Thursday, October 30, 2008

Mfululizo wa Semina za GDSS.

Mada ya Jumatano hii ya tarehe 29/10/2008 ilikuwa ni mrejesho wa Mwenge wa Kampeni ya Lengo la Tatu la Milenia: Kupunguza Vifo Vya Watoto wachanga na akina Mama Wajawazito. Mapema mwaka huu FemAct walikabidhiwa mwenge kama ishara ya kupewa jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa Lengo la Tatu la Millenia.

Wawasilishaji wakuu walikuwa ni dada Jesca Mkuchu(Pichani) Mwenyekiti wa FemAct na Ussu Mallya- Mkurugenzi wa TGNP. Lengo la Mrejesho huu ni; kukabidhi mwenge kwa wanaharakati na kupata fursa ya kutandaa na kupashana habari zaidi juu ya utekelezaji wa lengo la namba tatu la malengo ya millenia.

Katika kufanya uchambuzi yakinifu wanaharakati walinabaini kuwa lengo hilo la millenia linakabiliwa na changamato kadhaa wa kadha baadhi ni kama zifuatazo: Lengo hilo lina ufinyu wa dira, kwa sababu halilengi kumkomboa mwanamke katika kila nyanja, pili Malengo haya hajatilia mkazo maazimio ya Beijing ya mwaka 1995, kwa sababu katika maazimio Kumi na mbili ya Beijing ni azimio moja tu ndio lililochukuliwa.

Wanaharakati waliangalia uwezekano wa serikali yetu kutimiza malengo hayo kabla ifikapo mwaka 2015 kama ilivyoahidiwa, na kujaribu kuangali ni kwa kiasi gani malengo hayo yamekamilishwa.

Dada Halima Mselem kutoka TAMWA aliangalia uwezo wa serikali katika kudhibiti unyanyasaji wa kijinsia na upatikanaji wa haki sawa katika elimu kati ya watoto wa kike na wakiume. Na alishauri pawepo na mpango maalumu wa serikali wa kutenga fedha kwa ajili ya kukomesha unyanyasaji wa kijinsia.

Dada Jonoveva Katto kutoka TAWALA, yeye aliangalia utekelezaji wa lengo la tatu hasa katika upande wa sheria, ambapo alitanabaisha vipengele kadhaa vya sheria ambavyo bado vinaendeleza ukandamizaji kwa wanawake. Sheria hizo ni zile za Mirathi, kwa mfano, sheria ya mirathi ya kimila ya mwaka 1963 hamruhusu mwanamke kurithi na kumiliki mali. Na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, kifungu cha 60, kinaeleza wazi kwamba mali zinazopatikana katika ndoa zinapaswa kuandikishwa kwa jina la mwanaume, sheria hii mara nyingi huleta msuguano hasa pale mwanaume anapoamua kuoa mke mwengine na kumfukuza mwanamke bila kumpa kitu chochote walichochuma wote.

Dada Festa Andrew kutoka UTU Mwanamke yeye aliongelea juu ya hali ya afya ya Uzazi ambapo alitabanaisha kwamba hali bado si nzuri nchini Tanzania ambapo kwa wastani kila baada ya lisaa limoja mwanamke mmoja mazazi anafariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi salama. Hivyo bado kuna haja ya wanaharakati kuendelea kuisisitiza serikali kuongeza fedha zaidi katika swala hili la afya ya uzazi, tofauti na ahadi za sasa za wanasiasa ambazo zinaendeleza kuleta madhara kwa wazazi.

Changamato kwa wanaharakati ni pamoja na kuishinikiza serikali ili iweze kuongeza nguvu na kutekeleza makubaliano ya lengo la tatu la milenia kama lilivyoafikiwa na wakuu wa maataifa 189. Kwa sasa bado serikali inasusua katika utekelezaji wa lengo hilo kutokana na kutoa kipaumbele kidogo katika sekta hiyo.

Je Wanaharakati wanaweza kufanya nini ili kuhakikisha kwamba lengo hili la tatu linafanikiwa kwa wakati husika? Je, takwimu zinazotolewa na maofisa wa serikali zina ukweli ndani yake? Nini kifanyike ili kuboresha kampeni hii ya utekelezaji wa lengo la tatu la millenia?

Monday, October 27, 2008

MWENGE WA KAMPENI YA LENGO LA TATU LA MILENIA, KUPUNGUZA VIFO VYA AKINAMAMA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS)

UNAKARIBISHWA KATIKA MFULULIZO WA SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS) KILA JUMATANO AMBAPO WIKI HII JESCA MKUCHU MWENYEKITI WA FemAct NA USU MALYA MKURUGENZI WA TGNP WATAWASILSHA MREJESHO KUHUSU:

MWENGE WA KAMPENI YA LENGO LA TATU LA MILENIA: Kupunguza vifo vya Watoto Wachanga na Kina Mama Wajawazito

LINI: Jumatano Tarehe 29 Oktoba 20

Muda: Saa 9:00 – 11:00 Jioni


MAHALI: Viwanja vya TGNP, Barabara ya Mabibo Karibu na Chuo

Taifa Cha Usafirishaji Mabibo Sokoni


Tafadhali dhibitisha ushiriki wako kupitia
info@tgnp.org



KARIBUNI SANA !!!!!!

Friday, October 24, 2008

Mrejesho wa Semina za kila Jumatano (GDSS): Ushawishi na Utetezi

Idadi ya washiriki ilikuwa 128 kati yao wanawake walikuwa 72 na wanaume 56 kutoka sehemu tofauti kama vile Asasi za kiraia, vikundi vya kujitolea kupambana na maambukizi ya Ukimwi na VVU, wanafunzi kutoka taasisi za elimu ya juu, waandishi wa habari, FemAct, taasisi za walemavu, makundi maalumu na jamii kwa ujumla.

Kwa kuongozwa na mtoa mada (Anna Sangai), washiriki walijadili maana, mikakati / nyenzo, aina, madhumuni na taratibu katika ushawishi na utetezi ili kushawishi watunga sera na watekelezaji kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii iliyokandamizwa kwa kubadilisha sheria na kanuni.

Mada kuu mbili (mikakati na nyezo) zilijadiliwa kwa kina na kuwekwa bayana kutokana na umuhimu wake katika ushawishi na utetezi

Kuhusu mikakati, mtoa mada alikubaliana wazi kuwa lazima kuwepo dira ili kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii. Ili kukabiliana na changamoto kutoka kwa watunga sera na watekelezaji, yafuatayo lazima yazingatiwe: - Ufahamu / Elimu ya sheria, sera na mipango lazima vizingatiwe ili kufikia na kutekeleza mchakato mzima wa ushawishi na utetezi.

Kuhusu nyenzo, mtoa mada aliainisha njia tofauti kama vile mawasilianao ya nje na ndani kwa wadau wenyewe, elimu kwa makundi yanayostahili, jamii kuwa na ufahamu wa elimu, sanaa na michezo bila kusahau vyombo vya habari.

Mtoa mada aliendelea kuhafiki kwamba njia zote zilizotajwa na nyingine nyingi zinaweza kutumika kusaidia kupinga aina yoyote ya ukandamizaji.

Washiriki walipewa nafasi ya kujadili katika makundi, zikachaguliwa mada tano (5) ili kutathmini kiwango cha uelewa wa suala la ushawishi na utetezi. Mada zilizochaguliwa ni:- Ukimwi na VVU, Afya ya uzazi, Maji, Elimu na Unyanyasaji wa kijinsia.

Mwezeshaji na makundi yote kwa pamoja yalihitimisha kwa kupendekeza kuchagua ujumbe mbalimbali na kuwasilisha kwa mwezeshaji kwa kuupitia na kisha kupeleka kwenye vyombo vya habari kama njia mojawapo ya ushawishi na utetezi ili kuleta mabadiliko ya kweli.

Thursday, October 23, 2008

Mwalimu Nyerere: Mwanaharakati mchochezi wa maasi matakatifu

Wiki jana Oktoba 14, Watanzania waliadhimisha miaka tisa ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyefariki katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, Mjini London, Uingereza kwa ugonjwa wa kansa ya damu.

Ni kwa yapi Mwalimu anapaswa kukumbukwa? Ni kwa yapi anastahili kuigwa na jamii ya Kitanzania na Jumuiya ya kimataifa kwa ujumla?

Ukiachilia mbali ushupavu wake na heshima aliyojipatia kwa kupigania na kuleta Uhuru, Mwalimu ni mtu wa ngano na simulizi nyingi, kuanzia staili ya maisha yake, tabia na fikra zake.

Hakuna mazingira wala hali yoyote ya kuonyesha kwamba Mwalimu alijilimibikizia utajiri kihalali au vinginevyo wakati na baada ya utumishi wake, aliporejea na kuishi kijijini kama raia wa kawaida, mwaka 1985.


JK Nyerere
Mwalimu J.K. Nyerere

Nyumba yake ndogo imejengwa sehemu ile ile ilipokuwa nyumba ya baba yake, Chifu Nyerere Burito, imetuama juu ya miamba ya kilima cha asili cha Mwitongo, kijijini Butiama. Ni ndogo mno kutostahili hadhi ya mtu aliyekuwa kiongozi wa kimataifa.

Baada ya kuona kwamba kijumba hicho kidogo hakikustahili hadhi ya rais mstaafu kama Mwalimu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWT) lilijitoleaa kuipanua, kama alivyopata kusema yeye mwenyewe: “Vijana waliona vyema Amiri Jeshi wao Mkuu anastahili nyumba ya wageni, lakini ni masikini, hana fedha”, akimwambia mwandishi wa makala haya, alipomtembelea nyumbani kwake Butiama, Februari 1999, miezi kadhaa kabla ya kwenda London kwa matibabu.

Kuna kipindi kufuatia kupinduliwa kwa Rais Kwame Nkurmah wa Ghana, mwaka 1966, Dar es Salaam ilionekana kuchukua nafasi ya Accra kama “Makkah” ya Afrika kwa wanaharakati Weusi; na kwa kufuta mwangwi wa hotuba za nguvu na za kiimahiri za Nkurumah, Tanzania, chini ya Rais Nyerere, ilishika hatamu za fikra za kimapinduzi kwa ladha ya ukurasa wa Afrika ya kale.

Mwalimu hakupenda makuu, kujikuza au urasimu mwingi, alichukia utajiri: “Kimsingi mimi ni mkulima (mdogo) na Mjamaa. Hakuna mtu anayeweza kutajirika kwa kazi yake. Milionea hawi milionea kwa jasho lake; lazima atakuwa amewanyonga wengine; mpe mtu huyo kisiwa chake uone kama atatajirika”, alipata kusema.

Kuhusu wanasiasa wanaojikweza majukwani na kutoa misaada ya mamilionoi ya pesa kwa wengine, Mwalimu, katika kitabu “Binadamu na Maendeleo” , akimnukuu Mtakatifu Ambrose, anasema, “ Humpi masikini sadaka ya mali yako, unampa kilicho chake, maana wewe umenyakua na kukifanya chako peke yako. Kile kilichopo kitumiwe na watu wote”.

Anaendelea: “Hakuna yeyote mwenye haki ya kutumia mali (rasilimali za taifa) hiyo anavyotaka. Hakuna yeyote mwenye haki ya kulimbikiza mali, au kitu asichokihitaji akitumie peke yake, wakati wengine hawapati hata mahitaji ya lazima….”

Mwalimu aliwahi kutamka wazi kuwa hakuhitaji utajiri, alisema:
“Nihitaji utajiri kwa ajili gani? Nilikuja duniani uchi na nitarudi uchi; sioni sababu kwa nini nijihangaishe na mambo ya utajiri; natimikia watu wangu, utajiri kwangu wa nini?”

Mwalimu alikufa fukara, lakini kwa utumishi uliotukuka. Katika enzi hizi za ufisadi, mafisadi wangapi wanao ujasiri wa kuwaza au kusikiliza ujumbe wa Mwalimu? Na wameadhimishaje siku hiyo?.

Mwalimu alianza kufikiria juu ya “Ujamaa” alipokuwa Chuo Kikuu Nchini Uingereza, lakini hakuwa muumini wa sera za Ki-Karl Marx kwa sababu, anasema, Karl Marx alitawaliwa na nadharia za kibaguzi za ki – Darwin, zilizomwona Mwafrika kama binadamu wa daraja la pili.

Hakutaka kuigiza Ujamaa wa Ki – Ulaya kwa sababu ulijikita zaidi katika dhana ya migongano ya kitabaka, wakati huo Afrika haikuwa na matabaka, anasema, “Ujamaa wa ki – Ulaya (Socialism) ni matokeo ya upepari uliokomaa… (lakini) lengo letu lilikuwa ni kuleta maendeleo wakati huo huo tukibakiza moyo wa jumuiya asilia”.

