KAMBI ya Upinzani Bungeni imesema, kumekuwa upotoshaji wa kitakwimu na kimaudhui katika hotuba ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo aliyoitoa bungeni June 8 kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa kipindi cha mwaka fedha wa 2011/2012.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni, Kabwe Zitto, ilisema wakati Waziri Mkulo ametamka bungeni kuwa, Serikali imetenga shilingi bilioni 537 kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini , upembuzi wa kambi ya upinzani kwenye vitabu vya bajeti (Namba II NA IV) umebaini kuwa, Wizara hiyo imetengewa shilingi Milioni 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58.
“Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi kawaida shilingi Milioni 76, 953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya maendeleo zimetengwa shilingi Milioni 325, 448,137,000.
Shilingi Bilioni 325 zimetengwa katika bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa megawati 160, 100 Dar es Salaam na 60 Mwanza”alisema Zitto. Kwa mujibu wa Zitto hakuna ongezeko halisia lililofanyika.
Alisema, bajeti iliyopita ilikuwa shilingi Trilioni 11.6 wakati mwaka huu wa 2011/12 Serikali ina bajeti ya jumla ya shilingi Trilioni 13.525.
Kati ya fedha hizo za mwaka 2011/2012 kiasi cha shilingi Trilioni 1.901 ambazo ni sawa na 14.06% ya bajeti yote kitatumika kulipia deni deni ka taifa.
“Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya kuendesha serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zitabaki kuwa ni kiasi cha shilingi Trilioni 11.624 ambazo ni sawa na fedha za bajeti ya mwaka uliomalizika wa 2010/2011 (japo thamani ya shilingi imenguka ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2010/2011)”, alisema Zitto.
Alisema, wakati Mkulo akisema bungeni kuwa bajeti ya mwaka 2011/2012 itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa Serikali wa kudhibiti matumizi bajeti ya Serikali imetenga shilingi Trilioni 0.987 ambazo ni sawa na asilimia 13 ya bajeti yote ya Serikali kwa ajili ya kulipa posho chini ya vifungu vinavyojulikana kama “personnel allowances (non-discretionary na In-kind”).
Zitto alisema, wakati waziri akisema ili kudhitibi matumizi serikali itapunguza posho mbalimbali Waziri Mkulo amependekeza kufanywa kwa marekebisho ya sheria ya kodi ya mapato sura ya 332 na anasema “kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa Serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali.
Kwa mujibu wa Zitto, Serikali katika bajeti yake rasmi imeamua kufanya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani sura ya 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati wa kuendesha gari yaani (Traffic Notification Fee), kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 300,000.
Lakini waziri Mkulo katika hotuba ukurasa wa 74 alitamka kuwa serikali itaongeza kiwango cha faini hadi shilingi 50,000.
“Ni dhadhiri kuwa kauli ya Waziri ya kusema faini itafikia 50,000 wakati kwenye vitabu rasmi vya bajeti faini hiyo inaonekana itafikia 300,000, “alisema Zitto.
Zitto alidai kuwa, Kambi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na kushangazwa na hatua ya Serikali kutenga zaidi ya robo ya ya bajeti kulipa madeni na kulipana posho (asilimia 27-14% kulipa madeni na 13% kulipa posho mbalimbali).
No comments:
Post a Comment