Tuesday, June 28, 2011

Mukama-Mafisadi CCM lazima wavue gamba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, amesema yeye ni sawa na mtu aliyeteuliwa kufanya kazi ya kunyonga mkosaji aliyehukumiwa adhabu hiyo na Mahakama, hivyo hawezi kuogopa kutekeleza hukumu hiyo.

Akifafanua kauli hiyo jana mjini Morogro, Mukama alisema uamuzi wa ngazi za juu wa CCM ukishatolewa kuhusu kuvua gamba watuhumiwa wa ufisadi, hakuna kiongozi atakayepuuza kuutekeleza.

“Ufisadi unasemwa dhahiri na wananchi kwa kuwataja watuhumiwa hadharani wakiwahusisha ana EPA (Akaunti ya Malipo ya Nje ya Benki Kuu), Dowans, ununuzi wa rada na Richmond … na vikao vya chama vimetoa uamuzi.

“Kilichobaki ni utekelezaji tu…na hukumu ikishatolewa na Mahakama hakuna njia nyingine isipokuwa kutekeleza agizo hilo,” alisema Katibu Mkuu huyo alipokuwa akizungumzia madai, kwamba anaogopa kutoa barua za kujivua gamba kwa watuhumiwa wa ufisadi.

Akihutubia mahafali ya wanafunzi wanachama wa CCM wanaomaliza Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Mukama alisema hataogopa kusimamia kikamilifu uamuzi wa chama hicho wa kuwatosa watuhumiwa hao.

Alisema vitendo vyao vimesababisha CCM na Serikali ichafuke mbele ya Watanzania.

Mbali na kuwavua gamba, Mukama alisema CCM pia itashughulikia suala la wafanyabiashara wasio waadilifu wanaojipenyeza ndani ya chama hicho, na itapambana na saratani ya kujilimbikizia madaraka na kukiondoa chama hicho katika utegemezi wa matajiri na wahisani wanaokiweka pabaya.

Alisema, hakuna mwananchi asiyejua kuwa ndani ya CCM wapo viongozi wenye nyadhifa kubwa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kuanzia wa EPA, Richmond, Dowans, Rada na kashfa nyingine.

Katibu Mkuu huyo alisisitiza kwamba ili kukisafisha chama hicho mbele ya jamii na kukifanya kikubalike katika uchaguzi wowote, ni lazima watuhumiwa hao watoswe ili kurudisha imani kwa Watanzania.

Mukama alionesha katuni aliyodai imemchora hivi karibuni, akiwa na barua mkononi ikionesha kuwa ameshindwa kutoa uamuzi na kusisitiza kuwa uamuzi huo ni wa chama, hivyo utatekelezwa kama ilivyopangwa.

Awali katika risala ya wanafunzi hao, walitaka viongozi wote wa CCM kujikita kuwaletea maendeleo wananchi, ili baadaye wapimwe kwa kazi zao.

Wanachama hao waliwataka viongozi wahubiri amani badala ya kuendeleza malumbano na vyama vya upinzani na kuwataka watumishi wa Serikali kuachana na siasa wakati wakiwa watumishi wa umma.

No comments: