Monday, August 31, 2009

Zitto: Demokrasia Chadema imenisaliti

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kabwe Zitto, amesema hofu ya demokrasia waliyokuwa nayo wazee wa chama hicho, imemlazimisha kujiondoa katika kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho japokuwa anao uhakika kuwa kama angegombea, angeshinda.

Sanjari na hilo, mwanasiasa huyo kijana pia amesema kwa kuwa nia yake ilikuwa kugombea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho na kulazimika kuchukua uamuzi huo mzito juzi kinyume na matarajio ya waliomshawishi, sasa hahitaji kuwania nafasi yoyote katika chama hicho na atabaki kuwa mjumbe wa Kamati Kuu kama Katibu wa wabunge wa chama hicho.

Akiwasiliana kwa ujumbe mfupi wa simu na gazeti hili jana Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini alikiri kuwasilisha barua ya kuondoa jina lake na kuongeza kuwa chama hicho ni kikubwa zaidi kuliko yeye. Zitto alisema ametoa jina hilo baada ya kuombwa na wazee wa chama hicho ambao wamedai kuwa wanaogopa demokrasia ikifuatwa itazaa makundi ndani ya chama hicho.

“Ni kweli, wazee wa chama wameomba hivyo, chama ni kikubwa zaidi ya Zitto kwa ajili ya umoja na mshikamano, nimetoa jina na wazee wamesema tukichagua kidemokrasia chama kitapasuka, nikubali kujitoa,” alisema Zitto.

Mbunge huyo alisema uamuzi wake huo ni kuheshimu ushauri huo wa wazee na kwamba hana mpango wowote wa kuwania nafasi nyingine ndani ya chama hicho ila ataendelea kuwa mjumbe wa Kamati Kuu kama Katibu wa wabunge wa chama hicho.

Hivi karibuni Mbunge huyo alikaririwa na vyombo mbalimbali vya habari akielezea msimamo wake kuwa hatojitoa katika kinyang’anyiro hicho na kwamba hakutumwa na mtu kuwania nafasi hiyo ili kukivuruga chama.

Hata hivyo katika kikao cha wazee wa chama hicho ambacho waliitwa wagombea wote wa nafasi hiyo akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe, ilidaiwa kuwa wazee hao walimtaka Zitto ajitoe jambo ambalo hata hivyo baada ya kikao hicho hakutaka kulizungumzia.

Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Wilbroad Slaa alikaririwa akikiri kupokea barua ya Zitto ya kutaka kuondolewa kwa jina lake ambapo ndani ya barua hiyo alitoa sababu kuwa aliamua hivyo ili kuendeleza mshikamano ndani ya chama chake.

Akitoa maoni kuhusu hatua hiyo ya Zitto, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema alitarajia mwanasiasa huyo asingefika mbali kwa ‘mbio’ zake hizo za kuwania nafasi hiyo. Mohamed alitoa sababu mbili zilizosababisha yeye kuwa na matarajio hayo kuwa kwa jinsi ‘alivyomsoma’ Zitto, aligundua kuwa hana uwezo wa kuhimili shinikizo la wazee wa chama hicho.

Sababu ya pili alisema mwanasiasa huyo wa Chadema, alionesha kutojiamini tangu mwanzoni na alikuwa akisitasita kugombea. Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni alisema, katika matarajio yake alikuwa haamini kama Zitto angerudisha fomu na kwamba baada ya kurudisha alitarajia kuwa asingefika mbali na nia yake hiyo.

Alisema pamoja na hatua hiyo, CUF itaendelea kufanya kazi na uongozi wowote wa Chadema utakaochaguliwa baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, George Mkuchika, alisema yeye hawezi kujiingiza katika siasa za Chadema kwa kuwa kila chama kinazo taratibu zake na kufafanua kuwa CCM inawaachia Chadema waendeshe chama chao kama wanavyotaka.

Friday, August 28, 2009

Kikwete ana kwa ana na Maaskofu Katoliki

-Atarajiwa kupoza mtafaruku wa Waraka
-Kanisa lasita kumwalika kuwa mgeni rasmi wa hafla

WAKATI mjadala kuhusu waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki ukipamba moto, Rais Jakaya Kikwete, leo Jumatano, anatarajiwa kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Anthony Petro Mayala (69) atakapokutana uso kwa uso na Maaskofu wote wa Kanisa hilo ambao ndio waliobariki waraka huo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, mbali ya Rais Kikwete, viongozi wastaafu akiwamo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wanatarajiwa kushiriki mazishi hayo.

Askofu Anthony Petro Mayala ambaye alifariki dunia ghafla Jumatano wiki iliyopita atazikwa leo ndani ya Kanisa Kuu la Epifania-Bugando jijini Mwanza.

Taarifa zilizopatikana wiki hii, Rais Kikwete anatarajiwa kuwasili Mwanza leo asubuhi na anatarajiwa pia kutumia fursa hiyo ambayo inaelezwa amekuwa akiitafuta “kuweka mambo sawa”, baada ya kuwapo sintofahamu kati ya Serikali yake na Chama cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza upande mmoja na Kanisa hilo lenye nguvu kubwa duniani upande mwingine.

Habari za ndani ya Kanisa Katoliki zinasema tangu baada ya Waraka wao kutoka, limekuwa halifurahishwi na mashambulizi yaliyotoka serikalini na katika CCM na kwamba kwa sababu hiyo kumekuwako na hali ya kutaka kumgomea ama kumsusa Rais Kikwete.

Dalili za mwanzo za hali hiyo ni kwamba Kanisa hilo, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, limesita kumwita Rais Kikwete kuwa mgeni rasmi katika shughuli za uchangiaji wa shule moja ya jimboni humo.

Habari za ndani zinaeleza kwamba Rais Kikwete alikuwa awe mgeni rasmi katika shughuli ya uchangiaji wa shule moja inayomilikiwa na Kanisa Katoliki lakini kutokana na kile kilichoelezwa ya kuwa ni “uzito mkubwa” ratiba ikabadilishwa na badala yake akaombwa kiongozi mmoja, mstaafu ndiye awe mgeni rasmi.

“Awali walimwalika kiongozi wa juu serikalini lakini wenzake wakasema si vyema kumtumia kiongozi huyo ambaye ni Mkatoliki na badala yake aende Rais Kikwete ambaye ni Mwislamu. Lakini kukatokea uzito mkubwa kutoka ndani ya uongozi wa Kanisa Katoliki na sasa inaelezwa bado haijaamuliwa ni nani awe mgeni rasmi japokuwa anatajwa sasa Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi,” anaeleza ofisa mmoja wa Kanisa ambaye yuko karibu na Kanisa Katoliki Dar es Salaam.

Uzito huo wa kumwalika Kikwete kuwa mgeni rasmi unaelezwa ndani ya Kanisa Katoliki kuwa unatokana na tamko la CCM kupinga matamko ya Kanisa hilo, tamko lililotanguliwa na kauli tata zilizotolewa na mwanasiasa mkongwe anayetajwa kuwa karibu na Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru.

Pamoja na ukweli kwamba CCM haijaukemea rasmi Waraka huo wa Wakatoliki, matamshi ya baadhi ya vigogo kama Mzee Kingunge yamekuwa hayapokelewi vizuri ndani ya Kanisa Katoliki nchini.

Kikikariri maamuzi ya wiki iliyopita ya Halmashauri Kuu yake, CCM, katika taarifa yake, kilionyesha wazi kutoridhishwa na Waraka huo lakini kikakwepa kuukemea, na badala yake kikaelekeza viongozi wakuu wa nchi kukutana na viongozi wa dini kurekebisha hali hiyo, huku viongozi wa Kanisa Katoliki wakionyesha wazi kutotaka kurudi nyuma.

Tamko la NEC lililotolewa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, John Chiligati lilisema: “Baada ya NEC kuzingatia Waraka wa Maaskofu, na hasa malumbano na hisia tofauti zilizojitokeza kuhusu Waraka huo, imeelekeza kwamba viongozi wakuu wa nchi wafanye mazungumzo na viongozi wa dini zote ili kutafuta njia tulivu ya kusafisha hali ya hewa na kujenga umoja na utengamano katika jamii yetu.”

Habari zinasema kwamba huenda zikatolewa kauli za kujaribu kujibu mapigo kutoka kwa wanasiasa wakati wa mazishi ya leo.

Kanisa Katoliki ni moja ya makanisa yenye mtandao mkubwa wa kisayansi duniani kote na nchini Tanzania limejikita kwa kiwango kikubwa kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.

Pamoja na kutotaja chama, Waraka wa Kanisa Katoliki ambao sasa umekuwa ukienea kwa kasi nchi nzima umekosoa kwa kiasi kikubwa utendaji wa Serikali iliyoko chini ya Chama cha Mapinduzi na kutoa ushauri mbadala unaoelezwa kukera wakubwa.

Mbali ya kuandaa Waraka huo, Kanisa hilo tayari limeanza utekelezaji wa programu yake tokea Januari mwaka huu inayoishia mwaka 2011, ikiwa na lengo la kuwaandaa waumini wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na baadaye tathmini yake baada ya uchaguzi huo.

Sehemu ya programu ya Kanisa hilo inasema: “Watu wengi wanadhani kwamba mambo ya umma si sehemu ya majukumu yetu ya kidini na kiimani, na hivyo Kanisa halipaswi kujishughulisha na mambo hayo.

“Kinyume chake Kristo anatualika kuleta mafundisho ya Mungu, maadili ya asili yetu ya kibinadamu kama tulivyoumbwa na Mungu. Tunaalikwa kuyafanya hayo yawe ndio msingi na mwanga unaoongoza maamuzi na sera zetu.”

Katika programu hiyo ya kichungaji kumeandaliwa hatua madhubuti za ufuatiliaji ambao utaanzia kwa kufanyika mikutano ya makleri na viongozi wa halmashuri walei kujadiliwa katika ngazi ya Jimbo na kupewa umuhimu unaostahili.

“Katika kazi ya kuongoza mkutano wajumbe wa CPT (Wanataaluma Wakristo) na wawakilishi wa Serikali waalikwe kutoa maelezo juu ya hali halisi pale watu wanamoishi. Inapendekezwa paundwe timu ya Jimbo kwa ajili ya ufuatiliaji wa programu hii. Katika ngazi ya Parokia programu ilenge kufundisha wanavijiji/watu mitaani na katika jumuiya ndogo ndogo ili waweze kujadili masuala yaliyomo katika programu,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa kichungaji.

Pamoja na uongozi wa juu wa Kanisa kueleza kwamba hii si mara ya kwanza kwa Kanisa Katoliki kuandaa waraka wa kuongoza waumini wake na wananchi kuhusiana na mambo muhimu, hatua ya mwaka huu imeelezwa si ya kawaida na inaashiria kuwapo kwa ombwe kubwa katika mfumo wa kiuongozi na kijamii.

Tangu Waraka huo kutolewa na kuibua mjadala mkubwa, hiyo itakuwa mara ya kwanza Rais Kikwete kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa Katoliki akiwemo Polycarp Kardinali Pengo. Watakutana ana kwa ana mjini Mwanza mjini Mwanza wakati wa mazishi ya Askofu Mayala.

Thursday, August 27, 2009

Kesi za mauaji ya Albino kuanza kusikilizwa mwezi ujao

KESI za mauaji ya albino zilizokuwa zimesitishwa kusikilizwa katika mahakama za Kahama na Shinyanga, zitaanza kusikilizwa mwezi ujao kwa siku 30 mfululizo. Hatua hiyo imekuja baada ya Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu kukamilisha utaratibu ikiwemo baadhi ya masuala yaliyochangia kusitishwa, Juni mwaka huu.

Msajili wa Mahakama Kuu, John Utamwa alisema jana kwamba ipo bajeti ya kutosha na mchakato wa malipo umekamilika kabla ya kesi hizo kuanza kusikilizwa kuanzia Septemba 7, mwaka huu. Alisema ingawa kesi hizo tano zimepangwa kusikilizwa katika siku hizo 30, lakini zisipotosha, wataongeza ili kuhakikisha kwamba zinaendeshwa kikamilifu.

“Tumejipanga kwa maana kwamba tumejiandaa vizuri,” alisema Utamwa na kuongeza kwamba wamehakikisha mambo yote muhimu ikiwemo bajeti, yanakamilika kabla ya kesi hizo kuanza.

Kesi tatu zinasikilizwa Kahama chini ya Jaji Gabriel Rwakibalira anayetoka Mwanza na kesi mbili zinasikilizwa Shinyanga na Jaji Gadi Mjemmas kutoka Dodoma.

Msajili huyo wa mahakama kuu, akizungumza na gazeti hili wiki iliyopita, alisema kesi hizo za mauaji ya albino ni miongoni mwa kesi ngumu kutokana na mazingira yake. Alitoa mfano wa viungo vya binadamu vinavyotoa harufu ambavyo hulazimika kuwasilishwa mahakamani kama vielelezo.

Waraka ni Neno la Mungu-Pengo

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema ujumbe na nyaraka mbalimbali zinazotolewa na makanisa kupitia kwa viongozi wake, wakiwamo maaskofu na mapadri kwa waumini na wananchi, si lazima zipate baraka za Serikali.

Pengo alisema hayo jana kwenye Kanisa la Kawekamo wakati akiendesha misa maalumu ya maziko ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Anthony Mayala (69) ambaye alifariki dunia wiki iliyopita kwa ugonjwa wa moyo.

Mbali ya kutoa wasifu wa Askofu Mayala kwa maelfu ya waumini na wananchi waliofurika kanisani hapo, ambaye alimwelezea kuwa kiongozi wa kiroho mwadilifu asiyekuwa na makuu, alikiri Kanisa kupoteza mtu hodari.

"Anthony ingawa amekufa akiwa kijana, amestarehe, Mungu amemstarehesha tu, alikuwa mtu mwema, sina shaka na hilo, maana nilimfahamu siku nyingi tuliishi naye," alisema.

Pengo alisema hivi sasa kuna hali ambayo inawabana viongozi wa madhehebu ya dini ambayo hailengi kuwapa uhuru wa kutekeleza wajibu wao kwa waumini na kuhoji Tanzania ya leo inaelekea wapi.

“Tunapoambiwa, maaskofu msiandike barua mpaka tuzione, tutafika wapi? Maaskofu wanapoandika barua na ujumbe kwenda kwa waumini, hutekeleza Neno la Mungu, msiwafundishe namna ya kuandika mambo ya kimungu,“ alisema Pengo.

Pengo alifananisha hali hiyo na mfumo wa kikomunisti uliokithiri katika Poland, na kwamba nchi hiyo ilifikia mahali ikaamua Ukomunisti uhubiriwe baada ya kushindwa kuizima imani ya Mungu.

“Poland waliposhindwa kuzima imani ya Mungu waliamuru Mungu ahubiriwe kutokana na imani ya ukomunisti, je Tanzania ya leo iko tofauti na hapo? Je, tunakoelekea ni wapi?” alihoji Kardinali Pengo ambaye hata hivyo alisisitiza kuwa alikuwa Mwanza kwa lengo la kufanya ibada ya maziko na hakuwa na nia ya kujiingiza kwenye ajenda za kisiasa.

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alionekana kukerwa na maneno yanayoendelea hivi sasa nchini, akiweka bayana kuwa umetokea mfumo unaokuja kwa kasi wa wananchi kulaani ufisadi na mauaji ya vikongwe na suala zima la rushwa bila kuja na njia mbadala wa utatuzi wake.

“Kila siku tunasikia mauaji ya albino, vikongwe na watu wasiokuwa na hatia, tunasikia juu ya watu wanaojihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa na malalamiko mengi katika Taifa letu hivi sasa, jambo la kusikitisha ni kuwa wote tunalalamika na kulaani matendo hayo, lakini tungekuwa tunayachukia kutoka kwenye nyoyo zetu, yasingetokea,” alifafanua.

Alisema ambacho kingefanyika ni jamii kuchukua njia mbadala za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo na si kulaumu na kulaani na akasema huenda jamii imechukua hatua hiyo kwa lengo la kujenga chuki, lakini na wao wakipata nafasi ni dhahiri watajihusisha na ufisadi na rushwa.

“Kila mtu ajiulize, hizi kelele zinapigwa kwa dhati? Maaskofu nasi tujiulize je tunapiga kelele hizo tukiwa na uhakika zinatoka nyoyoni? Ama ni kama kuwaonea wivu hao walio kwenye ufisadi kwa sababu tu hatujaipata nafasi hiyo na tukiipata tutaitumia kuwa mafisadi?,” alisema na kuitaka jamii iache mijadala ya ufisadi kwa vile inachochea hasira kwa jamii kwa kumwona kila mtu ni fisadi.

Awali kabla ya maziko, maaskofu wote 31 waliohudhuria, walifanya maandamano kuelekea kwenye uwanja wa misa ambako mwili wa marehemu uliwekwa na viongozi wakiwamo mapadri na watawa walitoa heshima za mwisho. Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) lilimtangaza rasmi Padri Renatus Nkwande ambaye alikuwa msaidizi wa Mayala kuwa Msimamizi Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza hadi hapo Papa atakapofanya uteuzi rasmi.

Akimtangaza rasmi jana mbele ya baraza hilo la maaskofu, Askofu Nestor Timanywa wa Jimbo Kuu la Bukoba alisema kuwa uteuzi huo ulianza rasmi jana na maaskofu walimtakia kila la heri kwa majukumu yake mapya.

Naye Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwasili kanisani hapo mchana, akifuatana na mkewe Mama Salma, akitoa salamu za Serikali na Taifa kwa jumla, alisema huo ni msiba mkubwa wa kitaifa kwani aliyepotea si tu kiongozi wa kiroho, bali mtu makini na mahiri wa kuliletea Taifa maendeleo, hususani katika sekta ya elimu.

Rais pia alitoa salamu maalumu kwa Kardinali Pengo akimwelezea Mayala kuwa mtu mwenye hekima, busara na ambaye hakuwa na makuu wala makeke.

Baadaye msafara wa Rais uliondoka kwenda Kanisa Kuu la Bugando na kufuatiwa msafara wa viongozi wa dini na ibada ya maziko ilifanywa kanisani hapo na Rais wa TEC, Askofu Jude Ruwa'Ichi na marehemu alizikwa ndani ya Kanisa hilo.

Viongozi mbalimbali akiwamo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri na viongozi wengine wa Serikali na wananchi walifurika kanisani hapo kumsindikiza marehemu Mayala.

Tuesday, August 25, 2009

Mh. Spika Samwel Sitta alikula kiapo


Mh. Samwel Sitta akila kiapo kuwa Spika
Kama tulivyoanza wiki iliyopita,wiki hii tena tunagusa kwenye anga za siasa. Kama umekuwa ukifuatilia kwa makini yaliyojiri wiki hii, kubwa zaidi lilikuwa suala la Mheshimiwa Spika,Samuel Sitta, kukingiwa kifua na wapinzani kutokana na kile ambacho CCM(chama chake Sitta) wamekiona kama “kuwageuka” baada ya kuruhusu masuala ya mijadala ya ufisadi iendelee bungeni.

Walimtishia kumpokonya kabisa uanachama kama asiposikiliza.
Kinadharia wanachosema CCM ni kwamba ukiwa mwanachama au mbunge kupitia CCM,basi sio haki kunyooshea vidole mambo “mbofu mbofu” yanayoweza kuwa yanaendelea ndani ya CCM. Wanadai kama kuna kutofautiana,basi mambo hayo yamalizwe katika vikao vya chama na sio mahali pa wazi kama vile bungeni.

Wao CCM wanasema ni haki yao kumhoji au kumkemea Spika kwani yeye ni mwanachama wa CCM kama walivyo wengine. Anayesema hivyo ni Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba. Kisha anasema bunge ni mali ya chama tawala cha CCM!

Je unadhani nini kinaendelea ndani ya CCM? Spika Samuel Sitta yupo sahihi? Makamba yupo Sahihi?

Monday, August 24, 2009

Wanafunzi 12 wateketea kwa moto bwenini

Wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari ya Idodi inayomilikiwa na serikali, iliyopo Tarafa ya Idodi, Iringa Vijijini mkoani Iringa, wamefariki na kuteketea kabisa kwa moto baada ya bweni walimokuwa wamelala kuangamizwa kwa moto.

Wanafunzi hao ambao ni wasichana, wamepoteza maisha usiku wa kuamkia jana baada ya chumba kimojawapo cha bweni la wasichana (Nyerere Hostel), kushika moto kisha bweni zima kuteketea.

Katika tukio hilo la kusikitisha, wanafunzi wengine 22 wamejeruhiwa, kati yao 14 wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa na wanane wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Idodi. Shule hiyo ipo katika Jimbo la Ismani linaloongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk. Oscar Gabone alithibitisha kupokea miili ya marehemu na majeruhi wa ajali hiyo ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.

Umati mkubwa wa wananchi wa Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake, mapema jana asubuhi ulifurika nje ya chumba cha kulaza wageni cha hospitali hiyo baada ya kupata taarifa za ajali hiyo na kufikishwa kwa miili ya marehemu hao ambayo hata hivyo haitambuliki baada ya kuunguzwa vibaya na moto huo.

Katika tukio hilo, wanafunzi wengine 427 walinusurika kupoteza maisha yao baada ya jitihada za walimu na wananchi waliowahi kufika katika eneo la tukio, kuanza kuvunja madirisha ili kuwawezesha wanafunzi hao kupata sehemu za kupita na hatimaye kuokoa maisha yao.

Bweni hilo lililoteketea kwa moto, lina vyumba 25 na lina uwezo wa kulaza wanafunzi 461 na kwamba wakati moto unashika chumba kimojawapo, wanafunzi hao walikuwemo kwenye bweni hilo.

Taarifa zilizothibitishwa na uongozi wa shule hiyo zimesema kulikuwepo na mifupa ya marehemu hao katika lango kubwa la kutokea na inadaiwa kuwa wanafunzi hao huenda walikufa kabla kwa kukanyagwa na wenzao katika harakati za kujiokoa.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Salum Maduhu na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Evarist Mangalla, walisema chanzo cha ajali hiyo ni moto wa mshumaa kushika godoro na kuwaka katika chumba hicho.

Kwa mujibu wa Kamanda Mangalla, mshumaa huo uliwashwa na mwanafunzi, Naomi Mnyali wakati akijisomea, lakini baadaye alipitiwa na usingizi na kuuacha ukiwaka kabla ya kushika kwenye godoro.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Kamanda huyo wa Polisi ilisema, mwanafunzi huyo alinusurika katika tukio hilo japo haikuelezwa hali yake ikoje. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mangalla aliwataja marehemu katika ajali hiyo kuwa ni Matilda Mtewele, Adelvina Kwama na Elizaberth Mtavila ambao walikuwa wanasoma Kidato cha Kwanza.

engine ni Digna Ndunguru, Chake Kuyaa, Seciliana John, Lazia Kihwele, Witness Mbilinyi na Stellah Mwigavilo waliokuwa wanasoma Kidato cha Pili. Pia wamo Falha Abdallah na Jesca Wissa waliokuwa Kidato cha Tatu na Maria Ndole wa Kidato cha Nne. Kamanda Mangalla alisema kutokana na marehemu hao kuteketea kiasi cha kutotambulika, wametumia njia nyingine kupata majina yao.

Majeruhi wa ajali hiyo mbaya ni Mwizarubi Eliasi, Lucy Sawani, Faraja Sodike, Anoda Ambali, Lela Mkuya, Prisca Melele, Evamary Carlos na Sabrina Abdulrahaman. Wengine ni Lenna Barugu, Zuhra Mazora, Veronika Nyamule, Theresia Zuvapi, Esther Zayumba, Ando Mamba, Irene Mponzi, Ares Ndaga, Lucy Luvanda, Upendo Nyamadule, Fraja Palinoo na Helena Mapunda.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza alithibitisha pia kutokea kwa vifo hivyo akiwa Iringa ambako aliwasili jana asubuhi akitokea Songea mkoani Ruvuma kikazi. “Ni kweli bweni moja katika shule ya Idodi , Iringa Vijijini, limeshika moto usiku wa kuamkia leo (jana) na wanafunzi kumi na wawili wamekufa na wengine kama ishirini na tano wamejeruhiwa.

“Niko hapa shuleni tangu asubuhi, hivi sasa tuko katika kikao na uongozi wa Mkoa, Shule na Wazazi kuzungumzia namna ya kufanya maziko,” alisema Mahiza alipozungumza kwa mara ya kwanza na gazeti hili saa 10:32 jioni.

Alisema kikao hicho ndicho kilikuwa kikijadili namna ya maziko ya wanafunzi hao 12; kama wazikwe katika kaburi moja au kila familia ikaandae mazishi yake.

Lakini baadaye, Mahiza alilieleza gazeti hili kuwa wamekubaliana kwamba maziko ya wanafunzi hao yafanyike kesho saa nane mchana shuleni hapo kwa kufuata taratibu za dini zote kubwa mbili; Kiislamu na Kikristo na uongozi wa Mkoa wa Iringa utatafuta eneo hilo la kuzikia.

Kuhusu kutambuliwa kwa marehemu wakati miili yao ilikuwa imeteketea kabisa kwa moto, Mahiza alisema, “Tumetumia kitabu cha majina ya wanafunzi kuwaita walioko hosteli, waliokuwa wamelazwa hospitali ya mkoa na wale waliokuwa katika kituo cha afya Idodi. Kwa hiyo, tukaamini kabisa wale ambao hawapo hata majumbani, ndio waliofariki.”

Mahiza, ambaye wakati akizungumza na gazeti hili, alisema Waziri wake, Profesa Jumanne Maghembe alikuwa anaingia mjini Iringa, alisema shule hiyo iliyoko takribani kilometa 108 kutoka Iringa Mjini katika barabara ya kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ni ya kata na ina wanafunzi wa kike na wa kiume.

Mwalimu wa Idodi aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema kwa kawaida wanafunzi hutakiwa kuzima taa za umeme wa jenereta ifikapo saa sita usiku, lakini limekuwa jambo la kawaida kwa wanafunzi wanaotaka kuendelea kujisomea kutumia mishumaa au taa za mafuta.

Wanafunzi zaidi ya 400 hawana mahali pa kuishi kutokana na ajali hiyo, na jana jioni, mfanyabiashara maarufu wa Iringa, Salum Abri wa Kampuni ya Asas Dairies alijitolea msaada wa mablanketi 200 na magodoro 200 ili kunusuru vijana walionusurika katika ajali hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametuma salamu za rambirambi na pole kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari ya Idodi waliothibitishwa kufariki dunia, kutokana na ajali ya moto iliyotokea shuleni hapo usiku wa kuamkia jana.

Katika salamu hizo, Waziri Mkuu alisema, kwa niaba ya serikali na kwa niaba yake binafsi, amesikitishwa na kuhuzunishwa sana na tukio hilo na vifo hivyo na kuwaomba wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu kuwa wavumilivu na wavute subira katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

litaka waliojeruhiwa katika tukio hilo watibiwe vizuri ili wapate ahueni haraka. Ajali za moto katika shule nchini zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika miaka ya karibuni, huku mojawapo ya kukumbukwa zaidi ikiwa ni iliyotokea mkoani Kilimanjaro, katika Shule ya Shauritanga wilayani Rombo mwaka 1994 na kupoteza maisha ya wasichana 43.

Friday, August 21, 2009

Shahidi kesi ya EPA aeleza akaunti ‘ilivyochakazwa’

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh bilioni tatu za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu Tanzania (BoT) inayomkabili mfanyabiashara Shaaban Maranda na wenzake watano, jana aliieleza mahakama kuwa akaunti ya Mibale Farm iliyoko katika Bank of Africa (BOA), iliyokuwa na fedha hizo, ilichotwa yote ndani ya siku tisa.

Shahidi huyo, Meneja wa Operesheni wa Benki hiyo, Ronald Msafiri (50), alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Wakurugenzi wa Kampuni ya Mibale Farm ambao ni mshitakiwa Farijala Hussein na Kiza Selemani ambaye si mshitakiwa katika kesi hiyo, walikuwa wakichota fedha hizo katika tarehe tofauti Novemba 2005 huku wakidaiwa kuingiza Sh 60,000 tu katika akaunti hiyo.

Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Stanslaus Boniface, Msafiri alidai Selemani pamoja mshitakiwa huyo walifunguliwa akaunti ya pamoja kwa jina la biashara la Mibale Farm katika benki hiyo Septemba 12, 2005 baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa katika benki hiyo.

Alidai kuwa Novemba 3, 2005 benki hiyo ilipokea ujumbe kutoka BoT ikieleza kwamba akaunti ya benki hiyo iliyoko BoT imeingiziwa fedha Sh bilioni 3.8 inayotakiwa kuingizwa kwenye akaunti ya Mibale Farm na pia benki hiyo ilipokea nakala ya barua iliyotumwa kwa kampuni hiyo iliyotoka BoT.

Novemba 7, 2005 wabia hao waliomba kuandikiwa na benki hundi ya Sh milioni 580 ambayo benki hiyo iliwaandikia na kutolewa yenye namba 029498; siku hiyo hiyo waliomba hundi nyingine ya Sh milioni 460 na kutoa fedha taslimu Sh milioni 250. Alidai Novemba 8, 2005 waliomba hundi yenye thamani ya Sh milioni 16.5, na kutoa taslimu fedha Sh milioni 1.4 na kuchukua tena Sh milioni 100.

Alidai Novemba 9, 2005, Selemani na Hussein walituma fedha kwa njia ya telegramu Sh milioni 5.7 iliyokuwa imeandikwa kwenda India kwenye Kampuni ya Lakshmi Textile Mills.

Siku hiyo hiyo, walituma tena Sh milioni 394 na kuchukua fedha taslimu Sh milioni 7. Novemba 10, 2005 walituma tena katika kampuni hiyo ya India Sh milioni 465.6 na kutoa tena tofauti Sh milioni nne na Sh milioni 50.

Mbali ya kuchukua fedha hizo, katika tarehe tofauti walichukua fedha nyingine na waliweka Sh 50,000 Novemba 23, 2005 na Sh 10,000 Desemba 3, mwaka huu, na baada ya hapo, hakukuwa na shughuli yoyote ya kibenki waliyoifanya wabia hao katika benki hiyo.

Baada ya kuona akaunti hiyo haitumiwi tena kwa kipindi kirefu, shahidi huyo alisema benki hiyo iliandika barua kwa wahusika kuwataka kutumia akaunti hiyo. Alidai hawakupata majibu yoyote na ndipo walipoamua kuifunga akaunti Mei 22, 2006 na inadaiwa Sh 77,356.21 za makato ya kibenki.

Watuhumiwa mbali na Farijala ni Rajab Maranda, maofisa wa BoT, Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Larika, wanaokabiliwa na mashitaka ya kujipatia malipo isivyo halali. Kesi hiyo inaendelea leo.

Jaji: Hukumu ya Zombe ni sahihi

Mwenyekitiwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji mstaafu Amiri Manento, amesema Mahakama Kuu ya Tanzania imetekeleza wajibu wake katika kutoa hukumu ya aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi Abdallah Zombe na wenzake wanane, na kwamba anayesema kinyume cha hukumu hiyo anakiuka Katiba ya nchi.

Aidha, alisema kwa mujibu wa Katiba, haki za binadamu zimezingatiwa, maana mahakama ndicho chombo cha juu cha kutekeleza haki hiyo na hukumu hiyo haiwezi kutenguliwa kwa namna yoyote sasa, mpaka hapo itakapoamuliwa vinginevyo na Mahakama ya Rufaa, hatua hiyo ikichukuliwa.

“Mahakama imeshatoa uamuzi, hakuna anayeweza kuongeza hapo wala kupunguza, hakuna mwingine anayeweza kusema tofauti ya hukumu hiyo na ikatekelezeka na kama atatokea, atakuwa anakiuka Katiba,” alisema Jaji Manento ambaye alikuwa akifafanua Kifungu cha 107 (A) (1) cha Katiba.

Jaji Manento alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, waliomtaka afafanue mara baada ya kufungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Haki za Binadamu na Biashara, kwa viongozi wa kampuni na asasi mbalimbali nchini.

Akifafanua kifungu hicho, pamoja na mambo mengine, alisema kinaeleza kuwa mahakama ndiyo mamlaka ya juu inayohakikisha haki za binadamu zinapatikana na inatekeleza hilo kwa misingi ya Katiba ambayo ni sheria mama.

Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho, mahakama ikishatoa uamuzi, hakuna wa kuongeza wala kupunguza na akitokea mtu mwingine kutoa hukumu kinyume na iliyotolewa mahakamani si sahihi, kwa kuwa mahakama imetekeleza wajibu wake na haijafanya kitu nje ya sheria zilizopo.

Kuhusu malalamiko ya wananchi hasa ndugu wa wafanyabiashara waliouawa Januari 14, 2006, Jaji Manento alisema amesoma kwenye magazeti kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ameonesha nia ya kukata rufaa, ambayo alisema ndiyo njia sahihi ya kuendeleza haki za binadamu na si vinginevyo.

Alisema katika Mahakama ya Rufaa, kesi itasikilizwa na majaji watatu na si mmoja kama ilivyokuwa katika Mahakama Kuu na kuongeza, kuwa kinachofanyika si kumpinga Jaji aliyetoa hukumu, bali ni kupitia kesi kwa mara nyingine.

Hata hivyo, alisema wananchi wanaolalamika, wana haki ya kufanya hivyo, kwa kuwa wanatekeleza moja ya haki za msingi za mwanadamu za kujieleza na kusikilizwa, ili mradi havunji sheria za nchi, lakini akawataka wananchi waheshimu uamuzi wa mahakama.

Aidha alisema kwa misingi ya maadili ya ujaji, haruhusiwi kudadavua hukumu iliyotolewa na Jaji mwenzake, hata kama ingekuwa na upungufu na kuwaonya baadhi ya watu wenye nafasi kama hiyo, kuwa macho wasije kukiuka maadili ya kazi.

Zombe na wenzake waliachiwa huru na Mahakama Kuu, Dar es Salaam Jumatatu wiki hii baada ya Jaji Salum Massati kueleza kuwa watuhumiwa hao wameonekana hawana hatia huku akiwataka waendesha mashtaka kuwatafuta watuhumiwa wawili (Saad na James) ambao walitajwa kuhusika moja kwa moja kuwapiga risasi wafanyabiashara hao.

Wafanyabiashara waliouawa katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, Kinondoni, Dar es Salaam Januari 14,2006 ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi, Mathias Lung’ombe na dereva teksi wa Manzese, Dar es Salaam, Juma Ndugu.

Kutoka Ulanga, John Nditi anaripoti kuwa wanakijiji cha Ipango, wanakusudia kufanya maandamano ya amani hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo kutoa kilio chao juu ya kuachiwa huru kwa washtakiwa hao. Kutokana na uzito wa jambo hilo, Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ulanga ilitarajia kukutana jana katika kikao cha kawaida na kuingiza ajenda ya hali ya kisiasa kuhusu hukumu hiyo kwa kuwaita viongozi wa matawi wa Ipango na wa kata ya Mahenge ili kujadiliana.

Pamoja na msimamo wa wanakijiji hao wa kufanya maandamano, ndugu wawili wa kiume wa familia ya Chigumbi, Selestin na Franco, kwa nyakati tofauti walisema familia yao haijaridhika na hukumu.

Hata hivyo walisema familia iko tayari kuungana na Serikali kukata rufaa ya kupinga hukumu hiyo licha ya familia kukosa uwezo wa kifedha na kuwaomba wananchi kuwaunga mkono.

Naye Mzee Lunkombe, ambaye ni mzazi wa marehemu Mathias alisema ni mapema kuzungumzia hatua familia inayotaka kuchukua baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo. Ofisa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Ipango, Festo Uyalo, alisema moyo wa kujitolea kwa wananchi wa kijiji hicho baada ya hukumu hiyo umekufa.

Pamoja na kukusudia kufanya maandamano hayo, wanachama wa CCM wamesusa fomu za uongozi wa serikali za vitongoji na vijiji unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu na uchaguzi mkuu wa 2010 kwa madai kuwa serikali imewanyima haki.

Katibu wa tawi la CCM Ipango, Pacienci Lyahera, alithibitisha baadhi ya wanaCCM wa kijiji hicho kurudisha fomu walizochukua kuomba uongozi kupitia chama hicho ingawa hakutaja idadi yao, lakini hali haiko hivyo katika sehemu zote kwa mujibu wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Ulanga, Leticia Mtimba.

Hata hivyo alikiri kwamba eneo la kijiji cha Ipango, ambako ndiko kwao marehemu, upo ushawishi wa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kwa wananchi kuugomea uchaguzi huo wa Serikali za mitaa hasa kwa upande wa CCM.

Thursday, August 20, 2009

Kikwete amtega Spika Sitta

-Amweka kwenye kipindi cha majaribio
-Mengi naye aguswa ndani ya NEC
-Ya Mkapa yawatisha wajumbe

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amemtega Spika Samuel Sitta ambaye ana muda hadi Novemba mwaka huu kujirekebisha, Raia Mwema imeambiwa.

Mtego huo ambao kwa upande mmoja unapalilia zaidi mpasuko wa ndani baina ya kundi la Sitta na jingine ambalo yeye amekuwa akidai linamtafuta, ulihitimishwa juzi pale Sitta alipotakiwa kujitetea ili asinyang’anywe kadi ya uanachama hatua ambayo dhahiri ingeshusha kila aina ya ndoto aliyonayo.

Baadhi ya wana CCM waliozungumza na Raia Mwema wakirejea Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ulioanza mwishoni mwa wiki iliyopita wanasema mbali na kumpatiliza Sitta, Kikwete pia aliruhusu kutikiswa kwa mtu wa karibu na Sitta, mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi, ambaye kama Sitta, amekuwa akisema kwamba yumo katika vita dhidi ya ufisadi ili kumsaidia Rais Kikwete anayeiongoza.

Habari za ndani ya CCM kutoka katika vikao rasmi na visivyo rasmi, zinaeleza kwamba Rais Kikwete ameamua, kutumia mtindo wa “kuuma na kupuliza” kwa marafiki zake, Sitta na Mengi kwa kuruhusu mjadala kwenda katika mpangilio ulioandaliwa mahususi kwa ajili ya ‘kuwashughulikia’ Sitta na Mengi, na kwa maana hiyo kundi la wabunge ambalo limekuwa likijitambulisha na Sitta.

Taarifa za ndani zinasema, katika kikao hicho, mbali ya Sitta kujadiliwa, mmoja wa wabunge alibanwa kwa kumshirikisha Mengi katika shughuli za CCM ikidaiwa kwamba mfanyabisahara huyo si mwana CCM.

Hata hivyo, habari zinasema kwamba pamoja na Mengi kuwa mwana CCM na mtu anayekisaidia chama hicho kwa muda mrefu, mfanyabiashara huyo amekuwa karibu na Rais Kikwete na amekuwa akimtaja na kumsifia Rais hadharani.

“Karibu wajumbe 40 walizungumza dhidi ya Sitta. Walikuwa wakitoa wito afukuzwe kwa jinsi anavyoliendesha Bunge ambalo katika siku za karibuni limekuwa likiibana sana Serikali.

“Aliomba sana msamaha, lakini dhahiri hakuna hata mmoja aliyekuwa akimsikiliza, hata wachache waliojaribu kumuunga mkono walizomewa wasiweze kuendelea kusema lolote.

“Kwa hiyo kwa sasa ni kama Sitta yupo katika kipindi cha majaribio. Hatima yake itategemeana na jinsi anavyoliendesha Bunge kati ya sasa na Novemba. Hiyo kamati iliyoundwa imepewa mwanya wa kuitisha kikao cha dharura kama itaona kuwa anakwenda ndivyo sivyo,” anasema mmoja wa wajumbe wa NEC aliyezungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kuwa hatajwi kama chanzo cha habari hii.

Mjumbe mwingine aliiambia Raia Mwema kwamba pengine msumari wa mwisho katika jeneza la Sitta utakuwa umepigiliwa na mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alimsema Sitta kwamba japo amekuwa akidai kwamba anaendesha Bunge kwa mtindo wa Uingereza (Jumuiya ya Madola), uendeshaji wake haukuwa sawa na huo wa Uingereza.

“Kwanza Ngombale alichanachana Waraka wa Wakatoliki akidai ni ilani ya kisiasa na kwamba haiwezekani nchi ikawa na ilani zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kisha akamrukia Sitta.

Yalizungumzwa mengi, pamoja na kumtetea Mkapa (Benjamin) na wapo walioonya kwamba kwa kuruhusu Mkapa kukwaruzwa, Kikwete alikuwa anaandaa kaburi lake mwenyewe,” anasema mjumbe huyo.

Lakini mjumbe mwingine, mfuasi wa kundi moja kati ya makubwa yanayopingana kwa sasa ndani ya CCM ameiambia Raia Mwema hata hivyo kwamba msimamo wa Kikwete katika suala la Sitta unaweza usiwe na maslahi makubwa kwa chama siku za usoni.

“Kikwete anaonekana hataki kuwaudhi marafiki zake wote wakiwamo hata wale ambao alionekana kuwatosa kutokana na kuhusishwa kwao na kashfa mbalimbali ambazo Sitta na kundi lake wamekuwa wakizisemea. Nadhani alipaswa kuwa na msimamo wa wazi katika hili maana linahusu mustakabali wake kisiasa na wa chama chetu.

“Sasa wananchi wana uelewa kuliko wakati mwingine wowote na kwamba mwaka mmoja si mbali kuelekea kwenye uchaguzi mwingine na hii ni hatari sana kama hakutatokea jambo lolote zito,” alisema mwanasiasa huyo katika mazungumzo ya simu kutoka Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao hivyo.

Soma zaidi

Wednesday, August 19, 2009

Watakaokiuka maadili CCM kutimuliwa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitasita kuwavua uongozi na hata kuwafukuza wanachama wake watakaovunja maadili, imeelezwa. Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati alisema NEC imekemea tabia iliyoanza kujitokeza katika Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa wabunge na wajumbe wa CCM.

Alisema siku za karibuni kuliibuka tabia ya baadhi ya wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wa CCM kutoa matamshi hadharani yenye mwelekeo wa kuchafuliana majina na yanayoashiria kuvunjika kwa umoja na mshikamano ndani ya CCM na serikali zote.

Alisema hivi sasa Bunge la Tanzania na Baraza la Wawakilishi hali imekuwa mbaya kati ya wabunge na mawaziri kujibizana na kutoleana lugha kali na kutishana mpaka wengine kufikia hatua ya kuomba kuongezwa ulinzi.

“Viongozi watakaovunja maadili haya watakuwa wamejibainisha kwamba hawana nia njema na CCM na watahesabiwa ni wasaliti wa chama na hivyo chama hakitasita kuwapa adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa uongozi na hata kufukuzwa katika chama,” alisisitiza.

Alisema hali hiyo inatokana na kutambua matatizo ya matamshi na vitendo visivyoridhisha katika Bunge na Baraza la Wawakilishi, hivyo kuwapo haja ya kutafuta undani wa matatizo hayo na kupendekeza kwa Kamati Kuu njia za kuyatatua.

Chiligati alisema kamati hiyo itaongozwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi na kuwataja wajumbe wengine kuwa ni pamoja na aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara na aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana ambaye aliwahi pia kuwa waziri.

Kamati hiyo pia itaangalia utendaji kazi wa kamati za chama bungeni na katika Baraza la Wawakilishi, kwa nia ya kubaini upungufu uliopo ili kupendekeza kwa njia za kurekebisha upungufu huo. Chiligati alisema pia itaangalia uendeshaji wa shughuli za Bunge na Baraza na kushauri namna ya kuimarisha panapostahili.

Alilifananisha Bunge na kikundi cha Orijino Komedi, ambapo ukifika muda wake, watu wanawahi televisheni kuangalia nani atamnyooshea mwenziwe vidole. Aliongeza: “Matamshi haya yana mwelekeo wa kudhoofisha Muungano wetu, Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na kukemea tabia hii pia imetoa maagizo”.

Aliyataja maagizo hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa CCM kurejea katika nidhamu ya chama na kuzungumzia masuala ya chama katika vikao rasmi na si vinginevyo, kamati za wabunge wa CCM na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa CCM kutumika kujadili masuala yahusuyo chama ndani ya vyombo hivyo.

Alisema pia NEC imeziagiza Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kutumia taratibu zilizopo kushughulikia kero za Muungano badala ya kufanya suala la mafuta kuwa la upande wa Zanzibar.

Alisema NEC pia ilionya kuhusu dhana inayojengeka kwamba vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini, inahusu kundi dogo la wanachama wa CCM na kwamba usahihi juu ya suala hilo, ni kuwa vita hiyo ni ya wana CCM wote, kwa mujibu wa Katiba ya chama na ni lazima iendelee kuhusisha wanachama wote wenye mapenzi mema na nchi.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini, Chiligati alisema hali ni shwari isipokuwa malumbano yanayosababishwa na viongozi wachache wa ngazi za juu ndiyo yamekuwa yakitishia amani. “Inashangaza viongozi hawa wa kisiasa wa ngazi za juu badala ya kuwa mfano katika uongozi wao, ndio wanakuwa wa kwanza kuanzisha malumbano,” alisema Chiligati.

Wakati huo huo, NEC ilisikitishwa na hali iliyojitokeza bungeni ya kutoa maneno ya kejeli dhidi ya Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Chiligati alisema Mkapa katika kipindi chake, aliliongoza Taifa kwa ufanisi mkubwa kwa kuwa aliinua hali ya uchumi, aliendeleza miundombinu, huduma za kijamii hususan elimu, afya, maji na kulijengea heshima Taifa.

Alisema Mkapa anastahili pongezi si kejeli, anastahili heshima na si dharau na anastahili kuenziwa na si matusi na aliongeza kuwa kwa kuzingatia hayo, NEC iliwataka watanzania wote wenye nia njema na nchi, waache kumchafua na kumkejeli Mkapa na badala yake wampe heshima anayostahili na aachwe apumzike. Jana Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliripotiwa kunusurika kunyang’anywa kadi yake ya uanachama na NEC, baada ya baadhi ya wajumbe kudai kuwa anakigawa chama hicho.

Mtoto wa kike


Mtoto huyu anatakiwa akitoka shuleni tu achote maji na kufanya shughuli zingine za nyumbani kama kufua nguo za zake, za kaka zake na kisha apike, atasoma saa ngapi?

Picha na:
mjengwa.blogspot.com

Tuesday, August 18, 2009

Kesi za Epa zaahirishwa Kisutu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ililazimika kuahirisha kusikiliza kesi ya wizi wa zaidi ya Sh bilioni tatu za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu Tanzania (BoT) kutokana na mawakili kuwa Mahakama Kuu kwenye hukumu ya Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake.

Kesi hiyo inayomkabili mfanyabiashara Rajab Maranda na wenzake iliahirishwa baada ya wakili wa upande wa utetezi, Majura Magafu kuwa kuwa katika kesi hiyo Mahakama Kuu. Iliahirishwa baada ya kupokea taarifa hiyo kutoka kwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Boniface Stanislaus na imepangwa kuanza kusikilizwa leo mbele ya jopo la mahakimu Samwel Kirua na wenzake.

Mbali na Maranda, washitakiwa wengine ni Hussein Farijala, Ajay Somay na maofisa wa BoT, Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Larika.

Washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuiba Sh bilioni 3.8 kutoka BoT baada ya kughushi mkataba wa makubaliano wa kuhamishiwa deni na Kampuni ya Lakshimi Textile Co. Ltd ya India kwenda kwenye Kampuni ya washitakiwa hao ya Mibare Farm. Kati ya Januari 18 na Novemba 3, 2005, kinyume cha kifungu namba 384 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, walikula njama ya wizi wa fedha kutoka BoT.

Wanadaiwa kughushi hati ya usajili yenye namba 46218 na kuonesha kuwa zimesainiwa na kutolewa na Msajili wa Biashara kwa Kampuni ya Mibare Farm wakati si kweli. Washitakiwa Farijala, Maranda, Somani, Mwaposya, Komu na Kalika inadaiwa kuwa waliiba fedha hizo baada kudanganya kuwa imepewa deni na Kampuni ya Textile Mills Ltd ya India na kujipatia ingizo hilo.

Zombe na wenzake washinda kesi

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wanane waliokuwa wanashitakiwa kwa mauaji, wameachiwa huru na mahakama kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kupeleka ushahidi usio na mashaka kuthibitisha kushiriki kwao katika kufanya mauaji hayo.

Walioachiwa huru na Zombe ni Mrakibu wa Polisi (SP), Christopher Bageni, Mrakibu Msaidizi (ASP) Ahmed Makele, Konstebo Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula. Wengine ni Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.

Jaji Salum Massati katika hukumu yake aliyoitoa jana, alisema mahakama imeridhika kuwa wafanyabiashara watatu na dereva teksi waliuawa kwa risasi huko kwenye msitu wa Pande, Mbezi Dar es Salaam; lakini waliofanya mauaji hayo hawapo mahakamani.

Alisema upande wa mashitaka unapaswa kuendelea kuwatafuta na kuwakamata wale waliowaua; kwani walioko mahakamani hakuna ushahidi unaoonesha kuwa ndio waliofyatua risasi na kuwaua watu hao wanne.

“Wapo walioua ila hawapo mahakamani, polisi watafuteni waletwe mahakamani,” alisema Jaji Massati katika hukumu ambayo iliduwaza umati uliofurika mahakamani hapo. Jaji Massati alisema kitendo cha upande wa mashitaka kuegemea kwenye maelezo ya washitakiwa Rashid Lema na Koplo Rajabu Bakari hauwezi kuishawishi mahakama hiyo iwatie hatiani washitakiwa hao.

Lema alikufa wakati kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa. Alisema pamoja na kuwepo ripoti ya daktari inayoonesha marehemu kuuawa kwa kupigwa risasi, mahakama haiwezi kujiridhisha kuwa ni washitakiwa ndio waliofyatua risasi na kuwaua marehemu hao wakati ushahidi wa kuhusika kwao haupo.

Hukumu hiyo iliyosomwa kwa zaidi ya saa tano kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:25 alasiri, Jaji alikubaliana na hoja ya upande wa utetezi kuwa upande wa mashitaka walifanya upelelezi wa kesi hiyo haraka na kuwaacha wauaji wakiwa nje.

Akimchambua mshitakiwa wa kwanza Zombe, Jaji alisema mshitakiwa huyo wakati wa mauaji yanafanyika alikuwa ndiye Kamanda wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi; hivyo alikuwa na jukumu la kujua wahalifu hao walikohifadhiwa baada ya kukamatwa.

Alisema hata baada ya kusikia mauaji yametokea, Zombe hakuonesha nia ya kwenda kuona ambako ilidaiwa kulikuwa na mapambano kati ya polisi na majambazi badala yake alienda Kituo cha Polisi kuulizia fedha. “Hapa ni wazi kuwa ni kweli alijua kilichokuwa kinaendelea, lakini hata hivyo upande wa mashitaka umeshindwa kuonesha namna mshitakiwa huyu alivyoshiriki kwenye mauaji hayo,” alisema Jaji Massati.

Alikataa baadhi ya ushahidi uliotolewa kuwa Zombe aliwafundisha wenzake cha kujitetea kwenye Tume ya Jaji Kipenka Mussa. Lakini pia alisema madai kuwa Zombe siku ya tukio alikuwa anawasiliana na Bageni hazikuwa za kweli.

Kwa upande wa Bageni, Jaji Massati alisema licha ya kuwepo ushahidi wa kuongoza msafara hadi kwenye msitu wa Pande, na kutajwa na washitakiwa wawili kuwa ndiye aliyeamuru Koplo Saad afyatue risasi, ushahidi huo haukuungwa mkono na shahidi mwingine hivyo hauwezi kukubaliwa na mahakama.

“Kwa hali hiyo ushahidi wa namna hii hauwezi kukubalika kisheria, ni lazima uungwe mkono na mashahidi wengine jambo ambalo upande wa mashitaka walishindwa kulitimiza; hivyo nasema hana hatia juu ya kesi ya mauaji,” alisema.

Akimwelezea Mrakibu Msaidizi wa Polisi Ahmed Makelle, Jaji Massati alisema ushahidi uliopo mahakamani unathibitisha kuwa alikuwepo wakati washitakiwa wanakamatwa na alishiriki kuchukua mfuko uliokuwa na fedha.

Alisema kwa Ofisa Mwandamizi wa Polisi kama Makelle, alikuwa na wajibu wa kuchukua kielelezo hicho na kukihifadhi, lakini akasema kuwepo kwake pale hakuwezi kumtia hatiani kuwa alishiriki kwenye mauaji.

“Kinachomuunganisha mshitakiwa na marehemu ni hili begi la fedha, zaidi ya hapo hakuna mahali upande wa mashitaka umetoa ushahidi wa kuhusika kwake kuwaua marehemu, hivyo na yeye hana hatia,” alisema.

Pia akimwelezea Jane na Saro ambao walikuwa na Makelle siku ya tukio, Jaji Massati alisema pamoja na kuwepo eneo la tukio, lakini upande wa mashitaka haukupeleka ushahidi kama walihusika kuua.

Kwa upande wa Bakari ambaye alikuwa mshitakiwa pekee aliyekiri kuwepo eneo la tukio wakati mauaji yanafanyika, Jaji alisema mshitakiwa huyo licha ya kuungama kuwepo siku ya tukio; lakini kuna ushahidi kuwa hakushuka kwenye gari wakati mauaji yanafanyika.

Alisema alishuhudia Koplo Saadi anafyatua risasi, lakini alikataa maelezo yake aliyodai kuwa muuaji aliamriwa na Bageni. “Madai haya hayana msingi kwa namna yalivyo na yeye alisikia na hakushuhudia wakati Bageni anatoa amri hiyo,” alisema Jaji Massati.

“Huyu Saad anayetajwa hapa mahakamani hayupo, huyu ndiye anayedaiwa kuua,” alisema akimwelezea Mabula na Shonza, alisema ushahidi uliopo ni kwamba walikuwa kwenye doria siku ya tukio, lakini upande wa mashitaka haukupeleka ushahidi unaoonesha kuwa walikuwepo Pande ambako mauaji yalifanyika na kwamba walihusika kuwaua marehemu.

Akimwelezea Koplo Gwabisabi, Jaji Massati alisema hakuwepo Pande kwani siku ya tukio aliamriwa kuendesha gari la marehemu ambao walikamatwa na kushikiliwa na polisi. “Katika hali hii nashawishika kusema kuwa naye hakuhusika kwenye mauaji na wala Pande hakwenda,” alisema Jaji Massati.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Juni mwaka jana na imemalizika jana. Upande wa mashitaka uliita mashahidi 37 kuthibitisha mashitaka yao, lakini kati ya wote hao Jaji Massati alisema hakuna aliyethibitisha washitakiwa kuua.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Mugaya Mutaki alisema watawasiliana na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) wajue kama watakata rufaa ama la.

Monday, August 17, 2009

Hatma ya Zombe

JAJI wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Salum Massati, anaendelea kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake wanane.

Watu wamefurika ndani na nje ya jengo la Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kusikiliza hukumu ya kesi hiyo inayovuta hisia za wengi.

Jaji Massati anasikiliza kesi hiyo kwa sababu amekuwa akifanya hivyo tangu ianze mwaka 2006, na wakati huo alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Takribani watu 200 wapo ndani ya chumba namba moja cha mahakama hiyo, mamia wengine wapo nje.

Kwa kuzingatia idadi ya watu waliofika kusikiliza hukumu hiyo, Mahakama hiyo imeweka maspika ili kuwawezesha watu kusikia kinachoendelea ndani.

Zombe na wenzake wameshitakiwa wakidaiwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini na dereva wa teksi Januari 14 mwaka 2006 katika msitu wa Pande, Mbezi, mkoani Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi, na Mathias Lunkombe walikuwa wakazi wa Mahenge, Morogoro, dereva wa teksi, Juma Ndugu, alikuwa akiishi Dar es Salaam.

Zombe ni mshitakiwa wa kwanza kwenye kesi hiyo, amedai kuwa ametolewa kafara kama Yesu kwa kuwa maofisa ndani ya Jeshi la Polisi wanamuonea wivu.

Wazee wa Baraza wamesema, hakuna shahidi hata mmoja upande wa mashitaka aliyemtaja Zombe kwamba alihusika kuua hivyo wameshauri aachiwe huru.

Wazee hao wameishauri Mahakama Kuu iwatie hatiani washitakiwa saba kwa kuwa wamekubaliana(wazee) na upande wa mashitaka kwamba walihusika kuwaua wananchi hao.

Serikali yachambua zabuni za mikataba ya umeme

SERIKALI inaendelea na mchakato wa kuchambua zabuni kabla ya kusaini mkataba wa kuzalisha umeme zaidi nchini. Zabuni hizo zinalenga kuweka mtambo Dar es Salaam utakaozalisha megawati za umeme 100 wakati kwa upande wa Mwanza zitazalishwa megawati 60.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema jana kwamba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linaendelea na mchakato huo wa kuchambua zabuni kabla ya kutekeleza miradi hiyo itakayochukua siyo chini ya mwaka mmoja.

Ngeleja aliyekuwa akizungumza katika kipindi cha moja kwa moja cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na Televisheni ya Star, alisema hivi sasa serikali ipo katika kipindi cha kuimarisha miundombinu ya Tanesco ili kuhakikisha kuwa inatatua tatizo la upatikanaji umeme katika maeneo mbalimbali. Kwa mujibu wa Ngeleja, katika makusanyo ya kila mwezi ya Tanesco, asilimia 15 zinatumika kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shirika hilo.

Aliyataja maeneo mbalimbali ambayo serikali imeanzisha miradi kwa lengo la kuwapatia umeme wa uhakika ikiwamo Mkoa wa Ruvuma ambao katika miaka miwili ijayo, utaingizwa katika gridi ya taifa. Miradi mingine inahusisha wilaya za Bukombe, Bariadi (Shinyanga), Magu (Mwanza) na mkoani Arusha na akasisitiza kwamba miradi yote itatekelezwa.

Akisisitiza uamuzi wa serikali kuanzisha miradi hiyo, alisema utekelezaji wa miradi unaendelea kulingana na utaratibu uliopo na si kwa ajili ya kampeni kama ambavyo wengine wanachukulia.

Friday, August 14, 2009

Makamba atwishwa kuwalinda mafisadi

-Ushahidi uliommaliza waanikwa
-Ni mpasuko wa madiwani wa kinondoni

USHAHIDI uliowasilishwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, na Mbunge Halima Mdee, kuthibitisha tuhuma dhidi ya Yusuf Makamba kwamba amekuwa akimlinda Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Salum Londa, katika tuhuma za ufisadi ikiwamo ugawaji viwanja eneo la Kawe, Dar es Salaam, msingi wake ni mpasuko wa madiwani wasioridhishwa na mwenendo wa meya huyo, Raia Mwema imebaini.
Imebainika kuwa, madiwani hao waliwahi kumwandikia barua Katibu wa CCM, Wilaya ya Kinondoni na nakala yake kufikishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM- Taifa, Yusuf Makamba. Barua hiyo ni yenye kumbukumbu namba MAD/MK/01/08, ya Januari 24, mwaka 2008, inatoa ufafanuzi wa tuhuma za ubadhirifu na uongozi mbovu wa Manispaa ya Kinondoni, ikierejea barua ya awali, yenye kumbukumbu namba MAD/MK/01/08.
Inaelezwa kuwa baada ya madiwani kuchoshwa na kile kinachoelezwa kuwa ni "kumlinda" Meya Londa kwa gharama za walipa kodi wa manispaa, barua hiyo ambayo Raia Mwema imepata nakala yake, iliainisha tuhuma 10 dhidi ya Londa na kuhitimishwa kwa maelezo makali: "Kwa haya machache yanathibitisha kwamba Mstahiki Londa ameshindwa kusimamia utawala bora ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni."
Barua hiyo pia inaeleza ari ya madiwani hao kutaka kuitwa kwa Katibu wa CCM - wilaya na ngazi ya taifa ili kueleza kwa kina madhambi ya Londa ikisema; "Mheshimiwa Katibu utambue kuwa tunayo ya kuzungumza katika kikao ambacho chama mtatuita, lakini kwa haya machache yanathibitisha nani mbabaishaji."
Miongoni mwa tuhuma zilizoelezwa katika barua hiyo ni kuhusu kile kilichoelezwa kuwa; "Madiwani kugundua Halmshauri ya Manispaa ya Kinondoni imegubikwa na wizi wa mali unaotokana na vitendo vya kughushi nyaraka za malipo (payment vouchers).
"Juni, 2007, kwenye kikao cha bajeti tulipitisha kasma (fungu) ya kununua matrela 25 ya kubebea taka kwa thamani ya Sh milioni nane, kila moja baada ya zabuni kutangazwa na mshindi kupatikana. Lakini watendaji wa manispaa wakiwa na baraka za Mstahiki Londa walighushi nyaraka na kuongeza bei kutoka milioni nane hadi milioni 12. Matrekta hayo yakaagizwa tena kwa Sh milioni 15.5.
"Katika kikao cha kamati ya madiwani ya chama (CCM) Januari 7, mwaka 2008, Londa alitetea malipo hayo akidai walipwaji walisahau kuweka Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) walipowasilisha zabuni yao. Swali la kujiuliza hapa ni je, tangu lini VAT ikawa asilimia 50?''
Tuhuma nyingine inahusu ununuzi wa magari, ikidaiwa kuwa magari 15 aina ya Suzuki yalinunuliwa bila kuzingatia taratibu za ununuzi zinazotaka zabuni itangazwe kwanza na kuwa na profoma zaidi ya tatu.
Sehemu nyingine ya tuhuma katika barua hiyo inahusu uuzaji wa mali chakavu ya Manispaa ya Kinondoni na barua hiyo inaeleza; ''Mstahiki Londa aliamuru gari alilokuwa akitumia aina ya Toyota Land Cruiser GX ambalo lilikuwa kwenye orodha ya kupigwa mnada, likarabatiwe kwa kiwango cha juu kwa fedha za Manispaa na matengenezo yaligharimu Sh milioni 9, baada ya matengenezo hayo alilazimisha auziwe gari hilo kwa sh milioni 3.

Soma zaidi

Tuesday, August 11, 2009

Vijana walapo na vigogo mafisadi huisaliti jamii

WAKATI jamii ikiendelea kusukwa sukwa na mawimbi ya bahari iliyochafuka kutokana na ukinzani wa kitabaka, uonevu na ukandamizaji, vijana wa Tanzania nao sasa wanaona kumekucha kudai nafasi za uongozi wakisema wamepuuzwa na kunyanyaswa vya kutosha kwa kuitwa "Taifa la Kesho".

Lakini, pamoja na kujitambua hivyo, hawasemi wataitulizaje bahari iliyochafuka na ni vipi wataiongoza salama meli ya matumaini iliyo mikononi mwa manahodha wakongwe, bila kuzua mtafaruku.

Wakati nchi ikienda kombo kwa kukosa dira, uzalendo kuporomoka, maadili ya taifa kuyoyoma, ufisadi na rushwa kukithiri kwa kukingiwa kifua na vigogo wa Chama na Serikali; vijana wa leo ambao "sasa na kesho" yao inaangamizwa, wamekosa ubavu wa kutahadharisha; badala yake wameungana na wakongwe hao kama washika vipeperushi na mikoba ya vigogo wakati wa chaguzi za kuweka viongozi madarakani. Kama wamejiunga na uozo huu wa tabaka la machweo, nini maana sasa ya wao kudai madaraka?

Wakati nchi ikiangamia kwa kukosa sera makini, uwekezaji usiojali na uporaji wa rasilimali za taifa unaofanywa na wageni kwa kushirikiana na baadhi ya "vigogo" madarakani, na udini na ubaguzi wa kitabaka kutishia amani na utulivu nchini, vijana wamejenga tabia ya mbuni kwa kujivika taji la ukada wa vyama vya siasa, wakijiliwaza kwamba yote yanayotokea ni asali tamu. Je, vijana wa leo wamepeleka wapi ujasiri wa miaka ya 1960 na 1970, wasiweze kulaani maovu katika jamii?

Tusidanganyike, vijana wa leo wametupa zana zao za vita ya kujenga na kulinda taifa, na badala yake wamejiunga na uozo unaoangamiza jamii kwa matarajio ya kuokota ganda la muwa la jana; wakidhani kuwa hiyo ndiyo pepo inayowangojea, kana kwamba wanajiandaa kuishi ughaibuni, na kwamba hapa sio kwao.

Kama kuna mfano bora wa kuigwa na vijana, kuonyesha nguvu na nafasi yao katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini dhidi ya uozo wa wakongwe wenye kuangamiza nchi; basi, mfano huo ni ule mgomo wa vijana wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Oktoba 1966.

Kwa manufaa ya vijana wa leo nitauelezea mgomo huo, chimbuko lake, ulivyofanyika na jinsi ulivyobadilisha uwanja wa siasa na maisha ya Watanzania pamoja na fundisho tunalopata. Mmoja wa viongozi wa mgomo huo ni Spika wa sasa wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Samwel Sitta, ambaye umakini wake katika kuliongoza Bunge ni kielelezo tosha jinsi vijana wa zamani walivyopikika wakaiva, ikilinganishwa na vijana wa leo.

Februari 1966 Serikali ilichapisha Muswada kwa madhumuni ya kuanzisha Programu ya Jeshi la Kujenga Taifa [JKT] kwa lazima kwa vijana wote waliomaliza elimu ya Kidato cha Sita na Vyuo vya Elimu ya Juu kikiwamo Chuo Kikuu pekee cha Dar es Salaam.

Mpango huo, ulioendeshwa na kusimamiwa na wakufunzi wa kijeshi kutoka Israeli, uliwataka vijana kutumikia JKT kwa miaka miwili ambapo miezi sita ilikuwa kwa mafunzo ya kijeshi kambini na miezi 18 ya kutumikia Jeshi nje ya kambi kama watumishi wa umma, na kukatwa asilimia 60 ya mshahara kama mchango kwa taifa.

Soma zidi

Dk. Asha-Rose Migiro yuko juuNa Cecilia John wa Maelezo.

Naibu katibu mkuu wa umoja wa mataifa Dk. Asha Rose Migiro ameibuka kidedea katika kura za maoni za kumpendekeza Raisi mwanamke kati ya viongozi wanawake 9 Tanzania kwa asilimia 36.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Kampuni ya utafiti ya Synovate, zamani ikijulikana kama Steadman group, Aggrey Oriwo leo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es salaam wakati wa kuelezea matokeo ya kura za maoni ya wananchi kuhusu hali ya kiuchumi,kisiasa na kijamii.

Oriwo alisema kwamba Dk. Migiro alishinda kwa kiwango kikubwa dhidi ya wanawake wenzake kwa 36%, akifuatiwa na Anna Kilango Malecela 20%, Margaret Sitta 10%, Anna Tibaijuka 5%, Sophia Simba 4%, Getrude Mongela 2%,Mama Salma Kikwete 2%, na Hawa Ghasia 2%,.

Utafiti huo ulifanyika kati ya tarehe 9-17 mwezi juni mwaka huu ukihusisha wanaume ambao walikuwa 52%,na wanawake 48%, kutoka vijijini 56% ya idadi yote ya watu na mjini 44% ya idadi yote ya watu.
Aidha matokeo ya utafiti huo yametokana na maoni ya watu elfu mbili (2000) ambao walikuwa wanapatikana mikoa yote ya bara na visiwani kwa kuzingatia takwimu na idadi ya watu kama ilivyodhihirika kwenye sensa ya 2002.

Source: issamichuzi.blogspot.com

Friday, August 7, 2009

Sitta aanika majeruhi kashfa ya Richmond

-Hosea naye aligeuzia Bunge kibao
-Achunguza kamati za Shelukindo, Dk. Slaa, Zitto

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ameanika siri ya yeye kuandamwa akisema wanaomuandama wengi ni katika kundi la majeruhi wa tuhuma za ufisadi, hususan za kuhusiana na mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni tata ya Richmond Development LLC.

Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema kwa njia ya simu kutokea jimboni kwake Urambo Mashariki, mkoani Tabora, mwabzoni mwa wiki hii, Sitta alisema anaamini maadui zake kisiasa ndio wanaopandikiza tuhuma hizo ili ionekane mbele ya umma kuwa yeye ni kiongozi asiyefaa.

Katika hali inayodhihirisha kuwarushia kijembe baadhi ya wanasiasa wenzake, Sitta alisema watu wanaomuandama ni majeruhi wa msimamo mkali wa Bunge katika kupinga ufisadi akilenga moja kwa moja hasa kundi aliloliita kuwa ni 'genge' lililohusika na kampuni hewa ya Richmond.

Akijikita katika kuwaelezea watu hao, Sitta alisema: "Katika genge hili kuna watu watatu vinara. Wa kwanza ni mwanasiasa. Huyu kwa lugha ya kipolisi ni mhalifu sugu; amehusika katika uchotaji wa mabilioni kinyemela katika Commodity Import Support (CIS); amechota mabilioni kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT); na aliwahi nadhani mwaka 2004 kupewa tenda ya kuingiza mahindi kutoka nje ya nchi, na akapewa malipo ya awali na hakufanya kama ilivyotakiwa. Ni mhalifu sugu.

"Wa pili ni mwanasiasa ambaye amejipatia utajiri wa kupindukia katika hali ya maswali, yupo mwingine anajiita mfanyabiashara naye ameingia katika mkondo huo. Na kwa vigezo vya Tanzania hawa ni mabilionea.

"Tatizo hawa ni viongozi na wana-influence (nguvu kubwa ya ushawishi) na uhusiano mzuri na viongozi wengine wa kitaifa. Wamejenga mitandao ya kuiibia nchi, na wanafanikisha kazi hiyo kwa kutumia influence ya kisiasa na uhusiano kati yao na viongozi wa juu kutisha watendaji waaminifu serikalini.

"Kwa mfano, Richmond ambao ndiyo Dowans, walinunua mitambo mitatu, kwa Dola za Marekani milioni 30, wakapewa barua ya dhamana (letter of credit) na CRDB inayozidi dola milioni 30. Baadaye wakataka kuiuzia serikali mitambo hiyo kwa bilioni 69. Bunge tulitafiti bei hiyo kwa kuuliza inakouzwa na tukaambiwa mitambo mipya ni kati ya bilioni 25 na 30 na bei inaweza kupunguzwa. Tukazuia, wakachukia.

"Sasa watendaji dhaifu wamekuwa wakiwaogopa na hivyo kujikuta wakivunja sheria ili kuwaridhisha. Wamewekeza majengo katika mji wa Dubai, Afrika Kusini na Uingereza. Kinachotokea ni kwamba Bunge sasa linawanyima usingizi, linatibua mitandao yao ya wizi na ulaji, kwa hiyo lazima wawe na hasira.

"Bahati mbaya kwao, wamefuatilia rekodi yangu kiutendaji hawajakuta makosa yoyote na hivyo wamekosa pa kunibana nikiwa kama kiongozi wa Bunge linalowanyima usingizi. Wamegundua track record (utendaji kazi ) yangu ni excellent (nzuri sana). Nimekuwa Waziri wa Ujenzi na kufanikisha miradi mikubwa kama Kiwanja cha Ndege Dar es Salaam, ujenzi wa barabara ya Morogoro-Dodoma, ujenzi wa Daraja la Salender, Dar es Salaam (mwaka 1980), ujenzi wa barabara ya Makambako-Songea (1983).

"Nimesimamia ujenzi wa nyumba 252 kwa fedha za mkopo kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) na NPF (sasa NSSF). Mwaka 1988 nimekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, 1990 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, mwaka 1993 hadi 1995 nimekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, 1996 hadi 2005 nimekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kote huko hakuna ufisadi hata wa senti moja. Track record yangu ni uadilifu mtupu, wamekosa kwa kunikamata, wanahangaika sasa kupotosha ukweli," alisema Sitta.

Akijibu tuhuma zinazomhusisha kutaka gari la thamani kubwa na nyumba ya kifahari, alisema angetamani atumie usafiri hata wa 'Suzuki Vitara' lakini yeye si mwamuzi, bali jukumu hilo ni la vyombo vya usalama vinavyoamua gari gani linunuliwe ili kukidhi vigezo vyao vya ulinzi wa viongozi wa kitaifa dhidi ya changamoto za kisasa za uhalifu.

Amesema yapo magari yasiyopenyeza risasi yanayotumiwa na viongozi ambayo yamenunuliwa kwa Sh bilioni 1.2, na mwamuzi si "anayeendeshwa" bali ni vyombo vya Usalama wa Taifa, ambavyo ni lazima vifanye kazi kwa ufanisi wakati wote.

Kuhusu suala la nyumba, alisema amekuwa akiishi katika ambayo ilikimbiwa na Naibu Waziri, Dk. Makongoro Mahanga, kutokana na nyumba hiyo kuwa na mfumo wa majitaka unaopumulia ndani, na nyumba hiyo ilikuwa katika eneo la makazi ya mawaziri, jijini Dar es Salaam.

Amesema ameishi katika nyumba hiyo kwa takriban miaka minne, na baada ya Rais Jakaya Kikwete kupata taarifa hizo aliagiza ahamishwe na atafutiwe nyumba yenye hadhi yake kama kiongozi wa mhimili wa taifa (Bunge).

Aliongeza Sitta katika majibu yake kuhusu masuala hayo matatu:
"Tuanze kuzungumzia hoja ya ununuzi wa gari. Eti Spika nataka gari la kifahari. Sihusiki kabisa katika utaratibu wa kununua magari ya viongozi wa kitaifa. Nchi inaendeshwa kwa taratibu maalumu si ovyo ovyo namna hiyo, kwamba viongozi wa kitaifa wanalala na kuamkia asubuhi na kuagiza nunua gari jipya.

"Utaratibu ni kwamba kwa viongozi wa kitaifa kama Spika na wengine, anayehusika katika ununuzi wa magari ni Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye naye anazingatia maoni ya Usalama wa Taifa katika kufikia uamuzi.

Soma zaidi

Thursday, August 6, 2009

Tamasha la ukombozi wa Wanawake kimpinduzi lajaMtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP),umeandaa tamasha la ukombozi wa Wanawake katika mapinduzi kwa lengo la kuweka usawa wa jinsia kwa jamii.

Akizungumza na Waandishi wa habari hapo jana jijini dar,Mkurugenzi mtendaji wa TGNP (pichani) ,Usu Mallya alisema kuwa tamasha hilo pamoja na mambo mengine pia linalenga kuwahamasisha Wanawake kuwa na sauti ndani ya jamii.

Uchumi wa Tanzania kuimarika mwakani

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imesema hadi mapema mwakani uchumi wa nchi utakuwa umeimarika baada ya kutikiswa na msukosuko wa kifedha duniani na mfumuko wa bei.

Mchumi wa BoT, Mwigulu Mchemba, aliiambia HabariLeo jana katika viwanja vya Nane Nane Nzuguni mjini hapa, kuwa hivi sasa hali ya mfuko wa bei nchini imepungua ikilinganishwa na ilivyokuwa katika robo ya mwaka uliopita.

Mwigulu alisema mfumuko wa bei katika kipindi hicho ulisababishwa na mambo mengi ukiwamo ukame ambao ulisababisha uhaba wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

Alisema BoT imejitahidi kukabiliana na changamoto na kuongeza kuwa matarajio ya sasa ni kuhakikisha kuwa mfumuko unashuka na thamani ya sarafu itaimarika kutokana na kuimarika kwa ubadilishaji wa fedha za kigeni.

Aidha, alisema kuimarika kwa thamani ya sarafu nchini, kutaanza katika msimu wa kuanzia Julai mwaka huu ambapo mazao ya biashara yameanza kuvunwa na kuuzwa. Alisema pia katika kipindi hiki cha mwaka mpya wa fedha wafadhili kutoka nje wamekuwa wakitekeleza ahadi zao za kutoa fedha.

Kuhusu mtikisiko wa uchumi nchini, mchumi huyo aliwatoa wasiwasi Watanzania na kuongeza kuwa tayari hatua za kukabiliana na mtikisiko huo zimeshachukuliwa.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na BoT kulegeza sera ya kifedha, ili kuruhusu upatikanaji wa mikopo katika sekta binafsi na kulegeza sera ya mapato na matumizi ya serikali, ili iweze kutekeleza miradi yake ikiwamo ya barabara na maji. Alisema hali ya uchumi nchini hivi sasa ni nzuri na kuwa Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya uchumi wa nchi.

Wednesday, August 5, 2009

Madini kwa Mzungu, mashimo kwa Mtanzania!

HATA kama isingekuwa udadisi wa vyombo vya habari, hatimaye ingejulikana tu jinsi tunavyoporwa utajiri wa madini yetu kupitia mikataba mibovu yenye kufukarisha nchi.

Ingawa Serikali imejitahidi mara nyingi kuficha, na hata kupotosha kwa makusudi, ukweli juu ya jambo hili, hila hizi zimegonga mwamba kwa sababu Mtanzania wa leo sio yule wa mwaka 1947.

Katika hali ya kufadhaika juu ya siri za ufisadi huu kuendelea kufichuliwa na vyombo vya habari, serikali ilikurupuka kuandaa muswada wa habari ambao, kama ungewasilishwa bungeni na kupita, ingekuwa ni kosa la jinai kwa mwanahabari kuandika juu ya mikataba ya kibiashara ya serikali na ufisadi ambapo adhabu yake ingekuwa ni kifungo cha muda mrefu.

Madhumuni ya muswada huo ilikuwa ni kuwalinda kwa kuwakingia kifua, wahujumu wa uchumi wa taifa letu ili waweze kuvuna na kutumbua bila ya hofu kile wasichopanda.

Lakini, wakati uporaji huu wa madini ukiendelea na serikali kuvisakama vyombo vya habari eti kwa "kununua hoja [kelele] ya Wapinzani" bungeni juu ya jambo hili, uongozi wa juu wa serikali ulijaribu kujikosha kila mara, lakini bila kuchukua hatua stahili.

Wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye, pengine kwa kuona joto la uelewa wa wananchi juu ya hujuma inayofanywa, aliona bora awe upande wa [wanaolalamika] walio wengi, pale mwezi Agosti 2006, alipotamka kwa kukiri ukweli kwamba, "nchi yetu hainufaiki na mikataba ya uwekezaji wa kigeni katika sekta ya madini kutokana na kwamba, kile kidogo tunachopata ni sawa na kodi ya pango la ardhi pekee, huku wawekezaji wakikomba thamani na faida yote ya madini". Chini ya Mikataba ya sasa, wawekezaji hao wanalipa mrahaba wa asilimia tatu tu ya faida halisi.

Baada ya kuona bosi wake amevunja ukimya kwa kutoboa ukweli, Waziri Mkuu wa wakati huo, Mheshimiwa Edward Lowassa, ambaye ndiye huyo huyo aliyekuwa akizima hoja za wabunge juu ya uporaji huo bungeni, aliona aibu kuachwa nyuma, naye akakusanya ujasiri bila kupenda, akatamka kwa kutahadharisha kuwa, "kama hali hii [ya mikataba mibovu] itaruhusiwa kuendelea, katika miaka michache ijayo, Tanzania itaachiwa mashimo ardhini na mazingira yaliyoharibika kutokana na uvunaji madini usiojali".

Lakini pengine kwa hofu ya kuwaudhi waporaji hao na kwa kuwakingia kifua akasema kuwa Serikali haikuwa na mpango wa kukatisha mikataba na wawekezaji hao, kwa sababu kufanya hivyo kungeigharimu serikali kiasi kikubwa cha fidia kwa kuvunja mikataba hiyo.

Alichokuwa akiuambia Lowassa umma wa Kitanzania ni kwamba, Watanzania wavumilie kuendelea kunyonywa hadi tone la mwisho la damu kwa sababu tu viongozi wao walikwishaingia mikataba ya kipumbavu na wawekezaji matapeli.

Wakati Rais Kikwete na Waziri Mkuu Lowassa wakitahadharisha juu ya athari ya mikataba mibovu kwa jamii ya Kitanzania, mkataba mwingine, mbovu zaidi wa mgodi wa Buzwagi ulikuwa mbioni kutiwa sahihi mjini London kwa masharti yale yale ya kiporaji.

Hapo, Watanzania walianza kujiuliza: Je, kukiri udhaifu wa mikataba ya madini kwa viongozi wetu kulikuwa na dhamira njema au ilikuwa ni kulia machozi ya mamba?. Na kama ilikuwa ni dhamira njema, kwa nini Mheshimiwa Lowassa alikaa hoteli moja na Waziri Nizar Karamagi mjini London, ambamo Mkataba wa Buzwagi ulitiwa sahihi, bila yeye kumkemea?

Vitendo na kauli za viongozi wetu vinatuaminisha kwamba, kumbe enzi za karne ya 19 za mikataba ya kilaghai ya kina Karl Peters, Cecil Rhodes, Sir George Goldie na watemi wa kale – kina Mangungo wa Msovelo [Tanzania], Lobengula wa kabila la Ndebele [Zimbabwe], Premph [Kwaku Dua] [Afrika Magharibi] na wengine, zingali nasi karne ya 21!

Tunaweza kuwasamehe wafalme hao wa kale, kwa kudanganywa wakauza nchi zao kwa "zawadi" [takrima] ndogo ndogo za shanga, vioo vya kujiangalia, tumbaku, shanga na pombe, kwa sababu ya ujinga wao [kukosa shule]; lakini si hawa viongozi wetu wa leo ambao wameungana na ubepari wa kimataifa kuangamiza nchi na watu wake. Kauli zao za kujifanya kutambua matatizo ya nchi lakini wasichukue hatua kuyakomesha, ni za kisaliti na kihaini.

Wanatupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, kutupumbaza na kuuwa ujasiri wetu wa kimapinduzi kwa madai ya "kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji", wakati ukweli wanasafisha njia ya wakoloni na ukoloni kujirudia katika mazingira yetu.

Kilichowaleta wakoloni kwetu karne ya 19, ni hicho hicho kinachowaleta katika karne yetu, tena kwa kulakiwa na kutengenezewa mapito na watawala wetu, kama ilivyokuwa hapo mwanzo, wapate kuingia. Lakini ujinga wa kina Mangungo unazidiana kama tutakavyoeleza baadaye katika makala haya, Watanzania wakiongoza.

Ulaghai wa wawekezaji wa nchi za Magharibi unaweza kudhibitiwa tu na viongozi wenye maono, wasio na uchu wa utajiri na wenye kukerwa na shida na umasikini wa watu wao. Kiongozi mwenye maono hawezi kushindwa kuelewa kwamba sekta ya madini, kwa sasa, ndiyo yenye kuvutia kwa wawekezaji wa kigeni barani Afrika kuliko sekta zingine; na ndiyo ambayo, siyo tu itakayotuachia mashimo ardhini na mazingira yaliyoharibika, kama alivyobaini Mheshimiwa Lowassa miaka mitatu iliyopita [lakini bila kuchukua hatua tu], bali pia ndiyo itakayorejesha ukoloni mkongwe ili tuendelee kuporwa rasilimali zingine.

Kuthibitisha hilo tuangalie viashiria.

Afrika inakadiriwa kumiliki karibu asilimia 48 ya akiba ya madini yote duniani. Kimsingi, Afrika bado ni mzalishaji mkubwa wa mali ghafi [yakiwamo madini] kwa ajili ya viwanda vya nchi zilizoendelea.

Kwa mfano, kati ya mwaka 1970 – 1975, utafiti na uchimbaji wa mafuta barani Afrika ulichukua asilimia 54.5 ya sekta zote ambapo sekta ya madini ilichukua asilimia 20.3, na viwanda asilimia 9.6 tu. Lakini kati ya 1990 – 2002, uwekezaji katika madini ulipaa kufikia asilimia 54 wakati sekta ya mafuta iliporomoka hadi asilimia 26, na ile ya viwanda kushuka hadi asilimia 5.2 ya sekta zingine.

Kwa Tanzania, tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa, kati ya Kilometa 945,087 za mraba za nchi hii, Kilometa 886,037 za mraba zina utajiri wa madini mbalimbali, na eneo la Kilometa 59,050 lililosalia ni maji, lenye utajiri mwingine wa rasilimali.

Kwa hiyo, kama uvunaji wa madini na rasilimali zingine utaruhusiwa kwa kasi ya sasa, kwa kuwekwa mikononi mwa wawekezaji wa kigeni kwa kile kinachoitwa "kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji", muda si mrefu Tanzania itakuwa koloni la Wazungu kupitia makampuni ya kimataifa ya kuhodhi, yanayowakilisha matakwa ya nchi za Magharibi.

Licha ya utajiri mkubwa wa madini, Afrika bado ni moja ya mabara masikini sana duniani. Kwa mfano, hadi miaka ya karibuni, Angola, Botswana, Jamhuri ya Afrika ya Kati [CAR], Ghana, Liberia, Namibia, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tanzania na DRC, zilizalisha karibu asilimia 70 ya almasi yote duniani, lakini bado ni kati ya nchi masikini, zenye kutembeza "bakuli la omba omba".

Kwa madini ya dhahabu, shaba na vito vingine, Afrika inashikilia asilimia 51 ya soko la dunia, lakini haijaweza kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Kwa nini?

Tofauti na mikataba ya kilaghai ya karne ya 19, mikataba ya sasa ya madini inahusisha ndoa kati ya siasa [wanasiasa] na rushwa kubwa za kimataifa ili kuwapora wananchi haki zao.

Ni kwa sababu hii sasa tunaambiwa na viongozi wetu kwamba mikataba hiyo ni siri ya serikali wakati ni haki ya kila mwananchi kuijua. Kwa nini mikataba mingine ya kimataifa inatangazwa kwa mbwembwe na tafrija ila ya madini tu? Tofauti yake ni nini?

Vivyo hivyo, taarifa za mapato ya sekta hiyo, zenye kukinzana, zinaashiria ufisadi au kuficha ukweli. Kwa mfano, tunaambiwa, kati ya 1992 na 2000, uvunaji wa dhahabu nchini uliongezeka kwa asilimia 266.7; yaani kutoka kilo 409 hadi 15,000 ambapo uzalishaji wa almasi uliongezeka kutoka karati 67,300 hadi 354,500.

Lakini, licha ya ongezeko hilo, chini ya wawekezaji wa kigeni, sekta ya madini ilichangia asilimia 2.5 tu ya pato ghafi la Taifa, ikilinganishwa na asilimia 15 waliyochangia wachimbaji wadogo wadogo kabla ya kuenguliwa na Wazungu. Hii inaonyesha dhahiri kwamba kuna hujuma inayolindwa.

Serikali nayo, ama haina uhakika na kinachozalishwa au inaficha ukweli kwa hila. Kwa mfano, wakati Wizara ya Mipango ilisema kuwa mauzo ya madini yaliingiza dola milioni 396.1 mwaka 2002, Wizara ya Madini ilidai mauzo yalifikia dola milioni 432.3. Na wakati Wizara ya Mipango ilisema mauzo yalifikia dola milioni 491.1 mwaka 2003, Wizara ya Madini na Nishati ilidai yalikuwa dola milioni 560.2.

Tanzania ni nchi ya tatu duniani kwa uzalishaji dhahabu baada ya Afrika Kusini na Ghana, lakini inasaga meno kwa umasikini, licha ya utajiri mkubwa huo.

Kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya hujuma inayofanywa kwenye sekta ya madini, hatimaye Novemba 22, 2007, Serikali iliunda Tume ya Jaji [Mark] Bomani kuchunguza mikataba hiyo. Matokeo yake ni kuwa, "Ukishangaa la Mussa, la Firauni je?" Hapa ndipo "umangungo" [ujinga] wa Watanzania unapozidi ujinga wa watu wengine, kama inavyothibitishwa na ukweli ufuatao.

Mwaka 2008 uzalishaji dhahabu ulifikia wakia [ounces] 1,170,000. Kwa bei ya dola za Kimarekani 900 iliyotumika. Thamani ya dhahabu iliyouzwa ilikuwa dola bilioni 1,053 tu.

Na kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hulipa mrahaba [kodi] kidogo, kiwango cha asilimia tatu tu ya faida [net back value] kwa sasa, serikali ilipata [kama kweli imelipwa] dola 15,970,500 tu kutokana na uwekezaji huo!

Na kama serikali ingekubali na kuzingatia mapendekezo ya Tume ya Bomani ya kuongeza kiwango cha mrahaba kufikia asilimia 50 ya faida ya mwekezaji, kama zifanyavyo nchi zingine za Kiafrika, serikali ingeweza kujipatia dola 52,650,000, sawa na Shs. 68,445,000,000.

Ujinga wetu unajidhihirisha pale tunapokubali kudanganywa na makampuni kwamba, gharama za uzalishaji ni kubwa kiwango cha dola 445 kwa wakia. Ujinga huu umetukosesha mapato ya dola 36,680,000, sawa na Shs. 47,680,000,000 kwa mwaka 2008 pekee; ambazo zingetumika kuleta maendeleo kwa wananchi wetu.

Ujinga wetu unakwenda mbali zaidi: Wakati tumekubali kudanganywa kuwa bei ya dhahabu katika soko la dunia ni dola 900 tu kwa wakia, wanunuzi kutoka India, Pakistani na wengineo wanalipa kati ya dola 1,200 na 1,300 kwa wakia huku tukijifanya kutolijua hilo. Kwa nini? Eti tunaweka "mazingira mazuri kwa wawekezaji".

Ilivyo sasa, nchi yetu hainufaiki hata kidogo na sekta ya madini; wanaonufaika ni hawa Wazungu wanaopora utajiri wetu, na sisi kuachiwa mashimo na mazingira yaliyoharibiwa kama urithi wetu.


Simu:
0713-526972

Barua-pepe:
jmihangwa@yahoo.com

Tuesday, August 4, 2009

JK azindua Programu mpya ya Kilimo kwanza


JK akimkabidhi Mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo WAMA Mama Salma Kikwete kijitabu chenye mwongozo wa sera ya mpya ya kilimo nchini jana katika viwanja vya maonyesho ya Kilimo huko Nzuguni,nje kidogo ya mji wa Dodoma.Rais Kikwete alifungua rasmi maonyesho hayo

Monday, August 3, 2009

Siri za Meremeta kwenye Mtandao

-Serikali yatikisika, Usalama wa Taifa wafuatilia
-Nakala 100 za ripoti hiyo zaandaliwa

SAKATA la kampuni ya Meremeta Limited iliyochota Benki Kuu ya Tanzania Sh bilioni 155 na ambalo sasa serikali imetangaza kwamba inahusiana na mambo ya Usalama wa Taifa, limeingia katika hatua mpya, baada ya kuelezwa kwamba sasa ripoti kamili ya siri kuhusu ufisadi huo itaanikwa katika mtandao.

Taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya Mwanakijiji.com na jamiiforums.com imeeleza kwamba ripoti hiyo inafuatia kile ambacho kilichukuliwa kama tishio lililotolewa na mmoja wa wanachama wa mitandao hiyo kuhusu kuanika siri ya Meremeta.

Mwanachama huyo, ambaye alikuwamo ndani ya serikali wakati wa mchakato wa uanzishwaji wa Meremeta, alielezea kutoridhishwa kwake na maelezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kutaka aeleze kuhusu Meremeta; vinginevyo yeye na wenzake wataamua kufanya kazi hiyo ili kuhakikisha kuwa mjadala wa Meremeta unamalizwa.

Raia Mwema limefahamishwa kwamba tayari vyombo vya usalama vimeanza kufuatilia suala hilo na huenda kukatokea mtikisiko mkubwa serikalini baada ya kusomwa kwa ripoti hiyo.

Taarifa hizo ambazo zinaonekana kama kujichukulia majukumu mikononi, kundi la Watanzania hao limeamua kufichua siri ya "usalama wa taifa" inayohusisha kampuni hiyo ya Meremeta ambayo ilianzishwa kwa kazi ya ununuzi na uchimbaji dhahabu.

Kampuni hiyo, ambayo iliandikishwa Uingereza mwaka 1997 na baadaye kufilisiwa huko huko Uingereza mwaka 2006, imezua malumbano makali bungeni hivi karibuni baada ya baadhi ya wabunge kupinga matumizi mabaya ya fedha kuhusishwa na usalama wa taifa.

Ndani ya mtandao huo imeelezwa kwamba kufichuliwa kwa kampuni hiyo kunatarajiwa siku yoyote wiki hii baada ya uchunguzi wa muda mrefu na ukusanyaji wa taarifa mbalimbali ambao umefanywa na Watanzania hao katika ushirikiano wa aina ya pekee wakiwa wametawanyika sehemu nbalimbali duniani.

Akiandika katika mtandao wake, mwanachama huyo alimwambia hivi Waziri Mkuu:

"Kwa vile suala la usalama linahusu usalama wa Taifa letu na wanaoohoji ni wabunge wa Taifa hilo ambao ni wawakilishi wetu, basi hata kama suala la Meremeta haliwezi kuwekwa hadharani (kwa kurushwa kwenye Luninga) basi Bunge lifunge macho na masikio ya nje na Wabunge wote wawe briefed wazi na moja kwa moja kuhusu Meremeta, umiliki wake na uhusiano wake na jeshi na usalama wa Taifa.

"Na endapo wabunge wataridhika, basi, tutapenda kusikia kuwa wameridhika na maelezo hayo na kama wabunge wapige kura kama wasimamizi wa serikali kuamua kama habari hizo kweli zinatishia usalama wa Taifa na kama wananchi wanapaswa kuziona."

Maelezo ndani ya mtandao huo yameeleza kwamba tangu ombi hilo litolewe hakuna dalili yoyote ya serikali kuwa wazi juu ya Meremeta na kuwalazimu Watanzania hao kuunganisha nguvu zao na raslimali zao kufanya utafiti wa kina wa suala zima la Meremeta.

Soma zaidi

JK na Msajili wa Mahakama ya Rufani na Majaji wa Mahakama kuu wapya


JK akila pozi na Majaji wa Mahakama Kuu 10 wapya na Msajili wa Mahakama ya Rufaa baada ya kuwaapisha jioni hii Ikulu Dar.
Toka shoto mbele ni Wah. Majaji Hamisa Hamisi Kalombola,Fatuma Hamisi Massengi, JK, Pelaggia Barnabas Khaday na Frederica William Mgaya.

Wengine nyuma toka shoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufaa Francis Katabazi Mutungi, Wah. Majaji Ferdinand Wambali, Eliamani Mbise, Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi,Sekela Moshi,Moses Gunga Mzuna and Prof.Ibrahim Hamisi Juma. Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu.

TAARIFA YA IKULU KUHUSU SUALA LA KAMPUNI YA RICHMOND

Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na maneno na vijembe ati kuwa kuna mkono wa Rais Jakaya Kikwete katika kutoa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura iliyopata Kampuni ya Richmond.
Kiini cha maneno hayo ni kauli za baadhi ya wanasiasa zilizopazwa sauti na baadhi ya vyombo vya habari.

Tunapenda kusema, tena kwa msisitizo, kuwa maneno hayo si ya kweli na hayana msingi wowote.
Rais hajahusika na uamuzi wa tenda hiyo kupewa kampuni ya Richmond kama vile ambavyo hakuhusika na kupewa tenda kwa kampuni za Aggreko na Alstom.

Kama mtakavyokumbuka wakati ule kampuni hizo tatu ndizo zilizopewa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura. Kampuni ya Aggreko ilipewa tenda ya kuzalisha umeme wa megawati 40 na Richmond kuzalisha megawati 105.6 pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Kampuni ya Alstom ilipewa tenda ya kuzalisha megawati 40 za umeme pale Mwanza kwa kutumia mafuta ya dizeli.

Katika uamuzi wa kupewa tenda kampuni hizo, Rais hakujihusisha, hakuhusishwa na wala hapakuwepo na sababu ya kuhusishwa au kujihusisha . Hiyo siyo kazi ya Rais. Hiyo ilikuwa ni kazi ya TANESCO na Wizara ya Nishati na Madini na ndiyo walioifanya. Hayo ndiyo matakwa ya Sheria ya Manunuzi ya Umma na ndivyo ilivyofanyika.

Katika shughuli nzima ya uteuzi kulikuwa na Kamati mbili za kushughulikia upatikanaji wa makampuni ya kutoa huduma ya mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme wa dharura. Ya kwanza ilikuwa Kamati ya Watalaamu kutoka TANESCO, Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini iliyokuwa na jukumu la kutathmini wazabuni wote waliojitokeza kuomba na kupendekeza wanaofaa kufikiriwa kupewa kazi hiyo.
Kamati ya Pili ilikuwa ni ile ya Serikali ya Majadiliano (Government Negotiating Team) iliyokuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TANESCO, Benki Kuu na Shirikisho la wenye Viwanda kuwakilisha sekta binafsi. Kamati hii ilikuwa na jukumu la kufanya majadiliano na wale waliopendekezwa na Timu ya Wataalamu na hatimaye kupendekeza anayefaa kupewa.

Kamati ya Majadiliano ilipomaliza kazi yake ilikabidhi taarifa yake Wizarani kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ndugu Arthur Mwakapugi ambaye naye akaikabidhi kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Ibrahim Msabaha kwa uamuzi. Kama tulivyokwishasema mamlaka ya uamuzi yalikuwa chini yao. Hakuna wakati wowote katika mchakato wa kuamua kampuni ipi ipewe tenda alipofikishiwa Rais kwa uamuzi wake wala kutakiwa kutoa maoni.

Mambo aliyofanya Rais

Katika suala zima la kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme, Rais alihusika katika mambo manne. Kwanza, katika kuamua TANESCO itumie mitambo ya kukodi kuzalisha umeme na Serikali igharamie ukodishaji huo.

Suala hilo lilikuwa lazima liamuliwe na yeye kwa sababu lilikuwa linahitaji Serikali kugharamia ukodishaji. Kama si hivyo lisingefikishwa kwake kwani ni jambo ambalo lingekuwa juu ya TANESCO kuamua kukodisha na kulipia. Gharama hizo hazikuwa zimepangwa katika bajeti ya serikali hivyo ilikuwa ni lazima kupata idhini ya Rais ya kutafuta hizo pesa na kuzitumia kwa ajili hiyo.

Pili, Rais alihusika katika kuzungumza na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuwaomba wakubali sehemu ya pesa waliyopanga kuipa Tanzania kama msaada kutokana na mpango wa msamaha wa madeni itumike kugharamia ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme. Walikubali, na USD 225 milioni zilitumika kukodisha mitambo ya Kampuni za Aggreko, Alstom na Richmond (ambayo baadae ikawa Dowans) na matumizi mengine ya dharura za umeme. Matumizi hayo mengine yalijumuisha pia ununuzi wa mitambo ya aina ya Watsilla ya kuzalisha megawati 100 za umeme pale Ubungo kwa kutumia gesi asilia. Mitambo hiyo imeshanunuliwa, kufungwa na tayari inazalisha umeme.

Tatu, Rais alihusika katika vikao vya Baraza la Mawaziri vilivyojadili matatizo ya upungufu mkubwa wa umeme nchini na kuamua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo. Moja ya hatua zilizoamuliwa kuchukuliwa, ni hii ya kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Katika vikao hivyo vya Baraza la Mawaziri alitoa maelekezo ya mambo ya kuzingatiwa katika zoezi zima la kupata makampuni au watu watakaotoa huduma hiyo. Hususan, Rais alisisitiza kuwa pamoja na udharura uliokuwepo Kanuni na Sheria ya Ununuzi wa Umma zizingatiwe.

Nne, Rais alikataa Kampuni ya Richmond isipewe malipo ya awali (down payment) ya USD 10 milioni na kutaka ukweli kuhusu uaminifu na ukamilifu (integrity) wa kampuni hiyo ujulikane. Rais alikataa maombi yaliyopelekwa kwake na Wizara ya Nishati na Madini ya kumuomba aagize Wizara ya Fedha, iilipe kampuni hiyo fedha hizo. Rais aliagiza Wizara ya Fedha ibaki na msimamo wake na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TANESCO wafanye mambo mawili. Kwanza, wafanye utafiti zaidi kujua undani wa Kampuni ya Richmond. Isije kuwa ni kampuni bandia wakapewa fedha wakatokomea nazo na mitambo isipatikane na hukuna namna ya kuipata kampuni wala wahusika wake. Pili aliagiza wawatake viongozi wa Kampuni ya Richmond kwanza walete mitambo, ikishafika, ndipo walipwe. Maagizo hayo ya Rais yalizingatiwa na Kampuni ya Richmond ikapewa sharti hilo. Lakini, ikashindwa kulitekeleza na kuishia kuingia mkataba na Kampuni ya Dowans iliyokuja kuleta hiyo mitambo badala yake.

Hivyo ndivyo alivyohusika Rais katika suala zima la ukodishaji wa mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwa makampuni ya Aggreko, Alstom na Richmond. Kama kweli kungekuwa na mkono wake wa upendeleo kwa Kampuni ya Richmond kupata tenda, iweje tena yeye ndiye akatae kampuni hiyo isilipwe fedha za kianzio mpaka kuifanya ishindwe kazi? Ndiyo maana tunasema maneno hayo hayana msingi, yanasemwa na watu ambao ama hawaujui ukweli au wameamua kutokusema kweli kwa makusudi kwa sababu
wanazozijua wao. Tunatoa ufafanuzi huu kuwafanya Watanzania waelewe ukweli wa mambo.

Watumishi wa Umma

Kuhusu watumishi wa Umma waliohusika na uchambuzi wa zabuni, majadiliano na uamuzi, napenda kuwahakikishia kuwa, Serikali imelishughulikia jambo hili na sasa linafikia ukingoni.

Mamlaka za nidhamu zimeangalia mambo mawili: tuhuma za rushwa na uzembe. Tuhuma za rushwa hazijathibitika mpaka sasa na tuko tayari kuchunguza zaidi. Lakini tuhuma ya uzembe imethibitika kwa ukweli kwamba Kampuni ya Richmond haikufanyiwa uchunguzi wa kina kuijua kampuni hiyo kwa undani kabla ya kuipa tenda. Due diligence haikufanywa. Kwa sababu ya makosa hayo mamlaka za nidhamu husika kwa watumishi hao zitawachukulia hatua zipasazo kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi.

Wenzetu hawa waliridhika tu na maelezo ya mwakilishi wa Kampuni ya Richmond aliyetosheleza masuala ya kuwa na mitambo ya kuweza kuzalisha megawati 105.6, mitambo ambayo itafaa kwa mfumo wetu wa umeme, itapatikana kwa wakati na umeme kuuzwa kwa bei nafuu. Ni kweli kwamba kampuni hiyo iliwashinda wazabuni wote kuhusu masharti hayo lakini walisahau msemo wa wahenga kuwa “si kila king’aacho ni dhahabu.” Naamini wangefanya uchunguzi wa kina kuhusu kampuni ya Richmond wangegundua kuwa ni ya bandia na haikuwa na uwezo wa kifedha wa kutekeleza zabuni ile. Kwa sababu ya upungufu huo hatua zipasazo za kinidhamu zitachukuliwa kwa kila mmoja kwa kiwango chake cha kuhusika.Yaani kwa uzito wa kosa lake. Kazi hiyo imeanza na inaendelea kufanyika.

Imetolewa 01 Agosti, 2009

PHILLEMON LUHANJO
IKULU,
KATIBU MKUU KIONGOZI
DAR ES SALAAM.