Monday, June 27, 2011

Ngeleja-Umeme ni janga la taifa, vumilieni

WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema, mgawo wa umeme unaoendelea kote nchini ni janga la kitaifa linaloathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kwa taifa.

Hata hivyo, waziri huyo alisema kuna mipango ya Serikali na Shirika la Umeme (Tanesco) yenye tija ya kukabiliana na mgawo huo wa umeme na kuwaomba wananchi waivumilie Serikali na Tanesco wakati inaendelea kutekeleza miradi hiyo.

Ngeleja pia alisema makali ya mgawo huo yatapungua wiki hii baada ya kuhakikishiwa na Wizara ya Fedha kwamba fedha za kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ili izalishe megawati 100, zimepatikana.

“Hivyo kiwango cha uzalishaji umeme cha mitambo hiyo kitaongezeka kutoka megawati 10 kwa sasa hadi megawati 100 wiki ijayo,” alisema Ngeleja.

Alisema Serikali na Tanesco wanaguswa na kukerwa na adha na usumbufu unaosababishwa na mgawo wa umeme kama wanavyokerwa wananchi wote wa Tanzania.

Hata hivyo licha ya kuwepo kero hizo, amewaomba wananchi wapuuze dhihaka, kejeli na kebehi zinazofanywa na baadhi ya watu wasiothamini juhudi na jitihada za kweli zinazofanywa na Serikali na Tanesco yenyewe.

Alisema Serikali inaamini kwamba watu wote wanapuuza na kubeza jitihada hizi na Serikali na Tanesco wakati wanajua historia iliyopitia shirika la Tanesco kwa kutofanyika uwekezaji wowote kuanzia mwaka 1997 hadi 2005 kuwa wanafanya hivyo kwa makusudi.

Alifafanua kuwa watu hao wanafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi, ikiwemo kupata umaarufu wa kisiasa, “tunawaombaa wananchi wawapuuze watu wa namna hii.”

Ngeleja alijitetea kuwa tatizo la mgawo wa umeme kwa nchi yetu ni tatizo halisi kama vile tatizo hilo lilivyoikumba nchi ya Japan kwa sasa kutokana na matatizo halisi ya kuathirika kwa vyanzo vya umeme ambavyo ni mitambo ya nyuklia baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi.

Alisema suluhu ya tatizo hilo siyo kubeza juhudi zinazofanywa na Serikali na Tanesco, bali ni kuunganisha nguvu za wadau wote na kuitia moyo Serikali na Tanesco kwa hatua za dharura zinazochukuliwa na miradi inayoendelea kutekelezwa kukabiliana na mgawo wa umeme nchini.

“Tunawaomba wananchi waendelee kuvumilia, tuimarishe mshikamano, utulivu na amani na tuwaepuke wote wanaobeza juhudi za Serikali na Tanesco kutatua tatizo la mgawo wa umeme kwa maslahi yao binafsi, ikiwa ni pamoja na maslahi ya kisiasa.

Alijitetea kuwa mgawo wa umeme unaoendelea kwa sasa umesababishwa na upungufu wa mvua zilizonyesha mwaka huu, hivyo kutojaza mabwawa yanayozalisha umeme kwa kuzingatia kwamba takribani asilimia 55 ya umeme unatokana na maji.

Alisema, bwawa la Mtera litafungwa mwishoni mwa Agosti kutokana na kina chake kuendelea kuwa chini.

Alisema, suala la Taifa kutegemea umeme wa maji kwa asilimia 55, sio dhambi wala kosa la makusudi wala uzembe, bali ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali kwa nia njema kama zilivyofanya nchi nyingine duniani.

Alisema, mabadiliko ya tabia nchi katika miaka ya hivi karibuni duniani yamekuwa na changamoto kubwa kwa nchi nyingi zinazotegemea kwa kiasi kikubwa umeme wa maji na akatoa mfano wa nchi ya Ethiopia.

Alizitaja kampuni za Symbion na Aggreko kuwa zimepewa jukumu la kupunguza makali ya mgawo wa umeme katika kipindi hiki cha dharura kwa kuzalisha megawati zaidi ya 200.

Kikao cha Bunge la bajeti kinaendelea tena leo kwa wabunge kuendelea kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoiwasilisha Alhamisi iliyopita.

Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge wataendelea kuijadili hotuba hiyo ambayo itahitimishwa kesho kutwa kwa Waziri Mkuu kufanya majumuisho ya michango ya wabunge.

No comments: