Tuesday, October 27, 2009

'Vituko, uzembe vilitawala Uchaguzi Serikali za Mitaa’

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani amekiri kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika juzi ulitawaliwa na vituko, uzembe, vurugu za makusudi na mtu mmoja kujeruhiwa kwa risasi kwa bahati mbaya pamoja na uchaguzi huo kwenda vizuri.

Aidha, katika hatua nyingine matokeo ya awali yanaonesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kwa asilimia kubwa katika mikoa mingi nchini.

Kombani ambaye alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, alisema vurugu na vituko vilivyotokea katika maeneo mengi ni pamoja na baadhi ya watu kwa makusudi kukimbia na masanduku ya kura.

Alisema pamoja na vurugu hizo, uchaguzi huo katika wilaya 131 ulimalizika salama isipokuwa Kilwa ambayo kutokana na uzembe wa Mkurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya hiyo, vifaa vilichelewa kusambazwa kwenye vituo na hivyo wananchi wa wilaya hiyo kulazimika kupiga kura jana na leo.

“Yaani mpaka saa saba mchana jana (juzi), masanduku yalikuwa hayajafika katika vituo, hii yote ni kutokana na uzembe wa huyu Mtendaji kwani tulishampa masanduku hayo tangu Oktoba mosi mwaka huu, pamoja na fedha za uchaguzi ambazo zilipelekwa Septemba 11,” alisema Kombani.

Akizungumzia vituko na vurugu alisema katika Mkoa wa Mwanza, mtu mmoja alipigwa risasi kwa bahati mbaya na polisi, baada ya kutokea vurugu na askari huyo wakati akituliza ghasia hizo, akafyatua risasi hiyo ambayo ilimpata na kumjeruhi.

Pamoja na hayo, pia Kombani alisema katika wilaya za Rufiji, Kahama, Kilindi na Geita, baadhi ya watu walikamatwa na polisi baada ya kupora masanduku ya kura na kukimbia nayo, muda mfupi kabla ya matokeo kutangazwa.

“Yaani ilikuwa ni vituko, kwa mfano Kilindi, wakati masanduku ya kura yapo tayari kusomwa, walitoka watu na kupora masanduku hayo na kukimbia nayo, lakini kwa bahati nzuri walikimbizwa na polisi na kukamatwa, hii ni dalili kuwa kuna kundi la watu lilidhamiria kufanya fujo,” alisema.

Alisema pamoja na vurugu hizo, katika Wilaya ya Geita, mgombea wa CUF alinusurika kifo baada ya kuokolewa na polisi baada ya kutaka kujinyonga kutokana na kushindwa katika uchaguzi huo hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Simon Sirro, alisema bado hajapata taarifa za tukio hilo.

Alisema hata hivyo kuna baadhi ya vyama kikiwamo CUF katika baadhi ya maeneo vilikataa matokeo.

“Ila sisi tunawaambia kuwa ni ruksa kwao kwenda mahakamani ndani ya siku 30 baada ya uchaguzi.”

Kwa upande wa vyama vya upinzani vimeendelea kulalamika na kudai kuwa CCM ilishirikiana na watendaji wa ofisi za wakurugenzi na wilaya kuwahujumu wakati chama hicho cha CCM chenyewe kilisema kushinda katika maeneo mengi kunaonesha vyama vya upinzani vimedorora zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema wa Wilaya ya Kinondoni, John Mnyika, alisema wagombea walioonekana kuwa tishio walienguliwa kwa madai wamedhaminiwa na kata.

Baadhi ya maeneo ambayo walienguliwa ni Sinza B, Sinza C na mitaa ya wilaya yote ya Handeni na Nkasi.

"Sisi tunaamini serikali imevuruga uchaguzi huu na watu waelewe kuwa matokeo ya uchaguzi huu si kipimo cha uchaguzi mkuu, huu ni uchaguzi wa ovyo ovyo tu, kwa sababu umesimamiwa na halmashauri lakini uchaguzi mkuu utasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

“Hata hivyo tumeona asilimia 30 ya kura hadi sasa tumepata Chadema hivyo tumepanda, mfano Wilaya ya Kinondoni tumeshinda mitaa ya Bunju A na B, Makoka na Ali Maua A”, alisema.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alilaumu ofisi za wakuu wa wilaya kuwa zilitumika kuharibu uchaguzi huo na kuahidi kwenda mahakamani kushtaki maeneo ambayo walionewa.

“Tukishafanya tathmini na kuona maeneo tuliyoonewa, tutakwenda mahakamani kufungua kesi kwa hujuma za maeneo hayo pekee, kwa sasa Kasulu kati ya mitaa 48 tumeshashinda 12 na Nguruka kati ya mitaa 14 tumeshinda minane”, alisema.

Naibu Mkuu wa Propaganda wa CCM, Tambwe Hiza, alisema chama chake kilitarajia kusikia malalamiko kutoka Upinzani kutokana na tabia ya kulaumu pindi wanaposhindwa.

Hiza alisema matokeo ya uchaguzi huo ambapo CCM imeshinda katika maeneo mengi yamethibitisha kuwa upinzani umerudi nyuma zaidi ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita na kuongeza: “Mfano Chadema kwa Dar es Salaam wameshindwa kusimamisha wagombea kwa asilimia 85”.

Alisema “ushindi huu unaonesha uchaguzi mkuu mwakani CCM haitapata ushindani mkubwa”.

Naye Martha Mtangoo, kutoka Dodoma anaripoti kuwa CCM mkoani humo imeshinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa asilimia 82 katika vijiji, mitaa na vitongoji mbalimbali. Taarifa za matokeo ya awali iliyotolewa jana mjini hapa na Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kapteni mstaafu John Barongo, zilieleza kuwa katika Wilaya ya Bahi chama hicho kilishinda kwa asilimia 100 ambapo kati ya vijiji 56 imeshinda vijiji vyote na vitongoji 514 imeshinda vitongoji 508 ambapo bado taarifa za vitongoji vingine bado hazijapatikana.

Naye John Nditi, kutoka Morogoro anaripoti kuwa wanachama CUF Morogoro Mjini juzi usiku walikesha wakishangilia ushindi wa wenyeviti na wajumbe wa mitaa ya kata chache walizoshinda mjini humo ambapo chama hicho kilipata ushindi katika mitaa ya Unguu A na Manzese.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Raphael Ndunguru, alisema CUF katika uchaguzi huo ilitwaa mitaa 10, TLP minne na Chadema mmoja na kufanya idadi ya mitaa 15 wakati CCM ikishinda mitaa 259 kati ya 274.

Mugini Jacob kutoka Tarime anaripoti kuwa matokeo ya awali ya uchaguzi huo yanaonesha kuwa CCM iliibuka mshindi wilayani humo baada ya kutwaa viti 57 vya serikali za vijiji sawa na asilimia 78 huku Chadema ikiambulia viti 16 wakati katika mamlaka ya Mji wa Tarime CCM ilishinda viti 10 Chadema vinne.

Naye Anna Makange kutoka Tanga anaripoti kuwa matokeo ya uchaguzi huo yanaonesha CCM iliongoza kwa kupata mitaa 65 sawa na asilimia 74.7, CUF 22 sawa na asilimia 25.3 katika mitaa 87 iliyomo kwenye kata hizo na upande wa wenyeviti wa vijiji CCM ilipata viti saba sawa na asilimia 87.5, CUF kimoja sawa na asilimia 12.5 katika vijiji vyote vinane vilivyomo kwenye kata hizo 12.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Majuto Mbuguyu, kwenye ngazi ya vitongoji CCM pia iliongoza kwa kunyakua viti 18, CUF kitongoji kimoja na TLP kimoja cha uenyekiti katika vitongoji 20 vilivyomo kwenye kata hizo 12.

Naye Juma Nyumayo kutoka Songea anaripoti kuwa CCM mkoani humo pia iliongoza ambapo wagombea wake katika viti vya mitaa katika Manispaa ya Songea walishinda viti 63 kati ya 71 sawa na asilimia 89 ambapo Chadema na CUF vilijipatia viti vinane ikiwa ni ongezeko la viti sita ikilinganishwa na uchaguzi uliopita.

Bunge lamuapisha mrithi wa Mwanyika

BUNGE la Tanzania limemuapisha, Frederick Werema, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Werema ameapishwa leo saa tatu asubuhi hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania amekuwa sehemu ya Bunge.

Werema ameapa kuwa atakuwa muaminifu kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ataitumikia kwa moyo wake wote, ataihifadhi, atailinda, na kuitetea Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua Werema kuchukua nafasi ya Johnson Mwanyika.

MKUTANO wa 17 wa Bunge la Tanzania umeanza leo mjini Dodoma.

Monday, October 26, 2009

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA KIZAAZAA!

Wakati zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji likielezewa kwa ujumla wake kuwa limefanyika jana kwa amani nchini kote, hali ilikuwa tofauti katika baadhi ya maeneo ambapo kumeripotiwa kuibuka kizaazaa cha aina yake kutokana na vurugu, visa na vibweka vya kila namna.

Taarifa ambazo Alasiri imezipata toka kwa waandishi walio maeneo mbalimbali, zimeeleza kuwa katika baadhi ya maeneo, watu kadhaa wametiwa mbaroni kutokana na vitendo vya kutimka na masanduku ya kura na wengine wamedaiwa kuchanachana karatasi hizo za kura.

Aidha, kwenye baadhi ya vituo, polisi walilazimika kuingilia kati na kuwatuliza watu kwa risasi za moto na mabomu ya machozi, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa hakuna anayediriki kuharibu amani na utulivu wakati wa ukamilishaji wa zoezi hilo la kusaka wenyeviti na wajumbe wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Kwa ufupi, baadhi ya matukio yaliyozua kizaazaa ni kama yafuatayo:

Mabomu, risasi

Katika eneo la Kawe Ukwamani Jijini Dar es Salaam, askari wa jeshi la polisi walilazimika kutumia risasi za moto na pia kumwaga mabomu kadhaa ya machozi kutokana na vurugu zilizodaiwa kuanzishwa na shabiki mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa zinadai kuwa vurugu hizo zilizotokea katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Ukwamani, zilitokana na balaa lililoanzishwa na kijana huyo aliyefahamika kwa jina moja la Azimio, ambaye baadaye aliwafanya wafuasi wa vyama vyote vitatu vya CCM, CUF na CHADEMA kuzua vurugu kituoni hapo huku wengine wakichapana makonde kavukavu.

Hali hiyo iliyojiri mishale ya saa 12:00 jioni, iliwafanya polisi kuingilia kati na hatimaye kutembeza risasi hewani na kisha kumwaga mabomu kadhaa ya machozi.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mark Kalunguyeye, amethibitisha tukio hilo na kueleza zaidi kuwa hadi sasa, wanamshikilia mtu mmoja kutokana na tukio hilo.

Aidha, tukio jingine la kutembezwa kwa risasi za moto limeripotiwa kutokea Jijini Mwanza, ambapo mtu mmoja amejeruhiwa vibaya na kukimbiziwa hospitalini.

Taarifa hizo zilizothibitishwa leo asubuhi redioni na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serrikali za Mitaa, Bi. Celina Kombani, zinaeleza kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baadhi ya wananchi kuzua vurugu kituoni na kuwafanya polisi waingilie kati kwa kupiga risasi kadhaa hewani.

Hata baada ya risasi kupigwa hewani, baadhi ya wananchi hao walikaidi, hivyo polisi kujikuta wakimjeruhi mmoja wa wafanya fujo hao ambaye amekimbiziwa hospitalini.

Watu wasepa na masanduku

Kizaazaa kilichotokana na baadhi ya watu kukimbia na masanduku ya kura kimeripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini, ikiwa ni pamoja na kule Kilwa mkoani Lindi na Rufiji mkoani Pwani.

Taarifa za Kipolisi toka Lindi zinaeleza kuwa watu watatu wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kupora masanduku hayo ya kura na kutimka nayo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Sifuel Shirima, amesema tukio hilo limetokea jana saa 7:30 mchana katika kitongoji cha Mnazi Mmoja, eneo la Kilwa Masoko.

Amewataja watu wanaoshikiliwa kutokana na tukio hilo kuwa ni Haji Mponda Yahaya,18, Shaibu Abdulrahman Kandililo,18 na Haruni Makangala ,18.

Aidha, akasema kule Lindi Vijijini, nako kuna watu kadhaa wanasakwa kwa tuhuma za kuvunja masanduku ya kupigia kura na kuchana chana karatasi zote za kura zilizokuwamo ndani yake.

Amesema watu hao walifanya tukio hilo usiku wa kuamkia leo na hadi sasa wanaendelea kusakwa.

Nako Rufiji, kumeripotiwa tukio la baadhi ya watu kutimka na masanduku ya kura.

Imedaiwa kuwa hali hiyo ilitokea baada ya baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi, mawakala wa vyama, polisi na wapiga kura wasiojua kusoma na kuandika kutofautiana juu ya utekelezaji wa zoezi hilo la upigaji kura.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Kassim Majaliwa, amethibitisha juu ya kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilijiri katika kituo kimoja cha Kata ya Mgomba.

Imedaiwa kuwa baadhi ya wapiga kura wasiojua kusoma na kuandika katika eneo hilo waliomba kusaidiwa, na ndipo mawakala wa vyama walipotaka kuifanya kazi hiyo ya kuwapigia kura watu walioamini kuwa ni wafuasi wao.

Ikadaiwa kuwa jambo hilo lilizua ubishani mkali baina ya wasimamizi, polisi na mawakala wa vyama, hali ambayo baadaye ilitoa mwanya kwa baadhi ya watu kutwaa masanduku na kutimka nayo.

"Baada ya kutokea kutoelewana, ndipo baadhi ya watu walipovamia na kuchukua kura zilizopigwa na wengine kukimbia na masanduku ya kura," amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Majaliwa.

Saturday, October 24, 2009

Chagueni waadilifu, wachapakazi

UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa utafanyika kote nchini Jumapili ya wiki hii. Kwa mara nyingine mustakabali wa taifa letu utakuwa kwenye sanduku la kura.

Uchaguzi wa safari hii ni muhimu pengine kuliko chaguzi nyingine zilizopita. Tunaamini hivyo kwa sababu huu wa safari hii unafanyika wakati nchi yetu ikipitia kipindi kigumu na cha majaribu makubwa.

Si tu kwamba nchi yetu, hivi sasa, inatikisika kutokana na kushamiri kwa ufisadi nchini, lakini pia pengo kati ya matajiri na masikini linazidi kukua kwa kasi, na hivyo kutishia amani ya taifa letu.

Si siri vilevile kwamba nchi yetu imefikia hapa ilipo kwa sababu ya kuwa na viongozi dhaifu na waroho wa pesa kuanzia ngazi za chini kabisa hadi juu.

Viongozi hao dhaifu na waroho wa pesa wamefanikiwa kukamata madaraka baada ya kuwahadaa wananchi masikini kwa kuwapa vijisenti, khanga, fulana, kofia na hata wakati mwingine pilau tu! Kwa maneno mengine, wameutumia umasikini na ujinga wa wananchi kuingia madarakani.

Uzoefu umetuonyesha kwamba viongozi wa namna hiyo wanapoingia madarakani hujishughulisha tu na ufisadi na huitelekeza kabisa agenda ya maendeleo; kwa sababu wanajua kwamba uchaguzi mwingine utakapowadia watawaendea tena wapiga kura na kuwahadaa kwa vijisenti, fulana, khanga, kofia na pilau.

Kwa hiyo, kama hakuna maendeleo ya maana yanayoonekana katika mitaa yetu na vijiji vyetu, ni kwa sababu ya kuwaingiza madarakani viongozi dhaifu wa sampuli hiyo.

Ni mpaka hapo tutakapouvunja mzunguko huo wa kijinga kwa kukataa kuuza kura zetu kwa fulana, khanga, kofia na pilau; ndipo tutakapoweza kuwaweka madarakani viongozi waadilifu na wachapakazi wanaoweza kuchochea maendeleo na kuleta mabadiliko ya kweli mitaani mwetu na katika vijiji vyetu.

Ni kwa msingi huo, tunawasihi wapiga kura kutumia busara katika uchaguzi huo wa Jumapili. Wakipiga kura zao kwa busara wanaweza kuleta mapinduzi ambayo tumeyasubiri kwa muda mrefu sasa.

Tukumbushe tu kwamba kupiga kura si mchezo. Kupiga kura kunahitaji upembuzi yakinifu wa kila mgombea.

Tunawasihi wapiga kura hiyo Jumapili wasibweteshwe na vyama vyao; maana matatizo yao ni zaidi ya siasa za vyama. Wamchague mgombea aliye bora; na haijalishi ni wa CHADEMA, CUF au CCM.

Tunawasihi wajiridhishe kwamba huyo wanayempigia kura ndiye haswa anayefaa kuwaongoza; hata kama walipewe vijisenti, khanga,fulana au pilau na mgombea mwingine. Kila la heri.

Source:www.raiamwema.co.tz

Siri mpya ya ufisadi Benki Kuu yaanikwa

-Yahusisha mabadiko yaliyofanywa na Dk. Rashid

WARAKA unaoonyesha siri ya matukio ya ufisadi ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umepatikana ukionyesha kwamba, sehemu kubwa ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani walitokana na mabadiliko yaliyofanywa na aliyekuwa Gavana, Dk. Idris Rashidi.

Kwa mujibu wa waraka huo na maelezo kutoka kwa baadhi ya watumishi wa BoT, mabadiliko hayo yaliingiza timu mpya ambayo sehemu kubwa ni wale ambao wamehusishwa katika matukio ya ufisadi.

Baadhi ya watumishi wa BoT waliozungumza na Raia Mwema kwa nyakati tofauti wiki hii, wamesema matukio mengi ya kifisadi yalianza kufanyika mara baada ya mwaka 1994, kipindi ambacho timu mpya ya Dk. Rashidi ilianza kazi.

“Kwa muda wote tuliokuwa kazini tulikuwa tukisumbuliwa sana na wafanyabiashara na wanasiasa ambao sasa ndio tunawasikia wakiitwa mafisadi na ukiangalia utaona mahusiano yao na timu mpya yalikuwa makubwa sana na hata utajiri na umaarufu wao ulianza kipindi hicho,” anaeleza mstaafu mmoja wa BoT aliyekuwa kitengo nyeti.

Miongoni mwa walioingizwa katika timu mpya ya Dk. Rashidi iliyotangazwa rasmi Desemba 22, 1993 ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, ambaye kabla ya kuazimwa Hazina, alikuwa BoT kama Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha.

Mgonja na waliokuwa mawaziri wake wawili, Basil Mramba na Daniel Yona, wameshitakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi wakidaiwa kutumia vibaya nafasi zao kuhujumu serikali kwa kuisamehe kodi kampuni ya uhakiki wa hesabu za madini ya Alex Stewarts.

Wengine ambao walikuwamo katika timu mpya ya Dk. Rashidi ni Bosco Kimela ambaye pamoja na wenzake ameshitakiwa katika kesi ya wizi wa fedha kutoka katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Katika orodha hiyo ya timu ambayo Dk. Rashidi aliingia nayo BoT yumo Amatus Liyumba, ambaye baadaye alibadilishwa kitengo na kwa sasa ni mmoja wa watuhumiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayohusishwa na ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo.

Kesi nyingine ambayo inamuingiza ofisa aliyekuwa katika timu mpya ya Dk. Rashidi ni inayohusu zabuni ya uchapishwaji wa noti iliyoiingizia BoT hasara ya Sh bilioni 104, ikimhusisha Simon Jengo, aliyekuwamo katika timu mpya pamoja na mtuhumiwa mwingine Bosco Kimela.

Mbali ya walioshitakiwa, wamo baadhi ya watu ambao kwa sasa wametajwa kuwa mashahidi katika kesi ya EPA na inaelezwa kwamba orodha inaweza kuongezeka ama hata mashahidi wakaingizwa na kuwa washitakiwa kulingana na muendelezo wa ushahidi na uchunguzi.

Mashahidi hao ambao wametokana na timu mpya ya Dk. Rashidi ni pamoja na Athumani Mtengeti, Peter Noni, Emmanuel Boazi na Stela Chaula, ambao baadhi wanaelezwa kwamba ni watendaji waaminifu na baadhi wanatajwa tajwa kuwa na mahusiano na watuhumiwa wa ufisadi.

Maofisa waliozungumza na Raia Mwema kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na sababu za kiusalama, walisema pamoja na kuwapo kwa watendaji safi waliongia katika timu mpya ya Dk. Rashidi, kulikuwa na mikakati maalumu ya wafanyabiashara na wanasiasa waliokuwa na malengo maalumu ndani ya BoT.

Dk. Rashidi aliingia BoT akichukua nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Gilman Rutihinda aliyekuwa Gavana kati ya mwaka 1989 hadi 1993, alipoaga dunia.

Source:www.raiamwema.co.tz

Friday, October 23, 2009

Shahidi amkaanga Liyumba

SHAHIDI wa kwanza katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Benki Kuu Tanzania (BOT), Amatus Liyumba, amesema, mshitakiwa huyo alikuwa akifanya mabadiliko ya ujenzi wa jengo la BoT bila kuwahusisha wakurugenzi wa bodi kwenye taasisi hiyo ya Serikali.

Shahidi huyo kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Sief Mohamed (49) ameieleza mahakama kuwa, nakala ya mkataba wa ujenzi wa majengo hayo unaonyesha kipengelea kinachoeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unaweza kubalidika wakati wowote kutokana na thamani halisi ya fedha kwa wakati huo.

Mohamed alieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, Liyumba aliandika barua inayoagiza ujenzi wa upanuzi wa majengo pacha uendelee,na kwamba wajumbe wa bodi waliidhinisha ulipaji wa fedha za ujenzi huo.

Liyumba anadaiwa kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 221.

Amesema, uchunguzi aliofanya umebainisha kwamba, kulingana na mkataba,ujenzi wa majengo hayo 14 ungegharimu Dola milioni 73.6 za Marekani lakini kulingana na mabadiliko ya ujenzi huo, kulikuwa na nyongeza ya Dola milioni 253.9 za kimarekani, hivyo kwa ujumla ujenzi umegharimu dola milioni 357.7 za Marekani.Mohamed amesema, cha kushangaza, ghorofa zilizojengwa katika benki hiyo ni 18 badala ya 14, na kwamba, zimeongezeka ghorofa nne.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, ghorofa zilizoongezeka hazikuwa kwenye mkataba uliosainiwa kati ya BoT na kampuni ya Afrika Kusini iitwayo Group 5 East (PTY) Ltd.

Mohamed alizitaja sehemu za majengo hayo zilizoongezeka kuwa ni kiwanja cha kutua Helkopta, kuta za majengo zilizonakshiwa, minara miwili, vigae vya ukumbi wa mikutano pamoja na sehemu za ukuta wa uzio.

Amesema, badala ya rangi ya kawaida wameweka plasta, na kwamba,vitu hivyo vilivyoongozeka havikuwa kwenye mkataba halisi wa ujenzi wa majengo hayo pacha.

Mohamed ameieleza mahakama kuwa, ana barua za Liyumba zinazoonyesha kutoa maagizo ya ujenzi huo kwenda kwa bodi ya BOT kuiomba iidhinishe gharama za ujenzi huo lakini barua hizo hazionyeshi ni kiasi gani alichokuwa akikiomba.

Wakili Upande wa Utetezi, Majura Magafu, alimtaka Mohamed aonyeshe mahakamani hapo barua anazodai Liyumba alikuwa akiandika kwenda kwa Bodi ya Wakurugenzi BOT inayotaka waridhie ujenzi wa jengo hilo na malipo yafanyike baadaye.

Mohamed alishindwa kutoa nakala ya barua hiyo kwa madai hakuwa nayo mahakamani hapo, na kwamba, shahidi mwenzake atazitoa mahakamani hapo akija kutoa ushahidi wake kama zikitakiwa.

Magafu alimuuliza Mohamed kwamba, Liyumba alikuwa na mamlaka gani ya kutaka majengo hayo yaongezeke bila bodi kufahamu.Shahidi huyo aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa kuna barua zinazoonyesha Liyumba alikuwa akiiamuru bodi hiyo kuruhusu ujenzi uendelee.

Magafu alizidi kumbana shahidi huyo kwa kumwambia inakuwaje Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi aamuru Ujenzi wa BoT uendelee bila kupitia kwenye bodi na kusababisha hasara wakati jengo ni zuri na linaendelea kutumiwa.

Magafu: Hivi umekuja kucheza mpira au kutoa ushahidi kama Liyumba aliiba au la,sema ukweli kama wewe ni mchunguzi na si kusema uongo, ni kweli Liyumba amesababisha hasara mnayodai au ni chuki zenu?

Mohamed : Mahakama ndio itajua kama kweli kasababisha hasara au la, ila kuna baadhi ya mambo aliyafanya bila idhini ya Bodi.

Magafu: Je unadai katika barua alizoandika Liyumba hakuna sehemu inyoonyesha aliomba kiasi gani cha fedha sasa hapa anashitakiwa kwa kosa gani wakati jengo ndiyo lile mnaliona ni zuri na linatumika, huoni kama ushahidi unaoutoa mahakamani hapa si wa kweli, na kwa nini BoT iliamuru ujenzi wa ghorofa hizo uongezwe.

Mohamed : Yawezekana waliamua kuongeza ujenzi huo kwa sababu ya ongezeko la wafanyakazi ,nakubali jengo ni zuri lakini halikuwa kwenye makubalino ya mkataba.

Magafu: Kwa nini mlipoanza uchunguzi wenu msimuhoji aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Balali ambaye hivi sasa ni marehemu na angeeleza ukweli wa majengo hayo na kutaja nani alihusika badala yake mnadai Liyumba anahusika wakati hakuwa mjumbe wa bodi, pia ni kwa nini maelezo ya awali yapishane na kiasi cha fedha cha sasa unachosema.

