Wednesday, December 22, 2010

Tibaijuka ‘ang’ata’ usiku

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliposema atahakikisha watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi na yasiyoruhusiwa wavunje wenyewe majengo yaliyopo, hakuwa anatania na wale waliokuwa wakimvimbishia kichwa, watakuwa wamekosea.

Hali hiyo ilidhihirika jana jioni wakati tingatinga la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam, lilipofanya kazi ya kuvunja maeneo ambayo yameanza kujengwa majengo kinyume cha utaratibu na ambayo inaaminika kuwa ni ya wazi au hayaruhusiwi majengo hayo.

Jana majengo mawili katika Jiji la Dar es Salaam, kiwanja kilichopo karibu na Hoteli ya Palm Beach, ambacho ndio kwanza kilikuwa kimepandishwa ukuta pamoja na ukuta mwingine uliojengwa jirani na Hospitali ya Aga Khan katika Barabara ya Ocean Road, vilivunjwa jana jioni na askari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Licha ya mmiliki wa kiwanja cha jirani na Hoteli ya Palm Beach, Taher Muccadam kutoa notisi ya siku saba kwa Waziri Profesa Tibaijuka amuombe radhi na kumlipa fidia ya Sh bilioni mbili kwa madai kwamba alimvunjia heshima kwa jamii vinginevyo atamfikisha mahakamani, agizo hilo limepuuzwa.

Badala yake, umma wa wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa wakirejea majumbani mwao jana jioni, walishuhudia tingatinga la Manispaa ya Ilala, lenye namba SM 3937, chini ya ulinzi mkali, likifanya kazi ya kuangusha ukuta huo saa moja jioni kabla ya kuhamia ukuta wa jirani na Aga Khan nusu saa baadaye.

Kazi hizo mbili zilifanywa na tingatinga hilo chini ya ulinzi wa askari zaidi ya 50 waliokuwa katika magari mengine manne, Isuzu; Toyota Land Cruiser Hard Top, Toyota Double Cabin na Toyota Nissan Patrol yenye namba za usajili SM 3096, SM 4360 na STJ 5662, mali ya Manispaa ya Ilala.

Mara baada ya kazi hiyo kukamilika katika eneo la Palm Beach, wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, baadhi yao walisikika wakisema, “huyu ndiye Waziri, siyo viongozi wababaishaji. Watu wanamtisha eti wana vibali kutoka Ikulu, yeye aliwambia hatishiki na vibali vyao.”

Mwingine alisema, “huyu mama (Profesa Tibaijuka) hana mchezo, kama fedha anazo za kutosha, hasumbuliwi na vijisenti…tunahitaji viongozi wenye kusimamia sheria nchini mwetu.”

Mmoja wa viongozi waliosimamia kazi hiyo, hakutaja kutaja jina lake wala kueleza hatua hiyo imefikiwa na nani, akisema, “hatupo hapa kuongea na vyombo vya habari. Kazi mnaiona.”

Kiwanja hicho cha Palm Beach ambacho ni namba 1006 ni kati ya viwanja ambavyo Profesa Tibaijuka alidai kuwa ni cha wazi na kwamba hakiruhusiwi kuwa makazi.

Hivi karibuni, Profesa Tibaijuka akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam aliwataka wananchi waliopora viwanja na maeneo ya wazi nchini na kujenga, wajisalimishe kwa mazungumzo, kwa sababu huenda wakaokoa hata matofali kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.

Fedha za kashifa ya rada kurejeshwa Tanzania

KAMPUNI kubwa ya ulinzi ya Ulaya, BAE Systems, imekubali kuilipa Serikali ya Tanzania fidia ya Sh bilioni 67.29 (pauni milioni 30) kama walivyokubaliana na Taasisi ya Kuchunguza Makosa makubwa ya jinai ya Uingereza, SFO, ikiwa ni sehemu ya kumaliza shauri lililokuwa linawakabili mahakamani.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kampuni hiyo kuhukumiwa kulipa faini ya pauni 500,000 au dola za Marekani 775,000, sawa na Sh bilioni 1.12 baada ya kukiri kosa la ‘kushindwa kuweka kwa usahihi kumbukumbu za manunuzi.’

Viwango vya ubadilishaji kwa siku ya jana kwa mujibu wa Benki Kuu ni pauni moja sawa na Sh 2,243 wakati dola moja ni Sh 1,442.

Kampuni hiyo imesema kwamba kwa sasa inaangalia utaratibu wa malipo hayo ikiwa ni sehemu ya fedha zilizolipwa na Serikali ya Tanzania kununua rada hiyo ya kisasa.

Mpango huo ulikuwa na thamani ya dola milioni 40 sawa na pauni milioni 28. Mahakama ilitoa hukumu hiyo kwa kuzingatia shauri la kutoweka taarifa vyema.

Suala la kutoa mlungula ambalo awali lilitawala uchunguzi wa SFO halikufikishwa mahakamani.

Jaji David Bean alisema itakuwa ni kuukataa ukweli kufikiri kuwa wakala wa BAE nchini Tanzania, Shailesh Vithlani, alilipwa mamilioni ya dola eti kwa sababu tu anajua kuunganisha vyema masuala ya biashara.

BAE ilikubali kwamba inawezekana kwamba sehemu ya dola milioni 12.4 (waliyomlipa Vithlani) ilitumika kwa ajili kuisaidia kupata zabuni hiyo.

Hata hivyo waendesha mashtaka wamesema kwamba ni vigumu sana kuweza kujua Vithlani alifanya nini na fedha hizo na wala kuthibitisha kwamba sehemu ya fedha hizo zilitumika vibaya.

Kwa mujibu wa maelezo fedha hizo zililipwa kwa kampuni za Vithlani za British Virgin Islands na Kampuni ya Merlin iliyosajiliwa Tanzania.

Kampuni ya BAE imesema kwamba imefurahishwa na shauri hilo kumalizwa na kwamba inaandaa utaratibu wa kuilipa Tanzania fedha zake.

Hukumu hiyo iliyotolewa jana na Jaji David Bean mjini London inahitimisha miezi sita ya uchunguzi wa kina wa shauri hilo.

BAE ilikiri kosa hilo la kushindwa kutunza vyema kumbukumbu za manunuzi mwezi uliopita katika mpango wake na Taasisi ya Kuchunguza Makosa makubwa ya jinai ya Uingereza, SFO.

Kampuni hiyo iliridhia Februari kulipa pauni milioni 30 kama sehemu ya fidia na waendesha mashitaka walisema wangekubaliana na BAE ikiwa wangelipa faini hiyo na kutuma ‘chenji’ kwa Serikali ya Tanzania.

Kampuni hiyo ilikuwa katika uchunguzi nchini Uingereza kuanzia Novemba, 2004 kwa tuhuma za kutoa rushwa ili kushinda zabuni za manunuzi katika nchi sita ikiwamo Tanzania na Jamhuri ya Czech.

Februari mwaka huu BAE ilikubali kulipa karibu dola za Marekani milioni 450 kama fidia ili kumaliza shauri hilo baina yake na SFO na waendesha mashitaka wa Marekani.

Hata hivyo, BAE ililipa dola za Marekani milioni 400 kwa Marekani na kukiri kosa la kutoweka taarifa sahihi ya manunuzi hayo. Kampuni hiyo ilikanusha kutoa rushwa.

“Jukumu langu ni kufikisha kesi mahakamani na kuhakikisha kuwa Jaji anatoa adhabu stahili,” alisema Mkurugenzi wa SFO, Richard Aderman baada ya hukumu.

Alisema ana uhakika kuwa BAE itatekeleza makubaliano yaliyofikiwa ya kuilipa Serikali ya Tanzania ‘chenji’ ya pauni milioni 30 (zaidi ya Sh bilioni 60), baada ya kulipa faini nchini Uingereza.

Wakili aliyekuwa akiitetea BAE, Arno Chakrabarti, alikataa kusema chochote baada ya hukumu hiyo.

Shauri hilo la rada lililoelezwa kufanywa na mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye alihusika katika mpango huo kuinufaisha BAE, pia limemhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wahusika wa kashfa hiyo.

Tuesday, December 21, 2010

Hoseah akanusha uvumi wa Wikileaks

TAARIFA zilizovuja za mtandao wa Wikileaks, ambazo zilizotoka kwa Serikali ya Marekani, zimemgusa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Dk. Edward Hoseah, na kwa haraka, amekanusha kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa ni kikwazo cha utendaji wa taasisi hiyo, kama alivyonukuliwa humo.

Dk. Hoseah, anadai katika taarifa za mtandao huo zilizoripotiwa jana na gazeti la The Guardian la Uingereza kueleza kuwa Rais Kikwete alikuwa anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, na pia madai kuwa anahofia maisha yake kama Mkuu wa Takukuru.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Dk. Hoseah anakiri kukutana na ofisa wa Marekani ofisini kwake Julai 2007, lakini katika mazungumzo yake, anakanusha kuwa hakuna mahali popote alipoeleza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.

“Nilichosema ni kwamba Rais hataki kuruhusu uchunguzi wa maofisa waandamizi wa serikali au mtu yeyote yule kufanywa kwa kuegemea katika minong’ono au ushahidi dhaifu, kwa sababu kwa kufanya hivyo, serikali inaweza kuwa katika hatari ya kulipa fidia kubwa kama watuhumiwa watashinda kesi mahakamani,” alidai Dk. Hoseah katika taarifa yake jana.

Kuhusu madai ya ‘hofu ya maisha yake’, alisema anakumbuka kuulizwa na ofisa huyo kama anahofia uhai wake au la, akiwa ni Mkuu wa Takukuru, na kwamba jibu lake lilikuwa rahisi, “ndio, wakati unaposhughulika na vigogo au matajiri, ni lazima uwe mwangalifu na tahadhari na maisha yako.”

“Lakini hakuna mahali popote nilipotamka kuwa nina mpango wa kukimbia nchi kwa sababu maisha yangu yalikuwa hatarini. Ni jambo la kushangaza kwa mara nyingine, Ofisa huyo wa Ubalozi wa Marekani amenikariri kinyume na ukweli na sijui nia yake hasa ilikuwa nini.”

Dk. Hoseah alisema kupokea vitisho ni sehemu ya kazi yake kwa sababu anawachunguza watu matajiri na wenye nguvu, lakini kwa kuwa kila kitu kinafanyika kulingana na sheria iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, “hakuna cha kuhofia sana kwa sababu kila kitu kiko katika sheria.”

Aliihakikishia jamii kwamba ingawa kazi yao ni ngumu, wataendelea na dhamira yao ya kupambana na rushwa katika ngazi zote kwa kushirikiana na wadau wote nchini.

“Tunaamini kwa pamoja tutashinda vita hii, lakini tukigawanyika, itakuwa kazi ngumu kufikia dhamira yetu.”

Mgawo waanza tena, bei ya umeme juu

WAKATI Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ikiamuru wafanyakazi takribani 5,000 wa Tanesco kulipa viwango sawa vya bei za umeme kama ilivyo kwa wananchi wengine, na ikiridhia kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi, mgawo wa umeme unaanza tena leo.

Mgawo wa umeme uliositishwa wiki moja iliyopita, umetangazwa jana mjini Kilwa mkoani Lindi ikiwa ni kutokana na Kampuni ya Pan African Energy inayozalisha gesi asili katika kisiwa cha Songosongo kupunguza uzalishaji kwa ajili ya kufanyia matengenezo kisima kimoja kati ya vitano ilivyonavyo.

Mahitaji ya matengenezo ya kisima hicho yaligundulika Septemba mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema Tanesco imelazimika kuanza tena mgawo tena kutokana na upungufu wa megawati 40, akisema “tunalazimika kupunguza uzalishaji katika mtambo wa Ubungo ambapo baada ya kuzalisha umeme wa megawati mia moja, sasa tutalazimika kuzalisha megawati 60, na ratiba tutartoa baada ya kuipanga.”

Mramba alitangaza mgawo huo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakati alipotembea Kilwa Kisiwani kunakozalishwa gesi asilia kwa ajili ya kuiuzia Tanesco na Kampuni ya Songas.

Akitoa taarifa kuhusu kukifanyia matengenezo kisima hicho, Naibu Meneja Mkuu wa Pan African Energy, William Chiume alisema kutokana na matengenezo hayo, watapunguza uzalishaji kwa asilimia 16 kutoka futi za ujazo milioni 86 hadi 76, ambazo ni sawa na megawati 40.

Alisema matengenezo hayo yatachukua kati ya wiki nne na tano kuanzia sasa. Hata hivyo, alisema waathirika wakubwa ni Tanesco, kwani Songas wataendelea kupata gesi kutokana na mkataba walionao. Songas pia wanaiuzia umeme Tanesco.

Songas inaiuzia Tanesco megawati 182 za umeme kwa siku na wakati mitambo ya Tegeta inazalisha megawati 45, Ubungo megawati 100, yote ya gesi asili wakati mahitaji ni megawati 833 kwa siku.

