Wednesday, June 22, 2011

Bajeti yapita, Mbowe asusa shangingi

BAJETI ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2011/12, imepita jana.

Serikali imetangaza kodi na tozo ambazo imezipunguza katika bidhaa ya petrol kuwa ni Sh. 323.5 kwa lita ili kuhakikisha bidhaa hiyo inashuka bei na kutoa ahueni ya maisha kwa wananchi.

Akihitimisha hotuba ya Bajeti ya Serikali bungeni, Waziri wa Fedha, Mustafa
Mkulo alisema, Serikali imekubaliana na ushauri wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na ushauri wa wabunge wengine kuondoa kodi na tozo kwa bidhaa hiyo ya petroli.

Alifafanua kuwa, Serikali imepunguza kodi ya bidhaa ya petroli kutoka Sh. 314 kwa lita hadi Sh. 256 kwa punguzo ambao ni karibia Sh. 100 kwa lita lita na pia imepunguza tozo mbalimbali zinazotozwa kwa lita kwa kiasi cha Sh. 224.50.

Mkulo pia alisema, Serikali pia itapunguza tozo za mamlaka mbalimbali za huduma kama, Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Usafiri wa Nchikavu na Majini Sumatra.

Nyingine ambazo tozo zao katika petrol zitapunguzwa ni Kampuni ya Kusafisha Mafuta (Tipper), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Mamlaka ya Udhibi wa Huduma za Maji na Nishati (Ewura).

Lengo la kupunguza tozo hizo kwa mujibu wa Mkulo ni kushusha bei ya bidhaa ya petroli.

Pia Waziri Mkulo alisema, Ewura itakokotoa upya kiwango kinachotozwa na kampuni zinazoagiza mafuta ambacho ni asilimia 7.5 ili kufidia gharama zingine na kushusha gharama kwa mlaji.

Aliwaeleza wabunge kuwa, ushuru kwa upande wa mafuta ya taa utarekebishwa ili kukomesha vitendo vya ukwepaji kodi na uchakachuaji vinavyofanywa na wahujumu uchumi na Ewura imekabidhiwa kazi ya kufanya hesabu ili tozo za mafuta ya taa
zipitiwe upya.

“Lengo letu ni kuondoa uchakachuaji kabisa,” alisema Mkulo. Ingawa waziri huyo
hakutaka kueleza tozo hizo kwa upande wa mafuta ya taa, ni wazi kuwa tozo na ushuru utaongezeka ili viwango vyake viwiane na vile vinavyotozwa kwa mafuta ya petrol na dizeli.

Mkulo alitumia muda mwingi kuzungumzia suala hilo la mafuta alisema hata hivyo Tanzania haipangi bei ya mafuta katika soko la dunia.

Alitoa mfano kuwa ndani ya wiki moja, bei katika soko hilo, bei ya pipa imepanda kutoka dola za Marekani 116 hadi 131.

Pia alisema, kuimarika kwa dola na kushuka kwa thamani ya Shilingi nalo ni tatizo
lingine ambalo linachangia bei ya bidhaa ya petrol kupanda. Alitoa mfano kuwa kwa
sasa dola moja ya Marekani ni Sh. 1,600.

Hata hivyo waziri huyo alitamba kuwa marekebisho yaliyofanywa na Serikali yataleta nafuu na kuchagamsha uchumi wa nchi.

Alisema pia marekebisho hayo yataondoa uharibifu wa magari na yatapunguza bei na kushusha gharama za usafirishaji na Serikali itapata mapato yote yalikuwa yanapotea kwenye uchakachuaji wa mafuta.

Kwa upande wa posho, Waziri Mkulo alisema, uamuzi wa kuzifuta na kuzirekebisha baadhi ya posho hizo umefikiwa na Serikali yenyewe. Alisema katika hotuba yake alisisitiza kuwa ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Serikali itapunguza posho zisizo na tija na safari za nje ambazo hazina tija.

Alisema suala hilo la posho limekuzwa isivyo kawaida na kwa kutumia takwimu ambazo si sahihi. Alisema posho zote zimetengwa Sh. bilioni 312 na si Sh bilioni 980 kama zilivyokuwa zinadaiwa na Kambi ya Upinzani.

Kati ya Sh. bilioni 321.74, posho zilizometengwa kwa ajili ya vikao (Sitting allowance) ni Sh. bilioni 25.68 tu na kati ya hizo wabunge peke yao watatumia Sh. bilioni 4.92 tu.

“Kwa hesabu hizo wabunge pimeni kama tukiamua kufuta posho za vikao kwa wabunge tutaokoa Sh bilioni 4 tu na kama tukifuta kwa Serikali nzima zitaokolewa Sh bilioni 25.68.

Alisema posho zingine haziwezi kuondolewa kwani zipo kisheria hivyo hazifutwi na akatoa mfano wa posho za joho la jaji au posho za madaktari.

Alisema, kwa kuwa umeme ndio kipaumbele kikubwa cha bajeti ijayo, Mkulo ambaye
amekuwa anatuhumiwa kulidanganya Bunge kutokana na takwimu za miradi ya umeme, alibanisha kuwa wizara hiyo imetengewa zaidi ya Sh. bilioni 402 na ya hizo fedha za maendeleo ni Sh. bilioni 325.4 na Sh. bilioni 74 ni matumizi ya kawaida.

Pia alisema, kuna Sh bilioni 536.9 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya umeme
zikiwemo fedha zilizoko katika miradi ya MCC. “Sijaliongopea Bunge fedha za miradi ya umeme zipo.”

Alikiri kuwa ni kweli misamaha inapunguza mapato ya Serikali lakini akasisitiza kuwa
inatolewa kwa nia njema hivyo ni lazima iendelee kutolewa kwani inasaidia katika
huduma za kijamii.

Alisema, Serikali inapitia upya baadhi ya misamaha hiyo na ile inayotumiwa vibaya itafutwa.

Alifafanua kuwa hata hivyo misamaha hiyo imepungua kutoka asilimia 4.2 ya pato la Taifa katika bajeti iliyopita hadi kufikia asilimia 2.5 ya pato la Taifa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha.

Wabunge waliopitisha bajeti, 234 walikubaliana na bajeti hiyo,wabunge 81 wakikataa bajeti hiyo.

Pamoja na maelezo hayo ya Mkulo, Kambi ya Upinzani ilikataa Bajeti hiyo kwa madai kuwa hoja zao hazijazingatiwa hata baada ya baadhi kuelezwa na Mkulo kuwa zilikuwa za uongo.

Kutokana na madai hayo, kuwa hoja zao hazikuzingatiwa ikiwemo ya posho, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe jana alitangaza kurejesha gari , shangingi alilopewa na Bunge ili lipingwe mnada.

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya bajeti kupitishwa, Mbowe alisema
wamemwandikia Katibu wa Bunge wakimweleza pia kuwa wabunge wa Chadema hawatasaini fomu za posho pamoja na madai ya juzi kuwa baadhi ya wabunge wa chama hicho hawakupenda kususia posho.

"Tunawataka wabunge wengine waunge mkono hoja hizi kwa maslahi ya wananchi na Taifa
kwa ujumla," alisema Mbowe.

No comments: