Friday, June 24, 2011

Mahakama yaionya Serikali kesi ya Richmond

HAKIMU anayesikiliza kesi ya kughushi na kutoa taarifa za uongo kuhusu Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond inayomkabili Mfanyabiashara, Naeem Gire, ametoa onyo la mwisho kwa Wakili wa Serikali, Fedrick Manyanda akamilishe ushahidi wake haraka.

Onyo hilo lilitolewa jana na Hakimu Waliarwande Lema wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi hiyo ilipokuja kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka.

Alisema, kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuleta mashahidi wake kwa wakati na kuahirisha kwa mara ya mwisho Juni 28 mwaka huu ambapo watakaposikiliza shahidi wa mwisho.

“Nimekubeba vya kutosha mpaka sasa ninaona aibu, ninaomba ulete shahidi wako wa mwisho kabla ya kufunga kesi na mashitakiwa kuandaa utetezi wake,” alisema Hakimu Lema.

Awali wakili wa upande wa utetezi, Alex Mgongolwa aliitaka mahakama kufunga ushahidi wao kwa kuwa ni mara ya tatu wanaahirisha kesi kutokana na shahidi kutofika mahakamani na kumtaka Wakili Manyanda kutaja jina la shahidi huyo.

Juzi kesi hiyo iliahirishwa kwa kuwa shahidi aliyetakiwa kutoa ushahidi wake hakufika mahakamani.

Jambo hilo lilizua mjadala kati ya mawakili hao na Mgongolwa akalalamikia upande wa mashitaka kuchelewesha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Inadaiwa kuwa, Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa Gire alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya Serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme ili apewe zabuni.

Katika mashitaka mengine inadaiwa kuwa Gire, aliwasilisha hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, 2006 ikimuonesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Hemed Gire ambaye ni kaka yake kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

No comments: