Wednesday, June 8, 2011

Ikulu yawajibu Maaskofu, yaponda tamko lao

IKULU imemtaka yeyote anayejishuku au kushukiwa kujihusisha na dawa za kulevya, wakiwamo viongozi wa dini, wajisalimishe au wafichuliwe ili wachunguzwe na hatimaye sheria ifuate mkondo.

Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kwa vyombo vya habari, ilisema si vema mtu au watu hao wakasubiri kutajwa na Rais ndipo hatua zianze kuchukuliwa.

Taarifa hiyo ililenga kujibu mwito wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kumpa Rais Jakaya Kikwete saa 48 kutaja kwa majina viongozi wa dini wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.

Ilisema kauli ya maaskofu hao ni ya kusikitisha na ambayo haikutarajiwa kutoka kwa viongozi hao wa dini, kwani ni watu wa kutumainiwa sana katika jamii yeyote, huku “ikizingatiwa kuwa wao si malaika au watakatifu, kwani nao wanatumbukia katika majaribu na kujikuta katika vitendo au hali isiyotarajiwa kabisa”.

Maaskofu hao kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanatazamiwa waweke mikakati na vipaumbele vya kufanyia kazi changamoto hiyo na si kuahirisha tatizo ambalo linazidi kukua.

Ilisema hivi karibuni kuna viongozi wa dini walikamatwa kwa rushwa, ngono na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na maadili yasiyotarajiwa na jamii kwa ujumla.

“Wapo ambao wamekamatwa na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria, wapo wanaochunguzwa, tumeshawashuhudia na bado wataendelea kushuhudiwa. Hili si jambo dogo la kujitetea kwa kauli nyepesi kutoka kwa watu wanaotegemewa na jamii kwa kumpa Rais saa 48.

“Kazi hii ya kupambana na dawa za kulevya haimhusu Rais peke yake inamhusu kila Mtanzania, popote alipo katika nafasi yake na viongozi wa dini wana nafasi kubwa kwa sababu wanasikilizwa, wanatoa ushauri na wanatarajiwa kuwa na maelekezo yanayompendeza Mungu,” ilisema taarifa hiyo.

Katika hotuba yake kwenye sikukuu ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Mhashamu Askofu John Ndimbo kuwa Askofu wa Jimbo la Mbinga, Jumapili, Rais Kikwete alitoa ombi ambalo alishalitoa katika hafla zingine pia zilizohusisha viongozi wa dini, akiwataka viongozi hao kushiriki kikamilifu kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema tatizo hilo linalozidi kukua pamoja na jitihada za Serikali kupitia vyombo vya usalama kuwabana, kuwawajibisha watumiaji na wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

“Niruhusuni niseme tu, kwamba tusipofanikiwa kulidhibiti tatizo hili, hasara yake ni kubwa mno. Watoto wetu wengi wataharibika, uhalifu, hasa wa wizi na mauaji utaongezeka. Taifa litaharibikiwa,” alisema Rais na kuendelea :

“Siku hizi kila siku kuna watu wanaokamatwa kwa kujihusisha na dawa za kulevya. Inaashiria kuimarika kwa vyombo vyetu vya usalama, Lakini inasikitisha kuona kuwa biashara hiyo sasa inavutia hata watumishi wa Mungu. Huku sasa tunakoelekea kwa kweli ni kubaya sana.

“Nawaomba mtoe uzito unaostahili kwa tatizo hili. Viongozi wa dini mnasikilizwa, nawaomba kemeeni, onyeni na elimisheni jamii juu ya madhara ya dawa za kulevya, waelimisheni vijana ambao ndio walengwa wakuu, waepuke na waache kujihusisha na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.”

Kwa mujibu wa maelezo ya taarifa hiyo, kauli hii ya Rais ilitarajiwa ipokewe na viongozi wa dini kama ishara na kuifanyia kazi.

“Mtu akikuonya kuwa nyumbani kwako kumeonekana nyoka, huanzi kwa kuuliza kama ni kweli na ni wa rangi gani? Unatakiwa kushituka na kujiandaa kumsaka kwa nia ya kumwondosha nyumbani kwako hata ikibidi umwue ili asije akaleta madhara makubwa kwako na kwa familia yako.

Rais ana nia njema sana katika kulielezea jambo hili na mwenye nia njema haumbuki,” ilisema taarifa hiyo.

Akitoa maazimio ya Mkutano wa 45 wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo juzi, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk. Valentino Mokiwa, alisema kauli ya Rais imesikitisha kwa kuhusisha viongozi wote wa dini jambo ambalo alisema si zuri kwa jamii.

Alikaririwa akisema kama zitapita saa 48 kabla ya Rais kutaja majina ya wahusika wa mihadarati miongoni mwa viongozi hao wa dini, itakuwa ni aibu. Saa hizo zinatarajiwa kumalizika leo.

No comments: