BUNGE limekubali kujadili msimamo wa Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza kutoa fedha za tozo za rada kwa asasi za kiraia badala ya kuzitoa kwa Serikali ya Tanzania.
Hoja ya kujadili suala hilo ilitolewa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) na kuungwa mkono na baadhi ya wabunge baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kutoa kauli ya Serikali kuhusu suala hilo.
“Tutatafuta muda muafaka wa kulijadili suala hili,” alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda. Kampuni hiyo imeamua kutoa pauni milioni 29.5 (Sh bilioni 75) zinazotokana na tozo ya fidia ya mauzo ya rada kwa wananchi wa Tanzania kupitia asasi za kiraia za Uingereza badala ya Serikali ya Tanzania.
Akitoa kauli ya Serikali, Membe alisema Serikali ya Tanzania imetahadharisha kwamba haitaruhusu asasi ya kiraia yoyote ile ya Uingereza itakayonufaika na fedha hizo kuja kuendesha shughuli zake nchini.
“Tanzania ni nchi masikini, lakini haiko tayari kudharauliwa kiasi hicho kwa Serikali yake, taasisi zake na asasi zake kutoaminiwa,” alisema Membe na kuongeza kuwa, “kuruhusu kufanya hivyo ni kuruhusu kuibiwa kwa mara ya pili.” Aliliambia Bunge kuwa “tuwe tayari kupoteza fedha hizo kwa kulinda heshima ya Taifa letu. Tusiwe tayari kudhalilishwa na kuruhusu kampuni iliyotuibia iamue fedha zetu apatiwe nani huko Uingereza na zitumike vipi hapa nchini.”
Waziri huyo alitoa kauli hiyo wakati tayari Bunge limetuma wabunge wanne kwenda Uingereza kukutana na kamati husika iliyoundwa na BAE Systems na kufanya mazungumzo na wabunge wa Bunge la Uingereza.
Wabunge hao ni Naibu Spika Job Ndugai (Kongwa –CCM), Mussa Zungu (Ilala - CCM), Angellah Kairuki (Viti Maalumu –CCM) na John Cheyo (Bariadi Mashariki – UDP).
Wabunge hao pia watakutana na viongozi wengine wenye ushawishi mkubwa nchini Uingereza kuwashawishi waishinikize Kampuni ya BAE Systems kuzitoa fedha hizo kwa Serikali ya Tanzania bila masharti yoyote.
“Kampuni ya BAE Systems ina masikio, lakini haitaki kusikia kilio cha wengi, imeonyesha dharau ya wazi dhidi ya Serikali yetu na watu wake,” alisema Membe.
Alisema iwapo Serikali itapata fedha hizo, imedhamiria kuzielekeza fedha hizo kwenye sekta ya elimu ikiwemo kununua vitabu milioni 4.4 kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi, kununua vitabu 192,000 vya kufundishia kwa ajili ya walimu wa shule za msingi.
Pia alisema watanunua madawati 200,000 kwa ajili ya wanafunzi 16,000 wa shule za msingi na kujenga nyumba 1,996 za walimu wa shule za msingi vijijini na kujenga vyoo 200,000 kwenye shule za msingi nchini.
Kampuni ya BAE Systems iliamuriwa na Mahakama nchini Uingereza kulipa faini hiyo baada ya kugundulika kwamba ilikwenda kinyume katika kuiuzia Tanzania rada mwishoni mwa miaka ya 1990.
No comments:
Post a Comment