Mohamed:Kimya

Baada ya mawakili kumaliza kumhoji Shahidi huyo, jopo la mahakimu likiongozwa na Hakimu Edson Mkosinongwa, walimuuliza Mohamed Liyumba anashitakiwa kwa kosa lipi kati ya kuongeza jengo au yawezekana amenufaika kwa kitu chochote.

Mohamed alijibu hawezi kufahamu Liyumba ana kosa gani lakini ushahidi utaonyesha kama ana kosa au la kwa sababu hana chuki nae.

Wakati mwingine Mohamed alikuwa akiulizwa maswali ambayo yalikuwa yakimtatiza na kuwafanya baadhi ya ndugu waliokuwa mahakamani hapo kuanguka kicheko na wengine kuguna kutoka na kubanwa na mawakili upande wa utetezi kwa sababu ya majibu yake kujichanganya hali iliyomlazimu wakili wa Serikali, Juma Ramadhani kuingilia kati na kusaidia baadhi ya ushahidi kwa kumuuliza maswali Mohamed ili yarekodiwe vizuri na kutumika wenye mwenendo wa kesi hiyo.

Mei 28 mwaka huu, Liyumba alipandishwa kizimbani kujibu mashitaka mawili likiwemo kuhusika katika ujenzi wa ghorofa pacha za makao makuu ya BoT, akidaiwa kupandisha gharama. Kesi hiyo ina mashahidi 10 wakiwemo maprofesa watatu.

Thursday, October 22, 2009

Albino mwingine auawa Geita

Kunako majira ya saa 2:30 usiku oktoba 20 mwaka huko wilayani Geita katika kijiji cha mwamwilila kuna taarifa watu wawili wasiojulikana wamevamia nyumbani kwa Elikana kaswahili na kumshambulia kwa mapanga na kisha kumkata mapanga mwanae Gasper Elikana (10) na kumuua kisha kukata mguu na kuondoka nao.

kaimu kanada wa polisi elias kalinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa jeshi lake limetangaza dau la milioni moja kwa atakaesaidia kukamatwa kwa waalifu hao.

Wednesday, October 21, 2009

TEMCO TO OBSERVE VOTER REGISTRATION IN ZANZIBAR

The Tanzania Election Monitoring Committee (TEMCO) has deployed a team to observe voter registration and updating of the voter register on both Unguja and Pemba in Zanzibar.
Free and Fair elections are a cornerstone of democracy and this exercise will assess the transparency and fairness of election processes. TEMCO represents local Civil Society Organizations (CSOs) and has been monitoring general elections and by-elections in Tanzania since 1995.

The TEMCO observation team begun working in Zanzibar on the 10th of October, and observation of voter registration will continue for five months. The team includes two zone coordinators, two district coordinators and eight voter registration observers.
The Committee will observe the registration and updating of the voter register in each constituency according to the registration schedule established by the Zanzibar Electoral Commission (ZEC).

Election observing results will be published in a monthly Newsletter distributed to ZEC, political parties, Government institutions and other stakeholders. A dissemination workshop for stakeholders will be held following the conclusion of voter registration to discuss TEMCO’s findings and a final report on the voter registration and updating of the voter register will be distributed prior to the 2010 general elections.

TEMCO has received support for observation of voter registration and updating of the voter register from the American people through the United States Agency for International Development (USAID) and has received permission to observe voter registration from the Zanzibar Electoral Commission (ZEC).

TANZANIA ELECTION MONITORING COMMITTEE (TEMCO)
P. O. BOX 35039
DARES SALAAM
TEL. 255-22-2410207 FAX: 255-22-2410084

Tuesday, October 20, 2009

Shahidi kesi ya Liyumba mgonjwa

WATU wengi leo walitarajia kuanza kufahamu undani wa kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, lakini sasa itabidi wasubiri hadi Oktoba 22.

Upande wa mashitaka ulitarajiwa kuanza kutoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, haukufanya hivyo kwa madai kuwa shahidi wa kwanza anaumwa.

Mahakama hiyo imefahamishwa kuwa, shahidi huyo alianza kuumwa tumbo ghafla leo asubuhi wakati anajiandaa kwenda mahakamani.

Wakili upande wa Serikali, Juma Ramadhan, amedai mahakamani kuwa, shahidi (hakumtaja jina) aliyestahili kuanza kutoa ushahidi wake aliumwa tumbo ghafla na akaomba kesi iahirishwe kwa siku mbili ili apate nafuu.

“Kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuanza kutolewa ushahidi lakini shahidi wetu ameugua tumbo ghafla asubuhi hii wakati akijiandaa kuja kutoa ushahidi wake mahakamani hivyo tunaomba mahakama ipange tarehe nyingine ili shahidi wetu aweze kuja kuanza kutoa ushahidi wake”.

Wakili upande wa Utetezi, Majura Magafu, amesema upande wa mashitaka katika kesi hiyo unapaswa kuhakikisha kwamba unaanza kutoa ushahidi katika tarehe itakayopangwa kwa kuwa mteja wao anaendelea kusota rumande.

Magafu kama shahidi huyo ataendelea kuumwa, upande wa mashitaka utafute shahidi mwingine atakayeweza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.

Hakimu, Edson Mkasimogwa, ameuagiza upande wa mashitaka uhakikishe kwamba unakuwa na shahidi mahakamani Oktoba 22 ili kesi hiyo ianze kusikilizwa. Upande wa mashitaka una mashadihi 10 wakiwemo maprofesa watatu.

Mashahidi hao ni Mwanasheria wa BoT, Bosco Kimela, ambaye pia anakabiliwa na mashitaka ya kuidhinisha malipo kwa kampuni zilizochota fedha Katika Akaunti ya Malipo ya Nje iliyokuwa BOT, na kesi nyingine ya kuhujumu uchumi.

Maprofesa wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo ni Profesa Letice Rutashobya, Profesa Bruno Ndunguru, na Profesa Joseph Semboja.

Mashahidi wengine ni Michael Shirima, Seif Mohamed, Elisa Msangya, Jafar Uledi, Julius Ngelo na Yusto Tongola. Mei 28 mwaka huu, Liyumba alipandishwa kizimbani kujibu mashitaka mawili likiwemo kuhusika katika ujenzi wa ghorofa pacha za makao makuu ya BoT, akidaiwa kupandisha gharama.

Ameshitakiwa akidaiwa kutumia vibaya madaraka aliyokuwanayo na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 221.

Ofisa wa Bunge adaiwa kuchota sh milioni 70

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini kuwa Msaidizi wa Spika wa Bunge, Christopher Ndallo, amechukua sh milioni 70 kwa safari zake za ndani na nje ya nchi bila nyaraka zozote.

Aidha, PAC imetoa miezi sita kwa Ofisi ya Bunge kutoa vielelezo vya msingi kuhusu mkataba wa ukarabati wa ofisi ndogo ya Bunge, Dar es Salaam, unaodaiwa kugharimu Sh bilioni 1.1, tofauti na makubaliano ya awali yaliyoanzia Sh milioni 425 na kwamba kinyume na hivyo, wahusika lazima warudishe fedha hizo.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam, katika kikao cha Kamati hiyo, wakati Ofisi ya Bunge ilipokuwa ikitoa maelezo ya hesabu zake za mwaka 2006/07 na 2007/ 08 zilizopata hati chafu.

Akielezea kuhusu Msaidizi wa Spika, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, John Cheyo, alimtaka Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, kutoa maelezo kuhusu msaidizi huyo anayedaiwa kuchukua kiwango hicho cha fedha ambazo nyaraka zake hazikuonekana.

Kwa mujibu wa Cheyo, alisema msaidizi huyo amekuwa akichukua fedha kwa ajili ya safari za ndani na nje ya nchi, lakini amekuwa harudishi nyaraka zozote zikionesha malipo halali, akamtaka Katibu wa Bunge kujibu kama huwa anapata usingizi kutokana na matukio hayo ambayo hayafurahishi.

“Kabla hatujafika mbali katika kuchambua taarifa yenu, hebu nianze kwa kuuliza, wewe Katibu, hivi huwa unalala usingizi kwa mahesabu yanayoipatia taasisi hati chafu? Jambo la kushangaza ni pale ambapo katika vitabu vyenu mmemwandikia kuwa atarudisha kwa kukatwa mshahara wake, lakini je jambo la kujiuliza analipwa shilingi ngapi hadi aweze kulipa kiwango hicho chote?,” alihoji Cheyo.

Aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha fedha, taarifa inaonesha kuwa kuna wakati msaidizi huyo alichukua zaidi ya Sh milioni 30 kwa wakati mmoja, na Kamati inahitaji kujua kiwango hicho kitarudishwaje au Bunge litaendelea kukopeshana hadi lini.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Lucy Msafiri, alisema hilo ni jambo zito na inahitaji maelezo yenye uwazi kufahamu kama fedha hizo zilichukuliwa kwa matumizi binafsi au ya Spika.

Alisema taarifa inajichanganya, kwa kuwa pengine inasema ni kwa matumizi yake na sehemu nyingine ni kwa matumizi ya Spika, sasa iweje msaidizi akatwe kwenye mshahara.

“Suala la kujiuliza yeye anahusika vipi, kwani Oktoba mwaka huu, alitakiwa kukatwa Sh milioni nane nyingine milioni 2.4 nyingine milioni 4.5 na milioni 2.6 zilizochukuliwa kwa safari za ndani na nje ya nchi,” alihoji Lucy.

Hata hivyo baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walishauri msaidizi huyo aondolewe kama hana sifa zinazostahili kwa maana ya kwamba, harudishi nyaraka jambo ambalo linaweza kumharibia Spika, akaonekana yeye ndiye aliyehusika kwa njia moja au nyingine.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa ofisi za Bunge, Cheyo alisema tangu kuanza kwa ujenzi huo, taarifa zimekuwa zikibadilika mara kwa mara tofauti na mkataba wa awali, jambo ambalo Kamati ilihitaji Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kulifanyia kazi tena.

Alisema ipo haja ya CAG kufanya hivyo kutokana na kwamba hawajaridhika na taarifa hiyo na kwamba ili kujiridhisha kwa taarifa hizo na kuona kama hakuna msukumo wowote ambao ulionekana wakati wa ujenzi huo, lazima urudiwe.

Cheyo alisema ujenzi wa mradi huo umeishtua kamati, kutokana na kuonekana na kupata hati chafu katika kipindi cha mwaka 2006/07 na pia 2007/08 hati ambazo zimekuwa zikirithiwa katika ofisi na kuifanya kuonekana kama inadidimia.

“Kwa Bunge si jambo la kuvumilia hati chafu kutokana na kwamba wamekuwa wakieleza umma juu ya madhara ya matumizi mabaya ya fedha za umma, jambo ambalo Kamati haitawavumilia wanaokiuka,” alisema Cheyo.

Alisema ujenzi wa mradi huo awali uligharimu Sh milioni 425, baadaye kuongezeka Sh milioni 388 zilizotumika kwa ununuzi wa mitambo ya umeme katika ofisi hiyo na nyingine Sh milioni 365 kwa ajili ya samani za ofisini na kwa sasa taarifa zinaonesha kufikia Sh bilioni 1.1.

Akijibu hoja hizo, Kashilila alisema jambo hilo ameliona na amekuwa akijadiliana na wenzake akisema ujenzi huo ulikuwa na sura mbili tofauti, kwani awali ilikuwa yawe maegesho ya magari na baadaye kukawa na mabadiliko ya kujenga ofisi jambo ambalo liliongeza gharama.

Hata hivyo, alisema zipo hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kudhuibiti matumizi mabaya ikiwa ni pamoja na kudhibiti usimamizi wa matumizi ya fedha, lazima kuzingatia kanuni na taratibu za fedha na manunuzi.

Aliongeza kuwa kanuni za ujenzi hazikufuatwa kwa mkataba kusainiwa Juni mwaka juzi, wakati Bodi ya Zabuni iliidhinisha Oktoba mwaka huo, kwa sababu ilionekana kuwa wasingefanya hivyo, gharama ya ujenzi ingekuwa kubwa zaidi na kuanza upya kutokana na wakandarasi kuondoka eneo la tukio.

Monday, October 19, 2009

JK ateua makatibu wakuu wanne wapya, ahamisha wawili, ateua katibu wa rais mpya

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mabadiliko katika safu ya maofisa waandamizi wa Serikali kwa kuteua Makatibu Wakuu wa Wizara wanne wapya, kuhamisha wengine wawili, na kuteua Katibu wa Rais mpya.

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Oktoba 19, 2009, Ikulu, mjini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Philemon Luhanjo, imesema kuwa Mhe. Rais Kikwete amefanya mabadiliko hayo kufuatia kustaafu kwa baadhi ya Makatibu Wakuu wa Wizara.

Aidha, taarifa inasema kuwa mabadiliko hayo yanaanza leo, Oktoba 19, 2009.

Taarifa hiyo imesema kuwa Mhe. Rais Kikwete amemteua Bwana David Kitundu Jairo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Jairo alikuwa Katibu wa Rais.

Bwana Jairo anachukua nafasi ya Bwana Arthur Mwakapungi ambaye amestaafu.

Katika taarifa yake, Bwana Luhanjo amesema kuwa pia Mhe. Rais Kikwete amemteua Bwana Sazi Salula kuwa Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Salula alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Mhe. Rais Kikwete amemteua Bwana Mbarak M. Abdulwakil aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Bwana Abdulwakil anachukua nafasi ya Bwana Patrick Rutabanzibwa ambaye anahamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kama Katibu Mkuu. Ndugu Rutabanzibwa anachukua nafasi iliyoachwa na Bi. Salome Sijaona ambaye amestaafu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mhe. Rais Kikwete pia amemteua Bwana Christopher N. Sayi kuwa Katibu Mkuu wa Wizata ya Maji na Umwagiliaji.

Kabla ya uteuzi wake, Bwana Sayi alikuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara hiyo hiyo, na anachukua nafasi ya Bwana Wilson Mukama ambaye ameanza likizo ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.

Bwana Luhanjo amesema katika taarifa yake kuwa vile vile Mhe. Rais Kikwete amemteua Bwana Sethi Kamuhanda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.

Kabla ya uteuzi wake, Bwana Kamuhanda alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Anachukua nafasi Dkt. Florence Turuka ambaye anahamishiwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kama Katibu Mkuu. Bw. Turuka anachukua nafasi ya Dkt. Naomi Katunzi, ambaye anamaliza mkataba wake wa utumishi wa Serikali mwezi ujao, Novemba, 2009.

Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi pia inasema kuwa Rais Kikwete amemteua Prosper Mbena kuwa Katibu wa Rais. Kabla ya uteuzi wake, Bwana Mbena alikuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri, na anachukua nafasi ya Bwana Jairo.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

19 Oktoba, 2009

Vijana waaswa kutumia ICT kuwa wajasiriamali

VIJANA wanapaswa kuthamini na kutumia ipasavyo ujuzi katika mafunzo ya kompyuta kwa kuwa ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha kuwa wajasiriamali.

Ofisa Elimu Mkuu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Charles Philemon, amesema, ujuzi katika nyanja mbalimbali za teknolojia ya kompyuta pia ni muhimu kwa taifa ili kukabiliana na changamoto za utandawazi.

Philemon aliyasema hayo jana, Dar es Salaam, wakati wa mahafali ya 16 ya taasisi ya biashara na teknolojia inayotoa mafunzo ya masuala ya fedha, na teknolojia ya mawasiliano.

“Hii ni elimu, ni elimu ya kazi, ni elimu ya ujasiriamali” alisema Philemon katika mahafali hayo yaliyoshirikisha jumla ya wahitimu 211 wa ngazi za Shahada, Stashahada ya Juu na Stashahada.

Alisema, wahitimu hao wanapaswa kuwa na nidhamu wakati wa kutekeleza majukumu yao ili waongeze tija na wapate mafanikio. “Ukikosa nidhamu, hata ukiwa na taaluma nzuri utaua nchi” alisema baada ya kuwakabidhi wahitimu hao vyeti na zawadi.

Mwanafunzi bora katika mitihani iliyofanywa mwaka jana katika taasisi hiyo ngazi ya Stashada ya Kimataifa ya Kkompyuta, Elex Ongon, alisema, ujuzi katika nyanja mbalimbali katika teknolijia ya mawasiliano ni nyenzo muhimu kwa kuwa inawawezesha wahitimu wajiajiri.

Ametoa changamoto kwa vijana nchini wajifunze masuala ya teknolojia ya mawasiliano kwa madai kuwa, wahitimu wake wanahitajika sana kwenye soko la ajira nchini.

Alisema, kwa sasa yeye anahitaji mtaji mtu ili aweze kuwa mjasiriamali kwa kuwa, amejifunza kwa vitendo zaidi hivyo ana ujuzi kwenye masuala mbalimbali ya kompyuta.

Meneja wa mafunzo katika taasisi hiyo, Khamisi Mtajuka, alisema, elimu wanayoitoa ni nyenzo mojawapo ya kupambana na ukubwa wa tatizo la ajira nchini linalotokana na uhaba wa ujuzi hivyo kuwafanya wananchi watafute ajira badala ya kujiajiri.

Mtajuka alisema, taasisi hiyo yenye uwezo wa kufundisha wanafunzi 1200 kwa siku inashirikiana na taasisi za kimataifa ili kupata wahitimu wenye ujuzi wa kimataifa kwa lengo la kuwawezesha kuwa wajasiriamali au kumudu ushindani kwenye soko la kimataifa la ajira

Sunday, October 18, 2009

Si kweli kwamba Nyerere alikuwa haambiliki: Jaji Warioba

Unafahamu siku ambayo Mwalimu Julius Nyerere alipotaka kuteleza na hatimaye kukiuka sheria? Je, unafahamu ni kwa namna gani alivyokuwa akiendesha vikao muhimu kwa mustakabali wa nchi? Katika makala haya, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wake, na baadaye Waziri wa Sheria na Katiba, Jaji Joseph Warioba, anaelezea hayo ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 10 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

KATIKA mazungumzo yake aliyoyafanya mjini Dar es salaam na waandishi wa habari, hivi karibu, Jaji Warioba alizungumza mengi kuhusu hali ya sasa ya nchi, lakini pia alimgusia kidogo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Alianza kwa kuzungumzia madai yanayoelekezwa kwa Mwalimu Nyerere kuwa alikuwa haambiliki; kwa maana kwamba hakuwa akisikiliza wasaidizi wake.

Jaji Warioba anasema: “Unajua kuna watu walikuwa wanasema haambiliki, lakini Mwalimu Nyerere ni mtu aliyekuwa anasikiliza sana.

“Mimi nimefanya naye kazi kwenye serikali. Nilikuwa kwenye cabinet (Baraza la Mawaziri), nimekuwa kwenye chama, niliingia kwenye Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1976. Wakati alipokuwa mwenyekiti (wa CCM-Taifa) baada ya kutoka kwenye urais, mimi ndiye nilikuwa Katibu wake wa Ulinzi na Usalama.

“Staili ya Mwalimu, iwe kwenye cabinet, au iwe kwenye National Executive alikuwa na kakitabu kadogo. Mnaanza mjadala, mnanyoosha mikono tena anaandika… ataandika majina kisha ataita mmoja mmoja. Mnaweza kuendelea na mjadala siku nzima hamsikii akisema, anawasikiliza tu. Mkimaliza ana sum-up (anafanya majumuisho). Ni mtu ambaye alikuwa anajua, alikuwa mtaalamu kabisa wa kujenga consensus,” alisema Jaji Warioba.

“Unajua kila mahali kuna makundi. Sasa unaweza kuwa na kundi la viongozi hawa wanaona wale wenzao wanasema mambo ya ovyo ovyo hivi. Na kwenye cabinet mnaweza kumsikia mtu anazungumza, mnasema huyu anazungumza utumbo.

“Lakini Mwalimu akija ku-sum-up anasema kama fulani alikuwa amesema hivi… wote mnatoka pale mnaona uamuzi ule ni wenu wote, na ndiyo maana unaona kipindi chetu kile ilikuwa akizungumza Rais, utakuta wengine wanaozungumza walikuwa wanazungumza namna ile ile, kwa sababu ni kitu kilichozungumzwa na mnakielewa.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kauli za viongozi kupishana hazikuwapo enzi za utawala wa Mwalimu. “Baadhi wanafikiri tulikuwa parrots (kasuku) wa kuimba wimbo wa Mwalimu, lakini unawezaje kuimba exactly kama hukuelewa?,” aliuliza Jaji Warioba na kuongeza: “Ilikuwa ni kujenga ile consensus, ndiyo uongozi wake ulivyokuwa.

Jaribio la kuvunja sheria

“Na kinyume na wale wanaosema alikuwa haambiliki, si kweli. Alikuwa anakasirika kama mtu mwingine yeyote yule na aliweza kukufokea. Na wakati fulani alikuwa amemteua mtu katika nafasi fulani. Mimi kama Mwanasheria Mkuu wake nikaenda kumwambia: ‘Mwalimu hapa sheria inakataa, huwezi kumteua huyu.’

“Nikamwambia kuna kikwazo cha kisheria hapa, kwa kuwa alikuwa yule mtu (aliyepaswa kuteuliwa) alikuwa ameonewa mambo fulani. Mwalimu akakasirika, akaniambia wewe ndiye kikwazo. Wewe umezoea kila ukija hapa ni kuniambia usifanye hivi kwa sababu sheria inakataa, hapana hili sikubali.”

“Nikamwambia Mwalimu, hili ni suala la Katiba, ukifanya hivi kutakuwa na crisis (mgogoro) kwenye Bunge. Akasema si ndiyo demokrasi? Ngoja iende huko. Nikamwambia kwamba ni suala la Katiba, na yeye ndiye guardian (mlezi) wa Katiba.

“Nikaendelea kumwambia Mwalimu kwamba ikitokea crisis na yeye ndiye guardian; yaani imesababishwa na guardian, ni kitu serious. Akasema ndiyo demokrasi, haya mambo ya kufichaficha siyo mazuri; ngoja iende huko.”

Jaji Warioba anaendelea kulikumbuka tukio hilo na kusema: “Nikatoka pale, nikaenda kwa Waziri Mkuu, Sokoine (Edward) nikamwambia; ‘PM sasa kutakuwa na matatizo kwenye Bunge, boss hataki kubadili msimamo’, akasema aah hebu twende bwana tumshauri angalau asimwapishe huyu mpaka tuwe tumetoka bungeni.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, walipokwenda kumwona Mwalimu asubuhi nyumbani kwake, Msasani Dar es Salaam, yake mambo yakawa tofauti. Walikwenda kumwona Mwalimu Msasani, kwa kuwa alikuwa na ofisi yake ndogo aliyokuwa akiitumia na alikuwa akifika Ikulu kama kuna matukio rasmi, kama mkutano wa Baraza la Mawaziri au mengine.

“Alipotuona tu akaanza kucheka, akasema; ‘Edward (Sokoine), nilimfukuza huyu jana; lakini aliniambia kitu kimenisumbua sana usiku. Sasa sijui kimekuleta nini hapa? Waziri Mkuu akaelewa na akauliza, sasa nini kimekusumbua?

“Mwalimu akasema nimefuata ushauri wake. Akasema: ‘Joseph, wewe ni stubborn (msumbufu) eeh?’

Chimbuko la tukio hilo ambalo lingemweka Mwalimu Nyerere katika mgogoro wa kikatiba, lilihusu uamuzi wake wa kumteua mkuu wa mkoa.

Ilikuwa mwaka 1983, mtu huyo (jina linahifadhiwa), awali alikuwa na kesi mahakamani, na kwa mujibu wa sheria kwa wakati huo, ukifikishwa mahakamani unapoteza baadhi ya haki za kiraia kama kupiga kura kwa nyakati fulani.

Kwa hiyo kwa kuwa Mwalimu alitaka kumteua mtu huyo kuwa mkuu wa mkoa, ambaye kwa wakati huo moja kwa moja angekuwa mbunge, mgogoro ungejitokeza kikatiba kwamba, mbunge ni lazima awe na sifa kamili za kiraia (zikiwamo za kupiga kura), ambazo kama mhusika huyo angeteuliwa asingekuwa nazo.

Jaji Warioba anahitimisha simulizi ya tukio hilo kwa kusema: “Lakini sasa wakati mwingine kuwa stubborn kunasaidia; yaani usije ukaacha kusisitiza hoja yako kama unaamini uko sawa sawa. Kwa hiyo, ni kweli wakati mwingine Mwalimu alikuwa mbishi, lakini akikaa akitulia anajirudi.

“Kwa hakika, ni mtu mmoja ambaye, kwa viongozi niliowahi kufanyanao kazi, alikuwa haoni aibu kuja kusema hapa nilikosea.

“Mwalimu alikuwa giant kwenye intellectuals, no doubt about that, na he could stand his ground kwenye argument”, anasema Jaji Warioba na kuongeza: “Lakini alikuwa ni mtu ambaye yuko tayari ku-compromise. Ni mtu ambaye pamoja na kwamba alifika kiwango hicho cha juu, kimsingi alikuwa ni mtu wa kawaida.

“Kama ungefika Butiama ukakuta anacheza bao na wale wazee, na wewe humfahamu; na kisha wale wazee wakakuambia Rais yuko hapa, unaweza usiamini.

“Mimi ni Muikizu, siwezi kuzungumza Kiikizu kwa ufasaha. Nitachanganya na Kiswahili tu, lakini Mwalimu alikuwa anakaa na Wazanaki wale huku akizungumza Kizanaki kwa ufasaha.

“Alikuwa ni mtu wa kawaida. Mtaona hata msisitizo wake katika mambo ya maendeleo alipokuwa akisema people centred development ilikuwa ni hiyo ya kuwaweka mbele wananchi. Alikuwa akisema elimu ya Mtanzania ni primary school kwa sababu anawafikiria wale wananchi wa kawaida. Akisema afya ya Mtanzania ni zahanati, anamaanisha hivyo hivyo. Na alipata matatizo sana aliposema kuwa elimu ya Mtanzania ni primary school.”

Mbio za siasa baada ya Mwalimu

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, kisiasa hapa nchini kuna uhuru zaidi, na hilo ni lazima Watanzania walikubali. “Ule mfumo wa chama kimoja ulikuwa na nidhamu yake, sasa uhuru ni mpana zaidi wa kutoa mawazo, lakini tofauti mimi nafikiri chama na viongozi wakati ule walikuwa kweli wanajituma”.

“Kulikuwa na kujituma katika kuutumikia umma. Hivi sasa siasa zimekuwa za ubinafsi mno; yaani msisitizo kwenye utumishi kwa umma umepungua.

“Unajua mazoea bwana ni magumu sana, unajua mimi siku hizi huwa nasahau. Wakati mwingine ninaposema sistahili kutukuzwa, ninaonekana kama wa ajabu hivi. Stahili siku hizi ni uheshimiwa. Kuna kupenda ukubwa, na hata wanapojitambulisha husema kuwa mimi ni mheshimiwa mbunge fulani.

“Acha wengine wakuite mheshimiwa, siyo wewe mwenyewe ujiite hivyo. Kwa hiyo, nadhani uhuru wa mawazo umepanuka zaidi lakini ukichukua siasa kwa ujumla commitment yake ni kama imepungua.

Mwalimu dhidi ya ufisadi

“Kama kuna kitu Mwalimu alikuwa anachukia ni rushwa, ubadhirifu, wizi matumizi mabaya ya madaraka. Kuna wakati kuna mahali alisema kwamba pamoja na kujua kwamba kumchapa mtu mzima viboko ni kitu kibaya, lakini alikubali wala rushwa wakithibitishwa mahakamani wachapwe viboko.”

“Alikuwa na msemo wake: Caesar’s wife must be above suspicion; yaani ile suspicion tu inatosha kwamba uongozi wako umefika mwisho. Siku hizi inabidi uthibitishwe na Mahakama, lakini yeye kwake uaminifu ni kitu kikubwa, kwa hiyo hata kutuhumiwa tu inatosha kupoteza sifa za uongozi.

Kuhusu demokrasia, Jaji Warioba alisema hivi: “Nadhani demokrasia yetu (pamoja na malumbano yake yote) imepanuka. Nadhani mfumo wa vyama vingi umekuza demokrasia. Tatizo nadhani lipo kwenye vyama vyenyewe; yaani hakuna demokrasia.

“Tunasisitiza demokrasia ya nchi, lakini ni kama vile tunafumbia macho demokrasia ndani ya vyama vyetu. Tumekuwa zaidi watu wa kanuni na taratibu, lakini kama tukiimarisha demokrasia, hasa katika vyama, tutafika mbali; maana sasa hivi inaonekana demokrasia ni kama kupingana hivi”.

Wanamlilia Nyerere huku wakiendelea kumsaliti!

Leo Oktoba 14 mwaka huu, Taifa linaomboleza mwaka wa 10 tokea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, afariki dunia katika hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London, Uingereza.

Tokea afariki dunia, Taifa limefanya siku hiyo kuwa ‘Nyerere Day’ kumkumbuka kwa njia ya kufanya mikutano na makongamano.

Mwaka jana, kongamano kubwa la kimataifa likishirikisha watu maarufu kama mwanaharakati wa haki za binadamu na mwandishi wa vitabu, Wole Soyinka wa Nigeria lilifanyika kwenye Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka huu imetangazwa kwamba Mwalimu atakumbukwa kwa kongamano lililoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi ya Umma ingawa litafanyika Oktoba 12, Dar es Salaam, siku mbili kabla ya siku yenyewe iliyozoeleka ya ‘Nyerere Day.’

Katika kongamano la mwaka huu, miongoni mwa mada zitakazotolewa ni kuhusu ufisadi kwa mujibu wa mtazamo wa Mwalimu.

Nyingine itazungumzia mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika ujamaa, ubepari na ufisadi. Pia ipo itakayozungumzia mchango wa Mwalimu katika maendeleo ya jamii; hususan kilimo.

Aidha Chuo Kikuu cha Mzumbe cha Morogoro Oktoba 22 mwaka huu kitakuwa na Warsha ambayo mada kuu itakuwa ‘Kilimo Kwanza na mawazo ya Mwalimu Julius Nyerere.’

Ni vyema kumkumbuka Mwalimu kwa mtazamo na mawazo aliyokuwa nayo kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu yakiwamo yale ambayo hadi leo yanatuumiza vichwa.

Lakini vyema pia tukakumbushana kwamba kumkumbuka tu Mwalimu kwa msimamo aliokuwa nao na mchango wake kwa ustawi wa taifa hili hakutoshi.

Hatumtendei haki hata kidogo kwa kuwa hodari wa kumsifia kwa mtazamo na mawazo yake bila ya kutekeleza yale aliyokuwa akihubiri.

Kwa hakika, ufisadi wa kutisha tulioushuhudia nchini usingekuwapo kama watendaji wangezingatia yale yote yaliyokuwa yakizungumzwa na Mwalimu hata baada ya kuondoka madarakani.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba miongoni mwa viongozi wanaoendelea kuzisaliti fikra na miongozo ya Mwalimu, ni wale wale aliokuwa nao karibu mno wakiwamo hata baadhi ya wanafunzi wake.

Kwa mtazamo wetu (na tunapenda kusisitiza hili) ni unafiki kwa viongozi wetu hawa kujitia wanamlilia na kumkumbuka Mwalimu; huku wakiendelea kuyasambaratisha yale yote aliyoyasimamia wakati wa uhai wake. Ni vyema wakaacha unafiki huo.

Thursday, October 15, 2009

Hatimaye TGNP washinda kesi iliyodumu mahakamani kwa miaka 11






Wafanyakazi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) wakesheherekea ushindi wa hukumu ya kesi ya jengo lao mara baada ya kurejea kutoka mahakama kuu ya Tanzania ambapo jaji alisoma hukumu ya kesi majira ya saa tatu asubuhi iliyodumu mahakamani kwa takribani miaka 11.

Tuesday, October 13, 2009

'Wanaopinga ufisadi si malaika'

MWANAZUONI maarufu nchini, Profesa Issa Shivji, amesema wanaotajwa kuwa ni wapinga ufisadi nchini si malaika, na wanaodaiwa kutetea uovu huo si mashetani.

Profesa Shivji amesema, makundi yote hayo yanashabikia mfumo uliozaa ufisadi, na kwamba, vyombo vya habari na wanasiasa wamesababisha makundi hayo yalumbane.

"Lakini viongozi bora hawazaliwi..kwani wakati wa mwalimu viongozi hawakuwa na tamaa ya hela? walikuwanayo, walikuwanayo lakini wangefanya nini na mamilioni ya EPA? amehoji Profesa Shivji.

Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, ufisadi ni matokeo ya mfumo wa sasa wa uliberali mamboleo uliotokana na ubepari.

"Mtu hazaliwi na tabia ya ufisadi, mtu hazaliwi na tabia ya ubinafsi, ubinafsi unatokana na mfumo"amesema.

Amesema, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, ufisadi haukuwepo Tanzania ila rushwa ilikuwepo.

"Ubepari ndiyo unaoingiza ubinafsi, ni mfumo" amesema na kubainisha kuwa moja ya misingi ya ufisadi ni ubinafsi, na kwamba, hulka ya binadamu ni ushirikiano na si ubinafsi.

Profesa Shivji amesema, chanzo cha ufisadi si mtazamo wa jamii ila mfumo uliosababishwa na ubepari.

Kwa mujibu wa Profesa Shivji, hulka na tabia ya mwanadamu vinajengeka katika mfumo na si mtazamo wao.

"Je, ufisadi ulikuwepo enzi ya Mwalimu? hapana haukuwepo, rushwa ilikuwepo" amesema Profesa Shivji wakati akiwasilisha mada kwenye kongamano la kumuenzi Baba wa Taifa katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

Amesema, haitoshi kuhubiri uzalendo wakati mfumo wako ni kinyume cha uzalendo.

"Tunakubali tu kila kitu,kila kitu tunachoambiwa tunakubali tu, hatuwathamini watu wetu ndiyo shida yetu...kauli mbiu yetu ni moja tu, question everything (uliza/hoji) kila kitu"amesema.

Monday, October 12, 2009

Adhabu ya kifo ni 'msalaba' kwa majaji

JAJI Mkuu mstaafu Barnabas Samatta amesema majaji nchini wamekuwa ‘wakilazimishwa’ kutoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa mbalimbali na kushauri Serikali na Bunge kuipa Mahakama Kuu mamlaka itoe adhabu mbadala.

Wakati Jaji Samatta akitoa rai hiyo kuna taarifa kuwa Rais Jakaya Kikwete amebadilisha hukumu 400 za kifo kuwa za kifungo cha maisha.

Jaji huyo mstaafu alisema wakati mwingine jaji aliyetoa adhabu ya kifo kwa mshitakiwa na kamati maalumu inayomshauri Rais juu ya utekelezwaji wa adhabu za kifo zilizotolewa mahakamani, hupendekeza kwa Rais kuwa adhabu hiyo isitekelezwe na badala yake mshitakiwa apewe adhabu nyingine na mara nyingi ikiwa ni kifungo kirefu.

Samatta alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wanaharakati wa haki za binadamu katika maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya kifo duniani yaliyofanyika Dar es Salaam katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Kwa nini sheria imbebeshe jaji mzigo wa kutoa adhabu ya kifo wakati anaamini, na kila mpenda haki angeamini kuwa siyo haki kwa mshitakiwa, siyo haki kwa ndugu wa marehemu na siyo haki kwa jamii na kuwa nyufa iliyopo kati ya adhabu hiyo na uovu wa mshtakiwa haizibiki hata utaalamu wa juu ukitumika?” Alihoji Samatta.

Alisema pia washtakiwa wa kifo wamekuwa wakiteseka kisaikolojia wakati wakisubiri hatima yao katika kipindi cha kati siku ambayo jaji anatoa hukumu ya kifo na siku ambayo Rais anapunguza adhabu hiyo ya kifo.

Kwa mujibu wa Samtta dunia imekwishaanza safari ya kufuta adhabu ya kifo na kuisisitizia Serikali na Bunge, kama wanaona ugumu kushiriki katika safari hiyo katika kipindi kifupi kijacho, kwa nini wasianze kuipa Mahakama Kuu mamlaka hayo?

Akifafanua hoja yake hiyo, Samatta alitumia hoja za wanaotetea kufutwa kwa adhabu hiyo kwamba, kwa kuwa haki ya binadamu ya kuishi na kuzaliwa haitolewi na katiba, wafalme au watawala basi hakuna mwanadamu mwingine mwenye mamlaka ya kusitisha haki hiyo katika mazingira yoyote yale.

Alisema pia kuna hatari ya adhabu hiyo kutolewa kwa makusudi au kwa makosa kwa mtu ambaye hana kosa na kwamba ikitumika hivyo hakuna njia yoyote ya kumrudishia marehemu huyo maisha yake.

Katika kutetea hoja hiyo, alinukuu maneno ya mwandishi wa Kifaransa, Nicolas Chamfort aliyepata kusema katika hadithi, “asubuhi leo tumewahukumu watu watatu kunyongwa.

Wawili kati yao kwa kweli walistahili kupewa adhabu hiyo.” Samatta pia alitoa mfano wa tukio aliloliita kuwa la kusikitisha lililotokea wiki iliyopita huko Uingereza ambapo mfungwa mmoja aliachiliwa huru baada ya kutumikia kifungo cha miaka 27 jela kwa kosa la mauaji ya kukusudia baada ya kugundulika kuwa hakuhusika kwa namna yoyote ile na mauaji hayo kwa kuwa marehemu aliuawa na mtu mwingine.

“Mtu huyo ana bahati sana kuwa adhabu ya kifo haitumiki huko Uingrereza kwa kosa la mauaji. Isingekuwa hivyo, huenda angekuwa marehemu zaidi ya miaka ishirini iliyopita,” alisema Samatta.

Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za haki za Binadamu Kusini mwa Afrika (SAHRINGON), Dk Emmanuel Kandusi alisema adhabu ya kifo ni ya kulipa kisasi na kwamba si suluhisho la tatizo la mauaji duniani na kupendekeza elimu iongezwe zaidi kukomesha mauaji mbalimbali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, Tanzania inakadiriwa kuwa na wafungwa 2,246 ambao wanasubiria utekelezaji wa hukumu ya kifo katika magereza mbalimbali nchini huku watu 232 tu wakiwa ndio walitekelezewa hukumu hiyo tangu 1961.

Uandikishaji Uchaguzi Serikali za Mitaa wakosa mwamko

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda anafikiria kuunganisha uchaguzi wa serikali za mitaa na ule wa midiwani katika uchaguzi ujao wa 2015 baada ya kubaini uandikishaji wa wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu kukosa mwamko.

Aidha pamoja na kukosa mwamko huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Celina Kombani, amesisitiza kuwa muda wa kujiandikisha uliofikia tamati jana hautaongezwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana viongozi hao walitoa matamko hayo baada ya kupata habari ya kutokuwepo kwa idadi iliyotarajiwa ya wapigakura katika maeneo mbalimbali nchini.

Pinda ambaye alijiandikisha jana katika kituo cha Oysterbay Na.2B, jijini Dar es Salaaam ili aweze kushiriki uchaguzi huo, alisema serikali itaangalia uwezekano wa kurudisha uchaguzi wa madiwani kwenye uchaguzi huo.

“Wapo watu wanaohoji ni kwa nini madiwani wanachaguliwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wakati wanafanyakazi na Serikali za Mitaa…serikali itajadili na kuangalia uwezekano wa kurudisha uchaguzi wa madiwani kwenye serikali za mitaa,” Pinda alieleza.

Alisema huenda madiwani wakichaguliwa sanjari na viongozi wa Serikali za Mitaa, uchaguzi huo utakuwa na mwamko zaidi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi alimpatia Waziri Mkuu taarifa ya uandikishaji na kusema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na lengo la kuandikisha wapiga kura 1,200,573.

Lukuvi alisema hadi jana mchana ni watu 388,824 tu waliokuwa wamejitokeza kujiandikisha sawa na asilimia 32.38 ya matarajio yaliyowekwa.

Lukuvi alifafanua kuwa Wilaya ya Ilala ilikuwa na lengo la kuandikisha watu 189,5000, lakini waliojiandikisha mpaka wakati akimpa Pinda taarifa hiyo, walikuwa 96,885 sawa na asilimia 51.12.

Wilaya ya Temeke iliweka lengo la kuandikisha wapiga kura 509,000 na waliojiandikisha hadi jana mchana ni 151,333 sawa na asilimia 39.73

Kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni, Lukuvi alisema lengo lilikuwa kuandikisha wapiga kura 50,2037 lakini waliojitokeza walikuwa 140,606 sawa na asilimia 28 ya matarajio yaliyowekwa katika wilaya hiyo.

Lukuvi alisema kwa ujumla idadi ya waliojitokeza ni ndogo na kueleza kuwa hali hiyo imesababishwa na mazingira ya wakazi wa Dar es Salaam ambao wengi wao wametinga na shughuli mbalimbali.

“Wakazi wa Dar es Salaam ni wachakarikaji na wengi wao wanapata muda siku za mapumziko ya wiki. Uandikishaji ulianza Jumapili lakini kulikuwa upungufu hivyo kazi ilianza rasmi Jumatatu na kumalizika leo (jana) Jumamosi hivyo watu wengi wamejitokeza leo…kama siku zikiongezwa huenda watajitokeza wengi zaidi,” Lukuvi alisema.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu alisema muda hauwezi kuongezwa kwa sababu uliwekwa kwa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi ila kama sheria inaruhusu basi serikali itaangalia uwezekano wa kuongeza muda.

Hata hivyo alisema idadi ndogo imesababishwa na upungufu wa kibinadamu kwa sababu baadhi ya watu wanapuuzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa bila kujali kuwa umewekwa mahususi ili kuwapatiwa wananchi fursa ya kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao wenyewe.

Naye John Nditi anaripoti kutoka Morogoro kuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ( TAMISEMI), Celina Kombani, amesema kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza wa uandikishaji wa daftari wa wapiga kura la uchaguzi huo.

Wakati Waziri huyo wa akitoa msimamo huo, katika Manispaa ya Morogoro shughuli hiyo jana ilianza kwa kudorora kwa baadhi ya vituo vya kujiandikisha kwenye daftari hilo na kwamba hadi jana mchana watu walikuwa wakiendelea kujitokeza kujiandikisha kwenye vituo vyao.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Sabasaba, Haji Ngatumbula, alisema malengo ya uandikishaji katika Kata hiyo kwenye daftari hilo ilikuwa ni watu 1,560 na hadi kufikia Oktoba 9, mwaka huu watu waliojiandikisha walifikia 816 na kwamba hadi jana mchana baadhi ya vituo 12 vilivyopo viliandikisha watu wa kutosha.

Hata hivyo alisema siku ya kwanza ya uandikishaji jumla ya watu 281 walijiandikisha ambapo wanawake walikuwa 145 na wanaume 132 na siku iliyofuatia idadi yao ilianza kushuka na kufikia watu 145.

Hata hivyo baadhi ya vituo vilivyotembelewa jana mchana kabla ya kufikia muda wa kumalizika kwa shughuli hiyo, vikiwemo vya Ngoto B ambacho kiliandikisha watu sita, Ofisi ya Kata hiyo watu 57 na mtaa wa Betero watu 14 ambao ulivuka lengo waliokusudia la watu 100 na kufikisha 121.

Katika vituo vingine kikiwemo cha kata ya Mlimani iliweka makisio ya kuandikisha watu 2,368 kati ya wakazi 7,316 ambapo mtaa wa Liti wenye idadi ya watu 980 ulipanga kuandikisha watu 508 na ambapo hata hivyo bado hawakufikia lengo.

Naye Merali Chawe anaripoti kutoka Mbeya kuwa mkoa huo umeshindwa kufikia lengo la kuandikisha watu kwa ajili ya upigaji kura wa kuchagua viongozi wa serikali za mitaa ambapo hadi kufikia jana watu waliojiandikisha walikuwa ni 295,929 kati ya watu 665,277 waliotarajiwa.

Mratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Mbeya Prosper Roman aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumzia idadi ya watu waliojiandikisha, ambapo alisema sababu za idadi ndogo ya watu waliojiandikisha imetokana na watu kuchanganya uandikishaji huo na uboreshaji wa daftari la wapiga kura.

Kilimo Kwanza: Kitanzi kwa mkulima mdogo

KITANZI kimeandaliwa kwa mkulima mdogo nchini ategemeaye kilimo kwa maisha yake. Kitanzi kimeandaliwa anyongwe hadi kufa. Bado kitambo kidogo kamba itawekwa shingoni, mnyongaji ataivuta na huyo mkulima atakoroma, pumzi itamwishia na mwishowe kufa!

Kitanzi hiki kiliandaliwa mapema mwezi Juni mwaka huu na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Baraza la Biashara la Taifa [TNBC], uliofanyika Kunduchi Beach Hotel and Resorts, chini ya Uenyekiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na kuhudhuriwa na baraza lote la mawaziri, wafanyabiashara [wawekezaji] mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi, kuzungumzia hali ya kilimo nchini na mustakabali wake.

Mkutano huo uliokuwa na washiriki karibu 380, wasomi wenye kulelewa na kulewa itikadi na sera za maendeleo za uchumi za mrengo wa nchi za ubepari wa Magharibi, ulibaini, pamoja na mambo mengine kuwa, sababu kubwa kwa Tanzania kutofanikiwa kugeuza na kuboresha kilimo, ni “kuzalisha isichotumia, na kutumia isichozalisha”; kwa maana kwamba, tunazalisha zaidi mazao ya biashara kwa ajili ya kuuza nje; na tunatumia zaidi kile tunachoagiza kutoka nje.

Kwa hiyo, mkutano huo, chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, ukaja na “mwarobaini” wa matatizo ya kilimo chetu kwa njia ya kuanzisha Programu ya “Mapinduzi ya Kijani” [Green Revolution], yaliyopewa jina la “Kilimo Kwanza”.

Swali kuu la kujiuliza: Je, ni kwa kiasi gani wale waliokutana Kunduchi Beach Hotel and Resorts, wanawakilisha matakwa au kubeba dhamana ya wakulima wanaounda asilimia 80 ya Watanzania?

Tunahoji hilo kwa sababu sera nyingi, mikataba na hata miswada ya Bunge, imepitishwa bila kuwashirikisha wananchi kikamilifu; licha ya kwamba madhara yake yanabebwa na wananchi masikini wa Taifa hili kwa uchungu mkubwa. Na ndivyo programu hii ya “Kilimo Kwanza” inavyojionyesha.

Wasomi wetu, kwa kujasirishwa na ubepari wa kimataifa, wametenda mabaya kwa watu wao bila hofu; kana kwamba wamehakikishiwa ufalme: “Msiogope, enyi kundi dogo; kwa sababu baba yenu [Benki ya Dunia, IMF] ameona vema kuwapa ule [ulaji] ufalme” [Luka 12:32].

Hawa wanaoiangamiza nchi yetu kwa sera mbovu za mapokeo [ubepari, utandawazi, soko huria], ubinafsishaji usiojali, mikataba mibovu yenye kuitafuna nchi, ufisadi; lakini bila hofu ya kuhojiwa wala kuwajibishwa, si ndiyo hao ‘kundi dogo’ lenye fungate na ubepari wa kimataifa [baba yao], unaochafua sera zetu nzuri, maadili ya taifa na uzalendo?

Kama kweli hili si kundi dogo lililokabidhiwa “ufalme” [ulaji], kwa nini vigogo wa kashfa za IPTL, Deep Green, Meremeta, Tangold na baadhi ya vigogo wa EPA hawaguswi? Hao wameitafuna sekta ya umeme na madini wakaimaliza, na sasa, kwa kutuona wajinga, wanawania kuitafuna sekta ya ardhi na kilimo bila kuogopa; wakijiliwaza kwamba [kuna] amani [katika uwekezaji].

Ukweli ni kwamba amani haipo; bali wamemjeruhi mkulima mdogo kwa kumdunga sindano ya kuua maumivu na usingizi [kwa kumlewesha na njozi za injili ya Benki ya Dunia, IMF, WTO, FAO]. Itakuwaje atakapozinduka na kuyahisi maumivu hayo? Itakuwaje atakapoponyoka kuepuka kitanzi?

Angalia orodha ya walioalikwa kwenye mkutano wa TNBC/Kilimo Kwanza: Mawaziri (40) wanachama wa TNBC (125) wawakilishi kutoka Sekta ya Kilimo na sio vikundi vya wakulima wadogo (63) wawakilishi wa mabaraza ya biashara ya mikoa (35), maafisa wa Serikali (125) na wawakilishi kadhaa wa makampuni binafsi hapa nchini.

Kwa mujibu wa programu hiyo ya “Kilimo Kwanza”, nchi yetu inakusudia kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na cha kibiashara, chenye kutumia teknolojia ya hali ya juu; na wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wenye kutumia zana kubwa kubwa za kilimo [matrekta, mashine za kuvuna, mbegu za viini tete zinazozalishwa viwandani na pembejeo za kilimo za gharama], watapewa kipaumbele katika mpango huu.

Hao watapewa ardhi, mikopo ya mabenki, misamaha ya kodi na vivutio vingine chini ya kile kinachoitwa “mazingira mazuri ya uwekezaji” kutoka nje [FDI], kama ilivyofanyika katika sekta ya madini na nishati, na kufungua mlango kwa uporaji wa rasilimali zetu na jasho la wananchi.

Soma zaidi

Friday, October 9, 2009

Jalada kesi ya Jeetu kuhamishiwa Mahakama Kuu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa uamuzi kwa kukubali maombi ya kupeleka Mahakama Kuu jalada la kesi ya kujichotea fedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayowakabili mfanyabiashara maarufu Jeetu Patel na wenzake.

Mahakama hiyo chini ya Hakimu John Mgeta, jana ilikubali maombi kwa kukubali ombi la akina Jeetu la kutaka kesi zao zilizoko mahakamani hapo kusimama na kuruhusiwa kuhamisha jalada kwenda Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi ya kikatiba waliyoifungua mwaka huu.

Baada ya Hakimu Mgeta kukubali ombi lao ingawa upande wa mashtaka ulipinga, hakusema kama kesi hiyo imefutwa au itaendelea kutajwa, kama ilivyoelezwa katika uamuzi wa hakimu mwingine katika kesi kama hiyo inayowakabili washtakiwa hao mahakamani hapo ambapo waliruhusiwa pia kuhamishia jalada Mahakama Kuu kesi ya Kisutu ikiendelea kutajwa.

Washtakiwa katika maombi yao walidai kuwa tamko la Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi Aprili 23 mwaka huu, akiwataja kuwa mafisadi papa, limeifanya jamii iwaone wana hatia.

Walidai wamenyimwa haki yao ya kuonekana kuwa hawana hatia mpaka pale upande wa mashtaka utakapothibitisha bila shaka.

Aidha, upande huo uliomba jalada la kesi kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuamua kama tamko la Mengi halikukiuka haki za washtakiwa na baada ya serikali kutoa tamko kwamba Mengi ameingilia uhuru wa mahakama, je ilikuwa sahihi kuendelea na kesi hizo badala ya kuzifuta na kumshtaki Mengi kwa kuidharau mahakama?

Upande wa mashtaka ulipinga maombi hayo ukidai kuwa maneno hayo waliyodai ni ya barabarani na hayana uhusiano wowote na kesi iliyoko mahakamani na kuiomba mahakama kuyatupilia mbali.

Jeetu ambaye jina lake kamili ni Jayantkumar Chandubhai Patel, katika kesi hiyo anashtakiwa pamoja na Devendra Patel, Amit Nandy na Ketan Chohan na wanadaiwa kughushi na kujipatia ingizo kutoka BoT la Sh bilioni 3.9 na wanadaiwa kujifanya kuhamishiwa deni na kampuni iliyoko Japan.

Washtakiwa hao wanadaiwa kwa kutumia Kampuni ya Bina Resorts walijifanya kuhamishiwa deni hilo kutoka C.Iton & Company Limited na kuitaka BoT kuwaingizia fedha hizo na benki hiyo ilifanya hivyo.

Thursday, October 8, 2009

Raza: Mafisadi wanafanya nini Kamati Kuu?

MFANYABIASHARA maarufu wa Zanzibar na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM, Mohamed Raza amesema ni vyema wale wanaotuhumiwa na ufisadi waliomo katika Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) wakajiengua.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kwenye Hoteli ya Star Light mjini Dar es Salaam, Raza alisema cha kushangaza zaidi ni kwamba miongoni mwa wanaotuhumiwa wako kwenye kamati ya maadili ya chama hicho.

Alisema watu hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi walioko kwenye Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na bungeni, wangejiondoa ili kulinda heshima zao na chama chao.

“Mtu mzima akipewa tuhuma yakhe, hukaa pembeni, huo ndiyo ustaarabu,” alisema Raza ambaye hakuwa tayari kutaja majina yao lakini akasisitiza kwamba wanajulikana.

Alisema kujiondoa kwa watuhumiwa hao kutamsaidia Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho aliyeko msitari wa mbele katika kupiga vita ufisadi.

Raza alimsifu Spika wa Bunge, Samwel Sitta kwa msimamo wake uliolifanya Bunge kuwa la aina yake katika kusimamia maslahi ya wananchi, hasa katika vita dhidi ya ufisadi.

‘Kama siyo Bunge, Tanzania leo tungekuwa watumwa. Tanzania ingekuwa ya matajiri wachache,” alisema.

Aliongeza: “Spika ambaye ni kada wa CCM ameweka heshima kubwa katika nchi yetu (katika kupiga vita ufisadi).”

Alisema tuhuma za ufisadi walizonazo baadhi ya viongozi ni nzito. “Kuendelea kwao kuwa bungeni tunasononeka sana,” alisema.

Alisema wimbo unaoimbwa wa maisha bora kwa kila Mtanzania utabaki tu kuwa wimbo usiokuwa na vitendo kwa sababu ya matatizo mengi yakiwemo ya ufisadi. “Tujiulize je, nia ipo?” aliuliza.

Alisema kwa vile mpaka sasa wanachokabiliwa nacho ni tuhuma, waendelee kulipwa mishahara lakini wajiondoe bungeni na nyadhifa nyingine nyeti wanazoshikilia.

Alishangaa ni kwanini viongozi wa sasa hawataki kufuata mfano wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) alipojiuzulu uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa matatizo yaliyojitokeza ndani ya wizara yake.

Raza alisema haelewi kamati iliyoundwa hivi karibuni na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mzee Ruksa kufuatilia mambo yaliyofanyika bungeni ni ya nini hasa.

“Tunaunda kamati ya Mzee Ruksa. Mzee Ruksa afanye nini sasa hivi. Huyu mzee tusimtumie vibaya. Hakuna bwana kwenye CCM wala hakuna kundi linaloongoza CCM. JK (Jakaya Kikwete) kachaguliwa na wananchi wote,” alisema.

Alisema ili CCM iendelee kushinda ni lazima uadilifu uwepo hivyo waliojitokeza kuwa msitari wa mbele kupiga vita ufisadi ni budi kuwapongeza. “Iko wapi CCM ya mwaka 1977, vijana tunalia,” alisema.

Alisema ipo haja ya CCM kuwa na chuo cha maadili. “Katika masuala ya uongozi lazima tuwe wa kweli,” alisema.

Alisema CCM ingekuwa vizuri ingewapongeza yenyewe makada wake wanaopiga vita ufisadi badala ya kazi hiyo kufanywa na watu wa nje kama ilivyotokea kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela ambaye alipewa tuzo na Marekani .

Mbali ya kuzungumzia kashfa ya ununuzi wa rada, Raza pia alizungumzia kwa uchungu tuhuma za ufisadi katika mfuko wa kuwezesha uagizaji bidhaa nje ya nchi (CIS).

“Tumefika wakati wa kuzungumza hali halisi. Fedha hizi (za kashfa ya CIS) ni nyingi sana. Fedha zilizochotwa zinaweza zikajenga skuli na vituo vingi vya afya,” alisema.

Alisema maadili ya uongozi katika Tanzania yameporomoka kwa sababu ya kutozingatia yaliyokuwa yanasemwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. “Leo hatuna maadili hata kwenye sera zetu,” alisema.

Alisema kuna umuhimu wa wafanya biashara kuzirejesha fedha walizozipata za CIS zisaidie wenye matatizo luluki vijijini.

Raza alisema kwamba huwa anaachwa hoi anapomwona mkurugenzi wa wizara anapokwenda na gari la Sh milioni 100 kwa wanavijiji wanaohangaika kwa jumbe la mkono la Sh 2,000.

Kuhusu uandikishaji wa vitambulisho vya wakazi Zanzibar, Raza alisema ya kuwa ana imani kuwa kila Mzanzibari mwenye haki ya kupata kitambulisho hicho atakipata.

Alisema tatizo aliloliona ni baadhi ya watu kutokuwa wa kweli katika zoezi hilo la kujiandikisha.

Alisema ni kawaida mtu anazaliwa sehemu nyingine, akakulia kwingine na kuwa mkazi wa eneo jingine.

Alisema tatizo linalojitokeza ni baadhi ya watu kulazimisha kujiandikisha sehemu ambazo wanaona zina maslahi kwa chama chao. Wanafanya hivyo waaktik wanafahamu kwamba sheria inamtaka kila mmoja kujiandikisha kwenye makazi yake ya sasa.

Alisema badala ya kuandikisha kwenye makazi yao halisi huenda sehemu walikozaliwa baada ya kuona sehemu hiyo ina wafuasi wengi wa chama chao au sehemu waliokulia kwa sababu hizo hizo hivyo kuleta mtafaruku.

Aliwataka watu kuwa wa kweli wanapojiandikisha ili zoezi hilo liondokane na ghasia nyingi zinazojitokeza.

Tuesday, October 6, 2009

Kikwete hataki malalamiko Serikali za Mitaa

RAIS Jakaya Kikwete, amewataka wanaoandikisha wapiga kura na wasimamizi wa uchaguzi wafanye kazi zao kwa makini na weledi ili kuepuka malalamiko kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji, na Vitongoji utakaofanyika Oktoba 25.

Rais Kikwete amesema, iwapo uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru na haki, washiriki wote watayaheshimu matokeo hivyo kuepuka kurudia kufanya uchaguzi mwingine.

“Kama ilivyo kwa kila uchaguzi, kutakuwa na washindi na walioshindwa kinachotakiwa kuzingatiwa ni mwamba mshindi atapatikana kwa kuchaguliwa na idadi kubwa ya wananchi,” Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika amesema wakati anasoma hotuba ya Rais Kikwete.

Rais pia alitumia mkutano huo kuwaeleza wadau wa siasa kuwa Serikali ipo tayari kupokea mapendekezo kutoka kwao kwa ajili ya kumaliza malalamiko yaliyoko kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Amewataka wadau hao wa siasa wautumie mkutano huo kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuondoa mambo yenye utata.

Mpango wa Utafiti wa Demokrasia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Redet) ndiyo ulioandaa mkutano huo kuzungumzia hali ya siasa nchini.

Ametaja baadhio ya mambo yanayolalamikiwa kuwa ni kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa awamu mbili,ukiwemo uchaguzi wa madiwani mwaka mmoja baada uchaguzi mwingine wa Serikali za Mitaa.

Amesema, pia kuwepo kwa mamlaka mbili zinazosimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa kunasababisha malalamiko.

Tume ya Taifa ya uchaguzi(NEC) inasimamia uchaguzi wa madiwani, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inasimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na vitongoji.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, sifa za wagombea hususani ile inayohusiana na uanachama na udhamini wa chama cha siasa kwa mtu anayegombea nafasi ya uongozi katika ngazi ya kitongaoji/kijiji zimezua mjadala.

“Mjadala juu ya masuala haya ni muhimu ili kujenga na kuimarisha demokrasia nchini,” alisema Kikwete na kuongeza kuwa “naamini masuala haya yatajadiliwa na mkutano huu na kuyatolea mapendekezo.”

“Mimi nisingependa kumaliza utamu wa mjadala huo kwa kutoa maoni yangu mapema, ila niseme tu mapendekezo yenu tutayafanyia kazi kama itakavyofaa,” amesema Rais Kikwete.

Amewasihi wapiga kura wote wenye sifa kutumia haki yao ya msingi kujiandikisha na kupiga kura.

Amewakumbusha wananchi kwamba uchaguzi huo unagharimu fedha nyingi za walipa kodi hivyo kama hawatajitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura taifa litakuwa limepoteza rasilimali zake.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amesema, ingawa Rais Kikwete ametoa changamoto hizo, mapendekezo yao hayana maana katika uchaguzi ujao kwa kuwa zimebaki siku chache tu ufanyike.

“Kwa hali hiyo inatulazimu kusubiri hadi katika uchaguzi wa 2014 ili mapendekezo yetu yaweze kufanyiwa kazi kwa kweli hii sio kuwatendea haki wadau,” amesema Profesa Lipumba.

Naye Hellen Mlacky, anaripoti kuwa, Rais Jakaya Kikwete amewataka watanzania nchini wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura la uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili watumie haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka.

Ameyasema hayo leo baada ya kujiandikisha katika mtaa wa Kivukoni, kituo mamba moja Kivukoni. Rais alikuwa ni mtu wa 12 kujiandikisha katika kituo hicho tangu zoezi hilo lianze rasmi juzi.

Amesema, wananchi wengi wamekuwa na fikra potofu kwamba uchaguzi wenye maana ni ule wa kumchagua Mbunge au Rais.

Rais amesema, wananchi wanapaswa kuuthamini uchaguzi huo kwa kuwa,viongozi wa mitaa ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele kwa sababu kila wakati wanashughulikia matatizo ya wananchi.

“Napenda niwasisitizie wananchi kwamba viongozi wa mitaa ndio viongozi muhimu sana… sisemi hivyo ili kuwakataza wasipige kura mwaka kesho kwenye uchaguzi mkuu ila nataka muelewe viongozi wa mitaa ndio wa kwanza hata mtu unapopatwa na shida ya ghafla hata usiku.. hawa ni viongozi wetu wa usiku na mchana” amesema.

Monday, October 5, 2009

Warioba atema cheche


-Haoni tatizo la Waraka wa Wakatoliki
-Ataka majibu kwa Deep Green, Meremeta
-Ashangazwa na kauli baada ya NEC

WAZIRI Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, ameonyesha wasiwasi kuhusu uongozi wa nchi, akisisitiza kuwa umekuwa karibu mno na matajiri, na nchi inaendeshwa kwa kuwasilikiliza matajiri zaidi, kuliko wananchi wa kawaida.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hata katika sekta ya utumishi wa umma, viongozi wamekuwa wakilipwa mishahara minono yenye tofauti kubwa na ya kima cha chini.

Mbali na mtazamo huo, Warioba ameonyesha wasiwasi pia kuhusu kesi za ufisadi, kushangazwa na viongozi wa wanaotilia shaka viongozi wa dini wanaojitoa kutoa elimu ya uraia.

Katika mazungumzo yake na baadhi ya vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana Jumanne, Warioba alizungumzia pia kuporomoka kwa maadili, kuimarika kwa matabaka na mitandao ndani ya vyama vya siasa, kikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Tanzania bado ni nchi ya amani na utulivu, lakini kuna dalili za umoja kuanza kutoweka, tumeanza kugawanyika katika vikundi…kuna matabaka yapo wazi kabisa,” alisema na kuongeza:

“Tofauti ya kimapato ni kubwa hata ndani ya Serikali, kima cha chini kimetofautiana sana na mishahara ya wakubwa, achilia mbali posho wanazopata, kima cha chini 100,000 lakini cha juu kimefikia hadi milioni tano.

“Hii ni hatari, na matokeo yake ni kuwapo kwa watendaji wa chini walioamua kupigania maslahi yao hata kwa kuvujisha siri.

“Uongozi umekuwa karibu mno na matajiri kuliko wananchi wa kawaida, wanaovujisha siri ni hao wasioridhishwa na hali hii,”

“Wameanza kuchukua hatua za kutetea maslahi yao kwa migomo na mambo mengine kama kuvujisha siri. Nimeshangaa watu wanatoka Ngorongoro wameacha uongozi wa kijiji, wilaya na mkoa huko hadi wanafika mbele ya lango la Ikulu,”

“Tusipoangalia tutafika kubaya. Ni wazi viongozi wameanza kupoteza imani kwa wananchi, na wananchi wameanza kutenda mambo yao wenyewe ili kujitetea…kuna credibility gap na hii ni hatari,” alisema Warioba, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba katika Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Waziri Mkuu katika Serikali ya Ali Hassan Mwinyi.

Alishtushwa na kuibuka kwa udini na ukabila kiasi cha kuingia hata ndani ya mijadala bungeni, akitaja suala la Mahakama ya Kadhi, na kujiunga kwa Tanzania kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), akikosoa mijadala hiyo kwa kurejea hoja za Tanganyika zilizoanzishwa na kundi la Wabunge la G55.

“Mwaka 1993 kundi la G55 liliibuka baada ya Zanzibar kutaka kuingia OIC, ni kundi lililoijadili OIC kama hoja ya kitaifa na si ya dini fulani, kwenye kundi hilo walikuwamo Waislamu na Wakristo, walitetea utaifa na kusimamia hoja yao kitaifa.

“Leo hoja za Mahakama ya Kadhi na OIC zinajadiliwa kwa mgawanyiko wa kidini, Mwislamu anaunga mkono, Mkristo anapinga si kwa kuangalia tatizo au uzuri wa hoja kwa Taifa. Imejitokeza hata bungeni, hii ni hatari,” alisema na kuhimiza masuala hayo yajadiliwe kwa mtazamo wa kitaifa na si makundi au maslahi ya dini fulani.

Kwa upande mwingine, alijadili hoja hiyo kwa kuutazama waraka wa Kanisa Katoliki, akisema haoni tatizo lake zaidi ya kuhimiza elimu ya uraia na kupatikana viongozi waadilifu.

“Tutafikia mahala tutawataka viongozi wa dini kabla ya kwenda makanisani kuhubiri ubaya wa rushwa tutataka kushauriana nao kwanza, tunakwenda wapi?

“Mimi si Mkatoliki, lakini nasoma elimu ya uraia wanayotoa na si mwaka huu, kuanzia mwaka 1994, 1999 na 2004, lugha imekuwa ikibadilika kulingana na wakati…sasa tusijadili au kupinga mambo kwa kutazama mwingiliano wa maslahi ya vikundi, tutazame manufaa kwa Taifa.

“Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki mcha Mungu, kila siku ya kawaida alikuwa anakwenda kanisani saa 12 kusali, lakini hata siku moja hakuingiza masuala ya dini kwenye uongozi wa nchi.

“Leo viongozi wa siasa ndio tatizo, wanaingiza siasa kwenye dini. Viongozi wa dini si tatizo, tatizo viongozi wa kisiasa, kwenye Pasaka au Krismasi wanaandaa hafla na kukaribisha viongozi wa dini na kupiga siasa, mwezi Ramadhani hata wasio Waislamu wanaandaa futari, sikukuu za kidini zinatumiwa na wanasiasa kupiga siasa,” alisema.

Alionyesha wasiwasi wake pia kuhusu kesi za ufisadi, zikiwamo za EPA akitilia shaka kuwa zimekuwa na misingi ya kisiasa zaidi kuliko misingi imara ya kisheria.

“Niombe Rais asihusishwe kwenye masuala ya kesi hizi, vyombo vinavyohusika vichunguze na kufungua mashitaka wasimhusishe Rais kuelezea.

“Kwa sababu kwa mfano EPA, wametueleza kampuni 22 zimeiba na nyingine zimerudisha fedha na hiyo ni taarifa ya Rais, leo baadhi wameshitakiwa, lakini fedha walizorudisha zimepangiwa matumizi.

“Inakuwaje kama wakishinda kesi? Watendaji waliomshirikisha Rais wataweza kusema aliwashurutisha,” alisema Warioba.

Akitoa mfano, alisema kesi ya aliyekuwa Kamishna wa Polisi Abdallah Zombe, hakuna shaka kwamba watu waliuawa, lakini kwa nini wauaji hawapatikani?

“Kesi ziandaliwe mashitaka kwa misingi ya kisheria na si kisiasa, tuliwahi kufanya hivi kisiasa mwaka 1979 Operesheni Mitumba, na mwaka 1983 Operesheni Wahujumu Uchumi, lakini Taifa lilipata hasara kwa kuwalipa baadhi ya washitakiwa walioshinda kesi,” alionya Warioba.

Hata hivyo, katika hatua nyingine alitaka utata wa kifisadi katika masuala ya kampuni za Deep Green na Meremeta upatiwe majibu kwa wananchi ambao tayari wamepewa taarifa zinahusu masuala hayo.

“Jamii imekwishapewa taarifa kuhusu masuala kama ya Deep Green na Meremeta, yameshafika huko na wananchi wanasubiri taarifa, si vizuri kukaa kimya…ukimya ni kujiandalia matatizo makubwa zaidi,” alishauri Jaji Warioba.

Akizungumzia baadhi ya wabunge kuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi, Warioba alisema waachwe waendelee na angefurahi zaidi kama kundi hilo lingeongezeka idadi.

“Kumekuwa na kauli za utata miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM kuhusu kilichotokea kwenye kikao cha NEC Dodoma, sijui tumwamini nani kati yao, maana kila mmoja amekwisha kusema lake.

“Lakini ukiangalia utaona kuna wanaopinga maovu, na kuna wengine wanataka kasi ipunguzwe, mimi nataka waongezeke wanaopinga na kuungwa mkono,” alisema Warioba huku akionekana dhahiri kupinga mitandao ya kisiasa ndani ya vyama, hususan CCM.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba kwa ujumla, nchi inakabiliwa na ombwe la uongozi kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, wilaya na maeneo mengine.

Alisema yapo masuala kadhaa ya kuangalia kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani, ili kujiepusha na kile alichoita EPA na Deep Green nyingine.

“Wapo viongozi, na wengine wabunge wanalalamika fedha kutawanywa huko kwenye majimbo, haya yamesikika viongozi wamekaa kimya.

“Hivi karibuni nimesoma kwenye gazeti kuna kadi bandia za CCM zimekamatwa zilizochapishwa ili zitumike kumpa ushindi mgombea fulani.

“Sasa kwenye baadhi ya maeneo nchini, mshindi ndani ya CCM ndiye mshindi wa nafasi ya uongozi wa ki-serikali, matukio kama haya ni hatari. Tulipiga kelele kuhusu sheria ya takrima hadi tunakwenda kwenye uchaguzi bado msimamo halisi wa kisheria haujajulikana,” alisema katika mazungumzo hayo ambayo Raia Mwema itayachapisha katika toleo lijalo.

Friday, October 2, 2009

TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Jaji Kiongozi Mstaafu Amiri Manento, atazungumza na waandishi wa habari mnamo tarehe 04. 10. 2009 (Jumapili), Haki House, Barabara ya Luthuli, jijini Dar es Salaam saa 5.00 asubuhi.

Mazungumzo hayo yatahusu ziara ya utafiti na uchunguzi wa hadharani ikiwemo uelimishaji umma kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa makundi yanayohitaji ulinzi maalum (k.m. wanawake, watoto na walemavu) katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Thursday, October 1, 2009

'Watakaomkaanga' Liyumba hadharani kesho

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisabababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 200 kupitia ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayomkabili Amatus Liyumba, leo unatarajiwa kutaja idadi ya mashahidi wao.

Kesi hiyo iliyoko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, upande wa mashitaka umekamilisha upelelezi wake na mara ya mwisho kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani, Liyumba alisomewa mashitaka yake kwa mara nyingine ikiwa ni pamoja na maelezo ya mashitaka.

Imedaiwa mahakamani kuwa, Liyumba alifanya mabadiliko katika ujenzi wa majengo hayo bila kupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi ya BoT.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo wa zamani wa Utawala na Utumishi BoT, alishangazwa na madai hayo kuwa alifanya mabadiliko ya ujenzi wa majengo hayo bila kupata ruhusa ya Bodi ya BoT na kuhoji kuwa kama ruhusa haikutolewa, fedha zote hizo za malipo zilitoka wapi.

Mbele ya jopo la mahakimu wakiongozwa na Hedson Mkasmongwa, Liyumba alidai BoT ilisaini mkataba wa ujenzi wa majengo hayo Juni 25, 2002 na ujenzi ulitakiwa ukamilike kwa miaka mitatu.

Ilidaiwa mshitakiwa pamoja na aliyekuwa Gavana kipindi hicho, Dk. Daudi Ballali ambaye sasa ni marehemu, bila kupata ruhusa ya Bodi ya BoT, waliamua kubadilisha ujenzi wa mradi huo na kufanya mabadiliko katika ujenzi mzima jambo ambalo liliongeza gharama kwa asilimia 80.

Makala amshambulia Warioba

KIONGOZI mwandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makala, amemshambilia Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, kwa kudai kuwa ana ajenda ya siri dhidi ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete.

Makala amesema, Warioba ni sehemu ya matatizo yanayoendelea nchini kwa sababu haoneshi njia za kuyatatua.

"Kauli zake zimeelekea siku zote kutaka kuwaonyesha Watanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Nne haijafanya jambo hata moja jema.Ni lini atatoka akasifia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne imefanya mambo mazuri kwa wananchi,” amesema Makala.

Mwanasiasa huyo ni Katibu wa Idara ya Fedha na Uchumi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Taarifa ya Makala imemtuhumu Warioba kuwa ni mtu wa kulaumu tu na hatoi hoja za kujenga.

“Kuna usemi usemao kuwa ukiwa unajua tatizo na huonyeshi njia za kutatatua tatizo, wewe pia ni tatizo. Kwa muda mrefu, matamshi ya Mzee Warioba yamekuwa yakilenga kuilaumu Serikali ya Jakaya Kikwete. Mimi nachelea kusema kuwa Mzee Warioba amekuwa mzee mchochezi namba moja kutengeneza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali yake,” alisema Makala.

Amemshangaa Jaji Warioba kwa kutotaka kuamini utafiti uliofanywa na watafiti kuwa Serikali ya CCM inakubalika na imekuwa kushinda katika uchaguzi mdogo kuonesha kuwa bado iko imara.

“Hivi CCM kuendelea kushinda chaguzi nyingi ndogo, yeye haoni CCM bado imara na wananchi wana imani nayo? Au vita ya kupambana na ufisadi inayoendeshwa na wanaCCM haamini ni matendo ambayo CCM imetamka katika Katiba yake na ni ajenda ya kudumu,” amehoji Makala na kumtaka Jaji Warioba akosoe na ajue pia kusifu.

Amemuomba Warioba aiche Serikali ya Awamu ya Nne iendelee kuwatumikia wananchi kuwaletea maendeleo na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

“Msingi wa umoja, amani na mshikamano kwa Watanzania ni mambo muhimu kwa ustawi wa nchi yetu ambavyo kwa kauli za Warioba anataka kuvunja misingi hiyo. Nawataka Watanzania kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, na rais wao kipenzi Jakaya kikwete,” amesema Makala.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), Sophia Simba amesema,Jaji Warioba ana haki ya kusema aliyoyasema, lakini anaamini watendaji wa Serikali wakiwemo mawaziri wanafanya kazi zao ipasavyo na kwa misingi ya utawala bora.

Waziri Simba amesema, kutokana na vyeo alivyowahi kuwa navyo katika serikali kama Makamu wa Kwanza wa Rais; Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yeye(Simba) ni mtu mdogo kumjibu Jaji Warioba.

“Kwa kauli yake ni kama Rais anawashauriwa vibaya na pia labda watu hawatekelezi wajibu wao kuhusu kupambana na rushwa, ana haki kuzungumza haya, lakini marekebisho ya sheria yaliyofanyika ni pamoja na hayo ya kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa,” amesema.

“Sasa kwa sheria mpya ya rushwa ya mwaka 2007, imeongeza makosa zaidi ya 25 badala ya nane yaliyokuwepo awali, hii yote ni kuwezesha utekelezaji na tunaona kesi kubwa na watu wazito wanafikishwa mahakamani, huusio utani ni kazi inafanyika,” aliongeza Simba.

Simba amesema, hata Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeweka bayana mapambano dhidi ya rushwa hivyo kazi inafanyika na baadhi imeanza kuonekana.

Amesema, hiyo ni hatua ya kudhihirisha kuwa nchi inazingatia utawala bora na watendaji katika nafasi zao wanafanyakazi zao.

Kwa upande wake, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, John Chiligati amesema leo kuwa, CCM haina nafasi ya kulumbana na wazee wakongwe wa chama badala yake kusikiliza ushauri wao na unaofaa kuzingatiwa.

“Kwanza nisingependa kuingia katika malumbano na wazee wa chama, lakini pia mawazo yake tumeyasikia na tunashukuru,” amesema Chiligati.

Alisema hakuna nchi yoyote duniani ambayo mfumo wa utawala unaoongozwa na binadamu uliokamilika, bali wa Mungu pekee na kukiri upungufu upo kwa kuwa fikra na utendaji kazi unatofautiana.

Amesisitiza kuwa,suala la mpasuko ndani ya chama na mfumo huo wa utawala ni mambo ambayo tayari Rais Kikwete aliyazungumzia alipozungumza na wananchi, hivyo yeye hana cha kuongeza.

Warioba jana aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, mwelekeo wa nchi si mzuri hasa katika suala la kulinda amani, utulivu na mshikamano kutokana na mfumo dhaifu wa kupambana na rushwa uliopo na kutahadharisha kama hautafanyiwa kazi, nchi inaelekea kubaya.

Pia aliwashutumu watendaji na washauri wa rais hasa wa masuala ya rushwa kwamba wanamshauri vibaya kwa kile alichosema si sahihi rais kuzungumzia kesi za rushwa katika hatua za awali huku mfumo wa kisiasa ukilazimisha watu kufikishwa mahakamani bila uchunguzi wa kina kwani kuna hatari serikali ikajiingiza katika kuwalipa wa fidia itakaposhindwa.