Thursday, July 24, 2008

ANA KWA ANA.

Utangulizi.
Blogi hii itakuwa na sehemu ya mohojiano ya ana kwa ana na wanaharakati mbalimbali ambao ni wanachama wa GDSS wakitueleza historia yao kwa ufupi, kazi wanazojishughulisha nazo, changamoto wanazikutana nazo, ushiriki wao wa GDSS, na faida walizozipata kutokana na ushiriki huo. Lengo la mahojiano haya ni kupata uzoefu kutoka kwa wanaharakati wengine na kujifunza kutokana na uzoefu huo
.

Wiki hii tulipata bahati ya kufanya mahojiano mafupi na Bw. Albert Killango –Afisa Mipango wa asasi ya Precious Jewels Organization (PJO Tanzania) yenye makazi yake Mabibo Dar es Salaam. Ambaye alieleza historia yake ya harakati iliyoanzia alipokuwa shuleni mwaka 1996/7, walipoanzisha kikundi cha vijana cha Barcelona Family kilichojihusisha na maswala ya Michezo na Burudani. Mwaka 1998 akakutana na mama Ichikaeli Maro ambaye alimtambulisha TGNP na hapo alianza rasmi safari yake ya harakati. Semina za kwanza kwanza anazozikumbuka ziliwezeshwa na Richard Mabala, dada Ussu Mallya, na zilikuwa zinahusu VVU na Vijana na Mafunzo ya Uongozi katika asasi na Vikundi unaozingatia usawa wa kijinsia. Mafunzo hayo yalimuwezesha yeye na
wanaharakati wengine kuunda kikundi cha kupambana na UKIMWI kilichoitwa Tumaini Youth Movement mwaka 1999. Tumaini iliweza kuandaa na kufanikisha programu kadhaa za UKIMWI ndani ya wilaya ya Kinondoni, mojawapo ni Cheza Salama na HIV iliyofadhiliwa na UNICEF, ambayo ilihusu kutoa elimu ya UKIMWI kwa njia ya Matamasha ya wazi ya Burudani.

Mwaka 2005 waliona kuna haja ya kupanua wigo wa utetezi wa haki za kijamii na kuboresha maisha ya walio pembezoni, hivyo wakaanzisha rasmi asasi ya Precious Jewels Organization (PJO Tz) kwa lengo la utetezi wa haki za wanajamii hasa walio pembezoni.

Kaka Killango anasema kwamba “kuna faida nyingi nilizozipata kutokana na ushiriki wangu wa GDSS”, alizitaja baadhi ni; kuweza kupata elimu na ujuzi mbalimbali kupitia mada, mijadala, na shughuli za GDSS. Mfano wa ujuzi ni uwezeshaji (facilitations skills), ushawishi na utetezi, uongozi wa asasi na vikundi, na elimu ya usawa wa kijinsia. Ujuzi huu umemwezesha kusaidia jamii iliyomzunguka katika kutafuta suluhisho la matatizo mbalimbali, kwa mfano mwaka 2004 walitetea kufunguliwa kwa maji katika mitaa ya Jitegemee, Kanuni na Azimio, baada ya viongozi wachache wa serikali za mitaa na wafanyabishara kuyafunga ili waweze kuuza maji yao ya kibiashara.

Pia ushiriki wake katika semina hizi umemsaidia kuweza kujiamini, kujenga hoja na kuitetea mbele za watu mbalimbali. Kusimama katika majukwaa tofauti na kuongea kumjengea imani ya kuamini kama naye pia anaweza, kitu ambacho kwa maneno yake mwenyewe anasema “mwanzoni hakikuwepo ndani yangu”

Tatu, kupata Mbinu tofauti za kupambana na Matatizo na Changamoto zinazotokea katika maeneo yake kwa kusikia ama kujifunza kutoka kwa wengine jinsi wanavyotatua matatizo yanayofanana na hayo yanayowakabili. Visa mkasa vinavyotokea katika maeneo mengine na kuwakilishwa na wanaharakati vinasaidia kupata mbinu za kutatua matatizo yanayotokea katika eneo lake.

Semina pia zimempa fursa ya kutandaa (Networking), kitu ambacho anasema kimempa faida kuu mbali. Kwanza kupata taarifa mbalimbali muhimu, na pili kuweza kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja na wadau na asasi zingine. Mfano kwa sasa yupo katika Mtandao wa kufuatilia utekelezwaji wa bajeti ya afya na Ukatili wa Kijinsia wilayani Kinondoni ambao unajumuisha asasi kumi na mbili. Pia Kutandaa kunamsaidia kupata taarifa za mafunzo yanayoandaliwa na taasisi nyingine na kushiriki katika mafunzo hayo na matukio mbalimbali ya kinaharakati –forums, matamasha, warsha, mikutano- ndani na nje ya nchi, kwa mfano Januari 2007 alipata bahati ya kuhudhuria tamasha la World Social Forum jijini Nairobi, Kenya.


Baadhi ya harakati anazozikumbuka alizowahi kushiriki kama mwana GDSS ni pamoja na; Mwaka 2006 walitoa msaada kwa binti wa miaka 17 aliyebakwa na mwanamume wa miaka 28, maeneo ya Mabibo MCA ambapo walishirikiana na wananchi kumkamata mbakaji na kumpeleka kituo cha Polisi na kuhakikisha mbakaji amepelekwa mahakamani na mwishoni alifungwa miaka 15.

Ushiriki wa Maandamano ya kumtetea Amina Lawal kuelekea ubalozi wa Nigeria mwaka 2002. Amina alituhumiwa kwa kujamiana nje ya ndoa na kuhukumiwa kifo kwa sharia za kiislamu, kitendo ambacho wanaharakati wote wa haki za binadamu duniani walijitokeza kumtetea, na hatimaye alisamehewa.

Ushiriki wa Maandamano ya kushinikiza mabadiliko ya Sera za IMF na WB dhidi ya Mataifa maskini mwaka 2003 maandamano ambayo yalifanywa kwa lengo la kushinikiza Mataifa ya magharibi kurekebisha sera zao juu ya masoko huria zinazokandamiza nchi maskini.

Kwa kuhitimisha anasema “ushiriki wa semina za kila jumatano unaweza kumbadilisha mtu na mahusiano yake na jamii na kuweza kuleta maendeleo kwa jamii nzima. Wakati umefika sasa kwa wanaharakati kusogeza mikutano kama hii katika maeneo yetu. Vikundi vinaweza kufanya kitu kama hiki katika maeneo yao wanayotoka na kuwezesha kuinua uwezo wa jamii katika utetezi wa rasilimali zao na hivyo kuboresha hali za kimaisha za wananchi. Waandaji kuwaalika wanasiasa wa nchi yetu kuja katika semina hizi na tuweze kuwafahamisha ama kuwaleza maswala tunayohisi kuwa ni ya msingi kwa mustakabali wa nchi na maendeleo ya watu wetu”

Aliwashukuru TGNP kwa kuanda programu hii, na akamalizia kwa kusema, “tunaweza mimi na wewe tukiungana pamoja, Aluta Continua”

Friday, July 18, 2008

Mrejesho wa Mada Juu ya Kilimo Cha Bio Fuel Tanzania.

Mada hii ilijadiliwa tarehe 16/07/2008 na iliweza kuibua changamoto nyingi ambazo zinahitajika kufanyiwa kazi. Mada iliwakilishwa na Mtendaji Mkuu wa HakiArdhi, Bw. Myenzi na Bw William Olenasha kutoka Shirika la Oxfarm. Wawakilishaji walitoa mada kulingana na utafiti uliofanywa na mashirika yao katika maeneo ambayo tayari makampuni yapatayo 37 yameonesha nia ya kutaka ardhi na baadhi yamekwishapata ardhi katika maeneo hayo. Maeneo ambayo wawekezaji wameonekana kuweka msisitizo ni pamoja na; Lindi, Mtwara, Morogoro, Iringa, Tanga, Kigoma, Rukwa na Mara. Hadi sasa makampuni 16 yameomba na kupewa ardhi inayofikia hekta 641, 170 na ekari 1150. Kwa wastani yapo maombi ya ardhi kuanzia ekari 30,000 hadi 2,000,000, na makampuni hayo yamewekeza wastani wa dola 60 million hadi 1.5 bilioni.

Baadhi ya faida ambazo zinasemekana zinaweza kutokana na uwekezaji huo wa kilimo cha mazao ya biofuel ni pamoja na; fursa za ajira, fursa za masoko kwa bidhaa na mazao, upatikanaji wa nishati vijijini na mijini, kukua kwa uchumi wa wananchi, kupungua kwa umasikini, na kupungua kwa wimbi la nguvu kazi kukimbilia mijini.

Wahusika wakubwa wa miradi hii ya bio-fuel ni makampuni kutoka nchi za Sweeden, Uholonzi, Ujerumani, Uingereza, Ubelgiji, Australia, na Afrika Kusini. Makampuni mengine yamefikia hatua ya kufika vijijini na kuwashawishi wananchi hadi kupata ardhi ni pamoja na; Biofuels la Uingereza, awali waliomba hekta 20,000 katika vijiji vya wilaya ya Kisarawe na hadi mwisho wakapewa hekta 9,000. Kwa wilaya ya Bagamoyo wapo SEKAB kutoka Sweeden, wao walihitaji hekta 500,000 mpaka mwisho walipewa hekta 50,000 na mchakato wa kutafuta ardhi zaidi bado unaendelea.

Nchi kama Brazil ambayo inayotolewa mfano kama nchi iliyofaidika na kilimo cha bio-fuel, inatumia zaidi ya 85% ya ethanol yote inayozalishwa nchini humo. Sekta hiyo inaajiri kati ya watu laki saba hadi milioni moja, wengi wao ni vibarua tu na ujira wao ni mdogo sana na katika mazingira magumu ya kazi. Idadi ya ajira hizo imekuwa ikishuka kila siku kutokana na uvunaji wa kutumia mashine. Tayari mashine imeshachukua 40% ya nafasi za ajira na mwaka 2010 itachukua 70% na kuna sheria kuwa ifikapo 2017 uvunaji utakuwa kwa mashine tu. Swali la kujiuliza vipi hapa kwetu Tanzania?

Mapungufu Makubwa katika uwekezaji wa kilimo hiki cha bio-fuel hapa Tanzania ni pamoja na;
• Hakuna sera hadi sasa wala sheria au kanuni juu ya kilimo cha bio-fuel.
• NBTF ndio imeundwa tangu 2006 iko katika mchakato wa kutengeneza mwongozo (Guidelines) ambazo hazielewiki zitakuwa na hadhi gani, ya sheria au la?
• Wawekezji wanakwenda moja kwa moja kwa wanakijiji wasio na uelewa wa maswala ya ardhi hivyo uwezekano wa kuwarubuni ni mkubwa
• Uelewa wa jamii juu ya maswala haya bado uko chini kwani wengi wanavutwa na ahadi za haraka bila kujali athari za muda mrefu.

Athari tarajiwa kutokana na uwekezaji huu ni pamoja na;
• Uhaba wa ardhi ya kilimo kwa mazao ya kilimo.
• Bei za vyakula kuendelea kupanda zaidi.
• Kuendelea kwa hali duni ya tabaka la wanyonge hasa wanawake wa vijijini kwa sababu wao ndio wazalishaji wakubwa wa chakula cha familia.

Wanaharakati walipendekeza yafuatayo yafanyike:
• Zoezi zima la wawekezaji kuwinda ardhi vijijini lisitishwe hadi sera na sheria zitakapotungwa na kujadiliwa na wananchi kwa mapana wakizingatia tija na athari za bio-fuel.
• Elimu itolewe zaidi kwa umma juu ya bio-fuel.
• Wananchi wakatae kuondolewa kwa nguvu katika maeneo yao bila mjadala mrefu juu ya fidia kwa viwango vya soko badala ya kupangiwa viwango na mwekezaji.
• Uwekezaji mkubwa uelekezwe katika nishati mbadala zinazotokana na jua, upepo, na maporomoko ya maji.

Muda wa kushauriana sana umekwisha juu ya swala hili, wanaharakati wanapaswa kuchua hatua za haraka kuzuia uporaji huu wa ardhi ya Watanzania kwa kivuli cha uwekezaji. Nani yupo tayari kuwa mstari wa mbele kutetea ardhi ya Watanzania?

Tuesday, July 15, 2008

Kauli ya FemAct juu ya kifo cha mama mjamzito Mwananyamala Hospitali

15/07/2008


Tumepokea na kufuatilia mkanganyiko wa sababu za kifo cha mama mjamzito (Teddy Dimoso) na kichanga wake wakati wa kujifungua kwa masikitiko makubwa sana. Kwa mujibu wa barua kutoka kwa msimamizi wa mirathi kifo hiki kilitokea tarehe 01/06/2008 katika hospitali ya Mwananyamala. Barua hiyo ya tarehe 06/06/2008 kwenda kwa Waziri wa Afya inatoa maelezo kwa kina jinsi kifo hicho kinavyoweza kuwa kimetokea kwa uzembe.

Vyombo vya habari viliripoti kuhusu utawala wa Hospitali ya Mwananyamala na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam walivyokuwa wakitoa majibu yasiyoridhisha na yanayojikanganya juu ya kifo hicho. Mbali na Wanaharakati kudai iundwe tume huru kuchunguza mazingira ya kifo hicho na kutoa usahihi wa yaliyojiri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliamua kuunda tume bubu tarehe 18/06/2008.

Kwa mtazamo wetu tume hii ilikuwa na mapungufu yafuatayo; Wajumbe wake hawakujulikana hadi tarehe 11/07/2008 Kandoro alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ripoti yao. Wananchi hawakutangaziwa hadidu rejea za tume hii. Wananchi hawakutangaziwa tume itafanya kazi kwa muda gain na katika ofisi gani ili walio na maoni au ushahidi wapate kupeleka. Wajumbe wa tume hii wote ni watendaji wa serikali, hivyo kulikuwepo mgongano wa maslahi. Tume imetoa maelezo yale yale ambayo Mkuu wa Mkoa alikuwa akitoa kila siku, hivyo kutia shaka kama watu wote waliohusika na kushuhudia tatizo hilo wanafikiri kama Kandoro. Huu ni ushahidi wa usanii wa Kisiasa uliotukuzwa.

Kwa mujibu wa nakala ya taarifa kwa vyombo vya habari tarehe 11/07/2008 toka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado usahihi wa sababu za kifo cha marehemu Tedy Dimoso haujapatikana. Kwenye taarifa hiyo hakuna kabisa maelezo kutoka kwa ndugu wa marehemu na wala Mkuu wa Mkoa haonekani kuguswa na kifo hicho. Mkuu wa Mkoa pia hajawahi kuwasiliana na ndugu wa marehemu tangu kifo hicho kitokee.

Mkanganyiko wa maelezo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na hospitali ya Mwananyamala na namna jambo lenyewe lilivyoshuhulikiwa inatia mashaka makubwa. Femact bado tuanadai usahihi wa kilichotokea na kutaka haki itendeke pande zote mbili; upande wa marehemu na upande wa hospitali. Sisi tunadai masuala mahsusi kabisa siyo kinyume na majibu haya ya kisiasa.

Tunahitaji Mkuu wa Mkoa atoe ufafanuzi wa haya yafuatayo;
• Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hospitali ya Mwananyamala ilipangiwa pesa za dawa peke yake shilingi 174,502,463 katika mwaka wa fedha 2007/08. Ni kiasi gain cha pesa hizi zilitumika? Kwa nini Tedy Dimoso alifariki kwa kukosa dawa?
• Kwa mujibu wa Mpango wa Utoaji huduma za Afya (CCHP) wa Manispaa ya Kinondoni mwaka wa fedha 2007/08, Hospitali ya Mwananyamala ilipanga kutumia shilingi 22,000,000 kugharamia dawa na vifaa vingine kwa kitengo cha Uzazi hospitalini Mwananyamala. Ni kiasi gani cha pesa hizi zilitumika mwaka wa fedha 2007/08?
• Pia Hospitali ya Mwananyamala ilitengewa shilingi 210,000,000 kujenga jengo la ghorofa moja kwa ajili huduma za mama na mototo katika hospitali ya Mwananyamala. Ujenzi wa jengo hili umefikia wapi? Kwa nini Tedy Dimoso alifanyiwa upasuaji wodini?
• Kwa mujibu wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Sera ya Wananchi Kuchangia Gharama za Huduma za Afya katika Hospitali ya mwaka 1994, mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanastahili kupata huduma za afya bure bila malipo. Kwa nini ndugu wa marehemu Tedy dimoso waliambiwa wakanunue dawa?
• Kwa mujibu wa kifungu namba 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 toleo la 2005, kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake. Kwa nini serikali haikutimiza wajibu wake wa kutunza na kuhakikisha uhai wa Tedy Dimoso?

Tunahitaji kuona Mkuu wa Mkoa anafanya yafuatayo;
• Anatupilia mbali ripoti ya tume yake bubu na kuunda tume huru kuchunguza matatizo na vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5 katika Jiji la Dar es Salaam. Mama wote waliojifungua tangu January 2007 (au ndugu wa marehemu) ni vizuri wakahusika kuhojiwa.
• Mkuu wa Mkoa anaomba radhi kwa wananchi wa Manispaa ya Kinondoni kwa dharau aliyoonesha wananchi wanaolijua tatizo hili kwa kina pamoja na ndugu wa marehemu
• Mbunge wa Kinondoni anaomba radhi wapiga kura wake kwa kutoa kauli potofu Bungeni kuhusu tatizo hili.
• Mkuu wa Mkoa anawajibisha wote watakaobainika kuhusika na uzembe huo
• Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Kinondoni hawatumii vitisho na propaganda kutisha wananchi wanaojaribu kutetea haki na uhai wa wananchi
• Nakala za mpango kazi na bajeti ya utoaji huduma kwa kila Hospitali, Kituo cha Afya, na Zahanati zibandikwe sehemu ya wazi wananchi na wahudumu wa afya wafuatilie.

Imetolewa na Wanaharakati wa mtandao wa haki za binadamu na jinsia (FEMACT) na Kusainiwa naMs. Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
Kwa niaba ya FEMACT

Mrejesho wa Mada Juu ya Vurugu za Zimbabwe na Mustakabali Wake.

Mada hii iliwakilihwa na Carol Thompson jumatano tarehe 09/07/2008 na iliweza kuibua mjadala mkali kutoka kwa wana-GDSS. Mwezeshaji aliweza kutoa historia ya Vurugu zinazoendelea sasa na alizihusisha na vyanzo vikuu vitatu, ambavyo ni Mgogoro wa Kiuchumi, Kikatiba na Kiuongozi. Mgogoro kiuchumi ulianza kabla ya vurugu zinazoendelea sasa baada ya rais Robert Mugabe kufanya marekebisho ya sera ya ardhi mwaka 2000, ambayo yaliwapa Wazimbabwe weusi haki ya kumiliki ardhi iliyochukuliwa zamani kwa mabavu na wazungu. Mabadiliko hayo yalisababisha mataifa tajiri yakiongozwa na Marekani na Uingereza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi serikali ya Zimbabwe, na hapo mgogoro wa kiuchumi ukaanza. Huduma muhimu zikakosekana kabisa, afya, elimu, chakula, na mfumuko wa bei uliovunja rekodi ya dunia na kufikia 1000% kwa siku. Wazimbabwe zaidi ya milioni 3 wameshakimbia nchi yao kutokana na njaa na uoga walionao juu ya mstakabali wa maisha yao mpaka sasa, wanawake na watoto wakiwa ni kundi liloathirika zaidi katika dhahama hii.

Mgogoro wa kikatiba ambao nao umechangia vurugu zinazoendela ulianza baada ya Marekebisho ya kitiba ya Zim yaliyofanywa na serikali ya Mugabe mwaka 2002. Marekebisho hayo yalimpa rais mamlaka makubwa na kumfanya awe juu ya sheria na mwenye madaraka yote ya nchi, hata bunge la nchi halina uwezo wowote juu ya rais. Marekebisho haya ya katiba yamesababisha kusiwepo na mfumo mzuri wa uchaguzi huru na wa haki kitu ambacho kimechangia kuwepo kwa machafuko ya kisiasa.

Mgogoro wa kiungozi umechangia pia kuwepo kwa machafuko yanayoendelea hivi sasa. Kutoelewana kati ya viongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Bw. Morgan Tshangirai na Bw Mutambara kumechangia kukua kwa mgogoro huu. Tshangirai anamtuhumu Mtambara kwa kufanya majadiliano na Mugabe juu ya kuunda kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kitu ambacho kwa mujibu wa Tshingirai ni usaliti kwa Wazimbabwe. Pia kuna swala la mkanganyiko kuhusu uwakilishi wa chama cha MDC, kwa upande mmoja kinaonekana kama kinawakilisha wafanyakazi na kwa upande mwengine kinawakilisha mabepari, kitu ambacho kinazua hofu miongoni mwa wafuasi na wasio wafuasi wa chama hiko.

Uchaguzi wa tarehe 27 June, 08 uliendeleza tuu vurugu ambazo zilishaanza kuota mizizi tangu awali. Viongozi wa Umoja wa Africa na SADC walikubaliana kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki, na ulikuwa na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu. Lakini mpaka sasa viongozi wa Afrika wamegawanyika katika makundi mawili juu ya mgogoro huo, la kwanza ni lile linakubaliana na uumuzi wa serikali ya Mugabe na la pili ni lile linalomuona Mugabe ni chanzo cha matatizo yote yanayotokea Zimbabwe. Vurugu zinazoendelea zitaweza kukwamisha mazungumzo yanayoendelea katika kujaribu kuleta serikali ya umoja wa Kitaifa, na pia uchumi wa nchi kuanguka kabisa kitu ambacho kitaongeza machungu kwa wananchi maskini hasa wale wa vijijini.

Michango ya wana-GDSS iligawanyika katika makundi mawili, wapo waliomtetea Mugabe na sera zake na wapo waliomuona kama ni chanzo cha matatizo yote haya na ilipaswa awajibishwe kwa maslahi ya wananchi wa Zimbabwe. Makundi yote yanaweza kuwa hoja za kushawishi, lakini kinachotokea Zimbabwe sasa yapaswa kiunganishwe na chanzo chake halisia; kipindi cha awali wakati wa uvamizi wa mabepari wa kiingereza walipochukua kwa mabavu ardhi ya waafrika na kujimilikisha. Uhuru wa Mwaka 1980 uligusia kurudisha ardhi hiyo kwa Waafrika pindi hali ya kisiasa itakapotengemaa, kitu ambacho hakikutekelezwa mpaka Mugabe akaamua kuwafukuza wazungu kwa nguvu. Mapambano yanayoendelea sasa Zimbabwe ni muendelezo wa Waafrika katika kupinga uvamizi wa mataifa ya kibepari-ubeberu katika rasilimali za Afrika. Wana-GDSS wakajiuliza migogoro mingapi ambayo itatokea katika nchi za Afrika endapo Waafrika wataamua kuungana na kudai rasilimali zao zilizo na zinaporwa na mataifa ya Kibepari-ubeberu katika siku zijazo?

Friday, July 4, 2008

TANGAZO LA SEMINA ZA KILA JUMATANO

SEMINA ZA JINSIA NA MAENDELEO
KILA JUMATANO

9th July, 2008

3:00p.m. - 5:00p.m

MADA: Mgogoro wa Zimbabwe na Hatima Yake

Mwakilishi: Carol Thompson:

Wasifu: Alifundisha UDSM, 1977-79.
Aliishi Zimbabwe, Wakati akifanya kazi katika shirika la SADC kwa Miaka 10 tangu Mwaka 1984 (Miaka 23 iliyopita).

Mchepuo: Professor, Political Economy, Northern Arizona University, USA.

MAHALI: TGNP/GENDER RESOURCE CENTRE, MABIBO ROAD – ADJ. NIT, DSM

KARIBUNI WOTE!!!

Thursday, July 3, 2008

Mfululizo wa Semina za Jinsia na Maendeleo

Wiki ya tarehe 02/07/2008 katika mfululizo wa semina za GDSS mada ilikuwa ni juu ya Kampeni ya “Tunaweza” kuzuia ukatili dhidi ya wanawake “We Can Campaign on Violence Against Women - VAW” iliyowakilishwa na dada Rennie V. Gondwe na Prisca Kadege kutoka Wizara ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake na Watoto.

Chimbuka la Kampeni hii ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake ni makubaliano yaliyopo katika kifungu cha utekelezaji cha 113 cha Mkutano Mkuu wa wanawake uliofanyka Beijing China mwaka 1999. Mkutano huu uliazimia kukomesha unyanyasaji dhidi ya wanawake kutokana na ripoti kuonyesha unyanyasaji dhidi ya wanawake ni moja kati ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu duniani. Tafiti inaonyesha, mmoja kati ya wanawake watatu hunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine katika kipindi cha maisha yao.
Rejea; http://www.unifem.org/gender_issues/violence_against_women/

Mwaka huu baraza la umoja wa mataifa, liliridhia mapendekezo ya kukomesha unyanyasaji wa wanawake na kuanzishwa kwa kampeni ya kuzuia ukatili dhidi ya wanawake duniani kote. Nchini Tanzania Kampeni hii ilizinduliwa rasmi kitaifa na Mh. rais J. M Kikwete May 24, 2008.

Mtoa mada alieleza maana ya Ukatili dhidi ya wanawake “VAW” kulingana na tafsiri ya kifungu cha 113 cha ulingo wa Beijing kinachosema kuwa ni “aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia unaosababisha au utakaoleta madhara ya kimwili, kiakili, au kimapenzi, au utakaoleta madhara yoyote kwa mwanamke, pamoja na vitisho vya aina hiyo, kwa nguvu ama kwa vitendo vya ujeuri dhidi ya uhuru wa mwanamke katika hadhara ama faragha” (tafsiri isiyo rasmi) Kampeni ya tunaweza ina awamu kuu tatu ambazo ni; Kuhamasisha umma juu ya uelewa wa unyanyasaji wa wanawake, ujenzi wa mitandao ya kupambana na unyanyasaji kitaifa, na uchukuaji wa hatua za kukomesha unyanyasaji huo. Kampeni hii ina lengo la kufikisha watu milioni kumi na sita watakaosimama na kupinga unyanyasaji wa wanawake ifikapo mwaka 2012.


Wachangiaji waliweza kubainisha Changamoto mbalimbali katika kufika malengo ya kampeni hii ambazo ni pamoja na;

Changamoto ya mila na desturi za baadhi ya makabila hapa nchini zinazoendeleza unyanyasaji wa wanawake kwa makusudi ama bila kukusudia- kwa mfano mila za ukeketaji, kurithisha wanawake, kupiga wanawake n.k. Pili ni Upatikanaji wa taarifa za ukatili dhidi ya wanawake- wengi wa wahanga hawaripoti vitendo vya ukatili wanavyotendewa na waume zao ama watu wengine, pia mara nyingi kesi zilizoripotiwa polisi hufutwa ama kumalizwa nje ya vyombo vya sheria kwa wahanga kuwasamehe watuhumiwa. Tatu, uelewa mdogo wa jamii juu ya kupambana na ukatili dhidi ya wanawake, kitu ambacho kinashawishi kuwepo na mpango maalumu wa kuielimisha zaidi jamii yetu. Hali ya kiuchumi pia imeelezwa kuwa ni changamoto mojawapo inayowasababisha wanawake wengi kunyanyasika na kushindwa kujitetea dhidi ya manyanyaso hayo. Hivyo kampeni hii itafanikiwa vizuri zaidi endapo kutakuwepo na mkakati wa kuwawezesha wanawake kiuchumi ili kuweza kujitegemea katika maamuzi mbalimbali juu ya maisha yao.

Mapendekezo yaliyofikiwa na Wanasemina ni;

1. Kutangaza kampeni hii katika vyombo vya habari- Tv, redio, magazeti na blogu, na tovuti mbalimbali ili wananchi wengi zaidi waweze kujiunga nayo na hivyo kufanikisha malengo yake.
2. Kuwe na mpango maalumu wa kuwawezesha wanawake kujitegemea kiuchumi.
3. Polisi walielimishwe na kuacha kumaliza kesi za unyanyasaji wa wanawake vituoni na kuendelea kulea tabia hii. Pia kuwepo na mtu maalumu anayehusika na maswala yote ya jinsia “Gender Focal Person” katika vituo vya polisi atakayehusika na kesi na maswala yote yanayohusiana na unyanyasaji wa wanawake.
4. Majaji wapatiwe mafunzo ya jinsia ya awali yaweze kuwasaidia katika kazi zao.
Mshiriki akichangia hoja.