KAMBI ya Upinzani Bungeni imedai kushitushwa na upotoshaji wa kitakwimu na kimaudhui uliofanywa na Serikali katika Bajeti ya mwaka 2011/12.
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, ametoa kauli hiyo katika taarifa yake ya kurasa nne kwa vyombo vya habari jana mjini hapa.
Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo kuwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2011/12 ya Sh trilioni 13.525.9.
Zitto amesema Upinzani umeshitushwa na upotoshaji huo aliouelezea kuwa lengo lake ni kuwajengea matumaini hewa wananchi kuwa watapata nafuu ya maisha kupitia bajeti hiyo wakati hali halisi haiko hivyo.
Alitaja maeneo ambayo Mkulo amepotosha umma kuwa ni kutaja kipaumbele cha kwanza cha bajeti hiyo kuwa ni kumaliza tatizo la umeme na hivyo kutamka kwamba ametenga Sh bilioni 537, wakati vitabu vya bajeti, kwa mujibu wa Zitto, vimebaini fedha hizo si sahihi.
“Upembuzi uliofanywa na Kambi yetu ya Upinzani kwenye vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV) vilivyotolewa na Serikali, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa Sh milioni 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58,” alisema Zitto na kuongeza:
“Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi ya kawaida ya Sh milioni 76,953,934,000 na kwa bajeti ya Maendeleo, zimetengwa Sh milioni 325,448,137,000. Shilingi bilioni 325 zilizotengwa kwa Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160MW, 100 Dar es Salaam na 60 Mwanza.”
Zitto alisema hakuna mradi wowote mpya wa umeme unaoonekana katika bajeti, hivyo alidai ni dhahiri kuwa kauli ya Mkulo ililenga zaidi kuwajengea wananchi matumaini hewa kuliko kuchukua hatua za kweli za kumaliza tatizo la umeme.
Aidha, alieleza kuwa Waziri Mkulo anataka kuwaaminisha Watanzania kuwa bajeti ya mwaka huu imeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka 2010/11, na kudai kuwa ukweli hakuna ongezeko halisia, lililofanyika katika bajeti hiyo.
Alisema bajeti iliyopita ilikuwa ni Sh trilioni 11.1 wakati ya mwaka huu ni Sh trilioni 13.525; ambazo kati ya hizo, Sh trilioni 1.901 sawa na asilimia 14 ya bajeti yote, zitatumika kulipia deni la Taifa.
“Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya kuendesha Serikali pamoja na kugharamia miradi ya maendeleo zitabaki Sh trilioni 11.624 ambazo ni sawa na fedha za bajeti ya mwaka uliomalizika wa 2010/11 (japo thamani ya Shilingi imeanguka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2010/11),” alieleza Zitto katika taarifa yake.
Kuhusu kupunguza posho kama mkakati wa kudhibiti matumizi yake, Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, alisema bajeti hiyo imetenga Sh trilioni 0.987 kwa ajili ya kulipa posho, ambazo ni sawa na asilimia 13 ya bajeti.
Alisema hali hiyo pia ni tofauti na kauli ya Waziri Mkulo, kwani Serikali imetangaza kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa watumishi wa Serikali wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya Serikali, hivyo kauli yake haina udhati.
Alisema Kambi ya Upinzani itawasilisha bungeni bajeti mbadala Jumatano, ambayo itakuwa inajali maslahi ya Watanzania, yenye lengo la kukuza uchumi vijijini na itajikita katika kupata vyanzo hivyo vya mapato na kubana matumizi ikiwamo kufuta posho.
Mkulo hakupatikana jana kutoa ufafanuzi wa madai hayo ya Upinzani kwa kuwa simu
yake haikupatikana alipopigiwa na gazeti hili jana jioni.
Lakini katika hotuba yake juzi, alisema katika kudhibiti matumizi yake, Serikali katika mwaka wa fedha 2011/12, itasitisha ununuzi wa magari ya aina zote isipokuwa kwa sababu maalumu na kwa kibali cha Ofisi ya Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kuwapo kwa vyama vingi vya siasa nchini si uadui, bali ni kupanua demokrasia na kuleta utawala bora ili kupata maendeleo ya haraka.
Pinda alikuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa wanaounda Baraza la Vyama vya Siasa nchini, katika hafla aliyowaandalia kwenye makazi yake mjini Dodoma juzi.
Alisema kwa mantiki hiyo, ndiyo maana bungeni, pamoja na hoja kali, lakini wabunge wa vyama tofauti si maadui. “Tunafanya kazi pamoja, tunakula pamoja, tunacheka pamoja na wakati mwingine utafikiri wote tunatoka chama kimoja”.
Aliwaelezea wajumbe hao hatua ambazo Serikali inachukua katika mchakato wa Katiba mpya na utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12 iliyowasilishwa juzi.
Waziri Mkuu alisema pia Serikali itaziangalia na kuzifanyia kazi hoja za Baraza za kutaka liwezeshwe, litangazwe kwa wananchi, ili walitambue vizuri na lipewe nafasi kubwa ya kuishauri Serikali katika masuala ya kitaifa na ya kisiasa.
Hoja hizo zilitolewa na baadhi ya wajumbe waliopata nafasi ya kuzungumza katika hafla hiyo.
Wajumbe walimshukuru Pinda kwa kukutana nao kama Baraza. Vilevile walikiri kuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa kitaifa wa ngazi yake kukutana na viongozi wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa na kubadilishana mawazo kwa uhuru.
Walitaka mawasiliano baina ya Serikali na Baraza yaendelezwe kwa manufaa ya Taifa.
Baraza hilo limeundwa kisheria kwa marekebisho ya mwaka 2009 ya Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5 ya mwaka 1992.
Kazi yake kubwa ikiwa ni kuishauri Serikali katika mambo ya kitaifa na yanayovihusu vyama vya siasa, hasa katika kutatua migogoro ya vyama hivyo kila inapozuka.
Linaundwa na vyama 18 vya siasa vyenye usajili wa kudumu, kutoka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano na Sekretarieti yake iko chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, pia alikuwapo katika hafla hiyo na aliahidi kuwa ofisi yake itajitahidi kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za Baraza hilo.
No comments:
Post a Comment