WATANZANIA wengi hawaelewi kuwa ukatili wa kijinsia ni kosa kisheria ndiyo maana kesi hizo huishia katika familia badala ya kwenye vyombo vya sheria vinavyohusika.
Mkuu wa Huduma za Polisi Jamii, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Basilio Matei, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya wiki moja kwa maofisa, wakaguzi na askari.
Mafunzo hayo yalihusu kupambana na ukatili wa kijinsia na yalishirikisha askari kutoka mikoa ya Mwanza, Kagera na Shinyanga.
Matei alisema, kuna tatizo kwa wanawake wanaofanyiwa ukatili huo kulifanya jambo hilo la kifamilia na kulimalizia katika ngazi za chini bila ya wanaofanya vitendo hivyo kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Polisi imeliona hilo ndio maana limeamua kutumia ulinzi shirikishi kulifuatilia suala hili na kulikomesha kwa kuwa hatua zikishachukuliwa wengine nao wataacha vitendo hivi,” alisema Matei.
Naye Mshauri wa mambo ya jinsia kutoka Programu ya Maboresho ya Sekta ya Sheria nchini, Wanyanda Kuta alisema askari wakipata elimu ya unyanyasaji wa kijinsia, itasaidia kwa kuwa wao ndio watu wa kwanza kupokea mashitaka kutoka kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake (TPF-Net) Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Zuhura Munisi aliwataka wanaoendeleza unyanyasaji wa kijinsia kuacha mara moja kwa kuwa kila mmoja ana haki ya kuishi kwa uhuru na haki.
Alisema zama za sasa hakuna mtu aliye juu ya mwingine na baada ya mafunzo hayo washiriki wataelewa jinsi ya kuwapokea wahanga, na jinsi ya kutunza kumbukumbu zao hasa kesi za kubaka na kulawiti na kuzishughulikia haraka.
Munisi alisema mafunzo hayo yametolewa pia kwa askari katika mikoa ya kipolisi ya Ilala, Temeke, Kinondoni na Kilimanjaro na lengo ni kufikisha elimu hiyo kwa askari wote waliopo katika madawati ya jinsia katika vituo vya polisi.
No comments:
Post a Comment