Baadhi ya watu walihoji ni vipi Mwalimu aliweza kuchanganya harakati za kisiasa, dhana za Karl Marx, ibada na hata dhana ya kuwapo Mungu bila kuathiri kimojawapo.

Kwa hili Mwalimu alipata kusema: “Kama ningeziogopa harakati kwa kisingizio cha kulinda imani yangu ya dini, nisingeweza kuongoza mapambano ya Uhuru wa nchi hii; ingekuwa ni sawa na kudhalilisha Ukristo wangu na Kristo, ambaye yeye mwenyewe alikuwa mwanaharakati na mwanamapinduzi”

Msimamo huu wa Mwalimu umewekwa wazi katika kitabu chake “Binadamu na Maendeleo”, kwamba: “Kanisa likubali kuwa maendeleo ya watu maana yake ni maasi… watu hufikia hatua ya kuyakataa mambo yanayowabana katika Uhuru wao kama binadamu”

Mwaliimu aliasa, “Ikiwa hatutashiriki kwa vitendo katika mapambano ya kuondoa utaratibu wa maisha na wa uchumi unaowadidimiza watu kwenye umasikini, uonevu na unyonge, basi Kanisa litakuwa halina uhusiano na maisha ya binadamu, na dini itakuwa kama ni mkusanyiko wa imani za ushirikina zinazokubaliwa na wenye hofu tu”.

Mwalimu aliamini kuwa maendeleo lazima yamaanishe maasi matakatifu, kwa sababu ya kuleta mabadiliko, alisema: “Tunasema kwamba, binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu. Mimi nakataa kumfikiria Mungu aliyefukara, mjinga, mshirikina, mwoga, dhalili, ambayo ndiyo hali ya walio wengi kati ya wale aliowaumba kwa mfano wake mwenyewe”.

Mwalimu aliamini pia kwamba yote hayo yanasababishwa na binadamu kwa binadamu mwenzake, alisema: “ Lakini tulivyo hivi sasa tu viumbe, tena si viumbe wa Mungu, bali wa binadamu wenzetu… Kanisa lazima lishambulie wazi wazi mtu au kikundi chochote kinachosaida kudumisha unyonge huo wa mwili na roho, bila ya kujali misukosuko inayoweza kutokea kwa kanisa au kwa wafuasi wake.”

Mwalimu alichukia tabia ya kuiga kila kitu bila kuhoji sera, mifumo ya maendeleo na demokrasia ya kigeni kwa kutozingatia mazingira na hali halisi ya nchi yetu: “Angalia wanavyoishi kule Marekani; ni fujo na uhuni mtupu. Kama wanakuvutia kwa gharama ya watu wetu, fungasha mizigo uende ukaishi huko kama wao. Hapa lazima jicho lako liwe kijijini kwa wanavijiji; usiangalie hizo gari mbili na majokofu na vitu vyote katika nchi za kibepari, bado wanaendelea kutunyonya. Sisi tunataka kujenga jamii yenye usawa, jamii iliyostaarabika, tukipewa muda”, alisema.

Juu ya demokrasia na Maendeleo, Mwalimu aliona kuna mambo mawili muhimu: la kwanza, ni uongozi wa kueleza, na la pili, ni demokrasia katika kuamua mambo: “Maana uongozi si kukemea watu; maana yake si kuwatukana watu au kikundi cha watu usiokubaliana nao; wala maana yake si kuamuru watu kutenda lile wala hili. Uongozi maana yake ni kuzungumza na kushauriana na watu ukawaeleza na kuwashawishi. Maana yake ni kuwa mmoja wao na kutambua kwamba wao ni sawa na wewe”

Mwalimu aliamini kwamba uongozi hauwezi kuchukuwa nafasi ya demokrasia; uongozi lazima uwe sehemu ya demokrasia. Alihuzunika baada ya kustaafu kubaini kwamba rushwa serikalini ilianza kuchukua umbo la kulitaifisha Taifa.

Ni wakati huo pia alipong’amua kwamba chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM), kilikuwa kimekoma kuwa chama cha wanachama na kuwa chama cha viongozi. Na kwa sababu hiyo alianzisha mjadala juu ya mfumo wa vyama vingi nchini.

Mwalimu alinukuliwa akisema: “ Kiitikadi, mimi ni mtu wa Chama kimoja. Lakini nimeanzisha mjadala huu kwa sababu ile dhana kwamba ni mwiko kuhoji Katiba yetu si ya kidemokrasia…. Siwezi kukubali; nasema, kama hawa jamaa (watu) wanataka mfumo wa vyama vingi, waache waanzishe….”

Mwalimu alikwisha kututoka. Ni kweli alikuja mtupu duniani na amerudi mtupu, lakini fikra zake zinaishi. Hata hivyo, tumejionea jinsi fikra hizo zinavyopigwa vita na vikosi vya nyang’au wa uchumi na siasa ili washike hatamu za nyanja hizo kwa maangamizi ya uchumi, Taifa na watu wake.

Ilivyo sasa uzalendo unatoweka haraka, maadili yanayoyoma. Uongozi umenyakuliwa na wasomi wachache wanaojifanya kuyaelewa matatizo yetu, wakati ni kinyume chake. Wameunda mtandao na mabwana wa ubepari wa kimataifa; viongozi wamepungukiwa hisia za kitaifa zinazozaa uzalendo, ushujaa, kujitoa mhanga kwa nchi. Wamekuwa kama watu wanaojiaandaa kustaafu na kuishi ughaibuni.

Kwa tabaka hili dogo, lakini lenye nguvu, demokrasia sasa maana yake ni kukamata mawazo ya watu wasio na elimu ya demokrasia kwa kuwanunua kwa nguvu ya pesa na kunyakua madaraka ya kisiasa.

Viongozi wamebweteka na kubugia sera zinazowakamua masikini kuwatajirisha mabepari wachache. Badala ya kuwa watumishi wa watu wamegeuka kuwa mabwana zao. Wasomaji watajiuliza: Kwa nini Watanzania, kila wanapokerwa na jambo, wanaimba, “ Kama si juhudi zako Nyerere… x 3; … na uhuru, elimu, amani… tungepata wapi?”.

Ni kwa sababu Nyerere, kama mwanaharakati na mwana mapinduzi, alichochea moto wa maasi yasiyozimika, hadi ushindi upatikane kwa “Wasakatonge”.

Kupanda Mlima Kilimanjaro kutetea Haki za Binadamu

Wanaharakati,

Naomba fursa kwenye blogu ya jamii kuwatangazia Wanaharakati na watu wengine wote kuwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu [LHRC], kinaandaa maadhimisho ya miaka 60 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu ambapo kilele chake kitakuwa Tarhe 10 Disemba 2008.

Katika kuelekea huko, Kituo kitakuwa na mambo kadhaa, ikiwemo kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia (kama wanachama wa WiLDAF) kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Disemba, kuwa na jumuiko la wasaidizi wa kisheria (paralegal symposium), mkutano wa wasaidizi wa kisheria vijijini (village legal workers' meeting), wiki ya msaada wa kisheria (legal aid services) na mkutano w maadhimisho ya siku ya haki za Binadamu yenyewe tarehe 10 Disemba. Haya yatafanyika mjini Dodoma.

Pamoja na hayo, Kituo kinafanya mipango ya kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia Tarehe 22 Novemba, pamoja na mambo mengine kupinga ukatili wa kijinsia na kupandisha Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights) pale Uhuru Peak ili unaofahamu na usiofahamu tamko hili ili kuweza kuangaza na kutetea haki za binadamu kutoka kwenye kilele kirefu kuliko vyote Afika.
Watu wote wanakaribishwa.

Tuesday, October 21, 2008

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS)

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO (GDSS)

Unakaribishwa wiki hii katika mfululizo wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) ambapo Anna Sangai (TGNP) atatoa mrejesho kuhusu;

Maunzo ya Mbinu za Ushawishi ili Kupunguza Vifo vya Kinamama na Watoto Wachanga


Tarehe: 22/10/2008

Saa: 9:00 alasiri - 11:00 Jioni

Mahali: TGNP


Tafadhali dhibitisha ushiriki wako kupitia
info@tgnp.org


KARIBUNI SANA !!!!!!

Friday, October 17, 2008

MAANDAMANO YA AMANI KULAANI MAUAJI YA ALBINO NCHINI

MAANDAMANO!!!MAANDAMANO!


CHAMA CHA MAALBINO TANZANIA KWA KUSHIRIKIANA NA WANAHARAKATI NA WADAU MBALIMBALI WA HAKI ZA BINADAMU WANAKUALIKA KUSHIRIKI KWENYE MAANDAMANO YA AMANI;KULAANI MAUAJI YA ALBINO NCHINI


LINI: JUMAPILI TAREHE 19 OKTOBA 2008

Muda: Kuanzia Saa 2:00 Asubuhi HADI

SAA 6:00 Mchana

MGENI RASMI NI RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MH. JAKAYA MRISHO KIKWETE

MAHALI: KUANZIA SHULE YA MSINGI UHURU HADI VIWANJA VYA KARIMJEE



TUJITOKEZE KWA WINGI..!!!!!!



TAFADHALI ALIKA WATU WENGI SANA KUPITIA UJUMBE HUU!!!!!

Thursday, October 16, 2008

Mrejesho wa Semina ya GDSS ya Jumatano ya tarehe 15/10/2008

Mada ilikuwa ni Uibuaji wa Maswala Makuu Yahusuyo Ukatili wa Jinsia Katika Jamii.
Semina hii ilihudhuriwa na wanaharakati kutoka katika vikundi mbalimbali ndani ya jiji la Dar es Salaam na waliweza kuibua maswala ambayo yanasababisha ukatili wa kijinsia ama aina nyingine ya ukatili dhidi ya utu na watu wanyonge. Baadhi ya Vikundi hivyo ni pamoja na; Chama cha Viziwi (CHAVITA), Albino Revolution Cultural Troupe, Mbagala Group, Tegeta Group, Kagera Youth, Mwananyamala group, Kisarawe IGN, Kinondoni IGN, Youth and Women Program (KWYP- Kigogo), Segerea Group, Kamene Sec. School, Makuburi Women Deveolpment Association (MWDA), Tabata Youth, na Magomeni Group. Washiriki wa semina waliweza kuibua maswala mbalimbali katika maeneo yao ambayo yanasababisha ukatili wa kijinsia katika jamii, baadhi ya maswala hayo ni;

Maswala yanayosababisha Ukatili wa Kijinsia katika jamii ni pamoja na; Wanawake kunyimwa haki ya kumiliki mali ndani ya jamii na familia ama baada ya kufiwa; ukosefu wa haki katika mirathi kwa kigezo cha jinsia; rushwa ya ngono katika ajira ama kupandishwa vyeo makazini; ubakaji katika ndoa; unyanyasaji wa wasichana wanaofanya kazi za ndani; wanawake kutekelezwa na wanaume baada ya kupata ujauzito au watoto wao waliojifungua; na Wazazi kuwaachisha shule watoto wa kike kwa ajili ya ajira au kuolewa.

Katika elimu maswala yafuatayo yaliibuliwa; adhabu kali kwa wanafunzi ambazo hazilingani na makosa; wanafunzi kurudishwa nyumbani kwa makosa madogo-madogo; Tuition inawanyanyapaa watoto maskini wasio na uwezo wa kulipia; Usafiri kwa wanafunzi ni kero kubwa inayowasababisha wanafunzi kutumbukia katika matatizo makubwa –mf. Mimba; Watuhumiwa wanaowapa mimba wanafunzi mara nyingi hawachukuliwi hatua stahiki na serikali hii inachangia wanafunzi kuendele kupewa mimba kiholela; na Ubaguzi ndani ya familia dhidi ya mtoto wa kike katika kupata elimu na haki zingine.

Matatizo na kero za Walemavu; Unyanyasaji ndani ya jamii; Unyanyasaji ndani ya ndoa,hasahasa walemavu wanapoolewa na watu ambao hawana ulemavu; unyanyasaji ndani ya familia hasa kuachishwa shule na unyanyasaji mwengine; kutengwa katika maneo ya biashara; unyanyasaji katika elimu- ukosefu wa dhana za elimu; ukosefu wa wakalimani, hata katika taarifa Muhimu za kitaifa -mf. hotuba ya rais; Mauaji ya Albino, serikali imeshindwa kuwalinda albino; na Walimu kuwadharau Albino kwa uwezo wao wa kuona ni mdogo.

Kero za jumla zilizopo katika jamii ni pamoja na; ukosefu wa maji safi na salama; shida ya usafiri; serikali za mitaa kushindwa kukaa vikao vya maendeleo; Rushwa katika ofisi za serikali; kushamiri kwa biashara ya madawa ya kulevya; ukosefu wa huduma za afya; upungufu wa vituo vya usalama; unyanyasaji wa mama ntilie; na kushamiri kwa mabanda yanayoonyesha video za uchi wakati wa mchana kwa watoto walio na umri mdogo.


Wanaharakati waliazimia mambo yafuatayo ya kutekeleza kutokana na kero walizozioanisha; Jamii ielimishwe ili iweze kutoa taarifa endapo vitendo vya unyanyasaji vinatokea katika maeneo yao; Walemavu kujiunga katika mitandao mbalimbali ya wanaharakati ili kuweza kupata na kutoa taarifa mbalimbali na Jamii ielimishwe ili iweze kuwa na mtazamo sawa juu ya watu wenye ulemavu; Wanaharakati wakusanye nguvu za pamoja katika kuleta Mabadaliko katika jamii zao; na vikundi vikusanye nguvu zaidi katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

Thursday, October 9, 2008

Mrejesho wa Semina za GDSS

Mada: Changamoto Zilizopo Katika Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata na Ushiriki wa Wananchi Nchini..


Mada hii iliwakilishwa na Frank Samweli(Pichani) Mwanasheria wa Kujitegemea, jumatano ya tarehe 8/10/2008. Lengo la mada hii ni kuainisha changamoto zilizopo katika mchakato mzima wa uendeshaji wa mabaraza ya kata kwa kuangalia uundaji wake, muundo, utendaji wake wa kazi, ushiriki wa wananchi na Mapungufu yanayojitokeza katika uendeshaji wa mabaraza haya.

Mabaraza haya yalianzishwa kipindi cha ukoloni na baada ya uhuru yakaendelea kuwepo kwa lengo la kuamua kesi ndogo ndogo, kurahisisha mchakato wa kupata haki kwa wananchi, na kupunguza msongamano katika mahakama za wilaya. Mabaraza yanaundwa na sheria ya mabaraza ya kata namba 7 ya mwaka 1985, iliyorekebishwa katika sheria mpya sura ya 206 ya mwaka 2002.

Tangu yaliyoanzishwa tena, Mabaraza ya Usuluhishi ya Kata yamekuwa na mafanikio yafuatayo: kuleta hali ya utulivu na amani, kuleta upatanishi kati ya pande mbili zinazodaiana, kurahisisha upatikanji wa haki kwa wananchi, na kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama za wilaya.

Matatizo ambayo yamejitokeza katika uendeshaji wa mabaraza haya ya kata ni pamoja na yafuatayo;
Hakuna mishahara rasmi kwa wajumbe wa baraza. Wajumbe wa baraza wanapata posho kutokana na vikao wanavyokaa na kesi wanazosuluhusha. Kukosekanana kwa posho kwa wajumbe kumesababisha mabaraza haya kupungua ubora wake katika utendaji wake wa kazi kwa kulazimisha kutoza faini ili wajumbe wapate posho.(Dada Talaka Nyanja akichangia hoja, yeye pia ni Mjumbe wa baraza la Usuluhishi la kata ya Mabibo)

• Wajumbe walio wengi hawana ujuzi na mambo ya sheria, hii inasababisha kesi nyingi kuamuliwa kwa utashi wa wajumbe waliopo katika baraza hilo na hivyo kuwanyima haki wale ambao waliopeleka mashitaka katika baraza.
• Mabaraza haya hayapo kila siku. Mabaraza ya kata yanakaa kwa wiki mara moja ama mara mbili kutokana na wajumbe kuwa na shughuli zingine za kuwaingizia kipato cha kujikimu kimaisha, hii imesababisha kesi nyingi kuamuliwa katika siku moja na hukumu kutolewa bila kusikiliza maelezo zaidi kutoka kwa walalamikiwa.

• Uteuzi wa Wajumbe wa Mabaraza haya mara nyingi huzingatia utashi wa
Kisiasa Kwa sababu wajumbe wanateuliwa na kamati ya Maendekleo ya kata ambayo inaongozwa na diwani kitu ambacho kinapelekea wajumbe hawa kuwa na utashi wa kisiasa. Pia wajumbe wa mabaraza haya huchaguliwa kwa kificho sana kitu ambacho kinaleta manung`unuko kwa wananchi na kukosa imani na maamuzi yanayotolewa na mabaza haya mara kwa mara. (Dada Harieth Kabende akichangia hoja juu ya usiri wa Uteuzi wa Wajumbe wa Mabaraza)

Wanaharakati bado wana nafasi ya kuhakikisha kwamba kasoro hizi ndogondogo zilizopo katika mabaraza haya zinarekebishwa ili kongeza tija katika utendaji wa mabaraza haya, kwani mabaraza haya yakitumiwa vizuri yanaweza kupunguza mzigo wa wananchi katika kutafuta haki zao katika mahakama za wilaya.

Je, wanaharakati wanafanya nini kuhakikisha mabaraza haya yanaboreshwa? Je, Hatua zipi zitumike katika Kuboresha utendaji kazi wa mabaraza haya?

Monday, October 6, 2008

Uchaguzi Tarime kuna walakini !!

Wanaharakati, Tarime ina dalili ya kuelekea kwenye machafuko kwa kutaka kutawala kwa nguvu zote.

Nahisi ni upigaji wa kura ndani ya mfumo wa kijeshi. Hii inaonyesha bila kutumia jeshi ushindi ni kitendawili.

Pia kunavitendawili vingi sana Tarime,kama majina ya wapiga kura kokosekana, msimamizi wa uchaguzi kudai
Atahakikisha watu wanapiga kura pamoja na kasoro zilizojitokeza kwenye majina yao, komputa kukosea????

Hivi kati ya komputa na mtumiaji wa komputa ni nani anayekosea?

Inabidi tulivalie njuga suala la tume huru ya uchaguzi kama tulivyo livalia suala la EPA na kaka zake.

Wanaharakati mnasemaje?

Friday, October 3, 2008

Wabunge wa Afrika Mashariki wapigiwe kura na Wananchi wote– Wabunge

Wabunge wa Tanzania wametaka ubunge wa Afrika Mashariki uwe ni wa kupigiwa kura na wananchi wote ili kuongeza kasi ya uwajibikaji ya wabunge hao badala ya utaratibu wa sasa kuwa wabunge ndio wanaowapigia kura.

Maoni hayo ya Wabunge wa Tanzania yametolewa na Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania Mhe. Zuberi Ali Maulid alipokuwa akitoa salamu za Tanzania katika mkutano wa mahusiano ya Mabunge ya Afrika Mashariki unaofanyika mjini hapa.

‘’Katika kipindi hiki ambacho Bunge la Afrika Mashariki limekuwa likitunga sheria zenye kuathiri Wananchi kwa ujumla na kwa kuwa Wabunge wa Jamhuri hawana fursa ya kujadili maamuzi ya Bunge hilo, ni vyema wabunge hawa wa Afrika Mashariki wakawa wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi’’ alisema Mhe. Maulid.

Mheshimiwa Maulid aliongeza kuwa ni muhimu pia kwa Mkataba wa Afrika Mashariki na Sheria za Tanzania kurekebishwa ili kuruhusu Wabunge wa Bunge la Tanzania kujadili na kupitisha maamuzi ya Bunge la Afrika Mashariki, ‘’ Maamuzi wanayoyatoa yana athari kubwa kwa watanzania wote, hivyo ni vyema maamuzi yao kabla ya kutekelezwa yapate baraka za Bunge la Tanzania kwa kujadiliwa’’ aliongeza Mheshimiwa Maulid.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambae pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sasa akifungua mkutano huo alisema kuwa bado kuna vikwazo vidogo vidogo katika kufikia ushirikiano wa pamoja kutokana na hofu zisizokuwa na msingi.

‘’Katika kipindi ambacho mazungumzo ya kuwa pamoja zaidi yanasuasua ni vyama wananchi wakaelewa kuwa kwenye ushirikiano huwa siku zote kuna hasara za muda mfupi lakini faida zake ni za kudumu", alisema.

Katika mkutano huo, Tanzania inawakilishwa na Mheshimiwa Zuberi Maulid ambae ndio kiongozi wa msafara na wapo pia Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Waheshimiwa Godfrey Zambi, Masolwa Cosmas, Beatrice Shelukindo, Ruth Msafiri na Hassan Kigwalilo.