Wakati mgawo huo ukitangazwa Kilwa, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu alitoa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Ewura wa maombi ya Tanesco ya kubadilishiwa bei za umeme, na kueleza kuwa Bodi imekubali ombi hilo na imepandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari mosi.

Masebu alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakilipia viwango maalumu, hivyo Bodi imeamuru walipe kama ambavyo wananchi wengine wanalipia na endapo hawatotekeleza itaonekana wakati wa ukaguzi.

Akifafanua zaidi, Mkurugenzi wa Umeme wa Ewura, Anastas Mbawala alisema wafanyakazi wa Tanesco wanakadiriwa kufikia 5,000 na wamekuwa wakilipa Sh nne kwa kila uniti ya umeme, ingawaje kwa wale ambao ni mke na mume, alikuwa anapewa mmojawapo na sio wote.

Kuhusu bei ya umeme, Masebu alisema maombi ya Tanesco yalitolewa Mei 28, mwaka huu na mchakato ulianza mara moja wa kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili kwa kina suala hilo ili kila mmoja aridhike na hatua zitakazofuatia.

Masebu alisema mikutano ilifanyika Agosti katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Tabora na Dar es Salaam, na kwamba “baada ya kukutana na wadau mbalimbali na kujadili kwa kina suala la kubadilishiwa bei hizo, Ewura iliona kuna hoja ila hawawezi kukubali maombi hayo kama yalivyoletwa na Tanesco.”

Alisema Tanesco waliomba kuwe na mpangilio wa kubadilisha bei ya umeme kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2011 kwa asilimia 34.6, asilimia 13.8 na asilimia 13.9 ili waboreshe huduma zao na kuwa endelevu wakati wote.

Kadhalika alisema Tanesco waliomba pia mabadiliko hayo yaende pamoja na kuwa na uwezo wa kurekebisha viwango vya umeme wakati wowote, kuruhusiwa kubadilisha bei ya umeme katikati ya kipindi hicho kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta na kubadilika kwa viwango vya umeme kadri ya matumizi.

Alisema ni kweli Tanesco wanahitaji zaidi ya Sh bilioni 691 ili itoe huduma endelevu, hivyo Ewura imekubali ombi lao kwa asilimia 18.5 ikiwa ni pungufu ya asilimia 16.1 huku gharama nyingine kutokubaliwa hadi hapo watakapopata mtaalamu mshauri atakayefanyia kazi suala hilo na kuona kama viwango hivyo vinafaa.

Alisema kwa marekebisho hayo, bei ya umeme kwa watumiaji wadogo wanaotumia umeme usiozidi kilowati 50 watalipia Sh 60 kwa kila uniti kutoka Sh 49 za awali huku watumiaji wa kawaida watalipia Sh 157 kutoka Sh 129.

Kuhusu kufungua akaunti maalumu, alisema baada ya kukusanya fedha hizo za viwango vipya, Tanesco wanatakiwa kufungua akaunti ya fedha hizo na kuagiza kuwa zielekezwe katika kazi husika ambapo Ewura watakuwa wakikagua kila baada ya miezi mitatu.

Masebu alisema kutokuwakubalia Tanesco kupandisha umeme wasingekuwa na uwezo wa kujiendeleza na vilevile hatua hiyo inatoa nafasi kwa wawekezaji wengine kujiingiza katika sekta hiyo.

Monday, December 13, 2010

Chadema wamtambua Kikwete

JAKAYA Kikwete aliwaambia viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwamba hawana mwingine wa kumlilia kwa masuala yao, isipokuwa yeye; na kwamba watakwenda na kurudi kwake kwa sababu yeye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Novemba 18, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma wakati akihutubia Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 10,na sasa aliyoyasema yametimia.

Baadhi ya wabunge wa Chadema walitoka katika ukumbi wa Bunge wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe walitoka nje mara tu Rais Kikwete alipoanza hotuba yake, sasa wamekubali yaishe. Wanamtambua ndiye Rais halali wa Tanzania.

Lakini katika kauli iliyowalenga moja kwa moja wabunge wa Chadema wakati akimalizia hotuba yake bungeni, Rais Kikwete alisema wabunge hao hawana wa kumlilia zaidi yake, kwani yeye ndiye Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Watakwenda watarudi, hawana mwingine wa kumlilia kwa yao, isipokuwa Serikali ya CCM ambayo mimi ndiye Rais wake; Dk. Mohammed Gharib Bilal ndiye Makamu wake. Serikali ambayo Dk. Ali Mohammed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais na Balozi Seif Ali Idd ni Makamu wa Pili wa Rais,” alisema Rais Kikwete, Novemba 18, mwaka huu na kushangiliwa na wabunge.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho katika siku za karibuni, kilitangaza kutomtambua Rais Jakaya Kikwete, kimebadili msimamo.

Kimekubaliana kwamba Kikwete ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kinatarajiwa siku yoyote kuanzia leo kutangaza maazimio ya Kamati Kuu iliyokutana mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, ambayo moja ya maazimio yake, ni kumtambua kiongozi huyo wa nchi.

Kamati Kuu ya Chadema pia imeamua kusitisha uamuzi wa wabunge wa chama hicho kwa kumvua nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, mbunge mwenzao, Kabwe Zitto wa Kigoma Kaskazini.

Baada ya Rais Kikwete kutangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, Chadema ilikataa kumtambua, ikidai alichaguliwa kutokana na uchaguzi uliokuwa na udanganyifu.

Novemba 18, mwaka huu, wakati akianza hotuba ya kulihutubia Bunge jipya mjini Dodoma, baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa ndani ya ukumbi wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, walitoka nje ya ukumbi huo.

Lakini sasa, vyanzo vya habari kutoka ndani ya Kamati Kuu ya Chadema, vimeliarifu gazeti hili kuwa wamekubaliana kumtambua Rais Kikwete baada ya mjadala mzito na baada ya kupima athari za kutomtambua Rais Kikwete aliyeshinda kwa zaidi ya asilimia 60.

Kuhusu suala la Zitto, chanzo hicho cha habari, kilieleza kuwa wajumbe wakongwe wa Kamati Kuu walimtetea na kueleza kuwa mbunge huyo machachari hakupewa nafasi ya kujitetea.

Wabunge wa Chadema walikutana Bagamoyo wiki iliyopita na kupiga kura ya kutokuwa na imani na Zitto, wakimtuhumu kwa kwenda kinyume cha msimamo wa chama hicho wa kumsusa Rais Kikwete bungeni.

Zitto hakupatikana kuzungumzia hatua hiyo mpya ya chama chake jana, kwa sababu simu yake iliita bila kupokewa, ikiwa ni siku moja baada ya kutoka Hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa amelazwa tangu Alhamisi iliyopita, kwa kusumbuliwa na maumivu ya tumbo, ikidaiwa alikula chakula chenye sumu.

Kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa ndani ya chama hicho, Kamati Kuu iliamua pia kuunda kamati maalumu ya watu wanne ikiongozwa na Profesa Mwesiga Baregu, kwa nia ya kurejesha amani kundini.

Kamati hiyo kwa maudhui, inafanana na ile iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juni mwaka huu, ikiongozwa na Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi kupatanisha makundi hasimu yaliyokuwa yameibuka ndani ya wabunge wake.

Alipoulizwa kuhusu kamati hiyo, Profesa Baregu alithibitisha na kueleza kuwa Kamati yake imepewa jukumu la kuhakikisha amani inarejea katika chama hicho.

“Ndiyo, kuna kamati maalumu inayowahusisha wajumbe wakongwe wa Kamati Kuu iliyoundwa kwa ajili ya kuhakikisha umoja na amani zinarejea katika chama,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kurejeshwa kwa umoja na amani katika chama hicho, pia kutahakikisha umma haupotei imani yao kwa chama hicho cha upinzani.

“Tutazungumza na wanachama ambao wana malalamiko au wana matatizo, ili kumaliza tofauti zao na kurejesha tena mshikamano, amani na upendo katika chama…hatutaki kupoteza imani ya umma kwetu,” alieleza Profesa Baregu.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Shida Salim ambaye ni mama mzazi wa Zitto, Kitila Mkumbo ambaye ndiye Katibu na mjumbe mwingine aliyetajwa kwa jina la Shilungushela.

Katibu Mkuu wa Chadema, alikataa kuzungumzia maazimio hayo jana alipotafutwa kwa simu, lakini akaeleza kuwa watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho.

Friday, December 10, 2010

RAIS KIKWETE AMTEUA JAJI MSTAAFU SALOME SUZETTE KAGANDA KUWA KAMISHNA WA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Jaji Mstaafu Salome Suzette Kaganda kuwa Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma.

Taarifa iliyotolewa Ikulu, Dar es Salaam, leo, Jumatano, Desemba 8, 2010, na Katibu Mkuu Kiongozi, Mheshimiwa Phillemon Luhanjo, inasema kuwa uteuzi huo ulianza Jumamosi, Desemba 4, 2010.

Jaji Mstaafu Salome Kaganda anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ambaye amemaliza muda wake.


Kabla ya kustaafu, Mheshimiwa Salome Suzette Kaganda alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kusini, Songea.


Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

08 Desemba, 2010

Wednesday, December 8, 2010

MICHANGO YA KUANDIKISHA DARASA LA KWANZA

Tukumbuke kwamba wakati huu ni wakati wa kuandikisha watoto kwenda darasa la kwanza. na Serikali ya Tanzania inasema au tuseme sera ya elimu inasema kwamba elimu ya msingi ni bure. lakini sasa hivi inajitokeza kuwa kila mzazi anayekwenda kumwandikisha mtoto hasa katika shule ya Msingi Bryceson huko Mburahati jijini Dar es salaam kila mzazi/mlezi anayekwenda kuandikisha mtoto anadaiwa apeleke shilingi 22,400 ikiwa ni mchango wa madawati, mlinzi, na mengineyo lakini cha ajabu risiti hazitolewi.

Je uhalali uko wapi? Halafu hili suala la kutochangia kwa maana ya elimu ya msingi bure likoje mbona kama magumashi hivi????????

Najua tukifuatilia kuna mengi mno ambayo tunaweza kuibua. Kazi kwetu!!!

Tuesday, December 7, 2010

Waliokuwa CCJ waibukia CCK

CHAMA Cha Kijamii (CCK), kinaandaa waraka utakaochambua mapungufu ya Katiba ya sasa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

CCK watauwasilisha waraka huo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, ili kutoa hoja yao rasmi ya kwa nini Tanzania inahitaji kuwa na Katiba mpya.

Aidha, kimesema kinakusudia kushiriki katika kufungua au kuwa marafiki wa mahakama katika kesi za kikatiba zinazohusiana na masuala ya uchaguzi mkuu kwa madai kuwa si mambo yote yanaweza kumalizika au kubadilishwa kisiasa.

Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda, aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana ambapo pamoja na mambo mengine, alisema wanaendelea kufuatilia usajili wa kudumu.

Akitanda alisema karibu asilimia kubwa ya matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu yalitokana na kiashirio cha kutokuwepo kwa Katiba mpya yenye kutengeneza mazingira mazuri ya uhusiano kati ya watawala na watawaliwa, na yote yanaweza kusahihishwa vizuri endapo Katiba itaandikwa upya.

“Kama tulivyosema hapo awali kuwa kuna haja ya Katiba mpya, na kwa kuzingatia kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani kuwa hadi hivi sasa hakuna chama chochote kilichotoa madai rasmi ya hoja kuhusu Katiba mpya, sisi kama CCK tukizingatia nafasi iliyopo mbele yetu, tunaandaa waraka utakaochambua mapungufu hayo,” alifafanua Akitanda.

Kuhusu kushirikiana na mahakama katika kesi za kikatiba, alisema wameamua kufanya hivyo wakiamini kuwa mambo mengine katika suala hilo yanahitaji nguvu ya chombo hicho na watachukua njia hiyo wakati wowote wanapoiona njia hiyo ni bora.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Renatus Muabhi, alisema wapo mbioni kufanikisha azma ya kupata usajili wa kudumu ili hatimaye na chenyewe kitoe mchango wake wa kifikra na kiuongozi nchini.

Friday, December 3, 2010

Taarifa ya Lowassa kuchunguzwa balaa

-Raia Mwema lapata msukosuko
-Nakala 10,000 zaharibiwa zisisomwe

HABARI iliyoihusisha familia ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, imeibua utata mkubwa baada ya kuibuka kwa vitisho vilivyosababisha kuzuiwa kuchapwa kwa gazeti la Raia Mwema toleo lililopita Namba 161 katika mazingira ya kutatanisha; huku habari hiyo ikikanushwa kwenye gazeti jingine hata kabla haijatoka.

Utata huo ulisababisha uongozi wa Imprint iliyopo chini ya kampuni ya Jamana Printers kusitisha ghafla kuendelea kuchapwa kwa gazeti la Raia Mwema ikiwa tayari limeshachapwa nakala 10,000 katika mazingira yaliyoonyesha kuwapo shinikizo zito kutoka kwa kigogo mmoja aliye karibu na mwanasiasa huyo la kutaka habari inayomhusu Lowassa iondolewe ndipo gazeti lichapwe.

Raia Mwema ambalo lina makubaliano maalumu na wachapaji hao lilishtushwa na uamuzi huo wa ghafla wa wachapaji hao hasa baada ya uamuzi huo kuambatana na hali ya woga mkubwa uliotawala wafanyakazi wa kiwanda hicho usiku wa Jumanne ya wiki iliyopita.

Taarifa ya Meneja Usambazaji wa Raia Mwema, Omari Mwendapole, ambaye alikuwapo usiku huo, inaeleza kwamba hali ya uchapaji iliendelea katika hali ya kawaida kuanzia saa 11 jioni kabla ya kubadilika ghafla saa 1:30 usiku, ilipotolewa amri ya kusitisha uchapaji wakati zikiwa zimekwishachapwa nakala 10,000.

“Tulifika kiwandani mapema saa 11:00 na hakukua tatizo lolote baada ya wahusika kukagua gazeti letu na kuridhika nalo na wakaanza taratibu zote ikiwa ni pamoja na kuchoma plate saa 11:15 na saa 12:00 kazi ya uchapaji ilianza taratibu hadi saa 12:30 mashine zilipoanza kuchanganya na kutoa gazeti zuri.

“Lakini baada ya muda kidogo, msimamizi wa uchapaji wa Imprint akaitwa na mlinzi kwenda kusikiliza simu na aliporejea akawaagiza mafundi wazime mashine kabla ya kuamua kuzima mwenyewe baada ya kuona wanachelewa kufanya hivyo.

“Baadaye niliitwa kwa bosi wao na kuambiwa natakiwa kwenda kwa Meneja Mkuu, aitwaye Shaber, ambako nilijulishwa kwamba ni lazima habari kuu (inayomhusu Lowassa) iondolewe vinginevyo gazeti halitochapwa kabisa,” anasema Mwendapole.

Kutokana na amri hiyo ya wachapaji, wafanyakazi wote wa Raia Mwema na watu wengine wote waliokuwamo kiwandani wakati huo waliamriwa kutoka eneo la uchapaji na kupekuliwa kuhakikisha hawabebi hata nakala moja ya gazeti hilo.

Habari zinasema kuwa nakala 10,000 ambazo tayari zilishachapwa ziliharibiwa chini ya uangalizi mkali wa maofisa wa kiwanda hicho ili kuhakikisha kuwa haziingii kwenye soko, na hivyo habari hiyo kusomwa na wananchi.

Hata hivyo, wakati uongozi wa Raia Mwema ukihangaika kutafuta mahali pengine pa kuchapa, ilibainika kwamba kigogo huyo pamoja na mbunge mmoja walikuwa tayari na nakala ya gazeti hilo na ilidhihirika siku iliyofuata baada ya gazeti la Mtanzania lenye uhusiano wa karibu na kigogo huyo kuchapisha habari iliyokanusha habari hizo kabla hata ya habari husika kuchapishwa.

Katika habari hiyo, gazeti hilo lilielezea kwamba kuna taarifa “zilizochapwa katika magazeti” huku zikimnukuu Frederick Lowassa, ambaye ndiye aliyekuwa mhusika mkuu katika habari ya Raia Mwema, akijitetea kwa kudai kwamba hakuwahi kusafirisha fedha nyingine Uingereza kama ilivyoandikwa na ‘magazeti hayo.’

Katika tukio hilo la aina yake katika tasnia ya habari, Frederick Lowassa, alisema;

“Jamani mimi nashangaa sana. Watu hawa wanasahau kuwa mimi ni mfanyabiashara kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Na katika kufanya biashara ni lazima nisafirishe fedha nje ya nchi kwa nia ya kununua material (bidhaa). Nasafirisha fedha sehemu mbalimbali duniani, na sijui wameliokota wapi hilo.

“Hakuna wakati nimewahi kusafirisha paundi 495,000 nje ya nchi kwa mara moja, ila nasafirisha fedha nje ya nchi kununua bidhaa mara nyingi tu. Hili wanalozungumza la Uingereza ni kweli kati ya Machi na Aprili nilisafirisha kama Paundi chini ya 200,000 hivi, kwa ajili ya biashara kama kawaida. Benki kama kawaida walijiridhisha fedha hizo zilikotoka, tukawasiliana likaisha.

“Sasa nashangaa watu hawa hili wamelitoa wapi? Na ifahamike kuwa mimi nafanya biashara nyingi tu, na moja ya biashara zangu ni kampuni ya Alphatel. Sisi ni mawakala wa Vodacom. Tunover (mzunguko wa fedha) yetu kwa mwezi ni zaidi ya Sh bilioni 8.0. Hizi ni fedha zinazotumiwa kama sehemu ya mtaji na faida kwa kununua bidhaa na kuuza. Sasa walitarajia mfanyabiashara kama mimi nishindwe kutumia kiasi hicho nje ya nchi? Nanunua vitu kutoka Uingereza, China, Falme za Kiarabu (Dubai), Afrika Kusini, Italia na sehemu nyingine. Watu wa ajabu kweli hawa.

“Nasikitika jinsi wanavyoendelea kumchafua mzee wangu. Na ndio maana nimeelewa barua hiyo ya mwaka jana imeletwa leo wiki hii. Tayari nimewasiliana na mwanasheria wangu katika hili na nitatoa vielelezo vyote, hakuna cha kuficha…. Jamani siasa zao wazibakize huko, kazi waliyofanya kumchafua mzee wangu (Lowassa) hawajaridhika kweli? Katika hili nasema hapana.”

Habari hiyo ilifuatiwa na habari nyingine ambayo iliyomnukuu Lowassa mwenyewe akionyesha kwamba Lowassa anaandamwa na katika toleo hilo aligusia tena kuhusu mwanae Fredrick kuchukua hatua za kisheria kuhuhusiana na habari inayohusiana na usafirishaji fedha Uingereza. Habari hiyo imenukuliwa tena katika gazeti lingine jana.

Uongozi wa Raia Mwema tayari umeiandikia barua kampuni hiyo ya uchapaji ukilalamikia tukio hilo la kuzuia gazeti lisichapwe na kuharibu nakala ambazo tayari zilishachapwa, na pia kutoa usiku huo huo baadhi ya nakala za toleo hilo kwa watu wa nje bila idhini ya wamiliki wa gazeti. Pia unataka ulipwe fidia kwa hasara iliyopatikana kwani ililazimu gazeti kuchapwa kwingineko alfajiri, na hivyo kuchelewa kuingia sokoni.

Katika habari yake ya wiki iliyopita iliyoibua mambo yote hayo, Raia Mwema liliripoti kwamba Frederick Lowassa anachunguzwa na Kitengo Maalumu cha Polisi wa Kimataifa wa Uingereza wanaofuatilia utata wa uhamishaji fedha kutoka Tanzania.

Fedha hizo zinahusishwa na ununuzi wa nyumba yenye thamani ya pauni za Uingereza 475,000 (takriban Shilingi bilioni moja) katikati ya Jiji la London.

Hata hivyo, watu walio karibu na Frederick wameelezea kwamba kijana huyo hakuwahi kununua nyumba; bali aliwahi kutaka kupanga kwa ajili ya kuishi akiwa masomoni nchini Uingereza na fedha nyingine alizituma kwa ndugu yake aishie nchini humo.

Nyumba ambayo inatajwa katika maelezo ya awali iko mtaa wa Leinster Gardens, jijini London.

Hata hivyo, hakuna ofisa yeyote wa Serikali ya Tanzania aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo, pamoja na kuwapo taarifa kwamba tayari vyombo vya dola vya Tanzania vimekwisha kuhusishwa katika uchunguzi huo.

Maofisa wa Polisi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) wanaohusika na uchunguzi wa fedha haramu, wamekwepa kuzungumzia suala hilo na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, hakuweza kupatikana, na alielezwa kuwa nje ya nchi kikazi.

Ofisa wa CID aliyeelezwa kuongoza kitengo kinachochunguza makosa ya uhalifu wa fedha na nyaraka, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Samson Kasala, alikanusha kufahamu chochote kuhusiana na suala hilo, kabla ya kukata simu alipohojiwa na Raia Mwema kuhusu taarifa hizo.

Taarifa zinaeleza kwamba Kitengo cha Ufuatiliaji wa Fedha Haramu (Financial Intelligence Unit-FIU) kilichopo chini ya Wizara ya Fedha nchini, kilipokea taarifa kutoka Polisi wa Kimataifa wa London, Uingereza, wakitaka taarifa muhimu kuhusiana na Frederick, kabla ya kitengo hicho kuomba msaada wa polisi.

Hata hivyo, Kamishna wa FIU, Herman Kessy, hakutoa ushirikiano na Raia Mwema, kuhusiana na sakata hilo.

FIU imeanzishwa chini ya Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (Anti-Money Laundering Act-2006) kwa kuundiwa kanuni mwaka 2007, lakini hadi sasa kitengo hicho kimekuwa kikiendeshwa na maofisa watano tu, Kamishna Kessy, mchambuzi mmoja, mtaalamu wa mawasiliano na wasaidizi wawili wasio wataalamu, kitengo kilichopaswa kuendeshwa na watu wengi zaidi kutokana na unyeti wake.

Habari zinaeleza kwamba hata ofisa wa Polisi aliyewahi kuhamishiwa FIU kwa kazi maalumu alijikuta akitengwa na kutopangiwa kazi na maofisa hao ambao wengi wanatoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baada ya kuwa ‘wameaminiwa’ sana na uongozi wa juu wa serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo bado zinafanyiwa kazi, Frederick ambaye baba yake alijiuzulu Waziri Mkuu kwa kuhusishwa na kashfa ya ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyokabidhiwa kwa kampuni tata ya Richmond Development LLC, anadaiwa kufanya mawasiliano kupitia kampuni ya uwakala iliyotajwa kwa jina la ‘Mishcon’.

Nyaraka alizowasilisha, zilidai kuwapo ubia kati ya mtuhumiwa huyo na kampuni tatu ikiwamo Integrated Property Investment(T) Ltd na Barare Ltd Company.

Mkataba huo unaonyesha kuwa Frederick Lowassa ana hisa kwenye kampuni hizo, na kwamba fedha za ununuzi wa nyumba hizo zinatokana na fedha za malipo ya hisa anazopata kutokana na kampuni hizo.

Hata hivyo, mkataba huo unaonyesha kusainiwa Machi 25 mwaka 2009 siku moja baada ya Frederick Lowassa kusaini mkataba kati yake na kampuni ya Mishcon kama wakala wake katika ununuzi wa jengo hilo.

Pia aliwasilisha nyaraka zinazoihusisha kampuni ya Alphatel kama moja ya kampuni ambayo pia yeye ni mkurugenzi wake ambayo pia ni chanzo chake kingine cha fedha anazotumia kununua jengo hilo.

Taarifa zimedokeza kuwa ununuzi huo ulikwama baada ya kushindwa kutoa malipo hayo kwa mujibu wa mkataba kati yake na wakala wa ununuzi wa nyumba hiyo (kampuni ya Mishcon) ambao ulimtaka awe amekamilisha kulipa fedha hizo kabla ya Aprili 14, mwaka 2009.

Hata hivyo, siku chache baadaye ndani ya mwezi huo wa Aprili, Frederick aliipelekea Mishcon kiasi cha pauni za Uingereza 199,940 zikitokea kwenye kampuni ya ununuzi fedha ya Wall Street Exchange.

Aidha kiasi cha pauni 100,000 kiliingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo hiyo ya Mishcon kwa fedha taslimu katika mikupuo 12 tofauti zikitokea kwenye matawi tofauti ya benki ya NatWest Bank plc iliyoko Kaskazini mwa Jiji la London.

Raia Mwema limeelezwa kuwa mazingira ya kuingizwa fedha hizo kwenye akaunti ya wakala huyo ( Mishcon) ndiyo yameifanya Taasisi ya SCD 6 Economics and Specialist Proceeds of Corruption Unit ya Uingereza inayosimamia uchunguzi wa sakata hilo kuwa na mashaka makubwa kuhusu uhalali wa fedha hizo.

Kutokana na mazingira hayo, SCD 6 Economic and Specialist Crime Proceeds of Corruption Unit yenye ofisi zake Victoria Block, New Scotland Yard, London, ililazimika kuwasiliana na FIU ikitaka maelezo ya awali kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi kuhusu fedha hizo.

Raia Mwema iliwasiliana na Fred ambaye alikana kununua nyumba Uingereza lakini alikiri kuwahi kutuma fedha huko. Aliliambia Raia Mwema pia kwamba hajawahi kuhojiwa na yeyote kuhusu suala hilo, na pia kwamba hana taarifa kuwa polisi wa Uingereza wanampeleleza.

Hata hivyo kwa upande mwingine, gazeti hili limebaini kuwa, maelezo ya awali ambayo yalitakiwa kutoka Tanzania na makachero hao wa Uingereza, ni pamoja na kutaka kufahamu kama kweli Frederick Edward Lowassa amezaliwa Agosti 26, 1977, Mwanza Tanzania na anamiliki hati ya kusafiria yenye namba AB 109402 iliyotolewa Tanzania na kwamba anwani yake nchini Uingereza ni 71 Hendrix Drive, Milton Keynes, MK8 0DY.

Pia makachero hao waliitaka Serikali ya Tanzania kutoa ufafanuzi wakitaka kujua kama Frederick Lowassa ni mbia katika kampuni za Alphatel Partnership (Tanzania) Barare Ltd na Intergrated Tanzania Limited, kampuni ambazo zimefahamika kumilikiwa na familia ya Lowassa.

Asasi hiyo ya Uingereza pia imeomba kujua kama FIU wana taarifa zozote za uhalifu dhidi ya Frederick Lowassa na kama baba yake Edward Lowassa anachunguzwa kwa tuhuma yoyote ya rushwa na mamlaka za uchunguzi wa rushwa nchini Tanzania kuhusu fedha haramu.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na vyombo vya dola, ulielezwa na taarifa hizo kwamba Frederick Lowassa si mbia katika kampuni hizo na kwamba Barare Ltd wenye hisa ni Edward Ngoyai Lowassa mwenye hisa 500 na Regina Mumba Lowassa mwenye hisa 500 huku wakurugenzi wakiwa ni hao hao.

Ofisa wa Uingereza anayesimamia uchunguzi huo, George Simpson, ameliambia Raia Mwema kupitia barua pepe kwamba kanuni za uchunguzi kuhusiana na kesi zenye mguso wa kisiasa huwazuia kukanusha au kuthibitisha kuhusu uchunguzi unaoendelea hadi pale wanapofikia hatua ya kukamata mtuhumiwa ama anapofikishwa mahakamani.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata mwanzoni mwa wiki hii kutoka vyanzo vyake zinasema kwamba uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea, na kwamba watendaji wamepewa maelekezo ya kuendelea nao.

Thursday, December 2, 2010

Tohara ya ‘lazima’ kwa wanaume yaja

KUTOKANA na utafiti wa kisayansi kuonesha kuwa kutofanya tohara kwa wanaume ni moja ya sababu zinazochangia maambukizi ya Ukimwi, wanaume katika mikoa saba nchini wanatarajiwa kufanyiwa tohara kuanzia mwakani kwa sababu inayo idadi kubwa ya wanaume wasiotahiriwa.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema itaanza operesheni maalumu kwa kushirikiana na wadau wengine yakiwemo mashirika ya misaada kutoka Marekani, kufanya tohara kwa wanaume hao katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Kagera, Tabora, Shinyanga na Wilaya ya Rorya mkoani Mara.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Haji Mponda, jana mjini hapa, katika hotuba yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kumkaribisha Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Kitaifa mjini hapa.

Dk. Mponda alisema utafiti uliofanyika na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, imeonesha kuwa mikoa hiyo inaongoza kwa maambukizi na moja ya sababu ni kuwepo kwa idadi mkubwa ya wanaume wasiofanyiwa tohara.

“Mpango wa Wizara ni kutaka kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU na utafiti umeonesha mikoa hii ina idadi ndogo ya wanaume waliofanyiwa tohara, lakini ina viwango vya juu vya maambukizi,” alisema Waziri huyo.

Hivyo alisema mpango wa Wizara ambao tayari ulianza kwa majaribio katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Kagera, itaendelezwa zaidi katika mikoa iliyoainishwa kuanzia mwakani kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia mashirika yao ya misaada sambamba na marafiki wengine wa maendeleo.

Alisema mpango huo wa kuwafanyia tohara wanaume katika mikoa hiyo umelenga kuwafikia wanaume zaidi ya milioni 2.5 na wanaume wa mikoa hiyo wameonesha kufurahishwa na uamuzi huo wa kuwatahiri.

Katika takwimu zilizotolewa na TACAIDS ya viwango vya maambukizi ya VVU ya mwaka 2003/ 2004, Mkoa wa Iringa ulikuwa na maambukizi ya asilimia 13.4 ambapo kwa mwaka 2007/2008 maambukizi ni asilimia 15.7.

Mkoa wa Mara kwa miaka hiyo, maambukizi yalikuwa ni asilimia 3.5 na kuongezeka mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia 7.7 wakati Mkoa wa Shinyanga maambukizi yalikuwa ni asilimia 6.5 ambapo kwa mwaka 2007/2008 viwango vya maambukizi ni asilimia 7.4.

Naye Mwandishi Wetu, Flora Mwakasala anaripoti kuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chiku Galawa ametaka mabango yote ya waganga wa jadi yanayotangaza kuwepo kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume, yaondolewe kwa kuwa ni kichocheo cha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi yaliyofanyika jana kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Galawa alisema mabango hayo yamebandikwa mitaani kwa wingi.

“Huu ni utapeli mkubwa, nani kasema watu wanahitaji kuongezewa nguvu za kiume? Jambo hili ni sawa na kuwahamasisha watu waendelee kufanya uasherati na kuongeza maambukizi mapya ya VVU,” alisema.

Alisema kitendo cha watu kuongeza nguvu za kiume kinawashawishi kuendelea kufanya ngono, jambo linalosababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la maambukizi hasa kwa vijana ambao ni taifa la kesho.

“Tutashirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha mabango yote yaliyobandikwa mitaani na barabarani yanaondolewa,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Mafunzo Taifa wa Chama cha Waganga wa Tiba za Asili, Sadick Kalimaunga alisema kauli hiyo ya Galawa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, si sahihi kwa kuwa kazi yao ni kuwasaidia wanaume wenye matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume.

“Sisi hatuchochei maambukizi ya VVU kama wanavyodai bali tunawasaidia wanaume wenye matatizo hayo kudumisha ndoa zao kwa kuwaongezea nguvu za kiume ili waweze kufanya tendo hilo kikamilifu,” alisema.

Aidha, alisema kitendo cha Serikali kuondoa mabango hayo kitasababisha baadhi ya watu wanaohitaji tiba hizo ambazo zilikuwepo tangu enzi kukosa huduma na wengine ndoa zao kuvunjika.

Kwa mujibu wa takwimu, Dar es Salaam ni mkoa unaoshika nafasi ya pili nchini kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU cha asilimia 9.3. Iringa inaongozwa kwa kuwa na asilimia 15.7.

Wednesday, December 1, 2010

MAADHIMISHO YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


Watu mbalimbali waliofika kwenye maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia leo kwenye viwanja vya Mtandao wa Jinsia (TGNP) jijini leo.


Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Usu Mallya (Pili kushoto) akimkabidhi mlemavu wa viungo Maria Patrick baiskeli iliyotolewa na Mchungaji wa kanisa la Pentekoste Missionarieis, Gervas Masanja wakati wa maadhimisho ya siku ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya TGNP.



Mkurugenzi wa TGNP Usu Mallya akimkaribisha Mwenyekiti wa TGNP Mary Rusimbi pamoja na wageni waliohudhuria maadhimisho ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye viwanja vya TGNP

Prof.Tibaijuka aanza kwa kasi: Mliopora maeneo jisalimisheni

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amewataka wananchi waliopora viwanja na maeneo ya wazi nchini na kujenga, wajisalimishe kwa mazungumzo, kwa sababu huenda wakaokoa hata matofali kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.

Profesa Tibaijuka alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati ya wizara hiyo na kueleza kuwa masuala ya ardhi yasipofanyiwa kazi, sekta nyingine zitazorota.

“Umefika wakati sasa, tunataka kubadilisha mwonekano wa miji ... na kwa wanaosema wanatumia jeuri ya pesa, tutawashughulikia, lakini baada ya kufanya utafiti wa kutosha, kwa sababu hatuwezi kukurupuka, hivyo waliopora viwanja tunawataka wajisalimishe,” alisema Profesa Tibaijuka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Makazi (UN-Habitat).

Alisema, migogoro ya ardhi hawataimaliza bila wananchi kuwasaidia na kwa sasa, watarudisha askari wa ardhi ili kuhakikisha wanapunguza migogoro ikiwamo ya wanaojenga holela na katika maeneo ya wazi.

Tibaijuka alisema, kati ya hekta 900,000 ni asilimia mbili tu ya maeneo ndiyo yaliyopimwa, hivyo wizara yake itahakikisha inapimwa, ili miji iwe katika hali inayotakiwa kwa sababu kwa sasa hairidhishi.

Aidha, Profesa Tibaijuka alisema si maendeleo yote yanahitaji fedha, hivyo kwa muda huu waliopewa na Rais, kuna mambo ambayo watayafanyia kazi kwa haraka ikiwamo kuandika majina ya mitaa yote.

“Watu wengi hawatambui mitaa wanayoishi inaitwaje, kwa sababu wala haina majina na unakuta anashindwa kabisa kuelekeza, lakini tukiiandika tutawasaidia, hivyo tutafanya jambo hili kwa haraka maana haihitaji fedha,” alifafanua mbunge huyo wa Muleba Kusini.

Katika hatua nyingine, alisema kuna upungufu wa nyumba milioni tatu nchini, hivyo wanapaswa kujenga miji kwa kuboresha nyumba zilizopo na kuzijenga ambazo hazina viwango na kuziuza kwa wananchi.

“Wananchi wanatakiwa kutambua wanahitaji nyumba au ardhi, lakini watambue kama ni viwanja lazima waende nje ya mji, ila kama ni nyumba zipo ila zinahitaji maboresho na tutafanikiwa, kwa kuwa na benki za nyumba na mikopo ya nje, kwa sababu sekta binafsi pekee hazitaweza bila kuwa na fedha ... tuwaachie wahandisi wetu wajenge nyumba sisi tununue,” alisema.

Alisema, watafanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mazingira ili kuhakikisha miji inakuwa safi na salama; na kuboresha bonde la Mto Msimbazi, Dar es Salaam, ambalo limefanya hali ya hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa mbaya.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Patrick Rutabanzibwa, alikiri baadhi ya wafanyakazi wake kushiriki kugawa maeneo ya wazi na kueleza kuwa tayari ameanza kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwamo kufanya mabadiliko ya vitengo kwa nia ya kuboresha utendaji kazi.

“Uvamizi wa maeneo ni mtandao wa watu wa wizarani na manispaa nami nimejitolea kuwashughulikia na tayari kuna waliokuwa wamepora viwanja na nimewataka wavirudishe na wengine walipora na kuwauzia wafanyabiashara wakubwa,” alisema Rutabanzibwa.

Pia alisema wamesimamisha ujenzi wa eneo la wazi katika hoteli ya Palm Beach na kuahidi kufanya kazi bila kuhofia kashfa, kwani zipo tuhuma amevumishiwa na amezipeleka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Kwa upande wao, mawaziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mary Nagu (Uwekezaji na Uwezeshaji) na William Lukuvi (Sera, Uratibu na Bunge), waliripoti rasmi katika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuzungumza na wakuu wa idara, vitengo na taasisi chini ya Ofisi hiyo.

Mawaziri hao waliwataka watendaji kufanya kazi kwa ubunifu, ushirikiano, upendo, uwazi na bidii zaidi, ili kukidhi matarajio ya wananchi.

Nagu alisisitiza umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji bila ngojangoja ambayo ni chanzo cha kuwakatisha tamaa wawekezaji.

Alisema hakuna uchumi duniani uliofanya vizuri bila uwekezaji, iwe wa kutoka nje au ndani ya nchi husika. Alibainisha kuwa Watanzania ndio wanatakiwa kushika hatamu ya uchumi wao.

Lukuvi alisisitiza watendaji kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kuongeza ufanisi na hatimaye kufikia malengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taifa kwa jumla.

Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu aliwaambia watendaji wakuu wa wizara hiyo kuwa anawapa uhuru wa kufanya uamuzi wenye tija na ufanisi na atakayeshindwa atajiondoa mwenyewe.

Alizungumza na wakurugenzi wakuu wa idara za uchukuzi na wa taasisi mbalimbali akijitambulisha kwao rasmi na kuanza kazi.

Nundu aliwataka kufahamu dhima waliyonayo katika kuendeleza sekta ya uchukuzi ili katika kipindi cha miaka mitano ijayo, fursa zilizomo zitumike vyema pamoja na kuboresha huduma za usafiri.

Aliwataka kupeana ushauri ili wasonge mbele, kuwa wadilifu na waaminifu huku wakitoa huduma kwa dhati na kwa wakati muafaka.

“Hakikisheni mnawajibika kulingana na wakati, katika suala la uchukuzi hatupo peke yetu ulimwenguni, zingatieni matakwa ya wateja,” alisema Nundu na kuongeza:

“Fanyeni kazi kila mmoja kwa madaraka aliyonayo, toeni uamuzi wenye tija bila upendeleo na hata ubinafsi na hiyo iwe ahadi yenu kwetu,” alisema.

Alisema, anatarajia kuimarisha kampuni ya reli, kwa lengo la kuipa uwezo wa kutoa huduma bora kwa kusafirisha abiria na mizigo ya ndani na nchi jirani, na kuendelezwa kama mhimili wa mpango wa maendeleo wa eneo la ukanda wa kati.