KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amesema hana ugomvi na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, isipokuwa kilichopo ni utekelezaji wa uamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM yaliyotolewa Aprili.
Amesema kikao hicho kilichokuwa cha chama kujitathmini,kilipitia maazimio mbalimbali likiwamo la kuwataka wanaotuhumiwa kwa ufisadi wapime na kujiondoa katika uongozi wa ngazi za vikao vya uamuzi.
Nape amesema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari wa Kampuni ya Global Publishers Limited, Mohammed Kuyunga aliyetaka kufahamu ikiwa hatua za kushughulikia watuhumiwa wa ufisadi ndani ya CCM si mapambano binafsi kati ya Nape na watuhumiwa hao.
“Mheshimiwa, wewe umekuwa kinara wa kutangaza mapambano ya kuwang'oa ndani ya CCM watuhumiwa wa ufisadi, lakini inavyoonekana ni kama mwendelezo wa mapambano binafsi kati yako na Lowassa, je hili unaweza kulielezeaje?" aliuliza Kuyunga.
Nape aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Global Publishers, Mwenge, Dar es Salaam, alisema si kweli na hakuna kiongozi wa CCM mwenye uwezo wa kutumia chuki binafsi kutaka kiongozi au mwanachama mwenzake ang'oke.
"Binafsi namheshimu sana Lowassa, kwa sababu nyingi, kwanza ni mwanachama mwenzangu wa CCM, amewahi kuwa kiongozi wa nchi yetu, lakini kubwa zaidi ni mzee wangu, kwa hiyo namheshimu sana sana.
“Ninachokisema natekeleza uamuzi wa NEC ya CCM uliopitishwa na chama Dodoma, kama msemaji wa chama na si vinginevyo," alisema Nape.
"Kwa mujibu wa uamuzi ule wa chama Dodoma, hakuna anayelengwa binafsi, isipokuwa zinatekelezwa kanuni, taratibu na imani ya chama ambazo zipo tangu zamani na hizi kanuni na itikadi si za Nape.
“Hata kama sitakuwa katika nafasi hii au nisiwepo kabisa duniani, bado utekelezaji wake utaendelea, kwani zimekuwapo kabla sijazaliwa,” alisema Nape.
Akizungumzia taarifa iliyomkariri kuwa makatibu wa CCM wa mikoa takribani sita wamefukuzwa, Nape alisema makatibu hao hawakufukuzwa, isipokuwa wamestaafu baada ya kufikia umri wa kustaafu.
Akizungumzia umuhimu wa vyombo vya habari nchini, Nape alisema vina jukumu la kulinda uhuru na amani ya nchi, lakini pia kuendelea kuelimisha wananchi juu ya masuala ya kijamii na kufichua maovu kwa lengo la kujenga nchi na si kubomoa.
Alisema ili kuonesha utaifa wao, vyombo vya habari vijikite kuandika kwa marefu na mapana, mafanikio yaliyofikiwa kutokana na juhudi za Serikali iliyo madarakani, hadi sasa nchi inapokaribia kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wake.
Aliwataka kukumbusha hali ya uchumi, elimu, mazingira na mambo yalivyokuwa kabla ya Uhuru na kulinganisha na hali ilivyo sasa.
"Tunajua malengo hayajafikiwa yote na kwa kweli hayawezi kufikiwa yote, lakini itakuwa vizuri mkiyatangaza hata haya yanayoonekana madogo ambayo tumepata,” alisema Nape.
No comments:
Post a Comment