) na wanapiga kura za maoni” aliongeza Lamecky.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Isaya Moses, alisema yeye hakitambui kijiji hicho na yeye kama msimamizi mkuu wa uchaguzi wa jimbo hilo, hataweka kituo cha kupiga kura katika kijiji hicho.
“Mimi sikitambui kile kijiji, watu wamelipwa wanatakiwa kuondoka kama hawataondoka pale sisi tutawakamata, lile ni eneo la jeshi. Nimesema tena serikali imeshakifuta kijiji hicho” alisema Moses

Alipoulizwa kama ofisi yake imeandika barua ya kukifuta kijiji hicho kwa uongozi wa ngazi za chini na wanakijiji alisema “ kwakweli sijui kama wamepewa barua ya kufutwa kijiji, lakini ninakiri kuwa mimi sijawaandikia, kama hawana barua ni makosa yalifanyika huko nyuma. Lakini sikitambui kijiji hicho!” alimalizia Mkurugenzi huyo.

Alipotakiwa kulitaja aneo mbadala ambalo limetengwa kwajili ya wananchi hao, ili kulipisha jeshi, alisema yeye hajui kama eneo mbadala lilitengwa kwaajili ya wananchi, ila anaamini kuwa walioanza kuwahamisha watakuwa waliandaa sehemu nyingine.
“ Nafikiri waliofanya wakati huo, watakuwa waliandaa eneo lingine, la kwenda lakini sina uhakika”alisema Moses.

Wakazi hao wamedai kuwa wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo tangu mwaka 1976.
Agizo la kuondoka kwa wananchi hao lilitolewa na uongozi wa 83 KJ kilichopo wilayani humo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Halfa Karamagi.

Naye mkazi mwingine wa kijiji cha Mloganzila, Bi. Asha Shomari (80), alisema kitendo kinachofanywa na wanajeshi hao ni ukatili kwani yeye alianza kuishi hapo tangu akiwa msichana na hajawahi kulipwa fidia wala kuambiwa hatakiwi kukaa hapo.

Anasema katika jambo hilo, lazima serikali iingilie kati kwani na wao ni Watanzania sawa na wengine hivyo wanahitaji haki ya kulindwa wao na mali zao.
Amesema kuwa mwaka 1986 Wilaya ya Kisarawe ilitangaza kuwalipa fidia lakini walipokwenda wengine waliambulia Sh. 2,000 zikiwa ndani ya habasha ambapo wengi wao walizikataa.
Amefafanua kuwa, wananchi wengi walipofika njiani na wengine nyumbani, walichokikuta hawakuamini.

Umeme balaa jipya

-Bado miezi miwili kuwa giza totoro
-Sasa kudura za Mungu tu ndio mwokozi

HALI ya uzalishaji umeme nchini ni mbaya. Kiwango cha maji kwa ajili ya kuzalisha umeme kwas asa kina ukomo wa miezi miwili tu kama mvua za kutosha hazitanyesha, Raia Mwema imetafiti na kuthibitishiwa na uongozi wa shirika la umeme nchini, TANESCO,na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili, sekta ya uzalishaji umeme nchini inakabiliwa na matatizo makubwa matatu. La kwanza ni uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hususan bwawa muhimu la Mtera, mkoani Iringa.

Tatizo la pili ni uhaba wa gesi asilia ambayo imekuwa ikitumika na kituo cha kuzalisha umeme cha Songas kilichopo Ubungo, ikibainika kuwa upatikanaji wa gesi hiyo si wa kutosheleza mahitaji. La tatu ni uhaba wa mafuta ya kuzalisha umeme, hasa katika mtambo wa IPTL, chanzo kikiwa ni ukosefu wa fedha.

Hali ya umeme nchini Uchunguzi wa gazeti hili kwa miezi kadhaa sasa umebaini kuwa hali ni Mbaya mno, na hilo linathibitishwa na mgao wa umeme unaoendelea nchini hivi sasa.

Sababu ya mgao huo uliodumu kwa zaidi ya miezi miwili ni mbili. Taarifa za kiuchunguzi zinafichua kuwa, sababu ya kwanza ni matatizo katika mitambo ya gesi asilia iliyopo katika kisiwa cha Songosongo.

Gesi asilia huzalishwa Songosongo na hupelekwa kwa mabomba hadi kituo cha Songas, Ubungo, na kusambazwa kwenye vituo vinavyonunua gesi hiyo ili kuzalisha umeme.

Vile vile licha ya mitambo ya gesi kuwa mibovu na matengenezo yakeyakitajwa kuendelea vizuri, Raia Mwema imebaini kuwa kiasi cha gesi inayopatikana kwa ajili ya uzalishaji huo kinazidi kupungua.

Sababu ya pili ni uhaba wa maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme. Vituo vya Kihansi (megawati 180), New-Pangani Falls (megawati 68), Hale (megawati 21) na Nyumba ya Mungu (megawati 8), vinazalisha chini ya uwezo.

Hali ya kuzalisha chini ya uwezo inatokana na maji yanayoingia kwenye mitambo hiyo kuwa kidogo na kwa kuwa vituo hivyo havina mabwawa makubwa yanayohifadhi maji mengi. Kati ya vituo hivyo, ni Nyumba ya Mungu pekee yenye hifadhi ya maji.

Matokeo ya hali hiyo ya uzalishaji umeme kushuka ni kwamba TANESCO inawajibika kugawa umeme kwa sehemu na kwa awamu, maarufu kama “mgawo wa umeme”.

Mahitaji ya umeme ni makubwa kuliko uzalishaji. Mahitaji ya juu ya umeme hivi sasa nchini katika gridi ya taifa ni megawati 840 wakati mitambo ya kufua umeme (ya maji, gesi na mafuta kwa pamoja) inazalisha takriban megawati 670.

Kwa hiyo kuna upungufu wa kati ya megawati 170 na megawati 200, kulingana na mahitaji ya umeme ya kila siku.

Tutarajie nini siku zijazo?

Hakuna matarajio nje ya uwezo wa Mwenyezi Mungu kuihurumia nchi kwa kushusha mvua nyingi katika kipindi cha miezi michache ijayo ili ijaze mabwawa.

Ikiwa mvua za kutosha hazitanyesha ili kuongeza maji kwenye mabwawa, tutarajie kwamba hali ya umeme itakuwa mbaya zaidi.

Taarifa zilizopo zinathibitisha kuwa kwa kiasi kikubwa nchi inategemea umeme wa maji. Bwawa la Mtera ndilo linalohifadhi maji mengi yanayotegemewa kuzalisha umeme kwenye kituo cha Mtera kinachozalisha megawati 80.

Maji hayo ya Mtera pia huelekea bwawa dogo la Kidatu na kutumika kuzalisha umeme kituo cha Kidatu chenye uwezo wa megawati 200.

Raia Mwema imebaini kuwa maji kwenye bwawa la Mtera yamepungua na wakati huo huo yanayoingia bwawani hapo (inflows) ni kidogo.

Umebaki umeme wa miezi miwili

Kwa mujibu wa uchunguzi wetu, hadi Januari 28, mwaka huu, bwawa la Mtera lilikuwa lina mita 691.73 za ujazo tu kutoka usawa wa bahari.

Maana yake ni kwamba kuna mita 1.73 tu zilizobaki kabla ya kina cha chini cha bwawa hilo kufikiwa, ambacho ni mita 698.50, kutoka usawa wa bahari.

Kwa mujibu wa watalaamu wa TANESCO, mita 1.73 ya ujazo ziliyobaki za maji, zinatosheleza kuzalisha umeme kwa miezi miwili tu, ikiwa mvua haitanyesha na kuongeza maji kwenye bwawa hilo.

Kwa maana hiyo, watalaamu wa TANESCO wanaeleza kuwa kinachosubiriwa ni neema ya Mungu kuleta mvua.

“...ama tutarajie baada ya miezi miwili uwezekano wa kituo au bwawa la Mtera kufungwa maji yakiisha. Mtera ikifungwa, lazima Kidatu nayo itafungwa kwa sababu wote hutumia maji ya mto Ruaha.

“Matokeo ya kufungwa vituo hivi ni kuongezeka kwa “mgawo” kwa sababu vituo vya gesi na mafuta yaani Songas (megawati 189), Ubungo Gas Plant (102Mw); IPTL (100Mw) na Tegeta (45Mw) havina uwezo wa kutosheleza mahitaji ya nchi.

“Vituo vya nguvu ya maji (Kidatu, Kihansi, Mtera, New Pangani Falls,Hale na Nyumba ya Mungu) vina uwezo (installed capacity) ya Mw561 pamoja na vituo vya gesi, mafuta na dizeli-uwezo wa taifa ni Mw 1047 tu,” anasema mhandisi wa TANESCO, ambaye hakuwa tayari kuandikwa jina lake gazetini.

IPTL na ukosefu wa fedha

Kituo cha IPTL kwa wakati huu kinasuasua kwenye uzalishaji kwa sababu ya ukosefu wa mafuta ya kuzalisha umeme.

Wiki kadhaa, mitambo ya kituo hicho iliwashwa ili kupunguza ukali wa “mgawo” unaeondelea lakini kilizalisha megawati 20 tu badala ya megawati 100, kutokana na upungufu wa mafuta.

Vituo vya gesi (Songas, Ubungo na Tegeta) navyo vinazalisha chini ya uwezo wake kutokana na upungufu wa gesi kutoka Songosongo.

Upungufu wa gesi unaweza kuathiri hata miradi mingine mipya. Kwa mfano, mipango ya kuwa na kituo cha Kinyerezi, ifikapo mwaka 2013, haitafikiwa ikiwa bomba la Songosongo halitapanuliwa.

“Leo hii Serikali ikiruhusu Dowans kununuliwa na umeme wake ikauziwa TANESCO, Dowans haitafikia kiwango chake cha juu cha megawati 100 kutokana na uhaba wa gesi.

“Hili ni tatizo ambalo Wizara ya Nishati na Madini inapaswa kulichukua kwa uzito unaostahili na mitambo ya Songosongo inahitajiwa kupanuliwa na bomba lililopo kukarabatiwa ili gesi ya kutosha ifikishwe Dar es Salaam kwa mahitaji ya wateja wa viwandani na hasa vituo vya umeme,” anasema mtaalamu ndani ya TANESCO, akisisitiza kutoandikwa jina lake gazetini kwa kuwa si msemaji wa shirika hilo.

Tatizo kubwa zaidi

Mbali na matatizo hayo, tatizo kubwa zaidi ni kutokuwa na umeme wa zaida(reserve margin au spinning reserve) kwenye mifumo ya kuzalisha umeme.

Ndiyo sababu kukitokea hitilafu kidogo kwenye mifumo ya kuzalisha umeme, hakuna suluhisho mbadala zaidi ya kutangaza “mgawo”.

Kwa mfano, mtambo wa megawati 50 ukiharibika Kidatu au Songas, lazima “mgawo » wa umeme utatangazwa.

Umeme si kipaumbele cha serikali?

Tangu utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa JakayaKikwete, hakujawa na uwekezaji wa kutosha katika sekta ya umeme na pia, miradi ya ubabaishaji imekuwa ikiibuliwa mara kwa mara, kama vile Richmond.

Wataalamu ndani ya TANESCO wanaeleza kuwa katika Awamu ya Kwanza, ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, serikali ilikuwa makini katika nishati. Wanaeleza kuwa wakati huo, mitambo ya ziada ya kuzalisha umeme ilikuwapo na baadhi yaka ilipokuwa ikipata hitilafu, mitambo ya ziada ilikuwa tarari kuanza kazi na hapakuwahi kuwa na “mgawo”.

Utaratibu huo ndio unatajwa kutumika katika nchi zinazotambua kuwaumeme ni suala nyeti. Kwa mara ya kwanza nchini, mgawo wa umeme ulianza mwaka 1992 wakati wa utawala wa Mwinyi, ukaendelea wakati wa Mkapa na kushamiri wakati huu wa Kikwete.

Tafiti zinabainisha kuwa wakati Tanzania inahangaika na umeme wa kuvizia kutoka mitambo ya megawati 100 kama Dowans, nchini Afrika Kusini, watu binafsi wamekuwa na mitambo ya kuzalisha umeme wa megawati 100 ndani ya uzio wa nyumba zao.

Kauli ya bosi TANESCO

Raia Mwema iliwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando, ambaye alikiri kuwa hali ya uzalishaji umeme ni mbaya na kiwango cha
maji kilichobaki kinaweza kuzalisha umeme wa miezi miwili pekee, kama mvua hazitanyesha.

“Ni kweli, kiwango cha maji si cha kuridhisha. Kwa sasa ni mita za ujazo 691.95. tunategemea mwezi Machi mvua zinyeshe pamoja na mwanzoni mwa Aprili,” anasema Mhando.

Kiwango hicho kimetofautiana kidogo na kile kilichotokana na uchunguzi wetu ambacho ni 691.73, kilichopatikana Januari 28, mwaka huu.

“Ni kweli hizo mita za ujazo 691 zinaweza kuzalisha umeme kwa miezi hiyo miwili tu,” anasema.

Kuhusu upungufu wa gesi ya Songosongo, Mhando anasema: “Kiwango cha upatikanaji gesi kutoka Songosongo inayosafirishwa kwa mabomba hadiDar es Salaam ni kweli kilipungua.

“Upungufu huo ulitokana na ukarabati uliokuwa ukifanyika huko na matengenezo yalichukua mwezi mzima, lakini tangu Januari 25 hali imerudi ya kawaida.

Alisema kampuni ya Pan African Energy inayozalisha gesi hiyo na kuisafirisha, imelihakikishia TANESCO kiwango cha gesi kitakuwa kikipatikana katika hali ya kawaida.

Kuhusu kiwango cha gesi kushindwa kukidhi mahitaji kama vituo zaidi vya kuzalisha umeme kwa gesi vitaanzishwa alisema : “Ni kweli kiwango cha sasa hakitatosheleza kama itaanzishwa mitambo mipya tofauti na ya sasa.

Vipi kuhusu mradi wa Kiwira?

Kuhusu mradi wa Kiwira, Mhando anasema serikali inakusudia kuukabidhi mradi huo kwa TANESCO itakayoshirikiana na TAMICO ili kuzalisha umeme.

Alisema mradi huo utaendeshwa kwa fedha za mkopo, akijibainisha kuwa kwa sasa hali ya kifedha ndani ya TANESCO si ya hasara kama ilivyokuwa awali.

“Awali, mwaka 2006 tulikuwa na hasara ya takriban Sh bilioni 168, lakini sasa hasara imepungua hadi Sh bilioni tano na inazidikupungua...tunaweza kuvunja rekodi sasa na kwa hiyo tunaweza kukopeshena na wadau wengine, ikiwamo Benki ya Dunia,” alisema Mhando.

Kauli ya Waziri Ngeleja

Raia Mwema iliwasiliana na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ambaye naye alikiri kuwa hali ya umeme si nzuri na kwamba Mtera inaweza kuzalisha umeme wa miezi miwili tu.

“Ni kweli kiwango cha maji Mtera kinaweza kuzalisha umeme wa miezi miwili tu ijayo kama mvua haitanyesha,” alisema Ngeleja.

Kuhusu kusafirishwa kwa kiwango cha kutosha cha gesi kutoka Songosongo, alisema upanuzi wa miundombinu utafanyika kama ambavyo kampuni ya Pan African Energy ilivyoahidi.

“Kuhusu suala la gesi ya Songosongo, kuna kitu kinaitwa ‘re-rating’ ambacho ni kama upanuzi wa miundombinu ya kusafirisha gesi inayofanywa na kampuni ya Pan-African Energy.

“Bwawa la Mtera hali si nzuri lakini kuna dalili za mvua na naambiwa maji yameanza kuingia kidogo kutokana na mvua zilizonyesha kidogo. Unajua, bwawa hili linajazwa na maji kutoka mikoa ya Singida, Dodoma na Iringa.

“Kiwira, uzalishaji utaanza baada ya miezi 20, na Kinyerezi katika miaka miwili na nusu kuanzia sasa na Artmus itakayozalisha Mw300.

Akizungumzia hali ya IPTL kukosa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendesha mitambo hiyo na hivyo kupunguza mgawo nchini alisema mitambo hiyo itaanza uzalishaji wakati wowote baada ya mafuta kupatikana.

Mamlaka ya Hali ya Hewa

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Emmanuel Mpeta, aliieleza Raia Mwema kuwa, kunyesha kwa mvua mwezi Machi, mwaka huu kutategemea na mwenendo wa hali ya hewa.

“Hatutarajii mvua mwezi huu, pengine hadi Machi ambapo mifumo ya mvua inakuwa imesogea kutoka kusini,” alisema.

Ofisa mmoja wa TANESCO ameliambia Raia Mwema kwamba mvua zinazotarajiwa kunyesha kati ya Machi na Mei, hunyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi na kwamba hata zikiwa za kutosha zinaweza zisisaidie sana mabwawa ya kuzalisha umeme kwa kuwa huwa zinawahi kukatika katika maeneo hayo.

Anasema kawaida Januari huwa kina cha maji kinapanda, lakini mwaka huu kimeshuka katika mabwawa ya Mtera na Kihansi. Taarifa zinaeleza kwamba hali itakuwa mbaya zaidi katikati ya mwaka huu.

Chanzo: www.raiamwema.co.tz

Thursday, February 3, 2011

NSSF kufua umeme wa megawati 300 Desemba

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeanza mchakato wa kuzalisha umeme wa megawati 300 ifikapo Desemba mwaka huu, ili kusaidia kuondoa kero iliyopo nchini sasa.

Hayo yalisemwa jana mkoani hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dk. Ramadhani Dau, kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wa NSSF.

Dau alisema pamoja na kuzalisha umeme huo pia wanaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza, lengo likiwa ni kusambaza gesi inayozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema shirika hilo limeshateua mshauri ili kusaidia kufikia azma hiyo na kupunguza kero ya kukatika kwa umeme ambayo husababisha shughuli za jamii kusimama kwa muda.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, shirika hilo limeongeza idadi ya wanachama kutoka 380,693 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 33, na ifikapo Juni mwaka huu, wanachama wa shirika hilo wanatarajiwa kufikia 518,410.

Aliongeza kuwa kwa upande wa wanachama makusanyo yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126,96 hadi Sh. bilioni 315.31 sawa na ongezeko la asilimia 148, matazamio yao ni kukusanya Sh bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu.

Aidha, mwaka 2005/ 6 hadi 2009/10 shirika hilo liliongeza uwekezaji kutoka Sh bilioni 424.89 hadi Sh trilioni 1.03 sawa na ongezeko la asilimia 144, pia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa kushirikiana na Serikali NSSF imewekeza kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), nyumba za Polisi na nyumba za Jeshi la Wananchi.

Alisema miradi mingine imegharimu Sh bilioni 340.5 ambazo ni mkopo kwa Serikali na uwekezaji katika maeneo mbalimbali na kuongezeka kutoka Sh bilioni 477.76 mwaka 2005/06 hadi Sh trilioni 1.136 mwaka 2009/10 na Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha
pensheni kwa asilimia 52 na hivyo wastaafu kuongezwa pensheni kutoka Sh.52,000 hadi Sh.80,000 kwa mwezi.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, malipo ya wanachama yaliongezeka kutoka Sh bilioni 40.18 mwaka 2005/06 hadi Sh. bilioni 102.82 mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 156.

"Nawasihi waajiri kulipa michango ya wafanyakazi kwa wakati ili wanufaike na shirika letu pia tunajitahidi kukamilisha miradi ya ujenzi wa daraja la Kigamboni na kujenga upya makazi kuanzia Mchikichini, lengo likiwa ni kubomoa nyumba mbovu na kujenga mji wa kisasa unaojitegemea - Satellite City".

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilipongeza shirika hilo kwa kujenga majengo mbalimbali likiwamo la makazi na UDOM, daraja la Kigamboni na mpango wa kuzalisha umeme nchini, ili kuondoa kero kwa
wananchi.

Alisema wananchi watafarijika kusikia daraja la Kigamboni litajengwa wakati wowote lengo ni kurahisisha shughuli za maendeleo na alitoa angalizo kwa shirika hilo kutafiti sekta isiyo rasmi ambayo mchango wake ni mkubwa kwenye uchumi wa Taifa na kutoa angalizo kwa waajiri kupeleka michango ya wafanyakazi kwa wakati, ili kuepusha usumbufu baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Katika mkutano huo wanachama saba na wastaafu wawili waliotekeleza sheria za NSSF na kupeleka makato ya wafanyakazi kwa wakati walizawadiwa.

Wanachama hao ni Kampuni ya Madini ya Bulyanhulu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya simu ya Vodacom, Chuo Kikuu cha St. Augustine, Mwanza; Sekta Binafsi, Said Salum Barkhresa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kiwanda cha Tobacco Alliance,
Morogoro; hospitali ya Lugoda, Mufindi na wastaafu Joram Elirai na Joseph Sikira.

JK: Sitaingilia Mahakama

RAIS Jakaya Kikwete amesema hataingilia kamwe uhuru wa Mahakama na badala yake ameitaka taasisi hiyo kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu umuhimu na mipaka ya kiutendaji ya muhimili huo wa Dola.

Amesema kazi hiyo ya elimu itampunguzia adha anayoipata ya kuombwa aingilie kati uhuru huo kwa baadhi ya hukumu za kesi zinazotolewa.

Ingawa haukuwa utaratibu wake kuzungumza katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, Rais Kikwete jana alilazimika kufanya hivyo katika viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam alipoombwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, kusalimia hadhara katika sherehe hizo.

Akitoa salamu hizo, Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema: “Nashukuru Jaji Mkuu kunipa heshima ya kusalimia, nakubaliana nawe kuwa ni kweli wananchi wengi hawajui umuhimu wa Mahakama na elimu ni muhimu sana katika hili, natambua juhudi kubwa mlizofanya mpaka sasa, lakini ziongezwe, mahakama zipo kwa ajili ya kutumikia wananchi.

“Binafsi elimu ikifika sawa sawa itanipunguzia tabu hasa kwa wanaonitumia ujumbe wa kutaka niingilie kesi zao zilizotolewa hukumu, huwa nawajibu lililoamuliwa na mahakama sina uwezo nalo, lakini hawaamini, wananishangaa, mtu mmoja akaniambia ‘acha tumchague mwenzako, ndiyo maana tunataka Katiba mpya (kicheko), ndiyo maana nasisitiza elimu ni msingi wa ufafanuzi wa haya,” alisema Kikwete.

Alisema mahakama zipo kwa ajili ya kutumikia wananchi na kusisitiza kuwa Serikali itafanya kwa sehemu yake, kwa kuwa ni jukumu lake, lakini mahakama kwa kushirikiana na wadau kama vyombo vya habari, wana nafasi nzuri zaidi kutoa elimu hiyo.

Kauli ya Rais imekuja huku baadhi ya watu na taasisi zikimshinikiza atoe kauli ya Serikali kuhusu malipo ya Sh bilioni 94 ambazo zinatakiwa kulipwa na Tanesco kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans , ilyoshinda kesi ya kuvunjiwa mkataba.

Rais Kikwete pia aliuagiza uongozi wa Mahakama kuhakikisha utendaji wa uadilifu na haki, kwa kuwa bado kuna malalamiko kwa wananchi, kuwa baadhi ya mahakimu na majaji wanatumia uwezo wa fedha wa mtu, kama kigezo cha kupewa haki na kutaka kasi ya kuwashughulikia wanaoharibu taswira ya chombo hicho, iongezeke.

“Si mara ya kwanza kusema hili, nafahamu pia kuwa si wote wako hivyo, lakini kuna baadhi uadilifu wao una shaka, natambua pia kuwa wapo wawajibikaji wazuri, na pia nafahamu wapo waliogundulika na kuwajibishwa kwa kukosa uadilifu, juhudi ziongezwe ili kujenga taswira nzuri mbele ya wananchi na dunia,” alisema Rais.

Akizungumzia changamoto, Kikwete aligusia pia Mfuko wa Mahakama, na kusema utekelezaji wake uko katika hatua za mwisho na Muswada wa Sheria utapelekwa katika Bunge la Aprili mwaka huu, ili ufanyiwe kazi na matarajio ni kuanza katika mwaka wa fedha ujao (2011/12).

“Ni matumaini yangu kuwa Mfuko huo utakuwa ni maisha mapya kwa mahakama na uendeshaji mzima wa shughuli zake na mambo mengine yatashughulikiwa na Mfuko, mengine kama maslahi ya majaji tutayashughulikia katika mwaka huo huo wa fedha,” alisema Rais Kikwete.

Jaji Mkuu alimwomba Rais mara baada ya kuanzishwa Mfuko wa Mahakama, kianzio kiwe ni asilimia mbili ya bajeti ya Serikali. Hata hivyo, Rais katika salamu zake hakuzungumzia ombi hilo.

Pamoja na kueleza hayo, Rais aliitaka Mahakama kuongeza kasi ya utekelezaji wa programu ya maboresho ya sekta ya sheria, kwani wabia wa maendeleo wanalalamika na wengine wamerudisha fedha zao ambazo zingetatua matatizo mengi.

Akigusia changamoto zilizobainishwa na Jaji Mkuu, Rais alimhakikishia kuwa Serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa mhimili huo, ili haki itendeke ipasavyo na katika kupunguza msongamano wa kesi, ataendelea kuteua majaji kadiri atakavyoletewa mapendekezo.

“Nitaendelea kuteua majaji mkiniletea mapendekezo, maana watu wanadhani mimi ndio nawachagua, nitatekeleza uteuzi baada ya utaratibu wa uadilifu … katika miaka mitano mahakimu 256 waliajiriwa, mahakama 34 za mwanzo zilijengwa na tunaahidi tutaongeza bajeti,” alisema Kikwete.

Katika awamu yake ya uongozi wa nchi mpaka sasa Rais Kikwete ameteua majaji 52.

Rais Kikwete alisema hadi sasa Serikali imejenga Mahakama Kuu katika mikoa ya Kagera na Shinyanga katika miaka mitano iliyopita na kuahidi kuwa lengo ni kila mkoa uwe na mahakama hiyo.

Aliiagiza Mahakama kuharakisha utekelezaji wa mpango maalumu wa uendelezaji wa mahakama nchini, ili kuwezesha kujengwa kwa nyumba za mahakimu na mahakama na kuahidi kuhamasisha wananchi waliojitokeza kujenga sekondari 3,000 za kata nchini waone umuhimu pia wa kujenga mahakama.

Awali Jaji Mkuu alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili Mahakama ni upungufu wa mahakama hasa za mwanzo, na kutolea mfano kuwa majengo ya mahakama zilizopo mengi ni ya ‘mbavu za mbwa’ na mengine yapo katika majengo ya klabu za pombe, magulio na maghala
ya vijiji.

Akitoa kilio chake mbele ya Rais Jaji Mkuu alisema, “kwenye sera ya mikakati ya elimu, Serikali imeleta matumaini ya kishindo, hakuna Mkuu wa Shule ambaye anasimamia kwa wakati mmoja shule mbili ambazo ziko umbali wa kilometa 130 baina yao, kwa mantiki hiyo, hili la mahakama na mahakimu kuhudumia mahakama kwa umbali huo, linatibika.”

Alisema miongoni mwa mambo yanayowakwamisha ni kutopewa bajeti kamili kama wanavyoomba ambapo mwaka 2008/09 mahitaji yalikuwa ni Sh bilioni 93 lakini walitengewa Sh bilioni 50.2 sawa na asilimia 54 na kati yao zilizowafikia ni Sh bilioni 44.4.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisisitiza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu mhimili huo na usuluhishi uanzie nje ya mahakama kupunguza mlundikano wa kesi.

Rais wa Chama cha Mawakili Tanzania Bara (TLS), Felix Kibodya, akihutubia sherehe hizo, alisema Watanzania wachache wanazijua hivyo kuongeza ugumu katika utekelezaji wake na kudhihirisha hilo, ni katika suala la uundwaji wa Katiba mpya.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiwa mmoja wa viongozi wa kisiasa waliohudhuria sherehe hizo, aliliambia gazeti hili mara baada ya hafla hiyo kuwa utawala wa sheria utafanikiwa ikiwa watawaliwa watazijua sheria, hivyo kuitaka Serikali kuhakikisha hilo
linafanyiwa kazi.

Wednesday, February 2, 2011

Wazazi wadaiwa kuhusika sakata la vichanga

WATOTO 10 waliofukuliwa kwenye shimo la takataka kwa pamoja wakiwa wamekufa katika kitongoji cha Msisiri, Mwananyamala katika Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam juzi, wakiwa wamezungushiwa shuka la Hospitali ya Mwananyamala, inadaiwa walizaliwa wafu na miili yao kukabidhiwa kwa wazazi wao.

Kutokana na kadhia hiyo iliyoshitua wengi, uongozi wa Wilaya ya Kinondoni umeunda timu ya watu watano wakiwamo madaktari wawili kutoka hospitali hiyo kuchunguza tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana juu ya tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, alikiri kuwa watoto hao walitokea Hospitali ya Mwananyamala ambayo ndiyo hospitali ya wilaya na baada ya vifo vyao, hospitali hiyo ilikamilisha taratibu zote zinazohusika kwa wazazi wa watoto hao.

“Ni kweli tukio hili tumelisikia na kwa uchunguzi wetu wa awali tumebaini kuwa watoto hawa hawakuuawa, bali walizaliwa wakiwa wamekufa na kukabidhiwa kwa wazazi wao kama taratibu zinavyosema,” alieleza Rugimbana.

Alisema ,kati ya watoto hao 10, saba walikuwa ni watoto waliotokana na kuharibika kwa mimba na watatu walizaliwa katika mimba zilizokamilika, lakini walikufa kutokana na matatizo ya kiafya akiwamo mmoja aliyezaliwa nje ya hospitali hiyo.

Hata hivyo, alisema pamoja na taarifa hizo za awali, ofisi yake imeunda timu ya madaktari wakiwamo wa nje ya Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuchunguza kitaalamu zaidi juu ya kilichosababisha watoto hao kuzikwa nje ya utaratibu wa hospitali tena kwenye shimo moja la takataka.

“Inaelekea baada ya wazazi kukabidhiwa maiti za watoto wao kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, walitafuta msaada nje ya hospitali wa mazishi na mtu aliyepewa dhamana hiyo kutokana na kutaka urahisi, aliamua kutumia shimo lililochimbwa na kuwazika watoto hawa kinyama,” alieleza Rugimbana.

Alisema, suala la shuka ya hospitali hiyo ambayo imekutwa kwenye miili ya watoto hao, ni moja ya hadidu rejea ya timu iliyoundwa ambayo imepewa siku saba kukamilisha kazi yake na itaongozwa na Dk. Charles Kamhando kutoka Kituo cha Afya cha Sinza wilayani humo.

DC alisema watachunguza uhalali wa shuka hiyo “japokuwa katika hospitali zote za Dar es Salaam wana utamaduni wa kusaidia mtu asiye na uwezo wa sanda na kumpatia shuka.”

Naye Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Saphonias Ngonyani, alisema watoto hao saba waliotokana na kuharibika kwa mimba, walikuwa ni wa kuanzia wiki 28 na tayari walikuwa wameshabadilika na kuwa binadamu.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema tayari polisi inamshikilia na kumhoji mtu mmoja kwa sababu za uzembe kutokana na tukio hilo na mtuhumiwa mwingine anatafutwa.

“Siwezi kuwataja majina yao kwa sasa kwa sababu za uchunguzi, lakini mmoja tunamhoji na mwingine bado tunamtafuta. Na ninawaahidi kuendelea kulichunguza suala hili kwa kushirikiana na timu iliyoundwa hadi pale ukweli utakapobainika,” alisema Kamanda Kenyela.

Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Raphael Ndunguru, alisema timu hiyo iliyoundwa itachunguza kitaalamu kuanzia vifo vya watoto hao, utaratibu mzima wa makabidhiano ya maiti kwa mujibu wa taratibu za hospitali na kilichotokea hadi kuzikwa kwenye shimo moja.

“Pia kwa vile hospitali ina anuani za wazazi wa watoto hawa, kamati itawasiliana nao ili wawataje waliowasaidia kuhifadhi maiti za watoto wao na hapo ndipo ukweli utakapojulikana,” alisema Ndunguru.

Alisema anachofahamu yeye ni kwamba iwapo mtu atakumbwa na tatizo la kifedha juu ya maziko katika hospitali hiyo, Manispaa inayo bajeti ya kusaidia. “Tunaomba wale wote ambao wanakumbwa na matatizo haya wafuate mamlaka husika na kutoa taarifa, lakini si watu baki,” alisema Ndunguru.

Katika mkutano huo yalizuka malumbano baina ya waandishi wa habari na timu ya madaktari akiwamo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Judith Kahama, juu ya taarifa za madaktari hao kuhusu umri wa watoto waliokutwa kwenye shimo hilo.

Waandishi walidai kuwa umri wa watoto unaonekana ni mkubwa na si kama madaktari hao wanavyodai kuwa ni mimba zilizoharibika kwani wapo watoto ambao hata nywele zao zinaonekana zimeshakatwa.

“Mimi nazungumza kitaalamu, watoto hawa ni wa kuanzia wiki ya 28 na si premature (njiti) kama watu wanavyodai,” alisema Dk. Kahama.

Katika taarifa ya polisi iliyotolewa jana Dar es Salaam, ilifafanua kuwa mkazi wa Msisiri Mwananyamala, Amour Mbaga katika shimo lake la takataka, alikuta watoto wachanga 10, watano wa kike na watano wa kiume na kati ya watoto hao watatu walizungushiwa kwenye khanga zenye majina ya mama zao.

Majina ya akinamama hao ni Furaha Rajabu mkazi wa Manzese aliyejifungua mtoto wa kiume Januari 24, mwaka huu na kwa mujibu wa taarifa za hospitali, inaonesha alichukuliwa na baba yake, Idrisa Zuberi siku hiyo hiyo.

Pia Ruth Mtanga ambaye kumbukumbu za hospitali zinaonesha alijifungulia njiani mtoto wa kiume Januari 27, mwaka huu na mtoto huyo kufariki, kumbukumbu hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka hospitalini hapo, ingawa kumbukumbu za mama huyo kupokewa na kutibiwa zilikuwapo.

Aidha, mwingine ni Regina Samweli wa Kimara, ambaye kumbukumbu zinaonesha alijifungua hospitalini hapo mtoto wa kike mfu, lakini kumbukumbu za chumba cha maiti hazioneshi maiti hiyo kuingia wala kutoka.

“Watoto wengine saba walikuwa wamefungwa kwenye shuka la Hospitali ya Mwananyamala Wodi namba 1A na hakuna kumbukumbu yoyote inayoonesha kuwa wamezaliwa na kufa hospitalini hapo,” ilisema Polisi.

Tuesday, February 1, 2011

Mungai afutiwa kesi ya rushwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani Iringa imeifuta kesi ya kutoa rushwa iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mbunge wa Mufindi Kaskazini kwa miaka 35, Joseph Mungai.

Hakimu Mary Senapee wa Mahakama hiyo, alisema jana kwamba, pingamizi la kisheria lililowasilishwa Oktoba mwaka jana na mawakili wa Mungai, lilionesha kwamba mawakili wa upande wa mashitaka walifanya makosa wakati wa kufungua kesi hiyo.

Kwa mujibu wa Hakimu Senape, mawakili hao Alex Mgongolwa na Basil Mkwata, walionesha kuwa upande wa mashitaka uliowakilishwa na mawakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ulikosea kumfungulia Mungai na wenzake mashitaka 15 kwa kutumia hati moja ya mashitaka.

“Naitupilia mbali kesi hii kwa sababu upande wa mashitaka umetumia hati moja ya mashitaka, kumfungulia Mungai na wenzake wawili mashitaka tofauti yanayohusisha sheria mbili tofauti,” alisema Hakimu Senape wakati akitoa uamuzi huo.

Akiwa ameunganishwa na makada wengine wawili wa CCM, Fidel Cholela na Moses Masasi, Mungai alishitakiwa na Takukuru kwa makosa 15 ya kutoa rushwa kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Pia alishitakiwa kukiuka Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 kwa wapiga kura wa jimbo hilo.

Katika hati ya mashitaka hayo, ilidaiwa na Takukuru kwamba Julai 08, mwaka jana, katika Kata ya Ihalimba, Wilaya ya Mufindi, Mungai akiwa mmoja wa makada wa CCM waliokuwa wanawania kupitishwa katika kura za maoni kugombea ubunge wa jimbo hilo alitoa rushwa.

Kwa mujibu wa madai hayo, Mungai pamoja na watuhumiwa wenzake, walitoa rushwa ya kati ya Sh 5,000 na Sh 20,000 kwa wajumbe wa CCM tawi la Vikula kama kishawishi cha kumpigia kura wakati wa upigaji wa kura za maoni.

Hata hivyo, Hakimu Senape alisema Takukuru wanaweza kurekebisha hati hiyo ya mashitaka au kufungua hati mpya ya mashitaka kama wataona kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo.

Baada ya hukumu hiyo, Mgongolwa alisema mbali na kufarijika kwa uamuzi huo, Takukuru walifanya kosa kubwa la kisheria wakati wakifungua mashitaka hayo.

“Katika mashitaka hayo, Takukuru walitumia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Sheria ya Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, jambo lisilokubalika.

Alifafanua kuwa matumizi ya sheria hizo kwa pamoja ni kosa kwa kuwa zina makosa tofauti ndio maana hakimu amekubaliana na pingamizi lao kwa kutupilia mbali kesi hiyo.

Wakili wa Takukuru, Imani Nitumeni alisema Takukuru kama ilivyo kwa upande wa washitakiwa unakubaliana na uamuzi halali wa Mahakama.

“Hata hivyo ofisi yetu, itaupitia upya uamuzi wa Mahakama na kama tutaona inafaa, tutairekebisha hati hiyo ya mashitaka au kwa kuzingatia sheria hizo, kufungua upya mashitaka dhidi ya Mungai na wenzake,” alisema.

Akionekana kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama, Mungai alisema ni uamuzi alioutarajia kwa sababu sheria hizo anazifahamu.

Alisema pia alipokuwa akikamatwa na Takukuru alitoa tahadhari kwa maofisa hao kwamba wanatakiwa kufanya kazi yao kwa uangalifu kwa sababu hakufanya kosa kwa mujibu wa sheria hizo.

