RAIS Jakaya Kikwete amewashutumu watu na hasa asasi zisizo za Serikali (NGOs) kwa kukosa uzalendo na kutangaza mabaya ya nchi zao na kuacha mazuri kwa lengo la kupata ufadhili.
Amesema, mashirika hayo yanayochipuka kama uyoga, yamekuwa yakiainisha mabaya ya nchi zao kana kwamba hakuna kitu kizuri kinachofanyika nchini, huku wengine wakijifanya kutoona mazuri kwa sababu tu hawawapendi viongozi walio madarakani.
Kikwete alisema hayo juzi wakati akizungumza na mamia ya wajumbe kutoka nchi za Afrika waliohudhuria Mkutano Mkuu wa 100 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) unaohitimishwa leo jijini Geneva.
Alikuwa akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya washiriki wa mkutano huo muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano huo ulioshirikisha nchi 185 wanachama wa ILO.
Miongoni mwa maswali aliyoulizwa, mojawapo ni la mjumbe wa Cameroon, Bissala Isaac, aliyesema vyombo vya habari vimekuwa vikiandika mambo mabaya ya Afrika licha ya kwamba yapo maendeleo, huku viongozi wa nchi husika wakishuhudia bila kuchukua hatua.
Akimjibu, Rais Kikwete alisema hilo lipo, ingawa upo wakati vitakuja kubaini kwamba Afrika haitaendelea kuwa Bara la kuandikwa habari zisizopendeza.
“Afrika si ile ya miaka 30 iliyopita. Angalia nchi zetu; mfano Tanzania, tulikuwa na wahitimu wa chuo kikuu 12, lakini sasa tunazungumzia watu 124,000 wanaosomea shahada vyuo vikuu,” alisema.
Rais ambaye alitumia mifano ya Tanzania kuelezea suala hilo lakini bila
kutaja ama aina ya mashirika au watu wanaofanya hivyo, alisema tatizo
lililopo ni kuangalia mambo kwa kuzingatia NGOs zinazochipuka kutoka Ulaya, zenye mtazamo hasi kwa yanayofanywa na Serikali zao, wakilenga kupata misaada.
Akiendelea kutoa mfano wa maendeleo katika Tanzania, Rais Kikwete alisema, “tulitegemea wahandisi watatu … hadi sasa bado tuna tatizo hilo? Ni kilometa ngapi za barabara za lami tunazo? Wakati ule hazikufika hata kilometa 100 lakini sasa tunazungumzia kilometa zipatazo 7,000.
“Kwa kuwa mwanaharakati mmoja kapigwa na polisi, basi suala hilo linafanywa kuwa la kitaifa. Wanachojaribu kufanya ni kusema mabaya ili wafadhili wawape fedha, ukisema mazuri hupati,” alisema na kuendelea kushangiliwa.
Umati uliendelea kumshangilia kwa kupiga makofi zaidi aliposema, “uzalendo katika nchi zetu unapaswa ujengwe miongoni mwa wananchi. Si kusema mabaya pekee ya nchi. Hebu jaribu kumsema vibaya Obama (Barack-Rais wa Marekani) usikie; magazeti yote na hata yale ya kihafidhina yatakuandama. Lakini kwa Afrika, wanajivunia kusema mabaya”.
Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema ipo changamoto kubwa ya kuwa kiongozi katika nchi masikini.
Akijibu swali la mjumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambaye pamoja na mambo mengine, alihoji sababu za viongozi wa Afrika kutoweka mikakati ya uwekezaji, Rais Kikwete alisema ingawa binafsi anataka nchi ikue kiviwanda, vipo vikwazo pia.
Kwa mujibu wake, suala si kwamba hakuna malighafi, isipokuwa uwekezaji mkubwa unahitaji fedha nyingi. Alisema nchini hakuna benki za mitaji na matokeo yake, chache zilizopo ni za biashara hali ambayo inakwaza juhudi za kuhamasisha maendeleo ya viwanda.
Hata hivyo, alizihimiza nchi za Afrika kuwa kinachohitajika ni kuunganisha raslimali na kusaidiana. Alisema ana matarajio makubwa, kwamba katika miongo miwili ijayo, watakaokuwapo, watashuhudia mabadiliko makubwa barani.
Katika hatua nyingine, Rais alipokuwa akihutubia mkutano wa ILO, pamoja na mambo mengine, alisema panahitajika ushirikiano wa Serikali, jamii ya
wafanyabiashara, asasi za kijamii na wabia wa maendeleo kuhakikisha kasi ya
kutengeneza ajira katika nchi zinazoendelea inaongezwa.
Alisema tatizo la ajira linawakumba zaidi vijana katika nchi zinazoendelea na nyingi
zinazotolewa chini ya sekta binafsi hazikidhi mahitaji ya kazi za staha. Alisema wengi wanaingia kwenye sekta binafsi si kwa kuichagua, bali kujikimu.
No comments:
Post a Comment