Tuesday, January 29, 2013

Semina: Mrejesho wa Ukusanyaji wa Maoni ya Katiba Mpya na Mpango wa Kushiriki Mabaraza ya Katiba Mpya



SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO

UNAKARIBISHWA KATIKA JUKWAA LA WAZI LA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO, AMBAPO WIKI HII MTOA MADA NI DIANA KIDALA WA JUKWAA LA KATIBA

MADA:  Mrejesho wa Ukusanyaji wa Maoni ya Katiba Mpya na Mpango wa Kushiriki Mabaraza ya Katiba Mpya
Lini: Jumatano Tarehe 16/01/2013

Muda: Saa 09:00 Alasiri – 11:00 Jioni

MAHALI:  Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni  


WOTE MNAKARIBISHWA

Thursday, January 10, 2013

TUCTA Wataka Haki Ya Maandamano Na Migomo

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limependekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, migomo na maandamano viwe haki ya msingi ya raia.

Wakati Tucta likitoa pendekezo hilo, Chama cha UPDP kimeungana na CCM kutaka mgombea binafsi aruhusiwe, huku NCCR Mageuzi kikiungana na Chadema kutaka umri wa urais ushushwe na apunguziwe madaraka

Tucta, mbali na kutaka maandamano na migomo viruhusiwe, limependekeza hayo yafanyike kisheria baada ya kufutwa sheria kandamizi zinazowabana wafanyakazi wanaodai haki na masilahi yao.

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholas Mgaya alisema jana baada ya kuwasilisha maoni ya shirikisho hilo kuwa Katiba Mpya lazima iwe mkombozi wa wafanyakazi.
Alisema wanataka Katiba itamke kwamba kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kugoma na kufanya maandamano wakati wanapoona haki zao hazizingatiwi.

“Sheria zilizopo zinazoruhusu maandamano na migomo ni kandamizi. Tunataka Katiba Mpya izifute na ziwepo sheria ambazo si kandamaizi ili kuwapa nafasi wafanyakazi kudai haki zao kwa maandamano bila vikwazo.”

Mgaya alisema Katiba Mpya iwe na kifungu kitakachoeleza uhusiano kazini ili kuhakikisha wafanyakazi wananufaika na kazi wanazofanya.

“Tunataka Katiba Mpya itamke kila mfanyakazi atakuwa na haki ya kushiriki na kushirikishwa kupitia vyombo mbalimbali vya mashauriano na vinavyohusika katika uamuzi wa kazi. Hiyo itakuwa njia sahihi ya kutoa nafasi kwa wafanyakazi kueleza mambo ambayo wanaona hawanufaiki nayo katika sehemu zao za kazi,” alisema.

Pia alisema: “Tunataka Katiba Mpya itamke kwamba ndani ya Bunge kutakuwa na uwakilishi wa wafanyakazi ili kutatua matatizo ya wafanyakazi.”

UPDP na mgombea binafsi
Mkurungezi wa Sheria na Katiba wa UPDP, Juma Nassoro alisema pamoja na mambo mengine, wamependekeza mgombea binafsi aruhusiwe katika nafasi zote za uongozi isipokuwa urais.

Alisema mfumo wa sasa unaolazimisha mgombea kutokana na chama cha siasa ni kuwanyima wananchi wasio na vyama kushiriki katika uongozi wa nchi kwa kutumia haki yao ya kuchagua na kuchaguliwa.

Alisema mantiki ya kutaka mgombea wa urais atokane na vyama vya siasa ni kutoa nafasi kwa wananchi kufanya tathmini za sera za vyama husika... “Yawezekana mtu akajitokeza kuwa mgombea urais na akawa na sera inayopingana na Katiba na maadili ya nchi. Ili kuepuka hilo Katiba Mpya isiruhusu mgombea binafsi kwa nafasi ya urais.”

Pia alisema wamependekeza muundo wa Serikali uwe wa Serikali tatu; Tanganyika, Zanzibar na Muungano... “Katika uongozi kwenye Serikali hizo kutakuwa na marais watatu kutoka kila Serikali huku Serikali za Tanganyika na Zanzibar zikiwa na mawaziri viongozi na ya Muungano ikiwa na waziri mkuu atakayeteuliwa na Rais wa Muungano na kuthibitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.”

Wednesday, January 9, 2013

TGNP Watoa Maoni Ya Mabadiliko Ya Katiba Mpya

Mwanachama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Asseny Muro akitoa maoni ya mtandao huo kuhusu Katiba Mpya katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Jumatano, Jan. 9, 2013), katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa TGNP Bi. Mary Rusimbi na Mjumbe wa Bodi ya mtandao huo Prof. Ruth Meena.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea katika mkutano na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) uliolenga kupata maoni ya mtandao huo kuhusu Katiba Mpya leo (Jumatano, Jan. 9, 2013), katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Jaji Warioba ni Bi. Ussu Mallya, Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao huo, Prof. Ruth Meena 9Mjumbe wa Bodi ya TGNP) na Mwenyekiti wa TGNP Bi. Mary Rusimbi.

Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Dkt. Sengondo Mvungi akiongea katika mkutano na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) uliolenga kupata maoni ya mtandao huo kuhusu Katiba Mpya leo (Jumatano, Jan. 9, 2013), katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Wajumbe wengine wa Tume Bi. Mary Kashonda na Bi. Salma Moulidi.

TGNP pamoja na Tume Ya Mabadiliko ya Katiba katika Picha ya Pamoja
Mwananchama wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Bi. Subira Kibiga akitoa maoni ya mtandao huo kuhusu Katiba Mpya katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba leo (Jumatano, Jan. 9, 2013), katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Wengine ni wananchama wenzake Bi. Diana Mwiru (kushoto) na Bi. Asseny Muro.


Na Deogratius Temba
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), leo wamekutana na Tume ya Kuratibu mchakato wa Katiba Mpya katika ofisi za Tume hiyo zilizoko jijini Dar es salaam.

TGNP waliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Usu Mallya, Mwenyekiti wa Bodi Mary Rusimbi naMkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia,  wakuu wa idara, wanachama, wafanyakazi na  wawakilishi wa vikundi vya kijamii vinavyoshiriki katika shughuli za harakati na TGNP.

Wakizungumza wakati wa kuwasilisha maoni yao kwa mtazamo wa Kijinsia, wanaharakati hao wamesema kuwa katiba mpya ni lazima itambue mchango wa wanawake katika maendeleo na uchumi wa taifa haswa kutambua shughuli za wanawake sizizo na kipato au sizizo rasmi. Haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika mgawanyo wa rasilimali na nafasi za kutoa maamuzi serikali, haki za msingi za kijamii kama maji, afya, elimu, kilimo na ufugaji.

TGNP wameshauri Tume kuhakikisha inachukua masuala ya msingi yanayohusu wanajamii walioko pembezoni hasa wanawake na kuyaingiza kwenye katiba mpya ili changamoto ambazo zimekuwa zikimkabali Mwanamke ziondoke kabisa au kupungua baada ya kupatikana kwa katiba mpya. 

Kwa upande wake Mjumbe wa Tume Mary Kashonda, alisema kuwa  wanaharakati kutoka TGNP wana nafasi kubwa katika kuhakikisha wanatoa maoni yanayobeba sauti za wanawake walioko pembezoni hata wasio jua kusoma kutokana na ukaribu wao na jamii hasa wanawake wa pembezoni.

“Wanawake wengi huko vijijini hawawezi kuzungumza mbele ya wanaume, na ukiwaambia waandike hawawezi kwasababu hawajui kusoma na kuandika. Hili ni tatizo, Nyie TGNP mna fursa ya kukutana nao na kuwasilikiza   wakizungumza maoni yao ni muhimu sana…. Bila shaka mnayo”alisema Kashonda.