Monday, June 27, 2011

Katiba mpya kuzinduliwa Aprili 26,2014

KATIBA MPYA ambayo mchakato wake umeanza inatarajiwa iwe imekamilika na kuzinduliwa rasmi Aprili 26, 2014 wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema mjini hapa.

Akifungua Semina Elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya kuhusu mchakato wa Katiba Mpya kwenye ukumbi wa Hoteli ya St. Gasper, alisema hayo ndiyo matarajio ya Serikali.

"Ni matarajio ya Serikali kuwa Katiba Mpya itakuwa imekamilika na kuzinduliwa ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014 katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kwamba kama mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Muswada wa Sheria kuhusu Mapitio ya Marekebisho ya Katiba utawasilisha bungeni mwishoni mwa Mkutano wa Nne wa Bunge unaoendelea hivi sasa au mwanzoni mwa Mkutano wa Tano Oktoba mwaka huu.

Aliwataka Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni itakayoundwa ili kuwezesha mikutano ya hadhara ya kukusanya maoni
kufanyika kama ilivyokusudiwa kwa kuhamasisha wananchi kuhudhuria na kutoa maoni yao.

“Katika suala hili kubwa na la kitaifa, ni vyema viongozi wasiingize siasa na wajiepushe kuwashawishi wananchi katika kutoa maoni yao, bali wawaache watoe maoni kwa uhuru au pasipo shinikizo lolote,” alisema.

Mchakato huo wa kuelekea uundwaji wa Katiba Mpya, umekwishaanza na katika hatua ya awali, Serikali imeandaa rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba ya Mwaka 2011.

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa hatua ya sasa siyo kutunga Katiba Mpya bali ni kuunda Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuelekea kutungwa kwa Katiba Mpya.

No comments: