Monday, June 20, 2011

TAHLISO yatoa tamko kuhusu UDOM

UMOJA wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) umeiomba Serikali iangalie kwa kina madai ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) na iyafanyie uchuguzi ili kufikia uamuzi wa msingi utakaowezesha kuwarudishwa chuoni waendelee na masomo.

Mwenyekiti wa Tahliso, Mathias Kipala ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) alisoma tamko la umoja huo baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa siku mbili uliohitimishwa mwishoni mwa wiki.

Jumatano wiki iliyopita, wanafunzi 400 walipewa saa nne wawe wameondoka chuoni hapo eneo la Chimwaga, kutokana na kile kilichoelezwa ni kukithiri kwa vurugu zilizokuwa zikifanywa na wanafunzi.

Licha ya wanafunzi hao kutoka Sayansi ya Sanaa, wengine 1,000 wa Chuo cha Sayansi ya Teknolojia ya Mawasiliano (CIVE) wana zaidi ya mwezi mmoja tangu chuo chao kifungwe kwa muda usiojulikana baada ya kuibuka vurugu zilizoambatana na maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakiwasilisha madai mbalimbali.

Katika tamko hilo, Tahliso inayoundwa na Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu 48, imeendelea kuiomba Serikali iridhie kutoa fedha ya chakula na malazi kutoka Sh 5,000 hadi Sh 10,000 kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Mweyekiti huyo alisema wajumbe wa Mkutano Mkuu wameiomba Serikali na Wabunge wapitishe inayozingatia maombi hayo.

“Hapa tunatahadharisha bayana kwamba ongezeko la fedha za chakula na malazi lisije kuwa ndicho chanzo cha kuongezeka kwa karo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika chuo chochote kile, kiwe cha binafsi au cha Serikali…ongezeko hili lipo katika kukidhi mahitaji ya chakula na malazi yaliyopo leo,”alisema Kipala.

Wakati huo huo tamko hilo lililotolewa na TAHLISO, limepinga waraka wa serikali namba 178 unaowalazimisha wanafunzi kubadili muundo wa Serikali bila ridhaa yao ya kubadili katiba zao kama ilivyo desturi ya taasisi yoyote. Walisema hali hiyo inachangia vurugu vyuoni.

Umoja huo ulisisitiza juu ya azma ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuendelea kuungana kuhakikisha msingi wa utawala bora unadumishwa nchini.

No comments: