Thursday, April 29, 2010

Baadhi wakataa matokeo ya utafiti wa Redet

UTAFITI uliofanywa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) kuhusu uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, umewasha moto miongoni mwa wabunge na wanasiasa, wengi wao wakiuponda huku wabunge wengi wakijiamini kushinda katika majimbo.

Wabunge na wanasiasa hao walizungumza jana na HABARILEO kwa nyakati tofauti, wengi wao wakionesha wasiwasi juu ya utafiti huo, huku wanasiasa wa vyama vya upinzani wakisema utafiti huo umetengenezwa kwa manufaa ya CCM.

Mbunge wa Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, aliliambia gazeti hili kuwa anashangazwa na jinsi utafiti huo ulivyofanywa jimboni mwake, ingawa alisema haujamshtua wala hautamnyima usingizi, kwa kuwa ana imani kuwa kazi aliyoifanya jimboni inampa dalili zote za kurudi.

“Nashindwa kuelewa hiyo asilimia wameitoa wapi, ila naichukulia kama changamoto kwangu, ninachofahamu mimi hawa Redet walikuja Mkuranga, wakapiga picha, jambo ambalo si sawa na mtu akiangalia mpira mwanzo mpaka mwisho, picha haisemi sana,” alisema Malima.

Alisema tangu kushika kwake madaraka Mkuranga hali ya mapato ya wilaya imeimarika kutoka makusanyo ya Sh milioni tisa hadi Sh milioni 100.

Kwa mujibu wa utafiti, asilimia 46.0 ya waliohojiwa katika jimbo hilo walisema hawatamchagua tena na asilimia 38.8 ndio waliothibitisha kumchagua.

Naye Mbunge wa Pangani, Mohammed Rished, alisema utafiti huo una walakini ingawa filimbi ya mwisho ni dakika 90 ambayo ni siku ya uchaguzi.

“Tusubiri uchaguzi ufike, kwa kuwa ninachojua, mimi sina tatizo jimboni kwangu, kama mbunge nimetekeleza Ilani ya chama changu na ziada.

Hivyo katika hili tuwaachie wananchi.” Asilimia 4.2 ya wahojiwa katika jimbo la Rished ndio watakaomchagua kwa mujibu wa utafiti, wakati asilimia 87.5 walisema watachagua mbunge mwingine.

Kwa upande wake, Mbunge Kasulu Mashariki, Daniel Nsanzugwanko, ambaye utafiti unaonesha asilimia 20 ya wahojiwa ndio watakaomchagua na asilimia 68 kumkataa, alisema utafiti huo haujaweka wazi ni jimbo gani ambalo linatajwa na wananchi, kwa kuwa katika wilaya hiyo kuna majimbo ya Kasulu Mashariki na Magharibi.

“Mwenzangu wa Magharibi, Kilontsi Mporogomyi ana vipindi vitatu vya ubunge katika jimbo lake, mimi viwili, waweke wazi ni nani anayetajwa na utafiti huu, hata hivyo kwa upande wangu nina kila dalili na vigezo vinaonesha nitarudi bungeni mwakani,” alisema Nsanzugwanko.

Naye Mbunge wa Tarime, Charles Mwera, alisema pamoja na kwamba hafahamu namna utafiti huo ulivyofanyika, lakini hawezi kupuuza matokeo.

“Inategemea ni akina nani walihojiwa, hasa kwa sisi wa vijijini ila kwa nafasi yangu nina imani nina nafasi nzuri ya kutetea nafasi yangu,” alisema Mwera ambaye asilimia 24.5 walionesha watamchagua huku asilimia 61.2 wakionesha kuchagua mwingine.

Pamoja na wabunge hao wengine wanaotajwa na utafiti huo wa Redet kuwa viti vyao si salama ni wa Njombe, Anne Makinda na Yono Kevela, wa Sumbawanga Mjini Paul Kimiti ingawa alishatangaza kutogombea na wa Iramba Mashariki na Magharibi, Mgana Msindai na Juma Kilimba.

Wengine ni wa Kiteto, Benedict Nangoro, Dodoma Mjini Ephraim Madeje ambaye pia ametangaza kutogombea; Wete, Mwadini Jecha; Micheweni, Shoka Khamis Juma; Chake Chake, Fatma Maghimbi; Mkoani, Ali Khamis Seif na Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.

Wengine ni wa Liwale, Hassab Kigwalilo; Mtwara Mjini, Mohammed Sinani; Kigoma Mjini, Peter Serukamba; Iringa Mjini, Monica Mbega; Bukombe, Emmanuel Luhahula; Lushoto, Abdi Mshangama; Biharamulo Phares Kabuye ambaye alifariki dunia na wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga.

Lipumba, alisema utafiti huo unaonesha ni wa kupikwa, kwa ajili ya kuipigia debe CCM. “Redet ilipaswa kuhamasisha demokrasia, lakini sasa inaikandamiza, matokeo haya ni kuhalalisha wizi wa kura kwenye uchaguzi ujao, inasikitisha sana.”

Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema utafiti huo umeonesha jinsi Kikwete alivyo maarufu na kuwataka wenzake wajifunze kupitia hapo.

“Tujifunze jamani, mwaka jana utafiti kama huu tuliudharau na huu wa leo unaonesha yale yale.” Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Pius Msekwa, alisema pamoja na kwamba utafiti huo umeonesha asilimia kubwa ya wabunge ambapo wengi wa CCM wanaweza wasirudi mwakani kwenye majimbo yao, chama hicho hakiwezi kuathirika kwa kuwa rungu la kumteua mgombea wa jimbo kwa kura za maoni wamepewa wananchi.

Juzi akitoa matokeo ya utafiti huo wa 16, Dk Killian, alisema anafahamu kuwa utafiti huo utakuwa gumzo na kila mtu atasema lake, lakini wao wanataaluma wanaamini utafiti huo ni huru. “Hatuogopi kusema ukweli na tunafanya kazi yetu kwa misingi ya uwazi na taaluma, hatujali tunamgusa nani.”

Kwa mujibu wa utafiti huo, uliofanywa Machi mwaka huu, asilimia 61.7 ya wabunge walioko madarakani wako katika hatihati ya kurudi bungeni baada ya uchaguzi huo ambapo pia umeonesha kuwa asilimia 85 ya Watanzania waliohojiwa, wanaridhishwa na chaguo lao; Kikwete.

Thursday, April 22, 2010

Wadau wadai mshahara mpya ni mzigo

INGAWA Serikali imeonesha kuwa sikivu na kusikiliza kilio cha wafanyakazi na kuamua kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi, wadau wa sekta hiyo wanasita kuikubali.

Hali hiyo inatokana na kinachoelezwa kuwa fedha hizo ni nyingi na ni vigumu kwa waajiri wengi wa sekta hiyo kulipa mishahara hiyo mipya kutokana na gharama za uendeshaji kupanda.

Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imesema utekelezaji katika kulipa mishahara mipya kwa asilimia 100 kama ilivyotangazwa na Serikali utakuwa mgumu na huenda ukaua viwanda nchini.

Aidha, matokeo yake yanaweza kusababisha watu kupunguzwa ajira kutokana na uchanga wa sekta hiyo kwa kuwa gharama za uendeshaji zitapanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Dk. Evance Rweikiza, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na gazeti hili, alipotakiwa kutoa maoni ya sekta hiyo juu ya kupanda kwa mishahara kama ilivyotangazwa juzi na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.

Waziri Kapuya alitangaza nyongeza hiyo alipozungumzia hatua iliyofikiwa na Serikali baada ya kumalizika kwa mazungumzo ya Shirikisho la Chama cha Wafanyakazi (TUCTA), Baraza la Ushauri la Uchumi na Jamii (LESCO) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kuhusu madai ya wafanyakazi.

Profesa Kapuya alisema kiwango hicho kitaanza kulipwa wakati wowote kuanzia sasa na kwa upande wa wafanyakazi wa Serikali walitakiwa kuvuta subira kwa kuwa mchakato unaendelea serikalini na Aprili 25 mwaka huu, wadau watakutana kwa maafikiano zaidi.

Dk. Rweikiza alisema baada ya kupata taarifa hizo katika vyombo vya habari, TPSF inajipanga kuwasiliana na wafanyabiashara ili kutoa tamko, ingawa inatambua kuwa kulipa mishahara mizuri ni jukumu lao, ili wafanyakazi waweze kuwa na tija, ila gharama za uendeshaji ni tatizo kwa sekta hiyo.

“Sekta binafsi ni changa, haina fedha na pia gharama za uendeshaji ni kubwa, hata Serikali yenyewe haiwezi kupandisha mishahara yake kwa asilimia 100,” alisema Dk. Rweikiza.

Alisema suala la kupatikana kwa umeme wa uhakika nchini ni tatizo, kodi ni kubwa na hata mazingira ya biashara nayo ni magumu na kutekelezwa kwa mshahara huo ni sawa na kuua viwanda na kuzalisha kundi lingine lisilokuwa na ajira kutokana na wengi kukumbwa kupunguzwa kazi.

Alisema kabla Waziri Kapuya hajatangaza nyongeza hiyo, alitakiwa kukutana na wahusika kujadiliana wafikie muafaka, ili isije kuzaa mgongano kama ilivyokuwa nyongeza ya mshahara ya mwaka 2007.

“Katika hili busara zaidi zitawale, hatua hii inaweza kuzalisha mgogoro kati ya waajiri na wafanyakazi, ni vyema wakutanishwe na ngazi husika kabla ya kutangazwa,” alisema Dk. Rweikiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, alisema hajauona waraka wa Waziri unaotangaza mishahara hiyo, hivyo hawezi kutoa maoni yoyote na ieleweke kuwa kila jambo lina utaratibu wake.

Alisema upo utaratibu wa kuongeza mishahara hata kama ni katika kima cha chini, ambapo hata Notisi ya Serikali (GN) bado haijatoka.

“Mimi nimeisoma taarifa hiyo kwenye magazeti, siwezi kutamka lolote, kwanza suala la kupandisha mishahara lina utaratibu wake unaopaswa kufuatwa,” alisema Dk. Mlimuka.

Wednesday, April 21, 2010

Wabunge wazidi kumbana Magufuli

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. John Magufuli, ameendelea kubanwa na wabunge wanaotaka baadhi ya vipengele kikiwemo cha usajili wa mifugo kiondolewe katika muswada ya Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo.

Dk. Magufuli aliamua kuutoa muswada huo na ule wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo za mwaka 2010 bungeni na kuurudisha tena katika Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji baada ya wabunge wengi kuipinga Alhamis iliyopita.

Alipourejesha tena katika kamati hiyo, wabunge walipata nafasi nyingine ya kuujadili baada ya wizara hiyo kuufanyia marekebisho lakini bila muafaka.

Katika kikao hicho kilichomalizika juzi usiku, Mbunge wa Simanjiro(CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema wameshindwa kuelewana na Dk. Magufuli kwa sababu hakutaka kutambua maeneo waliyotaka yafanyiwe marekebisho.

Aliiomba kamati huyo ambayo ilitegemea kuketi jana, kuangalia na kutafakari kuacha kukubali wazo la kuurejesha tena bungeni.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Ileje (CCM), Gedion Cheyo, alisema kamati yake itajadili na kutoa maamuzi kwa manufaa ya taifa yatakayoboresha huduma katika sekta hiyo.

Akizungumza awali kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Dk. Magufuli alisema kipengele cha usajili wa mifugo kimeongezewa muda kutoka siku saba hadi siku 30. Alisema pia mfugaji halazimiki kwenda kusajili mwendo mrefu bali shughuli za usajili zitafanyika vijijini hata kama ni anapokwenda kuogesha mifugo yake. Awali, akichangia katika kikao hicho, Ole Sendeka, alitaka sheria hiyo kurudishwa kwa wadau kwa kuwa wafugaji wengine hawakushirikishwa katika majadiliano ya kutengeneza miswaada hiyo.

Mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM), Jackson Makwetta, alisema sheria hizo zina mapungufu makubwa na kwamba hazitasaidia taifa kwenda mbele. Mbunge wa Kiteto (CCM), Benedict Ole Nangoro, alisema changamoto katika sekta hiyo zipo nyingi ambazo zinatakiwa kutatuliwa ili kuwezesha taifa kwenda mbele.

Mbunge wa Kalambo (CCM), Ludovick Mwananzila, alishauri kuwepo kwa benki maalum na utaratibu wa kuweka bima kwa wakulima na wafugaji ili panapotokea tatizo la kufa kwa wanyama waweze kupata mtaji wa kuanzia. Mbunge wa Rufiji (CCM), Profesa Athuman Mtulya, alisema ufugaji wa kuhamahama ni haramu na unaweza kujenga jangwa na kutaka kutengwa maeneo maalum.

Mbunge wa Bukombe (CCM), Emmanuel Luhahula, alisema maeneo mengi ya vijiji yamejaa na kuitaka serikali kutotumia sheria ya vijiji kugawa maeneo badala yake igawe yenyewe.

Tuesday, April 20, 2010

Wabunge wakosa imani na Kenya, Uganda

WABUNGE wametaka raia wa Kenya na Uganda walioajiriwa katika sekta mbalimbali nchini, kabla ya kuanza kwa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, warudishwe makwao.

Pia wameitaka serikali kuhakikisha inawanyang’anya ardhi raia wa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki walionunua ardhi nchini na irudishwe mikononi mwa Watanzania.

Wakijadili azimio la Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyowasilishwa na Waziri Dk. Diodorus Kamala, wabunge hao walisema haiwezekani raia hao wa nchi nyingine wajazane kwenye ajira za nchini wakati kuna Watanzania wengi hawana ajira.

Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM) ametaka kufanyike kwa sensa katika hoteli na sekta nyingine kubaini raia wa Kenya na Uganda wanaofanya kazi nchini na warudishwe makwao kusubiri kuanza utekelezaji wa Itifaki hiyo.

“Tunao vijana wengi tu hapa nchini wamesoma vizuri na wanaongea Kiingereza vizuri, lakini ukienda kwenye mahoteli waliojazana ni Wakenya, hawa naomba warudishwe makwao wasubiri mpira uanze tucheze sawa,” alisema mbunge huyo.

Kwa upande wa ardhi, alisema serikali ifanye utafiti kubaini raia wa kigeni hasa wanaotoka kwenye nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda walionunua ardhi katika mikoa ya mipakani wanyang’anywe ardhi hiyo.

“Ardhi ya nchi ndio mali yetu, wenzetu hawa wana matatizo ya ardhi, serikali itambue ardhi hii ni kwa ajili ya Watanzania, hivyo serikali ikafanye tafiti mipakani na kama kuna ardhi imeshanunuliwa kinyemela na wenzetu hawa irudishwe,” alisema.

Mbunge wa Masasi, Raynald Mrope (CCM), aliishambulia Kenya kuwa ndio chanzo cha kuvunjika kwa jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977 na akaonya kuwa vitendo vya Wakenya vinatishia uhai wa jumuiya ya sasa hasa vya kuibia rasilimali Tanzania kama madini ya tanzanite.

Alisema Serikali ya Kenya inawatia kiburi raia wao kuendelea kuibia Tanzania hivyo akaitaka serikali iwakemee haraka likiwemo hili suala la kupinga Tanzania kuuza meno ya tembo katika mkutano wa Cites huko Doha nchini Qatar.

Mbunge wa Makete, Dk. Binilith Mahenge alisema Tanzania sasa hivi inazalisha wasomi wengi kila mwaka na isipokuwa makini katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, vijana wengi wanaweza kujikuta hawana ajira.

Alitaka vyuo vikuu vinavyotoa elimu kuhakikisha vinawapa mafunzo na ujuzi vijana hao ili wamudu ushindani katika soko hilo. Pia aliwataka wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora ambazo zitakubalika katika nchi zingine za jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alisema kama ajira wataachiwa wageni hao kuingia holela, vijana wa Kitanzania wataenda wapi. Alitaka serikali ihakikishe kwenye sekta ya utalii inawapunguza raia hao wa Kenya ili Watanzania nao wapate ajira hizo.

Lakini alionya kuwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja, Wakenya wamejiandaa kujenga hoteli za nyota nne hadi tano katika sehemu mbalimbali nchini, hali itakayowezesha kumiliki uchumi katika maeneo hayo.

Soma zaidi

Monday, April 19, 2010

Wadau wauchambua muswada wa Sheria mpya ya Madini

MUSWADA wa Sheria ya Madini wa mwaka 2010 ambao kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa 19 wa Bunge unatarajiwa kuwasilishwa leo, jana ulichambuliwa vikali na wadau wa sekta ya madini akiwemo Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.

Wazungumzaji wengi akiwemo Waziri Wasira wamesema muswada huo haujali wachimbaji wadogo wala kutetea maslahi ya Taifa.

“Nchi inapata nini na wananchi watapata nini?” Alihoji Waziri Wasira na kuongeza kuwa lazima sheria iamue kwa makusudi kabisa kusaidia wachimbaji wadogo ambao ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya sekta ya madini kwa siku za usoni.

Waziri huyo ambaye alisema wazi, alizungumza kama mdau wa madini akiwa hana elimu ya sheria, alisema suala la madini ni suala nyeti nchini na kwa hali yoyote sheria inayotarajiwa kutoa mwongozo wa madini, lazima ijibu hoja muhimu za manufaa kwa Taifa na wananchi.

“Je haiwezekani kuwawezesha watu maskini, wawekezaji wa ndani?” Aliuliza Waziri Wasira ambaye alisema kwamba ni kuwawezesha wawekezaji wa ndani ni muhimu huku akitoa mfano wa Sweden ambayo alisema uchumi wake unaotegemea madini kwa kuwezesha wachimbaji wake wadogo wazawa.

Alisema alipokuwa katika mkutano wa Davos nchini Switzerland, Februari mwaka huu, alifanya mazungumzo na Waziri wa Madini wa Sweden ambaye hakumtaja jina lakini akasema Waziri huyo alimweleza wazi kwamba ni lazima kuweka mizania na kusaidia wawekezaji wadogo au la sivyo Taifa linaweza kubakia na mashimo kama litategemea wachimbaji kutoka nje.

Waziri Wasira alisema wazi kuwa sheria lazima ijibu hoja za sera, na ilani ya uchaguzi ambapo inategemewa na wachimbaji wadogo kuendelezwa na kuwa msingi wa uchumi hali ambayo kwa sasa sheria hiyo haina.

Soma zaidi

Thursday, April 15, 2010

Wabunge wabanwa

SERIKALI imewaagiza watumishi wa umma wasiwape wabunge taarifa za siri za Serikali zikiwemo zinazohusu mambo ya usalama wa Taifa.

Hata hivyo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Philip Marmo, amewaruhusu watumishi wawape wabunge taarifa muhimu kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Marmo amesema, wabunge hawaruhusiwi kudai taarifa zinazohusu ulinzi na usalama wa Taifa, mwenendo wa Majeshi ya Ulinzi na Polisi.

“Mkiomba taarifa hizo hamtapewa, alisema Marmo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Vijijini, Damas Nakei (CCM), ambaye alitaka kufahamu mipaka ya mbunge kupewa taarifa kutoka ofisi za umma.

Amesema, mipaka au masharti yaliyowekwa na kifungu cha 10 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, katika kutoa taarifa zinazoombwa na mbunge, ni ombi la kupewa taarifa husika na sharti liwe limetolewa na Mbunge mwenyewe na si mtu kwa niaba yake.

Sheria hiyo pia inasema ombi husika ni sharti lizingatie na kufuata masharti yaliyowekwa na sheria au kanuni nyingine yoyote kwa ajili ya kudhibiti utoaji taarifa kwa watumishi wa umma.

Pia alisema taarifa ambazo mbunge akiziomba anaweza kukataliwa ni zile ambazo hazizingatii na zinakiuka masharti yaliyowekwa na sheria au kanuni nyingine yoyote kwa ajili ya udhibiti wa utoaji wa taarifa husika.

Lakini Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alitaka kufahamu maana ya maneno yaliyoko kwenye sheria hiyo, ya bila kuathiri masharti mengine.

Waziri Marmo alisema masharti hayo ni yanayohusu mambo ya usalama wa Taifa na mengine aliyoyataja, lakini pia akaongeza kuwa masharti mengine ni yaliyoko katika sheria ya uhuru wa kupata habari.

Lakini hata hivyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliwataka wabunge wachangamkie kutumia kanuni ya 81 inayowataka kuwasilisha miswada binafsi na ya kamati hasa wanapoona kuna mambo ambayo yamepitwa na wakati katika sheria zilizopo.

Alisema ni wabunge peke yao ndio wanaweza kuleta mabadiliko katika nchi, kwa kuweka sheria nzuri na kuondoa zilizopitwa na wakati, kwani ndicho chombo pekee cha kutunga sheria.

Lakini alisema kamati zenyewe zimekuwa vyombo vya kupokea taarifa kutoka serikalini na miswada ili kuijadili, badala ya kuibua miswada yao na matokeo yake wamekuwa watu wa kulalamika kuhusu sheria hizo.

“Mkija hapa mnalalamika! Kwa nini wakati sisi ndio tunatunga sheria?” alihoji Spika Sitta.

Kuna madai kwamba, baadhi ya watumishi wa umma wanachomoa nyaraka nyeti za Serikali na kuwapa wanasiasa ambao wamekuwa wakizitumia katika majukwaa yao ya kisiasa.

Wednesday, April 14, 2010

Azimio la Arusha litalinda wote

MAGWIJI wa fani mbalimbali za jamii wamekuwa wakikutana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuzungumzia, pamoja na mambo mengine, uwezekano wa kurejesha Azimio la Arusha katika uendeshaji wa siasa na uchumi wa Tanzania.

Makamu Mkuu wa UDSM Profesa Rwekaza Mkandala; Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Julius Nyerere, Profesa Issa Shivji; Katibu Mkuu wa zamani wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU, sasa Umoja wa Afrika, AU, Salim Ahmed Salim na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Juma Mwapachu, kwa kutaja magwiji wachache, wote wamezungumzia Azimio la Arusha wakitaka lirejeshwe.

Na Azimio la Arusha wala si kitu kigumu kiasi hicho. Kwa ufupi, Mwalimu Nyerere na wenzake wenye uelewa wa aina moja, waligundua mapema kwamba katika dunia ya ubepari uliokomaa, raia wa kawaida wa nchi ambazo ndiyo kwanza zilikuwa zimejitawala kama Tanzania, asingeweza kufaidi matunda ya uhuru.

Wakaweka misingi ya kuhakikisha kila raia anapata haki na nafasi ya kuishi kama mtu katika nchi yake, hiyo ikiwa ni pamoja na kuainisha ni siasa ya mwelekeo gani Tanzania ifuate. Ujamaa na Kujitegemea yalikuwa ni matunda ya mawazo haya ya kina Mwalimu Nyerere na wenzake.

Kimsingi Azimio la Arusha liliweka miiko kadhaa, lakini hasa ya uongozi. Kwa tafsiri nyepesi, miiko hii ililenga kukabili choyo na ulafi katika mioyo ya waliokuwa na nafasi za maamuzi katika safu mpya za uongozi zilizokuwa zinajengwa, zilizotokana na makovu ya ukoloni uliohimiza matabaka ya kimapato katika jamii.

Wengi wetu, kama alivyopata kusema Mwalimu Nyerere mwenyewe, hatujawahi kuona hitilafu kubwa za Azimio la Arusha lililopatilizwa katika awamu ya pili ya utawala nchini, tena na watu walewale ambao mwanzoni waliliimba kama kasuku.

Lakini tumebahatika kuona hasara kubwa za huo mfumo unaonadiwa sana, mfumo mbadala wa Ujamaa na Kujitegemea ambao leo umesababisha kuibuka kwa pengo kubwa kati ya matajiri na masikini nchini. Mfumo ambao umezua chuki ambayo imeandikwa katika kila uso unaopishana nao, pale uso huo unapohisi ya kuwa wewe u ahueni kidogo, hata kama hiyo ni mara yenu ya kwanza kupishana barabarani.

Na chuki hii inachochewa na ukweli kwamba wengi wa walioshiriki kuua Azimio la Arusha ndio matajiri wa leo. Walizika Azimio la Arusha ili wale, wavune. Wangekuwa wamefanya biashara hahali ungeweza kusema wanastahili utajiri huo, lakini wapi. Wameneemeka kwa mikondo ileile ya umma, ambayo kimsingi ilipaswa kuwanufaisha Watanzania wote.

Hakika haiwezekani Azimio la Arusha la mwaka 1967, miaka sita tu baada ya uhuru, likawa ni lilelile miaka hii ya 2010. Litahitaji mabadiliko ili liende na wakati. Lakini yote kwa yote, yapo mambo ya msingi ambayo hayawezi kubadilika, na haya ni pamoja na maadili ya viongozi na maamuzi yanayotokana na viongozi wa umma wasiokuwa na maadili.

Hivi hatushangai kwamba katika Tanzania na Afrika yote matajiri wakubwa ni wanasiasa?! Na wengi wa hawa wanapoingia katika nyadhifa zao za siasa wanakuwa hawana kitu, hawana biashara wala hawamiliki makampuni. Wape miaka mitano tu katika siasa, basi watakuwa ndio wenye hodhi ya kila kitu na hasa : mali na akili. Wakati umefika tuanze kujadili kwa uwazi jinsi ya kurejesha Azimio la Arusha. Litatulinda wote, wasio nacho na wenye nacho.

Source:www.raiamwema.co.tz

Tuesday, April 13, 2010

Tuwe makini na ukarimu wa ghafla wa wanasiasa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) imebaini mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wanaowania kugombea uongozi katika jamii, kutoa rushwa kwa visingizio vya misaada na hivyo kushawishi wapiga kura.

Hali hiyo imejitokeza hata katika misiba, ambapo baadhi ya wawaniaji uongozi hao, hujitokeza na kushinikiza watambuliwe wao binafsi na michango waliyoitoa, ili kujionesha kuwa ni watu wema na wanaostahili kuchaguliwa na wananchi kuwaongoza.

Kinachosikitisha ni kwamba hata mambo ambayo yalikuwa ni sehemu ya utamaduni na yaliyoheshimika na kutohitaji majigambo na tambo, ndiyo sasa yamegeuzwa sehemu ya kampeni na hasa inapokuwa ni katika misiba.

Wakati huu wa kuelekea uchaguzi, tabia hiyo imejitokeza mpaka kuitia shaka Takukuru ambayo imeanza kuwachunguza watu wa aina hiyo, ambao bila shaka wanajaribu hata kukwepa Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete.

Si siri kuwa wanasiasa wamekuwa wakijipitisha majimboni wakiwamo wanaotaka kuwania kwa mara ya kwanza na wale wanaotaka kurudi bungeni, wakitoa misaada na pole kwa wafiwa na wanaouguza hata kama zamani hawakuwa wakiyafanya hayo.

Upole na ukarimu huu wa sasa, ndio unaotia shaka, wenye lengo la kuwapumbaza wananchi ili waone kuwa misaada misibani, utoaji zawadi za vyakula, vinywaji na nguo, ndivyo vigezo vya kupata kiongozi bora!

Sisi tunaungana na Takukuru kutaka watu wa aina hii wadhibitiwe na ikiwezekana waanikwe ili wananchi wawajue na wasithubutu kuwachagua, kwani ni wazi watu hao hawajiamini na wanajua hawana uwezo, hivyo wanatumia nguvu za ziada kurubuni wananchi.

Kwa upande wa wananchi ni vizuri wasibabaishwe na watu wa aina hii na badala yake waangalie uwezo wa mwombaji kura bila kuangalia ana mali au hana, lakini cha msingi ni kujiridhisha kuwa watakayemchagua ndiye kweli ana nia ya kuwasaidia.

Kumjua mwenye uwezo na asiye na uwezo havihitaji ramli wala dawa, bali atajulikana kwa mchango wake wa tangu zamani lakini pia maadili aliyonayo na si yule anayeomba leo akapewa na kesho akawatupa mkono.

Kiongozi safi ni yule anayeelewa matatizo ya anaowaongoza na aliye tayari kushirikiana nao kuyatatua kwa uwazi bila kuhitaji msukumo wa kivutio au kujifanya mkarimu na mpole; ni vizuri wakafahamika kuwa upole wao ni wa muda mfupi.

Watanzania wanapaswa kuwajua watu na hulka zao, wasije siku ya siku wakajikuta wanachagua chui waliojivika ngozi za kondoo na hatimaye wakajikuta wanalia kwa kufanya makosa katika uchaguzi, waelewe kuwa wanaojipitisha na misaada ya uongo na kweli, ni bora viongozi.

Monday, April 12, 2010

Sitta awaponda wanaosema yeye fisadi

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta amesema, maadui wake kisiasa wameshindwa kudhibitisha madai ya kuwa yeye ni fisadi.

Akizungumza kabla ya kuzindua programu ya Urejeshaji wa maadili kwa Umma (PIRI) unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sitta amesema, kama angekuwa na hata dola moja kwenye akaunti ya nje basi mpaka sasa adui zake wangeweza kuliweka peupe.

“ Maadui zangu wanapenda kunisema kuwa mimi ni mnafiki, na kama ningekuwa na dola moja nje ya nchi wangekuwa wameweka wazi, lakini sasa wameishia kusema natembelea benzi la gharama wakati si mimi ninayenunua, na hata waziri mkuu na Jaji Mkuu wanayo.

“ Pia wanasema kuwa ninaishi kwenye nyumba ya gharama, wameuza nyumba zote na nikipangishiwa wanasema inagharama kubwa.”

Sitta amesema, kama angekuwa fisadi basi angefanya hivyo tangu alipoteuliwa na Rais wa awamu ya Kwanza kuwa Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano mwaka 1974.

“ Nikiwa na miaka 34, niliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano na nikahusika katika kununua ndege za abiria tatu huko Canada baada ya Jumuia ya Afrika Mashariki kuvunjika, tulipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ( kwa wakati huo-Pierre Trudeau) aliniambia kunakamisheni ya dola za Marekani laki 3 na kupewa maelekezo hizo hela ziende wapi.

“ Kwa vile mimi nilikuwa na maadili, nilipiga simu nyumbani na Nyerere alinaimbia fedha hizo zichukuliwe na ndizo zilizosomeshea marubani wa kwanza wa ATC, lakini asilimia kubwa ya viongozi wa sasa wangepata nafasi hiyo fedha hizo zingekwenda mifukoni mwao.

Sitta aliongeza kuwa: “ Nilihusika kusaini mkataba ya ujenzi wa daraja la Salender mwaka 1981, barabara ya Moro-Dodoma mwaka 1983, ningeweza kupata fedha ambazo kwa sasa ningekuwa nawatemea mate, sio kama najivuna, mikataba yote hiyo sikuweza hata kujenga kibada. Mfano wa mikataba mibovu ni ule wa TRL.”

Amesema,kuna haja ya kuanza kufuata misingi iliyoweka na Nyerere inayozingatia usawa, kuwajali na kuwatumikia wanyonge, uadilifu na kuheshimu utu wa mtu bila kujali kabila, rangi, utajiri, jinsia au eneo wanaotoka ambayo imeifanya kuwa kisiwa cha amani na utulivu .

“ Hatuna budi kuidumisha misingi hiyo kwa nguvu zote kwa maslahi ya taifa na vizazi vijavyo. Nayasema haya kwa sababu zimeanza kujitokeza dalili na vitendo vya waziwazi vyenye mweleko wa kuibomoa misingi hii ambavyo ni rushwa, ufisadi, ubadhirifu, ubabe katika utawala na kuhubiri siasa za chuki. Vitendo hivi na vingine vimeanza kuzoeleka na kuwa sehemu ya utamaduni,”

Amesema,kwa muda mrefu taifa halikuwa na utaratibu rasmi wa kuandaa viongozi,wakati umefika kwa suala kupewa kupaumbele na uzito unaostahili kwa kuweka utaratibu wa kuandaa viongozi kwa kuwapatia nyezo na mafunzo katika nyanja za maadili, uzalendo na uadilifu.

“ Kizazi chenu kitafaidika na elimu ile, lakini wapo ambao kwa sasa ndio wanaoendesha mambo ya nchi ambao wataweza kutumia nafasi zao kutunga sheria za kukandamiza, na wale ambao wana miaka 40, ili watakapoaachia ninyi basi mambo yawe rahisi kwani kinyume cha hapo mtakapotaka kufanya mabadiliko basi mtaambiwa mnafanya mapinduzi.”

Pia Sitta ametaka programu hiyo ifike kwenye vyuo vya kati kama vyuo vya uwalimu, ufundi kutokana na kuwa navyo vinahusika kuzalisha wanafunzi wengi.

Sitta alisema ni vyema program hii ikafika katika ngazi za chini kama vijijini, kata na halmashauri ambao ndio waathirika wakuu wa mmomonyoko wa maadili.

Thursday, April 8, 2010

Tamasha la Nyerere kuanza Jumatatu

MTOTO wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Ghana Dk Kwame Nkurumah, Samia, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la pili la ‘Kigoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere’ litakaloanza Jumatatu ijayo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM).

Profesa wa ‘Kigoda cha Taaluma ya Mwalimu Nyerere' katika Chuo Kikuu hicho, Issa Shivji amewaeleza waandishi wa habari leo kuwa, tamasha hilo litakwisha Aprili 15.

Profesa Shivji amesema, wameandaa tamasha hilo kwa mara ya pili kwa kuwa walipata mafanikio katika tamasha la kwanza lililokuwa na kauli mbiu isemayo Binadamu Wote ni Sawa na Afrika ni sawasawa.

Tamasha hilo lilifanyika kuanzia Aprili 13, likaisha Aprili 17 mwaka jana.

Profesa Shivji amesema, kauli mbiu ya mwaka jana ilileta mtazamo ambao bado ni thabiti katika mapambano ya kukamilisha uhuru na ukombozi wa watanzania dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji wa mfumo wa kibeberu.

Amesema, mada kuu ya mwaka huu itakuwa ni Azimio la Arusha na kwamba, wamechagua mada hiyo ili kuenzi fikra na falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa ni kielelezo cha historia ya ukombozi nchini.

Kwa mujibu wa Shivji, tamasha hilo litawahusisha watafiti wa masuala mbalimbali ya kijamii watakaowasilisha utafiti wao na kuyawasilisha mapendekezo serikalini ili kuleta mfumo unaohitajika katika nchi nyingi.

“Katika miongo miwili iliyopita Azimio la Arusha limesahaulika na kugeuzwa kama ni tukio la kihistoria lisilokuwa na umuhimu katika zama hizi za utandawazi, sasa ni juu ya kizazi hiki kipya kama Azimio lingali hai au la?” amesema. Azimio la Arusha lilianzishwa mwaka 1967.

Tuesday, April 6, 2010

Mkulima ashauri posho za wabungwe zipunguzwe

SERIKALI imeshauriwa kuongeza fedha kwenye sekta ya kilimo kwa kupunguza matumizi mengine yakiwamo ya posho za wabunge na mafao yao.

Mkulima Zephania Lugembe, alitoa ushauri huo jana wakati akizungumza kwenye mkutano na timu ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, inayotathmini matumizi ya vocha za ruzuku za pembejeo za kilimo wilayani Bariadi.

Lugembe ambaye ni mkulima wa kijiji cha Nyakabindi, alisema “wakati tunapozungumzia Kilimo Kwanza, ni lazima Serikali ione umuhimu wa kuongeza fedha ili kumwinua mkulima.

“Mnazungumzia Kilimo Kwanza, lakini lazima mkumbuke kuwa fedha za kilimo hazitoshi, wakulima wawezeshwe zaidi tuachane na posho za wabunge, kila mara unasikia kuwa maslahi yao yako juu, na hivi karibuni watapewa furushi la pesa Bunge likivunjwa, lakini kwa wakulima fedha ni kidogo,” alisema Lugembe.

Alisema wabunge wanafikiria maslahi ya juu, lakini ni bora Serikali ikaona umuhimu wa kupunguza fedha kwa watunga sheria hao, ili zipelekwe kwa wakulima kuinua kilimo nchini.

Mkulima huyo alitoa ushauri huo baada ya wataalamu wa wizara hiyo kufafanua kwamba bajeti iliyotengwa kwa utaratibu wa vocha nchini isingeweza kutosheleza wakulima wote kupata pembejeo za kilimo.

Lugembe na wananchi wengine waliohudhuria mkutano huo, walilalamika kwamba vocha zilizotolewa kwa msimu huu ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji kwa kijiji cha Nyakabindi ambako wanufaika ni 1,800.

Mbali ya kulalamikia bajeti ndogo katika sekta ya kilimo, wananchi hao pia waligusia ucheleweshaji wa vocha na kutaka kamati za vocha za vijiji zilipwe posho.

Akijibu hoja hizo, Ofisa Kilimo wa Wizara hiyo, Samson Poneja, alisema ni kweli wanufaika wa mfumo wa vocha nchini ni wachache na kwamba hiyo ni moja ya changamoto zinazokabili mfumo huo.

Alisema ni nia ya Serikali kuwapa vocha hizo wakulima wote, lakini kwa sasa bajeti haitoshelezi mahitaji hayo na itaongezwa kadri fedha zinavyopatikana.

Wilaya ya Bariadi ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Shinyanga zinazopata ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha kwa zao la pamba ambapo wakulima huchangiwa asilimia 50 ya bei ya soko ya mbegu za pamba na dawa za kuulia wadudu.

Thursday, April 1, 2010

Watanzania kutotibiwa moyo nje kuanzia Juni 2011

KUANZIA Juni mwakani, Serikali haitagharimia watu safari na matibabu ya nje, hasa kwa wagonjwa wa moyo ikiwamo kufanyiwa upasuaji.

Hatua hiyo imefikiwa kutokana na ujenzi wa Kituo cha Upasuaji Moyo, Tiba na Mafunzo kinachojengwa na Serikali ya China katika eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambao unatarajiwa kuchukua miezi 14 kukamilika.

Akiweka jiwe la msingi kuashiria kuanza kujengwa kwa kituo hicho jana Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alisema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kupeleka wagonjwa wa moyo nje kutibiwa, hali ambayo hata hivyo haikutosheleza mahitaji kutokana na uhaba wa fedha uliopo.

“Tangu uhuru tumetumia fedha nyingi kupeleka ndugu zetu nje, lakini kutokana na uwezo mdogo si wote waliobahatika kwenda kutibiwa, mfano mwaka 2001 kulikuwa na wagonjwa 200 wa moyo na kati yao 156 walihitaji upasuaji lakini ni 60 tu ndio waliopelekwa nje kutibiwa,” alisema Rais.

“Sina uhakika hao wengine zaidi ya 100 waliobaki kama wako hai au wametangulia mbele za haki, kwa kweli inasikitisha na inauma sana. Kutokana na hali hii, ndiyo maana tuliamua ni bora tuanze wenyewe safari ya kujijengea uwezo wetu katika tiba ya maradhi hayo,” alisema
Rais Kikwete.

Alisema anaamini baada ya kukamilika kwa kituo hicho ambacho kitakuwa na wodi 11 na vitanda 36 na Chumba na Watu Mashuhuri (VIP), utaratibu wa kupeleka wagonjwa nje kutibiwa moyo utakwisha isipokuwa kwa wanaotaka kwa hiari yao kutembea nchi za nje.

Alisema pamoja na hayo, watakaomua kwenda nje hawatakuwa na tofauti na watakaotibiwa nchini, kwa kuwa vifaa, madaktari na huduma hazitatofautiana.

“Ila naupongeza uongozi wa MNH kwa kuanza mpango wa kupeleka madaktari nje kwa ajili ya mafunzo ya magonjwa moyo,” alisema.

Alisema tayari madaktari 26 wamerudi nchini na wameanza kutoa huduma hiyo na hadi sasa wagonjwa wa moyo 160 wamefanyiwa upasuaji ambao umekwenda vizuri bila matatizo, jambo ambalo ni la kujivunia.

Kikwete alisema nchi nyingi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, zimekuwa zikikabiliwa na matatizo makubwa katika matibabu ya magonjwa sugu kama vile kisukari, figo, saratani, moyo na mishipa ya fahamu, jambo ambalo Tanzania inajipanga kukabiliana nalo na kuondokana na adha hiyo.

“Kwa sasa tumeanza kuhangaika kuwa na kituo cha upasuaji wa mishipa ya fahamu ambacho kitakuwa kikubwa na cha kisasa katika nchi za Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara,” alisema.

Aliishukuru Serikali ya China kwa ushirikiano wake ambao umesababisha kujengwa kwa kituo hicho cha magonjwa ya moyo.

“Hii ni faida ya ziara yangu ya mwaka 2006 Uchina ambapo nilikutana na Rais wa nchi hiyo, Hu Jintao, na hata alipotutembelea aliahidi kutimiza ahadi yake hiyo,” alisema Rais.

Naye kiongozi wa ujumbe China, Sun Liang, alisema ujenzi wa kituo hicho ni katika kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na China. “Naamini baada ya jengo hili kukamilika, litatoa huduma bora za upasuaji kwa Watanzania wenye matatizo ya moyo,” alisema Sun.

Alitoa papohapo msaada wa dola za Marekani 20,000 kwa ajili ya kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo nchini ili wapelekwe nje kutibiwa, wakati ujenzi wa kituo hicho ukiendelea.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, alisema kwa muda mrefu Serikali imejitahidi kupambana na tatizo la kupeleka wagonjwa wa moyo nje ambalo limekuwa likiielemea kutokana na uwezo wake kuwa mdogo.

Alisema kutokana na hali hiyo, walipeleka madaktari 26 nje kwa kujifunza namna ya kutibu moyo na tayari wamerudi na kuanza upasuaji huku Serikali ikijiandaa kupeleka madaktari wengine katika awamu ya pili.

Balozi wa China nchini, Li Xinsheng, alisema kituo hicho ni alama ya ushirikiano wa miaka 46 wa Tanzania na China ambapo pamoja na jengo hilo, nchi hiyo pia imejipanga kutoa misaada mingine katika sekta za elimu, afya na kilimo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MNH, Adolar Mapunda, alisema pamoja na kwamba Serikali kwa sasa imetoa kipaumbele katika kilimo na kuanzisha mpango wa Kilimo Kwanza, anaomba pia masuala ya elimu na afya, yaingizwe katika vipaumbele muhimu vya nchi.