Friday, June 24, 2011

Wabunge waibue mijadala majimboni mwao

Kona ya Karugendo

Wabunge waibue mijadala majimboni mwao
Privatus Karugendo
22 Jun 2011
Toleo na 191
Raia Mwema

• Wengi hawana mawasiliano na wapiga kura wao

UKISIKILIZA jinsi mjadala unavyokwenda kwenye Bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma, utagundua kwamba wabunge wetu hawana mawasiliano na wananchi waliowatuma bungeni.

Wengi wao wanawasilisha maoni yao binafsi badala ya kuwasilisha maoni ya wananchi. Wanaunga mkono hoja zote, kana kwamba hoja hizo zimetengenezwa na malaika. Kama huo ndio ukweli, ya nini basi hoja hizo kuletwa Bungeni?

Kwa nini wabunge wapoteze miezi miwili wakijadili kitu ambacho wanafahamu fika kwamba mwisho wake ni kupitishwa kwa asilimia 100?

Kama mchango wa maoni ya wabunge hauwezi kusaidia kubadilisha chochote ndani ya bajeti inayowasilishwa na serikali, ina maana gani, basi, bajeti hiyo kupelekwa Bungeni? Huku si kufuja fedha za walipakodi wa Tanzania? Kama wabunge hawana mchango wowote kwa bajeti, kwa nini kuijadili?

Ni busara na ni kubana matumizi kama Serikali ingeandaa Bajeti na kutusomea, na maisha yakaendelea kama kawaida kuliko kupoteza muda na fedha nyingi kujadili kitu ambacho kimefanyiwa maamuzi tayari!
Inashangaza jinsi wabunge wetu wanavyoviogopa vyama vyao vya siasa kuliko wanavyowaogopa wananchi waliowatuma Bungeni. Nijuavyo mimi, mbunge anapotangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa mbunge, anakuwa si mbunge wa chama; bali ni mbunge wa wananchi wa jimbo zima; hivyo kukiogopa chama chake wakati wa kujadili masuala ya kitaifa, ni kuwasaliti wananchi waliomtuma Bungeni.

Kwa jinsi Bunge letu lilivyo hivi sasa ambapo lina wabunge wengi wa chama kimoja (CCM) chenye kujali maslahi yake na kuziba masikio kwa kilio cha wananchi walio wengi, hata muswada wa kutunga sheria ambao ni dhaifu mno ukiwasilishwa Bungeni utapitishwa tu; maana ni utamaduni wa “ndiyooo” na “kuunga mkono asilimia 100” bila kutafakari au kuzingatia maoni ya wananchi na maslahi ya Taifa.

Mfano mzuri ni Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano uliopitishwa, wiki iliyopita, Bungeni. Uliletwa Bungeni ujadiliwe; lakini jinsi mjadala ulivyokwenda ilijionyesha wazi kwamba mpango huo ulishapitishwa tayari, na yeyote aliyekuwa na maoni tofauti alionekana kama msaliti.
Swali la kujiuliza ni kama Mpango huo ulishapitishwa tayari, kwa nini ulipelekwa Bungeni? Ili wa wabunge wetu wapate posho? Ili tutambue kwamba CCM ndicho chama tawala?

Hoja hapa si kuupinga Mpango huo, na ni imani yangu kwamba hata wabunge waliokuwa na maoni tofauti si kwamba walilenga kuupinga. Lakini ukweli ni kwamba hata wale waliouandaa si malaika; na si kweli kwamba kabla ya kuuandaa walizunguka nchi nzima kuomba maoni ya wananchi juu ya Mpango huo.
Kuna wananchi wanaoishi pembezoni na hasa wanawake walioulizwa juu ya Mpango huo? Mbona hatuoni vizuri mikakati ya kuwanufaisha walio pembezoni ndani ya Mpango wenyewe?

Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika, alihoji juu ya Barabara ya Morogoro ambayo hivi karibuni itapanuliwa na mradi wa mabasi yaendeayo kasi. Lakini ndani ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano haionyeshi kwamba zitatengenezwa barabara mbadala za kuingia katikati mwa jiji wakati barabara ya Morogoro ikijengwa upya.

Pia Mnyika alihoji juu ya huduma ya maji wakati Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unazungumzia mpango mpya wa huduma ya maji, bado mpango uliokamilika “wa Wachina” bado maji hayajatoka!

Hizo ni hoja za msingi kuzipuuza. Kwa hakika kuzipuuza ni kujitangazia hali ya hatari, kama si leo ni kesho. Maana; kama ni mpango wa maendeleo ya Watanzania, ni lazima Watanzania wote washirikishwe.
Haifai kabisa yawe ni mawazo ya mtu mmoja; kwani siku akiondoka, basi, na mpango mzima unakufa. Usiwe mpango wa chama kimoja; kwani siku kikiondoka madarakani mpango mzima unakufa.

Mpango huu wa miaka mitano, kwa bahati mbaya au nzuri, unakuja wakati Tanzania inasherehekea miaka 50 ya uhuru wake. Lakini pia unakuja wakati tumeshuhudia mipango mingi ya maendeleo na kukuza uchumi ambayo mafanikio yake, kama yanaonekana, basi, ni kwa watu wanaoishi dunia nyingine, na wala si hapa Tanzania.

Ndio maana watu wanakuwa na maswali mengi juu ya tumefanya nini ndani ya miaka 50. Kwamba yaliyoshindikana ndani ya miaka 50 yatawezekana ndani ya miaka mitano?
Kuuliza hivyo haina maana kwamba hatujafanya chochote ndani ya miaka 50. Kuishikia bango hoja hii kwamba kuna watu wanasema Serikali haijafanya chochote ndani ya miaka 50, ni kutaka kuipotosha hoja yenyewe.

Tanzania imefanya mengi ndani ya miaka 50. Ukiachia mbali wimbo wetu wa taifa wa “Amani na Utulivu”, kwenye michezo tunakuwa wa mwisho. Tunaimba “Amani na Utulivu”, uchumi wetu unadidimia. Tunaimba “Amani na Utulivu”, kiwango cha elimu kinashuka. Tunaimba “Amani na Utulivu”, kipindupindu, malaria na magonjwa ya kusendeka yanatuteketeza hadi tunakimbilia Loliondo tukiimba, “Amani na Utulivu”! Aidha, raslimali zetu zinachotwa na wajanja wachache, lakini sisi tunaimba “Amani na Utulivu.

Tulijenga Siasa ya Ujamaa na kujitegemea, ikafa na tukaizika. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hiyo? Tulianzisha mashirika ya umma yakafa na kuzikwa. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii?

Tulianzisha maduka ya vijiji, yakafa yote. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulianzisha viwanda, vikafa vyote na kuzikwa. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii?
Tulikuwa na sekondari nzuri zikijulikana ndani na nje ya nchi, kama vile Ihungo, Tabora Boys, Milambo na nyingine nyingi. Ubora wa shule hizo umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani?
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilikuwa tishio Afrika nzima na duniani kote. Ubora wa chuo hiki umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hiyo 50?

Ndani ya 50 hatuwezi kutengeneza wembe! Hatujavumbua kitu chochote zaidi ya panya wa kutegua mabomu! Tunanunua hata njiti za kuchokonoa meno kutoka nchi za nje. Viongozi wetu wakiugua wanakimbilia nchi za nje na kule wanatibiwa na madaktari wetu walioikimbia nchi.

Ndani ya miaka 50 tumezalisha madaktari wengi na namba kubwa imekimbilia nchi za nje kutafuta maslahi zaidi. Ndani ya miaka 50 tumenunua ndege ya rais wakati tunaomba msaada wa kujenga vyoo kwenye mashule yetu!
Ndani ya miaka 50 tumenunua magari ya kifahari kwa viongozi wetu wakati tunaomba msaada wa fedha za kuiendesha serikali yetu!

Ndani ya miaka 50 Tanzania bado tuna matatizo mengi. Wale maadui tuliowatangaza wakati wa Uhuru: Ujinga, maradhi na umaskini, bado yametuzunguka.
Na ndio maana ninapendekeza kwamba kuna haja wabunge wetu kutengeneza jukwaa la majadiliano ndani ya majimbo yao ili wapate nafasi ya kuwasikiliza watu na kupokea maoni yao.

Hatua hiyo itawasaidia kuondokana na utamaduni huu uliojengeka wa mbunge kuwasilisha bungeni maoni yake binafsi na kuegemea zaidi kwenye chama chake badala ya kuegemea kwa wananchi waliomtuma bungeni.

Wabunge wetu waige mfano wa TGNP. Huu ni Mtandao wa Jinsia Tanzania. Ni shirika la kiraia na kiuanaharakati linalotetea mabadiliko ya kijamii kwa mtazamo wa wanawake; mabadiliko ambayo yanalenga kwenye usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake, haki za kijamii, kufikia na kumiliki raslimali kwa wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni.

TGNP ilianzisha jukwaa la majadiliano. Kila Jumatano jioni pale Mabibo, Dar es Salaam kuna mijadala inaendelea. Ni mijadala ya wazi inayomkaribisha kila mtu. Wanajadilia masuala mbalimbali ya kijamii, na siku hizi wanaendesha mijadala juu ya Katiba mpya.

Wabunge wetu wangekuwa wanatembelea jukwaa hili (wabunge wengi wa Tanzania wanaishi Dar es Salaam) wangeweza kupata mengi na kutambua mahitaji ya wananchi.

Aidha, wangeweza kujifunza mbinu za kuanzisha majukwaa kama haya kwenye majimbo yao. Ni kupitia kwenye majukwaa ya majadiliano tunaweza kuwa na uwakilishi wa kweli na wenye tija kwa taifa letu.
Mbali na jukwaa la majadiliano la kila Jumatano, TGNP inaandaa pia matamasha ya jinsia. Kila baada ya miaka miwili kuna tamasha la jinsia pale Mabibo. Tamasha la jinsia ni nafasi ya wazi kwa ajili ya watu binafsi, mashirika na mitandao, walio katika mapambano yanayofanana, kubadilishana uzoefu, taarifa na kujengana uwezo.


Mwaka huu, Septemba 13 hadi Septemba 16, TGNP itaendesha tamasha la jinsia la kumi. Mada kuu ya tamasha hili itakuwa ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na Maisha Endelevu.

Ni tamasha linalokuja wakati kumejitokeza wimbi kubwa la uporaji wa ardhi. Serikali bado ina kigugumizi juu ya wimbi hili na baadhi ya viongozi wa serikali wanashiriki wimbi hili la kupora ardhi.

Kwa maana hiyo, ni wakati mzuri wa kukutana na kujadiliana juu ya suala hili na mengine mengi. Haina maana kukaa na kupanga Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wakati ardhi inaporwa.

Tunajua kwamba uchumi wetu unategemea kiasi kikubwa sekta ya Kilimo. Kama wananchi wetu hawana uhakika wa ardhi yao, kama ardhi inaporwa na matajiri wakishirikiana na wageni, wananchi watapata wapi ardhi ya kulima na kuzalisha? Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba ardhi ndio uhai wa kila binadamu. Bila ardhi hakuna uhuru!

Ni bahati mbaya kwamba viongozi na wabunge wetu wanalikwepa tamasha hili. Tamasha la jinsia la tisa, sikubahatika kukutana na kiongozi yoyote kwenye tamasha hilo. Hata viongozi wanaojulikana kuwa wapambanaji na watetezi wa haki za binadamu na wapenda maendeleo ya Tanzania, sikuwaona kwenye tamasha hili.

Natumaini mwaka huu viongozi wetu na wabunge watafika kwenye tamasha hili la jinsia; maana kila mwenye akili nzuri na kujali uhai wa taifa letu anaona wazi kwamba, sasa tunayumba. Na bila kuwa na majukwaa kama hili la TGNP na mengine mengi, tutazama kabisa!

Napenda kuwashauri viongozi wetu na wabunge kwamba matamasha kama hili la TGNP na mengine yanayoruhusu mijadala ya wazi, ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu.

Ni muhimu kuwasikiliza watu kabla ya kukaa na kuwapangia mipango ya miaka mitano. Unaweza kufikiri wananchi wanahitaji maji, kumbe wao wanahitaji moto!

No comments: