Wednesday, March 31, 2010

Wataka bajeti ya matatizo ya wanawake iongezwe

WANAWAKE 500 wanakufa nchini Tanzania kila mwaka, kutokana na matatizo ya ujauzito na mengineyo ya wakati wa kujifungua; na serikali imeombwa kupunguza haraka matatizo hayo.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Utu Mwanamke, Abubakar Karsan, kwenye mkutano ulioandaliwa na taasisi hiyo kwa waandishi, jijini Dar es Salaam jana.

Pia, Karsan alisema kwamba bajeti inayotengwa, kwa ajili ya kupambana na matatizo ya wanawake ni ndogo, hivyo inatakiwa iongezwe.

Alisema katika maeneo mengine wajawazito wanapofika hospitalini, hulipishwa katika baadhi ya huduma, ambazo wanatakiwa kupewa bure: Alitolea mfano wa huduma ya kuwekewa mashuka safi vitandani, kuongezewa damu, kupigwa sindano za kupunguza maumivu au kuwekewa ‘dripu’.

Karsan alitaka waandishi kuongeza kasi ya kuripoti masuala ya afya ya uzazi na fistula katika magazeti, redio na televisheni, ili kuongeza uelewa wa wananchi ; na pia kuifanya serikali itekeleze mipango yake ya muda mfupi na mrefu ya kuboresha afya ya wanawake.

Mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Utu Mwanamke, Christine Matovu, alisema taasisi hiyo imepania kushirikiana na wadau wengine, mfano vyombo vya habari, kuhimiza uboreshaji wa afya ya uzazi na upunguzaji wa vifo vya wajawazito nchini.

Kuna vikwazo vingi vinavyochangia mjamzito kupoteza maisha wakati wa kujifungua, kama vile umbali wa kufikia huduma za dharura za uzazi, ukosefu wa fedha za maandalizi ngazi ya familia, ukosefu wa usafiri, huduma isiyo bora kwa mjamzito na ukosefu wa watumishi wenye ujuzi kwenye vituo vya kutolea huduma.

Mpendazoe ajiunga rasmi CCJ

BAADA ya Januari mwaka huu kuhojiwa na wanahabari kuhusu uvumi wa kujiunga na Chama Cha Jamii (CCJ) akakana, aliyekuwa Mbunge wa Kishapu kwa tiketi ya CCM, Fred Mpendazoe, ametangaza rasmi kujiunga na chama hicho.

Akihojiwa na gazeti hili mwanzoni mwa mwaka huu, kuhusu CCJ na uhusiano wake na viongozi wa chama hicho, Mpendazoe ambaye amekuwa pamoja na baadhi ya wabunge wakijinadi kupambana na ufisadi nchini, alisema: “Siwezi kuzungumzia mambo ya CCJ kwa sababu mimi ni CCM na huyo Mubhi (Renatus - Katibu Mkuu wa muda) si ndugu yangu na nasikia anatoka mkoa wa Mara … hata angekuwa ndugu yangu kuna tatizo? Mbona Slaa (Wilbrod) yuko Chadema na mkewe CCM na wanaishi pamoja? Kila mtu ni mtu mzima.” Aliongeza kusema yeye bado ni mwana CCM na ni mwakilishi wa watu na wanaomhusisha na CCJ wanaweza kuwa na nia yao mbaya.

Lakini akitangaza Dar es Salaam jana kuhama CCM, mbunge huyo wa zamani alisema: “Nimefuatilia kwa karibu na kusoma Katiba ya CCJ. Nimeishi kwa matumaini kwa muda mrefu, nikitarajia siku mambo yatabadilika ndani ya CCM, mpaka leo sioni dalili yoyote. Nimeona ni heri niheshimu dhamira yangu, kama Mwalimu Julius Nyerere, alivyotuasa kuwa CCM si Helena (mama yake mzazi).

”Nasononeka CCM imegeuka kimbilio la kila mwenye dhamira ya ulanguzi, CCM imepoteza maadili ya uongozi na imekuwa ngome ya mafisadi wanaotafuna utajiri wa nchi yetu.”
Aliongeza: “CCJ ni kama Yoshua aliyewapeleka Kanani. Hakuna ubishi CCM imetutoa Watanzania katika Ukoloni, imefanya kazi kubwa, imefikia kilele chake lakini nasema haiwezi tena kuwapeleka Watanzania kwenye mabadiliko ya karne hii, tunahitaji fikra na mtazamo mpya ambao haina.

CCJ ndiyo itakayotupeleka kwenye mabadiliko ya kweli na ya dhati.” Wabunge wengine wa CCM ambao walikana kuhusishwa na CCJ ni pamoja na John Shibuda (Maswa), Anthony Diallo (Ilemela) na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela). Vigogo wengine waliokana ni Mawaziri Wakuu wa zamani, John Malecela na Joseph Warioba. Naye Mubhi kwa upande wake, alikana kuwa na uhusiano na Mpendazoe, akisisitiza kuwa hata hamfahamu.

Mwenyekiti wa CCJ, Richard Kihabo alisema jana kuwa Mpendazoe amejiunga na chama chake si kwa sababu ya kutafuta cheo, bali kutoa mchango wake katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa. “Ametangaza kujiunga na chama kwa lengo la kutoa mchango wake na si kufuata cheo hapa, mtu yeyote anayetaka kujiunga na chama anaruhusiwa ili mradi asivunje sheria,” alisema. Kwa upande wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, alisema chama chake kimezisikia taarifa hizo kijuujuu, lakini kwa mujibu wa Katiba Ibara 13 (1) (a) mwanachama yeyote akijiunga na chama kingine amejivua uanachama CCM.

Alisema CCM pia inatambua kuwa ni haki ya mwanachama awe kiongozi au la, kuhama chama na kwenda kingine. “Na huyu Mpendazoe ametumia haki yake hiyo, CCM tuna wanachama zaidi ya milioni 4.6 hivyo hatotuathiri kuondoka kwake,” alisema.

Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 71, mbunge anapohama chama anapoteza moja kwa moja sifa ya kuwa mbunge. “Kwa lugha ya kibunge huwa tunaita crossing floor, hapo hupoteza ubunge na sifa zake zote,” alisema.

Alisema taarifa za Mpendazoe kujiunga CCJ wamezipata lakini si rasmi na chama chake cha awali cha CCM ndicho chenye jukumu la kutoa taarifa katika Ofisi za Bunge, kuhusu kujiondoa kwa mbunge huyo. Hata hivyo, Msekwa alipingana na hilo na kutoa mfano wa Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Mrema, ambaye akiwa mbunge wa Moshi Vijijini alihama CCM na kujiunga na NCCR-Mageuzi.

“Haikuhitajika kupelekwa taarifa, tamko alilotoa kwenye mkutano wa hadhara lilitosha kabisa kumwondolea sifa ya ubunge, hali ambayo ni sawa na hii ya Mpendazoe ambaye leo (jana) tumemsikia ametangaza mwenyewe tena hadharani kujiondoa CCM, inatosha kabisa kumwondolea sifa ya ubunge.” Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Rajab Kiravu, alisema hata kama mbunge huyo atakuwa amejiondoa na chama kilichompitisha kuridhia na jimbo kuwa wazi, nafasi hiyo haitazibwa mpaka uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, hakuwa tayari kusema lolote badala yake alimpa jukumu hilo Ofisa Habari Mwandamizi wa Bunge, Ernest Zulu, ambaye kama bosi wake, hakuwa tayari kuzungumza zaidi.

“Ninachoweza kusema hapa ni kwamba ofisi ya Bunge inasubiri barua kutoka wale waliowaletea orodha ya Wabunge ambao ni Tume ya Uchaguzi.” Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda aliyetakiwa kuzungumzia haki za mbunge anayehama chama, ikiwamo hatma ya mafao yake, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa alikuwa safarini.

“Nipo huku porini na sikusikii vizuri na nimechelewa utanisamehe.” Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alisema amepokea uamuzi wa Mpendazoe kwa mshtuko mkubwa na ataamini jambo hilo atakapoambiwa na Mpendazoe mwenyewe.

“Mpendazoe amekuwa karibu sana nami na hakuwahi kunielezea azma yake ya kuondoka CCM,” alisema Lembeli. “Kwa hali ya kawaida kuhama chama sasa hivi ni jambo zito, uamuzi wake ni sawa na mtu anayeamua kujinyonga anafikia hatua ya kufanya hivyo baada ya kuona hakuna suluhisho lingine,” alisema.

Naye Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), alisema amesikitishwa na uamuzi huo kwani ni habari mpya na ngumu kwake na hata kuelezea inakuwa ngumu. Selelii alipoulizwa kama na yeye ana nia hiyo alisema, “wapo watakaokwenda huko lakini si mimi … mimi ni mwanachama wa CCM na nitaendelea kubaki CCM hata kama si kiongozi.”

Lucy Owenya (Chadema) alisema, “kama kaamua kuhama Katiba inamruhusu…huyu anajua matatizo yaliyoko ndani ya CCM ndiyo maana kaamua kuondoka,” alisema Owenya.

Elieta Switi (CCM), alisema kuhama ndiyo maana halisi ya demokrasia, kwamba mtu habanwi kuwa katika chama kimoja na kuongeza, “kazi ni kwake huko alikokwenda, lakini nadhani yeye anaona amefanya uamuzi sahihi na ana sababu ya kufanya hivyo”.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kupitia mtandao wa kompyuta alisema ni uamuzi wa kishujaa kwamba anaweza kutoka na kujiunga na kambi ya Upinzani.

“Tunamkaribisha. Nina shaka na 'strategy (mkakati)' ya kutoka kwa kuzungumza na waandishi wa habari pale MAELEZO na si mkutano jimboni mwake maana hatakuwa mbunge tena kwa kipindi kilichobaki. “Inawezekana amenusa kitu kuwa jamaa wanamtosa, maana nimesikia kulikuwa na Kamati Kuu ya CCM,” alisema.

Kuhusu mafao, alisema hukokotolewa kwa mujibu wa muda ambao mbunge ametumikia. Hata mbunge akifariki dunia sehemu ya mafao yake hulipwa kwa familia yake.

Mbunge mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema huenda Mpendazoe amehisi kuwa hatapita katika kura za maoni CCM, kutokana na madai kuwa matajiri wameshammaliza, hivyo atapitia CCJ kuwania ubunge.

Kabla ya kuhama CCM, Mpendazoe amekuwa akikabiliwa na vitimbi mbalimbali jimboni mwake, ikiwa ni pamoja na kusambazwa vipeperushi kwenye mnada wa mifugo na mitaa ya mji mdogo wa Mhunze, wilayani Kishapu, vikimtuhumu kwa kutotimiza ahadi zake.

Baadhi ya vipeperushi vilisomeka: 'Mpendazoe ulitudanganya kuwa tukikuchagua ubunge utateuliwa kuwa Waziri, mbona hata unaibu Waziri hukuteuliwa!' 'Mpendazoe wananchi wa Kishapu hatukutaki uwe mbunge wetu, ukigombea tena 2010 tutakuaibisha!

Vingine: ‘Mpendazoe umeivuruga halmashauri ya wilaya ya Kishapu sasa unataka kukivuruga Chama Cha Mapinduzi, chunga kauli zako’. Hata hivyo akivizungumzia, alisema ni sehemu ya utekelezaji wa mafisadi kuwaondoa bungeni baadhi ya wabunge wanaopinga vitendo hivyo.

Alidai mafisadi wametenga Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuwang’oa na kuwamaliza wasisikike kabisa. Hata hivyo, alisema hatishiki na vipeperushi hivyo, kwa kuwa wanaovisambaza wamefilisika kisiasa na ni woga kwa kuwa hawajitokezi hadharani na kwenye vikao halali kutoa madukuduku yao.

Alijinasibu kuwafanyia mambo mengi wapiga kura wake na akawa na imani kuwa wananchi hao watavipuuza na kuendelea kumuunga mkono. Habari zaidi zilidai kuwa mbunge huyo alisababisha kuibuka makundi mawili jimboni mwake; linalomuunga mkono na linalompinga, huku ikidaiwa kuwa alishitakiwa kwa Spika Samuel Sitta na aliyekuwa msaidizi wake katika uchaguzi wa mwaka 2005 kwa madai ya kumdhulumu.

Katika kukanusha tuhuma hizo, Mpendazoe alikiri kufahamiana na msaidizi wake huyo na kusema alishamsaidia mambo mengi, lakini hakumlipa fedha zake kutokana na kumchafua na kutoa siri zake sehemu mbalimbali.

“Huyo bwana namjua ni ndugu yangu, ni kweli tulikuwa na makubaliano fulani ambayo mimi sijayatekeleza, lakini ameniudhi sana baada ya kuzunguka sehemu mbalimbali na kuanza kutoa siri zangu,” alikaririwa na gazeti moja nchini.

“Kote alikokwenda wamempuuza, amefika hadi kwa Spika, NEC, PCCB hadi Polisi ili kunichafua, lakini wamempuuza, sasa anatumia vitisho ili nimlipe, kwa nini?” Mpendazoe pia alituhumiwa kumtisha kwa bastola Abdulkadir Mohamedi, ambaye pia ni kada wa CCM Kishapu.

Ilidaiwa kuwa Mbunge huyo wa zamani alimshambulia Mohamedi kwa makofi, kumchania nguo na kumtishia bastola, lakini alikanusha akidai ni uongo dhidi yake wenye lengo la kumchafua kisiasa.

Monday, March 29, 2010

Tarime na mauaji ya vikongwe

AJUZA mwenye miaka kati ya 90-100 Sifia Makubo amenyofolewa miguu yake yote miwili kwa panga na sasa yupo hospitali akiwa mahtuti.

Ajuza huyo alikumbwa na mkasa huo mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Ngerengere kata ya Sirari tarafa ya Inchugu wilayani Tarime Mkoani Mara.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime /Rorya Costantine Massawe alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 27 mwaka huu na ajuza huyo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya Tarime.

Imedaiwa kwamba ukatili huo amefanyiwa na Mkazi wa kijiji cha Kubiterere ambaye hakufahamika jina lake mara moja.

Kamanda Massawe akielezea mkasa huo zaidi alisema mtuhumiwa huyo akiwa na panga alivamia nyumba ya bibi Huyo na kuanza Kumshambulia kwa Kumkata kata mapanga na kumwacha akivuja damu nyingi huku akilia kuomba msaada ,

Kamanda Massawe alisema kuwa Mjukuu wa Bibi huyo alisikia kilio cha bibi yake kuomba msaada na kuanza kupiga yowe ambapo wananchi Majirani walijitokeza mara moja na kumfukuza hadi walipomtia mikononi na kuanza kumpiga.

Mtuhumiwa huyo alikatwa panga tumboni hadi utumbo wote kutoka nje.

Polisi Kituo cha Sirari walifika waliwahi kufika kwenye kituo kumuokoa mtuhumiwa kwa kumfikisha hospitalini na ajuza huyo.

Mtuhumiwa alifariki siku hiyo hiyo na ajuza huyo bado amelazwa Wodi namba 6 kwa matibabu ya miguu yake yote Miwili na majeraha ya mkono wa kushoto.

Yona agombana na Wamarekani


-Yumo Balozi wa zamani wa Marekani Charles Stith
-Ni kuhusu mradi wa nyumba Kunduchi, Dar

FAMILIA ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona, iko katika mvutano unaomhusisha aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini, Mchungaji Charles Stith. Katika mvutano huo, Serikali ya Tanzania imeshtuka dakika za mwisho, ikishangaa na kuahidi kuchukua hatua stahili, Raia Mwema imebaini.

Mvutano huo unahusisha moja kwa moja kundi la wawekezaji wa Marekani waliokuwa tayari kuwekeza mamilioni ya dola nchini katika mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu, kwa makubaliano mahsusi na kampuni ya Yona.

Yona, ambaye kwa sasa anashitakiwa katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka alipokuwa Waziri, amejikuta katika mvutano baada ya kutaka kujitoa katika makubaliano ya uuzaji wa eneo kwa kampuni ya Kimarekani ya Enterprises Homes Tanzania Ltd (EHTL).

Kampuni ya Yona inayoitwa Devconsult International Ltd iliingia mkataba na Enterprises Homes Tanzania Ltd kuuza ardhi yenye hati namba (Plot No). 384, Block ‘A’ Kunduchi kwa bei ya Dola za Marekani 650,000 (zaidi ya Sh milioni 650).

Lengo la EHTL kwa kushirikisha wadau wengine ni kufanikisha ujenzi wa awali wa nyumba 45 za gharama nafuu, ambazo ni sehemu ya ujenzi wa nyumba nafuu mpya 5,000 utakaokamilika mwaka 2012.

Mradi huo wa aina yake unalenga kusaidia ndoto ya Serikali kuwapatia wananchi makazi bora ya gharama nafuu, lakini habari zinasema kampuni iliyokusudia kununua ardhi hiyo kwa familia ya Yona, ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba wa awali ikiwa ni pamoja na kulipa fedha kabla ya kukabidhiwa eneo husika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mfadhili wa mradi huo kupitia EHTL ni kampuni binafsi ya Marekani, Overseas Private Investment Corporation (OPIC), pamoja na taasisi nyingine za fedha zikiwamo Benki ya Eurafrican Bank na taasisi ya mikopo Ghana.

Kila nyumba ilipangwa kugharimu dola za Marekani 100,000 (zaidi ya Sh milioni 100) au pungufu ya kiwango hicho. Mkataba wa mkopo wa kuuziwa nyumba hiyo kwa mlalahoi wa Tanzania utadumu kwa miaka 15.

Hata hivyo, hivi karibuni Devconsult iliamua kujitoa katika mpango huo na hivyo kuhatarisha malengo yaliyokusudiwa, baada ya kampuni hiyo ya kina Yona kushindwa kuwashawishi wawekezaji hao kulipa fedha husika kwa mujibu wa mkataba.

Lakini pamoja na kitisho hicho, Wawekezaji wa Marekani wenye malengo hayo bado hawajakata tamaa isipokuwa wamekuwa wakifanya kampeni wakidai kwamba ni vigumu kuendesha shughuli za kiuwekezaji nchini Tanzania bila kueleza ukweli kwamba walishindwa kulipa fedha kwa wakati kama walivyokubaliana katika mkataba.

Taarifa kutoka kwa wawekezaji hao zinabainisha kuwa wana matumaini familia ya Yona itarejea katika mpango huo ili hatimaye kuufanikisha, huku kukiwa na taarifa za suala hilo sasa huenda likaingia katika mkondo wa kimahakama.

Habari zaidi zinasema kwamba mbali ya kuwa familia ya Yona kutaka kuuza eneo hilo, mmoja wa wanafamilia naye aliingizwa katika kampuni hiyo ya Wamarekani kama mwana hisa kwa nia ya kufanikisha malengo ya ujenzi wa nyumba hizo huku kukiwa na watu wengine maarufu nyuma yao.

Wakati mvutano huo ukiendelea, takwimu nchini hasa za Benki Kuu zinabainisha kuwa mahitaji ya nyumba bora Tanzania yemefikia nyumba milioni 2.

Dar es Salaam pekee, wastani wa mahitaji ya viwanja kwa ajili ya ujenzi ni 20,000 lakini uwezo wa utoaji kwa mwaka ni 700, na hivyo takriban asilimia 97 ya mahitaji hayatekelezwi.

Soma zaidi

Wednesday, March 24, 2010

Wanasiasa wataka mabilioni uchaguzi

WANASIASA wa vyama mbalimbali vya upinzani wamependekeza matumizi kwa wagombea katika kampeni za uchaguzi mkuu ziongezwe, kwa maana fedha zilizopendekezwa na Serikali ni kidogo.

Serikali ilipendekeza gharama za matumizi ya mgombea urais yasizidi Sh bilioni moja, huku ubunge na udiwani gharama zikiwa zinategemea eneo la jimbo, idadi ya watu na hali ya miundombinu.

Katika majadiliano ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi yaliyomalizika Dar es Salaam, jana, wanasiasa hao walisema gharama zilizowekwa hazilingani na hali halisi ya sasa na wala haziendani na kupanda kwa gharama za maisha mwaka hadi mwaka kutokana na sababu mbalimbali, likiwamo ongezeko la watu na ukame.

Aidha, walisema sheria hiyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho ya kina ili isilete usumbufu siku za baadaye kwa kutakiwa kubadilishwa kutokana na ongezeko la mahitaji au kupanda kwa gharama za maisha.

John Mnyika wa Chadema alisema viwango vilivyopendekezwa ni vidogo kutokana na maeneo mengine kuwa na majimbo makubwa na vituo vingi vya uchaguzi, hivyo Sh bilioni moja haitatosheleza shughuli zote za uchaguzi.

“Chadema tulifanya kampeni katika uchaguzi uliopita na tulitumia zaidi ya Sh milioni 700 na hatukuzunguka majimbo yote, hivyo Sh bilioni moja kwa sasa ni kiwango kidogo ikilinganishwa na gharama za maisha zilivyopanda, labda angalau Sh bilioni mbili au tatu,” alisema.

Alisema pamoja na viwango hivyo kuwa vidogo, lakini kinachopaswa kuangaliwa zaidi ni matumizi sahihi ya gharama ambapo pia alisema sheria hiyo imechelewa kujadiliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema ni ngumu kufanya makadirio ya gharama za uchaguzi kwa sababu kila chama kina mapendekezo yake ya jinsi ya kufanya kampeni ambapo wengine hutumia matangazo mengi kwenye vyombo vya habari na wengine magari na helikopta kufuata wananchi.

“Ni ngumu sana kufanya makadirio ya gharama za uchaguzi maana hata wananchi nao wana mtazamo tofauti, sasa hivyo mtu huwezi kuwaendea kwa miguu tu, wengine wanalazimika wakati mwingine kutumia magari na wengine helikopta,” alisema.

Alisema tatizo si fedha ila kinachopaswa kuangaliwa ni jinsi inavyotumika na kueleza kuwa wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakizitumia kununua watu na wengine kuzigawa kama njugu wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Kwa kipindi cha nyuma, tumekuwa tukivumilia uchaguzi wa aina hiyo ila kwa sasa uchaguzi wa ‘kumwaga’ fedha utadhibitiwa na wengi waliokuwa wakifanya hivi ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), maana walikuwa wanaona uongozi ni pesa,” alisema.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa, alisema uchaguzi ujao unaonekana kuwa mgumu kutokana na sheria hiyo na kueleza kwamba ingawa lengo ni kuzuia rushwa, lakini fedha hizo ni kidogo.

Aidha, wadau hao walitaka kifungu cha kuwapo kwa watu maalumu wa kampeni kubadilishwa, kutokana na kifungu kinachoonesha kwamba baada ya watu hao kutambuliwa, hatatakiwa mtu mwingine kumnadi mgombea kama si mwanakampeni.

Walisema hiyo ni kuwanyima Watanzania haki za msingi za kumnadi mgombea wanayemtaka na wakataka mgombea anapohitaji kubadilisha watu wanaomkampenia kutoomba kibali upya na badala yake kutoa taarifa tu kwa Mamlaka iliyopo.

Rais wa Tadea, John Chipaka, alisema haina haja ya kubanwa kwa fedha hiyo na badala yake wananchi wasimamie uchaguzi wenyewe na kutoa taarifa kwa wanaogawa vitenge au sukari, ili wapewe kura maana hao ndio wanaoua maendeleo ya nchi kutokana na kutorudi kuwaangalia wanapochaguliwa.

Tuesday, March 23, 2010

Sheria Gharama za Uchaguzi: Mgombea Urais matumizi mwisho bil 1/-

BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi wiki iliyopita, Serikali imependekeza matumizi kwa mgombea urais yasizidi Sh bilioni moja kuanzia kwenye mchakato wa kuteuliwa na chama hadi kampeni.

Kwa upande wa wagombea ubunge, gharama hizo zinategemea eneo la jimbo, idadi ya watu na hali ya miundombinu. Mgombea ubunge ambaye jimbo lake liko makao makuu ya mkoa ambalo watu wake ni zaidi ya 300,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 40.

Jana wadau mbalimbali zikiwamo asasi za kiraia na vyama vya siasa, walijadili rasimu hiyo ya kanuni na taratibu zitakazotumika wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, CCM haikuwakilishwa kwenye majadiliano hayo ambayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.

Kwa mgombea ambaye jimbo lake liko nje ya makao makuu ya mkoa na idadi ya watu haizidi 100,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 20 wakati kwa jimbo lenye watu ambao hawazidi 150,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 30.

Mgombea ambaye jimbo lake liko nje ya makao makuu ya mkoa na wapiga kura wake ni kati ya 150,000 na 300,000, atatumia fedha isiyozidi Sh milioni 35.

Lakini kwa mgombea ubunge katika majimbo yaliyoko kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza bila kujadili idadi ya watu, atalazimika kutumia fedha zisizozidi Sh milioni 20.

Katika mchanganuo huo pia wagombea ubunge wa Zanzibar ambao majimbo yako katika makao makuu ya mikoa na wapiga kura wanazidi 10,000 watatakiwa kutumia Sh milioni 10.
Wagombea ubunge wa Zanzibar ambao majimbo yao yako nje ya makao makuu ya mikoa na yana watu ambao hawazidi 10,000 watatumia si zaidi ya Sh milioni saba.

Kwa upande wa viti maalumu Tanzania Bara ambao wapiga kura ni zaidi ya 10,000 kiasi cha fedha kinachopendekezwa kutumiwa ni Sh milioni tatu.

Katika mpango huo wagombea udiwani katika maeneo ya mjini kiasi wanachotakiwa kutumia si zaidi ya Sh milioni saba na wale ambao kata zao ziko vijijini, matumizi yao yatatakiwa yasivuke Sh milioni 10. Wakati wagombea udiwani wa viti maalumu matumizi yao hayatakiwi kuzidi Sh milioni moja.

Kwenye rasimu hiyo ya kanuni katika kipengele kinachohusu timu ya kampeni kwa ajili ya gharama za uchaguzi, mgombea urais wajumbe hawatazidi 50, mgombea ubunge wajumbe hawatazidi 20 wakati mgombea udiwani wajumbe hawatazidi 10.

Wajumbe hao wa kampeni watatakiwa wathibitishwe baada ya mgombea kuwasilisha maombi kwenye Mamlaka iliyoamuliwa na sheria hiyo siku 10 kabla ya uteuzi au siku 10 baada ya uteuzi.

Mgombea ambaye atabadili timu yake ya kampeni, atalazimika kutuma maombi kwenye Mamlaka inayohusika kwa ajili ya mabadiliko hayo. Katika rasimu hiyo mamlaka inayohusika inaweza kukataa kufanya mabadiliko kama itaridhika kuwa mjumbe huyo hawezi kuathiri kampeni za uchaguzi.

Katika rasimu hiyo, licha ya kupendekezwa kuwa mgombea aliyepata kura nyingi kwenye chama ndiye ateuliwe na chama chake kugombea urais, ubunge na udiwani, lakini wadau walikikataa kifungu hicho.

Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, alisema kipengele hicho hakifai kwani kuna baadhi ya wagombea wanaweza kutumia fedha kurubuni wapiga kura; hivyo akapendekeza kifungu hicho kiongezwe maneno kuwa “itakapothibitika kuwa aliyeongoza alitumia rushwa basi chama kitumie taratibu zake kumpata mgombea”.

Mwenyekiti wa Chausta, James Mapalala, alisema eneo hilo ndilo msingi wa demokrasia na kama kanuni hazitasema wazi kuwa mtoa rushwa aondolewe, anaweza kuingia mtu madarakani akaharibu Taifa kwa rushwa.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alisema lazima kifungu hicho kirekebishwe, ili kuvipa vyama fursa ya kupokea malalamiko ya walioshindwa na ikithibitika kuwa aliyeshinda alitumia rushwa, aondolewe.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema utaratibu uliopo ndani ya vyama utumike. Alisema iwapo kifungu hicho kitaachwa kilivyo, CCM itasaidia wagombea wa upinzani ambao ni dhaifu, ili kushinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama.

“Tukikiacha hivi hiki kifungu vyama vingine vinaweza kupata wagombea dhaifu ambao hawauziki … na hii ndiyo kazi ya Kamati Kuu na Baraza Kuu kuchambua ni mgombea gani anakubalika anayeweza kukipa ushindi.

“Ili kutopata mgombea dhaifu, tupeni nafasi ya kurekebisha hili, wewe Msajili (wa Vyama vya Siasa) na meza yako hiyo hamna vyama, sisi ndio tunajua mambo yaliyoko ndani ya vyama vyetu, tunaomba mturudishie taratibu za kupata wagombea,” alisema Profesa Lipumba.

Msajili wa Vyama John Tendwa alikubaliana na mapendekezo ya wadau hao “hizi ni kanuni zenu na wala si za CCM. Kwa mapendekezo yenu na sisi tunakubaliana nayo,” alisema Tendwa ambaye alifuatana na Mwandishi wa Sheria, Casmir Kyuki.

Monday, March 22, 2010

Malaigwanani wamtetea Lowassa

MBUNGE wa Monduli Edward Lowassa ametetewa na wazee wa jamii ya Wamasai (Laigwanani) kuwa bado ni kiongozi wao kwani tararibu zote za kumchagua zilifuatwa ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Malaigwanani wa ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo ilisemwa na Malaigwanani kutoka katika wilaya za Mkoa wa Arusha waliofanya kikao katika kitongoji cha Nanja wilayani Monduli mkoani Arusha kutafakari hali halisi ya mwenendo wa baadhi ya Malaigwanani kutumiwa na wanasiasa kupotosha ukweli.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho Katibu wa Malaigwanani Sigit Ole Kibiriti alisema kitendo cha baadhi ya Malaigwanani kuhoji uteuzi wa Lowassa aliyeteuliwa kuwa Alaigwanani ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu.

Ole Kibiriti alisema mchakato wa kumteua Lowassa kuwa Alaigwanani ulizingatia sifa zote za mila ya jamii ya Kimasai ikiwemo upendo, huruma, unyenyekevu na mwenye kujali jamii. Sifa nyingine ni pamoja na kukubalika katika jamii kuwa Lagwanani wao na kutotiliwa shaka, uwe mtu unayeweza kukabiliana na majukumu mbalimbali ndani ya jamii na awe na uwezo wa kuwaunganisha watu unaowaongoza na pia uwe na maono ya mbali vitu ambavyo Lowassa anavyo.

''Sisi Malaigwanani wa Maa tunasikitishwa na hali hiyo na kuhoji kama kweli waliotamka ni viongozi wa Maa ama ni vibaraka? Na kama ni viongozi wa Maa kweli basi wanatumiwa na wanasiasa kuchafua mila za Kimasai pasipo kujua,'' alisema Ole Kibiriti.

Mbali ya hilo katika jamii ya Maa Kisongo ndio wenye mamlaka yote ya kimila na ndio makao makuu ya mila na desturi ya Maasai na ndio wenye mamlaka ya kumteua Oloiboni, Alaunoni, Oloboruengeene na viongozi wengine wa kimila.

Ole Kibiriti aliwataka malaigwanani kuacha kutumiwa kuchafua na kuvuruga utaratibu wa kimila na inasikitisha kusikia maneno ya kuvuruga taratibu za kimila kwa kutumiwa na wanasiasa.

Malaigwanani waliohudhuria kikao hicho cha siku moja ni kutoka katika wilaya za Monduli, Arumeru, Simanjiro na Longido .

Thursday, March 18, 2010

Wanaokampeni kwa fedha ‘watiwa pingu’

RAIS Jakaya Kikwete amesaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, katika moja ya matukio ya nadra kwa mkuu wa nchi kusaini sheria kwa mbwembwe tofauti na mazoea ya kusainiwa kimyakimya na kisha kuwekwa katika Gazeti la Serikali.

Februari 25 mwaka huu, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mwanza, Rais Kikwete aliahidi kuisaini sheria hiyo kwa mbwembwe kutokana na umuhimu wake, jambo lililothibitishwa na shughuli ya jana Ikulu.

Shughuli hiyo ilitangazwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni nchini na ilihudhuriwa na waalikwa mbalimbali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi wa nje, viongozi wa vyama vya siasa, majaji na waalikwa wengine.

Mbali na hao walikuwapo pia, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah.

Miongoni mwa watu maarufu waliokosekana katika shughuli ya jana ni Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta ambaye anaongoza moja ya mihimili mitatu ya Dola.

Aidha, wakati Rais Kikwete akisaini sheria hiyo saa 5.55 asubuhi, alikuwa amezungukwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na viongozi wa vyama vya siasa kutoka vyama 12 ikiwamo CCM.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati walioshiriki ni wabunge Pindi Chana, Kingunge Ngombale-Mwiru na Nimrod Mkono, walioungana na viongozi wa vyama 12 vya CCM, CUF, Chadema, TLP, AAPT, Jahazi Asilia, Chausta, SAU, Tadea, UDP, NRA na UMD.

Alipomaliza kusaini sheria hiyo, wageni walipiga makofi kupongeza hatua hiyo kabla ya wimbo wa Taifa kupigwa, ikiwa ni ishara ya kuhitimisha moja ya shughuli ambazo matunda yao yanasubiriwa na wadau wengi hasa kutokana na ukweli wa kuwapo malalamiko mengi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi.

Baada ya kusaini sheria hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa nchi kufanya hivyo hadharani tangu Uhuru, Rais Kikwete alipiga picha na viongozi waliomshuhudia akisaini sheria hiyo, kisha akapiga picha na viongozi wakuu aliokaa nao meza kuu, kabla ya kujumuika na wageni kupata viburudisho.

Awali, kabla ya Rais kusaini sheria hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, alitoa maelezo ya utangulizi, kwamba kutungwa kwa sheria hiyo ni ishara ya azma ya Serikali ya Awamu ya Nne ya mapambano yake dhidi ya rushwa na kudhamiria kuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Marmo alisema tangu Uhuru umekuwapo uchaguzi wa aina mbalimbali, lakini pia malalamiko zaidi kuhusu matumizi ya fedha katika miaka ya karibuni kwenye uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005.

“Yamekuwapo malalamiko kwamba kuna fedha zisizo na ukomo, ushindani usio dhahiri na kwamba wapiga kura wamekuwa wakichagua watu si kwa uzuri wa sera za vyama vyao, bali kwa misingi ya fedha,” alisema Marmo na kuongeza kuwa sheria hiyo imezaliwa kutokana na kusudio la Rais Kikwete alipolihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Desemba 30, 2005; mara alipoingia madarakani.

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alizungumzia kutoridhishwa kwake na hali ya matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na baina ya vyama vya siasa, katika uchaguzi wa Serikali na kueleza nia yake ya kutaka kuchukua hatua thabiti za kuweka utaratibu utakaoongoza na kudhibiti fedha katika uchaguzi.

Marmo alisema sheria hiyo inakusudia kuweka utaratibu wa kusimamia gharama za uchaguzi kwa vyama na viongozi wao; kuweka utaratibu wa kisheria kwa kuwa na uwanja sawa na halisi wa ushindani; kudhibiti rushwa kwa vyama vya siasa na wagombea; kudhibiti zawadi, misaada na michango katika kampeni na kuwapo kwa uwajibikaji wakati wa kampeni na kuoanisha adhabu kwa watakaokwenda kinyume.

“Hii ni sheria nzuri, lakini si mwarobaini wa matatizo yote ya fedha katika uchaguzi. Ni mwanzo, lakini si haba,” Marmo alimweleza Rais Kikwete na wageni wengine waliohudhuria shughuli hiyo.

Tendwa alisema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuridhia Azimio la Maputo la mwaka 2003, lililoelekeza nchi wanachama kuwa na sheria inayokataza matumizi na upatikanaji wa fedha haramu kwa vyama vya siasa na kuweka vifungu vyenye kuonesha uwajibikaji kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi na kampeni.

Tendwa, ambaye alisema sheria hiyo itatumika Tanzania Bara kwa nafasi zote tatu huku kwa Zanzibar ikihusika na uchaguzi wa Rais na wabunge tu, ni jambo jipya na ili kuepuka kuanza vibaya, “tumefanya utafiti wa kutosha na kujifunza kutoka mifano ya nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii.”

Alisema nchini, walihusisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wa dini, asasi zisizo za Serikali, NEC na watu mbalimbali. Msajili, ambaye alisema sheria hiyo imetungwa kwa nia ya kuelewa (kuondoa) tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi, aliwasihi wadau wote wa sheria hiyo, kila mmoja kwa nafasi yake, ahakikishe inafanya kazi ili kuona matunda ya kweli na umuhimu uliokusudiwa katika kutungwa kwake.

Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, gharama za uchaguzi ni fedha zote ambazo zimetumika au gharama zote zilizotumika kwa ajili ya mgombea wakati wa mchakato wa uteuzi, wakati wa kampeni na uchaguzi kwa chama cha siasa, mgombea na Serikali.

Akielezea namna walivyojipanga kutekeleza sheria hiyo, Msajili Tendwa alisema hadi Aprili 15 mwaka huu, ofisi yake itakuwa imekamilisha ufunguzi wa kanda tatu za Arusha, Mwanza na Mbeya na tayari imeomba ajira ya dharura ili kukamilisha rasilimaliwatu kwa ajili ya Mratibu wa Elimu ya Uraia na wanasheria sita kwa ajili ya kanda hizo tatu mpya.

Aidha, watakutana na wadau wa vyama vya siasa Machi 22 na 23, mwaka huu, kujadili kanuni zilizoandaliwa na kikosikazi kabla ya Waziri Mkuu kuzisaini kwa utekelezaji na pia kutakuwa na elimu ya uraia itakayoanza Machi 25 katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

Akizungumzia sheria hiyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu, alisema ni nzuri, lakini utekelezaji wake ndio changamoto kubwa inayoikabili Serikali na wadau wake. Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema ni nzuri na imemsafishia njia ya kuwania ubunge Vunjo, akisema “watu walikuwa wakishinda kwa fedha haramu, fedha za wizi na ufisadi, lakini sasa wananchi, polisi, Takukuru wawe makini, wagombea wachaguliwe kwa ridhaa ya watu.”

Jaji Mkuu Augustino Ramadhani alisema sheria hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa, wakati Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alidai itakuwa ngumu kutekelezwa kwa sababu Ofisi ya Msajili wa Vyama ina upungufu wa watumishi.

Naye John Cheyo ambaye ni Mwenyekiti wa UDP, alisema sheria hiyo ni nzuri, lakini itategemea utekelezaji wake kwa vitendo, huku akisema anawaonea huruma CCM kwa sababu ndio wenye fedha.

Tuesday, March 16, 2010

Hatma ya Liyumba kortini Aprili 9

UPANDE wa mashitaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, umefunga ushahidi wake na kuiachia Mahakama kuamua kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, wamepanga kutoa uamuzi wa kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la Aprili 9 mwaka huu.

Mara ya mwisho upande huo uliodai kuwa utakuwa na mashahidi wawili wa mwisho huku mmoja wao akiwa nje ya nchi, jana uliiambia mahakama kuwa umefikia uamuzi wa kufunga ushahidi ili kesi iendelee, ombi ambalo lilikubaliwa na Mahakama.

Mwendesha Mashitaka Juma Ramadhan alidai “shauri lilipangwa kuendelea kusikilizwa, lakini baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanane wa upande wetu na vielelezo 13, tumefikia uamuzi wa kufunga ushahidi na kuiacha kesi iendelee kwa mujibu wa sheria.”

Wakili wa Liyumba, Majura Magafu, aliiomba Mahakama kufanya majumuisho wakati huo, kwa kuwa kwa upande wa utetezi ulikuwa tayari umepinga ombi la Jamhuri kwa maelezo kwamba ni vema majumuisho yapangiwe siku nyingine, ili yatolewe ili kuwe na rekodi nzuri ya mahakama.

Mahakama ilikubaliana na upande wa Jamhuri na kupanga kupokea majumuisho ya upande wa utetezi Machi 22 mwaka huu na upande wa Jamhuri uwasilishe Machi 29 mwaka huu.
Liyumba anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka na kuisababisha Serikali hasara ya Sh bilioni 200 kwa kufanya mabadiliko katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT.

Shahidi wa saba wa Serikali, Harold Herbert Webb, aliyekuwa na jukumu la kukadiria gharama za ujenzi katika mradi huo kupitia kampuni yake ya Webb and Uronu, alidai mahakamani katika mabadiliko hayo fedha zote zilitumika.

Hata hivyo, alidai taarifa kamili juu ya gharama za mradi huo haijakamilika wala hawajaiwasilisha. Naibu Gavana wa BoT, Juma Reli alidai mahakamani pia kuwa hatambui hasara iliyotokea katika benki hiyo kutokana na mradi huo.

Monday, March 15, 2010

Turudishe Azimio la Arusha – Sumaye


WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameonesha wasiwasi kuhusu sheria inayotarajiwa kutungwa ya kutenganisha siasa na biashara, huku akipendekeza kurudishwa kwa misingi ya Azimio la Arusha kwani itasaidia nchi kurudi katika maadili.

Licha ya kuweka wazi utenganishaji huo kuwa ni jambo jema na kuliunga mkono, alisema utekelezaji wake utakuwa mgumu kutokana na kutokuwapo mipaka ya biashara na ya maadili.

“Tukitaka kufanikiwa kwa kutenganisha siasa na biashara, turudi kwenye maadili na turudishe Azimio la Arusha,” alisema Waziri Mkuu huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 10. Azimio la Arusha lilianzishwa mwaka 1967 ambapo misingi yake ilikuwa kujenga usawa baina ya watu, kuweka maadili katika uongozi kwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa rushwa katika uongozi. Lilizikwa mwaka 1992 Zanzibar.

Katika hotuba yake ya kila mwezi ya Januari mwaka juzi pamoja na kurudia mara kwa mara, Rais Jakaya Kikwete alieleza nia ya serikali ya kupeleka muswada bungeni wa kuanzishwa kwa sheria ya kutenganisha siasa na biashara, kwa kile alichokieleza kumekuwapo na mgongano wa kimaslahi.

Aliwataka mawaziri na wabunge kuchagua siasa au biashara, lakini si vyote kwa wakati mmoja. Sumaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotoa Sh milioni tano kwa Jukwaa la Wahariri jana Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa mafunzo ya maadili kwa waandishi wa habari.

Waziri Mkuu huyo mstaafu aliwahi kuahidi kutoa fedha kwa wanahabari wapewe mafunzo kutokana na fedha alizokuwa akidai mahakamani dhidi ya gazeti la Tanzania Leo ambalo alilishitaki kwa madai ya kumdhalilisha.

Fedha hizo ni sehemu ya malipo hayo. Aliunga mkono hatua ya wanachama mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpigia debe Rais Jakaya Kikwete aweze kuendelea kuiongoza Tanzania katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, Sumaye ambaye aligombea urais pamoja na Kikwete mwaka 2005 na kutopitishwa na chama chake, alisema si vibaya watu wengine wakajitokeza kugombea urais na kupigiwa debe huku kwa upande wake, akiweka wazi kutogombea nafasi yoyote katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Alipoulizwa juu ya kuwepo makundi ndani ya CCM, alisema “suala hilo halininyimi usingizi kwani CCM ni chama kikubwa makundi lazima yawepo, lakini CCM ina utaalamu wa kutatua matatizo yake, hivyo tutakwenda katika uchaguzi vizuri.” Sumaye ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alipongeza kupitishwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi, akisema sasa wagombea wasiokuwa na fedha, lakini wanapendwa na wananchi watashinda.

Mwanasiasa huyo alitetea kuwepo kwa mgombea binafsi, lakini akasema kwa Tanzania haitawezekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutokana na marekebisho ya sheria kuchukua muda mrefu.

Akizungumzia sakata la ununuzi wa rada, alisema uamuzi wa serikali ulikuwa sahihi ila matatizo yalitokea kwenye utekelezaji wake.

“Kuna wakati ndege ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ilitaka kuanguka hapa nchini kutokana na kutokuwa na rada, mataifa mbalimbali yalishatishia kusimamisha ndege zao kuja nchini hivyo ilitulazima kununua rada,” alifafanua Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wote wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye sakata hilo la rada lilitokea wakati wa utawala wake, alisema waliosimamia ununuzi huo walileta matatizo, lakini sasa wanachunguzwa hivyo uchunguzi ukikamilika wafikishwe mahakamani.

Miongoni mwa viongozi wanaotuhumiwa kupokea rushwa katika ununuzi huo na kuilazimu serikali kununua kwa gharama kubwa kuliko gharama halisi ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge.

Kwa upande wa suala ya wizi katika fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Sumaye alisema suala hilo halifahamu na wakati wake serikali isingeweza kuingilia mambo ya ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwani ilikuwa na Bodi ya Wakurugenzi waliokuwa wakifanya uamuzi.


Kuhusu kutangaza mali zake, Sumaye alisema kwa sasa haoni sababu ya yeye kutangaza na kusisitiza, “nilipoingia madarakani kila mwaka nilikuwa natangaza na baada ya kumaliza muda wangu nilitangaza, sasa nimeshakaa miaka mitano kama raia sihitaji kutangaza labda kuwe na tuhuma, nako si kuwaambia ninyi, bali vyombo vya usalama."

Alipotakiwa kuzungumzia mapigano yanayotokea katika maeneo ya Hanang mkoani Manyara na Tarime, Mara, alisema, “Tangu enzi za Mwalimu Nyerere (Julius), Tarime kumekuwa na mapigano ingawa sasa yamezidi hii inaonesha mmomonyoko wa maadili, Hanang tatizo si kubwa, viongozi wanaweza kushughulikia.”

Awali, alieleza kusudio lake la kulishitaki gazeti la Changamoto mahakamani kwa kumshushia hadhi yake, kwa kuandika habari inayoeleza kuwa akishirikiana na aliyekuwa Waziri wa Mipango na Ubinafsishaji, Dk. Abdallah Kigoda, walipora shamba la Mamlaka ya Chai la Mlangali Lupembe, mkoani Iringa lenye hekta 200 bila kulipa malipo yoyote serikalini.

Friday, March 12, 2010

Rushwa ya wazi katika majimbo

MATUMIZI ya fedha kwa ajili ya kujiweka katika nafasi nzuri kuteuliwa kugombea ubunge katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) yameshika kasi miezi minne kabla ya uteuzi rasmi utakaodhibitiwa kwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambayo imepitishwa na Bunge hivi karibuni, badala ya kanuni za chama hicho zisizoheshimika tena miongoni mwa vigogo wake, Raia Mwema imefahamishwa.

Uchunguzi wa Raia Mwema na taarifa za ndani ya CCM na vyombo vya dola, vimethibitisha kuwa kuna majimbo katika mikoa zaidi ya 14 ya Tanzania Bara na Visiwani, ambako tayari fedha zimekwisha kuanza kutolewa kufanikisha ushindi, kila mwanasiasa kwa staili yake, baadhi wakiwa ni viongozi waandamizi wa serikali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu na hata maofisa wa ofisi nyeti za umma walio karibu na ‘wakubwa.’

Hali hiyo inaendelea wakati tayari utafiti wa wasomi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) ukibainisha kuwa CCM ambayo miongoni mwa ahadi kwa wanachama wake ni kutambua kuwa “rushwa ni adui wa haki,” kinaongoza katika masuala ya utoaji rushwa wakati wa michakato ya uchaguzi, na uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa umedhihirisha usugu wa chama hicho katika vitendo vya rushwa.

Utafiti huo wa UDSM, ulitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita, jijini Dare es Salaam, ukipewa jina la Mapambano ya Rushwa kwenye Serikali za Mitaa, ukigusa vijiji, vitongoji, mitaa na kata. Katika utafiti huo, CCM inaongoza katika kujihusisha kwenye vitendo vya rushwa kwa kupata asilimia 49.5, Chadema kikipata asilimia saba, CUF 2.7, NCCR-Mageuzi kikipata asilimia 0.5 kama ilivyo pia kwa TLP.

Kutokana na mkanganyiko huo, CCM makao makuu kupitia kwa Katibu wake wa Uenezi, John Chiligati imetangaza rasmi kuwa yeyote mwenye malalamiko ya viongozi kutaka ubunge kwa kutoa rushwa wakaripoti (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) TAKUKURU moja kwa moja kwa kuwa hayo ni makosa ya jinai, yaliyo nje ya chama.

Soma zaidi

Thursday, March 11, 2010

Waomba dawa kwa watoto waathirika vituoni

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeombwa kuvipatia vituo vinavyolea watoto waishio katika mazingira magumu dawa za kurefusha maisha ili viwapatie watoto walioathirika na ambao wamesahaulika na serikali.

Ombi hilo limetolewa jana na Mkurugenzi wa Kituo cha kulea yatima cha Huruma Childrean Trust, Godliver Kugumamu.

Mkurugenzi huyo alikuwa akizungumza wakati wa kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa watumishi wanawake wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Manispaa ya Arusha (AUWSA).

Wanawake hao waliotembelea kituoni hapo na kutoa misaada kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa duniani kote juzi.

Rugumamu alisema vipo vituo vingi ambavyo vinalea watoto walioathirika lakini vimekuwa vikikabiliwa na ukosefu wa dawa hizo kutokana na kutowekwa kwa utaratibu wa kuvipatia dawa hizo.

Alisema imekuwa vigumu kwa vituo hivyo kupatiwa dawa katika vituo maalumu vinavyogawa dawa hizo zikiwemo hospitali kutokana na kutoaminiwa.

Kwa upande mwingine aliwashukuru wafanyakazi hao wanawake wa AUWSA kwa kujitolea kiasi kidogo katika mishahara yao na kuwapatia misaada watoto hao ambao wamekosa misaada baada ya kuwakosa wazazi wao wawili kutokana na majanga mbalimbali.

Kiongozi wa watumishi hao Vick Mgongolwa alisema pamoja na misaada hiyo wataendelea kuhamasisha watumishi wenzao wengine, jamii pamoja na uongozi ili kukisaidia kituo hicho pamoja na kuchukua baadhi ya watoto na kwenda kuishi nao kama mchango wao kwa watoto hao.

Watumishi hao walikabidhi misaada mbalimbali kama vile mchele kilo 50, unga wa ngano kilo 50, sukari kilo 50 mafuta ya kupikia lita 50, sabuni za kufulia katoni 10, kiasi cha Sh 150,000 taslimu kwa ajili ya ununuzi wa kuni pamoja na chakula cha mchana ambacho walikula na watoto hao vyote vikiwa na thamani ya Sh 884,000.

Wednesday, March 10, 2010

Mrema ataka alipwe Sh bilioni 1 na Sitta

MWENYEKITI wa Chama chaTanzania Labour (TLP) amemtaka Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amlipe fidia ya Sh bilioni moja ndani ya wiki moja kuanzia juzi, vinginevyo atamfungulia kesi ya madai Mahakama Kuu kwa kile anachodai kwamba amedhalilishwa.

Mrema amempa Sitta taarifa ya kusudio la kumfungulia kesi ya madai mahakamani endapo hatatimiza masharti ya kumfidia na kumwomba radhi.

Katika barua aliyoiandika juzi, Mrema amempa Sitta siku saba hadi Jumatatu ijayo, kutimiza masharti yake kabla ya kumfikisha mahakamani.

“Naomba kukufahamisha, kwamba ninakusudia kukufungulia kesi ya madai Mahakama Kuu ya Tanzania kutokana na wewe Mheshimiwa Sitta kunitukana, kunikashifu, kunivunjia heshima na kunidhalilisha kupitia magazetini,” inasema sehemu ya barua ya Mrema kwa Spika Sitta.

Barua hiyo inaendelea: “Vinginevyo, uniombe radhi kupitia magazeti yale yale na kwa uzito ule ule katika kipindi cha siku saba tangu utakapopokea barua hii; unilipe fidia ya Sh bilioni moja.”

Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili, Mrema alikuwa na kawaida ya kutoa siku saba kwa wahusika kutekeleza maagizo yake kabla hajachukua hatua.

Alinukuu gazeti la Mwananchi la Machi 5 mwaka huu, ambalo lilimkariri Sitta akimwita Mrema mhuni na aliyepitwa na wakati, aliyefilisika kisiasa na kifedha na kwamba sasa anatafuta njia ya kujinasua kutoka hali hiyo.

Mrema anadai kwamba kauli hizo, akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, zimesababisha wanachama wapatao 500,000 nchini wakose imani naye. Na pia kauli hizo anadai zimemvunjia heshima aliyojijengea kutokana na utumishi wake wa zaidi ya miaka 30 akiwa Ofisa Usalama wa Taifa, Mbunge, Waziri na Naibu Waziri Mkuu.

Alisisitiza: “Kauli zako zimeniathiri, kwa sababu nimeshajitangaza kugombea ubunge wa jimbo la Vunjo.

Hivyo kauli zako zinaweza kutumiwa na wapinzani wangu dhidi yangu.” Akizungumza na gazeti hili, Mrema alisema anaendelea na mchakato wa kuandaa mwanasheria atakayesimamia shauri lake.

Alisema Mahakama pekee ndiyo itakayotoa tafsiri halali kama Sitta alimdhalilisha au la. Gazeti hili lilimtafuta Spika Sitta kwa simu kwa lengo la kumuuliza kama amepokea taarifa ya Mrema, lakini simu yake haikupatikana.

Mazingira ya kutofautiana kati ya Spika Sitta na Mrema yamekuwa yakidhihirika kupitia vyombo vya habari.

Mrema aliitisha mkutano wa waandishi wa habari hivi karibuni na kudai kwamba Sitta ni mchochezi, mjenga makundi na mtu anayehatarisha amani na usalama wa nchi, kauli ambayo inadaiwa pia Spika aliijibu kupitia Mwananchi.

Tuesday, March 9, 2010

Monday, March 8, 2010

Wanawake walilia faragha na waume zao

WANAWAKE wanaoishi katika makambi ya waathirika wa mafuriko Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, wamesema wanahofu kubwa juu ya kuvunjika kwa ndoa zao kutokana na kutengwa na waume zao kwa muda mrefu kufuatia adha ya mafuriko iliyowakumba mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu.

Wakiongea na HabariLeo jana, katika kambi ya Mazulia (mojawapo ya kambi zinazowahifadhi), waathirika hao walisema hofu hiyo imekuja baada ya kutengana na wazazi wenzao tangu mwezi Januari mwaka huu hadi sasa.

Walisema makazi yao ya sasa hayaruhusu faragha inayostahili. Wanawake hao walisema wanaishi familia nne katika hema moja hivyo kuwalazimu kuishi wanawake pamoja na watoto wao wa kike peke yao , huku waume zao wakiishi katika mahema mengine na watoto wa kiume.

Wamesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri sana kisaikolojia kutokana na mazoea ya hapo awali ya kuishi na wazazi wenzao pamoja, na kueleza kuwa hali hiyo imekuwa ikiwakosesha raha kutokana na kuingiwa na hofu ya kuhatarisha ndoa zao.

“ Tangu tumehamia kwenye haya mahema tumekuwa na mawazo sana juu ya hizi ndoa zetu…tutaishi hivi hadi lini, maisha haya kwa kweli ni magumu sana , japokuwa serikali inajitahidi kutupatia chakula, lakini ndoa zetu zipo matatani” walisema.

Walisema licha ya kuhofia kuporomoka kwa ndoa hizo, pia wamekuwa na hofu kubwa ya kupata magonjwa ya zinaa ikiwa ni pamoja na kupata maambukizo mapya ya virusi vya Ukimwi kutokana na wanaume hao kupata nafasi ya kutoka nje ya ndoa zao kutokana na visingizio vya kuishi tofauti na wake zao.

“Kama unavyojua hawa wakina baba kipindi hiki kwao wanaona ni neema, kwa kuwa wana uhuru wa kuzurura na kurudi kwenye mahema muda wanaotaka kwa kuwa hatupo nao, wanafanya maamuzi yao, jambo ambalo ni hatari sana linaweza huko baadaye likatuletea magonjwa ya zinaa hata maambukizi ya Ukimwi” walisema kwa masikitiko.


Wanawake hao walisema kutokana na adha hiyo ya mafuriko hivi sasa gharama za nyumba za kupanga zimepanda mara mbili, na kueleza kuwa chumba cha bei ya shilingi elfu tano hivi sasa ni shilingi elfu kumi, huku bado kukiwa na uhaba mkubwa wa nyumba za kupanga.

Waliongeza kuwa kutokana na kupanda gharama za nyumba hizo, ili hali wakiwa na kipato kidogo wanalazimika kuendelea kuishi kwenye mahema hayo ili kuweza kupunguza gharama zaidi za maisha.

Wakizungumzia juu ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo ilianza tangu Machi mosi, walisema hawawezi kuifurahia siku hiyo kutokana na matatizo yanayowakabili hususani katika kipindi hiki kigumu ambacho wamelazimika kutengana na wazazi wenzao kufuatia adha hiyo ya mafuriko.

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Kambi hiyo Said Madogoya alisema imelazimu familia hizo kuishi kwa mtindo huo kutokana na uhaba mkubwa wa mahema unaowakabili, na kueleza kuwa mahema hayo yasingetosha kuhifadhi familia moja katika kila hema kutokana na uchache huo.

Kambi hiyo ya Mazulia ina idadi ya mahema 744 yaliyojengwa, ikiwa ni sambamba na vyumba 57 vilivyogawanywa ndani ya kiwanda cha Mazulia.

Huku wanawake wengine duniani leo wakiadhimisha sikukuu yao, wanawake wa Wilaya ya Kilosa wataingia wakiwa na dhiki kubwa za kifamilia.

Thursday, March 4, 2010

MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI YAFANA VIWANJA VYA TGNP










Jana tarehe 3/3/2010 wanaharakati wa masuala ya jinsia waliadhimisha siku ya wanawake duniani katika viwanja vya TGNP, hakika sherehe hizo zilifana sana kwa wanataaluma mbalimbali kutoa mada na wengine waliohudhuria kutoa visa mkasa, michezo ya kuigiza na mijadala.

Wednesday, March 3, 2010

Ananilea Nkya apata tuzo ya Mwanamke JASIRI wa mwaka 2010



Mkurugenzi wa TAMWA, Bi. Ananilea Nkya akipokea tuzo ya Mwanamke Jasiri wa Tanzania kwa mwaka 2010 kutoka kwa Balozi wa Marekani nchini Alfonso Lenhardt. Kapata tuzo hiyo kutokana na juhudi na ubunifu wa TAMWA wa kutumia vyombo vya habari katika kuimarisha usawa, fursa na haki za wanawake na watoto wa kike wa Tanzania

Tuesday, March 2, 2010

HALI YA WANAWAKE BADO NI NGUMU - DK. MIGIRO


Ikiwa ni miaka kumi na tano sasa tangu kupitishwa kwa Tamko la Beijing kuhusu Hali ya Wanawake, imeleezwa kuwa pengo la usawa wa kijinsia kati ya mwanamke na mwanaume bado ni kubwa. Na kwamba hali hiyo ipo katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro ameyasema hayo wakati alipokuwa akifungua mkutano wa 54 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake.

Ajenda kuu ya mkutano huo kwa mwaka huu, pamoja na mambo mengine, ni kufanya tathimini ya Tamko la mkutano wa nne wa Beijing na mpango wake wa utekelezaji. Mkutano uliofanyika mwaka 1995 rais wake walikuwa alikuwa Mhe, Getrude Mongela ambaye hivi sasa ni mbunge wa jimbo la Ukerewe ni mmoja ya washiriki wa mkutano huu.

Mkutano huo wa wiki mbili umeanza siku ya jumatatu na unafanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na wanawake akiwamo makamu wa rais wa Ghambia ambaye ni mwanamke, mawaziri, wabunge, makatibu wakuu na makundi kutoka asasi zisizo za kiserikali.

Akitoa mfano, Migiro anaeleza kuwa bado idadi kubwa ya maskini ni wanawake kuliko wanaume, wasioujua kusoma au kuandika wengi ni wanawake kuliko wanaume, hata wanaofanya kazi katika mazingira magumu, kwa ujira mdogo na bila kinga au bima yoyote ni wanawake zaidi kuliko wanaume.

Kama hiyo haitoshi, Naibu Katibu Mkuu anabainisha kuwa hata mtizamo kuhusu masuala ya wanawake bado ni hasi ingawa kuna mwamko kidogo, na kwamba utekelezaji wa mambo mengi bado unamtizamo wa kibaguzi. Huku kukiwa na utofauti kati ya upitishwaji wa sheria na utekelezaji wa sheria hizo.

Anasema Migiro. “ Bado wanawake wengi ni maskini, wanaofanya kazi ngumu au za majumbani ni wanawake na watoto wakike , robo tatu ya wanawake hawajui kusoma wala kuandika na hali hii haijabalikia kwa zaidi ya miaka 20 sasa“.

Kuhusu nafasi ya uwakilishi katika vyombo vya kutunga na kupitisha sheria, Migiro anasema kasi yake si ya Kuridisha kwani hadi mwaka 2009 ni nchi 25 tu ambazo zimeweza kufikisha lengo la kuwa na asilimia 30 ya wabunge wanawake.

Kwa upande wa huduma za afya ya uzazi, Naibu Katibu Mkuu, anaeleza kwamba, bado ni eneo ambalo halijawa na nafuu yoyote, idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi bado ni kubwa. vifo ambavyo siyo tu havipashwi kutokea lakini pia vinaweza kuzuilika.

“ Kwa hiyo, wakati tunaona kuwa kuna dalili zuri za mafanikio mbalimbali kuhusu hali ya wanawake miaka 15 baada ya tamko la Beijing, ukweli ni kwamba bado hakuna mabadiliko ya kuridhisha na kujivunia.

Pamoja na mapungufu hayo, Naibu Katibu Mkuu ametumia fursha hiyo kuwapongeza na kuwashukuru wanawake, katika nafasi zao mbalimali kwa kazi kubwa wanaoifanya ya ubinifu wa kuzishinikisha na kuziwajibisha serikali zao zitekeleze sera, sheria na mipango inayolenga kuleta usawa na uwezeshwaji wa wanawake.

Akasema jitihada zao hizo zimeweza kulete mwamko na uelewa miongoni mwa viongozi wanawake kwa wanaume ya kuwa suala la usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa mwanamke na mtoto wa kike si jambo la kupita na badala yake ni moja ya nguzo muhimu katika upatikanaji wa maendeleo endelevu, ukuaji wa uchumi, amani na usalama.

Akasema yeye na Katibu Mkuu Ban Ki Moon wamedhamiria kuhakikisha kwamba Umoja wa Mataifa unaweka mazingira bora yatakayoziwezesha serikali na asasi za kijamii kuhakikisha kuwa masuala ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake yanaingizwa katika Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs).

Monday, March 1, 2010

Kibao cha ufisadi chazigeukia NGOs

BAADA ya viongozi wa asasi za kiraia (NGOs) kutajwa katika nafasi ya chini miongoni mwa makundi za wananchi wanaoaminiwa katika jamii, asasi wanazoziongoza zimeshutumiwa kwa kuwanufaisha watu binafsi zaidi ya jamii ambayo ndiyo chimbuko lake.

Utafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Foundation For Civil Society kuhusu maoni ya umma juu ya asasi za kiraia Tanzania kwa mwaka 2009, umebaini kuwa sehemu kubwa ya wananchi wanazilaumu asasi hizo kwa kuwatajirisha watu binafsi zaidi ya jamii.

Shutuma hizo zimetolewa na jamii ya watu wanaozunguka miradi ya maendeleo ya asasi hizo walipotakiwa kuelezea mambo wanayoyachukia kuhusu asasi hizo.

Katika utafiti huo, watu 800 kwa kuzingatia jinsia kutoka mikoa minane iliyowakilisha kanda nane za Tanzania na Zanzibar, walihojiwa kwa njia ya ana kwa ana kwa dakika 20 kwa kila mwanajamii.

Kabla ya utafiti huo, utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2007 kwa kuhoji jumla ya Watanzania 7,879 kuhusu makundi ya watu wanaoaminika sana na jamii, kati ya makundi 18 ya jamii yaliyotajwa kuaminiwa, viongozi wa asasi hizo walitajwa katika nafasi ya 13.

Walioongoza kwa kuaminiwa zaidi na Watanzania ni ndugu zao wa familia wakifuatiwa na viongozi wa dini, ndugu wa ukoo, walimu, watu wa kabila moja, wazee wa kike, wazee wa kiume, wenyeviti wa vijiji na kata, madaktari na wauguzi na viongozi wa mitaa huku vijana wa kiume na wageni wasio Watanzania wakishika nafasi za 17 na 18 ambazo ni za mwisho.

Utafiti huo wa mwaka 2007 uliofanywa na Asasi ya Utafuti wa Kuondoa Umasikini (Repoa), ambao ulikuwa moja ya tathimini za utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (Mkukuta), ulionesha pia kuwa wanasiasa walishika nafasi ya 11, wafanyabiashara 12 na polisi nafasi ya kumi na tatu.

Licha ya asasi hizo kushutumiwa kwa kuwatajirisha watu binafsi zaidi ya jamii, wananchi hao waliohojiwa katika utafiti wa Foundation For Civil Society pia walisema wanachukizwa na kukosekana kwa muundo sahihi wa menejimenti katika asasi hizo.

Kikwete: Kununua uongozi sasa basi

RAIS Jakaya Kikwete, amesema Sheria ya Gharama za Uchaguzi ambayo atasaini muswada wake karibuni ili ianze kazi, ikitekelezwa ipasavyo itazuia kugeuza uongozi kuwa kitu cha kununuliwa kama bidhaa na wenye fedha.

Akihutubia Taifa jana katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi, Rais Kikwete alisema chimbuko la kutungwa sheria hiyo ni mwenendo usioridhisha wa matumizi ya fedha katika uchaguzi nchini.

“Kuna matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na baina ya vyama vya siasa katika chaguzi za kiserikali,” alisema Rais Kikwete aliyetumia hotuba yake hiyo kuzungumzia Muswada huo wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi uliopitishwa na Bunge katika Mkutano wake wa 18 mwezi uliopita mjini Dodoma.

Aidha, amesema itakomesha kabisa tabia mbaya inayoanza kujitokeza ya wapiga kura kugeuza kura yao kama bidhaa ya kuuza kwa wagombea.

“Hivi sasa kwa sababu ya kutokuwepo ukomo, wako watu wenye pesa ambao wanafanya matumizi kupita kiasi. Wapo wanaopitiliza au hata kukufuru na kuwadhalilisha wenzi wao wasiokuwa na uwezo kama wao,” alieleza Rais Kikwete.

Wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Takukuru mjini Mwanza wiki iliyopita alisema atasaini muswada huo kuwa sheria kwa mbwembwe ili kuwabana wanaotumia fedha kupata uongozi.

Alisema sheria hiyo mpya imetungwa kwa nia ya kupata majawabu kwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi.

“Tunatambua kuwa matatizo haya si mageni, yamekuwepo tangu miaka mingi huko nyuma na hata historia ya Bunge letu ina ushahidi wa ushindi wa baadhi ya wabunge kutenguliwa kwa makosa ya rushwa.

“Lakini, siku hizi matatizo ya matumizi mabaya ya fedha yamekuwa makubwa zaidi na yanakua kwa kasi inayotishia kugeuzwa kuwa ndiyo utaratibu wa kawaida au utamaduni katika chaguzi zetu,” alisema na kuongeza:

“Ni hali ambayo haifai kuachwa kuendelea na kuzoeleka. Hatuna budi kuchukua hatua za dhati kurekebisha mambo na kulirejesha taifa katika mstari ulionyooka.”

Alisema serikali iliamua kuwa hatua muafaka ya kuchukua ni kutunga sheria ya kuongoza na kudhibiti matumizi katika uchaguzi.

“Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo itazuia kugeuza uongozi kuwa ni kitu cha kununuliwa kama bidhaa na wenye pesa au wanaoweza kupata pesa za kufanya hivyo. Aidha, itakomesha kabisa tabia mbaya inayoanza kujitokeza ya wapiga kura kugeuza kura yao kama bidhaa ya kuchuuza kwa wagombea,” alieleza Rais Kikwete. Alisema ametumia muda mwingi katika hotuba yake kuelezea mambo ya msingi yaliyomo katika sheria hiyo, akilenga mambo matatu muhimu.

“Kwanza, kuwathibitishia Watanzania wenzangu kwamba tunalitambua tatizo la rushwa katika uchaguzi na tunayo dhamira ya dhati ya kupambana nalo. Kukemea peke yake hakutoshi, lazima tutumie nguvu ya sheria kudhibiti vitendo vya rushwa na kuwaadhibu ipasavyo wahusika,” alisema Rais Kikwete.

Soma zaidi