WANAFUNZI 400 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) jana walipewa saa nne waondoke chuoni hapo kutokana na kukithiri kwa vurugu zilizokuwa wakizifanya.
Uamuzi wa uongozi kukifunga chuo hicho na kuamuru wanafunzi kuondoka eneo la chuo, utawafanya wanafunzi hao kukosa masomo kwa kipindi kisichojulikana kuanzia jana.
Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Idris Kikula, alisema jana kuwa, uamuzi wa kukifunga chuo hicho una lengo la kuepusha baadhi ya wanafunzi na majanga yanayoweza kujitokeza kutokana na baadhi yao kukaidi amri ya kusimamisha mgomo wao.
“Tumefunga chuo na tumewapa muda wa saa nne wawe wameondoka chuoni hapa kuanzia saa tatu asubuhi,” alisema Profesa Kikula.
Akifafanua juu ya uamuzi huo, Makamu Mkuu huyo wa Chuo, alisema wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu ambao wanachukua kozi ya Sayansi ya Jamii, waliitisha mgomo tangu Jumatatu kwa lengo la kuilazimisha Serikali kuwapa posho za mazoezi kwa vitendo.
“Uongozi wa Chuo umeshangazwa na hatua hii, kwani suala hilo lilishajadiliwa tangu Desemba mwaka jana na kupatiwa ufumbuzi kuwa Serikali itatoa posho hizo kwa muda muafaka na mimi niliongea nao wakakubali kuwa hakuna haja ya kufanya mgomo,” alisema.
Profesa Kikula alifafanua kuwa wanafunzi wanatakiwa waende kwenye mafunzo kwa vitendo katikati ya mwezi ujao, hivyo kwa sasa ni mapema kuilazimisha Serikali kuwapa posho hizo.
Alisema kutokana na uamuzi wa wanafunzi kuandamana kinyume cha sheria Jumatatu hadi kwenye majengo ya Bunge, baadhi yao walikamatwa na uongozi wa chuo ulikubaliana kuwapa barua za kuwasimamisha masomo wanafunzi 400 ambao walishiriki maandamano hayo.
“Habari za kusimamisha wanafunzi hao 400 zilisababisha taharuki miongoni mwa wenzao wakaanza kushambulia kwa mawe magari ya chuo na kuwapiga wanafunzi wengine ambao walionekana hawaungi mkono,” alisema.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alisema kuanzia leo, uongozi wa chuo utachapisha katika tovuti yake majina ya awamu ya kwanza ya ambao watatakiwa kurudi chuoni.
“Kuna wanafunzi wengi tumewasimamisha, lakini hawana hatia, na baadhi yao walisaini makubaliano kuwa hawatashiriki mgomo, lakini hatukuwa na namna zaidi ya kuwasimamisha wote kutokana na hali ilivyokuwa,” alisema.
Baadhi ya wanafunzi ambao walizungumza na gazeti hili muda mfupi kabla ya kuondoka chuoni hapo, walilaani uamuzi huo na kutaka uongozi uwarudishe haraka masomoni.
“Si haki kutoa adhabu hii kwa watu wote; viongozi wa mgomo wanajulikana, ni vyema uongozi wa chuo ungechukua hatua za kinidhamu dhidi yao,” alisema mwanafunzi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Wanafunzi hao walikuwa wakidai kuwa walipewa ahadi tangu Februari ya kulipwa posho hizo Juni 7, lakini haikutekelezwa.
Rais wa Wanafunzi wa Chuo cha Sanaa na Lugha, Mwakibinga Phillipo, alisema chuo hicho kimefungwa kutokana na wanafunzi wake kushiriki maandamano juzi wakishinikiza wanafunzi wenzao waliosimamishwa chuo kurudishwa bila masharti.
Philipo alisema, wanafunzi 374 wanasomea Uhusiano wa Kimataifa mwaka wa pili, na wengine 59 ni wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii na ndio walisimamishwa juzi na kusababisha wenzao kuandamana wakiwatetea.
Alisema, katika maandamano yao ya mwanzoni mwa wiki kupitia viwanja vya Nyerere hadi vya Bunge walikokutana na ulinzi mkali wa Polisi, wanafunzi 71 walikamatwa na na kuachiwa kwa dhamana iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo.
No comments:
Post a Comment