TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wasichana 40 wa Tanzania kwenda Swaziland kujifunza Reed Dance!!
Huu utamaduni ni kwa faida ya nani?
Sisi Muungano wa Asasi za Kiraia zipatazo 50 zinazotetea Usawa wa Jinsia, Haki za Binadamu, Maendeleo na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct) hapa nchini,tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa zilizoandikwa kwenye gazeti la Daily News la tarehe 11 June 2011 , kwamba Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia mkataba wa makubaliano na Mfalme Mswati 111, wa Swaziland unaohusu wasichana 40 toka Tanzania kwenda Swaziland mwezi Oktoba mwaka huu 2011, kwa ajili ya kujifunza na kusherehekea ‘reed dance’(utamaduni wa Waswaziland ambao unaruhusu wasichana waliyo bikira kucheza dansi hii ya jadi mbele ya mfalme, malikia na viongozi wengine wakiwa nusu uchi. Kila mwaka takribani wasichana 40,000 wa Swaziland husherekea siku hii, ambayo hapo awali ilikuwa ni njia moja ya kumuezi Malkia wa nchi hiyo. Baadaye dansi hii imekuwa ikitumiwa na mfalme kuchagua mke kutoka kwa mabinti hawa ambao kwa hali ya kawaida sheria zetu hapa Tanzania zingalikataza kwani ni ukiukwaji wa haki za watoto wa kike.
Vile vile, dansi hii imekuwa ni kivutio cha watalii nchini Swaziland, hivyo wasichana katika nchi hiyo ya Swaziland wamekuwa wakitumiwa kama kitega uchumi. Wale wanaounga mkono dansi hii wanadai kwamba inajenga utamaduni wa kuthibiti wasichana wasijiingize katika masuala ya ngono kabla ya umri wao. Lakini cha kushangaza ni kwamba Mfalme wa Swaziland amekuwa akitumia nafasi hii kama njia rasmi ya kuchagua mke kutoka kwenye kundi hili la Mabinti wenye umri mdogo wa Kiswazi. Hii inamaanisha kwamba Mfalme hakutaka kuchagua mwanamke wa kuoa ambaye ameshafanya mapenzi na mwanaume mwingine. Mfalme huyu ana wake takribani kumi na moja na watoto ishirini na tatu.
Sisi wanaharakati wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi tumesikitishwa na taarifa hizi zilizochapishwa na gazeti la Serikali “ Daily News” katika makala maalum iliyosomeka” When Tanzania Deserve not the Best” ambapo mwandishi amedai kwamba Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wamekubaliana na Mfalme Mswati 111 kwa kile alichokiita “ Ridance Diplomacy” kwamba wasichana 40 wataenda huko Swaziland kujifunza hii dansi!!! Tunajiliuliza huu utamaduni ni wa nani? Kwa manufaa ya nani? Ni watoto wa nani watakaoenda kujifunza hii dansi na kwa madhumuni gani?.
Huko Swaziland wasichana bikira wakiwa nusu uchi hucheza mbele ya Mfalme na Malkia, na umati wa watu. Kwa nini miili ya wasichana itumike kuwavutia watalii? Kwa nini watanzania tukubali kuiga mambo ya kikoloni ya kuuza watu ili kupata fedha? Je kwa kuingia mkataba na Swaziland tunawatayarisha watoto wetu ili waweze kuwachezea “ wafalme wetu na malkia wao?” Je tunataka kujitayarisha kuuza miili ya watoto wetu wa kike ili wavutie watalii kwa madhumuni ya kitega uchumi wa taifa hili? Je ni watoto kutoka familia zipi watakaotumika?
Ndugu zetu Watanzania, katika karne hii, viongozi wetu wanataka kuwatumia watoto wetu wa kike kama viburudisho na kama vitega uchumi? Hili linaashiria taifa kuelekea kubaya na huenda katika kundi hili wafalme wetu wakapata fursa ya kuchagua wake, vimada, au nyumba ndogo. Wakati “ watalii” wakiweza kupata windo lao kwa njia rahisi kwa ajili ya biashara ya ngono. Matukio kama haya yanafanyika katika nchi nyingi. Kwa mfano Waarabu matajiri huenda India katika familia maskini kununua mabinti wazuri kwa ajili ya kuwatumia kama watumwa wa ngono” Sexual slaves” Je, hiki ndicho tunachotaka kifanyike kwa watoto wetu wa Tanzania katika miaka ijayo?
Tunamtaka Rais wetu Jakaya Kikwete atumie busara katika hili, kama kuna fedha za kudhamini basi fungu hulo litumike kusomesha watoto wanatoka kwenye familia zilizoko pembezoni. Rais asitumie fedha za walipa kodi kuwapeleka wasichana wadogo katika matayarisho ya kuja kutumiwa kama vyombo vya burudani. Huu ni utumwa wa kisasa (modern slavery) na haikubaliki.
Tunataka mkataba uvunjwe mara moja na asitokee binti wa Kitanzania kwenda kufundishwa hiyo ngoma ya unyanyasaji huko Swaziland.Wakati tulio nao sasa mabinti wanatakiwa wapewe elimu ya kuwawezesha kukuza vipaji vyao vitakavyowawezesha kujiendeleza kama binadamu si kujifunza ngoma za tamaduni za watu ambazo hata kwa wao wenyewe hazina tija. Hii ni fedheha wakati huu tunapojaribu kukuza heshima na utu wa watoto wa Afrika na husasani watoto wa kike.
Wanaharakati wa Swaziland, wanapambana na hii mila potofu, yenye kuwadhalilisha watoto wa kike na kuwanyima haki zao za msingi hususani haki za kuendelea na masomo. Sisi wapenda na watetezi wa haki za wanawake na watoto hapa Tanzania, tunapinga vikali kitendo hiki kinachoashiria kuwadhalilisha watoto wetu wa kike, na kutuvunjia heshima wanawake wa Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla.
Tunawaomba Watanzania wote tuungane kupinga vikali hatua ya kuingiwa kwa mkataba wa kuwapeleka wasichana 40 kwenda Swaziland kujifunza ngoma ya Reed dance kwa sababu ni udhalilishaji wa watoto wa kike na ni sawa na taifa kuingia katika biashara ya utumwa wa kisasa.
Imetolewa na:
Usu Mallya
Kny. Sekretarieti ya FemAct
No comments:
Post a Comment