“Kuna uwezekano uamuzi wa kunikamata ulikuwa na shinikizo la kisiasa kutoka kwa watu waliokuwa wanataka jimbo langu na nisiendelee kuwa Mbunge,” alidai.

Alisema alishangazwa sana na wepesi uliotumiwa na maofisa hao wa Takukuru wa kumkamata bila woga na kumfungulia mashitaka kwa makosa ambayo hakuyafanya hasa kwa kuzingatia kwamba yeye amekuwa mtunga sheria kwa zaidi ya miaka 35.

“Hata hivyo ninafurahi kwamba nimepata haki yangu, kitakachofuata, nawaachia wanasheria wangu, kwa sababu suala hili limenilitea matatizo makubwa mimi na familia yangu, kwa hiyo tukiiona hukumu yote tutajua nini cha kufanya,” alisema.

Kwa mara ya kwanza Mungai alipandishwa kizimbani akihusishwa na madai hayo Agosti 12,mwaka jana.

Uamuzi huo umeelezwa na baadhi ya wana CCM waliohudhuria mahakamani hapo kwamba unamfagilia njia ya kugombea uenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Iringa baada ya mkoa huo kugawanywa.

Mkoa huo umegawanywa na kuwa na mikoa ya Iringa na Njombe ambayo mpaka sasa inaongozwa na Mwenyekiti mmoja, Deo Sanga (Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini) anayepewa nafasi kubwa ya kuwa Mwenyekiti wa mkoa mpya wa Njombe.

Watoto 10 wachanga wafukiwa shimoni

MIILI ya watoto 10 wachanga imekutwa imefukiwa pamoja katika shimo, Dar es Salaam.

Marehemu hao walikutwa jana katika eneo la makaburi ya Mwananyamala wilayani Kinondoni wakiwa katika kaburi la pamoja wakiwa wameviringwa shuka lenye nembo ya Hospitali ya Mwananyamala.

Pamoja na shuka hilo ni khanga zilizokuwa na namba ya moja ya wadi za hospitali hiyo nazo zikiwa zimewaviringa maiti hao na kufukiwa katika shimo la taka karibu na makaburi hayo.

Watoto hao ambao wanapishana umri na ambao walikutwa tayari wamefariki dunia ndani ya shimo hilo, ni wa kike watano na wa kiume watano pia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo ambaye ndiye mmiliki wa shimo hilo, Amour Mbaga, wakati akienda kutupa taka kwenye shimo hilo alilosema alilichimba mwenyewe, alishangaa kulikuta limefukiwa huku udongo ukionekana mpya.

“Nilishituka kuona shimo langu la taka limefukiwa, nikaenda kuchukua jembe na kufukua na ghafla nikaona mkono wa mtoto, nilishituka zaidi na kukimbilia kwa majirani kuwataarifu,” alisema.

Alisema majirani walimshauri akaripoti tukio hilo Polisi na kufanya hivyo kwenye kituo cha Polisi cha Oysterbay na kurejea nyumbani kwake na askari ambao walifukua shimo hilo wakakuta miili hiyo.

Baada ya miili hiyo kuopolewa shimoni, polisi walimwita Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, ambaye aliwapekua watoto hao na kubaini wameviringwa khanga nyingi na shuka moja lililoandikwa MSD Mwananyamala Hospital Ward 1A.

Aidha, katika moja ya khanga zilizotumika kuwaviringa maiti hao ilikuwa na nembo iliyobandikwa jina la B/0 Ruth Mtanga male 1.6 Premature – uzao wa Ruth Mtanga mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo 1.6 aliyezaliwa njiti.

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk. Kariamel Wandi, alipohojiwa kuhusu tukio hilo, aligoma katakata kulizungumzia akiahidi kuzungumza baadaye.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa polisi wameanza uchunguzi ili kubaini wahusika. Alisema pia maiti hao wamehifadhiwa katika mochari ya Mwananyamala.

Ingawa hakuna mtu au watu wanaoshukiwa hadi sasa kuhusika na tukio hilo la kutisha na kusikitisha, lakini wachunguzi wa masuala ya kijamii wanahisi kuwa mchezo huo mchafu umefanyika katika hospitali hiyo.

Kuwapo kwa shuka lenye nembo ya hospitali hiyo lakini pia khanga zilizobandikwa jina la mzazi na maelezo ya kidaktari, ni uthibitisho mwingine kuwa hospitali hiyo kwa namna fulani inahusika na tukio hilo.

Zipo pia hisia kuwa kuna kitu kinafichwa ama na watumishi au uongozi wa hospitali hiyo, kwani kwa kawaida, hata mtoto anapofariki wakati anazaliwa, kuna jinsi ya kumsitiri na si kumtupa kwa kumfukia holela kama walivyofanyiwa watoto hao.

Siku za nyuma, hospitali hiyo imekuwa na sifa mbaya zikiwamo za kunyanyasa wagonjwa, ikiwa ni pamoja na kuwatelekeza, hali ambayo ilimlazinmu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, mwaka jana kuhamisha idadi kubwa ya wauguzi.

Hili litakuwa ni doa lingine kwa hospitali hiyo ambayo ni kimbilio la wanyonge kutokana na kuwa ni hospitali ya Serikali ambayo inahudumia idadi kubwa ya wakazi wa Wilaya ya Kinondoni na hata wilaya jirani.

Hili ni tukio la kwanza la aina yake kutokea Dar es Salaam na pengine nchi nzima katika miaka ya karibuni kutokana na kugundulika ‘kaburi’ la pamoja.